Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/8 kur. 21-23
  • Jitihada Yangu ya Kukabiliana na RSD

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jitihada Yangu ya Kukabiliana na RSD
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kinachofanana na RSD
  • Kitulizo Fulani Hatimaye!
  • Nini Yaweza Kuwa Matokeo ya RSD?
  • Jinsi Ninavyokabiliana na Hali
  • RSD—Ugonjwa wa Kukoroweza na Wenye Maumivu
    Amkeni!—1997
  • Maumivu Ambayo Hayatakuwapo Tena
    Amkeni!—1994
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Maendeleo Katika Kutibu Maumivu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/8 kur. 21-23

Jitihada Yangu ya Kukabiliana na RSD

NIMO katika miaka yangu ya mapema ya 40 na ninafanya kazi nikiwa mjitoleaji wa wakati wote katika ofisi nikitumia kompyuta. Miaka michache iliyopita nilifanyiwa upasuaji katika uti wa mgongo wangu, na nilifikiri kwamba nafahamu barabara maumivu ni nini. Hivyo katika Januari 1994 nilipopasa kupasuliwa kwa sababu ya uvimbe wa ganglioni katika kifundo cha mkono wa kushoto, nilitarajia maumivu fulani na usumbufu—ambayo ningeweza kukabiliana nayo.

Majuma machache baada ya upasuaji, ambao ulikuwa wenye mafanikio, nilianza kuhisi maumivu makali katika mkono wangu wa kushoto. Pia ulikuwa unavimba na kubadilika rangi. Kucha zangu za vidole zilikuwa ndefu na ngumu lakini nyepesi, na kwa sababu ya maumivu, sikuweza kuzikata. Kulala usingizi kulikuwa karibu hakuwezekani. Kwanza, madaktari na mwanatiba walitatizwa, lakini dalili zilipozidi kuwa mbaya, daktari-mpasuaji aligundua kwamba nilikuwa na RSD (Reflex Sympathetic Dystrophy), pia wajulikana kuwa Chronic Regional Pain Syndrome. Wakati huo, miezi mitatu ilikuwa imepita baada ya upasuaji.

Kinachofanana na RSD

Sikuwa nimesikia kamwe kuhusu RSD, lakini kutokana na yale yaliyonipata niligundua RSD ilikuwa nini—MAUMIVU. Aina ya maumivu yaliyo mabaya sana. Maumivu yasiyokwisha katika mkono wangu. Nilihisi maumivu wakati mkono wangu ulipovimba mara tatu zaidi ya ukubwa wake wa kawaida. Aina ya maumivu ambayo yalikuwa yenye kuwaka moto wakati wote. Ilikuwa kana kwamba nilikuwa katika nyumba inayoungua, na nisingeweza kutoroka. Sitii chumvi! Kwangu, yalikuwa maumivu mabaya zaidi na yenye kudumu zaidi niwezayo kuwazia. Nilipatwa na maumivu ya aina nyingi kwa viwango tofauti. Nyakati nyingine, maumivu hayo yalikuwa kama bumba la nyuki wakiniuma. Nyakati nyingine, yalikuwa kama jiliwa ya seremala ikinifinya sana na kama nyembe zikinikatakata. Sikuweza hata kuvumilia nywele zangu ndefu kugusa ngozi yangu—wakati zilipogusa, zilikuwa kana kwamba miiba ilikuwa ikinichoma. Nilitaka sana kupata kitulizo kutokana na maumivu.

Wakati fulani nilikuwa nikisumbuliwa sana na maumivu ya wakati wote, maumivu makali sana hivi kwamba hata nilifikiria kukata mkono wangu nilipokuwa bafuni. Nilijiuliza ningehitaji kukata mara ngapi ili kuondoa maumivu haya. (Baadaye, madaktari waliniambia kwamba kukata kiungo hakumalizi tatizo.) Nilihisi kama mbweha aliye katika mtego atafutaye kitulizo kwa kutafuna kiungo chake kilichonaswa.

Kitulizo Fulani Hatimaye!

Hatimaye, ikiwa jitihada ya mwisho, nilipelekwa katika kliniki ya maumivu ili kupata matibabu. Hapo nilikutana na Dakt. Mathew Lefkowitz, ambaye ni mtaalamu wa maumivu aliye pia mtaalamu wa nusukaputi ambaye afanya kazi New York, katika Brooklyn Heights. Alikuwa mwenye huruma sana na mwenye kuelewa. Hiyo kliniki ya maumivu ikawa kimbilio kwangu, hasa nilipoanza kuelewa ugonjwa wangu na matibabu.

Dakt. Lefkowitz alianza na matibabu ya kuondoa maumivu—kudungwa sindano kwa ukawaida katika neva shingoni mwangu, ambazo zingezuia kwa muda ujumbe wa neva unaosababisha maumivu. Kulingana na maelezo yake, maumivu yanasababishwa na sympathetic nervous system. Hili ni itikio la kawaida la ubongo kwa jeraha au upasuaji. Nadharia ni kwamba mfumo huu unapaswa kufanya kazi kama lango. Hisi za neva hupita tu jeraha linapopona. Wakati fulani, ubongo usipoendelea kutuma mipwito ya neva, lango hilo hujifunga na maumivu hupotea. Katika RSD, lango hilo halifungiki. Hiyo sympathetic nervous system haitulii kamwe. Huendelea kufanya kazi kana kwamba bado kuna jeraha katika sehemu hiyo ya mwili. Huyo daktari aliniambia niende katika kliniki hiyo mara moja wakati wowote maumivu yaongezekapo. Hivyo, nimekuwa nikienda kwa ukawaida kwa ajili ya sindano za kuzuia maumivu kwa muda fulani.

Sindano hizo zilinisaidia kuvumilia matibabu ya kuzoeza mwili, ambayo huniwezesha kujongea kiungo kilichoathirika na ni yenye kufaa sana kwa ugonjwa huu wa RSD. Wakati ulipoendelea kupita, nilianza kufanya kazi ndogo-ndogo, nikitumia mikono yote miwili. Ulikuwa mwanzo mzuri.

Nini Yaweza Kuwa Matokeo ya RSD?

Maumivu ya wakati wote yaliniathiri kwa njia mbalimbali. Nilitaka kuwa peke yangu, kuwa mbali na watu; lakini popote nilipoenda, maumivu yangenifuata. Kwa hiyo, hiyo haikuwa suluhisho. Mkono ulianza kuwa kama kitu tofauti ambacho kiliendelea kuharibu maisha yangu na ndoa yangu. Mume wangu hata hakuthubutu kunikaribia ili kunionyesha shauku. Kwa hakika alikuwa mwenye subira na mwenye huruma. Nilikuwa nimekuwa mke mwenye mkono mmoja, asiye na uwezo wa kufanya jambo lolote. Kujaribu tu kuchukua karatasi kwa mkono wangu wa kushoto kulileta maumivu makali.

Hadi sasa, hakuna tiba kwa RSD, ingawa mara nyingine huisha yenyewe. Katika hatua ya mwisho, ugonjwa wa kudhoofika kwa mifupa uitwao osteoporosis huanza na kiungo hicho hunyauka. Hii ndiyo maana tibamaungo ya mara nyingi inasaidia sana. Kwa shukrani, sipo katika hatua hiyo.

Jinsi Ninavyokabiliana na Hali

Ingawa bado nina maumivu, lakini si makali kama yalivyokuwa katika pindi zilizokuwa mbaya zaidi. Hata hivyo, bila sindano, nisingeweza kuvumilia. Ni nini imenisaidia kuvumilia? Mtazamo ufaao wa baadhi ya madaktari, wanatiba, na marafiki. Pia nimejifunza mbinu za kukabiliana na hali hiyo. Kwa ajili ya kujistahi na heshima yangu, nilipaswa kuwa na ukawaida fulani katika maisha yangu, japo hali yangu isiyo ya kawaida. Kuwa karibu na wafanyakazi-wenzi ambao walinipa tegemezo, bila ya kunikaza, kulinisadikisha kwamba bado ninaweza kuwa mwenye kufaa. Pia nilitambua, na bado ninatambua kwamba muziki wa kutuliza na mazoezi ya kuvuta pumzi hunisaidia kupumzika. Moja kati ya mambo ninayopenda sana ni kulala katika kikao cha starehe na kuangalia anga na mawingu yenye kubadilika wakati wote. Kisha ninatafakari na katika akili yangu husafiri mahali mbalimbali penye kupendeza. Kicheko wakati wote ni dawa nzuri, kwani ni mtazamo ufaao—na zaidi sana unapojua kwamba una tegemezo lenye upendo la familia na marafiki. Ni muhimu kutambua kwamba RSD si lazima ikushinde. Wataalamu wazuri wa kitiba waweza kukusaidia kushinda pigano hilo.

Mambo yaliyonipata yamenifanya niwe mwenye hisia-mwenzi zaidi kuelekea yeyote mwenye kusumbuliwa na maumivu, na ninachochewa kusaidia na kufariji wengine. Itikadi zangu zimekuwa msaada mkubwa sana. Ninajua ni kwa nini hili limetokea. Mimi si mchaguliwa kipekee kuwa mhasiriwa. Mungu hapaswi kulaumiwa. Maumivu ni moja kati ya matukio mabaya katika maisha yanayoweza kumpata mtu yeyote. Sala yenye bidii imekuwa baraka kwangu. Nina imani katika Mungu kwamba utafika wakati ambapo maumivu hayatakuwapo tena. Nimesaidiwa kwa kushiriki maoni hayo na wengine ambao nimekutana nao. Ingawa RSD bado ni tatizo kwangu, ninashukuru kwa maendeleo ambayo nimehisi. (Ufunuo 21:1-4)—Kama ilivyosimuliwa na Karen Orf.

[Sanduku katika ukurasa wa 22, 23]

Maoni ya Daktari

Amkeni! lilimhoji Dakt. Lefkowitz ili kupata maelezo yake juu ya matibabu hayo. Alieleza: “Tunashughulikia maumivu ya aina zote, si RSD pekee. Maumivu ya kawaida sana ni maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo, ambayo mara nyingi huongoza katika maumivu makali ya nyonga. Ingawa kwa wazi maumivu ni ya kimwili kwa asili, lakini pia upo uvutano wa kisaikolojia.”

Amkeni!: Je, RSD waweza kushambulia watu wa umri wowote na wa jinsia tofauti bila kubagua?

Dakt. Lefkowitz: Ndiyo, ugonjwa huu haubagui. Hata hivyo, hatuwezi kutabiri ni nani ana mwelekeo zaidi wa kushambuliwa na ugonjwa huu. Kile ninachojua ni kwamba kwa kawaida wanawake huvumilia maumivu zaidi ya wanaume. Wanaonekana wana uwezo zaidi wa kuvumilia maumivu.

Amkeni!: Unapendekeza matibabu gani kwa ajili ya maumivu?

Dakt. Lefkowitz: Kuna njia mbalimbali tuwezazo kutumia, ikitegemea chanzo na kiasi cha maumivu. Kwa vyovyote, maumivu humaanisha kuteseka, na twapaswa kuondoa mateso hayo. Katika visa fulani twatumia vidonge visivyo na steroid, kama vile aspirini, na aina zake nyingine. Katika visa vingine, kama kile cha Karen, twatumia dawa za kuzuia neva mahali penye maumivu. Katika visa vya kupita kiasi twaweza kutumia dawa za kutia usingizi. Tatizo la kutumia dawa ya kutia usingizi ni kwamba twapaswa kuwa waangalifu kwa uwezekano wa uraibu.

Amkeni!: Je, ni lazima RSD upitie hatua zote unapoendelea?

Dakt. Lefkowitz: Hapana, si hivyo. Ikiwa twaweza kugundua ugonjwa huo ukiwa katika hatua ya mwanzo, twaweza kuzuia maendeleo yake. Chukua Karen kama kielelezo. Yupo katika hatua ya katikati, na si lazima aendelee hadi hatua ya mwisho ya kudhoofika kwa kiungo.

Amkeni!: Unapendekeza nini ili kumsaidia mgonjwa kukabiliana na hali hii?

Dakt. Lefkowitz: Vile tu Karen alivyofanya. Amekabili maumivu yake kisaikolojia kwa kukengeusha mawazo yake kwa mawazo mazuri na picha nzuri. Pia atumia matibabu ya kuzoeza mwili. Na ninaamini kwamba imani yake imekuwa msaada mkubwa sana. Imemsaidia kuona hali hiyo kwa njia ifaayo. Ndiyo, siwezi kukazia imani sana.

Amkeni!: Asante sana kwa wakati wako na subira.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Pamoja na Dakt. Lefkowitz katika kliniki yake

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki