Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Karne ya Ukatili Leo nilipokea toleo la Amkeni! la Agosti 8, 1998, kutoka kwa posta. Nilipoona tu jalada la juu, nililazimika kuketi na kusoma habari yenye kichwa “Karne ya Ukatili—Je, Tuisahau?” Kwa kweli ninasikitika kuona maovu ambayo wanadamu wanaweza kufanya. Jinsi ninavyotamani wakati ambapo wanadamu wote wataishi kwa amani ya kweli!
T. D., Marekani
Toleo hili lilijibu maswali ambayo nimekuwa nayo kwa kipindi fulani sasa. Nahisi kwamba Mungu anafanya kazi ya kuwasaidia watu walio na maswali kama yangu kupitia vichapo vyenu.
T. C., Marekani
Muziki wa Kilatini Asanteni sana kwa ajili ya makala “Uvutio wa Tufeni Pote wa Muziki wa Kilatini.” (Agosti 8, 1998) Napenda muziki na kucheza dansi. Asanteni kwa kuonyesha baadhi ya zile ziwezazo kuwa hatari, kama vile muziki uitwao narco corrido. Nisingeweza kuipata habari hii mahali penginepo pote. Nilithamini sana.
J. B., Marekani
Fumbo la Shakespeare “Yenye kustaajabisha” ndiyo maneno pekee niwezayo kutumia kueleza ile makala “Fumbo la William Shakespeare.” (Agosti 8, 1998) Mimi hufunza wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari lugha na fasihi ya Kireno na mara nyingi ninatumia makala zenu darasani.
J. S. G., Brazili
Ningependa kuwapongeza kwa ajili ya makala yenu juu ya utungaji wa tamthilia za Shakespeare. Inaonyesha kwa nini watu wengi hawasadiki nadharia iliyokubaliwa ya kwamba Shakespeare ndiye aliyetunga tamthilia hizi.
F. C., Uingereza
Usanii Wenye Kuvutia Nilijifunza kazi ya uchoraji miaka kadhaa iliyopita, nami nafikiri toleo la Amkeni! la Agosti 8, 1998, ni lenye kuvutia sana. Lenye kupendeza zaidi ni pambizo lake lenye mchoro wa seng’enge lililofuatwa na pambizo lenye waridi na picha zenye rangi za “Vito vya Anga la Kiafrika” pamoja na zile picha zenye kustaajabisha zilizoko katika sehemu ya ndani ya jalada la nyuma.
S. K. C., Uingereza
Matangazo ya Biashara Binti yangu si mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Kwa kuwa anafanya kazi ya matangazo ya biashara, nilimpelekea toleo la Amkeni! la Agosti 22, 1998, lenye mfululizo wa makala “Matangazo ya Biashara—Yanakuathirije?” Alilisifu sana akasema kwamba waandishi wenu walielewa lengo la ustadi wa kushawishi.
R. S., Marekani
Ladha Tangu binti yangu mwenye umri wa miaka 13 alipokuwa mtoto mchanga, amekataa kuonja vyakula vipya. Na kwa hiyo ninashukuru sana kwa ajili ya makala “Ladha—Zawadi ya Muumba Mwenye Upendo.” (Agosti 22, 1998) Nilithamini hasa madokezo yenu ya kuwasaidia watoto kupenda vyakula vipya. Nilianza kumwomba binti yangu anisaidie kutayarisha baadhi ya vyakula ambavyo hakuvipenda hapo awali. Dokezo lenu lilifanya kazi! Sasa anakula vyakula vyenye lishe ambavyo hakuwa akivipenda.
B. M., Poland
Je, Tumlaumu Shetani? Nina umri wa miaka 17 na ni juzi tu niliposoma Amkeni! kwa mara ya kwanza. Sasa mimi huvutiwa sana kulisoma! Lilikuwa na habari yenye thamani, kama vile “Maoni ya Biblia: Je, Tumlaumu Shetani kwa Dhambi Zetu?” (Septemba 8, 1998) Mpaka wakati niliposoma habari hii, nilifikiri kwamba ningeweza kumlaumu yeye kila nilipofanya dhambi. Kwa vyovyote vile, gazeti lenu ni bora sana, nami nalipendekeza kwa kila mtu. Tafadhali niwekeni kwenye orodha yenu ya watu wanaopelekewa magazeti!
M. M., Marekaniy