-
“Heri Mtu Yule Aonaye Hekima”Mnara wa Mlinzi—2001 | Machi 15
-
-
“Nalitukuka Tokea Milele”
Katika sura ya 8 ya Mithali hekima haifananishwi na mtu ili kufafanua sifa fulani ya kuwazia tu. Kwa njia ya ufananisho, hekima yarejezea pia uumbaji wa Yehova ulio wa maana zaidi. Hekima yaendelea kusema: “BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde wala chanzo cha mavumbi ya dunia.”—Mithali 8:22-26.
Ufafanuzi uliotangulia wa hekima inayofananishwa na mtu walingana kama nini na yale yanayosemwa na Maandiko kuhusu “Neno”! “Hapo mwanzoni Neno alikuwako, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa mungu,” akaandika mtume Yohana. (Yohana 1:1) Hekima inayofananishwa na mtu yawakilisha kwa njia ya mfano Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, kabla ya kuwa mwanadamu.b
Yesu Kristo ni “mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote; kwa sababu kwa njia yake vitu vingine vyote viliumbwa katika mbingu na juu ya dunia, vitu vinavyoonekana na vitu visivyoonekana.” (Wakolosai 1:15, 16) Hekima inayofananishwa na mtu yaendelea kusema: “[Yehova] alipozithibitisha mbingu nalikuwako; alipopiga duara katika uso wa bahari; alipofanya imara mawingu yaliyo juu; chemchemi za bahari zilipopata nguvu; alipoipa bahari mpaka wake, kwamba maji yake yasiasi amri yake; alipoiagiza misingi ya nchi; ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; nikawa furaha yake kila siku; nikifurahi daima mbele zake; nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.” (Mithali 8:27-31) Mwana mzaliwa wa kwanza wa Yehova alikuwa kando ya Baba yake, akifanya kazi kwa bidii pamoja naye—Muumba asiye na kifani wa mbingu na dunia. Yehova Mungu alipoumba mwanadamu wa kwanza, Mwana Wake alishiriki kazi hiyo akiwa Stadi wa Kazi. (Mwanzo 1:26) Si ajabu kwamba Mwana wa Mungu anawapenda sana wanadamu!
“Ana Heri Mtu Yule Anisikilizaye”
Akiwa kama hekima inayofananishwa na mtu, Mwana wa Mungu asema: “Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, akisubiri sikuzote malangoni pangu, akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, na wao wanichukiao hupenda mauti.”—Mithali 8:32-36.
Yesu Kristo ndiye mfano halisi wa hekima ya Mungu. “Zenye kusitiriwa kwa uangalifu ndani yake ni hazina zote za hekima na za ujuzi.” (Wakolosai 2:3) Acheni basi, tumsikilize kwa makini na kufuata hatua zake kwa ukaribu. (1 Petro 2:21) Kumkataa ni kuangamiza nafsi yetu wenyewe na kupenda kifo, kwa kuwa “hakuna wokovu katika mwingine yeyote.” (Matendo 4:12) Kwa kweli, acheni tumkubali Yesu kuwa mtu ambaye Mungu ametoa kwa ajili ya wokovu wetu. (Mathayo 20:28; Yohana 3:16) Kwa kufanya hivyo tutapata furaha inayotokana na ‘kuona uzima na kupata kibali kwa Yehova.’
-
-
“Heri Mtu Yule Aonaye Hekima”Mnara wa Mlinzi—2001 | Machi 15
-
-
b Uhakika wa kwamba neno la Kiebrania “hekima” sikuzote huwa katika ngeli ya kike haupingani na matumizi ya hekima kuwakilisha Mwana wa Mungu. Neno la Kigiriki “upendo” katika usemi “Mungu ni upendo” liko katika ngeli ya kike pia. (1 Yohana 4:8) Hata hivyo, linatumiwa kurejezea Mungu.
-