Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo
    Amkeni!—1998 | Juni 22
    • Jitayarishe Vizuri

      Waenda-likizoni wenye hekima hupanga mambo yao kimbele. Hujipatia vibali vya kusafiri na vyeti vya afya ili viwe katika hali nzuri wakati safari yao ianzapo. Uchunguzi kuhusu hatari za kiafya wanazoweza kukabili huwasaidia kuamua ni dawa gani za kuzuia maradhi wanazoweza kuchukua.

      Kwa kujitayarishia kufunga safari kuelekea maeneo ya malaria, wengi huanza kutumia dawa za kujikinga na malaria siku chache kabla ya kuondoka. Ingawa hivyo, kama kinga, mara nyingi hushauriwa waendelee kutumia dawa hizo wakati wote wa likizo yao na hata majuma manne baadaye. Hii ni kwa sababu vimelea vya malaria hupevuka ndani ya mwili kwa muda huo. Lakini tahadhari nyingine ni muhimu pia.

      Dakt. Paul Clarke, wa Shule ya London ya Usafi wa Kiafya na Dawa za Kitropiki, ashauri hivi: “Vya maana pia ni vizuia-wadudu vinavyopakwa mwilini au kwenye kiwiko, na vifundo vya miguu, nyavu za kuzuia mbu na kiua-wadudu chenye kuvukizwa kitumiacho nguvu za umeme.” Kwa kawaida huwa bora zaidi kuvinunua vifaa hivyo kabla hujaondoka kwenda likizoni.

      Kichefuchefu hufanya safari yoyote isipendeze. Ni nini hukisababisha? Mtafiti mmoja hudai kwamba kichefuchefu hutukia akili inapojazwa mambo mengi mapya ambayo hutokana na kuwa katika mazingira ya kigeni. Ikiwa mwendo wa meli, mtetemo wa ndege, au mvumo wa injini ya gari lako husababisha tatizo hili, jaribu kukaza uangalifu kwa kitu kilicho thabiti, labda upeo wa macho au barabara iliyo mbele. Hewa safi ya kutosha itaandaa oksijeni yenye kuhitajiwa sana. Katika visa vyenye kupita kiasi vya kichefuchefu dawa za mizio zaweza kutuliza dalili. Hata hivyo, yafaa kutahadhari: Jihadhari na athari zinazoweza kutukia, kama vile kusinzia, kwa kuwa chini ya hali fulani usalama wako ungeweza kuhatarishwa.

      Safari ndefu za ndege zina madhara yake ya kiafya, kama vile kuishiwa na maji mwilini. Kwa wengine, kukaa bila utendaji fulani kwa vipindi virefu kwaweza kuongeza hatari ya kuganda kwa damu mguuni. Ikiwa damu hiyo iliyoganda inatoka na kufikia mapafu au moyo, matokeo yaweza kuwa mabaya hasa. Kwa hiyo, wanapokuwa kwenye safari ndefu za ndege huenda wengine wakahitaji kufanya mazoezi kwa kutembea katika njia zilizo katikati ya viti au kwa kukunja na kukunjua mguu wanapokuwa wameketi. Na ili kupunguza kuishiwa na maji mwilini, kunywa vinywaji vingi visivyo na alkoholi.

  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo
    Amkeni!—1998 | Juni 22
    • Kulingana na kadirio moja, angalau nusu ya mamia ya mamilioni kadhaa ya watu ulimwenguni pote ambao husafiri ng’ambo kila mwaka hushikwa na ugonjwa au kujeruhiwa. Hivyo, kama vile Dakt. Richard Dawood, mhariri wa Travellers’ Health, anavyoeleza, “kinga ni muhimu kwa afya na hakuna msafiri anayepaswa kuipuuza.” Kwa kuwa mwili wa msafiri wahitaji kujipatanisha na aina mbalimbali za bakteria zilizo katika hewa, chakula, na maji, ni muhimu hasa kuwa mwangalifu kuhusu unachokula katika siku chache za kwanza.

      “Chakula hakipasi kudhaniwa kuwa ni salama kamwe,” aonya Dakt. Dawood, “isipokuwa ijulikane kuwa kimepikwa vizuri na kikamili (bakteria zimefishwa kwa kukipasha joto)—na kama ni nyama, mpaka rangi nyekundu isibaki.” Na bado, hata chakula kilichopashwa moto chaweza kushukiwa. Hivyo, “hakikisha kwamba chakula chako cha mchana si masalio ya chakula cha jioni cha jana kilichopashwa moto na kutayarishwa vizuri.”

      Hivyo, ikiwa uko likizoni katika eneo lililo tofauti kabisa na unakoishi, huenda sikuzote usiweze kula wakati uleule, mahali palepale, na kula kile utakacho. Lakini huu ni usumbufu kidogo tu kwa kuwa kwa kufanya hivyo waweza kuepuka kuharisha ambako kunaripotiwa kuwa kumeathiri sehemu mbili kwa tano za wasafiri wote wa kimataifa.

      Kuhusu vinywaji, maji ya chupa mara nyingi huwa salama kuliko yale yapatikanayo kutoka kwa wenyeji. Ingawa hivyo, ili kuepuka matatizo ni jambo la hekima vinywaji vya chupa au vya mikebe vifunguliwe unapoona. Laweza kuwa jambo la hekima pia kuepuka vipande vya barafu. Vishuku sikuzote isipokuwa unafahamu kuwa ni salama.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki