Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/22 kur. 3-4
  • Je, Uko Tayari kwa Ajili ya Likizo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Uko Tayari kwa Ajili ya Likizo?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Likizo Zaweza Kunufaisha
  • Kusafiri Kwenyewe ni Elimu
  • Kujitayarisha Kufaako
  • Furahia Likizo Bila Majuto!
    Amkeni!—1996
  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo
    Amkeni!—1998
  • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho
    Amkeni!—1996
  • Twaa Fursa Utoe Ushahidi Wakati wa Desemba
    Huduma Yetu ya Ufalme—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/22 kur. 3-4

Je, Uko Tayari kwa Ajili ya Likizo?

KIANGAZI kimekaribia katika Kizio cha Kaskazini. Baada ya muda mfupi mamilioni yatakuwa yakienda likizoni. Lakini likizo si za wakati wa kiangazi pekee. Utalii umekuwa biashara ya mwaka mzima, ukileta faida ya mabilioni ya dola kila mwaka. Ingawa waenda-likizo wengi husafiri ndani ya nchi yao wenyewe, usafiri wa nchi za kigeni, ambao wakati mmoja ulifanywa na matajiri, sasa ni jambo la kawaida.

Muda wa likizo unaoruhusiwa na waajiri hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Katika 1979, ni asilimia 2 tu ya wafanyakazi wa Ujerumani waliopata likizo ya majuma sita, lakini sasa wengi mno huipata. Likizo ya wastani kwa wafanyakazi wa viwanda katika Ulaya Magharibi ni zaidi ya majuma matano.

Likizo Zaweza Kunufaisha

Mwanzoni likizo ilimaanisha kitu tofauti sana na inachomaanisha leo. The New Encyclopædia Britannica hueleza: “Zoea la kisasa la likizo . . . lina maana iliyo kinyume kabisa na maana ya kale. Zaidi ya siku 100 za mwaka zilikuwa siku zilizowekwa kando kwa miungu tofauti-tofauti ya Kiroma ya kike na ya kiume. Kwenye siku zilizokuwa misherehekeo mitakatifu, na hivyo kuwa siku takatifu, watu walipumzika kutoka kawaida yao ya utendaji wa kila siku. Siku ambazo hazikuonwa kuwa takatifu ziliitwa dies vacantes, siku zisizo na chochote, ambapo watu walifanya kazi.” Badala ya kuwa siku za kazi, “siku zisizo na chochote” za nyakati za kisasa ni siku za mapumziko.

Wajerumani hupenda kuita likizo “majuma bora zaidi ya mwaka.” Waraibu wa kazi, kwa upande ule mwingine, huenda wakaona “siku zisizo na chochote” za leo kuwa zisizo na chochote kwelikweli, zisizo na utendaji wenye maana. Lakini haya yangekuwa maoni ya kupita kiasi. Maoni yaliyosawazika hukubali hekima ya kuacha kawaida ya utendaji wa kila siku, kufanya jambo tofauti, na kustarehe.

Sehemu chanya za likizo zilithibitishwa katika uchunguzi wa 1991 wa wafanyabiashara wakuu wa Ulaya, ambao 78 kati ya kila 100 walisema likizo “ni muhimu kabisa ili kuzuia kuungua-nishati kwa wafanyabiashara wakuu.” Asilimia 75 walihisi kwamba likizo ziliboresha matokeo ya ufanyaji kazi, na zaidi ya thuluthi mbili walisema likizo ziliboresha uwezo wa kubuni. Lenye kupendeza zaidi, asilimia 64 ya wanawake na asilimia 41 ya wanaume walikubali hii taarifa: “Ningepoteza usawaziko wangu ikiwa ningekosa likizo ya ukawaida.”

Kusafiri Kwenyewe ni Elimu

Tabibu na mwandishi Mwingereza wa karne ya 17, Thomas Fuller aliandika: “Yeye asafiriye sana hujua mengi.” Kusafiri hutuwezesha kufahamiana na watu kutoka sehemu nyinginezo, kujifunza juu ya desturi zao na njia yao ya maisha. Kusafiri katika nchi zilizo na hali ya chini ya maisha kuliko nchi yetu wenyewe kwaweza kutufunza kuwa na shukrani kwa kile tulicho nacho na kuamsha hisia-mwenzi kuelekea watu wasio na mafanikio kama sisi.

Tukiruhusu maono ya kusafiri yawe na uvutano juu yetu, kusafiri kwaweza kusahihisha dhana mbaya na kuondosha ubaguzi. Huko huandaa fursa ya kujifunza sisi wenyewe angalau sehemu ndogo ya lugha mpya, kujaribu vyakula ambavyo huenda vikatufurahisha, au fursa ya kuboresha kiwekeo cha picha cha familia, ukusanyaji wa slaidi, au maktaba ya video kwa vielelezo vya urembo wa uumbaji wa Mungu.

Bila shaka, ili kunufaika kabisa, ni lazima tufanye mengi zaidi ya kusafiri tu. Mtalii anayesafiri nusu ya mwendo kuzunguka ulimwengu ili kujibanza katika hoteli miongoni mwa watalii wenzake—wengi wao wakiwa watu kutoka nchi yake mwenyewe—ili kuogelea kwenye kidimbwi au ufuo wa kibinafsi wa hoteli, na kula chakula kilekile alacho nyumbani hatajifunza mengi. Ni sikitiko lililoje! Kulingana na ripoti, wasafiri wengi kwa wazi hukosa kuwa na upendezi mwingi katika nchi wanazozuru au katika watu wa huko.

Kujitayarisha Kufaako

Samuel Johnson, mtunga-insha na mshairi Mwingereza wa karne ya 18, alisema kwamba mtu asafiriye “ni lazima aende na ujuzi, ikiwa atarudi na ujuzi nyumbani.” Kwa hiyo ikiwa una nafasi ya kusafiri, jitayarishie safari yako. Soma kuhusu mahali unapokwenda kabla ya kwenda. Pangia unachotaka kuona, na uamue unachotaka kufanya. Kisha pangia vilivyo. Kwa kielelezo, ikiwa wataka kutembea-tembea ufuoni au kutembea milimani, beba viatu na nguo zifaazo.

Usijaribu kujaza mambo mengi sana katika ratiba yako na kuingiza mkazo wa maisha ya kila siku katika likizo yako. Weka kando wakati mwingi usiopangiwa chochote kwa ajili ya kufanya mambo yasiyotarajiwa. Moja ya manufaa za kweli za kuwa likizoni ni kuwa na wakati wa kufikiri na kutafakari bila msongo wa ratiba isiyonyumbulika, kujihisi huru kutokana na mkazo na vikwazo vya kuishi kulingana na ratiba isiyonyumbulika.

Likizo yenye kuthawabisha sana huenda hata ikahusisha kazi ngumu. Kufanya jambo tofauti kwa kawaida ni ufunguo wa likizo nzuri. Kwa kielelezo, shirika moja lisilo la kibiashara katika Marekani liitwalo Volunteer Vacations hupangia wajitoleaji watumie likizo katika kudumisha hifadhi na misitu ya kitaifa. Mjitoleaji mmoja alisema alifanya kazi ngumu, lakini alifurahia sana hivi kwamba aliamua kurudia jambo hilo mwaka uliofuata.

Mashahidi wa Yehova mara nyingi hutumia likizo zao kusafiri kwa mikusanyiko ya Kikristo au kuendeleza utumishi wao wa hadharani. Wengine hutumia likizo zao kufanya kazi kwenye makao makuu au makao ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika nchi zao nao hufurahia jambo hilo. Baadaye, wengi wa hawa huandika barua za uthamini kwa ajili ya pendeleo hilo.

Ndiyo, likizo zaweza kufurahisha sana, hata kuwa majuma bora zaidi ya mwaka. Si ajabu watoto hungojea kwa hamu na ghamu hadi siku za likizo zifike! Hata hivyo, kuna mambo unayohitaji kujilinda dhidi yayo. Makala ifuatayo itaeleza.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki