Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 6/22 kur. 5-7
  • Maumivu Ambayo Hayatakuwapo Tena

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maumivu Ambayo Hayatakuwapo Tena
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jitihada za Kuelewa Maumivu
  • Akili na Mwili Vyahusika Vyote
  • Jinsi Hisia za Maumivu Zirekebishwavyo
  • Maendeleo Katika Kutibu Maumivu
    Amkeni!—1994
  • Ni Nani Anayehitaji Maumivu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Ni Zaidi ya Adui Mkatili
    Amkeni!—1994
  • Waja—Ulimwengu Usio na Maumivu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 6/22 kur. 5-7

Maumivu Ambayo Hayatakuwapo Tena

MAUMIVU yatakayokomeshwa kwa utimizo wa ahadi ya Biblia yatakuwa yale maumivu yaonwayo kutokana na kutokamilika kwa yule mtu wa kwanza. Maumivu haya yatia ndani yale yawezayo kuelezwa kuwa maumivu ya daima.

Badala ya kuwa ni mfumo wa kuonya mwili juu ya ugonjwa au jeraha, maumivu ya daima yamefananishwa na “king’ora bandia” ambacho hakinyamazi kamwe.[1][2] Haya ndiyo maumivu yasababishayo watesekaji watumie mabilioni ya dola kila mwaka kwa jitihada ya kupata kitulizo, nayo huharibu uhai wa mamilioni.

Mstadi wa maumivu Dakt. Richard A. Sternbach aliandika hivi: “Tofauti na yale maumivu makali ya muda, maumivu ya daima hayawi dalili ya kuonyesha kitu; maumivu ya daima si kiishara cha kuonya.”[3] Emergency Medicine lilikazia hivi: “Maumivu ya daima hayana kusudi lolote.”[4]

Hivyo, madaktari wengi katika miaka ya majuzi wamekuja kuyaona maumivu kuwa ni ugonjwa halisi hayo yenyewe.[5] “Katika maumivu makali ya muda maumivu yenyewe huwa ni dalili ya ugonjwa au jeraha,” aeleza Dakt. John J. Bonica katika The Management of Pain, ambacho ndicho maandishi sanifu ya leo kuhusu maumivu. “Katika maumivu ya daima maumivu yenyewe ndio ugonjwa wenyewe.”[6]

Jitihada za Kuelewa Maumivu

Maumivu bado hayaeleweki kikamili. “Ule msisimko wa sikuzote wa kujaribu kuchunguza kwa undani maumivu ni nini,” likasema gazeti American Health, “hufanya wanasayansi wajibidiishe sana.”[7] Miongo michache iliyopita, wao walichukulia kwamba maumivu ni namna ya mwasho wa hisia, kama kuona, kusikia, na kugusa, ambao huhisiwa na miisho maalumu ya mishipa ya fahamu katika ngozi na kupitishwa katika nyuzi za mishipa ya fahamu hadi kwenye ubongo.[8] Lakini wazo hilo la kufanya maumivu yaonekane sahili hivyo lilipatikana kuwa lisilo la kweli.[9] Jinsi gani?

Jambo moja lililoongoza kwenye ufahamu mpya wa kindani lilikuwa uchunguzi uliofanywa kwa msichana asiyekuwa na hisi ya maumivu. Kufuatia kifo chake katika 1955, uchunguzi wa ubongo wake na mfumo wa mishipa ya fahamu uliongoza kwenye wazo jipya kabisa juu ya kisababishi cha maumivu.[9a] Madaktari “walitafuta miisho ya mishipa ya fahamu,” likaeleza The Star Weekly Magazine, Julai 30, 1960. “Kama [yeye] asingalikuwa na yoyote, hiyo ingeonyesha sababu ya msichana huyo kutokuwa na hisia ya maumivu. Lakini ilikuwako, tena ilionekana kuwa mizuri kabisa.

“Halafu, madaktari wakachunguza zile nyuzi za mishipa ya fahamu zipaswazo kuunganisha miisho ya mishipa ya fahamu na ubongo. Hakika kasoro ingepaswa kupatikana hapa. Lakini haikupatikana. Nyuzi zote zilikuwa nzuri kabisa, kwa kadiri ambayo zingeweza kuonekana, isipokuwa zile zilizozorota kwa sababu ya jeraha.

“Mwishowe, machunguzi yalifanywa kwenye ubongo wa msichana huyo, na, kwa mara nyingine, hakuna kasoro ya aina yoyote ingeweza kupatikana. Kulingana na ujuzi na nadharia zote zilizopo, msichana huyu angalipaswa kuhisi maumivu kikawaida, hata hivyo hangeweza hata kuhisi akitekenywa.” Hata hivyo, alikuwa mwepesi wa kuhisi akibanwa kwenye ngozi na angeweza kupambanua kati ya mguso wa kichwa cha pini na ncha ya pini, ingawa mdungo wa ile pini haukumtia maumivu.[10]

Ronald Melzack, ambaye katika miaka ya 1960 alishiriki kutunga nadharia mpya iliyopendwa na wengi ya kueleza maumivu ni nini, aandaa kielelezo kingine cha utata wayo. Yeye aeleza hivi: “Bi. Hull alifuliza kuelekeza kidole kwenye mguu wake wa chini ambao haukuwapo [ulikuwa umekatwa], na kueleza kwamba alihisi maumivu yakimchoma kama kwamba chuma cha kuchokora moto kilikuwa kikisukumwa ndani ya vidole vyake vya mguu.” Melzack aliambia gazeti Maclean’s katika 1989 kwamba alikuwa bado “anatafuta maelezo juu ya yale ayaitayo maumivu ‘ya kuwazia.’”[11] Kwa kuongezea, kuna yale yaitwayo maumivu ya uhamisho, ambamo huenda mtu akawa na kasoro ya utendaji katika sehemu moja ya mwili kisha ahisi maumivu katika sehemu nyingine.[12]

Akili na Mwili Vyahusika Vyote

Sasa maumivu yatambulishwa kuwa “utendeshano tata kabisa wa akili na mwili.”[13] Katika kitabu chake Pain in America cha 1992, Mary S. Sheridan asema kwamba “kuona maumivu kwategemea sana mawazo ya mtu hivi kwamba akili nyakati fulani yaweza kukana kuwapo kwa maumivu na nyakati fulani iyabuni na kuyaendeleza muda mrefu baada ya kumalizika kwa lile jeraha lenye maumivu makali ya muda.”[14]

Hali ya moyoni ya mtu, uwezo wake wa kukaza fikira juu ya jambo, utu wake, na mambo mengineyo yote yahusika sana kuamua jinsi aitikiavyo maumivu. “Hofu na hangaiko husababisha itikio lililotiliwa chumvi,” akasema Dakt. Bonica aliye mtaalamu wa maumivu.[15] Hivyo, huenda mtu akajifunza kuhisi maumivu. Dakt. Wilbert Fordyce, profesa wa saikolojia ambaye ni mtaalamu wa matatizo ya maumivu, aeleza hivi:

“Suala si kama maumivu yenyewe ni halisi. Bila shaka ni halisi. Suala ni mambo gani muhimu yasababishayo maumivu. Nikiongea nawe kabla tu ya mlomkuu kuhusu mkate uliopachikwa nyama ndani, utaanza kudondosha mate. Hilo ni jambo halisi sana. Lakini latukia kwa sababu ya uchocheo wa hisia. Hapo hapana mkate uliopachikwa nyama ndani. Wanadamu ni wepesi sana kuitikia uchocheo wa hisia. Uchocheo huo huongoza mwenendo wa kijamii, udondoshaji-mate, msukumo wa damu, mwendo wa kuyeyusha chakula, maumivu, mambo ya namna zote.”[16]

Sawa na vile hisiamoyo zako na hali ya akilini ziwezavyo kuongezea maumivu, zaweza pia kuyakandamiza au kuyafisha ganzi. Fikiria kielelezo: Mpasuaji wa mishipa ya fahamu alisema kwamba alipokuwa kijana aliingiwa sana na mahaba juu ya msichana mmoja akiwa ameketi naye juu ya ukuta wenye barafu hivi kwamba hakuhisi baridi yoyote kali wala maumivu matakoni. “Karibu barafu inigandishe mwili,” yeye aeleza. “Bila shaka tuliketi hapo dakika 45, nami sikuhisi kitu.”[17]

Vielelezo hivyo ni vingi. Wachezaji wa mpira wa miguu wenye kujihusisha sana mchezoni au askari kwenye kivumbi cha pigano huenda wakajeruhiwa vibaya na bado wasihisi maumivu mengi au wasihisi yoyote wakati ule.[18] David Livingstone mvinjari maarufu katika Afrika alieleza kwamba alishambuliwa na simba aliyemtikisa “kama vile mbwa-mawindo amfanyavyo panya. Ule mshtuko . . . ulisababisha hali fulani ya ndoto ambamo hamkuwa na hisi ya maumivu.”[19]

Yastahili kuangaliwa kwamba watumishi wa Yehova Mungu, ambao humtumaini kwa utulivu wakiwa na uhakika na tegemeo kamili, wameona pia maumivu yao yakikandamizwa nyakati fulani. “Ni ajabu kwamba baada ya mapigo machache ya kwanza, kwa kweli sikuyahisi tena,” akaripoti Mkristo mmoja aliyepigwa. “Badala ya hivyo, ilikuwa ni kana kwamba nawasikia wakipiga ngoma kwa umbali.”—Amkeni! la Februari 22, 1994, ukurasa 21.[20]

Jinsi Hisia za Maumivu Zirekebishwavyo

Kwa jaribio la kueleza baadhi ya mafumbo ya maumivu, katika 1965 profesa mmoja wa saikolojia, Ronald Melzack, na profesa mmoja wa mwili wa binadamu, Patrick Wall, walitunga ile nadharia iliyoshangiliwa sana ya kwamba kuhisi maumivu hutegemea udhibiti wa lango la hisia katika uti wa mgongo. Chapa ya 1990 ya kitabu cha Dakt. Bonica cha masomo juu ya maumivu ilisema kwamba nadharia hii ilikuwa “miongoni mwa matokeo ya maana zaidi katika utafiti na matibabu ya maumivu.”[21][22]

Kulingana na nadharia hiyo, kufunguka na kufungika kwa lango fulani la kinadharia lililo katika uti wa mgongo huruhusu au kufungia mpito wa viishara vya maumivu katika ubongo. Ikiwa hisi zilizo tofauti na maumivu zajazana kwenye lango, basi viishara vya maumivu vinavyoufikia ubongo huenda vikapungua.[22a] Kwa kielelezo, basi, maumivu hupunguzwa kwa kufikicha au kutikisa kidole kilichochomwa na moto kidogo, kwa kuwa viishara vilivyo tofauti na vile vya maumivu hupelekwa kwa njia hiyo kwenye uti wa mgongo kuzuia mpito wa viishara vya maumivu.[23]

Ugunduzi uliofanyika katika 1975 kwamba miili yetu hufanyiza vitu vyao wenyewe viitwavyo endofini vilivyo kama mofini ulisaidia zaidi katika uchunguzi wa kuyaelewa mafumbo ya maumivu.[23a][24] Kwa kielelezo, huenda watu fulani wakawa na hisi kidogo tu ya maumivu au wasiwe na yoyote kwa sababu wao hufanyiza endofini nyingi mno.[25] Endofini huenda zikaeleza pia sababu ya lile fumbo la kwa nini maumivu hupunguzwa au hata kukomeshwa na utibabu wa kupachikapachika visindano mwilini.[26] Kulingana na ripoti za walioshuhudia kwa macho, upasuaji wa kufungua moyo wazi umefanywa mgonjwa akiwa macho, akiwa na fahamu zake, na akiwa amestarehe, huku dawa pekee ya kumaliza maumivu ikiwa ni utibabu wa kupachikapachika visindano mwilini![27] Kwa nini hakuna maumivu yaliyohisiwa?

Watu fulani huamini huenda ikawa visindano hivyo huchochea mfanyizo wa endofini ambazo huondosha maumivu kwa muda.[28] Uwezekano mwingine ni kwamba utibabu wa kupachikapachika visindano mwilini hugandisha maumivu kwa sababu vile visindano huchochea nyuzi za mishipa ya fahamu ambazo hupeleka viishara vilivyo tofauti na maumivu. Viishara hivyo hujazana katika uti wa mgongo, vikizuia viishara vya maumivu kujisukumiza kuufikia ubongo, ambamo maumivu huhisiwa.[29]

Ile nadharia ya udhibiti wa lango la uti wa mgongo, na uhakika wa kwamba mwili hufanyiza vigandisha-maumivu vyao wenyewe, huenda ikaeleza pia kwa nini hali ya mtu ya moyoni, mawazo yake, na hisiamoyo zaweza kuathiri kipimo cha maumivu ahisiyo.[29a] Hivyo, ule mshtuko wa kushambuliwa ghafula na simba huenda ukawa ulichochea ufanyizaji-endofini wa Livingstone, na vilevile ukamimina viishara vingi sana vilivyo tofauti na vile vya maumivu katika uti wake wa mgongo. Tokeo ni kwamba hisia zake za maumivu zilipunguzwa.[29b]

Hata hivyo, kama ilivyotangulia kusemwa, hali ya mtu ya akilini na hisiamoyo zake zaweza kuwa na tokeo la kinyume. Kuwa na mkazo mwingi mno kila siku kutokana na maisha yaliyo kawaida ya ki-siku-hizi huenda kukaongeza hisi ya mtu ya maumivu kwa kufanyiza wasiwasi, hangaiko, na mikunjamano ya misuli.[30]

Ingawa hivyo, wenye kuteswa na maumivu wana sababu ya kuwa na tazamio zuri. Hii ni kwa sababu wagonjwa wengi sasa wananufaika na njia zilizoboreshwa za utibabu. Maboresho hayo yametokana na uelewevu mzuri zaidi wa ugonjwa huu mbaya sana. Dakt. Sridhar Vasudevan, msimamizi wa Chuo cha Amerika cha Tiba ya Maumivu, alieleza hivi: “Wazo la kwamba nyakati fulani maumivu yaweza kuwa ugonjwa wenyewe lilianzisha badiliko kubwa la utibabu katika miaka ya 1980.”[31]

Utibabu wa maumivu umefanyiwaje mabadiliko makubwa? Ni matibabu gani yanayothibitika kuwa yenye matokeo?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Utibabu wa kupachikapachika visindano mwilini hupunguzaje au hukomeshaje maumivu?

[Hisani]

H. Armstrong Roberts

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki