Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ubishi wa Shakespeare Ile makala “Fumbo la William Shakespeare” (Agosti 8, 1998) ilinichochea nifanye uchunguzi zaidi. Kitabu The Real Shakespeare: Retriving the Early Years, cha Eric Sams, kilitaja mambo fulani yawezayo kupendeza. Kwa mfano, maswali mengi yaweza kujibiwa kwa kuelewa kwamba labda Shakespeare alikuwa Mkatoliki katika Uingereza ya Uprotestanti. Hivyo, kutoroka mnyanyaso wa kidini kungeweza kuwa sababu ya ile miaka yake inayosemekana kuwa ilipotea. Pia, vitabu vinavyodaiwa kuwa vya Shakespeare vina habari nyingi za maisha yake ya mapema. Majina ya watu kadhaa katika vitabu vyake ni majina yaliyotolewa kutoka kwa familia na marafiki wake, kutia ndani jina Hamlet—jina la mwana wake. Michezo yake ya kuigiza ina habari nyingi sana ambazo zingeweza kuwa zilitokana na mambo aliyojionea kibinafsi kama vile uchinjaji nyama.
J. A., Marekani
Yaelekea ubishi kuhusu mshairi huyo hautatatuliwa hivi karibuni. Hata hivyo, tunathamini maelezo hayo.—Mhariri.
Wapenda Ndege Asanteni kwa ufafanuzi wenu wenye kupendeza juu ya uumbaji wa kustaajabisha wa Yehova katika makala “Cock-of-the-Rock—Mrembo wa Msitu wa Amazon.” (Septemba 22, 1998) Makala yenu ilinisafirisha kwa kitambo kidogo hadi kwenye msitu wa Amazon.
E. L. V., Brazili
Kwa njia fulani makala hii ilivutia uangalifu wangu kwa njia tofauti. Iliandikwa kwa njia yenye kuchangamsha, na ilikazia kwamba Yehova aliumba viumbe hawa wote ili kutufurahisha!
L. H., Barbados
Nilifurahia sana makala “Kuwatazama Ndege—Je, Kwavutia Kila Mtu?” (Julai 8, 1998) Lakini ndege-mvumi, mnayerejezea kuwa ndege kutoka “Amerika Kaskazini/Kati,” aweza pia kuonekana Amerika Kusini.
J. P., Argentina
Maelezo yaliyokuwa chini ya picha yetu hayakuwa kamili, na tunathamini ufafanuzi huo.—Mhariri.
Kukaza Akili Nilikuwa na tatizo la kukaza fikira mwalimu alipokuwa akizungumza. Lakini makala yenu “Vijana Huuliza . . . Naweza Kukazaje Fikira?” (Septemba 22, 1998) imenisaidia kubadili mazoea yangu darasani. Tangu nisome makala yenu, nimeshinda tatizo hilo, na sasa nimejitia nidhamu zaidi.
M. A. M., Brazili
Nina tatizo la kukaza fikira. Sikung’amua kwamba jambo linalohitajika ili kukaza fikira lilikuwa kichocheo kidogo na kujitia nidhamu. Jambo hili litahitaji jitihada nyingi, lakini nafikiri naweza kulifanya!
D. R. A., Marekani
Gazeti la Amkeni! lina habari nyingi sana zenye kupendeza vijana kama mimi. Nilinufaishwa na makala hii kwa sababu nina tatizo la kutokaza fikira. Nawapa shukrani za kuhisiwa moyoni.
M. N., Italia
Magarimoshi Nilifurahia kwelikweli kusoma makala “Je, Reli Itadumu?” (Oktoba 8, 1998) Nimekuwa nikivutiwa na magarimoshi tangu nilipokuwa mvulana mdogo. Habari yenu juu ya historia kuhusu tekinolojia ya reli kuanzia mwanzo-mwanzo wa miaka ya 1800 hadi sasa ilikuwa sahihi kabisa. Asanteni kwa makala hii yenye kupendeza.
L. M., Marekani
Ninafanya kazi katika mojawapo ya viwanda vya hali ya juu zaidi vya magarimoshi ulimwenguni, na ninawapongeza kwa kuandika makala bora namna hiyo. Makala yenu ilikuwa na mambo hakika na yaliyothibitishwa vema. Ningependa tu kutaja kwamba magarimoshi fulani ya mwendo wa kasi hutumia vifaa kama vile alumini badala ya chuma cha pua. Kama ilivyoonyeshwa na aksidenti ya garimoshi ya hivi majuzi huko Ujerumani, huenda ikawa mwendo wa kasi huhatarisha usalama.
I. D. C., Ureno