Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 5/15 kur. 8-9
  • Biblia ya Kigothi—Utimizo wa Ajabu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Biblia ya Kigothi—Utimizo wa Ajabu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ulfilas—Mmishonari na Mtafsiri wa Biblia
  • Historia ya Mapema ya Biblia ya Kigothi
  • Hati za Mkono Zilizookoka
  • Kuhifadhi Maandiko ya Biblia ya Kigothi
  • Kodeksi ya Vatikani—Kwa Nini Ni Yenye Thamani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Kutangaza Neno la Mungu Katika Hispania ya Enzi za Kati
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Kugunduliwa Kwa Hazina ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Tarehe ya Hati za Zamani Hujulikanaje?
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 5/15 kur. 8-9

Biblia ya Kigothi—Utimizo wa Ajabu

WAGOTHI walikuwa shirikisho la makabila ya Ujerumani, labda wakitoka Skandinevia. Katika karne za mapema za Wakati Wetu wa Kawaida, wao walihamia mbali kusini kufikia Bahari Nyeusi na mto Danube, hadi sehemu za mbali za Milki ya Roma.

Kazi ya kwanza kabisa ya uandishi iliyopata kutokezwa katika lugha yoyote ya Kijerumani ilikuwa Biblia ya Kigothi. Leo visehemu-visehemu tu vya tafsiri hiyo ndivyo vinavyopatikana. Hata hivyo, bado yabaki ikiwa tafsiri isiyo na kifani na yenye thamani ya Maandiko Matakatifu. Kwa nini?

Ulfilas—Mmishonari na Mtafsiri wa Biblia

Mtafsiri wa Biblia hiyo aliitwa Ulfilas, ambaye ajulikana kwa jina lake la Kigothi Wulfila. Kulingana na mwanahistoria Philostorgius, Ulfilas alikuwa mzao wa watu waliotekwa katika mashambulizi ya Wagothi wakati hao walipovamia Kapadosia, ambayo sasa ni sehemu ya mashariki mwa Uturuki. Akiwa amezaliwa karibu na mwaka 311 W.K., aliwekwa rasmi na Eusebio wa Nicomedia miaka yapata 30 baadaye naye alijizoeza kufanya kazi miongoni mwa Wagothi akiwa mishonari.

“Ili afundishe na kuongeza waongofu wake,” asema mwanahistoria Will Durant, “yeye alitafsiri kwa saburi Biblia nzima isipokuwa Vitabu vya Wafalme kutoka kwa Kigiriki hadi Kigothi.” (The Age of Faith) Leo hii, hati za mkono za Biblia za Kigothi zinazopatikana pekee ni visehemu vya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo pamoja na kisehemu cha kitabu cha Nehemia.

Kigothi hakikuwa lugha ya kuandikwa. Kwa hiyo Ulfilas alikabiliwa na ugumu wa kutafsiri uliohitaji akili ya hali ya juu sana. Wanahistoria wa kale wa mambo ya makasisi wasema kwamba ni yeye aliyevumbua alfabeti yenye herufi 27 za Kigothi, iliyotegemea sanasana Kigiriki na Kilatini. Na zaidi, The New Encyclopædia Britannica yataja kwamba “alivumbua maneno ya Kikristo katika Kijerumani, baadhi yayo yangali yanatumiwa.”

Historia ya Mapema ya Biblia ya Kigothi

Ulfilas alimaliza tafsiri yake kabla ya 381 W.K. na kufa miaka miwili au mitatu baadaye. Kupendwa kwa kazi yake kwaonyeshwa na The Encyclopedia Americana, isemayo kwamba “tafsiri hiyo ilikuwa ikitumiwa hasa na Wagothi waliohamia Hispania na Italia.” Kwa kweli, kwa kutazama hesabu ya visehemu ambavyo vimeokoka, yaonekana kwamba nakala nyingi za Biblia hiyo ya Kigothi zilitengenezwa. Yaelekea kwamba hati nyingi za mkono zilitokezwa katika skriptoria ya Ravenna na Verona, katika eneo ambalo Wagothi walikuwa wamesimamisha ufalme wao. Skriptoria zilikuwa vyumba katika makao ya watawa ambamo hati za mkono ziliandikwa na kunakiliwa.

Wagothi walikoma kuwa taifa karibu na mwaka 555 W.K., baada ya maliki wa Bizantini Justinian 1 kushinda tena Italia. Baada ya Wagothi kuisha, asema Tönnes Kleberg, “lugha na desturi za Kigothi zilitokomea katika Italia, bila kuacha masalio. Hati za mkono katika Kigothi hazikupendeza tena. . . . Kwa sehemu kubwa ziliondolewa na kufutwa maandishi. Kisha ngozi hiyo iliyokuwa na thamani kubwa ilitumiwa tena kuandika mambo mapya.”

Hati za Mkono Zilizookoka

Baadhi ya hati hizo za mkono hazikufutwa vizuri zikiacha maandishi ya awali zingali zikionekana kwa umbali. Baadhi ya hati hizo za mkono zimepatikana na maandishi yayo kutambuliwa. Kwa kutokeza, ile Kodeksi Argenteus iliyo maarufu sana, yenye zile Gospeli nne kwa mfuatano wa Mathayo, Yohana, Luka, na Marko, iliokoka bila kuguzwa.

Inafikiriwa kwamba kodeksi hiyo nzuri ajabu ilitoka skriptoriamu ya Ravenna mwanzo-mwanzo wa karne ya sita W.K. Inaitwa Kodeksi Argenteus, linalomaanisha “Kitabu cha Fedha,” kwa sababu kiliandikwa kwa wino wa fedha. Kurasa zacho za ngozi zina rangi ya zambarau iliyokaushwa, jambo linaloonyesha kwamba labda ilitengenezwa kwa ajili ya mtu wa kifalme. Maandishi ya rangi ya dhahabu yaanzisha mistari mitatu ya kwanza ya kila Gospeli na vilevile vyanzo vya visehemu tofauti-tofuati. Majina ya waandikaji wa Gospeli pia yameandikwa kwa dhahabu juu ya “mafungu” manne yenye kuambaana yaliyowekwa chini ya kila safu ya maandishi. Hayo yanarejezea mafungu yanayofanana nayo katika zile Gospeli.

Kuhifadhi Maandiko ya Biblia ya Kigothi

Baada ya kutokomea kwa taifa la Gothi, Kodeksi Argenteus ya thamani kubwa ilipotea. Haikuonekana tena mpaka ilipopatikana katikati ya karne ya 16 ikiwa ndani ya makao ya watawa ya Werden, karibu na Cologne, Ujerumani.

Katika mwaka wa 1569, tafsiri ya Kigothi ya Sala ya Bwana ilichapishwa, ikielekeza uangalifu kwenye Biblia iliyonakiliwa. Jina Kodeksi Argenteus lilionekana kwa mara ya kwanza katika 1597. Kutoka Werden hati hiyo ya mkono ilitiwa ndani ya mkusanyo wa sanaa wa maliki katika Prague. Hata hivyo, kwenye mwisho wa Vita ya Miaka Thelathini katika 1648, Wasweden walioshinda vita hiyo waliibeba pamoja na vitu vingine vya thamani. Tangu 1669 kodeksi hiyo imepata makao ya kudumu katika Uppsala University Library, Sweden.

Hapo awali Kodeksi ya Argenteus ilikuwa na kurasa 336, na 187 kati yazo ziko katika Uppsala. Ukurasa mwingine mmoja—wa mwisho katika Gospeli ya Marko—ulivumbuliwa mnamo 1970 katika Speyer, Ujerumani.

Kutoka wakati kodeksi hiyo ilipatikana tena, wanachuo walianza kusoma maandishi ili watambue maana ya lugha ya Kigothi ambayo haikuwa ikitumiwa tena. Wakitumia hati zote za mkono zinazopatikana na majaribio ya awali ya kuandika tena maandishi hayo, mwanachuo Mjerumani Wilhelm Streitberg aliunganisha na kuchapisha “Die gotische Bibel” (Biblia ya Kigothi) katika 1908, ikiwa na maandishi ya Kigiriki na Kigothi kwenye ukurasa mkabala.

Leo, Biblia ya Kigothi hupendeza hasa wanachuo. Lakini jambo la kwamba ilitokezwa na kuthaminiwa katika nyakati za mapema za kutafsiri Biblia lathibitisha tamaa na azimio la Ulfilas la kutafsiri Neno la Mungu kwa lugha ambayo wakati huo ilikuwa ya kisasa. Alitambua kwa usahihi kwamba ni kupitia njia hiyo pekee Wagothi wangetumaini kuelewa kweli ya Kikristo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

Kwa hisani ya Uppsala University Library, Sweden

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki