Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/8 kur. 21-24
  • Kuelewa na Kuvumilia Uyabisi wa Misuli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuelewa na Kuvumilia Uyabisi wa Misuli
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kufafanua Uyabisi wa Misuli
  • Kisababishi cha Uyabisi wa Misuli
  • Matatizo ya Kugundua Uyabisi wa Misuli
  • Tiba
  • Ugonjwa Huo Unapoathiri Kazi Yako
  • Jinsi Unavyoweza Kusaidia
  • Kujipatanisha na Mabadiliko
  • “Mliandika Kuhusu Mambo Yanayonipata!”
    Amkeni!—2000
  • Maumivu Ambayo Hayatakuwapo Tena
    Amkeni!—1994
  • Maendeleo Katika Kutibu Maumivu
    Amkeni!—1994
  • Je! Wewe Huumwa na Mgongo?
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/8 kur. 21-24

Kuelewa na Kuvumilia Uyabisi wa Misuli

JE, UNAUMWA mwili wote? Je, wewe huchoka kupita kiasi? Unapoamka asubuhi, mwili wako hautaki kujikunja na unajihisi mchovu sana? Je, nyakati nyingine hukumbuki vizuri mambo? Hizi huenda zikawa dalili chache za ugonjwa wa uyabisi wa misuli (FMS).

“Sitasahau kamwe asubuhi moja mnamo 1989 nilipoamka nikiwa nimepooza kwa dakika 45,” asema Ted.a Ndipo Ted alipoanza kung’ang’ana na uyabisi wa misuli, ambao hasa ni “maumivu ya kano na misuli.”

Labda rafiki yako mmoja au mtu mmoja katika familia yenu ana uyabisi wa misuli. Unaweza kusaidiaje? Au kama ni wewe unao, ni nini kinachoweza kufanywa? Kujua habari zinazohusu ugonjwa huu kunasaidia sana kuuelewa na kuuvumilia. Hata hivyo, si lazima kila mtu aliye na dalili hizo awe na uyabisi wa misuli.

Kufafanua Uyabisi wa Misuli

Kulingana na Chuo cha Marekani cha Magonjwa ya Baridi Yabisi, “kugunduliwa kwa uyabisi wa misuli kunategemea historia ya mtu ya maumivu yenye kuenea na yenye kudumu na kwa tabibu kupata sehemu fulani-fulani zenye kuuma mwilini.” Pia kuna dalili nyinginezo, nyingine zinazofanana na zile za ugonjwa wa uchovu wa daima (CFS).

Kwa kweli, watu wengi ambao wana uyabisi wa misuli pia wana ugonjwa wa uchovu wa daima na magonjwa mengineyo. Mshuko wa moyo na hangaiko kupita kiasi ni kawaida miongoni mwa watu wenye uyabisi wa misuli, na inaonekana kwamba uyabisi wa misuli kwa ujumla ndio huyasababisha na wala si matokeo ya hayo magonjwa. Uyabisi wa misuli waweza kuzidishwa na hali zinazotokea nje ya mwili kama vile utendaji mwingi sana au utendaji kidogo sana, baridi, ukosefu wa usingizi usiku, au mkazo wa ziada.

Awali ugonjwa huu uliitwa kwa majina tofauti-tofauti kutia ndani fibrositis, nao hauharibu mwili wala kuulemaza, wala wenyewe hautishi uhai. Ingawa haiwezi kusemwa kwa uhakika kama uyabisi wa misuli unarithiwa, imepatikana kwamba zaidi ya mtu mmoja katika familia fulani wanao. Ugonjwa huu hushika mamilioni ya watu na kushika watu wazima wenye umri wowote ule, na unashika wanawake wengi kuliko wanaume.

Kisababishi cha Uyabisi wa Misuli

Mambo mengi yametajwa kuwa visababishi vya uyabisi wa misuli. Inaweza kuwa virusi au ukosefu wa usawaziko wa kipitisha-habari kiitwacho serotonini, ambacho huathiri usingizi, na ukosefu wa usawaziko wa kemikali kama endofini, ambazo ni vitu vya asili vya mwili vinavyozuia maumivu. Utafiti ungali unaendelea juu ya dhana hizo na nyinginezo.

Kupitia hadubini, misuli ya watu wenye uyabisi wa misuli huonekana kuwa yenye afya, lakini sehemu za chembe za misuli zenye kutokeza nishati huonekana kana kwamba hazitendi kwa njia ya kawaida. Kisababishi na tiba bado hazijulikani. Mara nyingi mtu husema juu ya tukio fulani lenye kuhofisha kihisia-moyo au kimwili kabla ya kuanza kuona dalili hizo, ingawa kwa wengine dalili hizo zilianza polepole.

Matatizo ya Kugundua Uyabisi wa Misuli

Kwa kuwa nyingi za dalili zake zinaweza kupatikana katika magonjwa mengine, Dakt. Carla Ockley, wa Kanada, asema: “Mara nyingi uyabisi wa misuli haufikiriwi mgonjwa aendapo kumwona daktari akiwa na maumivu kwenye mafundo. Matatizo yakidumu baada ya ziara kadhaa, ndipo uchunguzi hufanywa kindani. Uyabisi wa misuli ukitambuliwa, mara nyingi mimi humtuma mgonjwa kwa mtaalamu wa magonjwa ya baridi yabisi ili athibitishe ugonjwa huu.”

Lakini, hadi hivi majuzi hakukuwa na njia ya kugundua uyabisi wa misuli, basi hilo tatizo lilikuwa limejulikana tu kwa mgonjwa mwenyewe, na matokeo ya kupimwa yalionyesha hakuna shida. Kwa hiyo, madaktari wengi hawakuufahamu. Mwanamke mmoja aitwaye Rachel aomboleza hivi: “Niliwaendea madaktari tofauti-tofauti kwa miaka 25, nikatumia maelfu ya dola kabla ya ugonjwa wangu wa uyabisi wa misuli kugunduliwa.”

Basi, msaada waweza kupatikana wapi ukifikiri kwamba una uyabisi wa misuli? Katika kitabu chake When Muscle Pain Won’t Go Away, Gayle Backstrom apendekeza kwamba unaweza kuwasiliana na shirika lililo karibu la Wakfu wa Baridi Yabisi.

Tiba

Kufikia wakati huu, hakuna tiba ambayo imethibitishwa kuwa inaweza kutibu uyabisi wa misuli, basi mara nyingi tiba hujaribu kuondoa dalili zinazotokea. Jambo moja kuu ni maumivu, ambayo, kama ilivyo na dalili nyinginezo, hutofautiana kwa watu na hubadilika-badilika kila siku hata kwa mtu yuleyule.

Kwa kuongezea tatizo hilo, tiba ya kuondoa maumivu na aina nyinginezo za tiba huonekana kupoteza nguvu baada ya muda. Gayle Backstrom adokeza: “Mara nyingi ukizijaribu tena baadaye, utapata nafuu tena kwa kipindi fulani.” Bila shaka, unapaswa kumwona daktari wako kwanza. Pia kuna hatari ya athari za dawa au uzoelevu. Kwa hiyo, “dawa zenye nguvu za kuondoa maumivu zapasa kuepukwa,” chapendekeza Chuo cha Marekani cha Magonjwa ya Baridi Yabisi.

Dalili nyingine muhimu ni ukosefu wa usingizi kwa sababu ya maumivu na mivurugo mingine. Melanie hutumia mto wa mwili kwa ajili ya maumivu na mlio wa chombo cha unyevu ili kuondoa kelele. Visaidizi vingine vyaweza kutia ndani vifuniko vya masikio na sponji.b Dakt. Dwayne Ayers wa North Carolina asema: “Mara niwasaidiapo kuboresha usingizi wao, wagonjwa wangu hufanya maendeleo zaidi kwa tiba nyinginezo.”

Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Maradhi ya Baridi Yabisi, Misuli na Kiunzi, na Ngozi, “wenye kuugua uyabisi wa misuli wanaweza kupata manufaa kupitia mazoezi, tiba, tiba ya maungo, na mapumziko.” Tiba nyinginezo zinatia ndani kukandwa, kudhibiti mkazo, na mazoezi ya kujinyoosha. Lakini, kwa mtu ambaye anapatwa na maumivu ya daima au uchovu, huenda isiwezekane kufanya mazoezi. Kwa hiyo, wengine waweza kupendekeza kuanza mazoezi polepole sana. Na uhakikishe umemwona daktari wako kabla ya kuanza programu yoyote ya kufanya mazoezi.

Katika toleo lake la Julai 1997, kijarida Fibromyalgia Network chanukuu Sharon Clark, ambaye ni tabibu wa mazoezi ya viungo vya mwili na aliye pia mtafiti katika Portland, Oregon, akisema kwamba kama huwezi kufanya mazoezi kwa dakika 20 au 30, “unaweza kutembea-tembea kwa dakika tano-tano mara sita kwa siku na utapata manufaa.” Mazoezi ya kiasi ya kuingiza hewa mwilini huongeza kutokezwa kwa endofini, huboresha usingizi, na kuingiza oksijeni kwenye mwili na misuli.

Lakini watu hutofautiana, nao waweza kuwa na uyabisi wa misuli kwa viwango tofauti-tofauti. Elaine atuambia: “Utimizo mkubwa kwangu ni kutembea huku na huku kwenye njia inayoingia kwangu mara moja, ingawa rafiki yangu wa karibu ambaye pia ana uyabisi wa misuli hutembea kwa kilometa moja hivi.” Hii si hali ya “usipofanya mazoezi, hutafaidika,” lakini kwa wazi ni hali ya “usiache kufanya mazoezi.” Ted, ambaye ana ugonjwa wa uchovu wa daima na vilevile uyabisi wa misuli, asema: “Mara ya kwanza niliweza tu kutumia baiskeli ya kufanyia mazoezi mara moja kwa juma kwa dakika mbili au tatu. Sasa mimi hufanya mazoezi kwa karibu dakika 20 mara tatu au nne kwa juma. Lakini ilinichukua zaidi ya miaka minne kufikia hatua hiyo.”

Suala la tiba nyinginezo, kama vile tiba ya vitobozi, tiba ya kurekebisha maungo, na nyinginezo au hata miti-shamba au nyongeza fulani za vyakula, limetokea. Ingawa wengi hudai kwamba wamepata nafuu kwa kutumia baadhi ya tiba hizo zilizotajwa, wengine hawakufanikiwa. Watafiti wanachunguza tiba kadhaa kati ya hizo, lakini matokeo hayajawa dhahiri bado.

Nyakati nyingine tiba hutokeza njaa, au kula kunakuwa njia ya kukabiliana na hangaiko. Lakini, unene zaidi huweka mkazo kwenye misuli, na kutokeza maumivu zaidi. Katika hali fulani, daktari atapendekeza upunguze uzito wako kwa kilogramu kadhaa.

Kugunduliwa kwa uyabisi wa misuli kwaweza kumfanya mtu awe na wasiwasi na hasira. Lakini kuna njia salama za kushughulikia hisia za kawaida kama hizo ili mtu yeyote asiumie. Huzuni ni hisia nyingine ya kawaida. Ni kawaida kuhuzunika tukipoteza kitu chenye thamani kama vile afya yetu.

Ugonjwa Huo Unapoathiri Kazi Yako

Wale wanaougua uyabisi wa misuli huenda wakapata matatizo kazini. Li alikuwa amefanya kazi kwa miaka mingi, lakini ikawa vigumu kuendelea na kazi kwa sababu ya afya yake. Baada ya kuzungumza na waajiri wake, alifaulu kupata kazi ya nusu-wakati katika kampuni iyo hiyo, mkazo wake ukapunguka. Pia aliongezwa mshahara kwa kila saa afanyayo kazi.

Tabibu wa mambo ya kazi au wa maungo aweza kukusaidia utafute njia za kufanya kazi yako bila mkazo mwingi mwilini mwako. Lisa alipata kwamba kutumia kiti chenye viegemeo kulisaidia sana. Ilipendekezwa kwamba Yvonne apate kiti kingine na vilevile dawati nyingine. Lakini kama ni lazima ubadili kazi, kuna mashirika yawezayo kukusaidia.

Jinsi Unavyoweza Kusaidia

Kila mtu katika familia, hata wale wachanga, aweza kujifunza kuhusu uyabisi wa misuli na kuelewa kwamba ingawa mwenye kuugua uyabisi wa misuli aonekana kuwa mwenye afya, yeye ana ugonjwa wa kudumu wenye kusababisha maumivu na uchovu. Ni muhimu pia kuwa na mawasiliano mazuri. Jennie asema hivi: “Sisi huwa na mazungumzo ya pindi kwa pindi ya familia ili kuona jinsi kila mmoja awezavyo kusaidia.” Jambo muhimu la kuishi na uyabisi wa misuli kwa mafanikio ni kwa mgonjwa kujifunza kuhifadhi nishati na bado anatimiza mambo yake. Hilo laweza kuhitaji uwezo wa kukabiliana na hali hiyo, na vilevile ushirikiano wa wengine. Kwa jambo hili pia, tabibu wa mambo ya kazi aweza kuwa mwenye msaada.

Unaweza kumsaidia rafiki anayeugua uyabisi wa misuli kwa kutokuwa “msikilizaji” mwenye kuhukumu. Jaribu kudumisha mazungumzo yakiwa mazuri, bila kuacha uyabisi wa misuli kuwa jambo kuu la mazungumzo. Ni nini lipaswalo au lisilopaswa kusemwa? Kwa madokezo, ona sanduku lililo kwenye ukurasa wa 23. Kama una uyabisi wa misuli, jaribu kuzungumza na watu tofauti-tofauti ili usichoshe mtu mmoja kwa tatizo lako. Na ukumbuke kwamba si kila mtu atataka kusikia sikuzote kuhusu ugonjwa wako wa uyabisi wa misuli.

Kujipatanisha na Mabadiliko

Nyakati nyingine sisi hatupendelei mabadiliko, hasa yale yanayolazimishwa. Lakini tabibu wa maungo ambaye amewasaidia karibu watu mia moja wenye kuugua uyabisi wa misuli atuambia hivi: “Najaribu kuwafanya waelewe kwamba wao wanahitaji kukubali hali yao. Pia wanahitaji kufanya mabadiliko katika maisha zao bila kuvunjika moyo kwa vizuizi vya muda tu au wakishikwa na hasira. Wakijisimamia vizuri, wawe na ujuzi, uelewevu, na mazoezi, wao waweza kudhibiti ugonjwa wao wa uyabisi wa misuli badala ya kuacha ugonjwa huo uwadhibiti.”

Dave, ambaye ana FMS, asema: “Ingawa kuna mwelekeo wa kufanya mengi katika siku ambazo unajisikia vizuri, inaweza kuwa jambo la hekima kuhifadhi nishati zako kwa ajili ya siku ifuatayo ili usiwe mgonjwa kwa juma lote.” Lakini, nyakati nyingine huenda ukahisi kwamba hakuna ubaya kuhudhuria sherehe fulani au onyesho fulani hata kama utaumia baadaye. Si vema sikuzote kuwaficha wengine juu ya ugonjwa wako wa uyabisi wa misuli, hasa kuwaficha wale ambao wanajali. Na ujaribu kudumisha hali ya ucheshi. “Nimeona kwamba mimi hulala vizuri baada ya kucheka sana au baada ya kuona sinema nzuri yenye kuchekesha,” asema André.

Pia kumbuka kwamba Yehova halinganishi kiwango chako cha utendaji na kile cha wengine lakini yeye huthamini imani na upendo wa ndani uonyeshao. (Marko 12:41-44) Jambo kuu ni kujifunza kuishi kulingana na mipaka yako, bila kuwa mwenye kujilinda kupita kiasi wala asiyejali. Mtegemee Yehova Mungu akupe hekima na nguvu ya kufanya kadiri uwezayo. (2 Wakorintho 4:16) Na ukumbuke ahadi ya kwamba karibuni wakati utakuja ambapo dunia itakuwa paradiso ambamo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Ndiyo, siku moja utakuwa mwenye afya nzuri tena!

[Maelezo ya Chini]

a Baadhi ya majina yamebadilishwa.

b Amkeni! halipendekezi kitu fulani hususa cha kusaidia usingizi, wala halipendekezi tiba fulani hususa ya uyabisi wa misuli.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Faraja Kutoka Katika Biblia

• Yehova huwaokoa waliopondeka roho.—Zaburi 34:18.

• Yehova atakutegemeza.—Zaburi 41:3.

• Umtwike Yehova mizigo yako yote; anakujali.—Zaburi 55:22; 1 Petro 5:7.

• Yehova afurahia jitihada zako za kumtumikia kwa nafsi yote, hata utumishi huo uwe kidogo kadiri gani.—Mathayo 13:8; Wagalatia 6:4; Wakolosai 3:23, 24.

• Sisi hatuchoki.—2 Wakorintho 4:16-18.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Mambo ya Kusema

• Nimefurahi kukuona.

• Umejitahidi sana kufika hapa.

• Nimekuja kukusaidia. Nakujali.

• Nathamini kile uwezacho kufanya.

Mambo Yasiyopasa Kusemwa

• Naelewa kile unachopitia.

• Unaonekana una afya nzuri. Inawezekanaje kwamba wewe ni mgonjwa?

• Uniite ukihitaji chochote.

[Mchoro katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Madoa meusi ni baadhi ya sehemu zenye maumivu ambazo hutafutwa wakati wa kujaribu kugundua uyabisi wa misuli

[Picha katika ukurasa wa 24]

Ni muhimu kuwa na mawasiliano na mazungumzo mazuri ya familia

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki