Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/22 kur. 15-17
  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jitayarishe Vizuri
  • Unapowasili
  • Mambo ya Maana ili Kufurahia Likizo
  • Furahia Likizo Bila Majuto!
    Amkeni!—1996
  • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho
    Amkeni!—1996
  • Je, Uko Tayari kwa Ajili ya Likizo?
    Amkeni!—1996
  • Twaa Fursa Utoe Ushahidi Wakati wa Desemba
    Huduma Yetu ya Ufalme—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/22 kur. 15-17

Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo

WAKATI wa likizo utajwapo—ni mawazo gani huja akilini? Je, ni mapumziko kwenye fuo zenye jua, zilizojaa michikichi yenye kutokeza kivuli chenye kupendeza? Au labda wafikiria furaha ya kupumua hewa baridi, safi itokayo mlimani?

Na bado, huenda ukawa na wasiwasi kuhusu halihewa isiyofaa, kukawizwa katika uwanja wa ndege, kichefuchefu, na kadhalika. Hata mawazo yako yawe nini, ni nini uwezalo kufanya ili likizo yako iwe yenye kufurahisha kadiri iwezekanavyo?

Jitayarishe Vizuri

Waenda-likizoni wenye hekima hupanga mambo yao kimbele. Hujipatia vibali vya kusafiri na vyeti vya afya ili viwe katika hali nzuri wakati safari yao ianzapo. Uchunguzi kuhusu hatari za kiafya wanazoweza kukabili huwasaidia kuamua ni dawa gani za kuzuia maradhi wanazoweza kuchukua.

Kwa kujitayarishia kufunga safari kuelekea maeneo ya malaria, wengi huanza kutumia dawa za kujikinga na malaria siku chache kabla ya kuondoka. Ingawa hivyo, kama kinga, mara nyingi hushauriwa waendelee kutumia dawa hizo wakati wote wa likizo yao na hata majuma manne baadaye. Hii ni kwa sababu vimelea vya malaria hupevuka ndani ya mwili kwa muda huo. Lakini tahadhari nyingine ni muhimu pia.

Dakt. Paul Clarke, wa Shule ya London ya Usafi wa Kiafya na Dawa za Kitropiki, ashauri hivi: “Vya maana pia ni vizuia-wadudu vinavyopakwa mwilini au kwenye kiwiko, na vifundo vya miguu, nyavu za kuzuia mbu na kiua-wadudu chenye kuvukizwa kitumiacho nguvu za umeme.” Kwa kawaida huwa bora zaidi kuvinunua vifaa hivyo kabla hujaondoka kwenda likizoni.

Kichefuchefu hufanya safari yoyote isipendeze. Ni nini hukisababisha? Mtafiti mmoja hudai kwamba kichefuchefu hutukia akili inapojazwa mambo mengi mapya ambayo hutokana na kuwa katika mazingira ya kigeni. Ikiwa mwendo wa meli, mtetemo wa ndege, au mvumo wa injini ya gari lako husababisha tatizo hili, jaribu kukaza uangalifu kwa kitu kilicho thabiti, labda upeo wa macho au barabara iliyo mbele. Hewa safi ya kutosha itaandaa oksijeni yenye kuhitajiwa sana. Katika visa vyenye kupita kiasi vya kichefuchefu dawa za mizio zaweza kutuliza dalili. Hata hivyo, yafaa kutahadhari: Jihadhari na athari zinazoweza kutukia, kama vile kusinzia, kwa kuwa chini ya hali fulani usalama wako ungeweza kuhatarishwa.

Safari ndefu za ndege zina madhara yake ya kiafya, kama vile kuishiwa na maji mwilini. Kwa wengine, kukaa bila utendaji fulani kwa vipindi virefu kwaweza kuongeza hatari ya kuganda kwa damu mguuni. Ikiwa damu hiyo iliyoganda inatoka na kufikia mapafu au moyo, matokeo yaweza kuwa mabaya hasa. Kwa hiyo, wanapokuwa kwenye safari ndefu za ndege huenda wengine wakahitaji kufanya mazoezi kwa kutembea katika njia zilizo katikati ya viti au kwa kukunja na kukunjua mguu wanapokuwa wameketi. Na ili kupunguza kuishiwa na maji mwilini, kunywa vinywaji vingi visivyo na alkoholi.

Je, mambo hayo pekee yanathibitisha hofu yako ya kusafiri kwa ndege? Ikiwa ndivyo, waweza kuhakikishiwa kwamba kusafiri kwa ndege ni salama kwa kadiri fulani. Kusafiri kwa njia hiyo kunasemekana kuwa salama mara 500 kuliko kuendesha pikipiki na ni salama mara 20 kuliko kusafiri kwa gari! Ingawa hivyo, wengine hudai kwamba takwimu hizo zinategemea ulinganisho wa umbali wa safari na si muda uliotumiwa safarini.

Kusafiri na watoto wadogo hutokeza ugumu wa kipekee. “Panga safari yako kwa usahihi kabisa,” apendekeza mtangazaji Kathy Arnold. Hata ingawa waweza kushindwa kufanya hivyo, beba vitabu, michezo, au vitu fulani ili kuvutia upendezi wa watoto. Hili litafanya kusafiri kupendeze familia nzima zaidi.

Unapowasili

‘Hunichukua siku nne au tano kupumzika kabla sijaanza kufurahia likizo yangu,’ ndiyo maelezo ya waenda-likizoni wengi. Kweli, kubadilikana ili ufae mazingira mapya huchukua muda. Kwa hiyo laweza kuwa jambo lenye hekima kutotembea-tembea siku ya kwanza au siku mbili za kwanza unapowasili. Ruhusu mwili wako na akili zako zizoeleane na ratiba mpya. Kukosa kufanya hivi kwaweza kusababisha mkazo na kuharibu likizo yako.

Kulingana na kadirio moja, angalau nusu ya mamia ya mamilioni kadhaa ya watu ulimwenguni pote ambao husafiri ng’ambo kila mwaka hushikwa na ugonjwa au kujeruhiwa. Hivyo, kama vile Dakt. Richard Dawood, mhariri wa Travellers’ Health, anavyoeleza, “kinga ni muhimu kwa afya na hakuna msafiri anayepaswa kuipuuza.” Kwa kuwa mwili wa msafiri wahitaji kujipatanisha na aina mbalimbali za bakteria zilizo katika hewa, chakula, na maji, ni muhimu hasa kuwa mwangalifu kuhusu unachokula katika siku chache za kwanza.

“Chakula hakipasi kudhaniwa kuwa ni salama kamwe,” aonya Dakt. Dawood, “isipokuwa ijulikane kuwa kimepikwa vizuri na kikamili (bakteria zimefishwa kwa kukipasha joto)—na kama ni nyama, mpaka rangi nyekundu isibaki.” Na bado, hata chakula kilichopashwa moto chaweza kushukiwa. Hivyo, “hakikisha kwamba chakula chako cha mchana si masalio ya chakula cha jioni cha jana kilichopashwa moto na kutayarishwa vizuri.”

Hivyo, ikiwa uko likizoni katika eneo lililo tofauti kabisa na unakoishi, huenda sikuzote usiweze kula wakati uleule, mahali palepale, na kula kile utakacho. Lakini huu ni usumbufu kidogo tu kwa kuwa kwa kufanya hivyo waweza kuepuka kuharisha ambako kunaripotiwa kuwa kumeathiri sehemu mbili kwa tano za wasafiri wote wa kimataifa.

Kuhusu vinywaji, maji ya chupa mara nyingi huwa salama kuliko yale yapatikanayo kutoka kwa wenyeji. Ingawa hivyo, ili kuepuka matatizo ni jambo la hekima vinywaji vya chupa au vya mikebe vifunguliwe unapoona. Laweza kuwa jambo la hekima pia kuepuka vipande vya barafu. Vishuku sikuzote isipokuwa unafahamu kuwa ni salama.

Mambo ya Maana ili Kufurahia Likizo

Baada ya kuwafanyia wasomaji wake uchunguzi, mhariri mwenye kusafiri aliripoti hivi: “Ikiwa hali ya hewa ilichangia sana mafanikio ya likizo yako, marafiki walichangia hata zaidi.” Kwa kweli, “uandamani mzuri” ulisemwa kuwa unachangia likizo nzuri “hata zaidi ya hoteli zilizo na huduma bora, safari zisizo na matatizo, chakula kizuri, na mandhari nzuri za kutazama.”

Lakini ni wapi uwezapo kupata marafiki wanaofaa unapokuwa likizoni? Njia moja ya kufanya hivyo ni kwa kutangulia kuandikia barua ofisi ya Watch Tower Society inayosimamia kazi katika nchi ambayo unapangia kwenda wakati wa likizo. Watakueleza mahali lilipo Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova karibu na mahali utakapokuwa na vilevile watakueleza saa za mikutano ya mahali hapo. Anwani chache za ofisi hizi zapatikana katika ukurasa wa 5 wa gazeti hili, na orodha ndefu zaidi yaweza kupatikana kwa kutazama Yearbook ya karibuni ya Mashahidi wa Yehova.

Jambo lililo muhimu pia katika kufurahia likizo yako na wakati uleule kuepuka majuto yoyote ni kutii shauri hili lenye hekima la Biblia: “Msiongozwe vibaya. Mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa.” (1 Wakorintho 15:33) Ukihisi tamaa yoyote ya kupuuza viwango na mazoea ya Kikristo unapokuwa likizoni mahali fulani pa mbali, kwa hekima tambua kwamba huu ni udhaifu na omba msaada wa kimungu ili kushinda tamaa hiyo. Pia wazazi wahitaji kuangalia utendaji wa watoto wao. Popote unapokuwa, kumbuka kwamba hizi ni “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.”—2 Timotheo 3:1.

Mnapoenda likizoni mkiwa familia, msidhani kwamba Mama atafanya yote afanyayo kwa kawaida anapokuwa nyumbani. Uwe tayari kusaidia katika kazi za kila siku. Onyesha roho ya ushirikiano. Mtazamo huo huwafanya wote wafurahie likizo.

Je, likizo yako itapendeza? Picha, hedaya chache zilizochaguliwa kwa makini, postikadi, na sanaa fulani za huko zaweza kwa kweli kutokeza kumbukumbu zenye kupendeza. Watakaokumbukwa hasa ni marafiki wapya utakaowapata. Wasiliana nao. Andikianeni barua ili kusimuliana mambo yenye kuwapendeza. Kuna njia nyingi zinazoweza kufanya likizo yako ifurahishe kikweli.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Vikumbusha Fulani vya Likizo

Kabla haujaondoka

• Uwe na hati halali zinazohitajiwa za kusafiri na za afya

• Uwe na dawa za kujikinga

Wakati wa safari

• Kunywa vinywaji vingi visivyo na alkoholi, na ufanye mazoezi unaposafiri safari ndefu kwa ndege

• Beba vitu vitakavyowapendeza vijana

Uwasilipo

• Ruhusu mwili na akili zako zijipatanishe na hali

• Kula vyakula na unywe vinywaji vilivyo salama tu

• Dumisha hadhari ya kiadili

• Shiriki kazi za kila siku na washiriki wengine wa familia

[Picha katika ukurasa wa 16]

Unapokuwa likizoni, chunga mashirika yako

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki