Maisha na Huduma ya Yesu
Taifa Lapotea, Lakini Si Watu Wote
MUDA mfupi baada ya zungumzo la Yesu pamoja na wale waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba ya Farisayo mmoja, watu fulani wanamwambia “habari ya Wagalilaya wale ambao [gavana wa Kiroma Pontio] Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.” Wagalilaya hao labda ndio wale ambao waliuawa wakati maelfu ya Wayahudi walipoteta kwa kukataa utumizi wa Pilato wa pesa zilizotolewa kwenye hazina ya hekalu ili kujenga mtaro wa kuleta maji ndani ya Yerusalemu. Wale wenye kusimulia jambo hilo kwa Yesu huenda wakawa wanadokeza kwamba Wagalilaya hao walipatwa na lile afa kwa sababu ya matendo maovu yao wenyewe.
Hata hivyo, Yesu anawanyoosha, akiuliza hivi: “Je! mwadhani ya kwamba Walilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo,” Yesu anajibu. Ndipo yeye anatumia kituko hicho kuonya Wayahudi hivi: “Msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Akiendelea, Yesu anakumbuka tanzia nyingine ya huko, labda ikiwa pia inashirikishwa na ujenzi wa mtaro ule. Yeye anauliza: “Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?” Hapana, haikuwa kwa sababu ya ubaya wa watu hao kwamba wao walikuja kufa, Yesu anasema. Badala ya hivyo, “wakati na tukio lisilotazamiwa” ndio kwa ujumla husababisha tanzia kama hizo. Hata hivyo, Yesu anatumia tena pindi hiyo kuonya hivi: “Msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Ndipo Yesu anaendelea kutoa kielezi kinachofaa, akieleza hivi: “Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona [huo unaiharibu, NW] hata nchi? . . . Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! la, usipozaa, ndipo uukate.”
Yesu alikuwa ametumia zaidi ya miaka mitatu akijaribu kusitawisha imani miongoni mwa taifa la Kiyahudi. Lakini ni wanafunzi wachache tu kama mia moja hivi wanaoweza kuhesabiwa kuwa tunda la kazi zake za jasho. Sasa, wakati wa mwaka huu wa nne wa huduma yake, yeye anazidisha sana jitihada zake, akichimba kwa njia ya ufananisho na kutia samadi kuuzunguka ule “mtini” wa Kiyahudi kwa kuhubiri na kufundisha kwa juhudi katika Yudea na Perea. Lakini wapi! Taifa lile linakataa kutubu na kwa hiyo limo katika mstari wa kupatwa na uharibifu. Ni mabaki tu ya taifa hilo wanaoitikia.
Muda mfupi baadaye Yesu anafundisha katika sinagogi siku ya Sabato. Humo anaona mwanamke mmoja, ambaye kwa sababu ya roho mbaya mwenye kumsumbua, amekuwa ameinamilia kwa kupindana mgongo muda wa miaka 18. Kwa huruma, Yesu anamwambia hivi: “Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.” Hapo yeye anaweka mikono yake juu ya mwanamke yule, na papo kwa hapo ananyooka wima na kuanza kutukuza Mungu.
Hata hivyo, afisa msimamizi wa sinagogi anakasirika. “Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo,” yeye anateta kwa kukataa. “Basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.” Hivyo afisa yule anakiri nguvu ya Yesu ya kuponya lakini anawashutumu watu kwa kuja kuponywa siku ya Sabato!
“Enyi wanafiki,” Yesu anajibu, “kila mmoja wenu, je! hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?”
Basi, kusikia hivyo, wale wenye kupinga Yesu wanahisi aibu. Hata hivyo, umati ule unashangilia mambo yote matukufu wanayoona Yesu akifanya. Kwa kuitikiza Yesu anarudia vielezi viwili vya kiunabii kuhusu Ufalme wa Mungu, ambavyo yeye alisimulia akiwa mashuani katika Bahari ya Galilaya karibu mwaka mmoja mapema kidogo. Luka 13:1-21; Mhubiri 9:11, NW; Mathayo 13:31-33.
◆ Ni tanzia gani ambazo zinatajwa hapa, na ni somo gani ambalo Yesu anachota kutokana nazo?
◆ Ni utumizi gani unaoweza kufanywa kuhusu ule mtini usio na matunda, na pia yale majaribio ya kuutanya uwe na mazao?
◆ Ni jinsi gani yule afisa msimamizi anakiri kwamba Yesu ana uwezo wa kuponya, hata hivyo Yesu anafichua jinsi gani unafiki wa mwanamume huyo?