-
Sayansi: Je! Imethibitisha Biblia Kuwa Yenye Makosa?Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
-
-
Sura 8
Sayansi: Je! Imethibitisha Biblia Kuwa Yenye Makosa?
Katika 1613 mwanasayansi Mwitalia Galileo alitangaza kitabu kinachoitwa “Letters on Sunspots.” Humo, alitokeza ushahidi wa kwamba dunia huenda ikilizunguka jua, badala ya jua kuizunguka dunia. Kwa kufanya hivyo alianzisha mfululizo wa matukio ambayo mwishowe yalimfikisha mbele ya Mahakama ya Katoliki ya Kuhukumu Wazushi kwa “shuku kali ya uzushi.” Hatimaye, alilazimishwa ‘atangue maneno yake.’ Ni kwa nini wazo hili kwamba dunia hufanya mwendo wa kulizunguka jua lilionwa kuwa uzushi? Kwa sababu washtaki wa Galileo walidai kwamba lilipinga yale inayosema Biblia.
1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Ilitukia nini Galileo alipodokeza kwamba dunia ilifanya mwendo wa kulizunguka jua? (b) Ingawa Biblia si kitabu cha mafundisho ya sayansi, twapata nini tunapoilinganisha na sayansi ya ki-siku-hizi?
YASHIKILIWA sana leo kwamba Biblia si ya kisayansi, na wengine huelekeza kwa yaliyompata Galileo kuthibitisha hilo. Lakini je! ndivyo ilivyo? Tunapojibu swali hilo, lazima tukumbuke kwamba Biblia ni kitabu cha unabii, historia, sala, sheria, shauri, na maarifa juu ya Mungu. Haidai kuwa kitabu cha mafundisho ya kisayansi. Hata hivyo, Biblia inapogusia mambo ya kisayansi, inayosema ni sahihi kabisa.
Sayari Yetu Dunia
2. Biblia yasimuliaje kituo cha dunia katika anga?
2 Kwa kielelezo, fikiria, inayosema Biblia juu ya sayari yetu, dunia. Katika kitabu cha Ayubu, twasoma: “[Mungu] hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.” Linganisha hayo na taarifa ya Isaya, anaposema: “Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia.” (Isaya 40:22) Wazo linalotolewa la dunia mviringo ‘iliyotundikwa pasipo kitu’ “nafasi isiyo na kitu” hutukumbusha kwa nguvu juu ya picha zinazopigwa na wanaanga za duara la dunia linaloelea katika anga isiyo na kitu.
3, 4. Mrudio wa maji wa dunia ni nini, na Biblia yasema nini juu ya hilo?
3 Pia, fikiria mrudio wa kustaajabisha wa maji. Hivi ndivyo Compton’s Encyclopedia kinavyoeleza yanayotukia: “Maji . . . huvukiza kutoka uso wa bahari mpaka kwenye anga . . . Mikondo ya hewa yenye kuzidi kusonga katika anga la dunia huipeleka hewa hiyo yenye unyevu barani. Hewa hiyo inapokuwa baridi, mvuke huganda kufanyiza matone ya maji. Kwa kawaida hayo huonekana kuwa mawingu. Mara nyingi matone hayo huungana kufanyiza matone ya mvua. Anga likiwa baridi vya kutosha, chembe za theluji hufanyika badala ya matone ya mvua. Vyovyote vile, maji ambayo yamesafiri mamia au hata maelfu ya kilometa kutoka baharini huanguka kwenye uso wa dunia. Hapo hukusanyika katika vijito au kupenya ndani ya udongo na kuanza safari yayo ya kurudi baharini.”1
4 Utaratibu huo wa kutokeza, unaofanya maisha kwenye nchi kavu yawezekane, ulielezwa vizuri miaka karibu 3,000 iliyopita katika semi sahili, za moja kwa moja: “Vijito vyote huenda katika bahari, hata hivyo bahari haifuriki kamwe; vijito huenda tena mahali vilipotoka.”—Mhubiri 1:7, The New English Bible.
5. Maelezo ya mtunga zaburi juu ya historia ya milima ya dunia ni ya kisasa kwa kutokeza jinsi gani?
5 Labda lililo la kutokeza hata zaidi ni mwono-ndani wa Biblia katika historia ya milima. Hivi ndivyo kitabu kimoja cha mafundisho juu ya jiolojia kinavyosema: “Tangu nyakati za Kabla ya Cambria kufikia wakati huu, utaratibu wa kudumu wa kujenga na kuangamiza milima umeendelea. . . . Si kwamba tu milima imetokea katika sakafu za bahari zilizotoweka, bali pia mara nyingi imezama muda mrefu baada ya kuundwa kwayo, na kisha kuinuliwa tena.”2 Linganisha hilo na lugha ya kishairi ya mtunga zaburi: “Uliifunika [dunia] kwa vilindi kama kwa vazi. Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, mpaka mahali ulipoyatengenezea.”—Zaburi 104:6, 8.
“Katika Mwanzo”
6. Ni taarifa gani ya Biblia inayopatana na nadharia za kisayansi za wakati huu juu ya chanzo cha ulimwengu wote mzima?
6 Mstari wa kwanza kabisa wa Biblia husema: “Katika mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.” (Mwanzo 1:1, NW) Mambo yaliyochunguzwa yameongoza wanasayansi watokeze nadharia kwamba ulimwengu wote mzima uonekanao kweli kweli ulikuwa na mwanzo. Haukuwapo tangu kale na kale. Mtaalamu wa elimu-nyota Robert Jastrow, mwagnosti katika mambo ya kidini, aliandika: “Habari zatofautiana, lakini mambo ya msingi katika masimulizi ya kielimu-nyota na ya kibiblia ya Mwanzo ni yale yale: mfululizo wa matukio wenye kuongoza kwa binadamu ulianza ghafula na kwa mshtuko katika punde fulani kamili ya wakati, katika mmweko wa nuru na nishati.”3
7, 8. Ingawa hawakubali yaliyotimizwa na Mungu katika jambo hilo, wanasayansi wengi wanalazimika kukubali nini kwa habari ya chanzo cha ulimwengu wote mzima?
7 Ni kweli, wanasayansi wengi, wajapoamini kwamba ulimwengu wote mzima ulikuwa na mwanzo, hawakubali taarifa ya kwamba “Mungu aliumba.” Hata hivyo, baadhi sasa hukubali kwamba ni vigumu kupuuza uthibitisho wa aina fulani ya akili iliyotokeza kila kitu. Freeman Dyson, Profesa wa fizikia aeleza hivi: “Kwa kadiri ninavyozidi kuuchunguza ulimwengu wote mzima na kujifunza habari za muundo wao, ndivyo ninavyoona uthibitisho zaidi kwamba tulikusudiwa tutokee.”
8 Dyson aendelea kukubali hivi: “Nikiwa mwanasayansi, aliyezoezwa tabia za kufikiri na lugha ya karne ya ishirini badala ya ile ya kumi na nane, sidai kwamba muundo wa ulimwengu wote mzima wathibitisha kuwapo kwa Mungu. Nadai tu kwamba muundo wa ulimwengu wote mzima wapatana na lile dhana ya kwamba akili hutimiza fungu muhimu katika kutenda kwayo.”4 Bila shaka maelezo yake yaonyesha mtazamo wenye shaka wa wakati wetu. Lakini tukiachana na utiaji shaka huo, mtu anaona kuna upatano kati ya sayansi ya ki-siku-hizi na taarifa ya Biblia kwamba “katika mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.”—Mwanzo 1:1, NW.
Afya na Usafi
9. Sheria ya Biblia juu ya maradhi ya ngozi yenye kuambukia yaonyeshaje hekima yenye kutumika? (Ayubu 12:9, 16a)
9 Fikiria mazungumzo ya Biblia juu ya uwanja mwingine: afya na usafi. Endapo Mwisraeli alikuwa na waa la ngozi lililotiliwa shaka kuwa ukoma, alitengwa na wengine. “Sikuzote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.” (Mambo ya Walawi 13:46) Hata mavazi yaliyoambukiwa yalichomwa. (Mambo ya Walawi 13:52) Katika siku hizo, hiyo ilikuwa njia iliyofanikiwa ya kuzuia kuenea kwa ambukizo hilo.
10. Wengi katika baadhi ya mabara wangefaidikaje kwa kufuata shauri la Biblia juu ya elimusiha?
10 Sheria nyingine ya maana ilihusu uondoaji wa takamwili (mavi) ya mwanadamu, ambayo ilipasa izikwe nje ya kambi. (Kumbukumbu la Torati 23:12, 13) Bila shaka sheria hiyo iliokoa Waisraeli na maradhi mengi. Hata leo, matatizo makubwa ya afya husababishwa katika mabara fulani na uondoaji usiofaa wa takamwili ya mwanadamu. Kama watu katika mabara hayo wangefuata tu sheria iliyoandikwa katika Biblia maelfu ya miaka iliyopita, wangekuwa wenye afya zaidi.
11. Ni shauri gani la Biblia juu ya afya ya kiakili limepatikana kuwa lenye kutumika?
11 Kiwango cha juu cha Biblia cha elimusiha (elimu ihusuyo afya) kilihusu pia afya ya kiakili. Mithali moja ya Biblia ilisema: “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; bali husuda ni ubovu wa mifupa.” (Mithali 14:30) Katika miaka ya karibuni, utafiti wa tiba umeonyesha kwamba kwa kweli afya yetu ya kimwili huathiriwa na mtazamo wetu wa kiakili. Kwa kielelezo, Daktari C. B. Thomas wa Johns Hopkins University alichunguza wahitimu zaidi ya elfu moja kwa kipindi cha miaka 16, akilinganisha tabia zao za kisaikolojia na kuambukiwa kwao na maradhi. Aliona jambo moja: Wahitimu walioambukiwa zaidi na maradhi walikuwa wale waliokuwa wenye kasirani zaidi na wenye wasiwasi zaidi chini ya mkazo.5
Biblia Husema Nini?
12. Ni kwa nini Kanisa Katoliki lilisisitiza kwamba nadharia ya Galileo juu ya dunia ilikuwa ni uzushi?
12 Ikiwa Biblia ni sahihi hivyo katika nyanja za kisayansi, ni kwa nini Kanisa Katoliki likasema fundisho la Galileo la kwamba dunia ilienda ikilizunguka jua halikuwa la kimaandiko? Kwa sababu ya namna ambavyo wenye mamlaka walifasiri mistari fulani ya Biblia.6 Je! walikuwa sahihi? Acheni tusome vifungu viwili walivyonukuu tuone.
13, 14. Kanisa Katoliki lilitumia vibaya mistari gani ya Biblia? Fafanua.
13 Kifungu kimoja chasema: “Jua huchomoza, jua hutua; kisha huharakisha kwenda mahali palo na hapo huchomoza.” (Mhubiri 1:5, The Jerusalem Bible) Kulingana na hoja ya Kanisa hilo, semi kama vile “jua huchomoza” na “jua hutua” humaanisha kwamba jua, wala si dunia, husonga. Lakini hata leo sisi husema kwamba jua huchomoza na kutua, na wengi wetu twajua kwamba dunia ndiyo husonga, si jua. Tunapotumia semi kama hizo, twafanya kueleza tu mwendo uonekanao wa jua kama ionekanavyo kwa mtazamaji wa kibinadamu. Mwandikaji wa Biblia alikuwa akifanya vivyo hivyo.
14 Kile kifungu kingine husema: “Wewe uliiimarisha dunia juu ya misingi yayo, isitikisike milele na milele.” (Zaburi 104:5, The Jerusalem Bible) Hilo lilifasiriwa kuwa lilimaanisha kwamba baada ya kuumbwa kwayo dunia haingeweza kusonga. Lakini, kwa kweli mstari huo hukazia udumifu wa dunia, wala si hali yayo ya kutosonga. Dunia haitapata kamwe ‘kutikiswa’ isiwepo, au kuangamizwa, kama inavyothibitishwa na mistari mingine ya Biblia. (Zaburi 37:29; Mhubiri 1:4) Andiko hili, pia, halihusu mwendo husianifu wa dunia na jua. Katika wakati wa Galileo, Kanisa, wala si Biblia, ndilo lililozuia mazungumzo huru ya kisayansi.
Mageuzi na Uumbaji
15. Nadharia ya mageuzi ni nini, nayo yapingaje Biblia?
15 Hata hivyo, kuna eneo ambalo wengi wangesema kwamba sayansi ya ki-siku-hizi na Biblia zapingana kabisa. Wanasayansi walio wengi huamini nadharia ya mageuzi, inayofundisha kwamba vitu vyote vilivyo hai viligeuka-geuka kutoka namna ya uhai iliyo sahili iliyokuja kuwapo mamilioni ya miaka iliyopita. Kwa upande mwingine, Biblia hufundisha kwamba kila kikundi kikubwa cha vitu vilivyo hai kiliumbwa kwa njia ya pekee na huzaa “kwa jinsi yake” tu. Husema binadamu aliumbwa “kwa mavumbi ya ardhi.” (Mwanzo 1:21; 2:7) Je! hilo ni kosa katika Biblia linaloonyeshwa wazi kabisa kisayansi? Kabla ya kuamua, acheni tutazame kwa uangalifu zaidi yale ambayo sayansi yajua, kinyume cha yale ambayo yatokeza kuwa nadharia.
16-18. (a) Ni uchunguzi gani mmoja aliofanya Charles Darwin ambao ulimwongoza aamini mageuzi? (b) Twaweza kutoaje hoja kwamba alichochunguza Darwin katika Visiwa Galápagos hakipingi inayosema Biblia?
16 Nadharia ya mageuzi ilifanywa na Charles Darwin kuwa maarufu wakati wa karne iliyopita. Alipokuwa kwenye Visiwa Galápagos katika Pasifiki, Darwin alivutiwa sana na namna tofauti za ndege-chiriku kwenye visiwa tofauti, ambao, yeye alikata kauli, lazima wawe walitokana na namna moja tu ya wazazi wa kale. Kwa sehemu, kwa sababu ya uchunguzi huo, alikuza nadharia ya kwamba vitu vyote vilivyo hai vimetoka kwa umbo moja sahili la awali. Yeye alisisitiza kwamba nguvu yenye kuongoza kwenye mageuzi ya viumbe vya juu kutoka kwa vile vya chini, ilikuwa ni uteuzi wa asili, kuokoka kwa vyenye nguvu zaidi. Akadai kupitia mageuzi, wanyama wa bara walisitawi kutoka kwa samaki, nyuni kutoka kwa jamii ya watambaachi, na kadhalika.
17 Kwa kweli, kile ambacho Darwin alichunguza katika visiwa hivyo hakikuwa kisichopatana na Biblia, ambayo huruhusu kuwapo kwa namna-namna ndani ya aina moja kubwa iliyo hai. Kwa kielelezo, jamii zote za ainabinadamu zilitokana na wanadamu wawili wa kwanza tu. (Mwanzo 2:7, 22-24) Kwa hiyo si jambo geni kwamba namna zote hizo za ndege-chiriku zingetokana na namna moja ya wazazi wa kale. Lakini waliendelea kuwa ndege-chiriku. Hawakugeuka kuwa mwewe au tai.
18 Wala namna mbalimbali za ndege-chiriku wala kingine chochote alichoona Darwin hakikuthibitisha kwamba vitu vyote vilivyo hai, iwe ni papa au shakwe, tembo au nyungunyungu, vilikuwa na mzazi mmoja wa kale. Hata hivyo, wanasayansi wengi husisitiza kwamba mageuzi si nadharia tena bali ni uhakika. Wengine, wajapotambua matatizo ya nadharia hiyo, husema kwamba wanaiamini vyovyote vile. Ni jambo la umaarufu kufanya hivyo. Hata hivyo, sisi twahitaji kujua kama mageuzi yamethibitishwa kwa kadiri ambayo lazima Biblia iwe imekosea.
Je! Yamethibitishwa?
19. Vizibiti huunga mkono mageuzi au Biblia?
19 Nadharia ya mageuzi yaweza kutiwaje kwenye mtihani? Njia iliyo wazi kabisa ni kuchunguza vizibiti ili kuona kama badiliko la hatua kwa hatua kutoka aina moja mpaka nyingine lilitukia kweli kweli. Je! lilitukia? La, sawa na ambavyo idadi fulani ya wanasayansi inakubali kwa kufuatia haki. Mmoja, Francis Hitching, aandika: “Unapotazama uone viunzi kati ya vikundi vikubwa vya wanyama, havipo kamwe.”7 Ukosefu huo wa uthibitisho katika kumbukumbu ya vizibiti uko wazi sana hivi kwamba wanamageuzi wametokeza nadharia zilizo badala ya ile ya Darwin ya badiliko la hatua kwa hatua. Lakini, ukweli ni kwamba kutokea kwa ghafula kwa aina za wanyama katika vizibiti kwaunga mkono uumbaji wa kipekee zaidi sana kushinda mageuzi.
20. Ni kwa nini jinsi ambayo chembe-chembe zilizo hai huzaana hairuhusu mageuzi kutukia?
20 Zaidi ya hayo, Hitching aonyesha kwamba viumbe vilivyo hai vimeamriwa vizae vingine vinavyofanana navyo kabisa badala ya kugeuka kuwa kitu kingine. Asema: “Chembe-chembe zilizo hai hujinakili kwa ufanano unaokaribiana kabisa. Kiwango cha kosa ni kidogo sana hivi kwamba hakuna mashine yoyote iliyoundwa na binadamu iwezayo kukikaribia. Pia kuna mipaka ya kindani iliyofanyizwa. Mimea hufikia ukubwa fulani na kukataa kukua zaidi. Nzi wa matunda hukataa kuwa kitu kingine ila tu nzi wa matunda katika hali zozote zilizobuniwa.”8 Mageuzi ya kutokeza hitilafu yaliyochochewa na wanasayansi katika nzi wa matunda kwa makumi ya miaka yameshindwa kuwalazimisha wageuke kuwa kitu kingine.
Chanzo cha Uhai
21. Ni mkataa gani uliothibitishwa na Louis Pasteur unaotokeza tatizo kubwa kwa wanamageuzi?
21 Swali jingine lenye kusumbua ambalo wanamageuzi wameshindwa kujibu ni: Chanzo cha uhai kilikuwa nini? Aina ya uhai ya kwanza iliyo sahili—ambayo sisi sote twapaswa kuwa tulitokana nalo—ilikujaje kuwapo? Karne nyingi zilizopita, hilo halingalionekana kuwa tatizo. Wakati huo watu walio wengi walifikiri kwamba nzi wangeweza kusitawi kutokana na nyama yenye kuoza na kwamba rundo la matambara lingeweza lenyewe kutokeza panya. Lakini, miaka zaidi ya mia moja iliyopita, mwanakemia Mfaransa Louis Pasteur alionyesha waziwazi kwamba uhai waweza kutoka tu kwa uhai uliotangulia kuwapo.
22, 23. Kulingana na wanamageuzi, uhai ulianzaje, lakini mambo ya hakika yaonyesha nini?
22 Kwa hiyo wanamageuzi hufafanuaje chanzo cha uhai? Kulingana na nadharia yenye kupendwa na wengi, muungano wa nasibu wa kemikali na nishati ulitokeza kizazi cha uhai chenye kujifanyiza chenyewe tu mamilioni ya miaka iliyopita. Vipi juu ya kanuni ile aliyothibitisha Pasteur? The World Book Encyclopedia chaeleza: “Pasteur alionyesha kwamba uhai hauwezi kujifanyiza wenyewe tu chini ya hali za kemikali na fizikia zilizopo duniani leo. Hata hivyo, mabilioni ya miaka iliyopita, hali za kemikali na fizikia duniani zilikuwa tofauti sana”!9
23 Hata hivyo, chini ya hali tofauti sana kuna pengo kubwa kati ya mata ambayo haiko hai na kitu sahili zaidi kilicho hai. Michael Denton, katika kitabu chake Evolution: A Theory in Crisis, asema: “Kati ya chembe-chembe iliyo hai na mfumo usio wa kibayolojia wenye utaratibu wa juu zaidi, kama vile fuwele au chembe ya theluji, kuna shimo kubwa sana na pana kwa kadiri iwezekanayo kuwaziwa.”10 Wazo la kwamba kitu kisicho na uhai kingeweza kuja kuishi kwa nasibu fulani ya kihobelahobela ni dogo mno hivi kwamba ni lisilowezekana. Maelezo ya Biblia, kwamba ‘uhai ulitoka kwa uhai’ ikimaanisha kwamba uhai uliumbwa na Mungu, yanapatana kabisa na mambo ya hakika.
Kwa Nini Si Uumbaji
24. Nadharia hiyo ijapokuwa na matatizo, ni kwa nini wanasayansi walio wengi wangali wanashikilia nadharia ya mageuzi?
24 Ijapokuwa matatizo yanayoambatana na nadharia ya mageuzi, imani katika uumbaji huonwa leo kuwa isiyo ya kisayansi, hata kuwa ya kiajabu-ajabu. Ni kwa nini? Ni kwa nini hata mtaalamu kama Francis Hitching, ambaye kwa kufuatia haki anaonyesha udhaifu wa mageuzi, anakataa wazo la uumbaji?11 Michael Denton aeleza kwamba mageuzi, yajapokuwa na kasoro, yataendelea kufunzwa kwa sababu nadharia zinazohusiana na uumbaji “kwa wazi hutolea dua wafanyizaji wenye nguvu zinazozidi zile za kawaida.”12 Ndiyo kusema, uhakika wa kwamba uumbaji watia ndani Muumba waufanya uwe usiokubalika. Hakika, huko ndiko kusababu kulikoenea tulikokabili katika kisa cha miujiza: Miujiza haiwezekani kwa sababu ni ya kimwujiza!
25. Kisayansi, ni udhaifu gani wa mageuzi, unaoonyesha kwamba mageuzi si jambo linalostahili kuchukua mahali pa uumbaji katika kueleza chanzo cha uhai?
25 Isitoshe, nadharia ya mageuzi yenyewe inatatizika sana kwa maoni ya kisayansi. Michael Denton aendelea kusema: “Hiyo ikiwa kwa msingi ni nadharia ya kuwazia yaliyotukia kihistoria, haiwezekani kuhakikisha [nadharia ya Darwin] kwa kufanya jaribio au kuchunguza moja kwa moja kama ilivyo kawaida ya sayansi. . . . Zaidi ya hayo, nadharia ya mageuzi hushughulika na mfululizo wa matukio yasiyo ya kawaida, chanzo cha uhai, chanzo cha akili na kadhalika. Matukio yasiyo ya kawaida hayawezi kurudiwa na hayawezi kufanyiwa uchunguzi wowote wa kuyajaribu.”13 Ukweli ni kwamba nadharia ya mageuzi, ijapopendwa na wengi, imejaa mapengo na matatizo. Haitoi sababu nzuri ya kukataa simulizi la Biblia la chanzo cha uhai. Sura ya kwanza ya Mwanzo yatoa simulizi lenye sababu nzuri kabisa juu ya jinsi ‘matukio hayo yasiyo ya kawaida yasiyoweza kurudiwa’ yalivyokuja kutukia wakati wa “siku” za uumbaji ambazo zilihusisha mamileani ya wakati.a
Vipi Juu ya Furiko?
26, 27. (a) Biblia yasema nini juu ya Furiko? (b) Kwa sehemu, lazima maji ya furiko hilo yawe yalitoka wapi?
26 Wengi huelekeza kwenye jambo jingine linalodhaniwa kuwa ni kupingana kati ya Biblia na sayansi ya ki-siku-hizi. Katika kitabu cha Mwanzo, twasoma kwamba maelfu ya miaka iliyopita uovu wa binadamu ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba Mungu akaazimia kuwaharibu. Hata hivyo, aliagiza yule binadamu mwadilifu Nuhu ajenge chombo kikubwa cha mbao, safina. Kisha Mungu akaleta furiko juu ya ainabinadamu. Ni Nuhu na familia yake tu waliookoka, pamoja na viwakilishi vya namna-namna za wanyama. Furiko hilo lilikuwa kubwa sana hivi kwamba “milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa.”—Mwanzo 7:19.
27 Maji hayo yote yaliyofunika dunia yote yalitoka wapi? Biblia yenyewe yajibu. Mapema katika utendaji wa uumbaji, eneo la angahewa lilipoanza kuumbika, kulikuja kuwa “maji yaliyo chini ya anga” na “maji yaliyo juu ya anga.” (Mwanzo 1:7; 2 Petro 3:5) Furiko lilipokuja, Biblia yasema: “Madirisha ya mbinguni yakafunguka.” (Mwanzo 7:11) Bila shaka, “maji yaliyo juu ya anga” yalianguka na kutoa mengi ya maji yaliyofunikiza.
28. Watumishi wa kale wa Mungu, kutia ndani Yesu, walionaje Furiko hilo?
28 Vitabu vya ki-siku-hizi vya mafundisho vyaelekea kukanusha furiko la ulimwengu wote mzima. Kwa hiyo lazima tuulize: Je! Furiko hilo ni ngano tu, au je! lilitukia kikweli? Kabla ya kujibu hilo, twapaswa kuangalia kwamba waabudu wa baadaye wa Yehova walikubali Furiko kuwa historia ya kweli; hawakuliona kuwa ngano. Isaya, Yesu, Paulo, na Petro walikuwa kati ya wale waliolirejezea kuwa kitu kilichotukia kikweli. (Isaya 54:9; Mathayo 24:37-39; Waebrania 11:7; 1 Petro 3:20, 21; 2 Petro 2:5; 3:5-7) Lakini kuna maswali ambayo lazima yajibiwe juu ya Gharika ya ulimwengu wote mzima.
Maji ya Furiko
29, 30. Ni mambo gani ya hakika juu ya ugavi-maji wa dunia huonyesha kwamba Furiko hilo lasadikisha?
29 Kwanza, je! wazo la dunia yote kufurikwa ni la kutilika shaka? Sivyo. Kwa kweli, kwa kadiri fulani dunia ingali imefurikwa. Asilimia 70 yayo imefunikwa na maji na ni asilimia 30 pekee iliyo nchi kavu. Na zaidi, asilimia 75 ya maji yote yasiyo na chumvi ya dunia yamegandamana katika barafuto (mitiririko mikubwa ya barafu) na katika ncha za dunia zenye barafu. Kama barafu hii yote ingeyeyuka, usawa wa bahari ungeinuka zaidi sana. Majiji kama New York na Tokyo yangetoweka.
30 Na zaidi, The New Encyclopædia Britannica chasema: “Kina cha wastani cha bahari zote kimekadiriwa kuwa meta 3,790, tarakimu iliyo juu sana zaidi ya ile ya mwinuko wa wastani wa nchi kavu juu ya usawa wa bahari, ambao ni meta 840. Kina cha wastani kikizidishwa na eneo lacho la uso, mjao wa Bahari ya Ulimwengu ni mara 11 ya mjao wa nchi kavu iliyo juu ya usawa wa bahari.”14 Kwa hiyo, kama kila kitu kingelainishwa—kama milima ingefanywa kuwa tambarare na mabonde ya bahari ya kina kirefu kujazwa—bahari ingefunika dunia yote kufikia kina cha maelfu ya meta.
31. (a) Ili Furiko hilo liwe lilitukia, lazima hali ya dunia ya kabla ya Furiko iwe ilikuwaje? (b) Ni nini kinachoonyesha yawezekana kwamba milima ilikuwa chini zaidi na kwamba mabonde ya bahari yalikuwa ya kina kifupi zaidi kabla ya Furiko hilo?
31 Ili iwe Furiko lilitukia, mabonde ya kabla ya Furiko lazima yawe yalikuwa ya kina kifupi zaidi, na milima kuwa ya chini zaidi ya ilivyo sasa. Je! hilo lawezekana? Kitabu kimoja cha mafundisho chasema: “Ingawa milima ya ulimwengu yainuka urefu mkubwa sana sasa, wakati mmoja, mamilioni ya miaka iliyopita, bahari na nyanda zilinyooka zikiwa tambarare hali moja. . . . Kusonga kwa mabamba ya miamba ya kontinenti husababisha nchi kavu kuinuka kufikia urefu ambao ni wanyama na mimea yenye uvumilivu zaidi yaweza kuishi na, kwa upande ule mwingine, hutumbukia na kukaa katika uzuri uliofichwa kina kirefu chini ya sakafu ya bahari.”15 Kwa kuwa milima na mabonde ya bahari huinuka na kushuka, ni wazi kwamba wakati mmoja milima haikuwa mirefu kama ilivyo sasa na mabonde ya bahari kuu hayakuwa ya kina kirefu hivi.
32. Lazima kuwe kulitukia nini kwa maji ya Furiko? Fafanua.
32 Kulitukia nini kwa maji ya furiko baada ya Furiko hilo? Lazima yawe yaliingia katika mabonde ya bahari. Jinsi gani? Wanasayansi huamini kwamba kontinenti hukalia mabamba ya miamba mikubwa. Kusonga kwa mabamba ya miamba hiyo kwaweza kusababisha mabadiliko katika usawa wa uso wa dunia. Katika sehemu fulani leo, kuna mashimo makubwa sana ya chini ya maji yenye kina cha zaidi ya kilometa kumi kwenye mipaka ya mabamba ya miamba hiyo.16 Yawezekana sana kwamba—labda kwa kusababishwa na Furiko hilo lenyewe—mabamba ya miamba hiyo yalisonga, sakafu ya bahari ikazama, na mitaro hiyo mikubwa ikafunguka, hivyo kuruhusu maji yabubujike kutoka nchi kavu.b
Alama za Furiko?
33, 34. (a) Tayari wanasayansi wana uthibitisho gani ambao waweza kuwa ni uthibitisho wa Furiko hilo? (b) Je! ni jambo la kufikiri kuzuri kusema kwamba yawezekana wanasayansi wanafasiri kimakosa uthibitisho huo?
33 Tukikubali kwamba furiko kubwa lingeweza kuwa lilitukia, ni kwa nini wanasayansi hawajaona alama yoyote yalo? Labda wameona, lakini wanafasiri uthibitisho huo kwa njia nyingine. Kwa kielelezo, sayansi inayokubaliwa na wengi hufundisha kwamba uso wa dunia umeundwa katika sehemu nyingi na barafuto zenye nguvu wakati wa mfululizo wa enzi za barafu. Lakini uthibitisho ulio wazi wa utendaji wa barafuto nyakati nyingine waweza kuwa ni tokeo la tendo la maji. Basi, yaelekea sana, baadhi ya uthibitisho wa Furiko unafasiriwa kimakosa kuwa ni uthibitisho wa enzi ya barafu.
34 Makosa kama hayo yamefanywa. Kuhusu wakati ambao wanasayansi walipokuwa wakisitawisha nadharia ya enzi za barafu, twasoma: “Walikuwa wakipata enzi za barafu kwenye kila hatua ya historia ya jiolojia, kwa kufuatia falsafa ya ufanano. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni uchunguzi mpya wa uangalifu juu ya uthibitisho huo, umekanusha nyingi za enzi hizi za barafu; maumbo ambayo wakati mmoja yalitambulishwa kuwa kokoto iliyorundikwa na barafuto imefasiriwa tena kuwa matuta yaliyotandikwa na mtiririko wa tope, maporomoko ya ardhi iliyofunikwa na maji na mikondo yenye tope: maporomoko ya maji yenye tope yanayopeleka changarawe, mchanga na kokoto kwenye sakafu ya bahari yenye kina kirefu.”18
35, 36. Ni uthibitisho gani katika vizibiti na katika jiolojia unaoweza kuwa wahusiana na Furiko hilo? Fafanua.
35 Uthibitisho mwingine wa Furiko waonekana upo katika vizibiti. Wakati mmoja, kulingana na kizibiti hiki, simba-milia wakubwa wenye meno mawili yaliyochomoza waliotea-otea mawindo yao katika Ulaya, farasi wakubwa zaidi ya wowote walio hai sasa walizunguka-zunguka Amerika Kaskazini, na tembo-majitu walitafuta-tafuta chakula katika Siberia. Kisha, ulimwenguni pote, namna-namna za wanyama wanyonyeshao (mamalia) zikatoweka. Wakati uo huo, kulikuwako badiliko la ghafula la hali ya tabia ya nchi. Makumi ya maelfu ya tembo-majitu yaliuawa na kugandishwa upesi katika Siberia.c Alfred Wallace, mrika wa Charles Darwin ajulikanaye sana, alionelea kwamba uharibifu huo mkubwa lazima uwe ulisababishwa na tukio fulani la ulimwengu lisilo la kawaida.19 Wengi wametoa hoja kwamba tukio hilo lilikuwa ni Furiko.
36 Makala moja ya mhariri katika gazeti Biblical Archaeologist ilionelea hivi: “Ni jambo la maana kukumbuka kwamba hadithi ya furiko kubwa ni mojawapo mapokeo yaliyoenea sana katika utamaduni wa kibinadamu . . . Hata hivyo kisababishi cha mapokeo ya kale zaidi yanayopatikana katika vyanzo vya Mashariki ya Karibu, yawezekana sana kuwako na furiko halisi la viwango vikubwa la wakati wa tarehe mojawapo vipindi vya mvua nyingi . . . maelfu ya miaka mingi iliyopita.”20 Vipindi hivyo vya mvua nyingi vilikuwa nyakati ambapo uso wa dunia ulikuwa umelowa zaidi ya ulivyo sasa. Maji yasiyo na chumvi ya maziwa kuzunguka ulimwengu yalikuwa makubwa zaidi. Nadharia moja hutolewa kwamba uowevu huo ulisababishwa na mvua kubwa zilizoshirikishwa na mwisho wa enzi za barafu. Lakini wengine wamedokeza kwamba katika pindi moja uowevu mkubwa wa uso wa dunia ulikuwa ni tokeo la Furiko.
Ainabinadamu Haikusahau
37, 38. Mwanasayansi mmoja aonyeshaje kwamba, kulingana na uthibitisho, yaelekea kuwa Furiko hilo lilitukia, nasi twajuaje lilitukia?
37 Profesa wa jiolojia John McCampbell aliandika hivi wakati mmoja: “Tofauti za msingi kati ya msiba [lile Furiko] na ufanano wa kimageuzi hazihusu data ya hakika ya jiolojia bali mafasirio ya data hizo. Ufasiri unaopendelewa utategemea kwa kadiri kubwa malezi na dhana za kimbele za mwanafunzi mmoja mmoja.”21
38 Kwamba Furiko lilipata kutukia yaonyeshwa na uhakika wa kwamba ainabinadamu haikulisahau. Ulimwenguni pote, katika sehemu zilizo mbali mbali kama vile Alaska na Visiwa vya Bahari ya Kusini, kuna hadithi za kale juu yalo. Wazaliwa wa Amerika wa staarabu za kabla ya Columbus, na pia Waaborijini wa Australia, wote wana hadithi juu ya Furiko hilo. Ingawa baadhi ya masimulizi hayo hutofautiana katika vijambo vidogo, uhakika wa msingi kwamba dunia ilifurikwa na ni wanadamu wachache tu waliookolewa katika chombo kilichotengenezwa na binadamu huonekana karibu katika namna zote. Sababu pekee ya ukubali huo ulioenea sana ni kwamba Furiko hilo lilikuwa tukio la kihistoria.d
39. Ni uthibitisho gani wa ziada ambao tumeona wa uhakika wa kwamba Biblia ni Neno la Mungu, si la binadamu?
39 Hivyo, katika mambo ya msingi Biblia yapatana na sayansi ya ki-siku-hizi. Kunapokuwa mgongano kati ya hizo mbili, uthibitisho wa wanasayansi watilika shaka. Zinapokubaliana, mara nyingi Biblia inakuwa sahihi sana hivi kwamba twapaswa kuamini ilipata habari zayo kutoka kwa akili inayozidi uwezo wa mwanadamu. Kweli kweli, kukubaliana kwa Biblia na sayansi iliyothibitishwa kwatoa ushuhuda zaidi kwamba hiyo ni Neno la Mungu, si la binadamu.
-
-
Unabii Mwingi UliotimizwaBiblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
-
-
Sura 9
Unabii Mwingi Uliotimizwa
Wanadamu hawawezi kutabiri wakati ujao kwa uhakika wowote. Tena na tena jitihada zao za kubashiri hushindwa vibaya sana. Kwa hiyo kitabu cha unabii mwingi uliotimia lazima kivute fikira zetu. Biblia ni kitabu cha namna hiyo.
1. (Tia ndani utangulizi.) Ni nini kinachothibitishwa na uhakika wa kwamba Biblia huandika unabii mwingi uliotimia?
UNABII mwingi wa Biblia umetimia katika vijambo vidogo hivi kwamba wahakiki hudai uliandikwa baada ya utimizo. Lakini madai hayo si ya kweli. Mungu, akiwa mweza yote, aweza kabisa kutabiri. (Isaya 41:21-26; 42:8, 9; 46:8-10) Unabii mwingi wa Kibiblia uliotimia ni uthibitisho wa upulizio wa kimungu, wala si utungaji wa baadaye. Sasa tutaangalia baadhi ya unabii mwingi wenye kutokeza uliotimia—unaotoa thibitisho la ziada kwamba Biblia ni neno la Mungu, si la binadamu tu.
Uhamisho Katika Babuloni
2, 3. Ni nini kilichoongoza kwenye Mfalme Hezekia kuonyesha wajumbe kutoka Babuloni hazina zote za nyumba na enzi yake?
2 Hezekia alikuwa mfalme katika Yerusalemu kwa miaka 30 hivi. Katika 740 K.W.K. alikuwa shahidi wa uharibifu wa Israeli jirani yake wa kaskazini mikononi mwa Ashuru. Katika 732 K.W.K. aliona uwezo wenye kuokoa wa Mungu, wakati jaribio la Kiashuri la kuteka Yerusalemu liliposhindwa, kukiwa na matokeo yenye msiba kwa mvamizi huyo.—Isaya 37:33-38.
3 Sasa, Hezekia anapokea ujumbe kutoka Merodaki-baladani, mfalme wa Babuloni. Kijuu-juu, mabalozi hao wamekuja kumpongeza Hezekia kwa ajili ya kupata nafuu kwa ugonjwa wake mkubwa. Ingawa hivyo, yaelekea, Merodaki-baladani amwona Hezekia kuwa aweza kujiunga naye kupigana na mamlaka ya ulimwengu ya Ashuru. Hezekia hafanyi lolote kuondoa wazo hilo anapowaonyesha Wababuloni hao wenye kutembelea utajiri wote wa nyumba na enzi yake. Labda yeye, pia, ataka mataifa ya muungano ili kupingana na Waashuri ambao yawezekana warudi.—Isaya 39:1, 2.
4. Isaya alitoa unabii wa tokeo gani lenye msiba la kosa la Hezekia?
4 Isaya ndiye nabii wa kutokeza wa wakati huo, na upesi atambua juu ya kukosa busara kwa Hezekia. Ajua kwamba kinga hakika zaidi ya Hezekia ni Yehova, wala si Babuloni, naye amwambia kwamba tendo lake la kuonyesha Wababuloni utajiri wake litaongoza kwenye tanzia. “Siku zinakuja,” asema Isaya, “ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli.” Yehova aliamuru: “Hapana kitu cho chote kitakachosalia.”—Isaya 39:5, 6.
5, 6. (a) Yeremia alisema nini katika kuthibitisha unabii wa Isaya? (b) Unabii mwingi wa Isaya na Yeremia ulitimizwa katika njia gani?
5 Nyuma katika karne ya nane K.W.K., huenda ikawa ilionekana haielekei unabii huo utatimia. Hata hivyo, miaka mia moja baadaye, hali ilibadilika. Babuloni ilichukua mahali pa Ashuru kuwa mamlaka ya ulimwengu yenye kutawala, na Yuda ikafisidika sana kidini, hivi kwamba Mungu akaondoa baraka yake. Sasa, nabii mwingine, Yeremia, alipuliziwa na Mungu arudie onyo la Isaya. Yeremia alitangaza hivi: “Nitawaleta [Wababuloni] juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake . . . Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.”—Yeremia 25:9, 11.
6 Miaka minne hivi baada ya Yeremia kutoa unabii huo, Wababuloni walifanya Yuda kuwa sehemu ya milki yao. Miaka mitatu baada ya hilo, walichukua mateka fulani wa Kiyahudi, pamoja na baadhi ya utajiri wa hekalu katika Yerusalemu, mpaka Babuloni. Miaka minane baadaye, Yuda iliasi na kwa mara nyingine ikavamiwa na Nebukadreza, mfalme wa Babuloni. Pindi hii, jiji hilo na hekalu lalo viliharibiwa. Utajiri walo wote, na Wayahudi wenyewe, walipelekwa mpaka Babuloni iliyo mbali, sawa na vile Isaya na Yeremia walivyokuwa wametabiri.—2 Mambo ya Nyakati 36:6, 7, 12, 13, 17-21.
7. Akiolojia yashuhudiaje utimizo wa unabii mwingi wa Isaya na Yeremia kuhusu Yerusalemu?
7 The Archaeological Encyclopedia of the Holy Land chasema kwamba wakati shambulizi la Kibabuloni lilipokwisha, “uharibifu wa jiji [Yerusalemu] ulikuwa kamili.”1 Mwakiolojia W. F. Albright asema: “Machimbuzi na uchunguzi wa sura ya nchi katika Yuda vimethibitisha kwamba miji ya Yuda haikuharibiwa kikamili tu na Wakaldayo katika mavamizi yao mawili, bali pia haikukaliwa tena kwa vizazi—kamwe tena katika historia.”2 Hivyo, akiolojia yathibitisha utimizo wenye kushtua wa unabii huu.
Yaliyopata Tiro
8, 9. Ezekieli alitamka unabii gani juu ya Tiro?
8 Ezekieli alikuwa mwandikaji mwingine wa kale aliyeandika unabii mwingi uliopuliziwa kimungu. Yeye alitoa unabii kuanzia mwisho wa karne ya saba K.W.K. kuendelea mpaka ya sita—yaani, wakati wa miaka iliyoongoza mpaka kwenye kuharibiwa kwa Yerusalemu na kisha wakati wa makumi ya miaka ya kwanza ya uhamisho wa Wayahudi katika Babuloni. Hata wahakiki fulani wa ki-siku-hizi hukubali kwamba kitabu hicho kiliandikwa karibu na wakati huo.
9 Ezekieli aliandika unabii wenye kutokeza juu ya kuharibiwa kwa Tiro, jirani ya kaskazini ya Israeli, lililokuwa limeacha urafiki na watu wa Mungu na kuwa adui. (1 Wafalme 5:1-9; Zaburi 83:2-8) Aliandika: “Bwana MUNGU [Yehova, NW] asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake. Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu. . . . Nao wataweka mawe yako, na miti yako, na mavumbi yako, kati ya maji.”—Ezekieli 26:3, 4, 12.
10-12. Unabii wa Ezekieli ulitimizwa lini mwishowe, na jinsi gani?
10 Je! hilo lilitukia kweli? Miaka michache baada ya Ezekieli kutoa unabii huo, mfalme wa Babuloni, Nebukadreza, alizingira Tiro. (Ezekieli 29:17, 18) Hata hivyo, hayakuwa mazingiwa rahisi. Kwa sehemu, Tiro lilikuwa kwenye bara (sehemu inayoitwa Tiro la kale). Lakini sehemu ya jiji hilo ilikuwa kwenye kisiwa karibu meta 800 ndani ya bahari kutoka ufuoni. Nebukadreza alizingira kisiwa hicho kwa miaka 13 ndipo kikajitiisha kwake.
11 Hata hivyo, ilikuwa katika 332 K.W.K. kwamba unabii wa Ezekieli ulipotimizwa hatimaye katika vijambo vyote vidogo. Wakati huo, Aleksanda Mkuu, yule mshindi kutoka Makedonia, alikuwa akivamia Asia. Tiro, likiwa salama kwenye kituo chalo cha kisiwani, lilisimama dhidi yake. Aleksanda hakutaka kuacha nyuma yeyote ambaye angeweza kuwa adui, lakini hakutaka kutumia miaka mingi katika kuzingira Tiro, kama alivyokuwa amefanya Nebukadreza.
12 Alitatuaje tatizo lake la kijeshi? Alijenga daraja la ardhi, au barabara ya baharini, kuvuka mpaka kwenye kisiwa hicho, ili askari zake waweze kuvuka na kushambulia jiji hilo la kisiwani. Ingawa hivyo, ona alichotumia kujenga barabara hiyo ya baharini. The Encyclopedia Americana charipoti: “Kwa vifusi vya sehemu ya bara ya jiji hilo, alilokuwa amebomoa, alijenga barabara kubwa ya baharini katika 322 ili kuunganisha kisiwa na bara.” Baada ya mazingiwa ya muda mfupi kwa kulinganisha, jiji hilo la kisiwani likaharibiwa. Zaidi ya hayo, unabii wa Ezekieli ulitimizwa katika vijambo vyao vidogo vyote. Hata ‘mawe na miti na mavumbi’ vya Tiro la Kale ‘viliwekwa kati ya maji.’
13. Msafiri mmoja wa karne ya 19 alielezaje juu ya mahali lilipokuwa Tiro la kale?
13 Msafiri mmoja wa karne ya 19 alieleza juu ya kilichokuwa kimesalia cha Tiro la kale katika siku yake, akisema: “Kati ya Tiro la awali lililojulikana na Sulemani na manabii wa Israeli, hakuna baki linalosalia isipokuwa katika makaburi yalo yaliyochongwa kwenye kando za mlima, na katika kuta za msingi . . . Hata kisiwa, ambacho Aleksanda Mkuu, katika mazingiwa yake ya mji, aligeuza kuwa rasi kwa kujaza maji kati yalo na bara, hakina aathari (masalio) za kipindi cha kale kuliko kile cha zile Krusedi. Mji wa ki-siku-hizi, ambao kwa kulinganisha ni mpya sana, unakalia nusu ya kaskazini ya ambacho wakati mmoja kilikuwa kisiwa, huku karibu baki jingine lote la eneo hilo likiwa limefunikwa na magofu yasiyotambulika.”3
Zamu ya Babuloni
14, 15. Isaya na Yeremia waliandika unabii gani mwingi juu ya Babuloni?
14 Nyuma katika karne ya nane K.W.K., Isaya, nabii aliyeonya Wayahudi juu ya kutiishwa kwao na Babuloni kulikokuwa kunakuja, alitabiri pia jambo lenye kustaajabisha sana: kuangamizwa kikamili kwa Babuloni lenyewe. Yeye alitabiri hilo kwa maelezo ya waziwazi: “Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao . . . Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi.”—Isaya 13:17-20.
15 Pia nabii Yeremia alitabiri anguko la Babuloni, ambalo lingetukia miaka mingi baadaye. Naye alitia ndani habari moja ndogo ya kupendeza: “Ukosefu wa mvua [ukiwa, NW] u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa. . . . Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana; wanakaa katika ngome zao. Ushujaa wao umewapungukia.”—Yeremia 50:38; 51:30.
16. Babuloni lilishindwa lini, na nani?
16 Katika 539 K.W.K., wakati wa utawala wa Babuloni ikiwa mamlaka kuu ya ulimwengu ulifikia mwisho wakati Koreshi, mtawala Mwajemi mwenye nguvu nyingi, akiandamana na jeshi la Umedi, alipokuja dhidi ya jiji hilo. Hata hivyo, alichokuta Koreshi kilikuwa kipingamizi kikubwa sana. Babuloni lilikuwa limezungukwa na kuta kubwa sana na lilionekana lisiloweza kuingiwa. Pia, mto mkubwa Frati, ulitiririka kupitia jiji hilo na kuchangia sana kinga zalo.
17, 18. (a) Ni kwa njia gani kulikuwako ‘ukiwa juu ya maji ya Babuloni’? (b) Ni kwa nini ‘mashujaa wa Babuloni waliacha kupigana’?
17 Herodoto mwanahistoria Mgiriki aeleza jinsi Koreshi alivyoshughulikia tatizo hilo: “Aliweka sehemu ya jeshi lake mahali ambapo mto huo uliingia katika jiji hilo, na kikosi kingine upande wa nyuma wa mahali pa chemchemi yao, wakiwa na maagizo ya kupiga hatua kuingia kwenye mji huo kupitia sakafu ya kijito hicho, mara tu maji yakipungua vya kutosha . . . Aligeuza Frati kupitia mfereji ulioingia katika bonde [ziwa la kujitengenezea lililochimbwa na mtawala wa awali wa Babuloni], ambalo wakati huo lilikuwa sehemu yenye tope, ambapo mto huo ulizama sana mpaka sakafu ya asili ya kijito hicho ikawa yenye kuvukika. Ndipo waajemi waliokuwa wameachwa Babuloni kwa kusudi hilo, wakaingia katika kijito hicho, ambacho sasa kilikuwa kimezama kiasi cha kufikia katikati ya paja la mwanamume, na hivyo wakaingia ndani ya mji huo.”4
18 Kwa njia hiyo jiji hilo likaanguka, sawa na vile Yeremia na Isaya walivyokuwa wameonya. Lakini angalia utimizo wa vijambo vidogo vya unabii. Kwa halisi kulikuwa ‘ukiwa juu ya maji yake, nayo yakakaushwa.’ Kushushwa kwa maji ya Frati ndiko kuliwezesha Koreshi aingie katika jiji hilo. Je! ‘mashujaa wa Babeli waliacha kupigana,’ kama alivyokuwa ameonya Yeremia? Biblia—na pia wanahistoria Wagiriki Herodoto na Xenophon—huandika kwamba kwa kweli Wababuloni walikuwa wanakula karamu wakati shambulizi la Kiajemi lilipotukia.5 Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido, mchoro rasmi wa maandishi-kabari, husema kwamba vikosi vya Koreshi viliingia Babuloni “bila pigano,” yaelekea kumaanisha bila pigano kubwa lenye mahandaki.6 Ni wazi, mashujaa wa Babuloni hawakufanya mengi kulilinda.
19. Je! unabii kwamba Babuloni ‘halingekaliwa na watu tena kabisa’ ulitimizwa? Fafanua.
19 Vipi juu ya ule utabiri kwamba Babuloni ‘halingekaliwa na watu tena kabisa’? Haukutimizwa mara moja katika 539 K.W.K. Lakini bila kukosea unabii huo ulitimia. Baada ya anguko lalo, Babuloni lilikuwa kitovu cha maasi kadhaa, mpaka 478 K.W.K. wakati lilipoharibiwa na Shasta (Sakse). Mwishoni mwa karne ya nne, Aleksanda Mkuu alipanga kulirejesha, lakini alikufa kabla kazi hiyo haijaendelea sana. Tangu wakati huo na kuendelea, jiji hilo lilizorota tu. Kulikuwa kungali watu walioishi humo katika karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu, lakini leo kinachobaki tu cha Babuloni la kale ni rundo la magofu katika Iraq. Hata kama magofu yalo yatarejeshwa kwa sehemu, Babuloni lingekuwa tu kitu cha kuonyesha watalii, si jiji lililo hai, lenye msisimuko. Kituo chalo kilicho ukiwa hutoa ushahidi wa utimizo wa mwisho wa unabii mwingi dhidi yalo uliopulizwa na Mungu.
Mwendo wa Mamlaka za Ulimwengu
20, 21. Danieli aliona unabii gani wa mwendo wa mamlaka za ulimwengu, nao ulitimizwaje?
20 Katika karne ya sita K.W.K., wakati wa uhamisho wa Kiyahudi katika Babuloni, nabii mwingine, Danieli, alipuliziwa na Mungu aandike njozi fulani zenye kutokeza zikitabiri mwendo wa wakati ujao wa matukio ya ulimwengu. Katika moja, Danieli asimulia juu ya idadi fulani ya wanyama wa mfano wanaopinduana katika tamasha ya ulimwengu. Malaika mmoja aeleza kwamba wanyama hao wawakilisha mwendo wa mamlaka za ulimwengu tangu wakati huo na kuendelea. Akinena juu ya hayawani wawili wa mwisho, asema: “Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi. Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake.”—Danieli 8:20-22.
21 Maoni hayo ya kimbele ya kiunabii yalitimizwa barabara. Milki ya Kibabuloni ilipinduliwa na Umedi-Uajemi, ambayo, miaka 200 baadaye, iliondokea mamlaka ya ulimwengu ya Ugiriki. Milki ya Ugiriki iliongozwa na Aleksanda Mkuu, “ile pembe kubwa.” Hata hivyo, baada ya kifo cha Aleksanda, majemadari wake walipigania mamlaka miongoni mwao, na hatimaye milki hiyo kubwa sana ikavunjika kuwa milki nne ndogo zaidi, “falme nne.”
22. Katika unabii wenye kuhusiana wa mwendo wa mamlaka za ulimwengu, ni mamlaka ya ulimwengu nyingine gani iliyotolewa unabii?
22 Katika Danieli sura 7, njozi inayokaribia kufanana na hiyo ilitazama pia wakati ujao ulio mbali. Mamlaka ya ulimwengu ya Kibabuloni ilifananishwa na simba, ile ya Uajemi na dubu, na ile ya Ugiriki na chui mwenye mabawa manne mgongoni mwake na vichwa vinne. Kisha, Danieli aona hayawani-mwitu mwingine, “mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi . . . , naye alikuwa na pembe nne.” (Danieli 7:2-7) Hayawani-mwitu huyo wa nne alifananisha Milki ya Kiroma yenye nguvu nyingi, iliyoanza kusitawi karibu karne tatu baada ya Danieli kuandika unabii huo.
23. Hayawani-mwitu wa nne wa unabii wa Danieli alikuwa “mbali na falme zile zote” katika njia gani?
23 Malaika huyo alitoa unabii huu kuhusu Roma: “Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande.” (Danieli 7:23) H. G. Wells, katika kitabu chake A Pocket History of the World, asema: “Mamlaka hii mpya ya Kiroma iliyoinuka kutawala ulimwengu wa magharibi katika karne za pili na kwanza B.C. kwa njia kadhaa ilikuwa kitu tofauti na milki zozote kuu zilizokuwa zimekuwapo katika ulimwengu uliostaarabika kufikia wakati huo.”7 Ilianza ikiwa jamhuri ikaendelea kuwa milki ya kifalme. Tofauti na milki zilizotangulia, haikutokezwa na mshindi yeyote mmoja bali ilizidi kukua kwa karne nyingi. Ilidumu muda mrefu zaidi sana na ilitawala eneo kubwa zaidi ya milki yoyote iliyotangulia.
24, 25. (a) Zile pembe kumi za hayawani-mwitu zilijitokezaje? (b) Danieli alitangulia kuona mng’ang’ano gani kati ya pembe za hayawani-mwitu?
24 Ingawa hivyo, vipi juu ya pembe kumi za hayawani huyu mkubwa? Malaika alisema: “Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.” (Danieli 7:24) Hayo yalitimiaje?
25 Basi, wakati Milki ya Kirumi ilipoanza kuzorota katika karne ya tano W.K., mahali payo hapakuchukuliwa mara moja na mamlaka nyingine ya ulimwengu. Badala yake, ilivunjika-vunjika kuwa falme kadha wa kadha, “wafalme kumi.” Mwishowe, Milki ya Uingereza ilishinda zile milki tatu zenye kushindana nayo za Hispania, Ufaransa, Uholanzi ikawa mamlaka kuu ya ulimwengu. Hivyo ndivyo “pembe” hii mpya ilivyoshusha hao “wafalme watatu.”
Unabii Mwingi wa Danieli—Ni wa Baada ya Matukio?
26. Wahakiki hudai Danieli kiliandikwa lini, na kwa nini?
26 Biblia yaonyesha kwamba kitabu cha Danieli kiliandikwa wakati wa karne ya sita K.W.K. Hata hivyo, utimizo wa unabii wacho mwingi ni kamili kabisa hivi kwamba wahakiki hudai lazima kiwe kiliandikwa karibu 165 K.W.K., wakati ambapo idadi fulani ya unabii huo mwingi ilikuwa imekwisha timizwa.8 Ijapokuwa uhakika wa kwamba sababu pekee halisi ya kutoa dai hilo ni kwamba unabii mwingi wa Danieli ulitimizwa, tarehe hii ya baadaye kuhusu uandikaji wa Danieli yatolewa katika vitabu vingi vya marejezo kuwa ni uhakika uliothibitishwa.
27, 28. Ni yapi baadhi ya mambo ya hakika yanayothibitisha kwamba Danieli hakikuandikwa katika 165 K.W.K.?
27 Ingawa hivyo, lazima tupime mambo ya hakika yafuatayo kwa kuyalinganisha na nadharia hiyo. Kwanza, kitabu hicho kilitajwa katika vitabu vya Kiyahudi vilivyofanyizwa wakati wa karne ya pili K.W.K., kama vile kitabu cha kwanza cha Wamakabayo. Pia, kilitiwa ndani ya tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint, ambayo ilianza kutafsiriwa katika karne ya tatu K.W.K.9 Tatu, vipande vya nakala za Danieli vilikuwamo miongoni mwa vitabu vilivyopatikana kwa ukawaida mwingi katika Hati-Kunjo za Bahari ya Chumvi—na vipande hivyo vyaaminiwa kuwa vya tarehe ya karibu 100 K.W.K.10 Kwa wazi, muda mfupi baada ya wakati ambao husemekana Danieli kiliandikwa, kilikuwa tayari kimejulikana sana na kuheshimiwa: ni uthibitisho wenye nguvu kwamba kilifanyizwa muda mrefu kabla ya wakati wanaosema wahakiki.
28 Zaidi, Danieli kina habari za kihistoria ambazo zingalikuwa hazijulikani kwa mwandikaji wa karne ya pili. Chenye kutokeza ni kisa cha Belshaza, mtawala wa Babuloni aliyeuawa wakati Babuloni ilipoanguka katika 539 K.W.K. Vyanzo vikubwa visivyokuwa vya Kibiblia tujuavyo juu ya anguko la Babuloni ni Herodoto (karne ya tano), Xenophon (karne za tano na nne), na Berossus (karne ya tatu). Hakuna yeyote wa hao aliyejua Belshaza.11 Ingalikuwa isivyoelekea kama nini mwandikaji wa karne ya pili angekuwa na habari ambayo haingalipatikana kwa watungaji hao wa mapema zaidi! Maandishi yanayohusu Belshaza katika Danieli sura 5 ni hoja yenye nguvu kwamba Danieli aliandika kitabu chake kabla waandikaji hao wengine hawajaandika vyao.a
29. Kwa nini haiwezi kuwa kwamba kitabu cha Danieli kiliandikwa baada ya utimizo wa unabii mwingi uliomo?
29 Mwishowe, kuna idadi fulani ya unabii mwingi katika Danieli uliotimizwa muda mrefu kabla ya 165 K.W.K. Mojawapo ulikuwa unabii juu ya Milki ya Kiroma, uliotangulia kutajwa. Mwingine ni unabii wenye kutokeza uliotabiri kufika kwa Yesu, Mesiya.
Kuja kwa Aliye Mpakwa Mafuta
30, 31. (a) Ni unabii gani wa Danieli uliotabiri wakati wa kutokea kwa Mesiya? (b) Twaweza kujuaje, kwa kutegemea unabii wa Danieli, mwaka ambao Mesiya alitazamiwa kutokea?
30 Unabii huu umeandikwa katika Danieli, sura 9, na husomwa hivi: “Majuma sabini [ya miaka, au miaka mia nne na tisini] imeamriwa juu ya watu wako na juu ya jiji takatifu lako.”b (Danieli 9:24, The Amplified Bible) Ni nini kingetukia wakati wa hii miaka 490? Twasoma: “Tangu kutolewa kwa amri ya kurejesha na kujenga Yerusalemu mpaka [kuja kwa] yule mpakwa mafuta, mkuu, kutakuwa majuma saba [ya miaka], na majuma sitini na mawili [ya miaka.]” (Danieli 9:25, AB) Kwa hiyo huu ni unabii juu ya wakati wa kuja kwa aliye “mpakwa mafuta,” Mesiya. Ulitimizwaje?
31 Amri ya kurejesha na kujenga Yerusalemu ‘ilitolewa’ katika “mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta” wa Uajemi, yaani, katika 455 K.W.K. (Nehemia 2:1-9) Kufikia mwisho wa miaka 49 (majuma 7 ya miaka), sehemu kubwa ya utukufu wa Yerusalemu ilikuwa imerejeshwa. Na kisha, kuhesabu ile miaka 483 kamili (majuma ya 7 ya miaka kuongeza 62) tangu 455 K.W.K., twafika kwenye 29 W.K. Kwa kweli, huo ulikuwa “mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio,” mwaka ambao Yesu alibatizwa na Yohana Mbatizaji. (Luka 3:1) Wakati huo, Yesu alitambulishwa waziwazi kuwa Mwana wa Mungu na kuanza huduma yake ya kuhubiri habari njema kwa taifa hilo la Kiyahudi. (Mathayo 3:13-17; 4:23) Akawa ndiye “mpakwa mafuta,” au Mesiya.
32. Kulingana na unabii wa Danieli, huduma ya kidunia ya Yesu ingekuwa ya urefu gani, na ni nini kingetukia mwishoni mwayo?
32 Unabii huo waongeza: “Na baada ya hayo majuma sitini na mawili [ya miaka] aliye mpakwa mafuta atakatiliwa mbali.” Pia wasema: “Naye ataingia katika agano lenye nguvu na lililo imara pamoja na wengi kwa juma moja [miaka saba]; na katikati ya juma hilo atasababisha dhabihu na toleo kukoma.” (Danieli 9:26, 27, AB) Kwa kupatana na hilo, Yesu aliwaendea tu wale “wengi,” Wayahudi wa kimwili. Pindi moja, alihubiria pia Wasamaria, walioamini baadhi ya Maandiko lakini waliokuwa wameunda farakano lililo tofauti na Dini ya Kiyahudi iliyo kubwa. Kisha, “katikati ya juma hilo,” baada ya miaka mitatu na nusu ya kuhubiri, alitoa uhai wake kuwa dhabihu na kwa njia hiyo ‘akakatiliwa mbali.’ Hilo lilionyesha mwisho wa Sheria ya Musa pamoja na dhabihu na matoleo yayo ya zawadi. (Wagalatia 3:13, 24, 25) Hivyo, kufikia kifo chake, Yesu alisababisha “dhabihu na toleo kukoma.”
33. Yehova angeshughulika na Wayahudi pekee kwa muda mrefu kadiri gani, na ni tukio gani lililotia alama mwisho wa kipindi hicho?
33 Hata hivyo, kwa miaka mingine mitatu na nusu kundi la Kikristo lililozaliwa juzijuzi lilitoa ushahidi kwa Wayahudi pekee na, baadaye, kwa Wasamaria waliokuwa wenye ukoo nao. Hata hivyo, katika 36 W.K., mwishoni mwa yale majuma 70 ya miaka, mtume Petro aliongozwa akahubirie Kornelio, Asiye Myahudi. (Matendo 10:1-48) Sasa, lile ‘agano pamoja na wengi’ halikuhusu Wayahudi peke yao. Wokovu ulihubiriwa pia kwa Wasio Wayahudi ambao hawakutahiriwa.
34. Kwa kupatana na unabii wa Danieli, ni nini kilichotukia kwa Israeli wa kimwili kwa sababu walimkataa Mesiya?
34 Kwa sababu taifa la Kiyahudi lilikataa Yesu na kufanya hila auawe, Yehova hakuwalinda wakati Warumi walipokuja na kuharibu Yerusalemu katika 70 W.K. Hivyo, maneno zaidi ya Danieli yakatimizwa: “Na watu wa yule mkuu mwingine atakayekuja wataharibu jiji hilo na patakatifu. Mwisho walo utakuja pamoja na furiko, na hata mwisho kutakuwako vita.” (Danieli 9:26b, AB) “Mkuu” huyo wa pili alikuwa ni Tito, yule jemadari wa Roma aliyeharibu Yerusalemu katika 70 W.K.
Unabii Uliopuliziwa na Mungu
35. Ni unabii gani mwingi zaidi ya huo kuhusu Yesu uliotimia?
35 Kwa njia hiyo, unabii wa Danieli wa majuma 70 ulitimizwa kwa jinsi ya kustaajabisha iliyo kamili. Kweli kweli, mwingi wa unabii ulioandikwa katika Maandiko ya Kiebrania ulitimizwa wakati wa karne ya kwanza, na idadi fulani yao ilihusu Yesu. Mahali pa kuzaliwa kwa Yesu, bidii yake kwa ajili ya nyumba ya Mungu, utendaji wake wa kuhubiri, kusalitiwa kwake kwa vipande 30 vya fedha, namna ya kifo chake, uhakika wa kwamba kura ingepigiwa mavazi yake—habari hizo zote zilitabiriwa katika Maandiko ya Kiebrania. Utimizo wazo ulithibitisha bila shaka kwamba Yesu alikuwa ndiye Mesiya, na ulionyesha tena kwamba unabii mwingi ulikuwa umepuliziwa na Mungu.—Mika 5:2; Luka 2:1-7; Zekaria 11:12; 12:10; Mathayo 26:15; 27:35; Zaburi 22:18; 34:20; Yohana 19:33-37.
36, 37. Twajifunza nini kwa uhakika wa kwamba unabii mwingi wa Kibiblia umetimia, na maarifa hayo yanatupa uhakika gani?
36 Kwa kweli, unabii mwingi wa Biblia uliotazamiwa kutimizwa umetimia. Mambo yametukia sawasawa kabisa na ambavyo Biblia ilisema yangekuwa. Huo ni uthibitisho wenye nguvu kwamba Biblia ni Neno la Mungu. Lazima kuwe kulikuwako hekima inayozidi ya kibinadamu iliyohusika na semi hizo za kiunabii ndipo zikaweza kuwa sahihi hivyo.
37 Lakini kuna matabiri mengine katika Biblia ambayo hayakutimizwa katika nyakati hizo. Kwa nini? Kwa sababu yalitazamiwa yatimizwe katika siku yetu, na hata katika wakati ujao wetu. Utegemeko wa unabii mwingi huo wa kale hutufanya tuwe na uhakika kwamba matabiri hayo mengine yatatimia bila kukosa. Kama tutakavyoona katika sura inayofuata, ndivyo ilivyo kweli kweli.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Sura 4, “‘Agano la Kale’ Ni Lenye Kusadikika Kadiri Gani?” mafungu 16 na 17.
b Katika tafsiri hii, maneno katika vifungo vya mraba yameongezwa na mtafsiri ili kufafanua maana.
[Blabu katika ukurasa wa 133]
Unabii wote mwingi uliotazamiwa kutimizwa ulitimia. Mambo yalitukia sawasawa na ambavyo Biblia ilisema yangekuwa
[Picha katika ukurasa wa 118]
Waakiolojia wamegundua kwamba kuharibiwa kwa Yerusalemu na Nebukadreza kulikuwa kamili
[Picha katika ukurasa wa 121]
Picha ya Tiro la ki-siku-hizi. Karibu hakuna salio linalobaki la Tiro walilojua manabii wa Israeli
[Picha katika ukurasa wa 123]
Watalii wanaotembelea mahali lilipokuwa Babuloni la kale ni mashahidi wa utimizo wa unabii mwingi juu ya jiji hilo
[Picha katika ukurasa wa 126]
Unabii mwingi wa Danieli juu ya mwendo wa mamlaka za ulimwengu ulitimizwa kwa usahihi sana hivi kwamba wahakiki wa ki-siku-hizi hufikiri uliandikwa baada ya utimizo
BABULONI
UAJEMI
UGIRIKI
RUMI
UINGEREZA
[Picha katika ukurasa wa 130]
Danieli alitoa unabii juu ya wakati kamili ambao Mesiya angetokea katika Israeli
-
-
Unabii wa Biblia Ambao Wewe Umeona UkitimizwaBiblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
-
-
Sura 10
Unabii wa Biblia Ambao Wewe Umeona Ukitimizwa
Je! umepata kuuliza ni kwa nini mambo ni tofauti sana leo yakilinganishwa na yalivyokuwa miaka mia moja iliyopita? Baadhi ya mambo yako afadhali. Katika mabara mengi, maradhi yaliyoua wakati uliopita sasa yanaponywa kikawaida, na mtu wa wastani hufurahia kiwango cha maisha ambacho hakikuwaziwa na wazazi wake wa kale waliokufa. Kwa upande mwingine, karne yetu imeona vita vibaya zaidi na baadhi ya mateso mabaya zaidi katika historia yote. Fanaka ya ainabinadamu—hata kuendelea kwayo kuishi—yatishwa na ongezeko la ghafula la idadi ya watu, tatizo la uchafuzi, na mrundiko mkubwa sana wa kimataifa wa silaha za nyukilia, za viini, na za kemikali. Ni kwa nini karne ya 20 ni tofauti sana na karne zilizotangulia?
1. (Tia ndani utangulizi.) (a) Karne ya 20 imetofautianaje na karne zilizotangulia? (b) Ni nini kitakachotusaidia tuelewe ni kwa nini nyakati zetu ziko tofauti sana?
JIBU la swali hilo lahusiana na unabii wa Biblia wenye kutokeza ambao wewe umeona ukitimizwa. Ni unabii ambao Yesu mwenyewe alitamka na ambao, licha ya kuthibitisha Biblia imepuliziwa na Mungu, waonyesha kwamba twaishi karibu sana na mabadiliko makubwa katika tamasha ya ulimwengu. Unabii huo ni upi? Nasi twajuaje kwamba unatimizwa?
Unabii Mkubwa wa Yesu
2, 3. Wanafunzi wa Yesu walimwuliza swali gani, na jibu twalipata wapi?
2 Biblia hutuambia kwamba muda mfupi kabla ya kifo cha Yesu, wanafunzi wake walikuwa wakizungumza juu ya yale majengo makubwa ya hekalu katika Yerusalemu; walivutiwa sana na ukubwa na ulioelekea kuwa udumifu wayo. Lakini Yesu alisema: “Hamyaoni mambo haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”—Mathayo 24:1, 2.
3 Lazima wanafunzi wa Yesu wawe walishangazwa na maneno yake na baadaye walimjia wapate habari zaidi, wakisema: “Tuambie, Mambo hayo yatakuwa wakati gani, na ni nini itakayokuwa ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?” (Matahyo 24:3, NW) Jibu la Yesu lapatikana katika sehemu inayobaki ya Mathayo sura za 24 na 25. Maneno yake yameandikwa, pia, katika Marko sura 13 na Luka sura 21. Bila shaka huo ulikuwa ndio unabii wa maana zaidi uliotamkwa na Yesu alipokuwa yungali duniani.
4. Wanafunzi wa Yesu walikuwa wakiuliza juu ya mambo gani tofauti?
4 Kwa kweli, wanafunzi wa Yesu walikuwa wakiuliza juu ya jambo zaidi ya moja. Kwanza, walitokeza swali: “Mambo hayo yatakuwa wakati gani?” yaani, Yerusalemu na hekalu lalo vingeharibiwa wakati gani? Na zaidi, walitaka kujua ishara ambayo ingeonyesha kwamba kuwapo kwa Yesu akiwa Mfalme wa Ufalme wa kimbingu wa Mungu kulikuwa kumeanza na kwamba mwisho wa huu mfumo wa mambo ulikuwa karibu.
5. (a) Kulikuwako utimizo gani wa kwanza wa unabii wa Yesu, lakini maneno yake yangekuwa na utimizo kamili wakati gani? (b) Yesu alianzaje jibu lake kwa swali la wanafunzi?
5 Katika jibu lake, Yesu alizungumza juu ya mambo hayo mawili. Kwa kweli mengi ya maneno yake yalitimizwa nyuma katika karne ya kwanza, wakati wa ile miaka iliyoongoza mpaka kwenye uharibifu mbaya sana wa Yerusalemu katika 70 W.K. (Mathayo 24:4-22) Lakini unabii wake ulipaswa kuwa na maana kubwa hata zaidi baadaye, kwa kweli katika siku zetu wenyewe. Basi, Yesu alisema nini? Alianza kwa kutamka maneno yaliyoandikwa katika mistari 7 na 8: “Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme, na kutakuwako upungufu wa chakula na matetemeko ya dunia mahali hapa na mahali hapa. Mambo hayo yote ni mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.”
6. Maneno ya Yesu katika Mathayo 24:7, 8 hutukumbusha juu ya unabii gani unaofanana na huo?
6 Kwa wazi, kuwapo kwa Yesu akiwa Mfalme wa kimbingu kungetiwa alama na mchafuko mkubwa duniani. Hilo lathibitishwa na unabii unaolingana ambao wapatikana katika kitabu cha Ufunuo: ile njozi ya wale wapanda-farasi wanne wa Apokalipsi. (Ufunuo 6:1-8) Wa kwanza wa wapanda-farasi hao afananisha Yesu mwenyewe akiwa Mfalme mshindi. Wale wapandaji wengine na farasi zao wafananisha matukio duniani yanayotia alama mwanzo wa utawala wa Yesu: vita, njaa, na kifo cha mapema kupitia visababishi mbalimbali. Je! tunaona matabiri hayo mawili yakitimizwa leo?
Vita!
7. Ni nini kinachotangulia kuonyeshwa kiunabii na upandaji wa mpanda-farasi wa pili wa Apokalipsi?
7 Acheni tuyaangalie kwa uangalifu zaidi. Kwanza, Yesu alisema: “Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme.” Huo ulikuwa unabii wa vita. Wa pili wa wale wapanda-farasi wa Apokalipsi alifananisha vita pia. Twasoma: “Mwingine akatokea, farasi rangi-moto; na yule mmoja aliyeketi juu yake alipewa ruhusa ya kuondolea mbali amani kutoka dunia ili wao wapaswe kuchinja mmoja na mwenzake; na upanga mkubwa akapewa yeye.” (Ufunuo 6:4, NW) Ilivyo ni kwamba ainabinadamu imekuwa ikipigana vita kwa maelfu ya miaka. Basi, ni kwa nini maneno hayo yawe na umaana wa pekee kwa siku yetu?
8. Kwa nini tungetazamia vita kuwa sehemu ya kutokeza ya ishara hiyo?
8 Kumbuka kwamba vita peke yake siyo ishara ya kuwapo kwa Yesu. Ishara hiyo imejumlisha mambo yote ya unabii wa Yesu yakitukia katika kipindi kile kile kimoja cha wakati. Lakini vita ndiyo sehemu ya kwanza inayotajwa, kwa hiyo tungetazamia kwamba sehemu hii ingetimizwa katika njia ya kutokeza ambayo ingevuta fikira zetu. Na kila mtu lazima akubali kwamba vita vya karne hii ya 20 havina kifani katika historia yote iliyotangulia.
9, 10. Unabii mwingi kuhusu vita ulianza kutimizwaje?
9 Kwa kielelezo, hakuna vita vyovyote vya mapema—vingi vijapokuwa vilikuwa vyenye ukatili na uharibifu—vilivyokaribia hata kidogo uharibifu wa vita vya ulimwengu viwili vya karne ya 20. Vita vya ulimwengu vya kwanza vilisababisha hatimaye karibu vifo milioni 14, zaidi ya idadi yote ya watu wa nchi nyingi. Kweli kweli, “alipewa ruhusa ya kuondolea mbali amani kutoka dunia ili wao wapaswe kuchinja mmoja na mwenzake.”
10 Kulingana na unabii huo, ‘upanga mkubwa alipewa’ mpanda-farasi wa pili wa Apokalipsi mwenye kufanana na vita. Hilo lahusuje? Hivi: Silaha za vita zilikuwa hatari zaidi sana. Akiwa na kifaru, ndege, gesi ya sumu yenye kuua, nyambizi, na mizinga ambayo ingeweza kulipusha risasi kwenda kilometa kadhaa, binadamu akawa hodari zaidi katika kuua jirani yake. Na tangu vita vya ulimwengu vya kwanza ule “upanga mkubwa” umekuwa wenye uharibifu hata zaidi—kwa sababu ya matumizi ya vitu kama mawasiliano ya redio, rada, bunduki za hali ya juu, silaha za viini na kemikali, bunduki za kutupa moto, makombora ya moto, aina mpya za makombora, makombora ya kulipua yenye kuruka kutoka kontinenti moja mpaka nyingine, nyambizi za nyukilia, eropleni za ufundi mkubwa, na manowari kubwa.
“Mwanzo wa Maumivu Makali ya Ghafula ya Taabu”
11, 12. Vita vya kwanza vya ulimwengu vilikuwaje “mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu”?
11 Mistari ya mapema ya unabii wa Yesu yamalizia kwa maneno haya: “Mambo hayo yote ni mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.” Kwa hakika ndivyo ilivyokuwa kwa vita vya ulimwengu vya kwanza. Mwisho wavyo katika 1918 haukuleta amani ya muda mrefu. Baada ya muda mfupi vilifuatwa na mapigano madogo lakini makali katika Ethiopia, Libya, Hispania, Urusi, India, na mabara mengine. Kisha vikaja vita vya ulimwengu vya pili vyenye kutisha sana, ambavyo viliua wanajeshi na raia milioni 50.
12 Na zaidi, yajapokuwa mapatano ya amani na utulivu wa pindi kwa pindi katika kupigana, ainabinadamu ingali katika vita. Katika 1987 iliripotiwa kwamba vita vikubwa 81 vilikuwa vimepiganwa tangu 1960, vikiua wanaume, wanawake, na watoto 12,555,000. Mwaka 1987 uliona vita zaidi vikipiganwa kuliko katika mwaka mwingineo wote uliotangulia wa historia iliyoandikwa.1 Kuongezea hayo, matayarisho na matumizi ya kijeshi, sasa yakifikia jumla ya karibu dola 1,000,000,000,000 kila mwaka, yanaharibu uchumi wa ulimwengu.2 Kwa hakika unabii wa Yesu juu ya ‘taifa likiinuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme’ unatimizwa. Yule farasi mwekundu wa vita aendelea na mbio zake kali duniani kote. Lakini vipi juu ya sehemu ya pili ya ishara hiyo?
Upungufu wa Chakula!
13. Yesu alitabiri matukio gani yenye tanzia, na njozi ya mpanda-farasi wa tatu iliungaje mkono unabii wake?
13 Yesu alitabiri: “Na kutakuwako upungufu wa chakula . . . mahali hapa na mahali hapa.” Ona jinsi hilo linavyopatana na upandaji wa farasi wa tatu wa wale wapanda-farasi wanne wa Apokalipsi. Juu yake twasoma: “Nikaona, na tazama! farasi mweusi ti; na mmoja aliyeketi juu yake alikuwa na jozi ya mizani katika mkono wake. Na mimi nikasikia sauti kana kwamba ni katikati ya viumbe hai wanne ikisema: ‘Kwarti moja ya ngano kwa dinari moja, na kwarti tatu za shayiri kwa dinari moja; na usidhuru mafuta ya zeituni na divai.’” (Ufunuo 6:5, 6, NW) Ndiyo, upungufu mkubwa wa chakula!
14. Ni njaa kubwa gani tangu 1914 zimetimiza unabii wa Yesu?
14 Je! yawezekana kwamba unabii huo unatimizwa leo, ambapo mabara fulani yamefikia kupata viwango vya juu vya maisha? Mtupio jicho kwa ulimwengu wote hauachi shaka lolote kwa habari ya jibu. Kihistoria, njaa kubwa zimesababishwa na vita na misiba ya asili. Basi, haishangazi kwamba karne yetu, ambayo imekuwa na misiba na vita vingi mno, imepatwa tena na tena na njaa kubwa. Sehemu nyingi za dunia zimepatwa na misiba tangu 1914. Ripoti moja yaorodhesha njaa kubwa-kubwa zaidi ya 60 tangu 1914, katika mabara yaliyotengana kama Ugiriki, Udachi, U.S.S.R., Nigeria, Chad, Chile, Peru, Bangladesh, Bengal, Kampuchea, Ethiopia, na Japan.3 Baadhi ya njaa hizo kubwa zimeendelea kwa miaka kadhaa na kusababisha mamilioni ya vifo.
15, 16. Ni upungufu gani mwingine wa chakula wenye kuleta uharibifu kweli kweli leo?
15 Ingawa kwa kawaida njaa kali hutangazwa sana, baada ya muda hizo hupita na waliookoka hurudia polepole maisha ya kawaida kwa kulinganisha. Hata hivyo, aina nyingine ya kutisha zaidi ya upungufu wa chakula imesitawi wakati wa karne ya 20. Hii haitokezi sana na kwa hiyo hupuuzwa mara nyingi. Lakini huendelea mwaka baada ya mwaka. Hii ni tauni kali ya ukosefu wa chakula kinachofaa mwili (utapiamlo) ambayo hupata kufikia sehemu moja kwa tano ya idadi ya watu wa sayari yetu na huua kati ya watu milioni 13 na 18 kila mwaka.4
16 Yaani, aina hii ya upungufu wa chakula huua kwa kawaida karibu watu wengi katika siku mbili kama waliouawa katika Hiroshima na lile kombora la atomi. Kweli kweli, kila miaka miwili, kuna watu wengi zaidi wanaouawa na matokeo ya njaa kushinda askari waliouawa na Vita vya Ulimwengu 1 na Vita vya Ulimwengu 2 vikiunganishwa. Je! kumekuwako “upungufu wa chakula . . . mahali hapa na mahali hapa” tangu 1914? Ndiyo, kabisa!
Matetemeko ya Dunia
17. Ni tetemeko gani la dunia lenye kuleta uharibifu lililotukia mara tu baada ya 1914?
17 Katika Januari 13, 1915, vita vya ulimwengu vya kwanza vilipokuwa na miezi michache tu, tetemeko moja la dunia lilitikisa Abruzzi, Italia, na kuua watu 32,610. Msiba huo mkubwa watukumbusha kwamba vita na upungufu wa chakula wakati wa kuwapo kwa Yesu vingeandamana na kitu kingine: “Kutakuwako . . . matetemeko ya dunia mahali hapa na mahali hapa.” Kama ilivyo kwa vita na njaa kubwa, lile tetemeko la dunia la Abruzzi lilikuwa tu “mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.”a
18. Unabii wa Yesu kuhusu matetemeko ya dunia umetimizwaje?
18 Karne ya 20 imekuwa karne ya matetemeko ya dunia, na kwa sababu ya usitawi wa vyombo vya kusambaza habari, ainabinadamu yote inajua sana uharibifu ambao yamesababisha. Kutaja machache tu, katika China 200,000 walikufa katika tetemeko la dunia 1920; katika 1923, watu wapatao 99,300 walikufa katika tetemeko katika Japan; katika 1935, tetemeko jingine liliua 25,000 katika ile ambayo sasa ni Pakistan, ambapo 32,700 walikufa katika Uturuki katika 1939. Kulikuwa na vifo 66,800 katika tetemeko la dunia na Peru katika 1970. Na katika 1976, wapatao 240,000 (au, kulingana na vyanzo vingine, 800,000) walikufa katika Tangshan, China. Hivi juzijuzi, katika 1988, kulikuwako 25,000 waliokufa katika tetemeko la dunia lenye nguvu katika Armenia.b Hakika, “matetemeko ya dunia mahali hapa na mahali hapa”!6
“Tauni Yenye Kufisha”
19. Ni jambo gani zaidi ya ishara hiyo lililotabiriwa na Yesu na kutangulia kufananishwa na yule mpanda-farasi wa nne wa Apokalipsi?
19 Jambo jingine la la unabii wa Yesu lahusiana na maradhi. Mwevanjeli Luka, katika simulizi lake, aandika kwamba Yesu alitabiri “mahali hapa na mahali hapa magonjwa ya kipuku.” (Luka 21:11, NW) Hilo pia lapatana na njozi ya kiunabii ya wale wapanda-farasi wanne wa Apokalipsi. Yule mpanda-farasi wa nne aitwa Kifo. Yeye afananisha kifo cha mapema kutokana na visababishi kadhaa, kutia ndani “tauni yenye kufisha na . . . hayawani-mwitu wa dunia.”—Ufunuo 6:8, NW.
20. Ni ugonjwa gani wa kuambukiza wenye kutokeza uliotimiza kwa sehemu unabii wa Yesu juu ya magonjwa ya kipuku?
20 Nyuma katika 1918 na 1919, watu zaidi ya 1,000,000,000 waliugua mafua makali ya Hispania, na zaidi ya 20,000,000 walikufa. Maradhi hayo yaliua wengi zaidi ya ile vita kuu yenyewe.7 Na “tauni yenye kufisha,” au “magonjwa ya kipuku,” yangali yanapiga kizazi hiki, ijapokuwa maendeleo mengi ya kitiba yenye kutokeza. Ni kwa nini? Jambo moja ni kwamba, sikuzote mabara maskini zaidi hayana maendeleo ya kisayansi. Watu maskini huugua na kuuawa na magonjwa ambayo yangeweza kuponywa kama pesa zaidi zingetolewa.
21, 22. Watu katika mabara tajiri na maskini wameuguaje kutokana na “tauni yenye kufisha”?
21 Hivyo, watu wapatao milioni 150 ulimwenguni pote huugua malaria. Wapatao milioni 200 huambukiwa na kichocho. Maradhi ya Chagas hupata watu karibu milioni kumi. Karibu milioni 40 huugua upofu unaoletwa na mainzi ya mto. Maradhi ya kuhara sana huua mamilioni ya watoto kila mwaka.8 Kifua kikuu na ukoma yangali ni matatizo makubwa ya afya. Hasa, maskini wa ulimwengu huu huugua ‘magonjwa ya kipuku mahali hapa na mahali hapa.’
22 Lakini hata na matajiri pia. Kwa kielelezo, mafua makali huambukia matajiri na maskini pia. Katika 1957 kiini kimoja cha mafua makali kilisababisha vifo 70,000 katika United States peke yake. Katika Ujerumani yakadiriwa kwamba mtu mmoja katika sita ataugua kansa hatimaye.9 Maradhi yenye kupitishwa kingono yanawapata pia matajiri na maskini. Kisonono, maradhi ya kuambukizana yanayoripotiwa mara nyingi katika United States, huambukia hesabu kubwa inayofikia asilimia 18.9 ya idadi ya watu wa sehemu fulani za Afrika.10 Kaswende, maradhi ya macho (chlamydia), na vidonda vya sehemu za uzazi ni baadhi ya “magonjwa ya kipuku” yanayopitishwa kingono.
23. Ni “tauni yenye kufisha” gani ambayo juzijuzi imekuwa kwenye vichwa vya habari za magazetini?
23 Katika miaka ya juzijuzi, “tauni yenye kufisha” ya UKIMWI imejiunga pia katika orodha ya “magonjwa ya kipuku.” UKIMWI ni ugonjwa wa kuogofya kwa sababu, wakati huu wa kuandika, hakuna ponya linaloonekana, na hesabu ya wanaouawa nao yazidi kuongezeka. Dakt. Jonathan Mann, mkurugenzi wa Programu ya Pekee ya WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) juu ya UKIMWI, alisema: “Pia twakadiria kwamba kuna watu milioni tano kufikia 10 ulimwenguni leo walioambukiwa na vairasi ya upungufu wa kinga ya mwili wa binadamu (HIV).”11 Kulingana na kadirio moja lililotangazwa, vairasi ya UKIMWI huambukia mtu mpya kila dakika. “Tauni yenye kufisha” kweli kweli! Lakini vipi juu ya unabii wa kifo kupitia hayawani-mwitu?
“Hayawani-mwitu wa Dunia”
24, 25. (a) Nabii Ezekieli alirejezea “hayawani-mwitu” wa aina gani? (b) Yesu alisema nini juu ya kuchacha kwa “hayawani-mwitu” duniani wakati wa kuwapo kwake?
24 Ukweli ni kwamba, hayawani-mwitu wanapotajwa siku hizi katika magazeti, ni kwa sababu namna-namna fulani zinahatarishwa au ziko karibu kutoweka. “Hayawani-mwitu wa dunia” wanatishwa kuuawa zaidi na wanadamu kuliko wanadamu wanavyotishwa kuuawa nao. Ingawa hilo, katika mabara fulani wanyama-mwitu, kama vile simba-milia katika India, wangali wanaendelea kuua wanadamu.
25 Hata hivyo, Biblia yavuta fikira kwenye aina nyingine ya hayawani-mwitu ambaye amesababisha hofu kweli kweli katika miaka ya juzijuzi. Nabii Ezekieli alilinganisha binadamu wenye jeuri na wanyama aliposema: “Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho [nafsi, NW] za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.” (Ezekieli 22:27) Alipotoa unabii juu ya “kuongezeka kwa kutokutii sheria,” kwa kweli, Yesu alikuwa akisema kwamba “hayawani-mwitu” hao wangekuwa wakichacha duniani wakati wa kuwapo kwake. (Mathayo 24:12, NW) Paulo mwandikaji wa Biblia aongeza kwamba katika “siku za mwisho” binadamu wangekuwa “wenye kupenda fedha . . . wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema.” (2 Timotheo 3:1-3) Je! imekuwa hivyo tangu 1914?
26-28. Ni ripoti zipi kuuzunguka ulimwengu zinazoonyesha kwamba “hayawani-mwitu” wahalifu wanaotea-otea duniani?
26 Hakika ndivyo. Ikiwa unaishi katika karibu jiji lolote kubwa la dunia, tayari wajua hilo. Lakini ikiwa unatia shaka, ebu fikiria manukuu ya magazeti ya juzijuzi yafuatayo. Kutoka Colombia: “Mwaka jana polisi waliandika . . . mauaji ya kukusudia karibu 10,000 na wizi wa kutumia silaha 25,000.” Kutoka Victoria, Australia: “Ongezeko Kubwa Katika Uhalifu Mkubwa.” Kutoka United States: “Machinjo Katika New York Yakaribia Hesabu Isiyopata Kufikiwa Tena.” “Detroit ilipita Gary, Indiana, mwaka jana kuwa jiji kubwa lenye hesabu ya mauaji mengi zaidi ya kukusudia katika taifa—58 kwa wakaaji 100,000.”
27 Kutoka Zimbabwe: “Kuua watoto kwa kukusudia kumefikia viwango vya kuhatarisha.” Kutoka Brazil: “Kuna uhalifu mwingi sana hapa, na matumizi mengi sana ya silaha, hivi kwamba habari za jeuri hazisisimui sana tena.” Kutoka New Zealand: “Mashambulizi ya kingono na uhalifu wenye jeuri waendelea kuwa hangaiko kubwa kwa polisi.” “Kiwango cha jeuri ya watu wa New Zealand kuelekeana chaweza kuelezwa tu kuwa ni unyama.” Kutoka Hispania: “Hispania yashindana na tatizo la uhalifu wenye kuongezeka.” Kutoka Italia: “Mafia wa Sicily, baada ya kudhoofika, wafufuka katika wimbi la mauaji.”
28 Hayo ni mfano mdogo tu wa ripoti za magazeti zilizotokea muda mfupi tu kabla ya kutangazwa kwa kitabu hiki (katika Kiingereza). Hakika, “hayawani-mwitu” wanaotea-otea duniani, wakisababisha watu watetemekee usalama wao.
Kuhubiri Habari Njema
29, 30. Hali ya kidini katika Jumuiya ya Wakristo ikoje, katika kutimiza unabii wa Yesu?
29 Dini ingeendeleaje wakati wa msukosuko wa kuwapo kwa Yesu? Kwa upande mmoja, Yesu alitoa unabii kwamba kungekuwako ongezeko katika utendaji wa kidini: “Manabii wengi wa uwongo watatokea na kupotosha wengi.” (Mathayo 24:11, NW) Kwa upande mwingine, yeye alitabiri kwamba katika Jumuiya ya Wakristo yote, kupendezwa na Mungu kungeshuka sana. “Upendo wa wengi zaidi utapoa.”—Mathayo 24:12, NW.
30 Kwa kweli hilo laeleza yanayotukia leo katika Jumuiya ya Wakristo. Katika upande huu, makanisa makubwa yanashindwa kwa kukosa kuungwa mkono. Katika mabara ambayo wakati mmoja yalikuwa ya Kiprotestanti sana ya Ulaya na Uingereza, dini imekufa. Wakati uo huo, Kanisa Katoliki linaugua kwa kukosa makasisi na kwa upungufu wa kuungwa mkono. Kwa upande mwingine, kumekuwako maongezeko katika visehemu vya dini ndogo. Vidhehebu vyenye kutegemea dini za Nchi za Mashariki vinavuvumuka sana, huku wainjilisti wa televisheni wenye pupa wakinyonya watu mamilioni ya dola.
31. Yesu alitabiri nini kinachosaidia kutambulisha Wakristo wa kweli leo?
31 Lakini, vipi juu ya Ukristo wa kweli, dini ile iliyoanzishwa na Yesu na kuhubiriwa na mitume wake? Bado ingekuwako wakati wa kuwapo kwa Yesu, lakini ingetambuliwaje? Kuna mambo kadhaa yanayotambulisha Ukristo wa kweli, na moja limetajwa katika unabii mkubwa wa Yesu. Wakristo wa kweli wangekuwa wakishughulika na kazi ya kuhubiri ulimwenguni pote. Yesu alitoa unabii huu: “Na habari njema hizi za ufalme zitahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ushahidi kwa mataifa yote; na ndipo ule mwisho utakuja.”—Mathayo 24:14, NW.
32. Ni kikundi gani pekee ambacho kimetimiza unabii wa Yesu ulioandikwa katika Mathayo 24:14?
32 Kuhubiri huku sasa kunatukia kwa kiwango kikubwa sana! Leo, kikundi cha kidini kinachoitwa Mashahidi wa Yehova kinashiriki katika utendaji mkubwa zaidi wa kuhubiri katika historia ya Ukristo. (Isaya 43:10, 12, NW) Nyuma katika 1919, wakati dini kubwa zenye akili ya kisiasa zilipokuwa zikitetea Ushirika wa Mataifa ulioelekewa na msiba, Mashahidi wa Yehova walikuwa wakitayarishwa kwa ajili ya shughuli hii ya kuhubiri katika tufe lote.
33, 34. Habari njema za Ufalme zimehubiriwa ulimwenguni pote kwa kadiri gani?
33 Nyuma wakati huo kulikuwa Mashahidi wapatao 10,000 tu, lakini walijua kazi iliyopasa kufanywa. Walitambua kwamba mgawanyo wa viongozi wa kidini na watu wa kawaida ulikuwa kinyume cha amri za Biblia na kigezo cha kimitume. Kwa hiyo wote kabisa, walijifunza kunena na majirani wao juu ya Ufalme wa Mungu. Wakawa tengenezo la wahubiri.
34 Kwa kadiri wakati ulivyopita, wahubiri hawa walivumilia upinzani mkali. Katika Ulaya, walipingwa na tawala za aina tofauti-tofauti za kiimla. Katika United States na Canada, walikabiliana na kesi za kisheria na harakati za wafanya ghasia. Katika mabara mengine, walipaswa kushinda chuki yenye kichaa ya kidini na mnyanyaso usio na huruma kupitia watawala wa mabavu wenye kudhulumu. Katika miaka ya juzijuzi, wamelazimika pia kukabiliana na roho ya kutia shaka na kutafuta anasa ambayo imesitawi. Lakini wamestahimili, mpaka wa leo, kuna zaidi ya milioni nne yao katika mabara 212. Habari njema za Ufalme hazijapata kuhubiriwa sana tena kama wakati huu—utimizo wenye kutokeza wa sehemu hii ya ishara!
Yote Hayo Yamaanisha Nini?
35. (a) Utimizo wa unabii leo unasaidiaje kuonyesha upulizio wa kimungu wa Biblia? (b) Utimizo wa ishara aliyotoa Yesu wamaanisha nini kwa siku yetu?
35 Bila shaka twashuhudia utimizo wa ile ishara kubwa aliyotoa Yesu. Uhakika huo waongezea uthibitisho wa kwamba kweli kweli Biblia imepuliziwa na Mungu. Hakuna mwanadamu yeyote ambaye angeweza kutabiri mapema sana matukio ambayo yangetukia wakati wa karne hii ya 20. Zaidi ya hayo, utimizo wa ishara hiyo wamaanisha kwamba tunaishi katika wakati wa kuwapo kwa Yesu na wa umalizio wa mfumo wa mambo. (Mathayo 24:3, NW) Maana yake hiyo ni nini? Ni nini kinachohusika katika kuwapo kwa Yesu? Na mfumo wa mambo unaomalizika ni nini? Ili kujibu maswali hayo, twahitaji kufikiria uthibitisho mwingine wenye nguvu wa Biblia: upatano wayo wa ndani wenye kutokeza. Tutazungumza hili halafu tuone jinsi kichwa kikuu cha Biblia kinavyokaribia hata sasa upeo wenye kuchochea hofu nyingi.
[Maelezo ya Chini]
a Kulikuwako angalau matetemeko ya dunia matano kati ya 1914 na 1918 yaliyoonyeshwa kuwa yenye ukubwa wa 8 au zaidi kwenye skeli (kipimo) ya Richter—yenye nguvu zaidi ya lile tetemeko la dunia katika Abruzzi. Hata hivyo, mitikisiko hii ilikuwa katika maeneo ya mbali ya tufe, na hivyo hayakuvuta fikira sana kama lile tetemeko la Italia.5
b Tarakimu zenye kutofautiana zimeripotiwa za hesabu ya waliouawa na baadhi ya misiba hii. Hata hivyo, yote yalikuwa yenye uharibifu mkubwa sana.
-
-
Upatano wa Biblia YoteBiblia—Neno la Mungu au la Binadamu?
-
-
Sura 11
Upatano wa Biblia Yote
Wazia maktaba ya vitabu 66 vilivyoandikwa na watu tofauti wapatao 40 kwa kipindi cha miaka 1,600. Lugha tatu zilitumiwa na waandikaji walioishi katika mabara kadhaa. Waandikaji wote walikuwa na nyutu, uwezo, na malezi tofauti. Lakini vitabu hivyo walivyoandika vilipokusanywa hatimaye, kweli kweli, ikawa kwamba vilijumlika kuwa kitabu kikubwa kimoja tu chenye kufuatia kichwa kimoja cha msingi tangu mwanzo mpaka mwisho. Ni vigumu kuwazia hilo, sivyo? Ingawa hivyo, Biblia ni maktaba ya jinsi hiyo.
1. (Tia ndani utangulizi.) Ni upatano gani wa kutokeza unaoshuhudia uhakika wa kwamba Biblia imepuliziwa na Mungu?
HAKUNA mwanafunzi yeyote mwenye kufuatia haki ambaye angekosa kuvutiwa na uhakika wa kwamba Biblia, ijapokuwa mkusanyo wa vitabu tofauti, ni kitabu kimoja chenye umoja. Ina umoja kwa maana, tangu mwanzo mpaka mwisho, inahimiza ibada ya Mungu mmoja tu ambaye sifa zake hazibadiliki kamwe, na vitabu vyayo vyote husitawisha kichwa kimoja kikuu. Upatano huo wa ujumla ni uthibitisho wenye nguvu kwamba kwa kweli, Biblia ni Neno la Mungu.
2, 3. Ni unabii gani uliotamkwa katika Edeni ambao ulitoa msingi wa tumaini, na ni hali gani zilizoongoza kwenye kutamkwa kwa unabii huo?
2 Kichwa cha msingi cha Biblia chaanzishwa katika sura za mapema zaidi za kitabu chayo cha kwanza, Mwanzo. Hapo, twasoma kwamba wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, waliumbwa wakiwa wakamilifu na kuwekwa katika shamba-paradiso, Edeni. Hata hivyo, Hawa, alifikiwa na nyoka aliyetilia shaka haki ya sheria za Mungu na kumshawishi kwa uwongo wenye hila aingie katika mwendo wa dhambi. Adamu alimfuata naye pia akamwasi Mungu. Tokeo? Wote wawili walifukuzwa kutoka Edeni na kuhukumiwa kifo. Sisi leo huteseka kutokana na matokeo ya uasi huo wa kwanza. Sisi sote hurithi dhambi na kifo kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza.—Mwanzo 3:1-7, 19, 24; Warumi 5:12.
3 Hata hivyo, katika wakati huo wenye tanzia, Mungu alitamka unabii uliotoa msingi wa kuwa na tumaini. Unabii huo ulinenwa kwa nyoka, lakini ulitamkwa Adamu na Hawa wakisikia ili waweze kuwaambia watoto wao. Hivi ndivyo alivyosema Mungu: “Na mimi nitaweka uadui kati yako na mwanamke na kati ya mbegu yako na mbegu yake. Yeye atachubua wewe kichwani na wewe utachubua yeye kisiginoni.”—Mwanzo 3:15, NW; Warumi 8:20, 21.
4. Ni sehemu gani zilizotajwa katika unabii wa Yehova katika Edeni, nazo zingehusianaje wakati wa karne nyingi?
4 Angalia sehemu nne zinazotajwa katika mstari huu wa msingi: nyoka na mbegu yake na pia mwanamke na mbegu yake. Sehemu hizo zingekuwa wahusika wakubwa katika matukio kwa maelfu ya miaka ambayo yangefuata. Uadui wa daima ungekuwako kati ya mwanamke na mbegu yake upande mmoja na nyoka na mbegu yake upande mwingine. Uadui huo ungetia ndani pambano linaloendelea sasa kati ya ibada ya kweli na ya bandia, mwenendo unaofaa na uovu. Katika hatua fulani, nyoka angeonekana kama kwamba amefaulu alipochubua kisigino cha mbegu ya mwanamke. Hata hivyo, hatimaye mbegu ya mwanamke ingeponda kichwa cha nyoka, na Mungu mwenyewe angeondolewa malawama wakati alama zote za uasi huo wa awali zingeondolewa.
5. Twajuaje kwamba Hawa hakuwa yule mwanamke wa unabii huo?
5 Mwanamke na nyoka ni nani? Na mbegu zao ni nani? Hawa alipozaa mwana wake wa kwanza, Kaini, alisema kwa mshangao: “Nimezaa mwanamume kwa msaada wa Yehova.” (Mwanzo 4:1, NW) Labda yeye alihisi kwamba alikuwa ndiye yule mwanamke wa unabii na kwamba mwana wake angethibitika kuwa mbegu hiyo. Hata hivyo, Kaini, alikuwa na roho mbaya kama ile ya nyoka. Akaja kuwa mwuaji wa kukusudia, akimwua Abeli ndugu yake mwenyewe mdogo. (Mwanzo 4:8) Kwa wazi, unabii huo ulikuwa na maana yenye kina kirefu, maana ya kimfano ambayo ni Mungu pekee angeweza kufafanua. Naye alifanya hivyo, kidogo kidogo. Vitabu vyote 66 vya Biblia vinachangia kwa njia hii au ile ufunuo wa maana ya hili, yaani, ule unabii wa kwanza katika Biblia.
Nyoka Ni Nani?
6-8. Ni maneno gani ya Yesu yanayotusaidia kutambua uwezo ulioongoza nyoka? Fafanua.
6 Kwanza, ni nani nyoka anayenenwa juu yake katika Mwanzo 3:15? Simulizi hilo lasema kwamba nyoka halisi alimfikia Hawa katika Edeni, lakini nyoka wa halisi hawawezi kunena. Lazima kuwe kulikuwa na uwezo fulani uliomwongoza nyoka huyo, ukisababisha afanye aliyofanya. Uwezo huo ulikuwa nini? Haikuwa mpaka karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu, wakati Yesu alipokuwa akifanya huduma yake hapa duniani, ndipo kitambulisho cha uwezo huo kikafunuliwa waziwazi.
7 Katika pindi moja, Yesu alikuwa akinena na viongozi wa kidini wa Kiyahudi wenye kujichukua kuwa waadilifu ambao walidai kwamba walikuwa wana wa Abrahamu. Na hali, wao walikuwa wamepinga kwa ushupavu kweli iliyohubiriwa na Yesu. Kwa hiyo Yesu akawaambia: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo [wakati alipoanza, NW]; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”—Yohana 8:44.
8 Maneno ya Yesu yalikuwa yenye nguvu na yalitoboa mambo waziwazi. Yeye alieleza Ibilisi kuwa “mwuaji” na ‘baba wa uwongo.’ Sasa, uwongo wa kwanza ulioandikwa ulinenwa na nyoka katika Edeni. Aliyesema uwongo huo kwa kweli ndiye aliyekuwa ‘baba wa uwongo.’ Zaidi ya hayo, uwongo huo ulitokeza kifo cha Adamu na Hawa, ukimfanya mwongo huyo wa kale mwuaji wa kukusudia. Kwa wazi, basi, uwezo ulioongoza nyoka katika Edeni ulikuwa ni Shetani Ibilisi, na kwa kweli Yehova alikuwa akiongea na Shetani katika unabii huo wa kale.
9. Shetani alitokeaje?
9 Wengine wameuliza: Ikiwa Mungu ni mwema, ni kwa nini aliumba kiumbe kama Ibilisi? Maneno ya Yesu yatusaidia pia kujibu swali hilo. Yesu alisema hivi kuhusu Shetani: “[Yeye] alikuwa mwuaji wakati alipoanza.” Kwa hiyo Shetani alipomwambia Hawa uwongo, wakati huo ndipo alianza kuwa Shetani—kutoka kwa neno la Kiebrania linalomaanisha “mpinzani.” Mungu hakuumba Shetani. Malaika aliyekuwa mwaminifu hapo awali aliruhusu tamaa mbaya isitawi ndani ya moyo wake hivi kwamba akawa Shetani.—Kumbukumbu la Torati 32:4; linganisha Ayubu 1:6-12; 2:1-10; Yakobo 1:13-15.
Mbegu ya Nyoka
10, 11. Yesu na mtume Yohana watusaidiaje kutambua mbegu ya Nyoka?
10 Lakini, vipi juu ya ‘mbegu [uzao, UV] ya nyoka’? Maneno ya Yesu yatusaidia pia kutatua sehemu hii ya fumbo. Yeye aliwaambia viongozi wa kidini wa Kiyahudi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda.” Wayahudi hao walikuwa wazao wa Abrahamu, sawa na walivyojivuna. Lakini mwenendo wao mwovu uliwafanya kuwa wana wa kiroho wa Shetani, mwanzilishi wa dhambi.
11 Mtume Yohana akiandika kuelekea mwisho wa karne ya kwanza, aeleza waziwazi ni nani walio wa mbegu ya Nyoka, Shetani. Aandika: “Yeye anayeendelea kutenda dhambi atokana na Ibilisi, kwa sababu Ibilisi amekuwa akifanya dhambi tangu mwanzo. . . . Watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi wako wazi kupitia uhakika huu: Kila mmoja asiyeendelea kufanya uadilifu hatokani na Mungu, wala yeye asiyependa ndugu yake.” (1 Yohana 3:8, 10, NW) Kwa wazi, mbegu ya Nyoka wamekuwa wenye kuchacha sana katika historia yote ya kibinadamu!
Ni Nani Mbegu ya Mwanamke?
12, 13. (a) Yehova alifunuliaje Abrahamu kwamba mbegu ya mwanamke ingetokea miongoni mwa wazao wake? (b) Ni nani aliyerithi ahadi iliyohusu Mbegu?
12 Basi, ni nani ‘mbegu [au uzao, UV] ya mwanamke’? Hilo ni mojawapo maswali ya maana zaidi yaliyopata kuulizwa, kwa maana mbegu ya mwanamke ndiyo ambayo hatimaye itaponda kichwa cha Shetani na kuondoa matokeo yote maovu ya ule uasi wa awali. Nyuma katika karne ya 20 K.W.K., Mungu alifunulia mwanamume mwaminifu Abrahamu kidokezi kikubwa juu ya kitambulisho cha huyo. Kwa sababu ya imani kubwa ya Abrahamu, Mungu alifanya mfululizo wa Ahadi kwake juu ya uzao ambao ungezaliwa kwake. Mojawapo hizo ilionyesha wazi kwamba ‘mbegu ya mwanamke’ ambayo ‘ingechubua kichwa cha nyoka’ ingetokea miongoni mwa watoto wa Abrahamu. Mungu alimwambia: “Uzao [mbegu, NW] wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao [mbegu, NW] wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”—Mwanzo 22:17, 18.
13 Kwa kadiri miaka ilivyopita, ahadi ya Yehova kwa Abrahamu ilirudiwa kwa Isaka mwana wa Abrahamu na kwa Yakobo mjukuu wake. (Mwanzo 26:3-5; 28:10-15) Hatimaye, wazao wa Yakobo wakawa makabila 12, na moja la makabila hayo, Yuda, lilipokea ahadi ya pekee: “Fimbo ya kifalme haitaondoka kwa Yuda, wala gongo la mwenye amri kati ya miguu yake, mpaka Shilo aje; ambaye watu watamtii.” (Mwanzo 49:10, NW) Kwa wazi, Mbegu angetokea katika kabila la Yuda.
14. Ni taifa gani lililopangwa kitengenezo liwe tayari kwa ajili ya kuja kwa Mbegu?
14 Mwishoni mwa karne ya 16 K.W.K., makabila 12 ya Israeli yalipangwa kitengenezo kuwa taifa wakiwa watu pekee wa Mungu. Kwa kusudi hilo, Mungu alifanya agano zito pamoja nao na kuwapa orodha ya sheria. Sababu kuu ya hilo ilikuwa kutayarisha kikundi cha watu kwa ajili ya kuja kwa Mbegu. (Kutoka 19:5, 6; Wagalatia 3:24) Tangu wakati huo na kuendelea, uadui wa Shetani kuelekea Mbegu ya mwanamke ulionekana katika uhasama wa mataifa kuelekea watu wachaguliwa wa Mungu
15. Ni kidokezi gani cha mwisho kilichotolewa juu ya familia ambayo miongoni mwa wazao wa Abrahamu ingetokeza Mbegu?
15 Kidokezi cha mwisho juu ya familia ambayo ingetokeza Mbegu kilitolewa katika karne ya 11 K.W.K. Wakati huo, Mungu alinena na Daudi, mfalme wa pili wa Israeli, na kumwahidi kwamba Mbegu angetoka katika ukoo wake na kwamba kiti cha ufalme cha Huyu ‘kingethibitishwa milele.’ (2 Samweli 7:11-16) Tangu hatua hiyo na kuendelea, Mbegu angeweza kurejezewa kwa kufaa kuwa mwana wa Daudi.—Mathayo 22:42-45.
16, 17. Isaya alielezaje juu ya baraka ambazo Mbegu angeleta?
16 Katika miaka iliyofuata, Mungu alitokeza manabii ili kutoa habari zaidi iliyopuliziwa naye juu ya kuja kwa Mbegu. Kwa kielelezo, katika karne ya nane K.W.K., Isaya aliandika: “Kwa maana kumekuwa na mtoto ambaye amezaliwa kwetu sisi, kumekuwa na mwana ambaye amepewa kwetu sisi; na utawala wa kimwana-mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mweza, Baba wa Milele, Mwana-Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa kimwana-mfalme na kwa amani kutakuwa hakuna mwisho, juu ya kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake.”—Isaya 9:6, 7, NW.
17 Isaya alitoa unabii zaidi juu ya Mbegu: “Kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili. . . . Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja . . . Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA [Yehova, NW], kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:4-9) Lo! jinsi mbegu angeleta baraka tele!
18. Danieli aliandika habari gani zaidi juu ya Mbegu?
18 Katika karne ya sita kabla ya Wakati wa Kawaida wetu, Danieli aliandika unabii zaidi juu ya Mbegu. Alitabiri wakati ambapo mmoja kama mwana wa Adamu angetokea mbinguni na alisema “naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie.” (Danieli 7:13, 14) Kwa hiyo Mbegu mwenye kuja angerithi Ufalme wa kimbingu, na mamlaka yake ya kifalme ingeenea juu ya dunia yote.
Fumbo Latatuliwa
19. Mariamu alipaswa atimize sehemu gani katika kuja kwa Mbegu, kama alivyofunua malaika?
19 Mwishowe kitambulisho cha Mbegu kilifunuliwa mwanzoni mwa Wakati wa Kawaida wetu. Katika mwaka 2 K.W.K., malaika mmoja alitokea msichana mchanga wa Kiyahudi aliyeitwa Mariamu, aliyekuwa mzao wa Daudi. Malaika alimwambia kwamba angezaa mtoto wa pekee sana naye akasema: “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana [Yehova, NW] Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:32, 33) Kwa hiyo kule kungoja sana “mbegu” mwishowe kulikuwa kunafikia mwisho.
20. Mbegu aliyeahidiwa ni nani, naye alihubiri ujumbe gani katika Israeli?
20 Katika mwaka 29 W.K. (tarehe iliyotajwa mapema sana na Danieli), Yesu alibatizwa. Ndipo roho takatifu iliposhuka juu yake, na Mungu akamkiri kuwa Mwana wake. (Danieli 9:24-27; Mathayo 3:16, 17) Kwa miaka mitatu na nusu baada ya hapo, Yesu alitoa ushahidi kwa Wayahudi, akitangaza: “Ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mathayo 4:17) Wakati huo, yeye alitimiza unabii mwingi sana kutoka Maandiko ya Kiebrania hivi kwamba kukawa hakuna nafasi ya kutia shaka kwamba yeye alikuwa ndiye Mbegu aliyeahidiwa.
21. Wakristo wa kwanza walielewa nini juu ya kitambulisho cha Mbegu?
21 Wakristo wa mapema walielewa na hilo vizuri. Paulo aliwaeleza Wakristo katika Galatia hivi: “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao [mbegu] wake. Hasemi, Kwa wazao [mbegu], kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao [mbegu] wako, yaani, Kristo.” (Wagalatia 3:16) Yesu angekuwa ndiye “Mwana-Mfalme wa Amani” aliyetabiriwa na Isaya. Baada ya yeye kuja kwenye Ufalme wake mwishowe, haki na uadilifu vingethibitishwa ulimwenguni pote.
Basi, Mwanamke Huyo Ni Nani?
22. Mwanamke anayerejezewa katika unabii wa Yehova katika Edeni ni nani?
22 Ikiwa Yesu ndiye Mbegu, mwanamke aliyerejezewa nyuma katika Edeni ni nani? Kwa kuwa uwezo ulioongoza nyoka ulikuwa ni kiumbe cha kiroho, hatupaswi kushangaa kwamba mwanamke huyo pia ni roho na si mwanadamu. Mtume Paulo alinena juu ya “mwanamke” wa kimbingu aliposema: “Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana [huru, NW], naye ndiye mama yetu sisi.” (Wagalatia 4:26) Maandiko mengine yaonyesha kwamba huyu “Yerusalemu wa juu” alikuwa tayari amekuwapo kwa mamileani. Yeye ndiye tengenezo la kimbingu la Yehova la viumbe wa kiroho, ambao kutoka kwao Yesu alishuka ili kutimiza fungu la ‘mbegu ya mwanamke.’ Ni “mwanamke” wa kiroho wa aina hii tu ndiye angeweza kuvumilia uadui wa yule “nyoka wa zamani” kwa mamileani.—Ufunuo 12:9; Isaya 54:1, 13; 62:2-6.
23. Kwa nini ufunuaji wa hatua kwa hatua wa maana ya unabii wa Yehova wa Kiedeni watokeza sana?
23 Pitio hili fupi la usitawi wa unabii huo wa kale katika Mwanzo 3:15 ni ushuhuda wenye nguvu wa upatano mtukufu wa Biblia. Ni jambo la kutokeza kweli kweli kwamba unabii huo waweza kueleweka tunapounganisha tu matukio na semi kutoka karne ya 20, ya 11, ya 8, na ya 6 K.W.K. pamoja na semi na matukio ya tangu karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu. Hayo hayawezi kuwa yalitukia kwa nasibu. Lazima kuwe kulikuwako mkono wenye kuongoza yote hayo.—Isaya 46:9, 10.
Maana ya Hayo Kwetu
24. Kutambulishwa kwa Mbegu kwamaanisha nini kwetu?
24 Yote hayo yamaanisha nini kwetu? Yesu ndiye ‘mbegu ya mwanamke’ iliyo kuu. Unabii huo wa kale katika Mwanzo 3:15, NW, ulitabiri kwamba kisigino chake ‘kingechubuliwa’ na Nyoka, na hilo lilitukia wakati Yesu alipokufa kwenye mti wa mateso. Chubuko si la kudumu. Hivyo, kulikoonekana kama kwamba ni kufaulu kwa Nyoka kuligeuzwa upesi kukawa kushindwa wakati Yesu alipofufuliwa. (Kama tulivyoona katika Sura 6, kuna uthibitisho mwingi sana kwamba jambo hilo lilitukia.) Kifo cha Yesu kikawa msingi wa wokovu kwa ajili ya ainabinadamu yenye moyo wenye haki, kwa hiyo Mbegu akaanza kuwa baraka, sawa na ambavyo Mungu alikuwa amemwahidi Abrahamu. Lakini vipi juu ya ule unabii mwingi kwamba Yesu angetawala kutoka ufalme wa kimbingu juu ya milki yake yote ya kidunia?
25, 26. Ni suala gani lililohusika katika uadui kati ya ‘mbegu ya mwanamke’ na Nyoka, kama inavyoelezwa katika Ufunuo?
25 Katika njozi ya kiunabii yenye kuonyesha mambo wazi iliyoandikwa katika Ufunuo sura 12, mwanzo wa Ufalme wake wafananishwa na kuzaliwa kwa mtoto wa kiume katika mbingu. Katika Ufalme huo, Mbegu aliyeahidiwa atwaa mamlaka chini ya cheo Mikaeli, likimaanisha “Ni Nani Aliye Kama Mungu?” Yeye aonyesha kwamba hakuna yeyote anayeweza kukaidi kwa haki enzi kuu ya Yehova, anapotupa yule “nyoka wa zamani” kutoka mbingu asiweze kurudi tena. Twasoma: “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi.”—Ufunuo 12:7-9.
26 Tokeo ni faraja kwa mbingu lakini taabu kwa dunia. “Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake,” ikatoka sauti ya shangwe ya ushindi. Na zaidi, twasoma: “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”—Ufunuo 12:10, 12.
27. Unabii juu ya Shetani kutupwa kutoka mbingu ulitimizwa wakati gani? Twajuaje?
27 Je! twaweza kusema unabii huu ulipasa utimizwe wakati gani? Kwa kweli, hilo ndilo swali lililotokezwa na wanafunzi walipouliza Yesu juu ya ‘ishara ya kuwapo kwake na ya umalizio wa mfumo wa mambo’—kama tulivyozungumza katika Sura 10. (Mathayo 24:3, NW) Kama tulivyoona, uthibitisho ni mwingi sana kwamba kuwapo kwa Yesu katika mamlaka ya Ufalme wa kimbingu kulianza katika 1914. Tangu wakati huo, tumeona kweli kweli “ole wa nchi”!
28, 29. Ni mabadiliko gani makubwa katika tamasha ya kidunia yaliyoko mbele, na twajuaje kwamba yatatukia karibuni?
28 Lakini angalia: Sauti hiyo ya kimbingu ilitangaza kwamba Shetani ana “wakati mchache tu.” Kwa hiyo ule unabii wa awali katika Mwanzo 3:15 unaelekea kwenye upeo wao usiokosea. Yule nyoka, mbegu yake, yule mwanamke, na mbegu yake wametambulishwa wote. Mbegu ‘alichubuliwa kisigino,’ lakini akapata nafuu. Karibuni, kupondwa kwa Shetani (na mbegu yake) kutaanza chini ya Mfalme wa Mungu anayetawala sasa, Kristo Yesu.
29 Hilo litahusisha mabadiliko makubwa sana kwenye tamasha ya dunia. Pamoja na Shetani, wale wanaojithibitisha kuwa mbegu yake wataondolewa. Kama alivyotoa unabii mtunga zaburi: “Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.” (Zaburi 37:10) Lo! hilo litakuwa badiliko kubwa kama nini! Kisha, maneno yanayofuata ya mtunga zaburi yatatimizwa: “Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11.
30. Kwa nini watiaji shaka wanaotilia shaka kupuliziwa kwa Biblia na Mungu na hata kuwapo kwa Mungu ndio wasioona uhalisi wa mambo?
30 Katika njia hiyo, mwishowe “Mwana-Mfalme wa Amani” ataletea ainabinadamu amani. Hiyo ndiyo ahadi ya Biblia, kama tulivyoona katika Isaya 9:6, 7. Katika kizazi hiki chenye kutia shaka, wengi huona ahadi kama hiyo kuwa si halisi. Lakini binadamu atoa nini badala? Hakuna! Kwa upande mwingine, ahadi hiyo imesemwa wazi katika Biblia, na Biblia ni Neno la Mungu lisilokosea. Kwa kweli watiaji shaka hao ndio wasioangalia uhalisi wa mambo. (Isaya 55:8, 11) Wanapuuza Mungu, ambaye alipulizia Biblia na ambaye ndiye uhalisi mkubwa zaidi ya wote.
-