Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Uchaguzi Wangu Kati ya Baba Wawili
    Amkeni!—1998 | Juni 8
    • Nilipokuwa nikijifunza juu ya Baba yangu wa kimbingu, Yehova, na kuzidi kumpenda, nilianza kuhofu kwamba siku moja ningekabili uamuzi mgumu—kuchagua familia yangu au Yehova Mungu.—Zaburi 83:18.

      Uchaguzi Mgumu kwa Kijana Mwenye Umri wa Miaka 17

      Hatimaye, Mama akasikia kwamba nilikuwa nikishirikiana na Mashahidi wa Yehova. Alikasirika sana naye akaniamuru niache kujifunza Biblia. Alipotambua kwamba sikuwa nikicheza na masadikisho yangu, alitisha kumwambia Baba. Wakati huo, sikujali kwa sababu nilidhani ningeweza kukabiliana na hali hiyo na kudumisha msimamo wangu dhidi ya Baba. Lakini nilikuwa nimekosea.

      Baba alipojua kwamba nilikuwa nikishirikiana na Mashahidi wa Yehova, alighadhibika. Alitisha kunifukuzia mbali nitoke nyumbani ikiwa singeacha kujifunza Biblia. Nikamwambia kwamba singeacha kwa sababu nilikuwa nikijifunza kweli. Baada ya kupiga kelele, na kunitukana, alianza kulia kama mtoto. Aliniomba sana niache kushirikiana na Mashahidi.

      Nilichanganyikiwa sana kihisia-moyo, kuchagua mmoja kati ya baba wawili—Yehova na yeye. Nilijua kwamba wote wawili walinipenda sana, na nilitaka kutosheleza mahitaji yao wote; lakini lilionekana kuwa jambo lisilowezekana. Sikuweza kustahimili mkazo huo. Nilimwambia Baba kwamba ningefanya vile alivyotaka, nikifikiri kwamba ningeweza kurudia kujifunza na kuwa Shahidi nitakapokuwa mkubwa. Nilikuwa na umri wa miaka 17 tu wakati huo.

      Siku zilizofuata, niliaibikia jambo nililokuwa nimefanya. Nilihisi kwamba Yehova hakufurahi na kwamba sikuwa nimetumainia maneno ya mtunga-zaburi Daudi, aliyesema hivi: “Baba yangu na mama yangu wameniacha, bali BWANA atanikaribisha kwake.” (Zaburi 27:10) Lakini bado nilikuwa katika shule ya sekondari, na wazazi wangu walikuwa wakinilipia karo.

      Msimamo Thabiti Zaidi

      Sikumtembelea mjomba wangu wala kuwasiliana na Mashahidi kwa zaidi ya miaka miwili kwa kuwa nilijua wazazi wangu walikuwa wakinichunguza kwa makini. Siku moja mwaka wa 1989, nikiwa na umri wa miaka 20, nilikutana na Shahidi mmoja niliyemjua. Kwa fadhili sana aliniomba nimtembelee. Kwa kuwa hakutaja lolote juu ya kujifunza Biblia, hatimaye nilienda kumwona.

      Punde si punde, nikaanza kujifunza Biblia na kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova kwenye Jumba la Ufalme. Nilijifunzia kazini, ambapo hakuna yeyote angeweza kunisumbua. Nikaja kufahamu vizuri zaidi utu wenye upendo wa Yehova hali kadhalika nikaelewa vizuri zaidi ubora wa kuwa na kudumisha uhusiano wa karibu naye kwa hali na mali. Agosti mwaka uo huo, hata nilianza kuambia wengine mambo niliyokuwa nimejifunza.

      Kufikia wakati huo familia yangu haikujua lolote. Lakini, siku kadhaa baadaye, baba yangu nami tulionana ana kwa ana tena, ila wakati huo nilikuwa tayari kumkabili. Alijaribu kuniuliza kwa utulivu hivi: “Mwanangu, je, ni kweli kwamba bado washirikiana na Mashahidi wa Yehova?” Machozi yalimlengalenga alipokuwa akisubiri jibu langu. Mamangu na dadangu walikuwa wakilia kimyakimya.

      Nilieleza kwamba nilianza kushirikiana na Mashahidi majuzi tu na kwamba nilikuwa nimeazimia kuwa mmoja wao. Papo hapo, mambo yakaenda mrama. Baba alipiga kelele akisema maneno yapatikanayo mwanzoni mwa makala hii. Kisha akanikamata na kuniambia kwa sauti kubwa kwamba hangeniacha niondoke nyumbani nikiwa hai. Niliweza kuponyoka, na nilipokuwa nikikimbia nikiteremka ngazi, nilimsikia ndugu yangu mdogo akijaribu kumtuliza Baba. “Kuanzia sasa na kuendelea wewe ndiwe Baba yangu,” nikasali kwa Yehova. “Nimekuchagua wewe, kwa hiyo unitunze tafadhali.”

      Kulipiza Kisasi

      Siku chache baadaye, Baba alienda nyumbani kwa mjomba wangu, akifikiri kwamba angenikuta huko. Alimshambulia na kutaka kumwua, lakini Mashahidi fulani waliokuwa wamemtembelea wakamzuia. Baba aliondoka, akitisha kurudi tena. Punde tu akarudi, akiwa na wanamgambo wenye bunduki. Waliwachukua Mashahidi hao na mjomba wangu, aliyekuwa mgonjwa mahututi, na kuwapeleka kwenye makao yao makuu ya jeshi.

      Baadaye Mashahidi wengine walisakwa katika eneo hilo. Nyumba ya mmoja wao ilivamiwa pia. Vitabu, kutia ndani Biblia kadhaa, vilirundikwa barabarani na kuchomwa. Na mambo bado. Mashahidi sita na pia watu waliokuwa tu wakijifunza nao, walikamatwa. Wote waliwekwa katika chumba kidogo, wakahojiwa, na kisha kupigwa. Baadhi yao walichomwa kwa sigareti. Habari juu ya matukio hayo zilisambaa haraka sana ujiranini. Wanamgambo walikuwa wakinitafuta kotekote. Baba yangu aliwaagiza wanitafute na kutumia njia yoyote ile ili kunifanya nibadili akili yangu.

      Siku chache baadaye, wanamgambo waliingia ghafula kwenye Jumba la Ufalme, ambamo mojawapo ya makutaniko lilikuwa likifanya mkutano. Walilazimisha kutaniko lote—wanaume, wanawake, na watoto—waondoke katika jumba hilo. Waliwanyang’anya Biblia zao na kuwafanya watembee hadi kwenye makao makuu ya wanamgambo, ambapo walihojiwa.

      Kutorokea Ugiriki

      Wakati wote huo, nilikuwa nikitunzwa na familia ya Mashahidi iliyokuwa mbali sana kutoka mahali penye msukosuko huo. Mwezi mmoja baadaye, niliondoka nchini na kwenda Ugiriki. Nilipofika huko, niliweka maisha yangu wakfu kwa Yehova Mungu na kuonyesha wakfu wangu kwa kubatizwa.

      Nikiwa Ugiriki nilihisi utunzaji wenye upendo wa udugu wa kiroho uliotia ndani watu kutoka katika mataifa mbalimbali—kutia ndani Waturuki. Nilijionea ukweli wa maneno haya ya Yesu: “Kwa kweli nawaambia nyinyi watu, Hakuna ambaye ameacha nyumba au akina ndugu au akina dada au mama au baba au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya habari njema ambaye hatapata mara mia sasa katika kipindi hiki cha wakati, nyumba na akina ndugu na akina dada na akina mama na watoto na mashamba, pamoja na minyanyaso, na katika mfumo wa mambo unaokuja uhai udumuo milele.”—Marko 10:29, 30.

      Miaka mitatu iliyofuata, nilikaa Ugiriki. Ingawa nilimwandikia Baba barua mara kadhaa, hakunijibu kamwe. Baadaye niliambiwa kwamba wakati wowote ambao marafiki walimtembelea na kumwuliza juu yangu, aliwaambia: “Sina mwana yeyote aitwaye hivyo.”

      Kuungana Tena Baada ya Miaka Sita

      Nilirudi kuishi Beirut mwaka wa 1992, vita ilipomalizika. Nilimtuma rafiki mmoja kumwarifu baba yangu kwamba nilitamani kurudi nyumbani. Akajibu kwamba ningekaribishwa—ikiwa tu ningeacha imani yangu. Kwa hiyo nikaishi katika nyumba ya kupanga kwa miaka mitatu iliyofuata. Kisha, Novemba 1995, bila kutazamia, Baba aliingia kazini kwangu na kuomba kuniona. Sikuwako wakati huo, kwa hiyo akaacha ujumbe kwamba alitaka niende nyumbani. Mwanzoni sikuamini. Kwa hiyo, kwa kusitasita, nikaenda kumwona. Ulikuwa muungano wa kihisia-moyo. Aliniambia kwamba hakujali tena kuwa kwangu Shahidi na kwamba alitaka niende nyumbani!

      Leo natumikia nikiwa mzee Mkristo na mhudumu wa wakati wote katika kutaniko la Kiarmenia. Mimi hukutana mara nyingi na watu kama baba yangu, ambao hupinga washiriki wa familia kwa sababu wanataka kumtumikia Yehova. Natambua kwamba Baba aliamini kwa moyo mweupe kwamba alikuwa akifanya lililo sawa kwa kupinga ibada yangu. Biblia hata huwatayarisha Wakristo kwa kusema kwamba wanaweza kutarajia kupingwa na familia.—Mathayo 10:34-37; 2 Timotheo 3:12.

      Natumaini kwamba siku moja baba yangu na washiriki wengine wa familia yangu watakuwa na tumaini la Biblia kama langu la ulimwengu bora zaidi ujao. Kisha hakutakuwako vita wala mauaji ya kinyama, na watu hawatafukuzwa tena kutoka nchini mwao au kunyanyaswa kwa sababu ya uadilifu. (2 Petro 3:13) Kisha watu hawatalazimika tena kuchagua kati ya mambo mawili wayapendayo sana.—Imechangwa.

  • Kuelewa na Kuvumilia Uyabisi wa Misuli
    Amkeni!—1998 | Juni 8
    • Kuelewa na Kuvumilia Uyabisi wa Misuli

      JE, UNAUMWA mwili wote? Je, wewe huchoka kupita kiasi? Unapoamka asubuhi, mwili wako hautaki kujikunja na unajihisi mchovu sana? Je, nyakati nyingine hukumbuki vizuri mambo? Hizi huenda zikawa dalili chache za ugonjwa wa uyabisi wa misuli (FMS).

      “Sitasahau kamwe asubuhi moja mnamo 1989 nilipoamka nikiwa nimepooza kwa dakika 45,” asema Ted.a Ndipo Ted alipoanza kung’ang’ana na uyabisi wa misuli, ambao hasa ni “maumivu ya kano na misuli.”

      Labda rafiki yako mmoja au mtu mmoja katika familia yenu ana uyabisi wa misuli. Unaweza kusaidiaje? Au kama ni wewe unao, ni nini kinachoweza kufanywa? Kujua habari zinazohusu ugonjwa huu kunasaidia sana kuuelewa na kuuvumilia. Hata hivyo, si lazima kila mtu aliye na dalili hizo awe na uyabisi wa misuli.

      Kufafanua Uyabisi wa Misuli

      Kulingana na Chuo cha Marekani cha Magonjwa ya Baridi Yabisi, “kugunduliwa kwa uyabisi wa misuli kunategemea historia ya mtu ya maumivu yenye kuenea na yenye kudumu na kwa tabibu kupata sehemu fulani-fulani zenye kuuma mwilini.” Pia kuna dalili nyinginezo, nyingine zinazofanana na zile za ugonjwa wa uchovu wa daima (CFS).

      Kwa kweli, watu wengi ambao wana uyabisi wa misuli pia wana ugonjwa wa uchovu wa daima na magonjwa mengineyo. Mshuko wa moyo na hangaiko kupita kiasi ni kawaida miongoni mwa watu wenye uyabisi wa misuli, na inaonekana kwamba uyabisi wa misuli kwa ujumla ndio huyasababisha na wala si matokeo ya hayo magonjwa. Uyabisi wa misuli waweza kuzidishwa na hali zinazotokea nje ya mwili kama vile utendaji mwingi sana au utendaji kidogo sana, baridi, ukosefu wa usingizi usiku, au mkazo wa ziada.

      Awali ugonjwa huu uliitwa kwa majina tofauti-tofauti kutia ndani fibrositis, nao hauharibu mwili wala kuulemaza, wala wenyewe hautishi uhai. Ingawa haiwezi kusemwa kwa uhakika kama uyabisi wa misuli unarithiwa, imepatikana kwamba zaidi ya mtu mmoja katika familia fulani wanao. Ugonjwa huu hushika mamilioni ya watu na kushika watu wazima wenye umri wowote ule, na unashika wanawake wengi kuliko wanaume.

      Kisababishi cha Uyabisi wa Misuli

      Mambo mengi yametajwa kuwa visababishi vya uyabisi wa misuli. Inaweza kuwa virusi au ukosefu wa usawaziko wa kipitisha-habari

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki