Tunda Lililokatazwa Katika Edeni Lilikuwa Nini?
MITI yote ya matunda ya Edeni ilikuwako ili mwanadamu ale kutokana nayo mpaka ‘atosheke.’ (Mwanzo 2:16, NW) Lakini binadamu hao wawili walikatazwa kula kutokana na mti mmoja, ule wa “ujuzi wa mema na mabaya.” Hawa alinukuu katazo la Yehova alilopewa na mume wake kuwa likitia ndani hata ‘kuugusa’ mti huo, adhabu ya kifo ikiwa tokeo la kutostahi na kuvunja sheria hiyo ya kimungu. (Mwanzo 2:17; 3:3) Mafundisho ya kimapokeo yamejaribu kulifafanua tunda hilo lililokatazwa katika njia mbalimbali: kuwa ufananisho wa uhusiano wa kingono, unaowakilishwa na “tofaa”; kuwa likisimamia ujuzi tu wa mema na mabaya; na kuwa ni maarifa yanayopatikana wakati wa kufikia ukomavu na pia kupitia mambo yanayoonwa, maarifa ambayo yaweza kutumiwa vibaya au vizuri. Hata hivyo, ni lazima uhusiano wa kingono uondolewe mbali kuwa jambo lililowakilishwa na tunda la mti huo kwa sababu amri ya Muumba husema, “Zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi” (Mwanzo 1:28), kwani kuzaa na kuongezeka kungeweza kutimizwa katika njia gani nyingine? Uwezo tu wa kutambua mema na mabaya kwa hakika hauwezi kumaanishwa, kwani kutii amri ya Mungu kulihitaji mwanadamu asiye na dhambi aweze kufanya upambanuzi huo wa kiadili. Wala hauwezi kumaanisha maarifa yanayopatikana wakati wa kufikia ukomavu, kwani kufikia hali hiyo si dhambi kwa upande wa mwanadamu, wala kulingana na kufikiri kuzuri Muumba wake asingemwajibisha abaki katika hali ya kutokomaa.
Kwa habari ya aina ya mti huo, rekodi ya Kimaandiko haisemi lolote. Lakini yawa wazi kwamba mti wa ujuzi wa mema na mabaya ulifananisha haki au mamlaka ya kimungu, inayoshikiliwa na Muumba wa mwanadamu, ya kuagiza viumbe wake yaliyo “mema” na yaliyo “mabaya,” kisha kuwataka kwa kufaa wazoee yale yanayotangazwa rasmi kuwa mema na kuepuka yale yanayotamkwa kuwa mabaya ili kubaki katika hali ya kukubaliwa na Mungu akiwa Mtawala Mwenye Enzi Kuu. Katazo na pia tamko la baadaye la hukumu iliyotolewa kwa watu hao wawili wasiotii hukazia uhakika wa kwamba tendo la kutotii kwa kula tunda lililokatazwa ndilo lililofanyiza dhambi ya kwanza.—Mwanzo 3:3.
Ingawa wachambuzi wengine wa ki-siku-hizi huenda wakakataa usahili wa usimulizi wa Kiedeni, yapasa iwe wazi kwamba hali zilizokuwako hasa zilifanya mtihani sahili ufae kabisa. Maisha ya mwanamume na mwanamke waliotoka tu kuumbwa yalikuwa sahili, bila kutatanika na kulemezwa na matatizo magumu, mashaka, na mahangaiko ambayo kutotii Mungu kumeletea jamii ya kibinadamu tangu wakati huo. Hata hivyo, kwa usahili wao wote, mtihani huo kwa ufupi na kwa kufaa unaonyesha ukweli wa ulimwengu wote mzima wa enzi kuu ya Mungu pamoja na utegemeaji Mungu wa mwanadamu na wajibu wake kumwelekea Mungu. Na ni lazima isemwe kwamba, ingawa ni sahili, usimulizi wa matukio ya Edeni unatokeza mambo kwenye kiwango cha juu zaidi ya zile nadharia zinazoweka mwanzo wa mwanadamu, si katika shamba, bali katika pango, zikimwakilisha akiwa mwenye kukosa maarifa kabisa na pia akiwa bila uwezo wa kupambanua mema na mabaya. Usahili wa mtihani katika Edeni unaonyesha kanuni iliyotaarifiwa mamileani mengi baadaye na Mwana wa Mungu, kwamba “aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.”—Luka 16:10.
Hata hivyo, kuwa na mti huo uliokatazwa katika shamba la Edeni kwa wazi hakukukusudiwa kuwe tatizo kwa binadamu hao wawili, wala agizo hilo halikutolewa ili kutokeza suala, au kutumika kuwa habari ya mjadala. Kama Adamu na Hawa wangalikubali mapenzi ya Mungu katika jambo hilo na kuheshimu maagizo yake, makao yao ya shambani yangaliendelea bila kuharibiwa yakiwa mahali pa furaha na pa kupendeza. Rekodi inaonyesha kwamba Adui ya Mungu alisukumia ainabinadamu suala na mjadala juu ya mti huo, pamoja na kishawishi cha kuvunja amri ya Mungu. (Mwanzo 3:1-6; linganisha Ufunuo 12:9.) Kutumia kwa Adamu na Hawa hiari yao, wakiwa viumbe wenye hiari ya kuchagua, katika kuasi enzi kuu ya Mungu iliyo halali kuliongoza kwenye kupoteza kwao Paradiso na hali yenye kubarikiwa ya mipaka yayo. La maana hata zaidi, walipoteza nafasi ya kula kutokana na mwingine wa miti ya Edeni, huo ukiwakilisha haki ya uhai wa milele. Hivyo usimulizi wasema kwamba Yehova “akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.”—Mwanzo 3:22-24.