-
Kizazi Kilicho HatariniAmkeni!—2001 | Septemba 8
-
-
Kizazi Kilicho Hatarini
“Kufikia miezi miwili iliyopita, nilikuwa mwenye furaha na nilikuwa chapuchapu. Sasa, kila mara nipatapo nafasi ya kufanya kitu, mimi huhisi nimechoka sana. Sina raha na mimi hukasirika haraka, sifikiri mtu aweza kuvumilia kuwa pamoja nami. Sielewi ni kwa nini mimi huhisi vibaya ghafula.”—Paul.
“Mimi hulia na kuumia sana moyoni. Wakati ambapo sina maumivu hayo, mimi huhisi ni kana kwamba nimekufa ganzi. Sifurahii chochote. Sifurahii kuwa na marafiki wangu tena. Mimi hulala sana. Kwa siku nyingi siwezi kuamka ili kwenda shule na maksi zangu zimeshuka sana.”—Melanie.
HALI hiyo haiwakumbi tu Paul na Melanie. Uchunguzi waonyesha kwamba karibu asilimia 8 ya vijana waliobalehe nchini Marekani wamekumbwa na mshuko wa moyo wa aina fulani na kwamba kila mwaka karibu asilimia 4 ya vijana hao hushuka moyo sana. Lakini takwimu hizo hazionyeshi waziwazi jinsi hali ilivyo, kwani mara nyingi mshuko wa moyo hautambuliwi vyema au hupuuzwa kabisa. David G. Fassler, mwanasaikolojia wa masuala ya vijana waliobalehe, aandika hivi: “Kwa hakika, baada ya kupitia uchunguzi uliofanywa kuhusiana na watoto na matineja, nafikiri kwamba zaidi ya robo moja ya vijana watashuka moyo sana kwa kipindi fulani kabla ya kufikia umri wa miaka kumi na minane.”
Matokeo Yanayofadhaisha
Mshuko wa moyo huwafadhaisha matineja. Kwa kweli, wataalamu wanaamini kwamba kushuka moyo huchangia sana matatizo ya kula miongoni mwa vijana wanaobalehe, magonjwa yanayosababishwa na matatizo ya akili, matatizo shuleni, na kutumia dawa za kulevya.
La kusikitisha hata zaidi ni kwamba matineja hujiua kwa sababu ya kushuka moyo. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili, asilimia 7 ya vijana walioshuka moyo sana hujiua.a Hata takwimu hiyo haifunui waziwazi tatizo lenyewe, kwani yaaminika kwamba kati ya kila kijana anayejiua, wengine wengi huwa wamejaribu kufanya hivyo. Basi ndiyo sababu ripoti moja ya Baraza la Carnegie la Ustawi wa Vijana Wanaobalehe yasema hivi kwa kufaa: “Siku hizi kupuuza matatizo ya vijana wanaobalehe ni kusababisha msiba. Kupuuza mambo hivyo huhatarisha kizazi.”
Eti Hawajali?
Wengine hawaamini kwamba matineja wanaweza kushuka moyo. Huenda watu wazima fulani wakasema: ‘Wao ni watoto tu. Wao hawajali, na bila shaka hawana mahangaiko ambayo watu wazima wanayo.’ Au, wanayo? Ukweli ni kwamba vijana wanaobalehe hukabili mikazo mingi ambayo watu wazima wengi hawatambui. Dakt. Daniel Goleman asema hivi: “Tangu karne [ya 20] ilipoanza, kila kizazi ulimwenguni pote kimekabili hatari kubwa ya kushuka moyo sana maishani kuliko hatari ambayo wazazi wao walikabili. Si kuhuzunika tu, bali ni kulegea legelege, kuwa na majonzi, kujihurumia, na kukosa tumaini kabisa. Na vipindi hivyo vya kushuka moyo huanza wakiwa wachanga zaidi na zaidi.”
Hata hivyo, wazazi wengi waweza kupinga jambo hilo hivi: ‘Sisi tulipita kipindi cha kubalehe bila kushuka moyo. Mbona mtoto wetu ana majonzi mengi?’ Lakini watu wazima hawapaswi kulinganisha maisha ya vijana ya sasa na maisha yao wakati walipobalehe. Kwani, watu huona na kuitikia mambo yanayowazunguka kwa njia tofauti.
Isitoshe, matineja wa leo wanakabili kibarua kingine. “Wanakua katika ulimwengu ulio tofauti kabisa na ule ambao wazazi wao walikulia walipokuwa vijana,” aandika Dakt. Kathleen McCoy katika kitabu chake Understanding Your Teenager’s Depression. Baada ya kutaja baadhi ya mabadiliko makubwa yaliyotukia katika miongo ya karibuni, Dakt. McCoy amalizia hivi: “Matineja leo hawajihisi salama sana, hawajiamini sana na hawana tumaini sana kama tulivyohisi katika kizazi kilichopita.”
Kwa kuwa matineja wengi wameshuka moyo sana, makala zifuatazo zitazungumzia maswali matatu:
• Ni nini baadhi ya dalili zinazoonyesha kwamba tineja ameshuka moyo?
• Ni nini husababisha hali hiyo?
• Matineja walioshuka moyo waweza kusaidiwaje?
[Maelezo ya Chini]
a Wataalamu fulani wanaamini kwamba takwimu sahihi ya vijana wanaojiua ni kubwa zaidi, kwani vifo fulani vinavyosemwa kuwa vya aksidenti vyaweza kuwa ni visa vya kujiua.
-
-
Kutambua DaliliAmkeni!—2001 | Septemba 8
-
-
Kutambua Dalili
“Huzuni ni hisia ya kawaida na inayofaa; mshuko wa moyo ni ugonjwa. Tatizo ni kuelewa na kutambua tofauti.”—Dakt. David G. Fassler.
KAMA ilivyo na magonjwa mengine mengi, mshuko wa moyo una dalili zilizo wazi. Lakini si rahisi sana kutambua dalili hizo. Kwa nini? Kwa sababu karibu matineja wote huhuzunika mara kwa mara, kama watu wazima. Kuna tofauti gani kati ya kuhuzunika tu na kushuka moyo? Tofauti kubwa hasa yahusu kiwango na kipindi cha hali hiyo.
Kiwango huhusisha kadiri ambavyo kijana ameathiriwa na hisia za huzuni. Mshuko wa moyo ni ugonjwa mbaya sana wa kihisia-moyo ambao hudhoofisha uwezo wa tineja wa kufanya mambo kama kawaida, na huumiza sana kuliko kuvunjika moyo tu kwa muda mfupi. Dakt. Andrew Slaby afafanua maumivu ya hali hiyo hivi: “Hebu wazia maumivu makali zaidi uliyowahi kupata—mfupa uliovunjika, maumivu ya jino, au maumivu ya kujifungua—ongeza maumivu hayo mara kumi na ujifanye hujui kisababishi cha maumivu hayo; basi huenda ukajua kwa kadiri fulani maumivu ya kushuka moyo.”
Kipindi humaanisha muda wa kuwa katika hali hiyo ya kulegea kabisa. Kulingana na maprofesa wa tiba Leon Cytryn na Donald H. McKnew, Jr., “mtoto asiyechangamka au asiyerudia hali yake ya kawaida katika muda wa juma moja baada ya kuhuzunika (kwa sababu yoyote ile)—au katika muda wa miezi sita baada ya kupata hasara kubwa sana—anakabili hatari ya kupata ugonjwa wa mshuko wa moyo.”
Dalili za Kawaida
Kijana husemwa kuwa ameshuka moyo baada ya kuwa na dalili kadhaa kwa saa nyingi kila siku, kwa angalau majuma mawili. Kipindi kifupi cha kushuka moyo huitwa tukio la kushuka moyo (depressive episode). Aina fulani ya ugonjwa wa kushuka moyo ambao huendelea kwa muda mrefu zaidi, hubainishwa wakati dalili zaendelea kuonekana kwa angalau mwaka mmoja bila kuacha kwa zaidi ya miezi miwili. Katika visa vyote hivyo, ni zipi baadhi ya dalili za kawaida za kushuka moyo?a
Badiliko la ghafula la hisia na tabia. Tineja aliyekuwa mtiifu abadilika ghafula na kuwa mkali. Vijana walioshuka moyo kwa kawaida huasi au hata kutoroka nyumbani.
Kujitenga. Kijana aliyeshuka moyo hujitenga na rafikize. Au huenda ikawa kijana aliyeshuka moyo akahepwa na rafikize wanapotambua badiliko fulani lisilopendeza katika mtazamo na tabia yake.
Kutopendezwa sana na karibu mambo yote. Kwa kustaajabisha, tineja hawi chapuchapu. Mambo aliyopenda kufanya kwa furaha hivi majuzi, sasa yamchosha.
Badiliko la ulaji linaloonekana wazi. Wataalamu wengi huonelea kwamba matatizo ya kula kama kukosa hamu ya kula, kuwa na hamu nyingi ya kula isiyo ya kawaida, na kula kupita kiasi, huonekana katika kipindi cha (na huenda nyakati nyingine yakasababishwa na) mshuko wa moyo.
Matatizo ya kulala. Tineja hulala ama kwa muda mfupi sana au kwa muda mrefu sana. Wengine hupata matatizo ya kulala yasiyo ya kawaida. Wao hukesha usiku kucha kisha hulala mchana kutwa.
Matatizo shuleni. Kijana aliyeshuka moyo hapatani vyema na walimu na vijana wenzake, na maksi zake huanza kushuka. Punde si punde tineja hukataa katakata kwenda shuleni.
Kufanya mambo yanayomhatarisha. Kijana anapozoea kufanya mambo yanayomhatarisha, hiyo yaweza kuonyesha kwamba hataki kuishi. Kujikatakata (kama vile kujikatakata ngozini) kwaweza kuwa dalili.
Kujihisi hafai au kujilaumu isivyofaa. Tineja ajichambua isivyofaa na kuhisi kuwa hawezi kufaulu maishani, hata ikiwa jambo hilo si kweli.
Shida zinazotokana na matatizo ya akili. Wakati kisababishi cha matatizo kama maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, maumivu ya tumbo, na maumivu mengine hakipatikani mwilini, hiyo yaweza kuwa dalili ya kushuka moyo.
Kufikiria mara kwa mara kuhusu kifo au kujiua. Kuzungumza sana kuhusu mambo yanayoogopesha kwaweza kuwa dalili ya kushuka moyo. Ndivyo ilivyo pia na vitisho vya kujiua.—Ona sanduku lililo chini.
Ugonjwa wa Hisia Zinazobadilika-badilika
Ugonjwa mwingine unaotatanisha huwa na baadhi ya dalili hizohizo—ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika. Kulingana na Dakt. Barbara D. Ingersoll na Dakt. Sam Goldstein, ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika (unaoitwa pia manic-depressive disorder) ni ‘hali inayotambuliwa kwa matukio ya kushuka moyo yanayofuatwa na vipindi vya kusisimuka kupita kiasi na kupata nguvu nyingi sana. Kusisimuka huko huzidi hali ya kawaida ya kuchangamka.’
Hali hiyo isiyo ya kawaida huitwa mania. Dalili zake zatia ndani kuruka ghafula kutoka wazo moja hadi lingine, kuzungumza kupita kiasi, na kutokuwa na usingizi. Kwa hakika, mgonjwa aweza kukosa usingizi kwa siku nyingi bila kuonyesha dalili zozote za uchovu. Dalili nyingine ya ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika ni tabia ya kufanya mambo hima-hima bila kufikiria matokeo. Ripoti moja ya Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili yasema hivi: “Mara nyingi hali hiyo ya mania huathiri fikira, maamuzi, na njia ya kushughulika na wengine na hivyo kutokeza matatizo makubwa na aibu.” Hali hiyo hudumu kwa muda gani? Nyakati nyingine kwa siku chache tu; katika visa vingine, hali hiyo hudumu kwa miezi kadhaa kabla ya ugonjwa wa mshuko wa moyo kuanza.
Wale wanaokabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo watia ndani watu wenye washiriki wa familia walio na ugonjwa huo. Jambo la kupendeza ni kwamba kuna tumaini kwa watu wanaougua ugonjwa huo. Kitabu The Bipolar Child chasema hivi: “Ugonjwa huo unapobainishwa mapema na kutibiwa vizuri, watoto hao na familia zao waweza kuishi maisha mazuri sana yaliyotulia zaidi.”
Ni muhimu kung’amua kwamba dalili moja tu haitoshi kuonyesha kwamba mtu ameshuka moyo au ana ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika. Mara nyingi, mshuko wa moyo hubainishwa baada ya dalili nyingi kuonekana katika kipindi fulani cha wakati. Hata hivyo, bado kuna swali, Kwa nini matineja hukumbwa na tatizo hili linalotatanisha?
[Maelezo ya Chini]
a Dalili zinazoonyeshwa hapa zakusudiwa kuandaa muhtasari tu wala si kuandaa njia ya kubainisha mshuko wa moyo.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Mtoto Anapotaka Kufa
Kwa mujibu wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti Magonjwa, katika mwaka mmoja hivi karibuni, idadi ya vijana waliojiua ilizidi jumla ya idadi ya wale waliokufa kutokana na kansa, ugonjwa wa moyo, UKIMWI, kasoro za maumbile, kiharusi, homa ya vichomi, mafua makali, na ugonjwa wa kudumu wa mapafu. Jambo jingine linalosikitisha ni kwamba: Visa vya kujiua vilivyoripotiwa vya watu walio kati ya umri wa miaka 10 na 14 vimeongezeka sana.
Je, vijana wanaobalehe wanaweza kuzuiwa wasijiue? Ndiyo, katika hali fulani. “Takwimu zaonyesha kwamba visa vingi vya kujiua huanza kwa majaribio au maneno na maonyo yanayodokeza kujiua,” aandika Dakt. Kathleen McCoy. “Tineja wako anapodokeza tu kwamba anafikiria kujiua, huo ni wakati wa kulizingatia jambo hilo na hata labda kutafuta msaada wa wataalamu.”
Kuongezeka kwa matineja wanaoshuka moyo huonyesha wazi uhitaji wa wazazi na watu wengine wazima kuchukua kwa uzito mambo yoyote yanayodokeza kwamba kijana ataka kujiua. “Katika karibu visa vyote vya kujiua nilivyopata kuchunguza, ishara zozote zilizoonyesha mipango ya kijana zilipuuzwa au hazikutiliwa maanani,” aandika Dakt. Andrew Slaby katika kitabu chake No One Saw My Pain. “Washiriki wa familia na marafiki hawakuelewa uzito wa mabadiliko waliyokuwa wakiona katika kijana. Walikazia fikira matokeo badala ya tatizo lenyewe, hivi kwamba wakakata kauli kwamba tatizo lilikuwa ‘matatizo ya familia’ au ‘kutumia dawa za kulevya’ au ‘kukosa hamu ya kula.’ Nyakati nyingine, badala ya kutibu mshuko wa moyo, jambo lililoshughulikiwa hasa ni ile hali ya kukasirika, kuchanganyikiwa, na kuudhika upesi. Tatizo lenyewe liliendelea kusababisha mateso na uchungu.”
Ujumbe u wazi: Chukua kwa uzito ishara zozote zinazodokeza nia ya kujiua!
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyakati nyingine, uasi ni ishara ya kushuka moyo
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mara nyingi, matineja walioshuka moyo hawapendezwi tena na mambo yaliyowafurahisha zamani
-
-
Kutambua VyanzoAmkeni!—2001 | Septemba 8
-
-
Kutambua Vyanzo
“Kwa kawaida, kushuka moyo kwa matineja hakusababishwi tu na jambo moja bali husababishwa na mikazo mingi.” —Dakt. Kathleen McCoy.
NI NINI huwafanya matineja washuke moyo? Mambo mengi yahusika. Kwanza kabisa, mabadiliko ya kimwili na ya kihisia-moyo yanayotokea vijana wanapobalehe yaweza kuwafanya wababaike na kuogopa sana, na kuwafanya watazamie mabaya. Vilevile, mara nyingi ni rahisi matineja kuhisi vibaya wanapoona kwamba wamekataliwa na rafiki zao au mtu waliyempenda kimahaba. Pia, kama ilivyoonyeshwa katika makala yetu ya kwanza, matineja wa sasa wanakua katika ulimwengu unaoweza kusababisha mshuko wa moyo. Kwa hakika, twaishi katika “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.”—2 Timotheo 3:1.
Isitoshe, vijana wanapata misongo ya maisha kwa mara ya kwanza kabisa, na hawana stadi wala ujuzi kama watu wazima. Hivyo, mara nyingi matineja huwa kama watalii wanaotafuta njia kwenye eneo wasilofahamiana nalo—wanafadhaishwa na hali hiyo na, kama inavyokuwa mara nyingi, hawataki kuomba msaada. Hali hizo zaweza kusababisha mshuko wa moyo.
Lakini kuna sababu nyingine kadhaa zinazoweza kuwafanya matineja washuke moyo. Acheni tuchunguze baadhi ya sababu hizo.
Mshuko wa Moyo na Hasara
Nyakati nyingine mshuko wa moyo hutokea baada ya kupata hasara kubwa—labda kifo cha mpendwa au kutenganishwa na mzazi kupitia talaka. Katika nchi fulani, hata kifo cha mnyama aliyependwa chaweza kumfadhaisha sana tineja.
Kuna hasara nyingine zisizotambuliwa wazi. Kwa mfano, mtu anapohamia eneo lingine yeye huacha mazingira aliyokuwa amezoea na rafiki wapendwa. Hata mtu anapofikia mradi ambao alitazamia kwa muda mrefu—kama vile kumaliza shule—aweza kuhisi kwamba amepata hasara. Kwani, anapoanza maisha mapya yeye hupoteza starehe na usalama aliofurahia hapo zamani. Kisha, kuna vijana wanaovumilia ugonjwa fulani wa kudumu. Katika hali kama hiyo, tineja anapofadhaika kwa sababu ya kuwa tofauti na rafikize—labda hata kupuuzwa nao—aweza kuhisi kwamba yeye si timamu.
Ni kweli kwamba vijana wengi hupata hasara kama hizo bila kufadhaika sana. Wao huhuzunika, hulia, husikitika, na kuomboleza—lakini baada ya muda wanazoea hali hiyo. Hata hivyo, mbona matineja wengine hushuka moyo, ilhali wengi hukabiliana na mikazo ya maisha kwa urahisi? Jibu kwa swali hilo lahusisha mambo mengi, kwa kuwa mshuko wa moyo ni ugonjwa tata. Lakini vijana wengine waweza kuathiriwa kwa urahisi zaidi.
Uhusiano na Utendaji wa Kemikali Mwilini
Wataalamu wengi wa masuala ya akili huamini kwamba kuvurugika kwa utendaji wa kemikali ubongoni huchangia sana mshuko wa moyo.a Mvurugo huo waweza kupitishwa katika chembe za urithi, kwa kuwa wachunguzi wamegundua kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa matineja walio na mzazi aliyeshuka moyo watapatwa na hali hiyo. “Mara nyingi watoto walioshuka moyo huwa na angalau mzazi mmoja aliyeshuka moyo,” chasema kitabu Lonely, Sad and Angry.
Jambo hilo lazusha swali hili, Je, kweli watoto hurithi mshuko wa moyo, au wao hujifunza kushuka moyo wanapoishi na mzazi mwenye ugonjwa huo? Ni vigumu kujibu swali hilo, kwani ubongo ni tata sana. Ndivyo ilivyo pia kuhusu mambo mengine ambayo yanaweza kuwafanya matineja washuke moyo.
Mshuko wa Moyo na Mazingira ya Familia
Kwa kufaa, mshuko wa moyo umetajwa kuwa suala la kifamilia. Kama ilivyokwisha kutajwa, kuna kitu fulani katika chembe za urithi ambacho hupitisha uwezekano wa kushuka moyo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Lakini mazingira ya familia huchangia pia. “Watoto wanaotendwa vibaya na wazazi wao wanaelekea zaidi kushuka moyo,” aandika Dakt. Mark S. Gold. “Ndivyo ilivyo pia kwa watoto ambao wazazi wao huwachambua kupita kiasi na kukazia kasoro zao.” Kushuka moyo kwaweza kutokea wazazi wanapomchunga na kumzuia mtoto kupita kiasi. Hata hivyo, kwa kustaajabisha, mchunguzi mmoja aligundua kwamba watoto hushuka moyo zaidi wanapopuuzwa tu na wazazi.
Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba matineja wote walioshuka moyo wamepata ugonjwa huo kwa sababu ya malezi mabaya. Kukata shauri hivyo kungekuwa kupuuza mambo mengineyo yanayoweza kuchangia tatizo hilo. Hata hivyo, katika visa fulani mazingira ya familia ni sababu kubwa inayochangia hali hiyo. “Watoto wanaoishi katika nyumba ambazo wazazi huzozana kila mara wanaelekea zaidi kushuka moyo kuliko watoto walio katika mazingira matulivu,” aandika Dakt. David G. Fassler. “Sababu moja ni kwamba wazazi wanaozozana hujihusisha sana katika migogoro yao hivi kwamba wanapuuza mahitaji ya watoto wao. Sababu nyingine ni kwamba wazazi hao hugombana kuhusu watoto wao, jambo linaloweza kuwafanya vijana wajilaumu, wakasirike, na kuudhika.”
Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoweza kusababisha matineja washuke moyo. Kuna mengine. Kwa mfano, wataalamu fulani wasema kwamba sababu za kimazingira (kama kukosa lishe bora, vichafuzi vyenye sumu, na utumiaji wa dawa za kulevya) zaweza kusababisha mshuko wa moyo. Wengine wadokeza kwamba dawa fulani (kama dawa fulani za kupunguza kemikali ya histamini na za kutuliza wasiwasi) zaweza pia kusababisha mshuko wa moyo. Pia, yaonekana kwamba watoto wenye kasoro za kujifunza wanaweza kushuka moyo kwa urahisi, labda kwa sababu pole kwa pole wanaacha kujiamini wanapotambua kwamba hawawezi kuwa sawa na wanadarasa wenzao.
Hata hivyo, haidhuru sababu ya kushuka moyo, ni muhimu kufikiria swali hili, Matineja walioshuka moyo waweza kusaidiwaje?
[Maelezo ya Chini]
a Wengine hufikiri kwamba japo watu fulani walioshuka moyo huzaliwa na mvurugo huo wa kikemikali, wengine huzaliwa wakiwa na afya njema kisha jambo la kufadhaisha hubadili utendaji wa kemikali ubongoni na kufanya iwe rahisi kwao kushuka moyo.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mara nyingi mizozo ya familia huchangia sana mshuko wa moyo
-
-
Namna Uwezavyo KusaidiaAmkeni!—2001 | Septemba 8
-
-
Namna Uwezavyo Kusaidia
“Watoto walioshuka moyo wanahitaji msaada. Lakini watoto hawawezi kujitafutia msaada. Ni lazima kwanza mtu mzima atambue tatizo hilo na kulichukua kwa uzito. Hilo ndilo jambo gumu.”—Dakt. Mark S. Gold.
WAWEZA kufanya nini ukishuku kwamba tineja wako ameshuka moyo? Kwanza, usikate kauli mara moja kuhusu jambo hilo. Kwani, dalili unazoona zaweza kuwa ni za tatizo lingine.a Na zaidi, vijana wote huhuzunika pindi kwa pindi. Lakini iwapo hali hiyo yaendelea na yaonekana kuwa ni tatizo kubwa zaidi ya kule kuhuzunika kwa kawaida, itakuwa vema kumwona daktari. Kwa habari hii, yafaa kukumbuka maneno ya Yesu: “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali wenye kuugua wahitaji.”—Mathayo 9:12.
Mtajie daktari wako waziwazi habari zozote zitakazosaidia, kutia ndani mabadiliko yoyote ya hivi karibuni katika maisha ya tineja huyo ambayo huenda yanamfanya alegee. Hakikisha kwamba daktari amesikiliza dalili zenyewe kwa muda mrefu vya kutosha kabla ya kubainisha ugonjwa. Dakt. David G. Fassler aonya hivi: “Haiwezekani kukusanya habari zote zinazohitajiwa ili kutambua ugonjwa wa mtoto katika kipindi kimoja cha dakika ishirini tu.”
Muulize daktari maswali yoyote uliyo nayo waziwazi. Kwa mfano, iwapo daktari akuambia kwamba tineja wako ameshuka moyo sana, huenda ukataka kuuliza ni kwa nini anafikiri hivyo wala si vinginevyo. Iwapo unashuku uchunguzi wa daktari, mwambie ungependa kupata maoni ya mtaalamu mwingine. Kwa wazi, daktari yeyote mnyoofu na mwaminifu hatakupinga usifanye hivyo.
Kukubali na Kukabili Hali Yenyewe
Kwa hakika, iwapo tineja wako ameshuka moyo sana, usiaibike eti kwa sababu ana ugonjwa huo. Ukweli ni kwamba vijana wazuri sana waweza kushuka moyo. Kwa kweli, Biblia huonyesha kwamba watu fulani waliojitahidi sana kumtumikia Mungu waliumia kihisia, haidhuru umri wao. Fikiria mfano wa Yobu mwaminifu, aliyehisi kwamba Mungu alikuwa amemwacha na akachukia kuishi. (Ayubu 10:1; 29:2, 4, 5) Hana alikuwa mtumishi wa Mungu aliyekuwa na “uchungu rohoni mwake” hivi kwamba hakuweza kula. (1 Samweli 1:4-10) Kisha kuna yule mtumishi wa Mungu, Yakobo, aliyeomboleza kwa siku nyingi baada ya kifo cha mwanaye na “akakataa kutulizwa.” Kwani, hata Yakobo alisema jinsi alivyotamani kujiunga na mwanaye kaburini! (Mwanzo 37:33-35) Kwa hiyo, mfadhaiko hausababishwi sikuzote na udhaifu wa kiroho.
Hata hivyo, tineja anaposhuka moyo wazazi waweza kuteseka sana. “Lazima niwe mwangalifu sana nisimuumize hisia,” asema mama ya tineja aliyeshuka moyo. “Nina wasiwasi, ninaogopa, ninakuwa mkatili, ninakasirika na kuchoka.” Mwingine akiri hivi: “Nilipoenda madukani na kumwona mama akinunua vitu pamoja na bintiye tineja nilivunjika moyo kwa kuwa nilihisi kwamba singeweza kufanya hivyo pamoja na [binti yangu] tena kamwe.”
Kuhisi hivyo ni kawaida. Hata hivyo, nyakati nyingine hisia hizo zaweza kuvunja moyo sana. Hilo litukiapo, mbona usizungumze na rafiki unayemwamini? Mithali 17:17 husema: “Rafiki hupenda sikuzote; na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.” Vilevile, usisahau kusali. Biblia hutuhakikishia kwamba tukimtwika Mungu mzigo wetu, atatutegemeza.—Zaburi 55:22.
Kulaumu-laumu
Wazazi wengi wa matineja walioshuka moyo huvunjika moyo sana na kuhisi kwamba walichangia hali hiyo kwa njia fulani. Mzazi mmoja akiri hivi: “Mtoto wako anaposhuka moyo, unajilaumu na hakuna awezaye kubadili maoni yako. Kila mara unajiuliza, ‘Tulikosea wapi? Tatizo lilianzia wapi? Mimi nilichangiaje tatizo hilo?’” Wazazi wanawezaje kufikiri ifaavyo wanapokabili hali hiyo?
Hapana shaka kwamba uhasama nyumbani waweza kumwathiri mtoto vibaya sana. Kwa kufaa, Biblia huwashauri akina baba hivi: “Msiwe mkichochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo.” (Wakolosai 3:21) Hivyo basi, wazazi wapaswa kuchunguza jinsi wanavyoshughulika na watoto wao na kufanya marekebisho yahitajiwayo. Hata hivyo, kushuka moyo hakusababishwi kila mara na malezi mabaya. Kwa kweli, ugonjwa huo waweza kuwakumba hata wale walio katika nyumba zenye upendo mwingi. Kwa hiyo, wazazi wanaojitahidi wawezavyo kuwasaidia watoto wao, hawapaswi kujilaumu.
Vivyo hivyo, ni jambo la maana kutomlaumu tineja aliyeshuka moyo. Kwani, yamkini yeye hawezi kuudhibiti ugonjwa huo. “Singemlaumu kamwe kwa kuugua tetekuwanga na homa ya vichomi,” asema mama mmoja. “Lakini aliposhuka moyo nilimlaumu,” yeye akiri. “Nilimlaumu mtoto wangu kwa kuwa mgonjwa—hilo lanifanya nijihisi vibaya sana.” Wazazi wanapoona mshuko wa moyo kuwa ugonjwa badala ya udhaifu, hiyo itawasaidia wao na wengine kukazia fikira jinsi wawezavyo kumtegemeza mgonjwa.
Kumlea tineja aliyeshuka moyo kwaweza kutokeza mikazo mingi katika uhusiano wa wazazi. Mke mmoja asema hivi: “Tulilaumiana, hasa tulipofikiria kuhusu maisha tuliyokuwa tumetarajia kuishi na maisha tuliyoishi kwa sababu ya hali ya mwana wetu.” Tim, aliye na binti aliyeshuka moyo, akiri hivi: “Ni rahisi kumlaumu mwenzi wako. Endapo wazazi wana matatizo ya ndoa kabla mtoto hajaanza kuonyesha dalili za kushuka moyo, vitabia vya kiajabu-ajabu vya mtoto vyaweza kusababisha ndoa kuvunjika.” Usiruhusu mshuko wa moyo wa mtoto uvunje ndoa yenu! Kwa hakika, hakuna faida yoyote ya kulaumu-laumu—iwe ni kujilaumu, kumlaumu mtoto wako, au mwenzi wako. Jambo la maana ni kumtegemeza mgonjwa.
Kuandaa Utegemezo
Biblia yawashauri Wakristo hivi: “Semeni kwa kuliwaza nafsi zilizoshuka moyo.” (1 Wathesalonike 5:14) Iwapo kijana aliyeshuka moyo anaona kwamba hafai, unaweza kusaidia. Vipi? Bila shaka, si kwa kukata shauri mara moja hivi, “Hupaswi kuhisi hivyo” au, “Hupaswi kuwa na mtazamo huo.” Badala yake, jitahidi kuwa mwenye huruma kwa kuonyesha “hisia-mwenzi.” (1 Petro 3:8) Paulo aliwashauri Wakristo ‘watoe machozi pamoja na watu watoao machozi.’ (Waroma 12:15) Kumbuka kwamba mtu aliyeshuka moyo kabisa huumia kikweli. Maumivu yake si ya kujitungia, wala hajifanyi tu ili wengine wampe uangalifu. Baada ya kusikiliza, jaribu kumfanya mgonjwa ajieleze waziwazi. Muulize ni kwa nini anahisi hivyo. Kisha, msaidie tineja kwa upole na kwa subira aone ni kwa nini hapaswi kujiona kuwa hafai. Kumhakikishia juu ya upendo na rehema ya Mungu kutasaidia kupunguza mahangaiko ya mgonjwa.—1 Petro 5:6, 7.
Kuna mambo mengine unayoweza kufanya. Kwa mfano, huenda ikafaa uhakikishe kwamba tineja wako aliyeshuka moyo anapumzika, anakula, na kufanya mazoezi ya kutosha. (Mhubiri 4:6) Ikiwa daktari ampendekezea dawa fulani, ni jambo la hekima kumwonyesha tineja umuhimu wa kutumia dawa hizo. Usikate tamaa kamwe unapomtegemeza, na usiache kumpenda.
Pasipo shaka, tineja anaposhuka moyo, yeye na washiriki wengine wa familia hufadhaika. Mwishowe, sifa za subira, uvumilivu, na upendo zitakuwa msingi wa kuwasaidia matineja walioshuka moyo.
[Maelezo ya Chini]
a Yasemekana kwamba magonjwa fulani—kutia ndani ongezeko lisilo la kawaida la chembe nyeupe za damu zenye kiini kimoja, ugonjwa wa sukari, upungufu wa damu, ugonjwa wa tezi ya koromeo, na kiwango cha chini cha sukari katika damu kuliko kawaida—yaweza kutokeza dalili zinazofanana na za kushuka moyo.
[Blabu katika ukurasa wa 11]
Mtu aliyeshuka moyo kabisa huumia sana. Maumivu si ya kujitungia
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
IWAPO WEWE NI TINEJA ALIYESHUKA MOYO
Kuna watu wanaoweza kukusaidia, na una matumaini. Huenda umeshuka moyo kwa sababu ya (1) mvurugiko wa utendaji wa kemikali mwilini au (2) hali za maisha ambazo huwezi kuzidhibiti. Vyovyote vile, si wewe uliyejiletea hali hiyo. Hata hivyo, wapaswa kufanya nini kuhusu hali hiyo?
Biblia husema kwamba “yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.” (Mithali 18:24) Mbona usitafute rafiki kama huyo na umweleze jinsi unavyohisi? Mzazi wako mmoja au mtu mwingine aliyekomaa aweza kuwa rafiki yako mkubwa unapopambana na mshuko wa moyo.
Wazazi wako wakishuku kwamba umeshuka moyo sana, huenda wakakupeleka kwa daktari aliye na ujuzi wa kutibu ugonjwa huo. Hilo ni jambo la hekima, kwani mara nyingi mshuko wa moyo waweza kupunguzwa sana kwa matibabu, mahala inapowezekana. Kwa mfano, iwapo kuna mvurugiko katika utendaji wa kemikali mwilini, dawa ya kupunguza mshuko wa moyo yaweza kupendekezwa. Iwapo una tatizo hilo, usione haya kutumia dawa. Dawa hiyo husaidia kiwango cha kemikali mwilini mwako kirudie tu hali ya kawaida, na hiyo yaweza kuwa njia ya kukusaidia kupata shangwe na nguvu maishani mwako.
Watu wengi walioshuka moyo wamefarijika kwa kusoma Biblia na kumkaribia Mungu kupitia sala. Biblia yatuhakikishia hivi: “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa.”b—Zaburi 34:18.
[Maelezo ya Chini]
b Kwa habari zaidi, ona makala “Vijana Huuliza . . . Je, Nimwambie Mtu Fulani Kwamba Nimeshuka Moyo?” katika gazeti la Amkeni! la Oktoba 22, 2000.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
MSAADA NA TUMAINI KWA WALIOSHUKA MOYO
Kwa kuwa kushuka moyo ni suala tata, mfululizo huu mfupi wa makala haungeweza kuzungumzia mambo yote kuhusu ugonjwa huo. Hata hivyo, wachapishaji wa gazeti la Amkeni! wana uhakika kwamba hoja zilizotajwa zaweza kuwasaidia matineja na wazazi wao kuvumilia ugonjwa huo unaofadhaisha.
Huenda umetambua kwamba mawaidha mengi yaliyotolewa katika makala iliyotangulia yalitegemea Biblia. Kwa kweli, hicho ni kitabu cha kale. Hata hivyo, shauri lake latumika leo sawa na lilivyotumika ilipoandikwa. Kwa nini? Kwa sababu, japo hali zimebadilika, wanadamu hawajabadilika. Twakabili mambo yale yale ya msingi ambayo vizazi vilivyopita vilikabili. Tofauti ni kwamba sasa matatizo hayo ni mengi na yameenea sana.
Hata hivyo, kuna sababu nyingine inayofanya Biblia iweze kutumika sana: Imepuliziwa na Mungu. (2 Timotheo 3:16) Akiwa Muumba wetu, yeye ajua tunachohitaji ili kufurahia maisha kabisa.
Bila shaka, Biblia si kitabu cha kitiba. Hivyo, haituondolei uhitaji wa kutafuta matibabu yanayofaa kwa magonjwa, kama vile mshuko wa moyo. Hata hivyo, Biblia ina kanuni zinazoweza kutusaidia kuwafariji wanaougua. Zaidi ya hayo, ina ahadi ya Mungu kwamba hivi karibuni atatuponya magonjwa yetu yote. (Zaburi 103:3) Naam, Yehova akusudia “kuifufua mioyo yao waliotubu [“wanaopondwa,” NW].”—Isaya 57:15.
Je, wataka kujifunza zaidi kuhusu tumaini hilo tukufu? Tafadhali wasiliana na Mashahidi wa Yehova walio karibu nawe au uwaandikie kwa kutumia anwani ifaayo iliyoorodheshwa katika ukurasa wa 5 wa gazeti hili.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Jitahidi kuonyesha hisia-mwenzi
[Picha katika ukurasa wa 11]
Iwapo tineja aendelea kushuka moyo, ni jambo la hekima kumwona daktari
[Picha katika ukurasa wa 12]
Ukiwa mzazi, usifanye haraka kujilaumu, kumlaumu mwenzi wako, au tineja wako
-