Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Uzawa wa Mtoto Ulio Mkuu Zaidi Duniani Watangulia Usalama Ulimwenguni Pote
    Mnara wa Mlinzi—1987 | Aprili 1
    • Uzawa wa Mtoto Ulio Mkuu Zaidi Duniani Watangulia Usalama Ulimwenguni Pote

      “Kwa maana kuna mtoto ambaye amezaliwa kwetu, kuna mwana ambaye tumepewa; na utawala wa mwana mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani.​—Isaya 9:6, NW

      1. Usalama ulimwenguni pote ni hakika chini ya nani, na tunajuaje hilo?

      USALAMA ulimwenguni pote! Chini ya “Mwana Mfalme wa ulimwengu huu,” Shetani Ibilisi, ni ndoto isiyowezekana. (Yohana 12:31, The New English Bible) Lakini usalama ulimwenguni pote chini ya “Mwana Mfalme wa Amani,” Yesu Kristo, ni hakika kabisa. Yehova anatuhakikishia jambo hilo katika unabii unaohusu kuzaliwa na kazi ya “Mwana Mfalme wa Amani.” Tunasoma hivi katika Isaya 9:6, 7, NW: “Kwa maana kuna mtoto ambaye amezaliwa kwetu, kuna mwana ambaye tumepewa; na utawala wa Mwana Mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho, juu ya kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake ili kuusimamisha kwa imara na kuuendeleza kwa njia ya haki na kwa njia ya uadilifu, kuanza sasa na mpaka wakati usiojulikana. Bidii yenyewe ya Yehova wa majeshi itafanya hilo.”

      2. (a) Unabii wa Isaya 9:6, 7 ulitolewa chini ya hali gani? (b) Tunajuaje kwamba Yehova atashikamana bila kushindwa na agano alilofanya pamoja na Daudi kwa ajili ya ufalme wa milele katika ukoo wa nasaba yake?

      2 Lo! ni unabii mzuri ajabu kama nini! Itasisimua kuuchunguza unabii huo juu ya uzawa wa mtoto ulio mkuu zaidi duniani. Lakini kabla ya kuweza kuthamini unabii huo kikamili, tunahitaji kukaza fikira kwenye hali ambazo chini yazo umetolewa. Ulikuwa wakati wa mpango wa kitaifa wa hila wakati wa siku za ufalme wa Yuda chini ya Mfalme Ahazi. Ingawa alikuwa asiyeaminika kwa Yehova, mfalme huyo aliruhusiwa aketi juu ya kiti cha ufalme cha Yehova. Alionyeshwa uvumilivu huo kwa sababu ya agano ambalo Yehova alikuwa amefanya pamoja na Daudi la ufalme wa milele katika nasaba yake. Ingawa Daudi alinyimwa pendeleo la kumjengea Yehova hekalu, Mungu alimpa yeye baraka tofauti. Baraka hiyo ilionyeshwa katika maneno yafuatayo ya nabii Nathani: “Tena [Yehova] anakuambia ya kwamba [Yehova] atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.” (2 Samweli 7:11, 16) Ahadi hiyo ya kimungu ilithibitika kuwa yenye kuridhisha sana kwa Mfalme Daudi hivi kwamba yeye alitazama mbele kwenye utimizo wayo wenye utukufu.

      3. (a) Agano hilo pamoja na Daudi linapata utimizo pamoja na nani, na agano hilo lilikuwa la pekee jinsi gani? (b) Ibilisi alifanya nini kuwa mradi wake kuhusiana na agano hilo la Ufalme?

      3 Agano hilo pamoja na Daudi linapata utimizo katika Mwana mkuu wa Daudi, Yesu Kristo, “Mwana Mfalme wa Amani.” Hakuna nyumba nyingine yo yote ya kifalme hapa duniani ambayo imefurahia agano kama hilo la ufalme, bila kuwa na mwisho kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme wayo, bila mwisho wa amani. Lakini agano hilo la Ufalme lilitoa mwito wa ushindani kwa falme zote za ulimwengu ambazo Shetani ndiye mwana mfalme, au mtawala wazo. Basi Ibilisi pamoja na mashetani wake walifanya uwe mradi wao kujaribu kuharibu nyumba ya Daudi na hivyo wakomeshe mataraja yayo ya kuwa na mrithi mwenye kudumu. Shetani aliona wafuatao kuwa vyombo vilivyo tayari kutumiwa, Mfalme Resini wa Shamu, Mfalme Peka wa ufalme wa Israeli wa kabila kumi, na mfalme wa Ashuru.

      Mpango wa Hila Dhidi ya Lile Agano la Ufalme

      4. Ibilisi aliendeleaje katika jitihada zake za kukomesha utendaji wa agano la Ufalme wa Yehova lililofanywa pamoja na Daudi?

      4 Mpango wa hila wa Ibilisi ulikuwa nini? Lengo lake lilikuwa kumlazimisha Mfalme Ahazi wa Yuda, kwa sababu ya woga, aingie katika muungano kwa kufanya mpango usiofaa pamoja na mfalme wa Ashuru. Ibilisi angefanyaje hivyo? Basi, alimfanya Mfalme Peka wa Israeli na Mfalme Resini wa Shamu waingie katika mpango wa hila dhidi ya nyumba ya Daudi. Walifanya mpango wa hila pamoja wa kumwondoa Ahazi kutoka kwenye kiti cha ufalme cha Yuda ili wamweke mwanamume wao, mwana wa Tabeeli, kuwa mfalme kibaraka wao. Huyu mwana wa Tabeeli alikuwa nani? Ni jambo la maana kwamba yeye hakuwa mzao wa nyumba ya Daudi. Hivyo, hakuwa mtu ambaye kwake agano la Mungu la Ufalme lingepitia mpaka lifikie Mrithi walo wa kudumu yule “Mwana Mfalme wa Amani.” Angekuwa mwanamume wao, si mwanamume wa Mungu, katika kiti cha ufalme cha Yuda. Hivyo Biblia inafunua wazi jitihada ya Shetani ya kukomesha utendaji wa agano la Ufalme wa Yehova lililofanywa pamoja na Daudi.

      5, 6. Mfalme Ahazi aliitikiaje ule mpango wa hila uliofanywa dhidi ya nyumba ya Daudi, na ni ujumbe gani wenye kutia moyo aliopewa na Yehova?

      5 Mfalme Ahazi aliitikiaje tisho hili? Yeye pamoja na watu wake walitetemeka sana kwa woga. Basi Yehova alimpa habari yenye kutia moyo ili amgeuze asifanye muungano wa ulinzi pamoja na mfalme wa mamlaka ya ulimwengu iliyokuwa ikiinuka, Ashuru. Yehova alimpeleka nabii wake Isaya akutane na Ahazi na kumpa ujumbe huu unaopatikana kwenye Isaya 7:4-9:

      6 “Usiogope . . . kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu [mshiriki anayeongoza ufalme wa Israeli] na mwana wa Remalia [Peka], wakisema, Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli. Bwana [Yehova] asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa . . . kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.”

      Ishara ya Kushindwa kwa Ule Mpango wa Hila

      7. (a) Ni nini kilichoongoza kwenye unabii wenye maana kubwa wa Isaya 7:14? (b) Uzawa wa Imanueli ulikuwa ishara yenye kutegemeka ya nini, nao wana wa Isaya walikuwa wakitumika kuwa nini?

      7 Hivyo, Yehova alitabiri kupinduliwa kwa wananjama hao. Pindi iyo hiyo ukafika wakati wa kutolewa unabii wa kimungu wenye umaana wa kutikisa ulimwengu, kwa kuwa ulielekeza kwa Mrithi wa kifalme wa agano la Ufalme lililofanywa pamoja na Daudi. Lakini, ni nini kilichoongoza kwenye unabii huo wenye maana kubwa? Basi, Yehova alikuwa akizungumza na Mfalme Ahazi. Alimwambia Ahazi aombe ishara yo yote ya kimuujiza ambayo angefikiria, na Yehova angeifanya kama uhakikisho thabiti kwamba Mungu angevunja mpango wa hila dhidi ya nyumba ya Daudi. Lakini Ahazi alikataa kuomba ishara ya namna hiyo. Ni jambo gani lililotukia baadaye? Isaya 7:14 inatuambia hivi: “Kwa hiyo [Yehova] mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.” Jina hilo linamaanisha “Mungu Pamoja Nasi.” Kwa kuwa Imanueli pamoja na wana wawili wengine wa Isaya wangetumika kama ishara, nabii alisema hivi kwenye Isaya 8:18: “Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na [Yehova] tu ishara na ajabu katika Israeli zitokazo kwa [ Yehova] wa majeshi.” Basi kuzaliwa kwa Imanueli kulikuwa ishara hakika kwamba wananjama wote pamoja na mpango wao wa hila dhidi ya agano la Ufalme wa Mungu na Mrithi wake hawangefaulu!

      8. (a) Unabii kwenye lsaya7:15, 16 ulisema nini juu ya kivulana Imanueli, nayo matokeo yalikuwa nini? (b) Inaweza kuwa ni kwa sababu gani utambulisho wa Imanueli katika siku za Isaya unabaki bila uhakika?

      8 Maandishi ya Biblia hayasemi ni nani aliyemzaa mwana aliyeitwa Imanueli. Huenda ikawa alikuwa bikira Myahudi aliyepata kuwa mke wa pili wa nabii Isaya. Kwa vyo vyote, unabii uliendelea kusema kwamba kabla kijana huyo hajawa na umri wa kutosha kutofautisha yaliyo mema na mabaya, wafalme wawili waliofanya mpango wa hila pamoja dhidi ya nyumba ya Daudi wangefikia mwisho wenye msiba. (Isaya 7:15, 16) Jambo hilo lilithibitika kuwa kweli. Uhakika wa kwamba utambulisho wa Imanueli katika siku za Isaya unaendelea kuwa bila uhakika kwetu yaweza kuwa ni kwa kusudi la kutokengeua fikira za vizazi vijavyo kutoka kwa Imanueli Mkubwa Zaidi wakati angetokea akiwa ishara ya kimuujiza kutoka mbinguni.

      9. (a) Kutimizwa kwa ishara hiyo na kupinduliwa kwa mpango wa hila dhidi ya agano la Ufalme kulihakikisha nini? (b) Ni nini mpango wa hila wa ulimwengu wote ulio mkubwa zaidi ya yote uliopata kufanywa wakati wo wote?

      9 Bila shaka, katika siku za Ahazi, kulikuwa na utimizo mdogo tu wa ishara na wa kupinduliwa kwa mpango wa hila wa ulimwengu dhidi ya agano la Mungu la Ufalme. Hata hivyo utimizo huo wa kwanza ulitoa uthibitisho wa kwamba ishara na mapinduzi ya mpango wa hila wa ulimwengu ungetimizwa kwa njia yenye maana kubwa katika wakati wetu wenye hatari. Leo tunakabiliana macho kwa macho na mpango wa hila wa ulimwengu wote ulio mkubwa zaidi ya wote uliopata kufanywa wakati wo wote. Katika maana gani? Katika maana ya kwamba mataifa yanapuuza kabisa mpango wa Yehova wa kuleta amani yenye kudumu, na hata yanapinga wajumbe wa “Mwana Mfalme wa Amani.” Mpango huo wa hila kwa kweli ni dhidi ya Mrithi wa agano la Ufalme, yule “Mwana Mfalme wa Amani.” Sasa, basi, namna gani kuhusu utimizo kamili wa unabii huu? Tukiifahamu ishara, basi tutathamini ya kwamba matokeo ya mwisho yatakayoupata mpango wa hila wa ulimwengu yamekwisha katwa.

      Uzawa wa Yule “Mwana Mfalme wa Amani”

      10. (a) Katika utimizo kamili wa Isaya 7:14, ni nani aliyetokeza mtoto akiwa ishara na Mrithi wa agano la Ufalme? (b) Mwanahistoria Mathayo anahusianishaje ishara ya Imanueli na nyumba ya Daudi?

      10 Katika utimizo kamili wa unabii huo, bikira aliyemzaa mwana kama ishara na Mrithi wa agano la Ufalme alikuwa Mariamu, bikira Myahudi wa ukoo wa Mfalme Daudi. Malaika Gabrieli alimwambia kwamba angemzaa mwana ambaye angeitwa Yesu, na kwamba Yehova Mungu “atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake,” na kwamba “ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:26-33) Mathayo mwanahistoria aliyeongozwa na Mungu anahusianisha ishara ya Imanueli pamoja na nyumba ya Daudi. Tunasoma hivi kwenye Mathayo 1: 20-23: “Malaika wa [Yehova] alimtokea [Yusufu] katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa roho [takatifu]. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na [Yehova] kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; yaani, Mungu pamoja nasi.”

      11. Uzawa uliotabiriwa wa Imanueli ulitukia wapi na lini?

      11 Kuzaliwa huku kwa Imanueli kulikota-biriwa kulitukia wapi na lini? Macho yote ya Wayahudi yalielekezwa upande uliofaa na maneno ya Mika 5:2, yanayoelezwa kwenye Mathayo 2:6: “Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakayewachunga watu wangu Isra-eli.” Ilikuwa katika mwaka wa 2 K.W.K. katika mji wa Bethlehemu kwamba “Mwana Mfalme wa Amani” alizaliwa, na unabii wenye kusisimua wa Isaya 9:6, 7 ukaanza kutimizwa.

      12, 13. Uzawa wa “Mwana Mfalme wa Amani” uliletea nani heshima kubwa, na uzawa huo ulikuwa pamoja na wonyesho gani wenye utukufu na wenye kustaajabisha?

      12 Ni nani kati yetu asingeiona kuwa heshima na furaha kuwa mzazi wa yule ambaye angekuwa na cheo “Mwana Mfalme wa Amani”? Basi, jambo hilo lilimletea utukufu mkuu Baba wa kifalme wa huyu Mwana Mfalme. Kwa kweli, hasha, la hasha, Tiapana wakati mwingine wo wote uliotangulia ambapo uzawa wa kibinadamu umepata kuwa pamoja na wonyesho wenye utukufu na wenye kustaajabisha sana hivyo.

      13 Malaika wa Yehova mwenye kung’aa aliwatokea wachungaji waliokuwa wakilinda makundi yao usiku makondeni nje ya Bethlehemu, na “utukufu wa (Yehova] ukawang’aria pande zote.” Halafu malaika akatangaza uzawa huo kwa kutimiza unabii wa kimungu, akisema: “Maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Kana kwamba jambo hilo halikuwa tukufu vya kutosha, kukatokea katika mbingu juu jeshi.la malaika wakimsifu Baba ya mwana huyo aliyezaliwa na kusema kana kwamba kwa sauti moja: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Inafaa jinsi gani malaika kutangaza wakati wa uzawa wa yule aliyekusudiwa kuwa “Mwana Mfalme wa Amani” kwamba kungekuwako amani ya kimungu kwa wote ambao wana nia njema ya Mungu!​—Luka 2:8-14.

      14, 15. (a) Ni juu ya matukio gani wana wa kimbungu wa Mungu walimsifu Yehova? (b) Ni kwa sababu gani hakuna uzawa wa mtoto mwingine katika historia yote ya kibinadamu ungelingana na huo?

      14 Muda mrefu kabla ya uzawa wa yeye ambaye angekuwa “Mwana Mfalme wa Amani,” malaika walikuwa wamemsifu Mungu katika pindi ya pekee. Huo ulikuwa wakati ambapo katika uumbaji, aliiweka misingi ya dunia. (Ayubu 38:4) Je! wewe umeona picha za dunia yetu ambazo zimechukuliwa na wasafiri wa anga za juu? Basi uliona jambo ambalo ni malaika tu waliokuwa wameona mpaka kufikia nyakati za karibuni. Na malaika waliitikiaje? Ayubu 38:7 hutuambia hivi: “Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha.”

      15 Uzawa ulio mkuu zaidi uliopata kuiheshimu dunia hungekuwa tukio dogo ambalo kwa sababu yalo wana wa Mungu wangeunganisha sauti zao kwa wimbo wa sifa. Kama vile baba ya kidunia anavyopongezwa kwa uzawa wa mwana wake mzaliwa wa kwanza, vivyo hivyo Baba wa kimbingu aliyekuwa na daraka kwa uzawa huo mkuu zaidi uliopata kutukia duniani anastahili kutukuzwa katika nyimbo na washiriki wa jamaa yake ya kimbingu. Kikundi hicho cha waimbaji kizuri mno lazima kiwe kilimfurahisha Mtu wa kimungu kama nini kwa yeye kuwa baba kwa mara ya kwanza katika hali mpya kabisa! Hakuna wakati wo wote uliotangulia katika historia ya ulimwengu wote ambapo kumepata kuwa na uzawa wa mtoto unaoweza kulingana na ule wa yule aliyekusudiwa kuwa “Mwana Mfalme wa Amani.”

      “Nuru Kuu” Yang’aa

      16.Ni lini na jinsi gani kulikuwako utimizo zaidi wa Isaya sura ya 9?

      16 Yesu alipoanza huduma yake ya hadharani, kulikuwako utimizo zaidi wa Isaya sura ya 9. Hii ilihusiana na mistari yake miwili ya kwanza, iliyotabiri kwamba “nuru kuu” ingeng’aa kwa watu “waliokwenda katika giza.” Tunaelezwa utimizo wa mistari hiyo na Mathayo mwanahistoria aliyeongozwa na Mungu kwenye sura ya 4, mistari 13 hadi 17: “[Yesu akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”

      17. Ni kwa sababu gani Yesu angewezesha nuru ing’ae juu ya watu katika Zabuloni na Naftali, na nuru hiyo ingemaanisha nini kwa watu waliokaa katika giza?

      17 Zabuloni na Naftali zilikuwa upande wa mwisho wa kaskazini mwa Israeli na zilitia ndani wilaya ya Galilaya. Naftali ilikuwa mpakani mwa pwani yote ya magharibi mwa Bahari ya Galilaya. Kwa hiyo, kuhubiri kwa Yesu pamoja na wanafunzi wake habari njema za Ufalme wa Mungu katika sehemu hizo ndiko kulikofanya nuru ing’ae kwa watu ambao walikuwa wameketi gizani kwa muda mrefu. Yesu alisema hivi katika Yohana 8:12: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Kwa hiyo, kupitia kwa Yesu wale “waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti” waliwezeshwa kuwa na “nuru ya uzima” kwa kuwa alitoa uhai wake “uwe fidia ya wengi.” Yeye ndiye aliyetumiwa na Yehova kutoa nuru juu ya njia ambayo kwayo watu wangepata uzima.​—Mathayo 4:23; 20:28.

      18. (a) Ni kwa sababu gani hii “nuru kuu” haingekuwa ya watu wa Galilaya peke yao? (b) Ni nini kitakachozungumziwa katika makala inayofuata?

      18 “Mwanga mkuu” huu unaotoa ukombozi kutoka katika kifo na udhalimu haukuwa kwa ajili ya watu wa Galilaya peke yao. Je! Isaya hakutabiri kwamba wingi wa serikali hiyo haungekuwa na mwisho? Na je! Isaya hakutabiri kwamba daraka la “MwanaMfalme wa Amani” lingekuwa kubwa mno? Ndiyo, kwa kuwa Isaya 9:6, 7, NW husema hivi: “Na jina lake ataitwa, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho.” Katika makala itakayofuata, tutazungumzia daraka la Yesu Kristo akiwa “Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele,” pamoja na “Mwana Mfalme wa Amani’’.

  • Usalama Ulimwenguni Pote Chini ya “Mwana-Mfalme wa Amani
    Mnara wa Mlinzi—1987 | Aprili 1
    • Usalama Ulimwenguni Pote Chini ya “Mwana-Mfalme wa Amani

      “Kwa wingi wa utawala wa mwana-mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho, juu ya kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake ili kusimamisha kwa imara na kuendeleza kwa njia ya haki na kwa njia ya uadilifu, kuanza sasa na kuendelea mpaka wakati usiojulikana. Bidii yenyewe ya Yehova wa majeshi itafanya hilo.”​—ISAYA 9:7, NW.

      1, 2, (a) Uzawa wa Ufalme wa Mungu ungekuwa pindi kwa ajili ya nini, na uzawa huo ulitukia lini? (b) Katiba ya Umoja wa Mataifa unalipa tengenezo hilo mgawo gani, lakini agano la Ufalme limempa Yesu Kristo mgawo gani? (c) Tunajuaje kwamba Yehova atashikamana bila kushindwa na agano hilo la Ufalme?

      KAMA vile uzawa wa Yesu akiwa mtoto mwanamume mkamilifu ulivyokuwa pindi ya furaha ipitayo ile ya kawaida, ndivyo na uzawa wa Ufalme wake ulioahidiwa kwa muda mrefu ungekuwa pindi ya furaha kuu sana. (Zaburi 96:10-12) Kulingana na mambo ya hakika ya historia ya kisasa, serikali hiyo iliwekwa begani mwa Yesu aliyetawazwa katika 1914. Kuwapo kwa tengenezo la Umoja wa Mataifa leo hakulifanyi jambo hilo la uhakika kuwa uwongo. Hakuna hata mmoja wa watawala wa mataifa wanachama 159 wa UM aliye wa nyumba ya Daudi. Hata hivyo, katiba ya mpango wa hila huo wa ulimwengu inawapa wao daraka la kuleta amani na usalama ulimwenguni pote kwa ajili ya wanadamu.

      2 Lakini agano la Yehova la Ufalme halijafutiliwa mbali kamwe. Kwenye Isaya 9:7 usemi huu “juu ya kiti cha ufalme cha Daudi” unathibitisha agano ambalo Mungu alifanya pamoja na Daudi la ufalme usio na mwisho. Kuongezea hilo, Yehova ameapa kwamba lazima likamilishwe kwa mafanikio. Kwamba Yehova atashikamana na agano hilo inaonyesha wazi kwa maneno haya kwenye Zaburi 89:3, 4, 35, 36: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia Daudi, mtumishi wangu. Mzao wako nitamfanya imara milele, nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu, hakika sitamwambia Daudi uwongo, wazao wake watadumu milele, na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu.” Agano hilo, pamoja na jina lake la cheo “MwanaMfalme wa Amani” vinampa Yesu Kristo daraka la kuleta usalama ulimwenguni pote.

      3. Ni kwa sababu gani wakati wa “Mwana-mfalme wa Amani” kuanza kutawala haukuwa wakati wa amani kwa mbingu au kwa dunia?

      3 Hata hivyo, wakati wa Yehova Mungu kuweka serikali ile juu ya bega la Mwana-mfalme Mwenye Haki ya Kurithi Ufalme haungekuwa mwaka wa amani katika mbingu juu wala chini duniani. Kulingana na Ufunuo sura ya 12, uzawa wa Ufalme wake ungefuatwa na vita mbinguni. Shetani Ibilisi na mashetani zake walipiga vita dhidi ya serikali hiyo mpya iliyosimamishwa, na Mfalme mpya aliyetawazwa pamoja na malaika zake watakatifu walipiga vita dhidi ya majeshi hayo ya kishetani. Matokeo yalikuwa kwamba Shetani na mashetani wake walitupwa kutoka katika mbingu mpaka chini kwenye ujirani wa dunia yetu. Kama matokeo, kulikuwa na mlio huu: “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” (Ufunuo 12:12) Tangu kushushwa kwa Ibilisi, dunia yetu imekuwa mahali pa ujeuri na vita visivyo na kifani. Lo! jinsi wanadamu wanavyohitaji utawala wa “Mwana-mfalme wa Amani kwa kuwa utatokeza usalama ulimwenguni pote”!

      4. Ni kwa sababu gani jina la cheo “Mungu Mwenye Nguvu” halipasi kuleta mvurugo likifikiriwa kuwa sawa na Mungu mwenye nguvu zote?

      4 Kulingana na Isaya 9:6, NW majina ya vyeo mengine, zaidi ya “Mwana-mfalme wa Amani,” yangeongezwa kwenye jina tukufu la Yesu Kristo. Mojapo la majina hayo ya vyeo lingekuwa “Mungu Mwenye Nguvu.” Hangeitwa Mungu mwenye nguvu zote, kana kwamba alikuwa mshiriki anayelingana na miungu ya utatu. Hata katika siku ya kufufuliwa kwake, yeye alifanya ijulikane kwamba alikuwa angali mdogo kwa Yehova. Alimtokea Mariamu Magdalene na kumtuma awaeleze wanafunzi wake wenye kuhangaika kwamba alikuwa akirudi kwa Baba yao na Baba yake na Mungu wao na Mungu wake. (Yohana 20:17) Mpaka leo hii, yeye anaendelea kuongoza viumbe vyote katika ibada ya “Mungu wa miungu,” Yehova. (Danieli 11:36) Aha, ndiyo, Yesu Kristo ana Mungu na Mungu huyo si Yesu mwenyewe bali ni yule Baba ya kimbingu Yehova. “Mwana-mfalme wa Amani” anatumika kwa njia nzuri kama nini akiwa mjumbe wa amani na usalama wenye kudumu wa ulimwengu wote mzima!

      5. Ni kwa sababu gani Yesu Kristo ndiye anayestahili zaidi kuongoza viumbe vyote vyenye akili katika ibada ya yule Mungu mmoja wa kweli anayeishi, Yehova?

      5 Kwa umilele wote, yule Mwana wa Mungu aliyetukuzwa ataendelea kuongoza viumbe wote wenye akili katika ibada ya Mungu huyo mmoja wa kweli aishiye, Yehova. Huyo Mwana wa Mungu aliyetukuzwa anastahili vya kutosha kwa ajili ya hilo. Kati ya viumbe vyote katika mbingu na duniani, Mwana wa Mungu aliyetukuzwa ndiye amemjua Yehova kwa kipindi kirefu zaidi cha wakati na kwa undani zaidi. Mtume Paulo anasema hivi kwenye 1 Wakorintho 2:11: “Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?” Ndivyo ilivyo katika habari ya Yesu Kristo. Ingawa alitumiwa na Yehova Mungu katika uumbaji wa wanadamu, lilikuwa jambo tofauti yeye mwenyewe kuwa mwanadamu, kuzungukwa na hali zote za duniani na kuhisi yeye mwenyewe binafsi hisia za wanadamu. Kwa hiyo imeandikwa kwamba “ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata” akiwa mwanadamu hapa duniani. (Waebrania 5:8) Kweli kweli yeye alithibitika kuwa anastahili kukabidhiwa kwa usalama ‘mamlaka yote mbinguni na duniani’ na kubeba jina la cheo “Mungu Mwenye Nguvu.”​—Mathayo 28:18; linganisha Wafilipi 2:5-11.linganisha Wafilipi 2:5-11.

      “Mshauri wa Ajabu” na “Baba ya Milele”

      6. Yesu Kristo amekuwa akitumikiaje akiwa “Msha-uri wa Ajabu,” na “mkutano mkubwa” umenufaikaje kutokana na shauri lake la ajabu?

      6 Kwa sababu zote hizi zenye nguvu, Mwana-mfalme. Wa kimbingu wa Mungu anaweza kutumikia akiwa “Mshauri wa Ajabu.” (Isaya 9:6, NW) Shauri lake sikuzote ni la hekima, kamilifu na lisilokosea. Akiwa Mpatanishi kati ya Yehova Mungu na wale ambao wameingizwa katika lile agano jipya, yeye amekuwa akitumikia kweli kweli kama mshauri wa ajabu kwa karne hizi 19 zilizopita. Sasa, tangu 1935, “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine “wake wamekuwa wakitwaa shauri lake la ajabu na wanapata maagizo na uongozi ulio bora zaidi. (Ufunuo 7:9-17; Yohana 10:16) Akiwa chombo cha kufanyia kazi hii ya kushauri, katika wakati huu wa “umalizio wa mfumo” wa mambo yeye ameinua jamii ya “mtumwa mwaminifu mwenye akili” na kuiweka juu ya vitu vyake vyote vya kidunia, au faida za kifalme. (Mathayo 24:3, NW; 45-47 Luka 12:42-44) Sasa “mkutano mkubwa” unapokea mashauri ya kiroho ambayo ni ya ajabu kweli kweli na amini kwa sababu yanategemea Neno la Mungu lililofunuliwa.

      7. Ni kwa sababu gani Shetani Ibilisi si mungu mkuu tena kwa watu wa Yehova?

      7 Kama matokeo ya kuitikia kwao shauri hilo, Shetani Ibilisi, “mungu wa huu mfumo wa mambo,” si mungu mkuu kwetu sisi tulio watu wa Yehova. (2 Wakorintho 4:4, NW) Sisi kwa kutii tumetoka katika Babuloni Mkuu, milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo, nasi hatushiriki tena dhambi zake mbovu. Sisi tumechukua msimamo wetu bila kuondoleka upande wa Yeye ambaye juu ya bega lake Yehova Mungu ameweka serikali Yake.

      8. (a) Ni kwa sababu gani jina la cheo “Baba wa Milele” ni lenye kupendeza sana hasa kwa “mkutano mkubwa”? (b) Ni nini litakalowapata wale wanaomruhusu Shetani Ibilisi awe baba yao wa kiroho?

      8 Lile jina la cheo “Baba ya Milele” ni lenye kupendeza sana. “Mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine” hasa wanathamini sana jina hilo. Ubaba wa Shetani Ibilisi hauwapendezi. Wao wanatetema kwa kuchukizwa wanapowakumbuka viongozi wa kidini Wayahudi ambao walimpinga Yesu naye akawaambia hivi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimana katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uwongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo [uwongo].” (Yohana 8:44) Huo “mkutano mkubwa” umeondoka miongoni mwa hao watoto wa kiroho wa Shetani Ibilisi, ambaye ubaba wake juu ya wanadamu wenye dhambi hautadumu. Wale wanaomruhusu awe baba yao wa kiroho wataangamia pamoja naye. Uharibifu kabisa, unaofananishwa na “moto wa milele” kwenye Mathayo 25:41, unamngojea Ibilisi pamoja na wanadamu wote ambao hawaondoki chini ya ubaba wake.​—Mathayo 25:41-46.

      9. “Mkutano mkubwa” unapataje mwonjo wa kimbele wa ubaba wa “Baba wa Milele”?

      9 Kwa upande mwingine, “mkutano mkubwa” unaonja kimbele ubaba wa “Baba wa Milele.”a Kwa njia gani? Kwa kusikiliza sauti yake na kuwa “kondoo wengine” wake na kushirikiana pamoja na mabaki ya Israeli wa kiroho. Uhusiano huu mchangamfu wa kijamaa unaonyesha amani. Akiandika chini ya uongozi wa roho, mtume Paulo alimtaja Yehova katika Warumi 16:20, NW kuwa “Mungu atoaye amani.” Basi inafaa sana kwamba, Mwanaye mzaliwa pekee aitwe “Mwana-mfalme wa Amani”! Kwa kuirudisha amani katika ulimwengu wote mzima, “Mwana-mfalme wa Amani” bila kushindwa atatenda kupatana na maana ya jina lake kuu la cheo.

      Ile Serikali ya Kifalme ya “Mwana-mfalme wa Amani”

      10, 11. Baada ya kutabiri uzawa wa mtoto ulio mkuu zaidi ambao umepata kutokea, Isaya aliendelea kusema nini, nayo maneno yake yanamaanisha nini?

      10 Baada ya Isaya kutabiri uzawa wa mtoto ulio mkuu zaidi ambao umepata kutokea—​ndiyo, ule wa Mwana wa Mungu ambaye angeheshimiwa kwa kupewa jina la cheo “Mwana-mfalme wa Amani”​—nabii alielekezwa na roho ya Yehova aseme hivi: “Kwa wingi wa utawala wa mwana-mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho . . . Bidii yenyewe ya Yehova wa majeshi inafanya hilo.”​—Isaya 9:7, NW.

      11 Katika kusema “wingi wa utawala wa mwana-mfalme,” unabii unaonyesha kwamba milki ya “Mwana-mfalme wa Amani” itatia ndani dunia nzima. Hakutakuwa na mipaka duniani ambayo itazuia milki yake. Itaenea na kufunika tufe lote. Zaidi ya hilo, katika dunia Paradiso itakayokuja, hakutakuwa na mwisho wa amani. Hakutakuwa kamwe na machafuko po pote. Amani itaenea duniani pote na sikuzote itakuwa tele. (Zaburi 72:7) Amani katika maana hii inamaanisha zaidi ya kutokuwa na vita; inatia ndani haki na uadilifu, kwa maana Isaya alisema kwamba utawala wa mwana-mfalme ungetegemezwa “kwa njia ya haki na kwa njia ya uadilifu, sasa na kuendelea mpaka wakati usiojulikana.” Kutakuwa na baraka tele kwa ajili ya wanadamu. Na bidii isiyochoka ya Yehova Mungu itatimiza hilo katika wakati wetu.

      12. Ile serikali iliyo begani mwa “Mwana-mfalme wa Amani” inawakilishwaje duniani pote?

      12 Hata sasa, serikali hii begani mwa “Mwana-mfalme wa Amani” inawakilishwa duniani kote. Kukubaliwa kwa serikali ya kifalme yake ya kimbingu kunaenea kwa haraka sana. Mabaki ya wanafunzi wa Yesu Kristo waliozaliwa kwa roho wamekusanywa kikamilifu kutoka katika mataifa. Kwa kuongezea, “mkutano mkubwa” unakusanywa kutoka katika nchi mbalimbali zaidi ya 200. Sasa kuna Mashahidi wa Yehova 3,229,022, na kazi yenye kufurahisha ya kukusanya haijakamilika bado. “Mkutano mkubwa” huu unashangilia serikali iliyo begani mwa “Mwana-mfalme wa Amani.” Washiriki wao wanashukuru sana kuwa chini ya serikali hiyo na kuwa wajumbe wayo duniani kote. wakishirikiana na “mabalozi walio badala ya Kristo, “yale mabaki ya wapakwa-mafuta.​—2 Wakorintho 5:20.

      Mpango wa Hila wa Kisasa Utavunjwa Vipande Vipande

      13. (a) Wajumbe wa Ufalme wanajitahidi kufanya nini miongoni mwao? (b) Mungu anauonaje Umoja wa Mataifa?

      13 Wajumbe wa Ufalme wanaendeleza pia amani miongoni mwao. Wao ‘wanajitahidi kuhifadhi umoja wa roho katika kifungo cha amani.’ (Waefeso 4:3) Wanafanya hivyo ijapokuwa ghasia zinazoendelea duniani pote. Mataifa moja moja ndani na nje ya tengenezo la Umoja wa Mataifa wamejipanga kihalisi dhidi ya serikali ya “Mwana-mfalme wa Amani.” Kama Mungu anavyoliona, tengenezo la Umoja wa Mataifa, ni mpango wa hila kubwa mno wa ulimwenguni pote. mno. Kwa nini? Kwa kuwa linajitangaza lenyewe kwamba limewekwa eti litimize malengo ambayo Mungu amemwekea “Mwana-mfalme wa Amani” wake pekee ayatimize. Nalo linaomba watu wa mataifa yote waliunge mkono katika kusimamisha usalama wa ulimwenguni pote kupitia jitihada za wanadamu. Hata lilitangaza 1986 kuwa “Mwaka wa Amani ya Kimataifa.” Hivyo lajionyesha lenyewe kuwa mpango wa hila dhidi ya “Mwana-mfalme wa Amani” na dhidi ya agano la Yehova pamoja naye la Ufalme wa milele.

      14. Nabii Isaya aliwatoleaje onyo wale wote wanaompinga Yehova na agano lake la Ufalme?

      14 Kwa sababu kama hiyo, huko nyuma nabii Isaya alimwonya Mfalme Ahazi na raia zake kuhusu kutafuta amani na usalama kwa kuingia katika mapatano ya kirafiki pamoja na Mamlaka ya Ulimwengu ya Ashuru. Onyo hilo linapatikana kwenye Isaya 8: 9, 10. Katika usemi mzuri sana wa kimashairi, nabii anawaonya hivi wote wanaompinga Yehova na agano lake la Ufalme: “Fanyeni ghasia, enyi kabila za watu, nanyi mtavunjwa vipande vipande; tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande. Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; semeni neno, lakini halitasimama; kwa maana Mungu yu pamoja nasi!”

      15. Ni nini litakalotukia kwa mpango wa hila dhidi ya agano la Ufalme leo, kama ilivyoonyeshwa na ule mpango wa hila katika siku za Mfalme Ahazi?

      15 Basi acheni mataifa yaliyo chini ya mwana-mfalme wa ulimwengu huu, Shetani Ibilisi, wafanye mpango wa hila pamoja dhidi ya agano la Ufalme na mwana-mfalme Mrithi walo na Mtawala. Mpango huo wa hila utavunjwa vipande vipande, kama vile mpango wa hila katika siku za Mfalme Ahazi ulivyovunjwa. Mfalme Resini wa Shamu na Mfalme Peka wa Israeli hawakumwogopa Yehova wa majeshi lakini walifanya mpango wa hila dhidi ya agano lake la Ufalme. Mpa-ngo wao huo wa hila ulivunjwa vipande vipande. Vilevile Mfalme Ahazi wa Yuda hakumwogopa Yehova lakini aliingia katika mpango wa hila pamoja na mamlaka ya ulimwengu ya Ashuru. Jambo hilo kwa kweli halikumsaidia Ahazi wala kumletea amani na usalama. Lilileta dhiki na utumwa. Jambo baya zaidi ya yote ni kwamba lilimfanya Ahazi akose upendeleo wa Yehova.

      16. Yehova alivunjavunjaje ule mpango wa hila wa Ashuru dhidi ya agano la Ufalme, na jambo hili lilitangulia kuonyesha nini kwa ajili ya siku zetu?

      16 Baada ya kifo cha Ahazi na katika siku za mwana wake Hezekia, Yehova wa majeshi alivunja mpango wa hila wa Ashuru dhidi ya agano la Ufalme. Mfalme wa Ashuru alilazimika kukimbia kutoka katika nchi ya Yuda baada ya malaika wa Yehova kuwaangamiza askari wake 185,000. Adui hao hakuweza hata kutupa mshale mmoja dhidi ya mji wa Yerusalemu. (Isaya 37:33-36) Ushinde wa namna hiyo juu ya mpango wa hila wa ulimwengu wa siku hizi dhidi ya agano la Ufalme wa Yehova na “Mwana-mfalme wa Amani” ni hakika, kwa kuwa Mungu yu pamoja na Mwana-mfalme wake Imanueli na wote wanaompokea kwa shangwe.

      Kusimama Bila Woga kwa Ajili ya Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote Mzima ya Yehova

      17. (a) Sehemu za kisiasa zitafanya nini kwa Babuloni Mkuu karibuni, nao watu wa Yehova watahitaji na kupokea nini? (b) Baada ya kuondoa Babuloni Mkuu, watawala wasioamini kuwapo kwa Mungu watafanya nini sasa, jambo hilo likimchochea Yehova kuchukua tendo gani?

      17 Karibuni sehemu za kisiasa zitaelekeza jitihada zazo si dhidi ya Jumuiya ya Wakristo tu bali pia dhidi ya Babuloni Mkuu, milki yote ya ulimwengu ya dini ya uwongo, ili kuifutilia mbali isiwepo tena. Wakati huo wenye hatari, ulinzi wa kimungu kwa watu wa Yehova utatenda kazi kwa kiwango kisicho cha kawaida. Wakichochewa na ushindi wenye kujaa damu juu ya Babuloni Mkuu, watawala wasioamini kuwapo kwa Mungu watawageukia kwa ukali mwingi wale ambao wako upande wa serikali ya Mungu kupitia Yesu Kristo. Ndipo Yehova atamtumia “Mwana-mfalme wa Amani” wake ili apige ile “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.” (Ufunuo 16:14) Yesu Kristo atathibitika kuwa Shujaa asiyeshindika ambaye serikali yake haitapatwa na upungufu. Yeye atathibitika kuwa “Mungu Mwenye Nguvu” chini ya Yehova, Mungu mwenye nguvu zote mwenye ushindi wenye shangwe. Huyu “Mungu Mwenye Nguvu” atafikia upeo wa kazi yake tukufu kwa ushindi huo penye Har–Magedoni ambao mshindo wao utaendelea bila kufifia kamwe kwa umilele wote! Pongezi kwa ushindi huo usio na kifani!

      18. Kwa kuelekeana na mpango wa hila wa kisasa dhidi ya agano la Ufalme, Mashahidi wa Yehova wameazimia kufanya nini, na kukiwa na matokeo gani?

      18 Haya, basi, songeni mbele enyi mashahidi wa Yehova wote, mpate kujulikana zaidi sana ulimwenguni kuliko hapo zamani, mkimtumainia kabisa Mungu wenu na Mfalme wake anayetawala, “Mwana-mfalme wa Amani”! Onyesheni ushujaa kabisa bila kuuogopa mpango wa hila wa sasa wa ulimwengu. Kwa kuutangaza kila mahali ujumbe wa Ufalme na ushindi wao unaokuja juu ya mpango wa hila wa ulimwengu katika Har–Magedoni, ninyi nyote iweni ishara na miujiza kwa utukufu wa Yehova. Shetani atakapoelekeza watawala wa ulimwengu dhidi yetu, kumbukeni, ushindi utakuwa na wale wanaosimama imara na waaminifu kwa Ufalme wa Imanueli, “Mwana-mfalme wa Amani,” kwa kuwa “Mungu yu pamoja nasi”! (Mathayo 1:23; linganisha Isaya 8:10.) Na acheni malaika wote wa mbinguni na wanadamu wote washika ukamilifu duniani waseme “Amina” kwa kuondolewa malawama enzi kuu ya Yehova juu ya viumbe vyote mbinguni na duniani, kukiwa na usalama ambao hautakoma kamwe!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki