-
Michezo Mipya ya KompyutaAmkeni!—2002 | Desemba 22
-
-
Michezo Mipya ya Kompyuta
Kulingana na gazeti la “Newsweek,” mchezo wa “Grand Theft Auto 3” ndio “mchezo wa video ulionunuliwa sana mwaka jana.” Katika mchezo huo, wachezaji hupata cheo katika shirika la wahalifu kwa kushiriki matendo mbalimbali ya uhalifu, kama vile ukahaba na kuua. Gazeti la “Newsweek” linasema kwamba “mambo yote unayofanya katika mchezo huo yana matokeo fulani.” Ukiiba gari kisha uwagonge na kuwaua watu wanaotembea kwa miguu, polisi watakuandama. Ukimpiga risasi polisi mmoja, majasusi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wataanza kazi. Ukimuua jasusi wa FBI, wanajeshi watajitahidi juu chini kukuangamiza. Ijapokuwa mchezo huo ulikusudiwa watu wenye umri wa miaka 17 na zaidi, watoto wadogo wameuziwa mchezo huo. Inasemekana kwamba, hata watoto wenye umri wa miaka 12 wanataka kuucheza.
MCHEZO wa kwanza wa kompyuta, unaoitwa Spacewar, ulibuniwa mwaka 1962. Mchezaji alipaswa kuepuka sayari ndogo na vyombo vya anga vya maadui. Baadaye, michezo mingi kama hiyo ilibuniwa. Kompyuta zenye uwezo mkubwa zaidi wa kuhifadhi habari zilipoanza kutumiwa sana katika miaka ya 1970 na 1980, michezo ya kompyuta pia ilienea. Kulikuwa na michezo yenye vituko, michezo ya kuchemsha bongo, michezo ya kupanga mikakati, na michezo ya kivita. Kwa mfano, katika mchezo mmoja wa kupanga mikakati, mchezaji huhitajika kupanga na kudhibiti ongezeko la watu katika majiji au tamaduni mbalimbali. Kuna michezo mingi ya kompyuta inayoigiza michezo ya kawaida kama vile hoki inayochezwa kwenye barafu na gofu.
Michezo mingine husifiwa kwa sababu inaelimisha na kufurahisha. Katika michezo fulani, unaweza kujaribu kuendesha ndege kubwa, gari linaloenda kasi, au hata gari-moshi. Unaweza pia kuteleza kwenye theluji kwa kutumia ubao au kutembelea sehemu mbalimbali za ulimwengu. Hata hivyo, michezo fulani ya kivita, kama ile inayohusisha sana kufyatua risasi, hushutumiwa kwa sababu ina jeuri nyingi. Katika michezo hiyo, mchezaji huchagua silaha kisha kuwapiga risasi na kuwaua wanadamu walio maadui au maadui wengine ambao si wanadamu.
Michezo ya Internet Imepamba Moto
Nchi ya Britannia ina wakazi 230,000. Wakazi hao ni watu wa aina zote—wanajeshi, washonaji wa nguo, wafua-vyuma, na wanamuziki. Wao hupigana vita, hujenga majiji, hufanya biashara, huoa na kuolewa, na kufa. Lakini nchi hiyo ya Britannia ni ya kuwaziwa tu. Wachezaji huona nchi hiyo ya zama za kati katika mchezo fulani wa Internet wanaposhindana na wachezaji wengine kwa wakati uleule. Mchezo huo umependwa na wengi na unatarajiwa “kupamba moto” hata zaidi katika biashara ya michezo ya kompyuta. Mchezo unaoitwa Ultima Online—ambao unatia ndani nchi hiyo ya kuwaziwa ya Britannia—ulianzishwa mwaka wa 1997 na ndio mchezo wa kwanza wa Internet. Tangu wakati huo, michezo mingineyo ya Internet imetokea, na mingine ingali inatayarishwa.
Michezo ya Internet inatofautianaje na michezo mingine ya kompyuta? Wahusika mbalimbali katika michezo hiyo hawaendeshwi kwa kompyuta, bali wanaendeshwa na wachezaji wengine ambao wanacheza wakati huohuo kupitia Internet. Maelfu ya watu wanaweza kucheza pamoja wakati uleule. Kwa mfano, inasemekana kwamba wakati fulani mchezo wa Ultima Online ulichezwa na watu kutoka nchi 114 wakati uleule. Huenda michezo hiyo inapendwa kwa sababu watu hupata nafasi ya kushirikiana. Wachezaji wanaweza kuwasiliana, na hilo linawafanya wahisi kwamba wao ni watu wa jamii moja.
Biashara Kubwa
Inatazamiwa kwamba biashara ya michezo ya kompyuta itapata ufanisi mkubwa. Kufikia mwaka wa 1997 mapato ya kila mwaka kutokana na biashara ya michezo ya kompyuta na ya video huko Marekani ilikuwa dola bilioni 5.3 za Marekani, na mapato ulimwenguni pote yalikuwa angalau dola bilioni 10 za Marekani. Na yaonekana kwamba biashara hiyo itazidi kutia fora. Biashara hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 50 hadi 75 katika miaka mitano ijayo.
Kulingana na shirika la Forrester Research, kila siku zaidi ya watu milioni moja huanza kucheza michezo mbalimbali ya Internet na yasemekana kwamba faida inayotokana na michezo hiyo itaongezeka wakati mbinu mpya ya kuwaunganisha watu haraka kwenye Internet itakapotumiwa katika sehemu nyingi. Watoto ambao wamecheza michezo ya kompyuta tangu utotoni huendelea kucheza hata wanapokuwa wakubwa. Mtu mmoja ambaye amecheza michezo hiyo kwa muda mrefu anasema: “Kucheza michezo ya kompyuta ni njia ya kushirikiana na marafiki kutoka sehemu zote za ulimwengu.”
Je, michezo yote ya kompyuta ni burudani tu, au kuna hatari fulani zinazohusika? Na tuone.
-
-
Je, Kuna Hatari kwa Wachezaji?Amkeni!—2002 | Desemba 22
-
-
Je, Kuna Hatari kwa Wachezaji?
Mvulana mwenye umri wa miaka 12 “alimzuia adui yake asiyekuwa na silaha asitoroke na akaweka bunduki karibu sana na kichwa chake. ‘Hutaponyoka!’ akasema mvulana huyo, huku akicheka kwa kichaa na kumdhihaki adui yake kwenye kompyuta. ‘Nimekushika!’ Kisha akabonyeza kidude fulani cha mchezo huo na kumpiga risasi adui huyo usoni. Adui akaanguka chini huku damu ikitapakaa kwenye koti lake jeupe. Mvulana huyo akacheka, akisema: ‘Nimekumaliza!’”
KICHWA cha makala yetu kinatokana na mchezo wa kompyuta unaoelezwa hapo juu, ambao umenukuliwa kutoka katika makala yenye kichwa “Je, Jeuri Kwenye Kompyuta Inaweza Kuwahatarisha Watoto Wako?” iliyoandikwa na Stephen Barr. Kuna zaidi ya michezo 5,000 ya kompyuta na video. Baadhi ya michezo hiyo huonwa kuwa burudani isiyodhuru na yenye kuelimisha.
Mchezo fulani hufundisha jiografia na mwingine huwafundisha watu kuendesha ndege. Mingine humzoeza mchezaji kufikiri na kutatua matatizo. Pia, kuna michezo iliyokusudiwa kumsaidia mchezaji kushinda udhaifu fulani. Kwa mfano, mchezo mmoja umetayarishwa ili kuwasaidia watu wenye tatizo fulani la kusoma. Michezo fulani inaweza pia kuwasaidia vijana kufahamu kompyuta vizuri zaidi, na jambo hilo ni muhimu sana katika enzi hizi za tekinolojia.
Wataalamu Waonyesha Hatari
David Walsh, rais wa taasisi moja inayohangaikia jinsi familia zinavyoathiriwa na vyombo vya habari anasema hivi: “Baadhi ya michezo huwa na mambo mabaya kama vile jeuri, ngono, na matusi. Kwa kusikitisha, inaonekana kwamba michezo hiyo inapendwa hasa na watoto wenye umri wa miaka minane hadi 15.”
Uchunguzi mmoja uliofanywa Marekani ulionyesha kwamba asilimia 80 hivi ya michezo ya video inayopendwa na vijana ni ile yenye jeuri. Rick Dyer, rais wa kampuni ya Virtual Image Productions, anasema hivi: “Hiyo si michezo tu bali ni njia za kujifunza mambo. Tunawafundisha watoto kwa njia ya ajabu sana jinsi ya kutumia bunduki. . . . Lakini hawajifunzi matokeo halisi ya matendo yao.”
Mnamo mwaka wa 1976, watu walilalamika kuhusu michezo yenye jeuri wakati mchezo fulani unaoitwa Death Race ulipotokea. Katika mchezo huo, mchezaji alipaswa kuwagonga na kuwaua kwa gari watu waliokuwa wakitoka upande mmoja hadi mwingine. Mchezaji aliyewaua watu wengi ndiye aliyeshinda. Michezo ya kisasa, ambayo ni ya hali ya juu zaidi, inaonyesha picha vizuri zaidi na kumwezesha mchezaji kushiriki matendo ya jeuri kwa uhalisi zaidi.
Kwa mfano, mchezaji anapomaliza kucheza mchezo wa Carmageddon, yeye huwa amewagonga kwa gari na kuwaua watu 33,000. Maelezo ya mchezo mwingine kama huo yanasema: “Unaweza kusikia sauti fulani wakati watu wanapokanyagwa na magurudumu ya gari lako, damu yao hutapakaa kwenye kioo cha gari, nao hupiga magoti na kukuomba uwahurumie, au wanajiua. Ukipenda, unaweza pia kuwakata vipande-vipande.”
Je, michezo hiyo yenye jeuri ni hatari? Miradi 3,000 hivi ya uchunguzi imefanywa kuhusiana na suala hilo. Wengi wamesema kwamba michezo yenye jeuri huwafanya wachezaji kuwa wajeuri. Visa vya jeuri miongoni mwa vijana huonwa kuwa uthibitisho wa jambo hilo.
Wataalamu fulani wanatilia shaka athari za michezo hiyo, na wanasema kwamba mambo mengine yanahitaji kufikiriwa. Kwa mfano, wanasema kuwa huenda watoto ambao wana mielekeo ya kuwa wajeuri ndio wanaopenda kucheza michezo hiyo. Lakini, je, inawezekana kwamba michezo yenye jeuri inachangia sana jeuri? Si jambo la akili kusema kwamba watu hawawezi kuathiriwa na mambo wanayoona. Ikiwa hilo lingekuwa kweli, je, mashirika ya kibiashara yangetumia mabilioni ya dola kila mwaka kuonyesha matangazo ya biashara kwenye televisheni?
“Ustadi na Nia ya Kuua”
Mwanasaikolojia wa jeshi David Grossman, ambaye ni mwandishi wa kitabu On Killing, anasema kwamba jeuri ya michezo ya kompyuta huwazoeza watoto sawa na vile wanajeshi huzoezwa kushinda woga wao wa kuua. Kwa mfano, jeshi liligundua kwamba wanajeshi wengi walipata ujasiri wa kuua kwa kulenga risasi zao kwenye shabaha zilizochongwa kama wanadamu badala ya zile shabaha za kawaida zenye duara nyeusi katikati. Grossman anasema kwamba hivyo ndivyo michezo yenye jeuri inavyowafundisha watoto wawe na “ustadi na nia ya kuua.”
Kulingana na utafiti ulioripotiwa katika jarida la Journal of Personality and Social Psychology, huenda ikawa jeuri iliyo kwenye michezo ya video na ya kompyuta ni hatari kuliko jeuri inayoonyeshwa kwenye televisheni na sinema, kwani mchezaji hujiona kuwa kama wale wahusika wanaotekeleza matendo hayo ya jeuri. Watu hutazama matendo ya jeuri kwenye televisheni, lakini wanapocheza michezo ya kompyuta wao huhisi kana kwamba wanashiriki katika matendo hayo. Isitoshe, mtoto anaweza kutazama sinema kwa saa chache tu, lakini anaweza kutumia muda wa saa 100 kujifunza kucheza vizuri mchezo wa video.
