Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mafigo Nataka kuwaambia jinsi nilivyoguswa moyo na makala “Mafigo Yako—Chujio la Kutegemeza Uhai.” (Agosti 8, 1997) Daktari wangu ameniarifu kuwa nina tatizo la figo. Kwa sababu ya makala hiyo, sasa sihisi upweke sana na ugonjwa wangu.
V. M., Marekani
Nina maradhi ya figo ambayo yalifanya nilazwe hospitali kwa miezi minne. Kusoma makala yenu kulinifanya nifahamu jinsi nisivyoujua mwili wangu. Sasa naweza kuwaeleza wengine hali yangu kwa njia bora.
S. H., Japani
Makala hii ilitokea wakati mke wangu alipoambiwa kwamba ana kansa ya figo. Ingawa kugunduliwa kwa ugonjwa huo kulitushtua, tuliweza kuelewa waziwazi utendaji mbalimbali wa figo wakati tulipoelezwa jambo hili na daktari mpasuaji. Mke wangu aliondolewa figo na sasa anapata nafuu kutokana na upasuaji.
G. S., India
Masimulizi ya Mchongaji Ilichangamsha moyo wangu kusoma “Kitu Bora Kuliko Kuwa Mashuhuri Ulimwenguni,” iliyosimuliwa na Celo Pertot. (Agosti 22, 1997) Kabla ya kuwa Mkristo, nilifuatia kazi-maisha ya muziki na maonyesho. Usiku kabla ya kubatizwa kwangu, nilipokea simu kutoka kwa waandishi wa mfululizo uliopendwa sana wa televisheni. Nilipowaambia kwamba sikuwa mtumbuizaji tena, walisema, “Una kichaa?” Kama Celo Pertot, nahisi kwamba Yehova amebariki uamuzi wangu kwa njia kubwa.
R. F., Marekani
Mwanatheolojia wa Urusi Asanteni sana kwa kuchapisha makala “Mashahidi wa Yehova Nchini Urusi.” (Agosti 22, 1997) Nina staha na kuvutiwa na Sergei Ivanenko kwa kuwa na moyo mkuu na tamaa ya kuchapisha ukweli kuhusu Mashahidi wa Yehova.
S. M., Marekani
Chuki Ule mfululizo “Kwa Nini Kuna Chuki Sana? Kwa Nini Hakuna Upendo Sana?” (Septemba 8, 1997) ulikuwa na mojawapo ya jalada bora zaidi ambayo mmepata kuchapisha. Makala hiyo ilinisaidia kuona waziwazi zaidi kwa nini watu hukosa kuwatumaini wageni na watu wa tamaduni tofauti.
J. M., Marekani
RSD—Ugonjwa Wenye Maumivu Nawajibika kuwaandikia baada ya kusoma ile makala “RSD—Ugonjwa wa Kukoroweza na Wenye Maumivu.” (Septemba 8, 1997) Mnamo Januari, niligundua kwamba nina RSD. Nilijaribu kutafuta habari fulani kuuhusu. Kwa hiyo nilitoa machozi ya shukrani nilipoona makala hii. Ilikuwa yenye kutumika, na ilijibu mengi ya maswali yangu.
W. B., Uingereza
Nimekuwa nikiugua RSD kwa miaka minne. Asanteni kwa kujitahidi kufanya utafiti kamili kuhusu habari hii. Kwa kweli ilionyesha upendo wa jirani kwa upande wenu.
G. S., Ujerumani
Mume wangu anaugua RSD, na ilikuwa vigumu sana kuwaeleza wengine juu ya maradhi haya. Sasa kwa vile yamezungumziwa kikamili katika makala hiyo, imekuwa rahisi zaidi kwetu. Pia tumepitisha habari hii kwa madaktari na ofisi zenye kutoa msaada. Kusoma masimulizi ya pambano la Karen Orf na RSD kulikuwa kama kusoma maisha ya mume wangu! Kama Karen, twatazamia kwa hamu ulimwengu mpya, ambamo hakutakuwa na maumivu tena.
K. P., Australia
Namshukuru Karen kwa masimulizi yake. Nawaza na kusali juu yake, na natumaini kwamba ataendelea kufanya maendeleo. RSD umeathiri mgongo na miguu yangu mpaka chini kwenye nyayo za miguu yangu. Kuketi mikutanoni na kutembea katika huduma ya shambani hunitatiza na kusababisha maumivu. Hata hivyo, kwa utegemezo wa Yehova, jambo hili halijanivunja moyo.
C. K., Uingereza