Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/8 kur. 22-24
  • Fumbo la WILLIAM SHAKESPEARE

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Fumbo la WILLIAM SHAKESPEARE
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matatizo ya Msingi
  • Je, Alikuwa Msomi?
  • Vitabu na Hati
  • Kwenda London—Na Kupata Umashuhuri
  • Watu Ambao Huenda Waliziandika Tamthilia Hizo
  • Kurudi kwa Jumba la Maonyesho la Globe la London
    Amkeni!—1998
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Unaweza Kutumaini Ahadi za Nani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/8 kur. 22-24

Fumbo la WILLIAM SHAKESPEARE

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

KWA kawaida William Shakespeare husifiwa kuwa mwandishi wa tamthilia aliye mashuhuri zaidi katika historia. Kitabu The New Encyclopædia Britannica chasema kwamba “anaonwa na wengi kuwa mwandishi wa tamthilia aliye mkuu zaidi. Tamthilia zake . . . zinaigizwa sana na katika nchi nyingi zaidi kuliko tamthilia za mwandishi mwingine yeyote.” Tamthilia zake zimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 70.

Kuhusu utungaji wa kitabu kikubwa ambacho inasemekana kwamba alikiandika, The World Book Encyclopedia chasema: “Hakuna msomi yeyote mashuhuri wa mambo ya Shakespeare anayetilia shaka kwamba Shakespeare hakuandika tamthilia hizo na mashairi hayo.” Lakini, wengine wanabisha jambo hilo. Kwa nini?

Shakespeare alizaliwa Stratford-upon-Avon mwaka wa 1564, akafa huko miaka 52 baadaye, mwaka wa 1616. Mabuku mengi sana yametokezwa kumhusu—miaka mingi baada ya kufanywa utafiti kwa subira—ili kusuluhisha swali moja la msingi na lenye kuvutia, Je, kweli William Shakespeare aliandika tamthilia zenye jina lake?

Matatizo ya Msingi

Tamthilia za Shakespeare zinaonyesha ujuzi mwingi sana wa maisha. Kwa mfano, yeye alifahamu vizuri sheria naye alitumia sana istilahi za kisheria na kuwekea wengine kielelezo. Mnamo 1860, Sir John Bucknill alionyesha katika Medical Knowledge of Shakespeare kwamba Shakespeare alifahamu sana mambo ya dawa. Vilevile alifahamu sana uwindaji, kuwazoeza ndege kuwinda, na michezo mingine, na pia adabu zilizotakikana katika makao ya kifalme. Mwanahistoria wa mambo ya Shakespeare, John Michell, asema kwamba alikuwa “mwandishi aliyejua kila kitu.”

Mivunjiko ya meli imetajwa mara tano katika tamthilia za Shakespeare, na njia ambazo misamiati ya bahari inavyotumiwa yadokeza kwamba mwandishi huyo alikuwa baharia mwenye ujuzi. Je, Shakespeare alipata kusafiri ng’ambo? Je, alisajiliwa katika jeshi la wanamaji? Je, alishiriki katika vita vya kushinda Meli za Hispania mnamo 1588? Yoyote kati ya mambo hayo yangemfanya Shakespeare aweze kuandika hivyo, lakini hakuna uthibitisho wowote uwezao kutolewa. Ndivyo hali ilivyo na maarifa yake ya misamiati ya mambo ya kijeshi na lugha ya wanajeshi wa miguu.

Amenukuu Biblia sana katika vitabu vyake. Huenda alifundishwa na mamake, lakini hakuna uthibitisho unaoonyesha kwamba mama yake alikuwa amejua kusoma. Jambo la kwamba alijua Biblia lazusha suala la elimu ya Shakespeare.

Je, Alikuwa Msomi?

Babake William, John, alikuwa mfanyabiashara wa glavu, sufu, na yawezekana alikuwa na bucha. Aliheshimiwa, ingawa hakujua kusoma na kuandika. Hakuna orodha ya wanafunzi waliohudhuria shule ya sekondari ya Stratford, lakini wengi leo huhisi kwamba William mchanga alihudhuria shule hiyo. Miaka mingi baadaye, rafiki ya William aliyekuwa pia mwandishi wa tamthilia Ben Jonson alimfundisha “Kilatini kidogo, na Kigiriki kidogo,” jambo ambalo huenda likaonyesha kwamba William alikuwa na elimu ya msingi tu.

Lakini, mwandishi wa tamthilia hizo alielewa sana fasihi za Ugiriki na Roma pamoja na fasihi—na labda lugha—za Ufaransa, Italia, na Hispania. Pia alifahamu maneno mengi sana. Leo, si rahisi kwa mtu ambaye ana elimu ya juu kutumia maneno 4,000 katika mazungumzo yake. John Milton, mshairi wa Uingereza wa karne ya 17, alitumia maneno 8,000 hivi katika vitabu vyake. Lakini mtaalamu mmoja asema kwamba Shakespeare alikuwa na msamiati wa maneno yasiyopungua 21,000!

Vitabu na Hati

Mali zote za Shakespeare ziliorodheshwa kwa uangalifu katika wasia wake wenye kurasa tatu, bila kutajwa kwa vitabu au hati. Je, viliachiwa binti yake mkubwa, Susanna? Ikiwa ndivyo, kwa wazi vingegawanywa miongoni mwa wazao wake. Akivutiwa na fumbo hili, kasisi mmoja wa karne ya 18 alichunguza maktaba zote za kibinafsi zilizokuwa umbali wa kilometa 80 kutoka Stratford-upon-Avon bila kugundua hata buku moja tu la Shakespeare.

Hizo hati za tamthilia zinatokeza tatizo kubwa hata zaidi—hakuna hati za awali zinazopatikana. Tamthilia 36 zilichapishwa katika Toleo la Kwanza mnamo 1623, miaka saba baada ya kifo cha Shakespeare. Wakati alipokuwa angali hai, matoleo mengi yaliyoibwa yalitokea, lakini Shakespeare, aliyekuwa mfanyabiashara mwerevu, hakuchukua hatua yoyote ya kisheria ya kuzuia zisichapishwe.

Kwenda London—Na Kupata Umashuhuri

Vikundi vya waigizaji wenye kutangatanga vilikuwa vya kawaida katika nyakati za Elizabeth, na wengine walizuru Stratford-upon-Avon mwaka wa 1587. Ikiwa Shakespeare alijiunga nao, inawezekana alikuwa London kufikia vuli ya mwaka huo. Twajua kwamba alijiunga na kampuni mashuhuri ya waigizaji ya London, ambayo iliitwa Lord Chamberlain’s Men, baadaye ikaitwa King’s Men. Tokea wakati alipofika jiji kuu, hali yake ilibadilika. Katika miaka iliyofuata alipata mali huko London na Stratford-upon-Avon. Lakini hakuna masimulizi dhahiri juu ya matendo yake tokea 1583 hadi 1592—ile “miaka [muhimu] inayokosekana.”

Jumba la michezo la Globe lilijengwa Southwark mwaka wa 1599. Kabla ya wakati huo, tamthilia zenye jina la Shakespeare zilijulikana London, lakini yeye hakupata umashuhuri akiwa mwandishi wa tamthilia hizo. Alipokufa, hakufanyiwa maziko yenye kufana, ingawa waandikaji wengine wa tamthilia, kama Ben Jonson na Francis Beaumont walizikwa kwa sherehe nyingi katika Westminster Abbey ya London.

Watu Ambao Huenda Waliziandika Tamthilia Hizo

Je, jina Shakespeare lilitumiwa kuficha jina la mtungaji halisi au hata watungaji wa tamthilia hizo? Watu wamedokeza zaidi ya watu 60 ambao huenda ikawa waliziandika. Orodha hiyo yatia ndani mwandishi wa tamthilia Christopher Marlowea na majina yasiyotazamiwa kama Kadinali Wolsey, Sir Walter Raleigh, na hata Malkia Elizabeth wa Kwanza. Watu wanaokisia wanasema ni yupi kati ya hao huenda ikawa kwa kweli ndiye aliyeziandika?

Mtu anayetajwa kwanza ni Francis Bacon, aliyesomea Chuo Kikuu cha Cambridge. Yeye alimzidi umri Shakespeare kwa miaka mitatu, akawa wakili mashuhuri na ofisa wa makao ya kifalme naye aliandika vitabu vingi. Dhana ya kwamba vitabu vya Shakespeare viliandikwa na Bacon ilitajwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1769 lakini ikapuuzwa kwa karibu miaka 80. Shirika la Bacon lilifanyizwa mwaka wa 1885 ili kuendeleza dhana hiyo, na mambo mengi yametajwa ili kuunga mkono dai hilo. Kwa mfano, Bacon aliishi kilometa zipatazo 30 kaskazini ya London, karibu na St. Albans, mji ambao umetajwa mara 15 katika vitabu vya Shakespeare—lakini mji alikolelewa Shakespeare, Stratford-upon-Avon, hautajwi kamwe.

Roger Manners, Mkuu wa tano wa Rutland, na William Stanley, Mkuu wa sita wa Derby, pia wanatetewa na mashabiki wao. Wote walisoma sana na walikuwa na ujuzi mwingi wa maisha ya makao ya kifalme. Lakini ni kwa nini yeyote kati yao angeficha uandishi wake? Profesa P. S. Porohovshikov, akiunga mkono kwa dhati dai la Rutland mwaka wa 1939, alisema: “Maandishi yake ya kwanza yalichapishwa bila jina, na mengine yalitumia lakabu kwa sababu tu haikuwa sawa kwa mtu mashuhuri kuandika tamthilia za kuigizwa katika majumba ya kawaida tu ya michezo.”

Wengine wadokeza kwamba tamthilia za Shakespeare ziliandikwa na kikundi cha waandikaji, kila mmoja akijazia utaalamu wake. Kwa upande mwingine, akiwa mwigizaji stadi, je, Shakespeare alihariri na kutayarisha tamthilia za wengine ambazo zingeigizwa jukwaani? Ilisemekana kwamba ‘hakufuta hata mstari mmoja’ katika hati zake. Hilo lingewezekana ikiwa alikuwa anahariri, akirekebisha kidogo, hati za waandikaji wengine alizokuwa amepewa.

Ni sababu ipi iliyo kubwa zaidi inayofanya watu watilie shaka kama kweli Shakespeare ndiye aliyeziandika? Kitabu The World Book Encyclopedia chasema kwamba watu “walikataa kuamini kwamba mwigizaji kutoka Stratford-upon-Avon angeziandika. Mahali pa kawaida tu ambapo Shakespeare alitoka hapakuonekana kuwa pangetokeza mtu mwenye akili nyingi aliyeandika tamthilia hizo.” Kinaongezea kwamba karibu wote ambao yasemekana kuwa waliandika tamthilia hizo “walikuwa watu wa ukoo bora au wa tabaka ya juu.” Hivyo, wengi wanaotilia shaka kwamba Shakespeare aliziandika waamini kwamba “ni mtu mwenye elimu na ustaarabu na aliye wa tabaka ya juu tu ndiye angeweza kuandika tamthilia hizo.” Lakini, kama ilivyotajwa awali katika makala hii, wataalamu wengi wa mambo ya Shakespeare waamini kwamba ni Shakespeare aliyeziandika.

Je, ubishi huo utapata kusuluhishwa wakati wowote karibuni? Haielekei hivyo. Ila tu hati za awali au mambo fulani ya hakika yapatikane ya kujazia ile miaka inayokosekana, William Shakespeare, “huyo mtaalamu mkuu wa lugha,” ataendelea kuwa fumbo lenye kuvutia.

[Maelezo ya Chini]

a Uvutano wa Christopher Marlowe wadhihirika katika tamthilia za awali za Shakespeare, lakini alikufa akiwa London mwaka wa 1593 akiwa na umri wa miaka 29. Wengine wamedokeza kwamba kuuawa kwake katika ghasia kwenye mkahawa mmoja kulikuwa udanganyifu tu na kwamba alienda Italia, ambako aliendelea na kazi ya kuandika. Hakuna rekodi ya maziko yake.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Usomi Wake na Jina Lake

Yawezekana kwamba William Shakespeare alitia sahihi yake mara sita katika hati nne ambazo bado zipo. Jina lake halisomeki vizuri, na limeandikwa kwa tahajia tofauti-tofauti. Wataalamu fulani wadokeza kwamba huenda mawakili walitia sahihi wasia wa Shakespeare kwa niaba yake, jambo ambalo lazusha swali jingine gumu, Je, William Shakespeare alijua kusoma na kuandika? Hakuna hati alizoandika. Binti yake Susanna angeweza kutia sahihi ya jina lake, lakini hakuna uthibitisho kwamba angeweza kuandika zaidi ya kutia tu sahihi. Binti mwingine wa Shakespeare, Judith, ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na babake, alikuwa akitia sahihi zake kwa kutumia alama. Hakujua kusoma wala kuandika. Hakuna mtu ajuaye ni kwa nini Shakespeare hakusomesha watoto wake ili wafurahie manufaa nyingi sana za kusoma fasihi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha za awali za Shakespeare, ingawa sura yake haijulikani vizuri

[Hisani]

Encyclopædia Britannica/11th Edition (1911)

Culver Pictures

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki