Kurudi kwa Jumba la Maonyesho la Globe la London
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
LILE jumba la Globe, jumba la maonyesho lililokuwa makao ya michezo ya William Shakespeare, limejengwa upya karibu na eneo lake la zamani katika Southwark, kwenye ukingo wa kusini wa Mto Thames wa London. Likiwa limejengwa kwa kutegemea muundo wake wa awali wa 1599, jengo hili lenye umbo la O, lenye pande 20 ni uvutio mkubwa wa watalii.
Kabla ya kuwapo kwa majumba ya maonyesho ya London, namna iliyopendwa ya vitumbuizo ilikuwa kuchokoza dubu au fahali aliyefungwa kwa kutumia mbwa. Mbwa, wakichochewa na watazamaji wenye makelele, walitesa-tesa mnyama aliyefungwa kwenye mti. Jambo hili lilitukia ndani ya nyanja za maonyesho za kiduara zenye viti vilivyopangwa kwa safu, zilizotangulia majumba ya maonyesho. Wanyama walifungwa kwenye kigingi katika eneo la katikati, ambalo baadaye likaja kuwa jukwaa la jumba la maonyesho.
Punde baada ya hapo michezo ikapendwa sana, na majumba mapya ya maonyesho yakaanza kujengwa kotekote katika London. Maelfu ya watazamaji waliihudhuria kila siku. Meya waheshimiwa walijaribu kupiga marufuku michezo hiyo chini ya misingi ya kwamba ilikuwa chafu na isiyo ya kidini. Waajiri walilalamika kwamba michezo hiyo iliwaondoa kazini wafanyakazi wao, kwa kuwa ilianza saa nane adhuhuri. Lakini utegemezo ulikuja kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Kwanza, mhudhuriaji wa kawaida wa hayo maonyesho. Baraza Lake la Kumshauri liliilinda ili kuhakikisha kwamba waigizaji wazoefu walipatikana ili kumtumbuiza. Kikundi cha Shakespeare mara nyingi kiliteuliwa kwa ajili ya uigizaji wa nyumba ya mfalme kuliko kikundi kingine chochote.
Mwaka ambao jumba la Globe la awali lilipofunguliwa, Shakespeare aliandika Henry V. Kwa hiyo ulikuwa uchaguzi mzuri kwa msimu wa kwanza wa jumba hili jipya la michezo la Shakespeare.
Ndani ya Jumba Jipya la Globe
Kabla ya kuingia kutazama mchezo utakaochukua muda wa saa tatu, tunatazama juu kwenye mawingu na kutumaini kwamba hakutanyesha, kwa kuwa miavuli hairuhusiwi na eneo la kati halina paa. Jukwaa hujitokeza kuwa duara la meta 30, ambalo huzungukwa na safu tatu za viti, ambazo zaweza kukaa karibu watu 1,000. Lakini tuko miongoni mwa watazamaji waliosimama, wale 500 ambao hulipa wasimame na kutazama mchezo katika eneo la kati. Jumba la awali la maonyesho lilitoshea watu 3,000, waliojaa kabisa. Lakini viwango vya usalama vya kisasa hukataza jambo hilo.
Paa lililo juu ya duara ya eneo la kuketia hutiwa kemikali ili kuzuia moto. Ubao usioshika moto na mfumo wa kunyunyizia huzidisha ulinzi. Jumba la Globe la awali liliharibiwa katika mwaka wa 1613 wakati cheche kutoka kwenye mzinga wa jukwaa ilipowasha paa lake.
Watu wanaosimama huruhusiwa kutembea huku na huku na hata kupumzisha mikono yao kwenye ukingo wa jukwaa. Miaka 400 iliyopita, umati wenye fujo ulikuwa ukinywa wakati wote wa michezo, na mara nyingi mapigano yalizuka miongoni mwao. Wakiwa wachambuzi wakali, walikatiza walivyopenda, walizomea au kupiga makofi. “Walisongamana kwa ukaribu,” kama awafafanuavyo mwandishi mmoja wa wakati huo, akiwaita “wahuni.”
Muundo wa msingi wa jumba la Maonyesho la Globe la kisasa umefanyizwa kwa mwaloni. Vigingi karibu elfu sita vya mwaloni vilivyo na ncha iliyochongoka hushikilia pamoja tunduunganishi. Mwaloni ulipatikana kwa utayari baada ya kimbunga kung’oa maelfu ya miti katika Oktoba 1987. Kipande kilichokuwa kigumu zaidi kupata kilikuwa mhimili wenye meta 13 ambao hufanyiza sehemu ya mbele ya paa inayoning’inia. Baada ya kutafuta sana, mti ufaao wenye urefu uzidio meta 20, ulipatikana kilometa 150 magharibi ya London.
Nguzo zinazoshikilia paa zaonekana kuwa za marumaru. Lakini sivyo, hizo pia zimefanyizwa kwa mbao, kama zile tu za jumba la kwanza la Globe, ambalo, kama alivyoeleza mtu mmoja mwenye kuvutiwa nazo, “zilipakwa rangi kwa mwigizo bora zaidi wa marumaru hivi kwamba yawezekana kudanganya hata fundi stadi wa marumaru.”
Kufika sasa viti vimejazwa. Watu fulani wenye kusimama wasongamana kando ya jukwaa huku wengine wakiegemea kuta za mbao za jumba la maonyesho. Makelele yapungua muziki unapochezwa. Katika orofa iliyo juu ya jukwaa, wanamuziki sita wakiwa na mavazi ya enzi ya kati wacheza vyombo vya muziki vya wakati wa Shakespeare: tarumbeta, buruji, na vyombo vya kugonganisha.
Mchezo
Muziki ufikiapo kilele, waigizaji watokea na kugonga kwa nguvu fimbo zao juu ya jukwaa wakifuatisha mdundo wa muziki. Watu wenye kusimama wajiunga nao, wakigongagonga miguu yao chini. Kwa ghafula huko kugonga kunakoma. Mwigizaji mmoja na utangulizi wa mwanzo waanzisha maonyesho. Kuna matarajio makubwa. Kwa ghafula, waigizaji wawili wenye mavazi mekundu watokea kwenye jukwaa—Askofu Mkuu wa Canterbury na askofu wa Ely. Mchezo waanza, na wakati wa uigizaji, unafiki na njama ya kanisa pamoja na Mfalme wa Uingereza Henry wa Tano hatimaye utafikia upeo kwenye ushinde wa Ufaransa kwenye nyanja za Agincourt zenye kujaa damu.
Punde si punde kiti cha ufalme chasimamishwa, na twampata Mfalme Henry akiongea na watumishi wake watatu. Ofisa wa nyumba ya mfalme wajipangapo kwenye jukwaa, twazidi kushangilia uasilia wa mavazi yao ya enzi za kati. Na bado kuna jambo fulani geni kuhusu waigizaji ambalo hatuwezi kupima. Twaangalia programu yetu. Ndiyo, bila shaka, wachezaji wote ni wanaume! Wanawake hawakuwa na sehemu yoyote katika drama za enzi ya Elizabeth. Kama vile mwanahistoria wa kijamii G. M. Trevelyan aelezavyo, wavulana “walizoezwa kabisa kuanzia utoto waigize sehemu za wanawake kwa adhama, kwa uchangamfu na kwa ustadi.” Wamefanya hivyo leo.
Makofi yanaisha, na twatoka nje. Twageuka kutazama jumba la Globe kwa mara ya mwisho, mwezeko wake wa kidhahabu, kama vile mbao za mwaloni, zikigeuka kuwa rangi ya kijivujivu. Limekuwa jambo la kipekee kutazama tukio la karibu miaka 400 iliyopita.
Baadaye, twazurura kupitia Maonyesho ya Shakespeare ya jumba la Globe. Jina Shakespeare laweza kuonekana kila pahali. Tunapofikiria kwa makini juu ya maonyesho, twatafakari kwa uzito swali hili, Kwa kweli mwandishi wa michezo ya kuigiza William Shakespeare alikuwa nani? Habari itakayozungumziwa katika makala ya toleo moja lijalo la Amkeni! itahusu fumbo la William Shakespeare.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mchoro wa Jumba la awali la Maonyesho la Globe
[Hisani]
Kutoka kitabu The Comprehensive History of England, Buku la pili
[Picha katika ukurasa wa 26]
Jumba la Maonyesho la Globe leo
[Hisani]
John Tramper
Richard Kalina