-
Samoa2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Baada ya safari hiyo yenye mafanikio nchini Samoa, Harold, alilazimika kurudi Australia. Hata hivyo, kijitabu kimoja alichoacha hatimaye kilifika mikononi mwa mfanyakazi mmoja anayeitwa Pele Fuaiupolu.d Ujumbe wa kijitabu hicho ulibaki moyoni mwa Pele, hadi Mashahidi waliporudi na kutilia maji kweli zenye thamani zilizokuwa zimepandwa.—1 Kor. 3:6.
Mwaka wa 1952, miaka 12 baadaye, John Croxford, Shahidi kutoka Uingereza, alifika Apia, jiji kuu la Samoa, kwenye kisiwa cha Upolu. Aliajiriwa katika ofisi ambayo Pele alikuwa akifanya kazi. John alikuwa mwenye urafiki naye alikuwa na hamu ya kuwahubiria wengine. Alipogundua kwamba Pele anapendezwa na Biblia, John aliamua kumtembelea nyumbani kwake. Pele aandika: “Tuliongea mpaka karibu mapambazuko ya Jumapili. Nilimwuliza maswali mengi, naye akanijibu yote kwa kutumia Biblia. Nilisadikishwa kabisa kwamba huu ndio ukweli niliokuwa nikiutafuta kwa muda mrefu.” Baadaye, mwaka huohuo, Pele na mke wake, Ailua, wakawa Wasamoa wa kwanza kujiweka wakfu kwa Yehova na kubatizwa.
Pele alijua kwamba hangeweza kuiacha dini ya mababu zake hivihivi tu. Kwa hiyo akajifunza mambo mengi awezavyo na kumwomba Yehova kwa bidii amsaidie. Alipoagizwa na chifu mkuu wa familia afike kwenye mkutano uliofanyiwa Faleasiu, kijiji cha nyumbani kwa akina Pele kilichokuwa kilomita 19 kutoka Apia, Pele na mtu mwingine wa familia yao ambaye pia alikuwa akipendezwa na kweli walijikuta mbele ya machifu sita, wasemaji watatu, mapadri kumi, walimu wawili wa masuala ya kidini, chifu mkuu aliyekuwa mwenyekiti katika kikao hicho, na wanaume na wanawake wazee wa familia.
“Walitulaani na kutushutumu kwa kuliaibisha jina la familia na kanisa la mababu zetu,” akumbuka Pele. Kisha chifu mkuu akapendekeza kuwe na mjadala, mjadala ambao uliendelea hadi saa 10 alfajiri.
“Ijapokuwa wengine walipiga kelele wakisema, ‘Mnyang’anyeni Biblia! Usitumie Biblia!’ niliitumia kujibu maswali yote na kukanusha madai yao,” asema Pele. “Mwishowe, wakabaki kimya, wakiinamisha vichwa vyao chini kwa aibu. Kisha chifu mkuu akasema kwa sauti hafifu: ‘Umeshinda, Pele.’”
“Samahani, Chifu,” Pele akumbuka akimwambia chifu mkuu, “hayakuwa mashindano. Furaha yangu ni kwamba usiku wa leo mmesikia ujumbe wa ufalme. Ni matumaini yangu kwamba mtaufikiria kwa uzito.”
Kwa sababu ya unyenyekevu wa Pele, na kumtegemea Yehova na Neno Lake, Biblia, mbegu ya kweli ya Ufalme ilikuwa imeanza kutia mizizi Upolu.
MIKUTANO YA KWANZA-KWANZA
Habari kuhusu dini mpya ya Pele zilienea kama moto katika jamii hiyo yenye uhusiano wa karibu. Kama Waathene wa karne ya kwanza ambao Paulo aliwahuburia, baadhi yao walikuwa na hamu ya kujua mengi zaidi kuhusu ‘fundisho hilo jipya.’ (Mdo. 17:19, 20)
-
-
Samoa2009 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
d Wasamoa huwa na jina moja, kama vile Pele, halafu jina la familia. Jina la familia la Pele ni Fuaiupolu.
-