Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yp2 sura 19 kur. 156-163
  • Ninaweza Kupangaje Matumizi ya Pesa Zangu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ninaweza Kupangaje Matumizi ya Pesa Zangu?
  • Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jifunze Mambo ya Msingi
  • Kutambua Magumu
  • Dhibiti Matumizi
  • Naweza Kutumiaje Pesa Zangu Vizuri?
    Amkeni!—2006
  • Ninaweza Kudhibitije Matumizi Yangu ya Pesa?
    Vijana Huuliza
  • Jinsi ya Kupanga Matumizi ya Pesa
    Unaweza Kuwa na Familia Yenye Furaha
  • Daftari—Pesa
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
Pata Habari Zaidi
Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
yp2 sura 19 kur. 156-163

SURA YA 19

Ninaweza Kupangaje Matumizi ya Pesa Zangu?

Ni mara ngapi unapohisi kwamba huna pesa za kutosha?

□ Sijawahi

□ Mara kwa mara

□ Mara nyingi

Ni mara ngapi unapolazimika kukopa ili kununua vitu ambavyo kwa kweli vinapita uwezo wako?

□ Sijawahi

□ Mara kwa mara

□ Mara nyingi

Ni mara ngapi unaponunua kitu kwa sababu tu kimepunguzwa bei ingawa kwa kweli hukihitaji?

□ Sijawahi

□ Mara kwa mara

□ Mara nyingi

JE, WEWE huona kwamba huna pesa za kutosha? Ikiwa ungeweza kupata pesa zaidi, labda ungenunua kitu fulani unachotamani sana. Kama tu ungekuwa na mshahara mkubwa, ungeweza kununua viatu “unavyohitaji.” Au huenda ukajikuta katika hali kama ya Joan, ambaye anasema: “Nyakati nyingine marafiki wangu huniomba twende kwenye burudani zinazohitaji pesa nyingi. Ninapenda kustarehe pamoja na marafiki wangu. Hakuna mtu hutaka kusema, ‘Poleni, sitaweza kwenda kwa sababu sina pesa.’”

Badala ya kuhangaikia pesa ambazo huna, mbona usijifunze kupanga matumizi ya pesa ulizo nazo? Unaweza kungoja mpaka utakapoanza kujitegemea ndipo ujifunze jinsi ya kutumia pesa. Lakini jiulize, Je, ungeruka kutoka katika ndege kabla ya kujifunza kutumia parachuti? Ni kweli kwamba huenda mtu akafaulu kuifungua huku akibingirika-bingirika kutoka juu. Hata hivyo, ingalikuwa afadhali kama nini ikiwa angalijifunza kanuni za msingi za kutumia parachuti kabla ya kuruka nje!

Vivyo hivyo, wakati bora zaidi wa kujifunza kutumia pesa ni wakati ungali nyumbani, kabla hujakabili maamuzi mazito ya kiuchumi. Mfalme Sulemani aliandika: “Pesa ni ulinzi.” (Mhubiri 7:12) Lakini pesa zitakulinda ikiwa tu unajua kuzitumia kwa hekima. Kufanya hivyo kutakupa uhakika na kufanya wazazi wako wakuheshimu hata zaidi.

Jifunze Mambo ya Msingi

Umewahi kuwaomba wazazi wako wakueleze mambo yanayohusika katika kutunza familia yenu? Kwa mfano, je, unajua inagharimu pesa ngapi kulipia stima na maji kila mwezi au bei ya petroli, chakula, au kodi ya nyumba? Kumbuka kwamba unafaidika na huduma hizo—na utakapoondoka nyumbani, wewe ndiwe utakayelipia gharama hizo. Kwa hiyo, ni vizuri kukadiria gharama zako zitakuwa kiasi gani. Waombe wazazi wako wakuonyeshe baadhi ya bili zinazoonyesha gharama za huduma au bidhaa mbalimbali za nyumbani, na usikilize kwa makini jinsi wanavyopanga bajeti, yaani, matumizi ya pesa.

Methali moja ya Biblia inasema: “Mtu mwenye hekima atasikiliza na kupata mafundisho zaidi, naye mtu mwenye uelewaji ndiye anayepata mwongozo stadi.” (Methali 1:5) Anna aliwaomba wazazi wake wampe mwongozo stadi. Anasema, “Baba yangu alinifundisha jinsi ya kupanga bajeti na kunionyesha umuhimu wa kupanga vizuri matumizi ya pesa za familia.”

Wakati huohuo, mama ya Anna alimfundisha mambo mengine muhimu. Anna anasema: “Alinionyesha umuhimu wa kulinganisha bei kabla ya kununua kitu.” Kisha anaongeza, “Mama, akiwa na pesa kidogo tu, angeweza kufanya miujiza.” Anna amepata faida gani? “Sasa ninajua jinsi ya kutumia pesa vizuri,” anasema. “Mimi hutumia pesa zangu kwa hekima na hivyo nina uhuru na amani ya akili inayotokana na kuepuka madeni yasiyo ya lazima.”

Kutambua Magumu

Huenda ikaonekana kuwa rahisi kutumia pesa vizuri, hasa ikiwa unaishi nyumbani na unapewa pesa za matumizi au unapata mshahara. Kwa nini? Kwa kuwa huenda wazazi wako wanalipia karibu kila kitu. Kwa hiyo, huenda ukaona kwamba una pesa nyingi za kutumia upendavyo. Na kuzitumia ni raha.

Hata hivyo, tatizo linaweza kutokea vijana wenzako wakikusukuma utumie pesa nyingi kupita ulivyopanga. Ellena, mwenye umri wa miaka 21, anasema: “Baadhi ya vijana wenzangu huona kwenda madukani kuwa tafrija. Na ikiwa hutanunua chochote, hakuna haja ya kwenda.”

Hakuna mtu anayetaka kutenda tofauti na rafiki zake. Lakini jiulize, ‘Je, ninapokuwa na rafiki zangu, ninatumia pesa kwa sababu ninazo au kwa sababu ninalazimika?’ Wengi hutumia pesa ili ‘kujitengenezea jina’ wanapokuwa na marafiki. Wanajaribu kuvutia watu kwa vitu walivyo navyo badala ya utu wao. Hilo linaweza kukuletea matatizo makubwa ya kiuchumi, hasa ikiwa una kadi ya mkopo. Unaweza kuepuka jinsi gani matatizo hayo?

Dhibiti Matumizi

Badala ya kuponda pesa zote na kumaliza kiwango kilichowekwa cha kadi ya mkopo au kuponda mshahara wako wote kwa siku moja, mbona usifanye kama alivyofanya Ellena? “Ninapoenda matembezi na marafiki,” anasema, “mimi hupanga mapema na kuamua kiasi nitakachotumia. Mshahara wangu huwekwa katika akaunti yangu ya benki, nami hutoa tu kiasi ninachohitaji wakati huo. Pia, mimi huona ni vizuri kwenda madukani na marafiki ambao hawatumii pesa ovyoovyo na ambao watanitia moyo kulinganisha bei katika maduka mbalimbali badala ya kununua vitu bila mpango.”

Yafuatayo ni mapendekezo mengine ambayo yanaweza kukusaidia ikiwa una kadi ya mkopo.

● Andika orodha ya vitu unavyonunua na uilinganishe na taarifa ya akaunti ya kila mwezi ili uwe na hakika kwamba umetozwa tu vitu ulivyonunua.

● Lipa gharama unazodaiwa za kadi ya mkopo bila kuchelewa. Ikiwezekana, lipa kiasi chote.

● Uwe mwangalifu unapotoa nambari ya kadi yako ya mkopo na tarehe ya mwisho ya kadi hiyo kwenye simu au katika Intaneti.

● Epuka kutumia kadi ya mkopo kama njia rahisi ya kupata pesa taslimu. Kwa kawaida, kutoa pesa kwa njia hiyo hufanya utozwe kiwango cha juu cha riba.

● Usimpe kamwe mtu yeyote kadi yako ya mkopo, hata awe rafiki yako.

Lakini je, mahitaji yako hayangetoshelezwa kama tu ungekuwa na pesa nyingi zaidi? Huenda isiwe hivyo! Tuseme kwamba una mazoea ya kuendesha gari bila kushika usukani au ukiwa umefunga macho, je, kuongeza petroli kutafanya ufike ukiwa salama unakokwenda? Vivyo hivyo, usipojizoeza kutumia pesa vizuri, hata ukichuma pesa nyingi zaidi itakuwa ni kazi bure.

Huenda unafikiri kwamba tayari unajua kutumia pesa zako vizuri. Lakini jiulize: ‘Nilitumia pesa ngapi mwezi uliopita? Nilinunua nini?’ Umesahau? Basi, kabla mambo hayajaenda mrama, chukua hatua zinazofuata.

1. Weka rekodi. Kwa mwezi mmoja hivi, andika kiasi cha pesa ulizopokea na tarehe uliyozipokea. Andika kila kitu ambacho umenunua na bei yake. Mwishoni mwa mwezi, jumlisha kiasi cha pesa ulizopokea na kiasi cha pesa ulizotumia.

2. Panga bajeti. Tazama chati kwenye ukurasa wa 163. Katika safu ya kwanza, andika mapato yote unayotazamia mwezi huo. Katika safu ya pili, orodhesha jinsi unavyopanga kutumia pesa zako; ukitumia rekodi iliyo katika hatua ya kwanza. Kadiri mwezi unavyosonga, andika kwenye safu ya tatu kiasi hususa ulichotumia kwa kila moja ya mambo uliyopanga. Pia, andika gharama zote ambazo hukupanga.

3. Badili mazoea yako. Ukiona kwamba unatumia pesa nyingi kuliko ulizopanga katika bidhaa fulani na madeni yanazidi kuongezeka, badili mazoea yako ya kutumia pesa. Lipa madeni yako. Dhibiti matumizi yako.

Pesa zina faida zinapotumiwa vizuri. Katika nchi nyingi maisha yanaweza kuwa magumu sana ikiwa huwezi kuchuma na kupanga vizuri matumizi ya pesa. Hata hivyo, jaribu kuwa na usawaziko. “Pesa zina kazi yake, lakini si dawa ya kila kitu,” anasema kijana anayeitwa Matthew. “Hazipaswi kamwe kuonwa kuwa muhimu kuliko familia au Yehova.”

KATIKA SURA INAYOFUATA

Je, familia yenu ni maskini? Ikiwa ndivyo, unaweza kufanya nini ili kuridhika?

MAANDIKO MUHIMU

“Pesa ni ulinzi; lakini faida ya ujuzi ni kwamba hekima huwahifadhi hai waliyo nayo.”—Mhubiri 7:12.

PENDEKEZO

Andika orodha ya vitu ambavyo ungependa kununua kabla ya kwenda madukani. Beba pesa unazohitaji tu, na usinunue vitu ambavyo hukupangia.

JE, WAJUA . . .?

Ikiwa kadi yako ya mkopo ina deni la dola 2,000, na unatozwa riba ya asilimia 18.5, nawe unalipa tu kiwango cha chini cha lazima kilichowekwa na kampuni, itakuchukua miaka 11 kumaliza deni lako na utalipa dola 1,934 za ziada zikiwa riba.

HATUA ZA KUCHUKUA!

Ninaweza kupangia matumizi ya pesa zangu kwa ․․․․․

Kabla ya kununua kitu kwa kutumia kadi ya mkopo, nita ․․․․․

Mambo ambayo ningependa kuuliza mzazi (wazazi) wangu kuhusu habari hii ni ․․․․․

UNA MAONI GANI?

● Kwa nini uanze kujifunza kutumia pesa vizuri ukiwa bado nyumbani?

● Kwa nini huenda ikawa vigumu kwako kutumia pesa vizuri?

● Unaweza kutumia jinsi gani pesa zako kuwasaidia wengine?

[Blabu katika ukurasa wa 162]

Ninapopanga bajeti, mimi huokoa pesa zaidi. Sinunui vitu ambavyo sihitaji.’’—Leah

[Sanduku katika ukurasa wa 158]

Pesa Zina Sauti

Wewe hutumia pesa zako kufanya nini? Ikiwa wewe hutumia pesa kuwasaidia wengine, basi pesa zako—mbali na maneno yako—zinasema kwamba unawajali wengine kikweli. (Yakobo 2:14-17) Ukitoa michango kwa ukawaida ili kutegemeza ibada ya kweli, ‘unamheshimu Yehova kwa vitu vyako vyenye thamani.’ (Methali 3:9) Kwa upande mwingine, ikiwa sikuzote wewe hutumia pesa kutimiza mahitaji yako tu na kununua vitu unavyotaka, pesa zako zinasema wewe ni mtu wa aina gani?

[Chati/Picha katika ukurasa wa 163]

Ukurasa wa Mazoezi

Bajeti Yangu ya kila Mwezi

Nakili ukurasa huu!

Mapato

MARUPURUPU

KAZI YA MUDA

MAPATO MENGINE

Jumla

$․․․․․

Kadirio la Matumizi nilichotumia

CHAKULA

․․․․․

MAVAZI

․․․․․

SIMU

․․․․․

BURUDANI

․․․․․

MICHANGO

․․․․․

AKIBA

․․․․․

MATUMIZI MENGINE

․․․․․

Jumla

$․․․․․

Kiasi hususa

CHAKULA

․․․․․

MAVAZI

․․․․․

SIMU

․․․․․

BURUDANI

․․․․․

MICHANGO

․․․․․

AKIBA

․․․․․

MATUMIZI MENGINE

․․․․․

Jumla

$․․․․․

[Picha katika ukurasa wa 160]

Kutumia pesa ovyoovyo ni kama kuendesha gari ukiwa umefunga macho

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki