Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Lile Jiwe la Moabu—Liliharibiwa Lakini Halikupotea
    Mnara wa Mlinzi—1990 | Aprili 15
    • Lile Jiwe la Moabu—Liliharibiwa Lakini Halikupotea

      LILE Jiwe la Moabu, au Mesha, lilivunjwa-vunjwa makusudi katika mwaka walo wa kwanza baada ya kugunduliwa katika 1868. Lilikuwa na umri unaokaribia miaka 3,000. Ni kipande cha jiwe la basalti jeusi lililosuguliwa likiwa na upande wa juu ulioviringishwa vizuri, lilikuwa na kimo cha karibu meta 1.2 likipita kidogo tu upana wa meta 0.6, na likiwa na unene unaokaribia meta 0.6. Wakati fulani baada ya kuvunjwa-vunjwa, vipande viwili vikubwa na vingine vidogo vidogo 18 vilipatikana, lakini theluthi ya jiwe hilo ilipotea kwa kadiri ya kutoweza kupatikana.

      Kifaa kama hicho kisicho na kifani kilikaribiaje sana hivyo kupotea? Nacho ni chenye thamani kadiri gani kwa wanafunzi wa Biblia?

      Hila na Mashaka

      F. A. Klein alikuwa ndiye Mzungu wa kwanza na wa mwisho kuona jiwe hilo katika hali yalo isiyovunjika-vunjika. Lilikuwa linakaa miongoni mwa magofu ya Diboni kaskazini-mashariki mwa Bahari ya Ufu (ya Chumvi). Alifanya michoro mifupi ya sehemu za mistari 35 ya maandishi kufikia ukingo wa sehemu yalo iliyoinuka na, aliporudi Yerusalemu, akaripoti pato hilo kwa mkuu wake. Mwandiko huo ulitambuliwa mara hiyo kuwa wa Kifoinike na umaana wao ukatambuliwa. Royal Museum ya Berlin ikatoa pesa kununua jiwe hilo, lakini upesi vikundi vingine vyenye kupendezwa vikalishindania. Wakijua thamani ya kifaa chao chenye thamani, mashehe wenyeji wakakificha na kuongeza bei yacho kwa kadiri ambayo hakingeweza kununuliwa.

      Mchimbuzi mmoja wa vitu vya kale Mfaransa alifaulu kupata maandishi hayo kwenye karatasi iliyozungushwa na kukazwa sana kwenye jiwe hilo, lakini kwa kuwa karatasi hiyo iliyozungushwa kwa kukazwa sana ililazimika kunyakuliwa kabla haijakauka, ilikuwa vigumu kusoma maandishi yaliyoandikwa juu yayo. Kwa wakati uliopo, amri zilitoka Dameski kwamba Wabedui watoe jiwe lao kwa maofisa wa serikali. Badala ya kutii, Wabedui waliazimia kuliharibu. Kwa hiyo waliasha moto kuzunguka kisalio hicho chenye thamani kubwa na kukimwagilia maji kwa kurudia-rudia. Jiwe hilo lilipovunjika vipandevipande, vipande hivyo viligawanywa upesi-upesi miongoni mwa jamaa wenyeji viwekwe katika ghala zao, kwa wazi ili kuhakikisha baraka kwa ajili ya mavuno yao. Pia ilikuwa ndiyo njia bora zaidi kwa watu mmoja mmoja kupiga bei kibinafsi ya uuzaji wa vipande hivyo vilivyotawanyika.

      Historia ya Biblia Yawa Hai

      Kwa msaada wa miundo iliyofanyizwa kwa plasta na maandishi kwenye karatasi ya kuongezea vile vipande vilivyonunuliwa, hatimaye yale Maandishi kwenye lile jiwe hatimaye yalipatikana tena. Maandishi yote yalipofunuliwa, wasomi walistaajabu. Nguzo hiyo ya ukumbusho ya kale ilielezwa kuwa ndiyo “nguzo moja ya jiwe yenye kustaajabisha zaidi ya yote iliyopata kugunduliwa.”

      Mfalme Mesha wa Moabu alijengea mungu wake Kemoshi Jiwe la Moabu kuadhimisha kufaulu kwa Mesha kujiondoa katika utawala wa Israeli, ambao, asema, ulikuwa umeendelea kwa miaka 40 na uliruhusiwa na Kemoshi kwa sababu alikuwa “amekasirishwa na bara lake.” Kwa kawaida uasi huu wa Moabu unafikiriwa kuwa wahusiana na matukio yaliyoandikwa katika sura ya tatu ya 2 Wafalme. Kwenye nguzo hiyo ya ukumbusho, Mesha alijisifia kuwa mwanadini sana, kujenga majiji na barabara kuu moja, na kupata ushindi juu ya Israeli. Katika hayo, yeye ampa sifa yote Kemoshi Mungu wake. Kushindwa kwa Mesha na kudhabihiwa kwa mwana wake mwenyewe—kunakoripotiwa katika Biblia—hakukutiwa katika maandishi haya ya kujitukuza, kama vile mtu angetazamia.

      Mahali pengi palipoorodheshwa na Mesha kuwa mahali alipoteka pametajwa katika Biblia, miongoni mwa mahali hapo ni Medeba, Ataro-thi, Nebo, na Yahazi. Hivyo, jiwe hilo hutegemeza usahihi wa habari ya Biblia. Hata hivyo, jambo la kutokeza zaidi ni kutumiwa na Mesha kwa ile Tetragramatoni, YHWH, jina la Mungu wa Israeli, katika mstari wa 18 wa maandishi hayo. Hapo Mesha ajisifu hivi: “Mimi nilichukua [vyombo] vya Yahweh kutoka huko [Nebo], nikiviburuta [kuvileta] mbele ya Kemoshi.” Nje ya Biblia, pengine haya ndiyo maandishi ya mapema zaidi ya yote ya utumizi wa jina la kimungu.

      Katika 1873 lile Jiwe la Moabu lilirudishwa katika hali ya zamani, miundo ya plasta ya maandishi yaliyokosekana ikiwa imeongezwa, na likawekwa kuwa la maonyesho katika miusiamu (nyumba ya vitu vya ukumbusho) ya Louvre, Paris, ambapo limebaki. Nakala sahihi yalo yaweza kuonwa katika Miusiamu ya Uingereza, London.

      [Picha katika ukurasa wa 31]

      (Juu) Bara la Moabu

      [Hisani]

      Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

      (Kushoto) Jiwe la Moabu lililojengwa upya

      [Hisani]

      Musée du Louvre, Paris

      (Kulia) Ile Tetragramatoni kama inavyoonekana kwenye kifaa hicho

      [Hisani]

      The Bible in the British Museum

  • Je! Wewe Ni Sanamu ya Kujiabudu Mwenyewe?
    Mnara wa Mlinzi—1990 | Aprili 15
    • Je! Wewe Ni Sanamu ya Kujiabudu Mwenyewe?

      Bila kung’amua hivyo, binadamu fulani hujifanya wenyewe kuwa sanamu. Biblia hueleza kwenye Waefeso 5:5, NW: “Kwa kuwa mwajua hili, mkilitambua nyinyi wenyewe, kwamba hakuna mwasherati au mtu asiye safi au mtu mwenye pupa—ambalo lamaanisha kuwa mwabudu sanamu—aliye na urithi wowote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu.” (Wakolosai 3:5; linganisha Wagalatia 5:19-21.) Tamaa za kimnofu zaweza kuja katikati ya mtu na Mungu. Paulo asema juu ya hao kwamba “mungu wao ni tumbo.” (Wafilipi 3:18, 19) Kwa maneno mengine, wana “mungu” mwingine kando na Yehova, wakiweka kwanza tamaa zao za kimnofu. Mwenendo kama huo unaweza kumwondoa mtu katika Ufalme wa Mungu. (1 Wakorintho 6:9, 10) Basi, kuna sababu nzuri ya kutii maneno ya mtume Paulo: “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.”—1 Wakorintho 10:14.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki