Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuwa na mwenendo wa kimungu kuwaelekea wengine
    Mnara wa Mlinzi—1982 | Januari 1
    • SI KUTENDA WATU KWA UKATILI

      13, 14. Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba Yesu hakuwa akiunga mkono kuwatenda watu kwa ukatili?

      13 Ili tusaidiwe kuamua tunavyopaswa kujiendesha kumwelekea mtu wa namna hiyo, tunahitaji kuyaelewa maneno haya ya Yesu: “Mwache yeye awe kwako kama mtu tu wa mataifa na kama mtoza kodi.” Katika karne za baadaye, marabi fulani wa Kiyahudi (waalimu wa kidini) walionyesha maoni ya kupita kiasi, kama yale ya kusema kwamba Myahudi hata asimsaidie mtu wa Mataifa yale mengine aliyekuwa katika hatari ya kufa. Ukatili huo wa moyo haukuonyeshwa kuwaelekea watu wa Mataifa yale mengine peke yao. Kwa mfano, katika mfano wa Yesu juu ya kuwa jirani wa kweli, Mlawi na kuhani pia walikataa kusaidia Myahudi mwenzao aliyeumia, ingawa baadaye Msamaria alimsaidia.​—Luka 10:29-37.

      14 Lakini katika Mathayo 18:17 Yesu hawezi kuwa alimaanisha kwamba wanafunzi wake wakatae kufanya tendo la fadhili za kibinadamu, kama wakati kunapokuwa na tukio baya lisilotazamiwa au la mtu kuwa na shida nyingi ya kuhitaji kitu fulani. Yesu aliwaonyesha fadhili hizo watu fulani wa Mataifa yale mengine. Kwa mfano, alimwonyesha fadhili hizo mwanamke Mfoinike-mshami. Ingawa Yesu, wanafunzi wake na mwanamke huyo walikubali maoni ya kwamba lilikuwa si jambo la kawaida kumfadhili mwanamke huyo kwa sababu yeye alikuwa mtu wa Mataifa naye Yesu alitumwa kwa Wayahudi, bado Kristo aliponya binti ya mwanamke huyo. (Mt. 15:21-28; Marko 7:24-30) Yesu alionyesha fadhili za kibinadamu kama hizo wakati afisi Mrumi wa kijeshi alipomsihi sana aponye mtumwa aliyepooza mwili na mwenye kutaabika. Afisa huyo alikubali maoni ya kwamba hakumtazamia Yesu, akiwa mwalimu wa Kiyahudi, aingie ndani ya nyumba yake. Na bado “wazee wa Wayahudi” walimwomba Yesu amwonyeshe rehema Mtaifa huyo mwenye kustahili, naye akafanya hivyo. (Luka 7:1-10; Mt. 8:5-13) Kwa hiyo kwa maneno aliyoyasema juu ya mtu kuwa “kama mtu tu wa mataifa na kama mtoza kodi,” Yesu hakukataza watu wasitendewe fadhili zenye rehema. Basi, yeye alimaanisha nini?

      “KAMA MTOZA KODI”

      15. Wayahudi waliwaonaje na waliwatendeaje watoza kodi?

      15 Kwanza, Wayahudi waliwaonaje na waliwatendeaje watoza kodi?

      “Watoza kodi wanaotajwa na Agano Jipya walionwa kuwa wasaliti na waasi-imani, waliochafuliwa kwa kushirikiana mara nyingi na waabudu wa miungu ya kishenzi, wakiwa kama vyombo vilivyo tayari kutumiwa na yule mwonezi. Wao walihesabiwa kuwa katika kundi moja na watenda dhambi . . . pamoja na makahaba . . . pamoja na waabudu wa miungu ya kishenzi. . . . Kwa kuwa watu wenye maisha ya adabu walijitenga nao, watoza kodi waliachwa peke yao kisha rafiki zao au wenzi wao wa pekee wakawa ni watu ambao walikuwa wamekataliwa mbali na kuepukwa kama wao wenyewe.”​—Kitabu “Cyclopaedia” ya M’Clintock na Strong, Vol. VIII, uku. 769.

      Naam, walioyasikia yale maneno ya Yesu walijua vizuri kwamba Wayahudi kwa ujumla waliwaepuka watoza kodi. Wayahudi walishughulika na watu hao mara chache sana walipokwenda kulipa kodi iliyotakwa na sheria, na hata nyakati chache hizo walishughulika nao bila kupenda.

      16, 17. Yesu alikuwa na mwenendo gani kuelekea watoza kodi fulani?

      16 ‘Lakini,’ huenda mtu akauliza, ‘Yesu hakushirikiana na watoza kodi?’ Eeh, acheni tuyachunguze mambo ya uhakika.

      17 Akiwa ndiye “Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu,” Yesu alikuwa nuru kwa watu wote, ingawa alikaza fikira zake juu ya Wayahudi wakati wa huduma yake ya kidunia. (Yohana 1:29; 8:12; Isa. 42:1, 6, 7; Mt. 10:5, 6; 15:24) Yeye alikuwa kama tabibu katika kuwasaidia Wayahudi wote wale waliohitaji zaidi msaada wake, kutia na watenda dhambi kama makahaba, walevi na watoza kodi, ambao mara nyingi walitumia njia za udanganyifu. Mathayo Lawi, mtoza kodi mwenye kudharauliwa, ni mmoja wa watu walioukubali ujumbe mpya wa wokovu ulioletwa na Yesu. Mathayo alimkaribisha Yesu aje nyumbani kwake kula karamu, na hivyo Mathayo na watoza kodi wengine wenye kupendezwa wakapata nafasi ya kuzisikia kweli nyingine mpya zilizokuwa nzuri sana. (Luka 5:27-32; 19:1-10) Hao ni watu waliokuwa ‘wametenda dhambi za kutokujua,’ lakini wakawa na utayari wa kuchukua hatua za ‘kufutiwa dhambi zao.’​—Matendo 3:19; Ebr. 9:7.

      18. Kwa sababu gani kushughulika kwa Yesu pamoja na watoza kodi fulani hakukuwa ndicho kielelezo kinachopasa kufuatwa ili kutenda kulingana na maneno yake katika Mathayo 18:17?

      18 Walakini, jitihada ya Yesu ya kuwapa ushuhuda watoza kodi ambao ‘walimkaribia wamsikilize’ na ‘kumfuata’ haikuwa kielelezo chenye kuonyesha jinsi watenda dhambi wasiotubu walivyopaswa kutendewa. (Marko 2:15; Luka 15:1) Tunawezaje kuwa na uhakika wa jambo hilo? Ingawa Kristo alikula na watoza kodi hao, mtume Paulo aliagiza kwamba Wakristo ‘hata wasile pamoja na’ mtenda dhambi aliyeondolewa awe nje ya kundi. (1 Kor. 5:11) Vilevile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake wamtendee mkosaji asiyetubu kama vile kwa kufaa wao waliwaona watoza kodi wa wakati huo. Tafsiri ya R. F. Weymouth inasema hivi: “Mchukue huyo sawasawa na vile wewe unavyomchukua Mtaifa au mkusanyaji-kodi.”​—Linganisha New International Version; The New English Bible.

      WATU WA MATAIFA YALE MENGINE WALIONWAJE NA WALITENDEWAJE?

      19. Biblia inaonyesha uhusiano kati ya Wayahudi na watu wasio Wayahudi ulikuwa namna gani?

      19 Mitume walioyasikia maneno ya Yesu yaliyoandikwa kwenye Mathayo 18:17 walikuwa Wayahudi na walijua kwamba wananchi wenzao hawakushirikiana kirafiki na watu wa Mataifa yale mengine. Torati iliwatofautisha Wayahudi na Mataifa yale mengine, nayo hiyo ikawa njia ya kutenganisha Waisraeli na mataifa yaliyowazunguka. (Kum. 7:1-4; Hes. 15:37-41; Efe. 2:11-14) Kwenye Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka wa 33 W.K. Wayahudi walikataa kuingia katika jumba la gavana Mrumi “wasije wakanajisika” (wakachafuka). (Yohana 18:28) Nao mtengano uliokuwa kati ya Wayahudi na Wasamaria, ambao hata waliikubali Pentateuko (vitabu vitano vya kwanza vya Biblia), ulikuwa mkubwa sana hata mwanamke mmoja aliyekuwa kisimani katika Samaria akaonyesha mshangao wa kwamba Yesu alimwomba maji ‘ajapokuwa ni Myahudi.’​—Yohana 4:9, NW.

      20. Tunaweza kujifunza jambo gani kutokana na yaliyotendeka kati ya Petro na Kornelio ili tujue jinsi Wayahudi walivyoshughulika na watu wa mataifa.

      20 Tena, katika mwaka wa 36 W.K., wakati Mungu alipokusudia kuonyesha kwamba wakati huo Mataifa wasiotahiriwa wangeweza kukubaliwa wawe warithi wa ule Ufalme, yeye alimwelekeza mtume Petro kwa yule afisa Mrumi wa kijeshi Kornelio. Lakini Petro akamwambia Kornelio: “Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine.” (Matendo 10:28) Maneno ya Petro yanaonyesha Wayahudi walijisikia sana kwamba hawakupaswa kuchangamana na mtu wa mataifa. Vilevile, wakati ilipojulikana kwamba Petro alikuwa amekwenda kwa Kornelio, Wakristo fulani wa Kiyahudi waliudhika sana kwa sababu Petro ‘aliingia kwa watu wasiotahiriwa akala nao.’ Naam, Wayahudi waliliona kuwa jambo la kushtua kuwa pamoja na ‘mtu wa mataifa.’​—Matendo 11:1-3; linganisha Wagalatia 2:12.

      21. Basi, wewe unayaelewaje maneno aliyoyasema Yesu kwamba mtenda dhambi asiyetubu awe “kama mtu tu wa mataifa na kama mtoza kodi”?

      21 Kwa njia hiyo Maandiko yanatusaidia tuelewe maana ya maoni ya Yesu yanayosema tumtendee mkosaji asiyetubu aliyekataa kulisikiliza kundi “kama mtu tu wa mataifa na kama mtoza kodi.” Kutumia shauri hilo la Kristo siku hizi bila shaka kusingemaanisha kumwona mkosaji kama mtu wa kawaida tu mtaani (katika jamii ya watu), kwa maana hivyo sivyo wanafunzi wa Yesu walivyoyaelewa maneno yake. Tunaweza kulifahamu vizuri zaidi jambo hili kwa kuchunguza mashauri zaidi katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, ambayo yatatusaidia tushughulike na hali za kweli zinazotokea katika maisha ya siku hizi kuhusiana na watu walioondoshwa katika kundi la Kikristo.

  • Kutenga na Ushirika—Jinsi Kunavyopasa Kuonwa
    Mnara wa Mlinzi—1982 | Januari 1
    • Kutenga na Ushirika​—Jinsi Kunavyopasa Kuonwa

      “Ee Yehova, . . . ni nani atakayekaa katika mlima mtakatifu wako? Yeye anayetembea bila kosa na kuzoea haki.”​—Zab. 15:1, 2, NW.

      1, 2. Tunajuaje kwamba Mungu anawatazamia wanaomwabudu watetee kanuni zake?

      YEHOVA ni mwenye haki na mtakatifu. Ingawa yeye anawaonyesha wanadamu rehema na ufahamu (huruma), anawatazamia wale wanaomwabudu wauonyeshe utakatifu wake kwa kujaribu kuzitetea kanuni zake za haki.​—Zab. 103:8-14; Hes. 15:40.

      2 Mwisraeli aliyevunja amri za Mungu kwa makusudi, kama zile zilizokataza kuasi imani, uzinzi au kuua, alipaswa akatiliwe mbali, auawe. (Hes. 15:30, 31; 35:31; Kum. 13:1-5; Law. 20:10) Uthabiti huo katika kuzitetea kanuni za Mungu zenye kiasi na haki ya hukumu uliwafaidi Waisraeli wote, kwa maana ulisaidia kuendeleza utakato (usafi) wa kundi. Tena ulisaidia kuzuia mtu ye yote asieneze uchafuzi kati ya watu wa Mungu waliokuwa wakiitwa kwa jina la Mungu.

      3. Hali ya Myahudi mwenye kuondoshwa sinagogini ilikuwa nini?

      3 Katika karne ya kwanza W.K. Wayahudi waliokuwa chini ya utawala wa Kirumi hawakuwa na mamlaka ya kutolea mtu adhabu ya kifo. (Yohana 18:28-31) Lakini Myahudi mwenye hatia ya kuivunja Torati angeweza kuondoshwa katika sinagogi. Matokeo ya adhabu kali hiyo yalikuwa kwamba Wayahudi wale wengine walikuwa wakimwepuka mtu huyo aliyeondoshwa. Inasemwa kwamba wengine hata walikataa kushughulika naye katika mambo ya kibiashara, wakamwuzia vitu vile tu vilivyokuwa vya lazima kwa maisha.a—Yohana 9:22; 12:42; 16:2.

      4, 5. Ililipasa kundi la Kikristo lishughulikeje na mtenda dhambi asiyetubu?

      4 Baada ya kundi la Kikristo kufanyizwa, lilichukua nafasi ya taifa la Kiyahudi kwa kuitwa kwa jina la Mungu. (Mt. 21:43; Matendo 15:14) Kwa hiyo, Wakristo wangeweza kutazamiwa kwa kufaa waitetee haki ya Yehova. Mtume Petro aliandika

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki