Kitendeshi cha Rh na Wewe
BABA mwenye fahari atazama chini kwa furaha akiangalia mtoto wake mgeni amelala kwa utulivu mikononi mwa mama yake. Usiku ulikuwa mrefu katika chumba cha kujifungulia, lakini sasa yote hayo yamepita. Daktari aingia ili kuchunguza wagonjwa wake na kuwapongeza wote. “Sina mengi, ni ile kawaida ya ukaguzi tu,” asema.
Damu ya mama ni Rh-hasi, na uchunguzi ulionyesha kwamba ya mtoto ni Rh-chanya, kwa hiyo mama atahitaji kupigwa sindano ya kuimarisha kinga. “Ni sindano ndogo tu yenye viuavijasumu vya kibinadamu lakini iliyo ya maana sana,” daktari awahakikishia, “kwa ajili ya kuzuia matatanisho kuhusiana na mimba za wakati ujao.”
Ingawa huenda daktari akaiona sindano hiyo kuwa kawaida yake, kutajwa kwayo na “matatanisho” yawezekanayo kutokea watokeza fungu la maswali katika akili za wale wazazi wenye hangaiko. Sindano hii hufanya nini hasa? Yahitajika kwa kadiri gani? Ingekuwaje kama wazazi hawangeitaka? Kwa Mkristo swali jingine laibuka. Kwa kuwa Biblia husema, ‘Jiepusheni na damu,’ je, Mkristo aweza kukubali sindano hiyo kwa dhamiri njema ikiwa ina viuavijasumu vya kibinadamu kutokana na damu ya mtu mwingine?—Matendo 15:20, 29.
Historia ya Tatizo la Rh
Miongo iliyopita wanasayansi waligundua kwamba damu ya kibinadamu ina vitendeshi vingi, au antijeni, vifanyavyo damu ya kila mtu iwe isiyo na kifani. Baada ya muda wakapata kujua kwamba mifumo miwili ya antijeni katika chembe nyekundu za damu ndiyo iliyosababisha yaliyo mengi ya matatizo ya kitiba ikiwa damu ya mtu mmoja iligusanishwa na ya mtu mwingine. Mojapo antijeni hizi huitwa “ABO” (kikundi cha aina za damu); ile nyingine hutajwa kuwa “Rh.” Pitio fupi la mfumo wa Rh litatusaidia tuyaelewe masuala ya maana waliyo nayo wazazi hawa wenye kuhangaika na ambayo wewe pia huenda ukawa umejiuliza.
Katika 1939, madaktari walichapisha kisa cha kutatanisha cha mwanamke mwenye miaka 25 ambaye mtoto wake wa pili alikufa wakati wa mimba. Baada ya kujifungua mtoto mfu huyo, mwanamke huyo alitiwa-tiwa damu mishipani na kuanza kutatizika vikali hata ingawa damu hiyo ilitoka kwa mume wake na yaonekana ilipatana na yake mwenyewe kwa habari ya zile antijeni za ABO. Baadaye madaktari walikisia kwamba kitendeshi fulani kisichojulikana kilichochangamana na damu yake kutoka kwenye damu ya mtoto wake wa kwanza kilikuwa ‘kimenyetisha’ damu yake, kikiongoza damu yake ikataane na damu ya mume wake na pia kuleta hasara ya kufiwa na mtoto wake wa pili.
Kitendeshi hiki kisichojulikana kilitambuliwa baadaye kupitia majaribio yaliyohusisha matumbili wa “rhesus,” kwa hiyo kikatajwa kuwa “kitendeshi cha Rh.” Kitendeshi hiki cha damu kilizungumzwa sana na wanatiba muda wote wa miaka ya 1960 kwa sababu kiligunduliwa kuwa ndicho kisababishi cha ugonjwa ambao kidogo ni wa kawaida na wenye kuua watoto mara nyingi uitwao erythroblastosis fetalis. Kadiri madaktari walivyochunguza kitendeshi cha Rh na maradhi hayo, kisa cha kusisimua kitiba kilifunuka.
Rh, Urithi wa Jeni, na Watoto Wagonjwa
Watu walio wengi huguswa moyo wakati mtoto mgeni awapo ni mgonjwa mahututi au afapo. Kuona tu kitoto kichanga kikiwa kigonjwa au kimesononeka huuma watu wengi, na madaktari si tofauti. Sababu nyingine mbili zilifanya hiki kitendeshi cha Rh chenye kuua watoto kiwahangaishe sana matabibu.
Ya kwanza ilikuwa kwamba madaktari walianza kuona kigezo fulani kuhusu maradhi hayo na kuelewa jinsi kitendeshi hicho cha Rh kilivyohusika katika ugonjwa na kifo. Kitendeshi cha Rh kimo katika chembe nyekundu za damu za watu karibu asilimia 85 hadi 95, wanaume na wanawake pia. Wao hutajwa kuwa “Rh-chanya.” Wale asilimia 5 hadi 15 wasio nacho hubandikwa jina “Rh-hasi.” Ikiwa mtu aliye Rh-hasi apatiwa damu ya mtu aliye Rh-chanya, huenda ndani yake mkafanyika molekuli ziitwazo mazindiko ambazo huangamiza damu ya Rh-chanya.
Kwa kweli hili ni itikio la kawaida, la kiafya katika mfumo wa kinga ya mwili wakati ufanyapo pambano la kuondosha wavamizi wa kigeni. Tatizo ni, mama aliye Rh-hasi huenda akapata mtoto arithiye damu ya Rh-chanya kutoka kwa baba yake. Hii haitokezi tatizo wakati plasenta ifanyapo kazi vizuri kabisa na damu ya mtoto huyo ikaendelezwa ikiwa imetengana na ile ya mama. (Linganisha Zaburi 139:13.) Lakini kwa sababu miili yetu ni isiyokamilika, kiasi kidogo cha damu ya mtoto huyo huenda nyakati fulani kikavuja na kuingiliana na ile ya mama. Pindi kwa pindi, hili hutendeka kwa sababu ya utaratibu fulani wa kitiba, kama vile amniosentesisi (kuvuta sampuli ya kimiminiko kilicho katika mfuko wa uzazi unaozunguka mtoto anayekua). Au huenda kiasi fulani cha damu ya mtoto kikachangamana na damu ya mama wakati wa kujifungua. Chochote kiwacho ndicho kisababishi, huenda mama akawa mwenye kunyetishwa na kufanyiza mazindiko dhidi ya ile damu ya Rh-chanya.
Wazia tatizo hilo: Mama akiisha kukuza mazindiko hayo, watoto wote wanaofuata huwa hatarini iwapo watarithi damu ya Rh-chanya kutoka kwa baba. Hii ni kwa sababu sasa mama ana mazindiko ya kukinza damu ya Rh-chanya.
Waona, mazindiko fulani hupita katika plasenta kwa kawaida nzuri. Hili ni jambo jema, linalosababisha watoto wote wazaliwe wakiwa wamepata kadiri fulani ya kinga asili iliyo ya muda kutoka kwa mama zao. Hata hivyo, kwa habari ya ugonjwa wa Rh, mazindiko ya Rh ya mama aliyenyetishwa hupita katika plasenta na kushambulia damu ya mtoto ya Rh-chanya. Ni mara haba jambo hili huathiri mtoto wa kwanza, nalo hufanyika kwa kawaida zaidi kuhusiana na watoto wowote wanaofuata. Husababisha ugonjwa, uitwao maradhi ya Rh yaangamizayo chembe nyekundu za damu ya mtoto mgeni (erythroblastosis fetalis ikiwa madhara ni makubwa).
Kuna njia nyingi za kudhibiti maradhi haya, ingawa mara nyingi mafanikio huwa machache, kama tutakavyoona. Sasa acheni tukaze fikira juu ya jambo moja la kitiba la tatizo hilo—njia iwezekanayo ya kuzuia.
Ugunduzi wa Kuzuia
Huenda ukakumbuka kwamba kulikuwa na sababu mbili zilizofanya maradhi haya yawe ya kuwasisimua sana madaktari. Ya kwanza ilikuwa kwamba utendaji wa ugonjwa huo ulipata kujulikana na kueleweka. Sababu ya pili ilikuwa nini?
Ilijitokeza katika 1968. Baada ya miaka mingi ya utafiti na majaribio ya madaktari ya kutibu watoto hawa wagonjwa sana, ambayo hayakufanikiwa sana, ukingaji fulani ulisitawishwa ukawa na matokeo ya kuzuia tatizo la “watoto wa Rh.” Hii ilikuwa habari njema. Lakini uliendeshwaje?
Kumbuka kwamba tatizo la Rh (kwa mtoto wa pili na wale wanaofuata walio wa Rh-chanya) lilisitawi wakati damu kutokana na mtoto wa kwanza wa Rh-chanya ‘ilipovuja’ kuingia katika mkondo wa damu ya mama wa Rh-hasi na kusababisha atokeze mazindiko. Je, kungeweza kuwa na njia ya kuzoa chembe nyekundu za damu ya mtoto katika mfumo wa mama kabla hazijapata nafasi ya kumnyetisha mama?
Njia iliyobuniwa ilikuwa kumpiga mama sindano ya kumtia kinga iitwayo globulini ya kinga ya Rh, au RhIG, ijulikanayo katika nchi fulani kwa majina ya kibiashara, kama vile RhoGAM na Rhesonativ. Imefanyizwa kutokana na mazindiko yaliyo dhidi ya antijeni ya Rh-chanya. Ni jambo tata kueleza ifanyavyo kazi hasa na hata haieleweki, lakini kwa msingi yaonekana hufanya kazi kwa njia inayofuata.
Wakati mama aliye Rh-hasi ashukiwapo kuwa ameingiwa na damu ya Rh-chanya, kama baada ya kujifungua mtoto aliye Rh-chanya, mama huyo hupigwa sindano ya RhIG. Mazindiko haya hushambulia haraka chembe nyekundu zozote za damu ya Rh-chanya zilizovuja kutoka kwa mtoto na kuziangamiza kabla hazijamnyetisha mama. Hii hukomesha hatari kwa mtoto afuataye, kwa kuwa hakuna mazindiko dhidi ya damu ya Rh-chanya yafanyizwayo na mama. Faida halisi ambayo madaktari huona katika jambo hili ni kwamba hilo hutumika kuzuia maradhi badala ya kujaribu kutibu ugonjwa baada ya kusitawi.
Hili lasikika sawa kinadharia, lakini je, limekuwa na matokeo? Yaonekana, ndiyo. Katika nchi moja, Marekani, mtukio wa maradhi ya kuangamizwa kwa chembe nyekundu za damu ya Rh ulipungua kwa asilimia 65 katika miaka ya 1970. Ingawa mambo mengi yangeweza kuwa yalichangia hili, asilimia 60 hadi 70 ya punguo hili ilihesabiwa kwa utumizi wa RhIG. Katika mkoa mmoja wa Kanada, idadi ya watoto wenye kufa kutokana na maradhi ya kuangamizwa kwa chembe nyekundu za damu ya Rh ilipungua kutoka 29 katika 1964 hadi 1 kati ya 1974 na 1975. Jumuiya ya kitiba iliona huu kuwa uhakikisho wa ile kanuni ya kwamba “usipoziba ufa utajenga ukuta.” Tukiwa na habari hizi za msingi, twaweza kufikiria maswali fulani hususa yatokeayo mara nyingi kuhusu maradhi ya Rh.
Ni nini hatari za kuwa na tatizo na maradhi ya Rh wakati wa mimba yangu?
Uchunguzi sahili wa damu waweza kupambanua namna za damu ya Rh za mama na baba; kama 1 kati ya ndoa 7 hivi ina mwanamke aliye Rh-hasi na mwanamume aliye Rh-chanya. Mambo yahusuyo umbo la urithi wa jeni la baba huipunguza hatari ya jumla kuwa karibu asilimia 10.a
Hata hivyo, hizo ni takwimu za idadi za jumla. Ikiwa wewe ni mwanamke aliye Rh-hasi aliyeolewa na mwanamume aliye Rh-chanya, uwezekano wenu ni ama asilimia 50 ama asilimia 100 wa kupata mtoto aliye Rh-chanya, ikitegemea umbo la urithi wa jeni la mume wako.b (Hakuna njia hakika ya kupambanua jeni za mume, sawa na vile hakuna bado njia sahili ya kupambanua kama mtoto katika tumbo la uzazi ni Rh-chanya.)
Kwa mama aliye Rh-hasi anayebeba mtoto aliye Rh-chanya, kuna uwezekano wa asilimia 16 kwa kila mimba kwamba yeye atanyetishwa, hivyo akihatarisha mimba za wakati ujao. Bila shaka, huo ni wastani tu. Kwa kuzuia kutia damu mishipani mapema au kutomwacha mama aingiwe na damu, yule mtoto wa kwanza wa ndoa kwa kawaida huwa huru na hatari ya maradhi ya Rh. Baada ya mtoto huyo wa kwanza, kwa kawaida hatari huwa ngumu kidogo kutabiriwa katika kisa chochote kile. Huenda mwanamke mmoja akanyetishwa na mtoto wake wa kwanza kabisa aliye Rh-chanya. Huenda mwingine akapata watoto watano au zaidi walio Rh-chanya na asinyetishwe kamwe. Ikiwa mama apata kunyetishwa, hatari ya kifo kwa kila kijusu cha Rh-chanya kinachofuata ni asilimia 30, na hili halibadilishwi na muda upitao kati ya mimba moja na nyingine. Kwa hiyo hili si jambo la kupuuzwa.
Je, uchunguzi wa maabara waweza kunijulisha kama mtoto wangu anayekua yuko hatarini?
Ndiyo, kwa kadiri fulani. Viwango vya mazindiko katika damu ya mama vyaweza kupimwa wakati wa mimba ili kujua kama anafanyiza mazindiko dhidi ya damu ya mtoto. Pia, amniosentesisi yaweza kusaidia kujulisha kama damu ya mtoto inaangamizwa na kama mtoto yumo hatarini. Hata hivyo, nyakati fulani amniosentesisi hutokeza matatanisho yayo yenyewe, na kwa hiyo kwapaswa kuwe na tahadhari juu ya kufanyiwa uchunguzi huo.
Je, ile sindano ya RhIG ina athari za kando?
Kungali na ubishi juu ya kutumiwa kwayo wakati wa mimba kwa sababu ya madhara yawezekanayo kupata mfumo wa kinga wa kijusu kinachokua. Hata hivyo wastadi walio wengi hukata shauri kwamba ufanyizaji kinga ni salama kiasi fulani kwa mama na kwa mtoto pia anayekua ndani yake.
Kulingana na madaktari, napaswa kupata sindano hiyo mara nyingi kadiri gani?
Wajuzi wasema kwamba sindano hiyo yapasa kuwa mara tu baada ya tukio lolote ambalo huenda likawa limesababisha damu ya Rh-chanya iingie katika mkondo wa damu wa mwanamke aliye Rh-hasi. Hivyo, mapendekezo ya sasa ni kwamba sindano hiyo ipigwe mnamo saa 72 za kujifungua mtoto ikiwa damu ya mtoto yapatikana kuwa Rh-chanya. Pendekezo hilohilo latumika kwa kisa cha amniosentesisi au kutunguka kwa mimba.
Zaidi ya hilo, kwa kuwa machunguzi yameonyesha kwamba kiasi kidogo cha damu ya mtoto huenda kikaingia katika mkondo wa damu ya mama wakati wa mimba iliyo ya kawaida nzuri, madaktari fulani hupendekeza kwamba sindano hiyo ipigwe kwenye majuma 28 ya muda wa mimba ili kuzuia unyetisho. Iwapo hivyo sindano bado ingependekezwa tena baada ya mtoto kuzaliwa.
Je, kuna matibabu yoyote kwa mtoto akiisha kupata maradhi ya Rh?
Ndivyo. Ingawa maradhi ya kuangamizwa kwa chembe nyekundu za mtoto mgeni ni ugonjwa mzito, kuna ithibati ya kutosha kuunga mkono matibabu yasiyo ya kutoa damu ya mtoto kwa kumtia nyingine ya badala. Utatanisho uhofiwao zaidi wa maradhi haya wahusisha mjazano wa kemikali iitwayo bilirubini, itokanayo na mvunjiko wa chembe nyekundu za damu. Hii hutokeza ugonjwa-njano wa nyongo na katika visa fulani yaweza kudhuru viungo vya mtoto. (Kando ya hilo, ugonjwa-njano mpole wa nyongo huenda ukasababishwa wakati ABO haipatani kati ya damu ya mama na damu ya mtoto, lakini kwa kawaida hili si jambo zito sana.)Kwa miaka kadhaa madaktari walifikiri kwamba kadiri hususa ya ugonjwa-njano wa nyongo ilionyesha ilifaa kutoa damu katika watoto hawa na kuibadilisha kwa nyingine, lakini utafiti zaidi umefunua matibabu mbalimbali ya badala. Kujifungua mapema au kujifungua kwa kupasuliwa kikaisari, matibabu-nuru (nuru ya buluu), na dawa kama vile fenobarbitali, makaa yaliyotiwa utendanisho, na matibabu mengine yamethibitika kuwa yenye msaada na yamepunguza sana himizo la kutia damu mishipani. Kwa kweli, ripoti fulani za majuzi zimekazia ubatili na hata hatari ya kutia damu ya mbadilishano katika damu ya watoto wenye maradhi ya Rh.—Ona sanduku, ukurasa 26.
Hata hivyo, kuna visa vya kupita kiasi ambapo bado madaktari wasisitiza kwamba kutoa damu na kubadilisha kwa nyingine ndiyo matibabu pekee yakubalikayo. Kwa hiyo, wazazi fulani huhisi kwamba ni afadhali kuepuka tatizo lote kwa kupata sindano itakayozuia maradhi hayo na hivyo kuzuia ule ugonjwa-njano wa nyongo.
Je, ile sindano ya RhIG hufanyizwa kutokana na damu?
Ndiyo. Mazindiko yafanyizayo ile sindano huvunwa kutokana na damu ya watu mmoja-mmoja ambao wametiwa kinga au wakanyetishwa kuhusiana na kitendeshi cha Rh. Huenda RhIG ya kufanyizwa kutokana na jeni ya urithi bila kutolewa katika damu ikapatikana wakati ujao.
Je, Mkristo aweza kukubali RhIG kwa kudhamiria?
Suala lihusikalo ni uwezekano wa kutumia damu vibaya. Maandiko hukataza kwa mkazo sana kula damu au kuitumia vibaya kwa njia nyinginezo. (Mambo ya Walawi 17:11, 12; Matendo 15:28, 29) Kwa kuwa RhIG hufanyizwa kutokana na damu, je, ingekuwa ni kuvunja amri ya Biblia kujiepusha na damu ikiwa mwanamke Mkristo angekubali sindano hiyo?
Jarida hili na jenzi lalo, Mnara wa Mlinzi, limetoa maelezo kwa upatani juu ya jambo hilo.c Tumearifu kwamba katika mimba zote mazindiko hupita katika plasenta bila kizuizi kati ya mama na mtoto. Kwa sababu hiyo Wakristo fulani wamekata shauri kwamba kwao haionekani ni kuvunja sheria ya Biblia kukubali sindano yenye mazindiko, kama RhIG, kwa kuwa utaratibu huo kwa msingi ni kama ule utukiao kiasili.
Ingawa hivyo, uamuzi wa kukubali au kutokubali RhIG hubaki hatimaye ukiwa jambo la uamuzi wa kuamuliwa kwa kudhamiriwa na kila mume na mke Wakristo. Hata hivyo, ikiwa mume na mke wanaokabili suala la Rh waamua kutoikubali RhIG ionyeshwapo kitiba, wao wahitajiwa wawe tayari kuikubali hatari ya kupata mtoto wa wakati ujao akiwa ameathiriwa sana na ugonjwa ambao yawezekana ungaliweza kuzuiwa. Katika hali hii wangeweza hata kuamua kwamba mwendo wa hekima ni kuchukua tahadhari za ziada ili wasipate watoto zaidi na kujiweka katika uwezekano wa msiba huo. Wazazi Wakristo wenye hangaiko wapaswa kufikiria mambo yote kwa sala kabla ya kufanya maamuzi mazito hivyo.
[Maelezo ya Chini]
a Takwimu hizi hutofautiana kwa watu wa jamii tofauti. Katika weupe walio wengi mtukio wa uhasi-Rh ni asilimia 15; weusi Wamarekani, asilimia 7 hadi 8; Wahindi-Wanaulaya-Asia, karibu asilimia 2; Wachina na Wajapani wa Kiasia, karibu sifuri.—Transfusion Medicine Reviews, Septemba 1988, ukurasa 130.
b Wanawake fulani walio katika hali hii wamepata watoto kadhaa, na wote walikuja kuonekana kuwa Rh-hasi, kwa hiyo mama hakupata kunyetishwa. Lakini katika visa vingine, mtoto yuleyule wa kwanza alikuwa Rh-chanya, na mama akanyetishwa.
c Ona Mnara wa Mlinzi la Juni 1, 1990, kurasa 30, 31; Novemba 15, 1978, kurasa 21-23 au Juni 15, 1978 (la Kiingereza), kurasa 30, 31; na Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Bilirubini Iliyopanda—Ni Sababu ya Kutiwa Damu Mishipani?
Madaktari wameogopa kwa muda mrefu matokeo ya bilirubini iliyopanda katika watoto, wakaogopa sana hivi kwamba wakati bilirubini hiyo ianzapo kupanda—hasa kuelekea hesabu ya miligramu 20 kwa kila mililita 100—mara nyingi madaktari husisitiza damu itolewe kwa kubadilishwa na nyingine “ili kuzuia madhara ya ubongo” (kernicterus). Je, hofu yao, na kadirio la ubora wa kutiwa damu mishipani, ina sababu za haki?
Dakt. Anthony Dixon ataarifu hivi: “Machunguzi kadhaa kwa watoto wachanga wa jinsi hiyo yameshindwa kugundua matokeo yoyote, yawe ni ya muda mfupi au mrefu, ya bilirubini iliyo kati ya miligramu 18 hadi 51 kwa kila mililita 100.” Dakt. Dixon aendelea kuzungumzia “vijintifobia: hofu ya 20.” Ingawa haijathibitishwa kuna faida yoyote ya kutibu kiasi hicho cha bilirubini, Dakt. Dixon akata shauri hivi: “Muhali uko wazi. Utibabu thabiti wa viwango vilivyopanda vya seramu ya bilirubini sasa ni zoea la kawaida. Matibabu yale ya kawaida hayapasi kupingwa mpaka yathibitishwe kuwa na kosa, na bado si tabia njema kufanya jaribio lolote la kuonyesha kwamba matibabu hayo yana kosa!”—Canadian Family Physician, Oktoba 1984, ukurasa 1981.
Kwa upande ule mwingine, mstadi Mwitalia, Dakt. Ersilia Garbagnati, ameandika juu ya fungu la ulinzi la bilirubini na “hatari ziwezazo kutarajiwa kutokana na kiasi cha chini isivyofaa cha seramu ya bilirubini.” (Italiki ni zetu.) (Pediatrics, Machi 1990, ukurasa 380) Kwa kuongezea kidogo, Dakt. Joan Hodgman aandika hivi katika Western Journal of Medicine: “Kutia damu mishipani kwa kuibadilisha na nyingine hakutazuia bilirubini isitie dosari katika ubongo wakati bilirubini itiwapo kwa kiasi kidogo na, kulingana na majaribio yaliyonukuliwa juu, huenda hasa kukadhuru.”—Juni 1984, ukurasa 933.