Nchi fulani zimeweka masharti kuhusu michezo ya kompyuta ili kuhakikisha kwamba michezo yenye jeuri nyingi inachezwa na watu wazima tu. Hata hivyo, masharti hayo huwa na faida wakati tu yanapofuatwa. Uchunguzi mmoja huko Marekani ulionyesha kwamba asilimia 66 ya wazazi waliohojiwa hawakuelewa masharti hayo. Mkurugenzi wa kamati moja inayoweka masharti kuhusu burudani ya kompyuta anasema kwamba masharti hayo hayakusudiwi hasa kuwazuia watoto wasinunue michezo fulani. Anaeleza hivi: “Wajibu wetu si kuwachagulia watu mapendezi yao. Sisi huwawezesha wazazi kuamua kile wanachotaka au wasichotaka kwa ajili ya watoto wao.”
Je, Inawezekana Kuwa Mchezaji Sugu?
Michezo mipya ya Internet, ambayo mtu anaweza kucheza pamoja na watu wengine ulimwenguni pote, humwezesha kila mchezaji kuchagua kuwa mhusika fulani anayeweza kushinda vizuizi mbalimbali na hivyo kumfanya ahisi kuwa amefanikiwa. Mchezaji hutumia wakati mwingi sana katika michezo hiyo, na anapofaulu yeye hutamani kucheza tena na tena. Ni kana kwamba wengine ni wachezaji sugu—na labda hiyo ni sababu moja inayoweza kufanya michezo ya Internet iendelee kwa miezi mingi au hata kwa miaka.
Gazeti la Time liliripoti kwamba hivi karibuni watu wengi nchini Korea Kusini wamependa mchezo wa Internet unaoitwa Lineage. Mchezo huo huonyesha maisha ya zamani na wahusika hupigania ushindi. Mchezaji hupitia hatua mbalimbali, akijaribu kupata cheo. Vijana fulani hucheza mchezo huo usiku kucha na husinzia shuleni siku inayofuata. Wazazi huhangaikia jambo hilo lakini nyakati nyingine hawajui la kufanya. Mchezaji mmoja kijana alisema hivi alipohojiwa: “Ninapowasiliana na watu kwenye Internet wao hufikiri kwamba nina akili nyingi, lakini wanapokutana nami uso kwa uso wao hunishauri nipunguze uzito.”
Joonmo Kwon, ambaye ni mwanasaikolojia huko Korea, anaeleza sababu zinazofanya mchezo wa Lineage upendwe na watu wengi sana: “Huku Korea, mtu hapaswi kuonyesha wazi tamaa yake. Lakini mtu anapocheza mchezo huo, tamaa hiyo huonekana wazi.” Hivyo, vijana hujaribu kusahau matatizo ya maisha kwa kuingia katika ulimwengu wa kuwazia. Mchanganuzi mmoja wa habari mwenye utambuzi aliwafafanua wachezaji hao hivi: “Mchezaji huvutiwa na ulimwengu wa michezo ya kompyuta zaidi ya maisha halisi. Yeye huona maisha halisi kuwa nafasi tu ya kupata pesa chache ili kuendeleza mchezo wake.”
Madhara kwa Afya
Takwimu za Marekani zinaonyesha kwamba mwanafunzi wa darasa la sita hutumia saa nne kila siku kutazama televisheni—bila kuhesabu muda ambao anatumia kucheza michezo ya kompyuta au ya video. Katika uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1995, zaidi ya asilimia 60 ya watoto walikubali kwamba mara nyingi walicheza kupita kiasi. Hivyo, huenda masomo yakapuuzwa. Uchunguzi uliofanywa huko Japan ulionyesha kwamba michezo ya kompyuta huzoeza tu sehemu ndogo ya ubongo wa mtoto. Kulingana na uchunguzi huo, watoto wanahitaji mazoezi zaidi ya kusoma, kuandika, na kufanya hesabu. Lakini wanahitaji pia kucheza nje na watoto wengine na kuchangamana na wengine ili akili zao zikomae kabisa.
Inasemekana kwamba asilimia 40 hivi ya watoto huko Marekani wenye umri wa kati ya miaka mitano na miaka minane ni wanene kupita kiasi. Inawezekana kwamba kutofanya mazoezi kwa sababu ya kutumia wakati mwingi sana kutazama televisheni au kutumia kompyuta kumechangia tatizo hilo. Kampuni moja hata imebuni kifaa cha kufanyia mazoezi wakati wa kucheza michezo ya kompyuta. Hata hivyo, ingekuwa afadhali zaidi kupunguza muda wa kucheza michezo hiyo, ili kuwa na wakati wa kutosha kwa ajili ya shughuli nyingine zitakazomsaidia mtoto kukuza uwezo na utu wake kikamili.
Kuna tatizo lingine la afya: Kutazama skrini ya kompyuta kwa muda mrefu sana kunaweza kusababisha matatizo ya macho. Uchunguzi unaonyesha kwamba angalau asilimia 25 ya watu wanaotumia kompyuta wana matatizo ya macho. Sababu moja ni kwamba wanapotumia kompyuta wao hupepesa macho mara chache na hilo hufanya macho yawe makavu na yawashe. Kupepesa macho husafisha jicho kwa kutokeza machozi yanayoondoa uchafu.
Kwa kuwa watoto hawajijali sana, wanaweza kucheza michezo ya kompyuta kwa muda mrefu sana bila kupumzika. Hilo laweza kusababisha uchovu wa macho na kuyafanya yasione vizuri. Wataalamu wanadokeza kwamba inafaa kupumzika kidogo kwa dakika kadhaa baada ya kutumia kompyuta kwa saa moja.a
Biashara ya Ulimwenguni Pote Inayotia Fora
Inaonekana kwamba wapenzi wa michezo ya Internet wanaongezeka zaidi na zaidi ulimwenguni pote. Katika sehemu nyingi sana, vyumba vya kutumia Internet vinaanzishwa. Vyumba hivyo huwa na kompyuta kadhaa, na wateja hulipa pesa ili kucheza michezo ya Internet. Amini usiamini, vijana wengine hutumia dola 200 za Marekani kwa mwezi katika vyumba hivyo.
Ama kwa hakika, biashara ya michezo hiyo inatia fora. Inatazamiwa kuwa biashara hiyo itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 katika miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, ni wazi kwamba biashara hiyo yenye ufanisi ina ubaya wake. Hatari zipo. Sisi hatutaki kuhatarisha afya yetu, kutumia vibaya wakati na pesa nyingi, wala kuzoea jeuri na mauaji. Watoto wetu wanaweza kuathiriwa hata zaidi. Basi, haifai kusema kwamba michezo yote ya kompyuta ni burudani isiyodhuru na yenye kuelimisha. David Walsh, aliyenukuliwa mwanzoni, anasema: “Vyombo vya habari vina uvutano mkubwa sana.” Anaongeza hivi: “Ikiwa wazazi wana daraka la kuwatunza watoto wao, basi ni lazima utunzaji wao ubadilikane kadiri vyombo vya habari vinavyobadilika-badilika.”
Naam, kama vile Biblia inavyosema, “mandhari ya ulimwengu huu inabadilika.” (1 Wakorintho 7:31) Na yaonekana kwamba vyombo vya burudani vinabadilika haraka kuliko kitu kingine chochote. Wazazi wengi hushindwa kufuatia uvutano na mitindo inayobadilika-badilika ambayo inawaathiri watoto wao kila siku. Hata hivyo, usivunjike moyo. Wazazi wengi wanafanikiwa kuwalea watoto wao kwa kuwasaidia kukazia fikira mambo ya maana zaidi. Kama watu wazima, watoto pia wanahitaji kufahamu kwamba mahitaji yetu makubwa zaidi hayawezi kutoshelezwa na burudani—iwe ni kupitia kompyuta, televisheni, au vyombo vingine. Kama vile Yesu alivyosema pindi fulani, watu walio na furaha ya kweli ni wale “wenye kuona uhitaji wao wa kiroho.”—Mathayo 5:3.
[Maelezo ya Chini]
a Isitoshe, wengine wanapendekeza kwamba inafaa watu wote wanaotumia kompyuta wapumzishe macho baada ya kila dakika 15 kwa kutazama vitu vilivyo mbali. Wengine wanapendekeza watu wakae angalau sentimeta 60 kutoka kwenye skrini na kwamba wasitumie kompyuta wakiwa wamechoka.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Muhtasari wa Hatari za MICHEZO YA KOMPYUTA
▸ Kucheza michezo ya kompyuta na video yenye jeuri kwaweza kumchochea mtu awe mjeuri.
▸ Mtu anapocheza michezo ya kompyuta, hatazami tu jeuri; michezo hiyo imekusudiwa kumfanya ahisi kana kwamba anashiriki katika matendo ya jeuri.
▸ Michezo hiyo inaweza kuwazuia wale wanaoathiriwa kwa urahisi wasitambue tofauti kati ya mambo halisi na yale ya kuwaziwa.
▸ Mtu anapozoea kucheza michezo ya kompyuta anaweza kupuuza madaraka yake muhimu na watu anaowajali.
▸ Michezo ya kompyuta inaweza kuwamalizia watoto wakati mwingi ambao wangetumia kufanya mambo muhimu, kama vile kujifunza, kuchangamana na wengine, na kucheza michezo ya kuchemsha bongo.
▸ Kutazama skrini ya kompyuta kwa muda mrefu kwaweza kusababisha uchovu wa macho.
▸ Mtu anaweza kunenepa kupita kiasi kwa sababu ya kutofanya mazoezi, hali hiyo inaweza kusababishwa na kucheza michezo ya kompyuta.
▸ Michezo ya kompyuta inaweza kukupotezea wakati na pesa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Njia Moja ya Kushinda Zoea Hilo
Thomas, Mkristo mwenye umri wa miaka 23, anakumbuka hivi: “Nilipokuwa shuleni, sikufanya kazi za shule kwa sababu nilicheza michezo ya kompyuta. Baadaye, jambo hilo liliathiri mambo mengine. Hata nilipokuwa mhudumu wa kujitolea wa wakati wote niliendelea kucheza michezo hiyo. Hatimaye nilitambua kwamba ilikuwa ikinipotezea wakati mwingi na nguvu zangu. Nyakati nyingine nilipokuwa nimecheza kabla ya kwenda kuhubiri au kabla ya kuhudhuria mkutano wa Kikristo, nilishindwa kukaza fikira. Mara nyingi nilifikiria jinsi ambavyo ningeshinda kizuizi fulani katika mchezo wa kompyuta wakati ningerudi nyumbani. Nilipuuza funzo la kibinafsi na kusoma Biblia kwa ukawaida. Shangwe yangu ya kumtumikia Mungu ilianza kupungua.
“Nilipokuwa kitandani usiku mmoja, niliamua kwamba singeendelea kufanya hivyo. Niliamka, nikafungua kompyuta, kisha nikafuta michezo yote. Niliifuta kabisa! Haikuwa rahisi kufanya hivyo. Nilitambua kwamba nilipenda sana michezo hiyo. Lakini pia nilihisi vizuri niliposhinda pambano hilo kwani ilikuwa kwa faida yangu. Nakubali kwamba nimenunua michezo kadhaa tangu wakati huo. Lakini sasa nimejitia nidhamu sana. Nikishindwa kudhibiti tamaa yangu ya kucheza, mimi hufuta michezo hiyo tena.”
[Picha katika ukurasa wa 6]
Wengine wanasema kwamba michezo yenye jeuri huwafanya wachezaji kuwa wajeuri
[Picha katika ukurasa wa 7]
Chumba cha kuchezea michezo ya Internet huko Seoul, Korea
-