Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 4/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Mwelekeo wa Kutilia Shaka”
  • Sio Kuchelewa Kamwe Kuacha
  • Ndoa Yaweza Kuleta Furaha
  • Je, Ni Damu Iliyotiwa Uchafu?
  • Mara Nyingi Kansa Hukosa Kuchunguzwa
  • Kimelea Kinachosumbua Daima
  • Dalili za Mshtuko wa Akili
  • Kuchoma Barua Zilizopelekewa Watu Wengi
  • Haki za Tembo
  • Je, Twaelekea Kuwa na Lugha Moja Ulimwenguni?
  • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake
    Amkeni!—1998
  • Kufuga na Kuzoeza Tembo
    Amkeni!—2009
  • Kukabiliana na Matokeo Yake
    Amkeni!—1998
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 4/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

“Mwelekeo wa Kutilia Shaka”

“Hali yenye kutatanisha imedhihirika kwenye kitovu cha Baraza la Makanisa Ulimwenguni,” lasema gazeti la habari la Ufaransa Le Monde. Baraza hilo ambalo mnamo Agosti uliopita liliadhimisha ukumbusho wake wa miaka 50, lilianzishwa ili kusaidia kuunganisha madhehebu ya Kikristo ulimwenguni pote. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, kumetokea “mwelekeo wa kutilia shaka” ambao “unatishia ushirika” wa dini za Othodoksi katika shirika hilo. Mojawapo ya malalamiko yaliyotajwa na makanisa ya Othodoksi ni kwamba nchi fulani za Mashariki zimeathiriwa kwa njia ya kwamba “watu wao wamegeuzwa kidini” na wamishonari Wakatoliki na Waprotestanti. Tayari Kanisa moja la Othodoksi la Georgia limejiondoa kwenye baraza hili lenye washiriki 330. Hivyo, “kujiondoa kwa Makanisa ya Othodoksi kutoka kwenye Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika Geneva si nadharia ya kipuuzi tena,” lasema gazeti hilo la habari.

Sio Kuchelewa Kamwe Kuacha

Uchunguzi wa muda wa miaka 40 umefunua kwamba watu wanaoacha kuvuta sigareti, hata wanapokuwa na umri wa miaka 60, hupunguza kwa kiwango kikubwa hatari za kupatwa na kansa, laripoti gazeti la Uingereza Daily Telegraph. Profesa Julian Peto, wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kansa huko Sutton, Uingereza, asema hivi: “Ni kufikia mwaka jana tu ndipo tulipogundua vitisho kamili vinavyoletwa na uvutaji sigareti, vikiua nusu ya wavutaji badala ya robo yao kama tulivyodhani hapo awali, lakini pia tuligundua manufaa kubwa zinazoletwa na kuacha [kuvuta sigareti], hata katika umri wa uzee.” Watoto wanaonywa kwa ukawaida kuhusu hatari za kuvuta sigareti. Hata hivyo, Peto aonyesha kwamba watu wenye umri mkubwa zaidi wanahitaji kujua kwamba kuacha kuvuta sigareti kwaweza kupunguza sana hatari za kupatwa na kansa ya mapafu.

Ndoa Yaweza Kuleta Furaha

Watu fulani hushutumu ndoa kuwa yenye uonevu, na vipindi vya televisheni vya kuonyesha hali zenye kuchekesha mara nyingi huionyesha kuwa bure na ya kikale. Lakini mambo ya hakika yanaonyesha nini? Je, watu wasiofunga ndoa wako katika hali bora? Sivyo, kulingana na mwanasoshiolojia mmoja aliyenukuliwa katika gazeti la Philadelphia Inquirer. Anasema kwamba watu waliofunga ndoa “kwa ujumla wanakuwa wenye furaha zaidi, wenye afya zaidi na mali nyingi zaidi.” Wakiwa kikundi, wale wanaofunga ndoa pia hupatwa na mikazo michache, hawaelekei sana kufanya uhalifu au kutumia dawa haramu, na huwa wa kwanza kujitegemea. Haishangazi basi, wataalamu wanasema kwamba watu waliofunga ndoa huishi maisha marefu zaidi pia.

Je, Ni Damu Iliyotiwa Uchafu?

Magazeti tisa ya habari yanayochapishwa kila siku katika eneo la New York City hivi karibuni yalikuwa na tangazo chini ya kichwa “Kwa Wote Waliopokea Damu Kuanzia Januari 1991 hadi Desemba 1996 katika Hospitali ya New York/New Jersey.” Ijapokuwa wafadhili wa tangazo hilo, Kitivo cha Damu cha New York, wanasema kwamba kusudi la tangazo hilo lilikuwa kuhakikishia mtu yeyote aliyepokea damu mapema katika miaka ya 1990 kwamba damu ilikuwa salama, huenda matokeo yalikuwa kinyume. Kwa nini? Bila shaka jambo moja lililosababisha hangaiko lilikuwa onyo la tangazo hilo lililosema: “Watu waliopokea vitu vyenye damu vilivyochangwa katika kipindi hicho waweza kukabili hatari ya kupatwa na maambukizo yanayopitishwa kwa kutiwa damu mishipani, kama vile HIV na mchochota wa ini.”

Mara Nyingi Kansa Hukosa Kuchunguzwa

“Huenda takwimu rasmi za kisababishi cha kifo zikakadiria kwa kiwango kidogo vifo vingi vinavyosababishwa na kansa,” laripoti gazeti New Scientist. Dakt. Elizabeth Burton, wa Kitivo cha Kitiba cha Louisiana huko New Orleans, alichunguza rekodi za wagonjwa 1,105 ambao maiti zao zilichunguzwa kati ya mwaka wa 1986 na 1995, ili kulinganisha uchunguzi wa daktari wa kansa na uchunguzi uliofanyiwa maiti. Kulingana na Burton, asilimia 44 ya wagonjwa, kansa haikuwa imechunguzwa au aina ya kansa ilikuwa imechunguzwa vibaya. Viwango vya sasa vya kuchunguza maiti ambavyo ni asilimia 10—vikilinganishwa na asilimia 50 katika miaka ya 1960—“huenda makosa mengi yasipatikane kamwe,” lasema gazeti hilo.

Kimelea Kinachosumbua Daima

Katika nchi fulani ambazo hazijasitawi, kimelea kinachoitwa taenia solium kinachosababishia wanadamu ugonjwa unaoitwa cysticercosis bado kinatatiza. Kwa kawaida ugonjwa huo hutokana na kula nyama ya nguruwe iliyoambukizwa ambayo haijaiva vizuri au kula chakula kilichochafuliwa na mabuu ya kimelea hicho. Kulingana na gazeti la habari la Mexico City Excélsior, kimelea hicho “huwa vigumu kukitambulisha,” kwa sababu hiyo “kinaweza kusitawi ndani ya mwili wa binadamu kwa miaka mingi bila mtu mwenye kimelea hicho kutambua.” Dalili zaweza kutia ndani homa, kuumwa kichwa, kifafa, na matatizo ya kuona. Gazeti hilo lasema kwamba ili kuondoa kabisa kimelea hicho, watafiti katika National Autonomous University of Mexico wanafanya kazi ili kutokeza chanjo ya nguruwe.

Dalili za Mshtuko wa Akili

“Watu wengi hawawezi kutambulisha hata dalili moja ya mshtuko wa akili,” laripoti gazeti FDA Consumer. Gazeti hilo laongezea hivi: “Kati ya waliochunguzwa ni zaidi ya nusu tu ambao wangeweza kutaja angalau dalili moja ya mshtuko wa akili, na ni asilimia 68 tu ambao wangeweza kutaja jambo moja linaloweza kusababisha hatari ya kupatwa na mshtuko wa akili.” Mambo yako hivyo ijapokuwa uhakika wa kwamba mshtuko wa akili ndio kisababishi kikuu cha kifo na kutojiweza katika nchi zilizositawi kiviwanda za Magharibi. Ili kupunguza madhara yanayosababishwa na mshtuko wa akili, ni muhimu mtu atafute msaada wa kitiba anapoona dalili yenye kuonya mara ya kwanza. Dalili za kawaida zaidi za mshtuko wa akili ni kudhoofika ghafula, kufa ganzi, au kulemaa uso, mkono au mguu; kutoona vizuri kwa ghafula au upofu, hasa katika jicho moja; kutatizika katika kusema au kuelewa usemi; na kizunguzungu kisichoeleweka au kupoteza usawaziko, hasa dalili hizi zinapojumlishwa na nyinginezo.

Kuchoma Barua Zilizopelekewa Watu Wengi

Tangu mwaka wa 1992 sherehe ya kila mwaka ya Wabudha ya kuchoma barua imekuwa ikifanywa katika jiji la Nagoya, Japani, ili kutupilia mbali barua zilizopelekewa watu wengi. Wasimamizi wa posta waliweka masanduku ya kukusanya barua zisizotakikana katika posta zote za jijini na kuomba hekalu la Wabudha lifanye sherehe ya kuzichoma. Gazeti la habari la Asahi Evening News lilieleza kwamba huduma hii imeandaliwa “kwa ajili ya watu wenye ushirikina ambao waliogopa kupuuza barua hizo au kuziharibu wenyewe.” Kwa nini waliogopa? Kwa wazi barua hizo hazitoi ahadi yoyote kwa wale wanaofuata maagizo. Pia zinatishia mtu yeyote atapatwa na jambo baya kwa kuchoma barua hizo za watu wengi. Mathalani, barua moja ilitoa onyo la kwamba mtu fulani katika Tokyo ambaye alichoma barua hizo za watu wengi aliuawa.

Haki za Tembo

Katika sehemu nyingi za India, tembo hufanyiza fungu muhimu la wafanyakazi. Gazeti The Week laripoti kwamba katika jimbo la kaskazini ya India la Uttar Pradesh, tembo wametiwa ndani ya orodha ya serikali ya kulipa mishahara ili wawe waajiriwa kamili. Tembo huanza kazi akiwa na umri wa miaka kumi hivi, na kutumikia waajiri wake kwa miaka 50. Tembo anapostaafu hupokea marupurupu kama wafanyakazi wa serikali, na mtu anayezoeza na kushughulikia tembo, hupewa mgawo wa kuhakikisha kwamba tembo anapewa utunzaji unaofaa na kulishwa pia. Manufaa ambazo tembo wa kike hupata muda wote wa kufanya kazi hutia ndani likizo ya kujifungua ya mwaka mmoja kwa kujistarehesha kwenye bustani ya wanyama kabla ya kurudi kwenye kazi ya maana ya kubeba mbao, kufungia zizini na kuzoeza tembo wa mwituni, na kupiga doria kwenye mbuga za kitaifa na maeneo ya msitu yaliyolindwa.

Je, Twaelekea Kuwa na Lugha Moja Ulimwenguni?

“Katika nchi moja iliyo katikati mwa Asia ambako lugha za nchi za Magharibi huzungumzwa kwa nadra sana,” mvulana mwenye umri wa miaka minane amwambia baba yake kwamba anapaswa kujifunza Kiingereza. Baba amwuliza kwa nini. “Kwa sababu, baba, kompyuta husema Kiingereza.” Gazeti Asiaweek lasema kwamba hadithi hiyo, “yatolea kielezi jambo ambalo watu wengi hulifikiria kuwa madhara yenye hila kwenye Internet . . . , uwezo wa kuhimiza badiliko ambalo tayari ni la kasi kuelekea kusema lugha inayotawala tufeni pote—Kiingereza.” Gazeti hilo laongezea hivi: “Jambo hili halitokani na jitihada za kuchochea udugu wa ulimwenguni pote. Ni jambo lenye kutumika tu. Ikiwa tutaweza kuendeleza mazungumzo kwa njia ya kielektroni na kuendeleza biashara kwa kutumia Internet, njia ya kuwasiliana itakayotumiwa na wote inahitajiwa.” Kwa nini Kiingereza kitumiwe kuwa njia hiyo? Kwa sababu “biashara ya kompyuta za kibinafsi ilianza Marekani, kama ilivyo na mfumo wa Internet. Asilimia 80 ya habari zinazopatikana katika mfumo huo leo zinatokana na nchi zinazozungumza Kiingereza.” Katika visa fulani inakuwa hatua ya polepole kutumia lugha nyinginezo kwa sababu ya ugumu wa kubadilisha kibodi iliyopangwa kwa Kiingereza ifaane na lugha hizo. “Itagharimu jambo fulani,” lasema gazeti Asiaweek. “Wajuzi wa lugha wanatabiri kwamba nusu ya lugha zipatazo 6,000 zinazozungumzwa leo zitatoweka kabisa ufikapo mwisho wa karne ijayo, labda katika miaka 20 ijayo.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki