RSD—Ugonjwa wa Kukoroweza na Wenye Maumivu
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kanada
UGONJWA wa Reflex Sympathetic Dystrophy (RSD) ni “moja kati ya magonjwa ya kukoroweza zaidi katika tiba na moja kati ya magonjwa yenye maumivu zaidi na pia yawezayo kulemaza,” aliandika Allison Bray katika gazeti la habari la Winnipeg Free Press. “Kwa kawaida [RSD] hautambuliki unapochunguzwa kitiba kwa sababu haueleweki vizuri,” akasema mgonjwa aitwaye Anna Alexander katika British Medical Journal. Jarida hilohilo lilisema kwamba RSD mara nyingi haudodoswi kwa usahihi katika watoto. Kwa miaka mingi madaktari hata walifikiri kwamba maumivu hayo yalikuwa ya kisaikolojia, ya kujiletea mwenyewe.
Wale ambao husumbuka kutokana na ugonjwa huu wa kifumbo hupatwa na maumivu makali sana na katika matukio fulani hawakumbuki ikiwa walifanya jambo lolote lililosababisha maumivu hayo makali. Sarah Arnold aandika katika Accent on Living: “Maradhi hayo husababishwa na jeraha katika eneo la mwili ambalo neva nyingi huishia, kama vile mkono au wayo. Jeraha laweza kuwa dogo kama vile kuchomwa na pini au kubwa kama vile la upasuaji. Ishara ya kwanza ya maradhi haya ni maumivu ya kudumu na yaliyo makali kuliko jeraha. Dalili ni kali sana, maumivu makali katika sehemu inayohusika, unyetivu sana kwa halijoto na nuru, nywele na kucha hubadilika na ngozi hubadilika rangi.”
Hayo maradhi hupitia hatua kadhaa. Kwanza, kuna uvimbe na uwekundu katika eneo lililoathirika na ukuzi wa nywele mahali ambapo hapakuwa na ukuzi wa wazi wa nywele awali. Dalili hizi zaweza kuwepo kwa mwezi mmoja hadi miezi mitatu. Kisha, eneo hilo labadilika na kuwa buluu na baridi, huku maumivu yakizidi na kushikamana kwa kano na viungo. Kisha ugonjwa wa kudhoofika kwa mifupa uitwao osteoporosis waweza kuanza. Hatimaye, misuli iliyoathirika hudhoofika, kano hujikaza, na kiungo kilichoathirika hunyauka.
Madhara yasiyoweza kurekebishwa yaweza kuzuiwa, kulingana na Dakt. Howard Intrater, mkurugenzi wa kliniki ya maumivu katika Health Sciences Centre huko Winnipeg. Mfumo wa neva uitwao sympathetic nervous system, wapasa kuzuiwa ili usitume ishara za maumivu.a Gazeti la habari la Winnipeg laripoti kwamba “matibabu hutofautiana kutoka kichocheo cha umeme hadi dawa za beta blockers, kichocheo cha epidural (ambapo elektrodi inawekwa katika uti wa mgongo ili kuamsha eneo lililoathirika hadi kuzuia sympathetic nerve kwa kutumia sindano.” Tibamaungo inatumiwa pamoja na tiba ya vitobo ili kupunguza maumivu na kuongeza uwezo wa kujongea. Jarida British Medical Journal lasema kwamba “matibabu yenye matokeo yatia ndani baadhi ya mchanganyiko wa kusisimua neva kwa umeme, kuzuia sympathetic nerve kwa kemikali, tiba ya kisaikolojia, na tiba ya mazoezi yenye juhudi nyingi ya kimwili.”
Kwa wazi kudodosa mapema ni kwenye faida. Lakini, madaktari wakiandika katika The American Journal of Sports Medicine wasema kwamba matokeo yao ya matibabu ya wagonjwa waliododoswa kuwa na dalili za RSD kwa muda upunguao miezi 6, au tokea miezi 6 hadi 12, au kwa zaidi ya miezi 12 “yalikuwa karibu sawa. Matokeo haya yanapingana na maoni ya wakati huu kwamba kipindi cha dalili kinachozidi mwaka 1 kabla ya matibabu si ubashiri mzuri.”
Inatumainiwa kwamba kadiri ujuzi wa kitiba unavyoongezeka, RSD utafahamika zaidi na kwamba watu wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa huu wataweza kupata matibabu yenye matokeo zaidi.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa maelezo ya kina juu ya suala la maumivu, ona mfululizo wenye kichwa “Je! Maisha Bila Maumivu Yawezekana?” katika toleo la Amkeni! la Juni 22, 1994.