Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wakati wa Kutahini (1914-1918)
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
    • Wakati wa uchaguzi ulipokuwa ukikaribia, swali lilibaki, Ni nani angechukua mahali pa Russell akiwa msimamizi? The Watch Tower la Januari 15, 1917, liliripoti tokeo la mkutano wa kila mwaka, likieleza waziwazi hivi: “Ndugu Pierson, akitumia maelezo na maneno yafaayo sana yenye uthamini na upendo kuelekea Ndugu Russell, alitaarifu kwamba alikuwa amepokea ujumbe akiwa mwekaji wa kura za kuwakilisha kutoka kwa ndugu kotekote katika nchi kwamba apigie Ndugu J. F. Rutherford kura zao kuwa Msimamizi, na aliendelea kutaarifu kwamba alikubaliana kabisa na jambo hilo.” Baada ya jina la Rutherford kutajwa na kuungwa mkono, hakukuwa na mapendekezo zaidi, kwa hiyo “huyo Mwandishi alipiga kura kama alivyoelekezwa, na Ndugu Rutherford alitangazwa kwa kauli moja kuwa chaguo la Mkusanyiko huo awe Msimamizi.”

      Uchaguzi ukiwa umekwisha kuamuliwa, msimamizi huyo mpya alipokewaje? The Watch Tower lililotajwa hapo juu liliripoti hivi: “Ndugu kila mahali walikuwa wamesali kwa bidii kwa ajili ya mwongozo na mwelekezo wa Bwana katika jambo hilo la uchaguzi; na ulipomalizwa, kila mtu alikuwa mwenye kuridhika na mwenye furaha, wakiamini kwamba Bwana alikuwa ameelekeza mazungumzo na mafikirio yao na kujibu sala zao. Upatani mkamilifu ulienea miongoni mwa wote waliokuwapo.”

      Lakini “upatani mkamilifu” huo haukudumu sana. Msimamizi huyo mpya alipokewa kwa uchangamfu na wengi lakini si na wote.

      Msimamizi Mpya Asonga Mbele

      Ndugu Rutherford hakuwa na nia ya kubadili mwelekezo wa tengenezo, bali kuendelea na kigezo cha kusonga mbele kilichowekwa na Russell. Wawakilishi wasafirio wa Sosaiti (waliojulikana kama mapilgrimu) waliongezwa kutoka 69 hadi 93. Ugawanyaji wa trakti za bure za Sosaiti mbele ya makanisa na kwa ukawaida katika huduma ya nyumba hadi nyumba uliongezwa mwendo katika Jumapili za pindi kwa pindi.

      Ile “kazi ya kipasta,” iliyokuwa imeanzishwa kabla ya kifo cha Russell, sasa ikaongezwa. Hiyo ilikuwa kazi ya kufuatia, kama ule utendaji wa ziara za kurudia unaoendeshwa sasa na Mashahidi wa Yehova. Ili kutia nguvu zaidi kazi ya kuhubiri, msimamizi mpya wa Sosaiti alipanua kazi ya kolpota. Makolpota (watangulizi wa mapainia wa leo) waliongezwa kutoka 372 hadi 461.

      “Mwaka 1917 ulianza ukiwa na maoni yenye kuvunja moyo kidogo,” likataarifu The Watch Tower la Desemba 15, 1917. Naam, kufuatia kifo cha C. T. Russell, kulikuwa maoni fulani yasiyo na hakika, shaka fulani, na hofu fulani. Hata hivyo, ripoti ya mwisho wa mwaka ilikuwa yenye kutia moyo; utendaji wa shambani ulikuwa umeongezeka. Kwa wazi, kazi ilikuwa ikisonga mbele. Je, Wanafunzi wa Biblia walikuwa wamepita mtihani mwingine—kifo cha C. T. Russell—kwa mafanikio?

      Jitihada za Kupata Udhibiti

      Si kila mtu aliyekuwa mwenye kumuunga mkono huyo msimamizi mpya. C. T. Russell na J. F. Rutherford walikuwa watu tofauti sana. Walikuwa na nyutu tofauti na walitoka katika malezi tofauti. Kwa wengine ilikuwa vigumu kukubali tofauti hizo. Katika akili zao, hapana yeyote ambaye angeweza kuchukua mahali pa Ndugu Russell kwa kufaa vizuri.

      Wachache, hasa kwenye makao makuu, kwa kweli walimchukia Ndugu Rutherford. Uhakika wa kwamba kazi ilikuwa ikisonga mbele na kwamba alikuwa akifanya kila jitihada kufuata mipango ambayo ilikuwa imewekwa na Russell haukuonekana ukiwavutia. Upesi upinzani ukaongezeka. Washiriki wanne wa baraza la waelekezi wa Sosaiti walifikia hatua ya kujaribu kunyakua udhibiti wa usimamizi kutoka mikononi mwa Rutherford. Hali ilifikia hatua hatari katika kiangazi cha 1917, kwa kutolewa kwa The Finished Mystery, lile buku la saba la Studies in the Scriptures.

      Ndugu Russell hakuweza kutokeza buku hili wakati wa maisha yake, ingawa yeye alikuwa ametumaini kufanya hivyo. Kufuatia kifo chake, Halmashauri ya Utekelezi ya Sosaiti ilipanga washiriki wawili, Clayton J. Woodworth na George H. Fisher, watayarishe kitabu hiki, ambacho kilikuwa ni maelezo juu ya Ufunuo, Wimbo Ulio Bora, na Ezekieli. Kwa sehemu, kilitegemea habari iliyokuwa imeandikwa na Russell juu ya vitabu hivyo vya Biblia, na maelezo na mafafanuzi mengine yakaongezwa. Maofisa wa Sosaiti walitoa kibali ili hati iliyokamilishwa itangazwe nacho kitabu kikatolewa kwa familia ya Betheli penye meza ya chakula siku ya Jumanne, Julai 17, 1917. Katika pindi hiyohiyo, tangazo lenye kugutusha lilitolewa—wale waelekezi wapinzani wanne walikuwa wameondolewa, na Ndugu Rutherford alikuwa ameweka wengine wanne wajaze nafasi zao zilizoachwa wazi. Itikio lilikuwa nini?

      Ilikuwa kama kwamba kombora lilikuwa limelipuka! Waelekezi hao wanne walioondolewa walitumia kwa hamu pindi hiyo ili kuchochea ushindani wa saa tano mbele ya familia ya Betheli juu ya usimamizi wa mambo ya Sosaiti. Idadi fulani ya familia ya Betheli iliwaunga mkono wapinzani. Upinzani huo uliendelea kwa majuma kadhaa, huku wachochezi hao wakitisha “kupindua uonezi ulioko,” kama walivyosema. Lakini Ndugu Rutherford alikuwa na msingi imara wa kuchukua hatua aliyokuwa amechukua. Jinsi gani hivyo?

      Ilitokea kwamba ijapokuwa waelekezi hao wanne wenye kupinga walikuwa wamewekwa na Ndugu Russell, kuwekwa huko hakukuwa kumethibitishwa kwa kura na washiriki wa shirika kwenye mkutano wa kila mwaka wa Sosaiti. Kwa hiyo, hao wanne hawakuwa hata kidogo washiriki halali wa baraza la waelekezi! Rutherford alikuwa anajua jambo hilo lakini hakuwa amelitaja mwanzoni. Kwa nini? Alikuwa ametaka kuepuka kutoa wazo la kwamba alikuwa akienda kinyume cha mapenzi ya Ndugu Russell. Hata hivyo, ilipopata kuwa wazi kwamba hawangeacha upinzani wao, Rutherford alitenda kulingana na mamlaka na madaraka yake akiwa msimamizi kuweka wengine wanne badala yao, ambao kuwekwa kwao kungethibitishwa kwenye mkutano wa kila mwaka wenye kufuata, ambao ungefanywa mnamo Januari 1918.

      Katika Agosti 8, wale waliokuwa waelekezi wasiotosheka na wenye kuwaunga mkono waliacha familia ya Betheli; walikuwa wameombwa waondoke kwa sababu ya usumbufu waliokuwa wakitokeza. Upesi wakaanza kueneza upinzani wao kwa kampeni iliyosambaa ya kutoa hotuba na kuandika barua kotekote katika Marekani, Kanada, na Ulaya. Kama tokeo, baada ya kiangazi cha 1917, idadi fulani ya makutaniko ya Wanafunzi wa Biblia iligawanyika vikundi viwili—wale waliokuwa waaminifu-washikamanifu kwa Sosaiti na wale waliopotezwa kwa urahisi na maneno laini ya wapinzani.

      Lakini je, waelekezi hao walioondolewa katika jitihada ya kupata udhibiti wa tengenezo, wangeweza kujaribu kuvuta wale waliokuwa wakihudhuria mkutano wa kila mwaka? Akitazamia itikio hilo, Rutherford alihisi ni jambo lenye kufaa kufanya uchunguzi wa makutaniko yote. Matokeo yalikuwa nini? Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika The Watch Tower la Desemba 15, 1917, wale waliokuwa wakipiga kura walionyesha uungaji-mkono wao mkubwa sana kwa J. F. Rutherford na waelekezi wenye kushirikiana naye! Jambo hilo lilithibitishwa kwenye mkutano wa kila mwaka.d Jitihada za wapinzani kupata udhibiti zilikuwa zimeshindwa!

  • Wakati wa Kutahini (1914-1918)
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
    • d Kwenye mkutano wa kila mwaka uliofanywa katika Januari 5, 1918, wale saba waliopokea idadi ya juu zaidi ya kura walikuwa J. F. Rutherford, C. H. Anderson, W. E. Van Amburgh, A. H. Macmillan, W. E. Spill, J. A. Bohnet, na G. H. Fisher. Kutoka washiriki hao saba wa baraza la waelekezi, wale maofisa watatu walichaguliwa—J. F. Rutherford akiwa msimamizi, C. H. Anderson akiwa makamu wa msimamizi, na W. E. Van Amburgh akiwa mwandishi-mweka-hazina.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki