-
Wafanyakazi wa Kujitolea KaziniAmkeni!—2001 | Julai 22
-
-
Wafanyakazi wa Kujitolea Kazini
KILA Ijumaa alasiri, Sirley, mwanamke wa makamo huko Brazili, hugeuza sebule yake kuwa darasa. Amélia, mmoja wa wanafunzi wake, huwasili saa nane hivi. Hakosi kamwe kufika na tayari anajua kusoma vizuri kuliko vijana wengi wa shule ya sekondari. Amélia ana umri wa miaka 82.
Amélia anafuata mfano wa wazee zaidi ya 60 ambao wamehitimu madarasa ambayo Sirley hufunza katika mji wa kwao bila malipo. Hivi majuzi, gazeti la Jornal do Sudoeste la Brazili lilikuwa na habari ya kindani juu ya kazi ya kujitolea ya Sirley. Baada ya kutaja kwamba “amesaidia sana watu wa jumuiya hii,” gazeti hilo lilisema kwamba njia ambayo Sirley hutumia kufundisha wazee ni yenye mafanikio hivi kwamba “baada ya kufundishwa kwa muda wa saa 120 tu, wanafunzi wanajua kuandika barua, kusoma magazeti, kufanya hesabu sahili, na kushughulikia mambo mengine ya kila siku.” Gazeti hilo laongeza kusema kwamba kitabu cha masomo ambacho Sirley hutumia darasani ni kijitabu kiitwacho Kujifunza Kusoma na Kuandika, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.a
Kuacha Kuaibika na Kuanza Maisha Yenye Heshima
Dona Luzia, mwanafunzi mwingine wa Sirley aliye na umri wa miaka 68, anaeleza kwamba kabla ya kujua kusoma na kuandika aliona haya kuongea na watu. Hata aliona vigumu kwenda dukani kununua vitu. “Sasa huwa ninawaandikia watu wa ukoo wanaoishi katika miji mingine barua, na ninashughulikia fedha zangu mwenyewe. Hakuna anayeweza kunidanganya tena kwa kunirudishia hela chache,” anasema akitabasamu. Maria, aliye na umri wa miaka 68 pia, akumbuka jinsi alivyokuwa akiaibika alipotia sahihi hundi ya malipo ya uzeeni kwa kuweka alama ya kidole-gumba. “Nilihisi kana kwamba nilikuwa mlemavu,” anasema. Lakini, sasa, kwa kuwa anajua kusoma na kuandika Maria anafurahia kutia sahihi kwa kuandika jina lake.
Wanafunzi na wahitimu wamesifu darasa ambalo Sirley hufunza bila malipo hivi kwamba sebule yake imekuwa ndogo. Hivi punde darasa hilo litahamishwa mahali pakubwa zaidi.
Programu Iliyotuzwa
Sirley ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Bila shaka unajua kwamba Mashahidi wa Yehova hujitolea kuwafundisha watu Biblia. Kuna wengi ambao wamefanikiwa kama Sirley. Watu zaidi ya 22,000 wamefundishwa kusoma na kuandika katika madarasa yanayofanywa katika mamia ya Majumba ya Ufalme kotekote nchini Brazili.
Madarasa kama hayo ya Mashahidi wa Yehova yamefanikiwa katika sehemu nyingine duniani vilevile. Kwa mfano, katika nchi ya Afrika ya Burundi, maofisa wa Idara ya Taifa ya Kufundisha Watu Wazima Kusoma na Kuandika (idara ya Wizara ya Elimu) walipendezwa sana na matokeo ya madarasa ya kusoma na kuandika ya Mashahidi hivi kwamba waliwapa walimu wanne tuzo kwa sababu ya “jitihada nyingi za kufundisha wengine kusoma.” Maofisa wa Serikali wanavutiwa hasa kuona kwamba asilimia 75 za wale waliojifunza kusoma na kuandika walikuwa wanawake—ambao kwa kawaida husitasita kuhudhuria madarasa kama hayo.
Wanafunzi 4,000 wanahudhuria madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika ya Mashahidi nchini Msumbiji, na wanafunzi zaidi ya 5,000 wamejifunza kusoma na kuandika katika muda wa miaka minne iliyopita. Mhitimu mmoja aliandika hivi: “Ninataka kutoa shukrani zangu za moyoni. Ninajua kusoma na kuandika kwa sababu ya shule hiyo.”
Misaada Ambayo Ni “Halisi, Wala Si ya Kijuujuu Tu”
Kutoa msaada ni kazi nyingine ya kujitolea ambayo Mashahidi wa Yehova hufanya. Hivi majuzi, kulikuwa na shughuli nyingi katika bohari moja huko Paris, Ufaransa. Watu 400 hivi walijitolea kutumia mwisho-juma wao kufunga chakula, nguo, na dawa katika masanduku. Kufikia mwishoni mwa mwisho-juma huo, makontena tisa makubwa, yaliyojaa vitu hivyo vyenye thamani ya dola za Marekani milioni moja, yalikuwa tayari kusafirishwa. Muda mfupi baadaye, vitu hivyo vilifika nchi za Afrika ya Kati zilizokumbwa na vita, ambapo Mashahidi waliojitolea waliwagawia wenye uhitaji bila kuchelewa. Karibu vitu vyote vilichangwa na Mashahidi vilevile.
Gazeti moja la Kongo (Kinshasa) lilisifu misaada ambayo Mashahidi wa Yehova hutoa, kuwa misaada ambayo ni “halisi, wala si ya kijuujuu tu.” Maofisa wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR) vilevile wamesifu jitihada hizo. Ofisa mmoja wa UNHCR huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alivutiwa sana na jinsi Mashahidi walivyofanya kazi hiyo kwa utaratibu sana hivi kwamba aliwapa waliojitolea ruhusa ya kutumia gari lake. Wenyeji pia wanavutiwa. Watazamaji walipoona jinsi vifaa hivyo vilivyogawiwa wenye uhitaji bila kuchelewa, wengine waliuliza hivi kwa mshangao: “Nyinyi mna mpango gani unaowawezesha kuwafikia watu wote wenye uhitaji?”
Kutoa misaada na kufundisha watu kusoma na kuandika ni baadhi tu ya utumishi mbalimbali ambao Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakifanya kotekote duniani kwa miaka mingi. Hata hivyo, Mashahidi wanafanya kazi nyingine ya kujitolea pia—utumishi unaowaletea wengine faida ya kudumu. Sehemu inayofuata itazungumzia habari hiyo.
-
-
Wafanyakazi wa Kujitolea KaziniAmkeni!—2001 | Julai 22
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Kutoa Msaada Huko Kobe!
Tetemeko la ardhi lilipokumba jiji lenye kusitawi la Kobe huko Japani, Januari 1995, lilisababisha uharibifu mkubwa sana. Watu zaidi ya 5,000 walikufa. Hilo lilikuwa tetemeko la ardhi lenye kusababisha vifo vingi zaidi tangu lile lililotukia mwaka wa 1923 huko Japani. Mara moja Mashahidi wa Yehova huko Japani na kotekote ulimwenguni walianza kusaidia walioathiriwa. Katika siku tatu tu dola za Marekani zaidi ya milioni moja zilichangwa. Vitu vingi vya aina yote vilichangwa na kusafirishwa mpaka Kobe.
Mzee mmoja Mkristo aliyeshughulikia kazi ya kutoa msaada alipata kwamba vitu vilivyochangwa kwenye Jumba la Ufalme la kwao vilikuwa vingi mno. Wangefanya nini na vitu hivyo vyote? Alidokeza vichangwe kwa hospitali moja ya karibu. Mashahidi walijaza vifaa hivyo kwenye gari la kubeba mizigo na kuvisafirisha. Safari hiyo ilichukua muda wa saa kadhaa badala ya dakika chache kama kawaida kwa sababu ya vifusi. Walipofika hospitalini walimpa daktari mkuu vitu hivyo vilivyotia ndani mablanketi, magodoro, nepi, matunda, na madawa yasiyohitaji maagizo ya daktari. Daktari alifurahi sana na kuwaambia kwamba wangefurahi sana kupokea chochote kile ambacho Mashahidi wangetoa. Hasa matunda yalithaminiwa sana kwa kuwa hakukuwapo chakula cha kutosha kwa wagonjwa wote.
Mashahidi walipoteremsha vitu hivyo, yule daktari—ijapokuwa alikuwa na kazi nyingi ya kufanya—alisimama kando na kutazama tu. Kisha aliinama kwa unyenyekevu na kuwashukuru. Walipoondoka aliendelea kusimama papo hapo ili kuonyesha uthamini wake. Mzee aliyeshughulikia jambo hili alisema kwamba baadaye madaktari katika hospitali hiyo walikubali kwa utayari zaidi kutibu wagonjwa walio Mashahidi wa Yehova.
-
-
Wafanyakazi wa Kujitolea KaziniAmkeni!—2001 | Julai 22
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Kazi ya Kujitolea Huleta Faida
Kikundi cha wafanyakazi waliojitolea katika kijiji cha Kabezi cha Burundi walipotaka kujenga Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova, ofisa wa sehemu hiyo aliwaomba jambo lisilo la kawaida. Aliwaomba Mashahidi waitengeneze barabara inayopita mahali walipotaka kujenga Jumba la Ufalme. Mashahidi walikubali kwa furaha kutengeneza barabara hiyo iliyoharibika, nao walifanya kazi yote kwa mikono. Wafanyakazi hao waliojitolea waliitengeneza vizuri sana hivi kwamba maofisa wa sehemu hiyo waliwashukuru kwa kazi yao na roho yao ya kujitolea. Baadaye, watu hao waliojitolea walijenga Jumba lao la Ufalme, linaloonekana juu. Sasa wana jumba zuri ambalo litaweza kuwasaidia kwa miaka mingi kuendeleza elimu ya Biblia. Naam, kazi ya kujitolea yaweza kuleta faida kubwa.
-