Hakukata Tamaa
MNAMO Oktoba 5, 1995, Matt Tapio mwenye umri wa miaka 14 alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe uliokuwa kwenye shina la ubongo wake. Uvimbe huo ukawa wenye kudumu. Upasuaji huu ulikuwa wa kwanza kati ya upasuaji mwingi ambao angefanyiwa katika muda wa miaka miwili na nusu ambayo ingefuata. Kisha alipewa tiba ya kemikali na matibabu ya mnururisho.
Matt aliishi Michigan, Marekani, ambapo alihudhuria shule ya umma na mikutano ya Kikristo. Alitumia fursa za kuongea na walimu na wanadarasa wenzake kuhusu imani yake na vilevile alishiriki kutembelea wengine kwenye huduma ya peupe. Katika pindi nyingi alipokuwa hospitalini—katika miaka yake miwili na nusu ya mwisho ya uhai wake, alitumia miezi 18 katika hospitali—aliwaangushia mamia ya fasihi za Biblia watu aliokutana nao huko.
Mara nyingi ilionekana kama Matt hangeokoka, lakini kila pindi alipata nafuu tena. Pindi moja, akiwa njiani kuelekea hospitali, alipatwa na mshtuko akaacha kupumua. Uhuishaji moyo na mapafu ulianzishwa, akahuishwa. Aliporudiwa na fahamu, alianza kulia na kusema kwa sauti kubwa: “Mimi ni mpiganaji! Mimi ni mpiganaji! Mimi sikati tamaa!” Watu walisema kwamba imani ya Matt katika Mungu ndiyo iliyomfanya aendelee kuishi kwa muda mrefu.
Matt alitimiza tamaa yake kubwa mnamo Januari 13, 1996, alipobatizwa katika ufananisho wa wakfu wake kwa Yehova Mungu. Alibatizwa katika kidimbwi cha faragha kwa sababu ya hatari ya ambukizo. Siku chache baadaye, alirudi hospitali tena kwa upasuaji zaidi. Katika Agosti 1997, Matt alitapika mfululizo kwa majuma kadhaa, lakini akapata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji zaidi.
Katika muda huu wote, Matt aliendelea kuwa mwenye ucheshi, akicheza na madaktari na wauguzi. Hawakuelewa kwa nini alikuwa na ucheshi wa ajabu namna hiyo. Mmoja wa madaktari alimwambia hivi: “Matt, ikiwa ningekuwa katika hali yako, ningezungusha pazia katika kitanda changu, nifunike kichwa changu, na kumwambia kila mtu aondoke kabisa.”
Mnamo Februari 1998, Matt alirudi nyumbani kutoka hospitali katika mara za mwisho. Alisisimuka sana kuwa hai na kuwa nyumbani hivi kwamba mara tu alipoingia katika mlango, alisema: “Nafurahi sana! Acheni tusali.” Kisha akaonyesha furaha yake kwa Yehova katika sala. Miezi miwili baadaye, mnamo Aprili 19, hatimaye alikufa kwa kansa.
Hapo mwanzoni, mahoji ya Matt yaliyorekodiwa yalisikizwa katika mkutano mmoja wa Mashahidi wa Yehova kwenye Jumba la Ufalme la mahali hapo. Aliulizwa hivi: “Ungewaambia nini wengine wetu tulio na afya ya kiasi kuhusu huduma na mikutano yetu ya Kikristo?”
Matt alijibu: “Fanyeni yote mwezayo sasa. . . . Hamjui kamwe ni nini liwezalo kutukia. . . . Lakini hata nini kitokee, msikome kamwe kutoa ushahidi juu ya Yehova.”