Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/22 kur. 5-7
  • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Linda Vitu Vyako vya Thamani
  • Epuka Aksidenti
  • Dumisha Afya Nzuri
  • Furahia Likizo Bila Majuto!
    Amkeni!—1996
  • Jinsi Uwezavyo Kuepuka Matatizo ya Likizo
    Amkeni!—1998
  • Je, Uko Tayari kwa Ajili ya Likizo?
    Amkeni!—1996
  • Twaa Fursa Utoe Ushahidi Wakati wa Desemba
    Huduma Yetu ya Ufalme—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/22 kur. 5-7

Kile Upaswacho Kulinda Dhidi Yacho

“KUSUDI lililo wazi zaidi la likizo ni kupata hali tofauti, kipumziko, badiliko katika kawaida ya kila siku,” akaandika mwandikaji wa habari Lance Morrow. Hata hivyo, alionelea kwamba wengine hurudi nyumbani kutoka likizoni wakiwa wameungua nishati hivi kwamba wanaapa kutoenda likizoni tena.

Hata hivyo, badala ya kusahau wazo la kwenda likizoni, lingekuwa jambo la hekima kuchunguza kimbele mitego iwezayo kutokea na kuchukua hatua za kuiepuka.

Linda Vitu Vyako vya Thamani

Wengi wamerudi kutoka likizoni na kupata kwamba wakati hawakuwapo nyumba yao ilivunjwa. Kwa hiyo kabla ya kwenda likizoni, waombe marafiki au majirani wawe wakitunza nyumba yako kwa ukawaida. Huenda hata wakaweza kutumia wakati fulani huko ili kuondosha wazo la kwamba hauko.

Pia wahitaji kulinda vitu vyako vya thamani mahali ulipo likizoni. Katika nchi fulani wageni huonwa kuwa matajiri, na kila mtalii aweza kunyang’anywa vitu. Kwa hivyo, zoea zuri ni kuacha pesa taslimu za ziada na hati zenye thamani katika mahali salama hotelini au mahali penginepo palipo salama. Uwe mwangalifu kuhusu watu usiowajua, bila kukosa fadhili.

Kila mwaka Miami, Florida, Marekani huwa na mamilioni ya waenda-likizo wa kigeni na wenyeji. Wahalifu hutenda kazi sana hasa katika maeneo hayo yenye watalii. Gazeti Time liliripoti, kwamba katika 1992, “katika Florida pekee, wageni 36,766 kutoka nchi nyinginezo na wenyeji, waliuawa kimakusudi, kulalwa kinguvu, kunyang’anywa au kuhasiriwa kwa njia fulani.”

Unapokuwa likizoni, jihadhari hasa na sinzia (wezi wa mifukoni). Wanaume wapaswa kuweka mapochi yao mahali pasipoonekana kwa urahisi na palipolindwa, kama vile mfuko wa ndani wa koti au mfuko wa mbele wa suruali. Wasafiri wazoefu mara nyingi huficha fedha zao kwa njia za kiakili. Kwa kielelezo, wengine hubeba fedha zao, pasipoti, na visa katika mapochi madogo yaliyo bapa yaliyofungwa shingoni na kutiwa ndani ya mavazi. Wanawake wapaswa kuwa waangalifu ama sivyo waendesha-baiskeli au pikipiki wanyakue mikoba isiyoshikiliwa kwa nguvu.

Wahalifu huendelea kupata njia mpya za kuwinda watalii. Kwenye magari-moshi ya moja kwa moja ya mwendo mrefu, abiria wanaolala katika nchi za Ulaya wamenyang’anywa wakati wa usiku. Vichochea usingizi vyaweza kuingizwa ndani ya vyumba ili kuhakikisha walio ndani ya vyumba hawaamki vitu vyao vinapoibwa. Katika pindi moja, kulingana na The European, “wanyang’anyi walifikiriwa kuwa waliondoka kimya-kimya katika gari moshi wakiwa na zaidi ya dola 845,000 pesa taslimu na vitu vilivyoibwa.”

Epuka Aksidenti

“Suluhisho langu la pekee kwa tatizo la aksidenti ambazo hunipata,” akasema mcheshi Robert Benchley, “ni kubaki kitandani siku nzima.” Lakini kisha akaongeza: “Hata wakati huo, sikuzote yawezekana kwamba utaanguka kutoka kitandani.” Kwa hakika, aksidenti hutokea kila mahali! Kwa hiyo hofu ya kupatwa na aksidenti unapokuwa likizoni haipasi kukutia woga na kukufanya ubaki nyumbani. Lakini kuna sababu ya pekee ya kuwa mwangalifu unapokuwa likizoni.

Hali za trafiki haziwezi kutegemeka katika pindi za likizo. Wajerumani wamezoea msongamano wa magari wenye urefu wa kilometa 80 katika nyakati hizo. Gazeti Time la Agosti 14, 1989, lilitaarifu hivi: “Kote katika Ulaya juma lililopita, mamilioni ya familia yalianza sikukuu yao ya kidesturi ya Agosti—na kila mtu alipatwa na wakati mbaya sana na wenye kuchosha. . . . Karibu kila barabara kuu itokayo Paris ilijaa na kusababisha magari kusimama. . . . Kati ya Julai 28 na Agosti 1, watu 102 walikufa katika migongano ya barabara kuu.” Kwa hiyo, kwa hekima simama kifupi ujipumzishe na mkazo uletwao na kusonga-songa na kusimama-simama.

Gazeti The European lilitoa ripoti ya mapendekezo kwamba waendesha-magari “wakawize safari zao hadi Jumapili—au wasafiri usiku.” Hata hivyo lilikubali kwamba waenda-likizo wengi “bado husisitiza kuondoka wakati huohuo.” Tokeo ni nini? Ulaya yenye msongamano wa magari. Ingawa ni jambo la hekima kusafiri wakati barabara hazijasongamana sana, usisahau uhakika wa kwamba kusafiri usiku kwaweza kuwa hatari. Mtu haoni vizuri sana usiku, na hivyo uwezekano wa kupata aksidenti waweza kuongezeka. Wakati mzuri zaidi wa kusafiri waweza kuwa mapema asubuhi.

Usipuuze vitu vingine viwezavyo kuwa vyanzo vya aksidenti baada ya kufika mahali unapoenda likizoni. Ikiwa hujatumia misuli yako kwa muda mrefu mwakani, hiyo itaumia unapojikaza sana usipokuwa katika hali nzuri sana. Kwa hiyo wekea mipaka michezo siku za kwanza-kwanza, wakati mwili wako uwezapo kujeruhiwa kwa urahisi.

Dumisha Afya Nzuri

Kulingana na kitabu 2,000 Everyday Health Tips for Better Health and Happiness, “matatizo ya kawaida sana ya afya ambayo wasafiri hukumbana nayo wakiwa safarini ng’ambo yanahusu hasa chakula, maji na maradhi machache yenye kuambukiza.” Maajenti wa usafiri wanaweza kuandaa shauri jinsi ya kuepuka matatizo hayo, nalo ni jambo lifaalo kufuata madokezo yao.

Katika maeneo mengi ni jambo la maana kuepuka kunywa maji ya mfereji. Na kumbuka, vijiwe vya barafu yaelekea vimetengenezwa kwa maji hayo. Huenda pia likawa jambo la hekima kuepuka kula mboga za majani, mayonnaise, vyakula vilivyotayarishwa kwa krimu, nyama mbichi au ambayo haijaiva vizuri ndani, kombe, na matunda yasiyopikwa, isipokuwa unaweza kuyaambua mwenyewe. Katika nchi za kitropiki, maziwa yapaswa kushemshwa kabla hujayanywa.

Chanzo kikubwa cha hatari kwa waenda-likizo wenye kuvaa mavazi mepesi ni jua, na katika miaka ya majuzi hatari hiyo imeongezeka kwa kutazamisha kwa sababu ya kupungua kwa ozoni katika angahewa. Idadi ya visa vipya vya malignant melanoma, aina hatari sana ya kansa ya ngozi, ilirudufika katika Marekani kati ya 1980 na 1993. T-shati zimeonwa katika Australia zenye maneno “Vaa shati na kofia na ujipake kizuia-miale ya jua.” Lakini usitulizwe na hisi bandia ya usalama. Vizuia-miale ya jua havitegemeki.

Usafiri wa hewani unaovuka kanda kadhaa za majira waweza kutokeza uchovu utokanao na kupitia kanda tofauti za majira. Ingawa wenyewe si maradhi, uchovu utokanao na kupitia kanda tofauti za majira waweza kuvuruga hali-njema ya kimwili ya mtu, hasa ikiwa mtu si mwenye afya nzuri. Uchunguzi uliofanyiwa wasafiri wa hewani kati ya London na San Francisco, tofauti ya muda wa saa nane, ulifunua kwamba “kujipatanisha kimwili . . . kulihitaji angalau siku kumi.” Kitabu The Body Machine pia kiliripoti kwamba wasafiri fulani ambao huvuka haraka kanda za majira walikuwa na “mwelekeo wa kuwa wasioweza kujieleza vyema, wenye kusita-sita na walielekea kufanya makosa mara mbili kuliko wengine. Kukaza fikira na kumbukumbu pia viliathiriwa.”a

Kwa kuongezea, usafiri wa ndege huwezesha kuenea kwa maradhi kutoka bara moja hadi jingine kwa muda wa saa chache tu. Gazeti la habari la Ujerumani Nassauische Neue Presse lilitaja: “Madaktari wana wasiwasi hasa kuhusu maradhi ‘ya kigeni’ kama vile malaria au mchochota wa ini ambayo waenda-likizo hurudi nayo kutoka Afrika, Asia au Amerika Kusini. Kila mwaka Wajerumani 2,000 hivi hurudi nyumbani wakiwa na malaria.” Baada ya tauni iitwayo bubonic plague kusababisha vifo katika India katika 1994, hatua kali za kuzuia zilichukuliwa ili kuizuia isienee katika nchi nyinginezo.

Watu wenye matatizo yenye kudumu ya afya, na vilevile wanawake wenye mimba, wapaswa kutahadhari zaidi wanaposafiri. Ingawa katika visa vingi hakuna sababu muhimu ya watu kama hao kuepuka kusafiri, wanapaswa kutafuta ushauri kutoka kwa daktari wao kimbele. Ni jambo la hekima kwa yeyote anayesafiri kubeba jina, anwani, na nambari ya simu ya rafiki au mtu wa ukoo awezaye kufikiwa wakati wa dharura.

Mtu anayehitaji sindano za kawaida za insulini ili kusawazisha kiwango chake cha sukari katika damu apaswa kukumbuka kwamba kuvuka kanda kadhaa za majira kutavuruga ratiba yake angalifu ya chakula na sindano. Atalazimika kupanga ifaavyo. Pia msafiri mwenye kisawazisha-mpigo-moyo apaswa kuhakikisha kwamba ana nambari ya simu ya daktari wake wa maradhi ya moyo.

Isitoshe, yeyote anayetegemea dawa fulani atataka kuibeba katika mzigo wake wa kuchukulika kwa sababu mzigo uliopotea au ulioelekea mahali pasipofaa waweza kusababisha msiba kwa msafiri. Kutokuwa na mavazi safi ya kubadilisha kwa siku kadhaa kwaweza kuudhi; kukaa bila dawa muhimu kwa saa chache kwaweza kutisha uhai.

Hatari za safari ya likizo hazipasi kuchukuliwa vivi hivi. Hata hivyo, hakuna sababu nzuri ya kuruhusu zikutie woga na kufanya ubaki nyumbani. Uwe mwangalifu tu. Kumbuka: Kujitayarisha kufaako husaidia kupambana na hatari ziwezazo kutokea. Fuata shauri lenye hekima: “Mtu mwerevu huona taabu ikija na kujibanza; yule mpumbavu huingia ndani yayo na kulipa adhabu.”—Mithali 22:3, The New English Bible.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa madokezo ya jambo la kufanya kuhusu uchovu utokanao na kupitia kanda tofauti za majira, ona Amkeni!, Juni 8, 1986, kurasa 19-21, la Kiingereza.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Unapokuwa likizoni, tahadhari kile unachokula

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki