Mahakama ya Juu ya Ulaya Yaunga Mkono Haki ya Kuhubiri Katika Ugiriki
KWA nini mtu anayesifiwa na majirani wake akamatwe zaidi ya mara 60 tangu 1938? Kwa nini mwenye-duka huyo mwenye kufuatia haki kutoka kisiwa cha Ugiriki cha Krete aletwe mbele ya mahakama za Ugiriki mara 18 na kutumikia zaidi ya miaka sita gerezani? Naam, kwa nini mtu huyo wa familia mwenye bidii ya kazi, Minos Kokkinakis, atwaliwe kutoka kwa mke wake na watoto wake watano na kuhamishwa apelekwe kwenye visiwa mbalimbali vya kifungo?
Sheria zilizopitishwa katika 1938 na 1939 za kukataza kugeuza watu kidini ndizo hasa zilizosababisha hilo. Sheria hizo zilisimamishwa na dikteta mmoja Mgiriki Ioannis Metaxas, aliyekuwa akitenda chini ya uvutano wa Kanisa Orthodoksi la Kigiriki.
Likiwa tokeo la sheria hiyo, Mashahidi wa Yehova walikamatwa mara 19,147, tangu 1938 hadi 1992, na mahakama zilifikiliza hukumu zilizojumulika kuwa miaka 753, ambazo 593 kati yazo ndizo zilitumikiwa hasa. Hayo yote yalifanywa kwa sababu Mashahidi katika Ugiriki, kama kwingineko, hufuata maagizo ya Yesu Kristo “kufanya wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, . . . kuwafundisha kuyashika mambo yote” aliyoamuru.—Mathayo 28:19, 20, NW.
Lakini katika Mei 25, 1993, ushindi mtukufu kwa ajili ya uhuru wa ibada ulipatikana! Katika tarehe hiyo Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika Strasbourg, Ufaransa, iliunga mkono haki ya raia Mgiriki ya kufundisha wengine itikadi zake. Kwa kutoa hukumu hiyo, mahakama ya juu hiyo ya Ulaya iliandaa ulinzi mpana kwa ajili ya uhuru wa kidini ambao huenda ukaathiri sana maisha za watu kila mahali.
Ebu tuangalie kwa ukaribu zaidi matukio, kutia na mambo ya kuvunjia heshima yaliyompata raia mmoja tu Mgiriki, ambayo yaliongoza kwenye uamuzi huo wa mahakama wenye maana sana.
Historia ya Mapema
Katika 1938 raia huyo, Minos Kokkinakis, alikuwa Shahidi wa Yehova wa kwanza kuhukumiwa chini ya sheria ya Ugiriki inayofanya kugeuza watu kidini kuwa kitendo cha uhalifu. Bila kujaribiwa mahakamani, alipelekwa akatumikie muda wa miezi 13 akiwa uhamishoni kwenye kisiwa cha Aegea cha Amorgos. Katika 1939 alihukumiwa mara mbili na kufungwa gerezani kwa miezi miwili na nusu kila mara.
Katika 1940, Kokkinakis alihamishwa kwa miezi sita kwenye kisiwa cha Melos. Mwaka uliofuata, katika Vita ya Ulimwengu 2, alifungwa katika gereza la kijeshi katika Athene kwa zaidi ya miezi 18. Kuhusu kipindi hicho, yeye akumbuka hivi:
“Ukosefu wa chakula gerezani ulizidi kuwa mbaya. Tulikuwa wanyonge sana hivi kwamba hatukuweza kutembea. Ikiwa isingalikuwa kwa sababu ya Mashahidi kutoka Athene na maeneo ya Piraeus waliotuandalia chakula kutoka ugavi wao mchache sana, tungalikufa.” Baadaye katika 1947, alihukumiwa tena akatumikia miezi mingine minne na nusu gerezani.
Katika 1949, Minos Kokkinakis alihamishwa apelekwe kwenye kisiwa cha Makrónisos, jina linalotokeza maono ya kuogofya akilini mwa Wagiriki kwa sababu ya gereza lililoko huko. Miongoni mwa wafungwa wapatao 14,000 waliofungwa katika Makrónisos wakati huo, 40 hivi walikuwa Mashahidi. Ensaiklopedia ya Kigiriki Papyros Larousse Britannica yaonelea hivi: “Njia za mateso makatili, . . . hali za kuishi, ambazo hazifai taifa lililoerevuka, na mwenendo wa walinzi wenye kushusha heshima kuwaelekea wafungwa. . . . ni fedheha kwa historia ya Ugiriki.”
Kokkinakis, aliyetumia mwaka mmoja katika gereza la Makrónisos, alisimulia hali hivi: “Askari-jeshi, kama vile washiriki wa Baraza la Kuhukumu Wazushi wa Kidini, walikuwa wakihoji kila mfungwa kutoka asubuhi hadi jioni. Maneno hayawezi kueleza yale mateso waliyosababisha. Wafungwa wengi walipoteza akili zao; wengine waliuawa; wengi sana waliachwa wakiwa wamelemaa kimwili. Katika masiku hayo mabaya sana tuliposikia vilio na kuugua kwa wale waliokuwa wakiteswa, tulikuwa tukisali tukiwa kikundi.”
Baada ya kunusurika magumu katika Makrónisos, Kokkinakis alikamatwa mara nyingine sita katika miaka ya 1950 akatumikia muda wa miezi kumi gerezani. Katika miaka ya 1960 alikamatwa mara nyingine nne akahukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani. Lakini kumbuka, Minos Kokkinakis alikuwa mmoja tu miongoni mwa mamia ya Mashahidi wa Yehova ambao kwa muda wa miaka iliyopita walikamatwa na kufungwa gerezani kwa sababu walisema na wengine juu ya imani yao!
Hayo mambo mabaya sana yasiyo ya haki yaliyoendelezwa dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika Ugiriki yalikujaje hatimaye kuwa mbele ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu?
Kesi Iliyoweka Mwongozo
Kesi hiyo ilianza katika Machi 2, 1986. Katika tarehe hiyo Minos Kokkinakis, ambaye wakati huo alikuwa mfanya-biashara aliyestaafu mwenye umri wa miaka 77, na mke wake walitembelea nyumba ya Bi. Georgia Kyriakaki katika Sitia, Krete. Mume wa Bi. Kyriakaki, aliyekuwa mwongoza-kwaya katika kanisa Orthodoksi la mahali hapo, aliwaarifu polisi. Polisi walikuja wakawakamata Bw. na Bi Kokkinakis, ambao walipelekwa kwenye kituo cha polisi cha mahali hapo. Walilazimika kulala usiku kucha huko.
Ni nini lililokuwa shtaka dhidi yao? Lilelile lililofanywa dhidi ya Mashahidi wa Yehova mara elfu nyingi katika ile miaka 50 iliyotangulia, yaani, kwamba walikuwa wakigeuza watu kidini. Katiba ya Ugiriki (1975), Kifungu cha 13, yasema hivi: “Kugeuza watu kidini kwakatazwa.” Fikiria pia sheria ya Ugiriki, sehemu ya 4, namba 1363/1938 na 1672/1939, inayofanya kugeuza watu kidini kuwa kitendo cha uhalifu. Hiyo yasema:
“‘Kugeuza watu kidini’ kwamaanisha, hasa, jaribio lolote la moja kwa moja au lisilo la moja kwa moja la kuingilia kwa jeuri itikadi za kidini za mtu wa dini tofauti . . . , kwa kusudi la kudhoofisha itikadi hizo, ama kwa aina yoyote ya kishawishi au ahadi ya kushawishi au kuunga mkono au kutegemeza kimwili, au kwa nia za kupunja au kwa kutumia kwa ubinafsi ukosefu wake wa maarifa, kutumaini kwake, uhitaji wake, akili zake chache au kutojua kwake.”
Mahakama ya Uhalifu katika Lasithi, Krete, ilisikia kesi hiyo katika Machi 20, 1986, ikawapata Bw. na Bi. Kokkinakis kuwa wenye hatia ya kugeuza watu kidini. Wote wawili walihukumiwa kifungo cha miezi minne gerezani. Katika kuwahukumu mume na mke huyo, mahakama ilijulisha kwamba washtakiwa hao walikuwa wameingilia kwa jeuri “itikadi za kidini za Wakristo wa Orthodoksi . . . kwa kutumia kwa ubinafsi ukosefu wao wa maarifa, akili zao chache na kutojua kwao.” Washtakiwa hao walishtakiwa pia “kumtia moyo [Bi. Kyriakaki] kwa kutumia maelezo yao yenye akili, na ustadi . . . ili kubadili itikadi zake za Kikristo za Orthodoksi.”
Uamuzi huo ulikatiwa rufani kwenye Mahakama ya Rufani ya Krete. Katika Machi 17, 1987, mahakama hiyo ya Krete ilimwachilia Bi. Kokkinakis lakini iliunga mkono hukumu ya mume wake, ingawa ilipunguza kifungo chake cha gerezani kuwa cha miezi mitatu. Hukumu hiyo ilidai kwamba Bw. Kokkinakis alikuwa “ametumia kwa ubinafsi ukosefu wa maarifa wa [Bi. Kyriakaki], akili yake chache na kutojua kwake.” Ilisema kwamba “alianza kusoma mafungu kutoka katika Andiko Takatifu, ambayo alichanganua kwa ustadi kwa njia ambayo mwanamke huyo Mkristo hakuweza kupinga, kwa sababu ya ukosefu wa maagizo ya msingi ya kutosha katika mafundisho.”
Katika maoni ya kupinga, mmoja wa mahakimu wa rufani aliandika kwamba Bw. Kokkinakis “alipasa kuachiliwa pia, kwani hakuna uthibitisho wowote unaoonyesha kwamba Georgia Kyriakaki . . . kwa kweli hakuwa na maarifa katika mafundisho ya Kikristo ya Orthodoksi, hasa akiwa ameolewa na mwongoza-kwaya, au kwa kweli alikuwa na akili chache au kwa kweli hakujua, hivi kwamba mshtakiwa aliweza kutumia hali hiyo kwa ubinafsi . . . [hivyo] akimshawishi kuwa mshiriki wa farakano la Mashahidi wa Yehova.”
Bw. Kokkinakis alikata kesi hiyo rufani kwenye Mahakama ya Juu Zaidi ya Ugiriki. Lakini mahakama hiyo ilikataa rufani hiyo katika Aprili 22, 1988. Kwa hiyo katika Agosti 22, 1988, Bw. Kokkinakis alitoa ombi kwenye Tume ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Hatimaye ombi lake lilikubaliwa katika Februari 21, 1992, akakubaliwa kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.
Masuala ya Kesi
Kwa kuwa Ugiriki ni taifa-shiriki la Baraza la Ulaya, ina wajibu wa kutii Vifungu vya Mkataba wa Ulaya juu ya Haki za Kibinadamu. Kifungu cha 9 cha Mkataba huo chasomwa hivi: “Kila mtu ana haki ya uhuru wa wazo, dhamiri na dini; haki hiyo yatia ndani uhuru wa kubadili dini yake au itikadi yake na uhuru wa, kudhihirisha dini au itikadi yake, katika kuabudu, kufundisha, kuzoeza na kushika, akiwa peke yake au pamoja na wengine na akiwa hadharani au faraghani.”
Hivyo, serikali ya Ugiriki ikawa mshtakiwa katika mahakama ya Ulaya. Ilishtakiwa kuvunja waziwazi haki ya msingi ya raia Mgiriki ya kuzoeza dini kulingana na amri ya Yesu Kristo, yaani, ‘kufundisha na kufanya wanafunzi.’ (Mathayo 28:19, 20) Zaidi ya hayo, mtume Petro alisema hivi: “[Yesu] a[li]tuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia.”—Matendo 10:42.
Toleo la pekee la 1992 la European Magazine on Human Rights lilikuwa na kichwa cha jalada “Ugiriki—Kuvunja Kimakusudi Haki za Kibinadamu.” Gazeti hilo lilieleza hivi kwenye ukurasa 2: “Ugiriki ndiyo nchi pekee katika EC [Jumuiya ya Ulaya] na katika Ulaya yenye sheria ya kuadhibu inayoandaa faini na vifungo vya gerezani vifikilizwe juu ya yeyote anayemsukuma mtu mwingine abadili dini yake.”
Kwa hiyo kufikia wakati huo kulikuwa msisimuko mwingi ndani na nje ya mazingira ya kisheria. Ni nini kingeamuliwa kuhusu sheria ya Ugiriki inayokataza mtu asifundishe wengine itikadi zake?
Kikao Katika Strasbourg
Hatimaye, siku ya kikao ikafika—Novemba 25, 1992. Kulikuwa mawingu mazito juu ya Strasbourg, na ilikuwa baridi sana, lakini ndani ya Mahakama mawakili walitoa hoja zao kwa uchangamfu. Kwa muda wa saa mbili uthibitisho ulitolewa. Profesa Phedon Vegleris, wakili wa Kokkinakis, alifikia kiini cha suala hilo, akiuliza hivi: ‘Je! sheria hiyo yenye kizuizi inayokusudiwa kuwalinda washiriki wa Kanisa Orthodoksi la Kigiriki dhidi ya kugeuzwa kwenye itikadi nyingine za kidini inapaswa kuendelea kuwako na kutumiwa?’
Akionyesha kufadhaika waziwazi, Profesa Vegleris aliuliza hivi: “Ninajiuliza kwa nini sheria hiyo ya [kugeuza watu kidini] husawazisha dini ya orthodoksi na ujinga na kutokujua kitu. Sikuzote nilikuwa nikijiuliza kwa nini dini ya orthodoksi yahitaji ulinzi dhidi ya ujinga, dhidi ya kutoweza kiroho . . . Hilo ni jambo linalonifadhaisha na kunishtua.” Kwa wazi, mwakilishi wa serikali hakuweza kuandaa tukio moja ambalo katika hilo sheria hiyo ilitumiwa kwa mwingine yeyote ila Mashahidi wa Yehova.
Wakili wa pili wa Kokkinakis, Bw. Panagiotis Bitsaxis, alionyesha jinsi sheria ya kugeuza watu kidini isivyofaa. Alisema hivi: “Kukubali kuvutiana ni jambo la lazima kwa maongezi kati ya watu wazima. Kama sivyo, tungekuwa jamii ya kiajabu-ajabu ya hayawani wanyamavu, ambao wangefikiri lakini wasijieleze, ambao wangeongea lakini wasiwasiliane, ambao wangekuwako lakini wasiishi pamoja.”
Pia Bw. Bitsaxis alitoa hoji kwamba “Bw. Kokkinakis alilaumiwa si kwa sababu ya ‘jambo fulani alilofanya’ bali [kwa] ‘vile alivyo.’” Kwa hiyo, Bw. Bitsaxis alionyesha kwamba, kanuni za uhuru wa kidini zilikuwa zimevunjwa na pia kupondwa-pondwa kabisa.
Wawakilishi wa serikali ya Ugiriki walijaribu kutoa wazo lililo tofauti na lile la kweli, wakidai kwamba Ugiriki ni “paradiso ya haki za kibinadamu.”
Uamuzi
Tarehe iliyotazamiwa sana ya kutoa uamuzi ikafika—Mei 25, 1993. Wakiwa mahakimu sita dhidi ya watatu, Mahakama ilitoa hukumu kwamba serikali ya Ugiriki ilikuwa imevunja uhuru wa kidini wa Minos Kokkinakis mwenye umri wa miaka 84. Zaidi ya kutetea mwendo wake wa maisha wa huduma ya hadharani, ilimpa ridhaa ya dola 14,400. Hivyo Mahakama ilikatalia mbali hoja ya serikali ya Ugiriki kwamba Kokkinakis na Mashahidi wa Yehova hutumia mbinu zenye msongo wanapozungumza itikadi zao pamoja na wengine.
Ingawa Katiba ya Ugiriki na sheria ya zamani sana ya Ugiriki huenda ikakataza kugeuza watu kidini, mahakama ya juu katika Ulaya ilihukumu kwamba kutumia sheria hiyo ili kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova hakufai. Hakupatani na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya juu ya Haki za Kibinadamu.
Uamuzi wa mahakama ulieleza hivi: “Dini ilikuwa sehemu ya ‘mtiririko wa wazo la kibinadamu wenye kufanyika upya daima’ na haiwezekani kuiona kutokuwa sehemu ya mabishano ya hadharani.”
Maoni ya kukubaliana ya mmoja wa wale mahakimu tisa lilisema hivi: “Kugeuza watu kidini, kunakofasiliwa kuwa ‘bidii katika kueneza imani,’ hakuwezi kuadhibiwa hivyo; ni njia—ambayo yenyewe ni halali kabisa—ya ‘kudhihirisha dini ya mtu.’
“Katika kesi hii, mwombaji [Bw. Kokkinakis] alihukumiwa kwa sababu tu ya kuonyesha bidii hiyo, bila kufanya jambo lolote lisilofaa.”
Matokeo ya Uamuzi
Mwelekezo wa wazi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu ni kwamba maofisa wa serikali ya Ugiriki waache kutumia vibaya sheria inayokataza kugeuza watu kidini. Kwa kutumaini, Ugiriki itafuata mwelekezo wa mahakama hiyo na kuacha mnyanyaso wayo wa Mashahidi wa Yehova.
Kusudi la Mashahidi wa Yehova si kutokeza mabadiliko ya kijamii au kugeuza mfumo wa kisheria. Hangaiko lao kuu ni kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu kwa kutii amri ya Yesu Kristo. Hata hivyo, ili wafanye hivyo, wanafurahia ‘kutetea habari njema na kuithibitisha kisheria,’ kama vile mtume Paulo alivyofanya katika karne ya kwanza.—Wafilipi 1:7, NW.
Mashahidi wa Yehova ni raia wenye kutii sheria katika nchi zote wanamoishi. Hata hivyo, zaidi ya yote wanashurutishwa kutii sheria ya kimungu kama ambavyo imerekodiwa katika Biblia Takatifu. Kwa hiyo, sheria ya bara lolote ikiwakataza kusema na wengine juu ya itikadi zao zenye msingi wa Biblia, wanalazimika kuchukua msimamo huu wa kimitume: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”—Matendo 5:29.
[Sanduku katika kurasa za 28 na 29]
MNYANYASO ZAIDI WENYE KUCHOCHEWA NA MAKASISI
Majaribio ya makasisi katika Ugiriki ‘kutunga madhara kwa njia ya sheria’ yamekuwa yakiendelea kwa miongo kadhaa. (Zaburi 94:20) Tukio jingine kwenye kisiwa cha Krete lilisuluhishwa hivi karibuni. Nyuma katika 1987 askofu mmoja wa huko na makasisi 13 walikuwa wameshtaki Mashahidi tisa juu ya kugeuza watu kidini. Mwishowe, katika Januari 24, 1992, kesi hiyo ilifika mahakamani.
Mahakama ilikuwa imejaa pomoni. Makasisi wapatao 35 walikuwako ili kuunga mkono upande wa mshtaki. Hata hivyo, viti vingi vilikuwa tayari vimekaliwa na Mashahidi waliokuwa wamekuja kutia moyo ndugu zao Wakristo. Hata kabla ya taratibu za kawaida kuanza, wakili wa washtakiwa alionyesha makosa makubwa ya kisheria yaliyofanywa na mshtaki.
Tokeo likawa kwamba wale waliohusika katika taratibu hizo waliondoka ili kufanya mkutano wa faragha. Baada ya muda wa saa mbili na nusu wa kushauriana, Msimamizi wa Mahakama alitangaza kwamba wakili wa washtakiwa alikuwa amesema kweli. Kwa hiyo mashtaka dhidi ya Mashahidi hao tisa yalifutwa! Alihukumu kwamba uchunguzi ungehitaji kuanzishwa tena ili kuthibitisha kama washtakiwa walikuwa na hatia ya kugeuza watu kidini.
Mara tangazo hilo lilipofanywa, fujo ilitokea mahakamani. Makasisi walianza kutoa matisho na matukano kwa sauti kubwa. Kasisi mmoja alimshambulia wakili wa Mashahidi wa Yehova kwa kutumia msalaba akajaribu kumlazimisha auabudu. Polisi walilazimika kuingilia, na mwishowe Mashahidi wakaweza kuondoka kwa njia ya unyamavu.
Kesi ilipofutwa, mshtaki wa umma alitayarisha shtaka jipya dhidi ya wale Mashahidi tisa. Kesi iliwekwa katika Aprili 30, 1993, majuma matatu tu kabla ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kutoa uamuzi wayo katika kesi ya Kokkinakis. Mara nyingine tena makasisi wengi walihudhuria.
Mawakili wa wale washtakiwa tisa walitoa upinzani rasmi kwamba washtaki wa Mashahidi hao hawakuwapo mahakamani. Akiwa na haraka ya kutayarisha shtaka jipya, mshtaki wa umma alikuwa amefanya kosa zito la kutowapelekea washtaki mialiko ya kuhudhuria kesi. Kwa hiyo mawakili wa Mashahidi waliomba mahakama ifute kesi hiyo kwa msingi wa kosa hilo zito.
Kwa hiyo, mahakimu waliondoka mahakamani wakashauriana pamoja kwa muda wa saa moja hivi. Waliporudi, Msimamizi wa Mahakama, akiwa ameinamisha kichwa chake, aliwajulisha Mashahidi wote tisa kutokuwa na hatia juu ya mashtaka hayo.
Mashahidi katika Ugiriki walishukuru sana kwa ajili ya tokeo la kesi hiyo, na pia kwa ajili ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu katika kesi ya Kokkinakis ya Mei 25 wa mwaka huu. Sala zao ni kwamba kwa sababu ya ushindi huo wa kisheria, wataweza kuendeleza maisha zao za Kikristo ‘kwa utulivu, kwa unyamavu, na kwa ujitoaji kimungu na uzito kamili.’—1 Timotheo 2:1, 2, NW.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Minos Kokkinakis pamoja na mke wake