Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb10 kur. 66-125
  • Uganda

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uganda
  • 2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • “LULU YA AFRIKA”
  • WATU WA UGANDA WENYE URAFIKI
  • MAPAINIA WA KWANZA
  • KAZI YA KUHUBIRI YAANZA TENA
  • KUTUMIKIA MAHALI PENYE UHITAJI MKUBWA
  • WALIJINYIMA MENGI NAO WAKAPATA BARAKA
  • WAMISHONARI WAFANYA KAZI MUHIMU
  • MAMBO YAFANYWA KWA UTARATIBU
  • KUWASAIDIA WAHUBIRI WAPYA
  • WAANGALIZI WANAOSAFIRI WACHANGIA UKUZI WA KIROHO
  • YEHOVA AKUZA
  • “UTAWALA WA KIMUNGU” AU WA MWANADAMU?
  • “MAJIRA YENYE TAABU”
  • ‘IMARA NA THABITI’
  • KUKUTANIKA KWA SHANGWE
  • ‘WENYE KUJIHADHARI KAMA NYOKA HATA HIVYO WASIO NA HATIA KAMA NJIWA’
  • MAPAINIA WENYE KUSTAHIMILI
  • “NDUGU ALIYEZALIWA KWA AJILI YA WAKATI WA TAABU”
  • “HATA IKIWA WATANIUA, NITAENDA”
  • NYAKATI HATARI
  • FURSA NA MATATIZO MAPYA
  • WAMISHONARI WAKARIBISHWA TENA
  • WENYE UMRI MKUBWA WATAKA KUFANYA MENGI ZAIDI
  • “MTU HUSEMAJE . . . ?”
  • KAZI YA UKUSANYAJI YATIA FORA
  • KUVUNA ENEO KUBWA ZAIDI
  • KUSHINDA VIPINGAMIZI
  • KAZI YA KUTAFSIRI YAHARAKISHA UKUSANYAJI WA WATU
  • SEHEMU ZAIDI ZA IBADA ZAHITAJIWA
  • KUSHUGHULIKIA ONGEZEKO LA HARAKA
  • “SASA TUKO PARADISO”
  • UJUZI WA KWELI WAONGEZEKA
2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb10 kur. 66-125

Uganda

KWA miaka mingi, wavumbuzi walitafuta chanzo cha Mto Nile, ambao hupinda-pinda sehemu kubwa ya Afrika na kumimina maji yake katika Bahari ya Mediterania. Hatimaye, wavumbuzi fulani waliangazia Ziwa Victoria na milima iliyo karibu nalo kuwa chanzo kikuu cha maji ya Mto Nile. Katika miaka ya karibuni, watu wengi katika eneo hilo wamefurahi kugundua chanzo cha maji yenye thamani zaidi—“maji yaliyo hai” ya “uzima wa milele.” (Yoh. 4:10-14) Haya ni masimulizi ya watu wa Uganda wenye “kiu kwa ajili ya uadilifu.”—Mt. 5:6.

“LULU YA AFRIKA”

Uganda ni nchi yenye kupendeza iliyo kwenye ikweta barani Afrika. Nchi hiyo ina hali nzuri ya anga. Mito na maziwa mengi hupata maji safi kutoka kwenye milima yenye barafu ya Ruwenzori, inayoitwa Milima ya Mwezi. Kwa sababu ya udongo wake wenye rutuba na mvua nyingi nchi hiyo huzalisha kahawa, majani chai, na pamba. Ndizi huzalishwa kwa wingi, nazo hutumiwa kutayarisha matooke, mojawapo ya vyakula vikuu vya Uganda. Mihogo, mahindi, ulezi, na mawele huliwa pia.

Wanyama kama vile simba, ndovu, kiboko, mamba, chui, twiga, paa, na pia sokwe walio katika hatari ya kutoweka, hali kadhalika tumbili wa aina mbalimbali hupatikana nchini humo. Kuna ndege wengi maridadi wenye sauti tamu. Kuna mengi ya kuvutia nchini Uganda hivi kwamba nchi hiyo inaitwa “lulu ya Afrika.”

WATU WA UGANDA WENYE URAFIKI

Uganda ina watu milioni 30 hivi kutoka katika makabila 30 hivi. Wengi wanapenda dini nao ni wafuasi wa makanisa mbalimbali; hata hivyo, kama ilivyo kwingineko, ibada yao hutia ndani pia mazoea ya dini za kitamaduni. Kwa kawaida wenyeji wa Uganda ni wenye urafiki na wakarimu, nao hupenda kupiga magoti wanapomsalimu au kumhudumia mtu mwenye umri mkubwa.

Hata hivyo, inasikitisha kwamba katika miaka ya 1970 na 1980, misukosuko ya kisiasa na vifo vya maelfu ya watu viliathiri sana “lulu” hiyo pamoja na watu wake. Isitoshe, ugonjwa wa UKIMWI umezidisha matatizo nchini Uganda. Katika hali kama hizo, Mashahidi wa Yehova wamewafariji na kuwapa tumaini watu hao ambao wamevumilia mengi maishani.

MAPAINIA WA KWANZA

Ujumbe wa Ufalme ulifika nchini Uganda kwa mara ya kwanza mwaka wa 1931, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ilipokuwa ikisimamia kazi ya kuhubiri katika eneo lote kusini mwa ikweta. Ofisi ya tawi ilituma mapainia wawili, Robert Nisbet na David Norman, kuhubiri eneo hilo kubwa ambalo leo ni Kenya, Uganda, na Tanzania.

Ndugu hao waliazimia kuhubiri habari njema ya Ufalme mpaka vijijini. Walianza kampeni yao Dar es Salaam mnamo Agosti 31, 1931 wakiwa na katoni 200 za vitabu. Kisha wakaelekea Zanzibar na baadaye bandari ya Mombasa, wakiwa njiani kuelekea nyanda za juu za Kenya. Walisafiri kwa gari-moshi, wakihubiri katika miji iliyokuwa njiani mpaka walipofika ufuo wa mashariki wa Ziwa Victoria. Kisha mapainia hao wawili wenye ujasiri wakaabiri meli na kusafiri hadi Kampala, mji mkuu wa Uganda. Baada ya kugawa vitabu na magazeti mengi, na pia kupata maandikisho ya gazeti la The Golden Age, ndugu hao wawili waliendelea na safari yao kwa gari mpaka ndani zaidi nchini.

Miaka minne baadaye, mwaka wa 1935, mapainia wengine wanne kutoka Afrika Kusini walifunga safari ya kuja Afrika Mashariki. Mapainia hao ni Gray Smith na mke wake, Olga, pamoja na Robert Nisbet na ndugu yake mdogo, George. Wakiwa na magari mawili makubwa ambayo yangeweza kutumiwa kama makao, mapainia hao wajasiri walipitia barabara mbovu na vichakani. “Mara nyingi walilala msituni,” yasema ripoti moja, “wakapata kionjo halisi cha Afrika na kuishi pamoja na wanyama-mwitu. Waliwasikia simba wakinguruma usiku, punda-milia na twiga wakilisha kwa utulivu, hali kadhalika wanyama wakubwa kama vifaru na tembo.” Yote hayo hayakuwazuia kutembelea miji mbalimbali ambayo kamwe haikuwa imepata ujumbe wa Ufalme.

Gray na Olga Smith waliamua kukaa Tanganyika (ambako leo ni Tanzania), naye Robert na George Nisbet wakaelekea Nairobi, Kenya. Baadaye, serikali ya kikoloni ilipomwamuru Ndugu na Dada Smith waondoke Tanganyika, walifunga safari hadi Kampala, Uganda. Hata hivyo wakati huo hali haikuwa nzuri, nao polisi mjini Kampala walikuwa wakifuatia nyendo zao. Licha ya hayo, kwa muda wa miezi miwili tu, Ndugu na Dada Smith waligawa vitabu na vijitabu 2,122 na kufanya mikutano ya watu wote mara sita. Hata hivyo, baadaye gavana akatoa amri ya kuwafukuza nchini nao wakalazimika kuondoka Uganda. Walisafiri hadi Nairobi ambako walikutana na kina Nisbet kabla ya kurudi Afrika Kusini.

Yehova alibariki kampeni hizo za pekee za kuhubiri na ushahidi mzuri ukatolewa. Licha ya upinzani wa kidini na mkazo mwingi kutoka kwa wenye mamlaka, mapainia hao waligawa vitabu zaidi ya 3,000 na vijitabu zaidi ya 7,000, pamoja na maandikisho mengi. Baada ya kampeni hizo, miaka mingi ilipita kabla ya nchi ya Uganda kuhubiriwa tena.

KAZI YA KUHUBIRI YAANZA TENA

Aprili 1950, Ndugu na Dada Kilminster kutoka Uingereza, walihamia Kampala. Walihubiri habari njema kwa bidii. Walifurahi sana familia mbili, moja ya Kigiriki na nyingine ya Kiitaliano, zilipokubali ujumbe wa Ufalme.

Kisha, Desemba 1952, Ndugu Knorr na Ndugu Henschel kutoka katika makao makuu ya Mashahidi wa Yehova mjini New York, wakazuru Nairobi, Kenya. Kwa kuwa Ndugu Kilminster hakutaka kukosa fursa ya kukutana nao, alisafiri kutoka Kampala hadi Nairobi. Ndugu Knorr na Ndugu Henschel waliwatia moyo ndugu hao na kupanga kutaniko lianzishwe Kampala. Muda usio mrefu baadaye, kutaniko hilo jipya lilianza kuzaa matunda, na kufikia mwaka wa utumishi wa 1954 kulikuwa na wahubiri kumi.

Mwaka huohuo, Eric Cooke, kutoka ofisi ya tawi ya Rhodesia ya Kusini (ambako leo ni Zimbabwe), alizuru Afrika Mashariki na kushirikiana kwa muda na kutaniko hilo jipya mjini Kampala. Ijapokuwa akina ndugu walikuwa na mkutano wa funzo la Mnara wa Mlinzi kila juma, hawakuwa wa kawaida sana katika huduma ya Kikristo. Hivyo, Ndugu Cooke alimtia moyo Ndugu Kilminster wawe na mikutano yote ya kutaniko, kutia ndani Mkutano wa Utumishi kila juma. Ili kuitimiza kikamili zaidi kazi ya kuhubiri, Ndugu Cooke alikazia huduma ya nyumba kwa nyumba na kuwazoeza wahubiri kadhaa jinsi ya kufanya hivyo.

Kufikia wakati huo, waliokuwa wakihubiriwa hasa ni Wazungu waliokuwa wakiishi Uganda. Hata hivyo, Ndugu Cooke alitambua kwamba watu wengi waliokuwa wakiishi Kampala walikuwa wakizungumza Kiganda. Alipendekeza kwamba ili kuchochea mioyo ya watu hao, ndugu wanahitaji kutafsiri angalau kitabu kimoja katika lugha ya Kiganda. Mwaka wa 1958 wahubiri wakaanza kutumia kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme” kilichokuwa kimetafsiriwa karibuni. Hilo lilikuwa jambo lenye kutia moyo kama nini! Kazi ilisonga mbele na katika mwaka wa 1961, kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 19.

Akiwa katika kazi yake ya kimwili, Ndugu Kilminster alikutana na George Kadu, mtu wa makamo na mwenye shauku, anayejua Kiingereza na Kiganda. George alivutiwa na kweli ya Biblia alipopata kujua kwamba jina la Mungu ni Yehova, naye akaanza kujifunza. Muda si muda akaanza kuambatana na Ndugu Kilminster nyumba kwa nyumba akitafsiri mahubiri yake. Kisha, mwaka wa 1956, ubatizo wa kwanza nchini Uganda ulipofanywa katika Ziwa Victoria karibu na Entebbe, George akabatizwa.

Hata hivyo, muda usio mrefu baadaye, kazi ya Ufalme ikapata pigo. Baadhi ya ndugu kutoka nchi za kigeni walirudi makwao baada ya kandarasi zao kwisha. Ndugu kadhaa walitengwa na ushirika, na wengine wakakwazwa na mienendo isiyopatana na Maandiko ya watu fulani kutanikoni. Hata hivyo, Ndugu Kadu alimpenda Yehova naye alijua kwamba ameipata kweli. ‘Katika majira yanayofaa na yenye taabu’ aliendelea kuwa mshikamanifu na kutumikia kwa uaminifu akiwa mzee wa kutaniko mpaka mwaka wa 1998, alipokufa.—2 Tim. 4:2.

KUTUMIKIA MAHALI PENYE UHITAJI MKUBWA

Shamba la Afrika Mashariki lilikuwa kubwa, na kulikuwa na uhitaji mkubwa wa wahubiri wa Ufalme. Kwa upande mwingine, serikali ya kikoloni haikuwaruhusu wamishonari kuingia nchini. Hali hiyo ingetatuliwaje?

Mwaka wa 1957 mwito ulitolewa ulimwenguni pote kwa wahubiri kutumikia mahali penye uhitaji mkubwa. Ndugu wakomavu kiroho walitiwa moyo kuhamia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa wahubiri wa Ufalme. Mwito huo ulikuwa sawa na ule wa Paulo katika maono, mwanamume fulani alipomsihi: “Vuka uingie Makedonia utusaidie.” (Mdo. 16:9, 10) Mwito huo ulikuwa na matokeo gani nchini Uganda?

Frank na Mary Smith walionyesha roho ya Isaya kwa kuukubali mara moja mwito huo na kuanza kufanya mipango ya kuhamia Afrika Mashariki.a (Isa. 6:8) Julai 1959 waliabiri meli kutoka New York kupitia Cape Town hadi Mombasa. Kisha wakasafiri kwa gari-moshi kwenda Kampala, ambapo Frank alipata kandarasi katika idara ya usoroveya ya serikali. Waliishi Entebbe, kilomita 35 hivi kusini mwa Kampala. Mji huo maridadi ulio kando ya Ziwa Victoria, haukuwa umehubiriwa hata kidogo. Ndugu na Dada Smith walikuwa wakihudhuria mikutano mjini Kampala katika kutaniko dogo lakini lenye ongezeko.

Muda mfupi baadaye, akina Smith walimhubiria Peter Gyabi, aliyekuwa na cheo katika serikali ya Uganda, pamoja na mke wake, Esther. Awali, Peter alikuwa amepata kitabu What Has Religion Done for Mankind?b lakini hakukisoma kwa makini kwa sababu ya shughuli zake nyingi kazini na kuhamishwa-hamishwa kikazi. Kisha, siku moja Peter alitumwa kutatua mzozo wa shamba kati ya makabila mawili. Alisali, “Mungu, iwapo utanisaidia, nitakutafuta.” Utatuzi ulipopatikana kwa amani, alikumbuka sala yake, naye akaanza kukisoma kile kitabu. Alitambua mambo aliyokuwa akijifunza ni kweli naye akaanza kuwatafuta Mashahidi. Alifurahi sana alipokutana na Frank Smith, aliyekubali kumfundisha yeye na mke wake Biblia kwa ukawaida! Wenzi hao wa ndoa wenye furaha walibatizwa, nao bado ni wahubiri wenye bidii wa Ufalme, zaidi ya miaka 40 baadaye.

Ndugu wengine pia kutoka nchi za kigeni walikubali mwito wa kutumikia katika nchi zenye uhitaji mkubwa. Baadhi yao walipata kandarasi zilizowapeleka mbali na kile kikundi kidogo cha wahubiri kilichokuwa Kampala. Ndugu mmoja na mke wake waliishi Mbarara, mji mdogo ulio katika sehemu yenye milima-milima upande wa kusini magharibi, kilomita 300 hivi kutoka Kampala. Walikuwa wakifanya Funzo la Mnara wa Mlinzi na funzo la kitabu katika nyumba yao. Hata hivyo, mara kwa mara walifunga safari ndefu ya kwenda Kampala au Entebbe ili kufurahia ushirika wa Kikristo. Pia waliendelea kuwasiliana na ofisi ya tawi ya Luanshya, Rhodesia ya Kaskazini (ambako leo ni Zambia), iliyokuwa ikisimamia kazi ya kuhubiri Ufalme katika eneo la Afrika Mashariki. Harry Arnott, aliyekuwa mwangalizi wa ofisi hiyo ya tawi, alitembelea Kampala akiwa mwangalizi wa eneo la dunia na kuwatia moyo wahubiri wachache waliokuwamo nchini Uganda. Wahubiri hao walithamini sana jinsi alivyowahangaikia kwa upendo.

Wengine waliotamani sana kutumikia mahali penye uhitaji mkubwa wa wahubiri wa Ufalme ni Tom na Anne Cooke kutoka Uingereza. Tom alituma maombi ya kazi katika nchi kadhaa naye akaajiriwa kuwa ofisa wa elimu katika Wizara ya Elimu ya Uganda. Mwanzoni, yeye, mke wake Ann, na binti yao, Sara, mwenye umri wa miaka minne walikaa Iganga, mji mdogo ulio kilomita 130 hivi upande wa mashariki wa Kampala. Baada ya kuzaliwa kwa Rachel, binti yao wa pili, Tom na familia yake walihamia Jinja, karibu na chanzo cha Mto Nile. Baadaye, wakahamia Kampala.

WALIJINYIMA MENGI NAO WAKAPATA BARAKA

Familia hizo zilichangia pakubwa kazi ya kuhubiri Ufalme nchini Uganda. Ni kweli kwamba walikuwa wameacha maisha na starehe walizokuwa wamezoea. Hata hivyo, walipata shangwe ya kuona watu wanyenyekevu wakibadili maisha yao na kuikubali habari njema ya Ufalme. Pia walipata marafiki wapya walipokusanyika kwa ajili ya ibada au ushirika na familia nyingine za Kikristo.

Tom Cooke anasema: “Tulivutiwa na heshima na unyenyekevu wa watu tuliowahubiria. Tuliliona kuwa pendeleo la pekee kuchangia ukuzi wa kutaniko angaa kwa kiasi kidogo.”

Alipoulizwa maoni yake kuhusu kuhama kwao, Tom anasema: “Tulikuwa katika mazingira bora zaidi ya kumtumikia Yehova tukiwa na watoto wetu wachanga. Kulikuwa na ndugu na dada kutoka nchi nyingi, ndugu wenyeji washikamanifu na wenye upendo, mapendeleo mengi ya utumishi, na mandhari zenye kupendeza za bara Afrika. Pia, tuliepuka uvutano wa televisheni. Hizo ni baadhi tu ya baraka tulizopata.”

Wale waliokuwa wakitumikia mahali penye uhitaji mkubwa walithamini sana ushirika wa Kikristo. Hilo lilionekana wazi kutokana na utayari wao wa kusafiri hadi Kenya, umbali wa kilomita 750, ili kuhudhuria makusanyiko ya mzunguko!

Makusanyiko ya Wilaya yalikuwa mbali hata zaidi. Kwa mfano, mwaka wa 1961, wajumbe kutoka Uganda na Kenya walihudhuria kusanyiko la wilaya mjini Kitwe, Rhodesia ya Kaskazini (Zambia). “Hiyo ilikuwa safari ya siku nne, kilomita 1,600 kwenye barabara mbovu za Tanganyika (Tanzania),” akumbuka mmoja wa wajumbe, “kisha safari nyingine ya siku nne, kupitia nyanda za Afrika zenye joto kali na vumbi, ya kurudi Uganda. Safari hiyo ilikuwa na panda-shuka nyingi, hata hiyo, ushirika wa ndugu na dada wengi hivyo ulikuwa baraka kwelikweli.” Ijapokuwa ilikuwa safari ndefu na yenye kuchosha sana iliyohitaji moyo mkuu, ilikuwa yenye kuburudisha kiroho kama nini!

WAMISHONARI WAFANYA KAZI MUHIMU

Mwaka wa 1962, nchi ya Uganda ilipata uhuru kutoka kwa serikali ya Uingereza. Mwaka uliofuata Ndugu Henschel alizuru Nairobi, Kenya, na kuzungumzia uwezekano wa kutuma wamishonari nchini Uganda. Ni nani wangepata mgawo huo?

Tom na Bethel McLain, wa darasa la 37 la Gileadi, walikuwa wamewasili kutumikia Nairobi. Walishangaa kupata mgawo wa kwenda Kampala! Hata hivyo, waliukubali mgawo huo nao wakawa wamishonari wa kwanza kutoka Gileadi kutumikia nchini Uganda. Tom anasema: “Mwanzoni tulitamani kurudi Kenya, lakini baada ya muda tuliipenda Uganda sana. Kulikuwa na watu wenye urafiki na waliokuwa tayari kusikiliza ujumbe wetu.”

Tom na Bethel walikuwa wameanza kujifunza Kiswahili nchini Kenya, lakini sasa walihitaji kujifunza lugha mpya—Kiganda. Hawakuwa na mwalimu. Walichokuwa nacho ni azimio lao, tegemeo lao kwa Yehova, na kitabu cha kujifunza wenyewe. Katika miezi ya kwanza nchini Uganda, mbali na saa 100 walizotumia katika huduma ya shambani, walitumia saa 250 kujifunza lugha hiyo mpya mwezi wa kwanza, na saa 150 mwezi wa pili. Hatua kwa hatua wakaijua lugha hiyo na kufurahia matokeo mazuri katika utumishi wa shambani.

Januari 1964, Gilbert na Joan Walters wa darasa la 38 la Gileadi walijiunga na Tom na Bethel. Wanafunzi wengine wa darasa hilohilo, Stephen na Barbara Hardy na Ron na Jenny Bicknell, walikuwa wametumwa Burundi, lakini kwa sababu hawakupata vibali vya kuingia nchini humo, wao pia wakatumwa Uganda. Makao mapya ya wamishonari mjini Kampala yalihitajiwa haraka!

Kutaniko la awali la Kampala haliwezi kamwe kusahaulika. Lilikuwa na Ndugu Kadu na familia yake; John na Eunice Bwali, mapainia wa pekee kutoka Rhodesia ya Kaskazini, na watoto wao; na Margaret Nyende na watoto wake. Hawakuwa na mahali pazuri pa kukutania. “Wapita-njia wangeweza kutuona na kutusikia, ingawa tulikuwa wachache,” akumbuka Gilbert Walters. “Familia ya Bwali iliimba kwa sauti nyimbo za Ufalme bila kinanda chochote, bila kuwaogopa wapita-njia. Hilo lilitupa ujasiri kuendelea.”

Baadaye, Gilbert na Joan Walters walipewa mgawo wa kuhamia Jinja, ambako kazi ya kuhubiri haikuwa imefanywa vizuri. Wamishonari wengine walitumwa Mbale, karibu na mpaka wa Kenya, na wengine wakatumwa Mbarara. Wamishonari wote hao walifanya kazi bega kwa bega na mapainia wa pekee waliokuwa wamekuja kutoka nchi nyingine. Ni wazi kwamba mashamba yalikuwa “meupe kwa ajili ya kuvunwa.” (Yoh. 4:35) Hivyo basi, ni nini kingeweza kufanywa ili kuharakisha kazi ya kuvuna?

MAMBO YAFANYWA KWA UTARATIBU

Watumishi wa wakati wote nchini Uganda walijitahidi kuhubiri eneo lao kubwa kwa mpangilio mzuri. Katikati ya juma, walikuwa wakihubiri mitaa yenye nyumba zenye mpangilio mzuri. Hata hivyo, vipi maeneo ambayo hayakuwa na mitaa yenye majina wala nyumba zenye nambari?

“Tuligawa maeneo hayo kulingana na vilima,” aeleza Tom McLain. “Wawili walihubiri upande mmoja wa kilima, huku wengine wawili wakihubiri upande wa pili. Tulifuata vijia, tukihubiri mpaka sote wanne tulipokutana.”

Baada ya muda, ndugu wa kigeni walianza kufaidika kutokana na ongezeko miongoni mwa wenyeji ambao walilifahamu vizuri eneo na utamaduni. Nao wenyeji walipata uzoefu. Kwa mfano, huko Jinja, tayari ndugu wenyeji walikuwa wakihubiri pamoja na wamishonari. Jumapili walikuwa wakihubiri nyumba kwa nyumba kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa nne. Kisha, ziara za kurudia kwa saa moja na kuongoza funzo la Biblia mpaka saa sita. Kwa kufanya hivyo, wote kutanikoni walifaidika kutokana na uzoefu wa kila mmoja na kutiana moyo.

Kwa kuwa Jinja, mji wa pili kwa ukubwa nchini, una kituo cha kuzalishia umeme, ni eneo lenye viwanda vingi. Wamishonari walipata matokeo mazuri kwa kuhubiri katika vituo vya magari ya umma. Wasafiri kutoka mbali walikubali magazeti na vitabu vya Biblia ambavyo walivisoma wakiwa safarini. Hivyo, mbegu ya Ufalme ilienezwa hadi vijijini.

Pia, ndugu walitumia redio kutangaza habari njema kwa watu wengi iwezekanavyo. Walipewa nafasi ya kila juma katika idhaa ya taifa ya kipindi kinachoitwa “Mambo Ambayo Watu Wanafikiria.” Akina ndugu walizungumzia habari zenye kusisimua kama vile “Kukabili Matatizo ya Familia” na “Jinsi ya Kujilinda Kutokana na Uhalifu na Jeuri,” kwa njia ya mjadala kati ya “Bwana Robbins” na “Bwana Lee.” Ndugu mmoja akumbuka: “Ilikuwa ajabu kusikiliza kipindi cha mazungumzo kati ya Mmarekani na Mskoti katika redio barani Afrika. Bila shaka, kipindi hicho kilitimiza mengi kwa sababu mara nyingi tulipokuwa katika huduma ya shambani watu walituambia jinsi wanavyokifurahia.”

KUWASAIDIA WAHUBIRI WAPYA

Wakati huo kikundi cha Jinja kilikuwa kikifanyia mikutano yao katika jumba la umma katika mtaa wa Walukuba. “Ndugu wengi walikuwa wapya,” akumbuka Tom Cooke, “nao walikuwa na vichapo vichache ambavyo wangeweza kutumia kutayarishia migawo yao.” Msaada ungetoka wapi?

“Wamishonari waliweka maktaba katika nyumba ya ndugu mmoja aliyekuwa akiishi katikati ya mtaa huo,” asema Tom. “Kila Jumatatu (Siku ya 1) usiku, waliokuwa na migawo walienda kwa ndugu huyo kutumia maktaba ili kutayarisha hotuba zao.” Leo, kuna makutaniko mengi Jinja yanayoendelea na kazi ya uvuvi wa kiroho katika eneo hilo ambalo ni chanzo cha Mto Nile.

WAANGALIZI WANAOSAFIRI WACHANGIA UKUZI WA KIROHO

Mnamo Septemba 1963, kazi ya kuhubiri nchini Uganda ilianza kusimamiwa na ofisi ya tawi ya Kenya iliyokuwa imeanzishwa karibuni, nao William na Muriel Nisbet wakapewa mgawo wa kutembelea Uganda, iliyokuwa sehemu ya mzunguko wao uliotia ndani Nairobi. William alikuwa anafuata hatua za kaka zake, Robert na George, ambao walikuwa wamehubiri Uganda miaka 30 mapema. Sasa, wahubiri walikuwa wakifaidika kutokana na bidii ya “kikosi cha pili” cha kina Nisbet.

Watu wengi zaidi walianza kupendezwa, vikundi vingi vikaanzishwa, nao wahubiri wakaenea. Hivyo, ziara za mara kwa mara za waangalizi wanaosafiri ziliwasaidia wengi kupata mazoezi na kitia-moyo na kuwahakikishia ndugu na dada waliokuwa maeneo hayo ya mbali kwamba “macho ya Yehova yako juu ya waadilifu.”—1 Pet. 3:12.

Mwaka wa 1965, Stephen na Barbara Hardy walikuwa na mzunguko ulioanzia Uganda hadi Ushelisheli, visiwa vilivyo umbali wa kilomita 2,600 katika Bahari ya Hindi. Pindi moja, walizuru sehemu mbalimbali za Uganda kuona ni wapi ambapo mapainia wangeweza kupata matokeo. Wakitumia gari aina ya Volkswagen Kombi la ofisi ya tawi ya Kenya walilotumia pia kama makao yao, walizuru sehemu nyingi za Uganda kama vile Masaka, Mbarara, Kabale, Masindi, Hoima, Fort Portal, Arua, Gulu, Lira, na Soroti, kwa muda wa majuma sita tu.

“Safari hiyo ilikuwa yenye kusisimua,” akumbuka Ndugu Hardy, “nayo kazi ya kuhubiri ilifurahisha kwelikweli.” Wote, kutia ndani wenye mamlaka, walikuwa tayari kusaidia na walikuwa wenye urafiki. Mara nyingi tulipofika boma fulani, muda si muda tulijikuta tukitoa ‘hotuba ya watu wote’ kwa kuwa majirani na wapita-njia walikuja kusikiliza. Hata tuliposimama katika eneo lisilo na watu wengi, watu walitujia wakitabasamu, wakiamini kwamba sisi ni wageni wao. Vichapo vyetu viliisha haraka. Tuligawa vitabu 500 hivi na kupata maandikisho mengi ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni!

Kwa kuwa wenyeji walikuwa wenye urafiki, wadadisi, na wanaopenda mambo ya kiroho, ilionekana wazi kwamba wengi wana njaa ya kiroho. Isitoshe, Yehova alibariki kazi ya Ndugu na Dada Hardy katika eneo hilo lenye rutuba.

YEHOVA AKUZA

Hatua kubwa ilipigwa katika historia ya watu wa Yehova nchini Uganda mnamo Agosti 12, 1965, shirika la International Bible Students Association liliposajiliwa, na hivyo kuhalalisha kazi yetu ya kufanya wanafunzi. Wakati huo kulikuwa na kikundi kidogo cha wenyeji wenye moyo mnyoofu kama vile George Mayende, Peter na Esther Gyabi, na Ida Ssali, ambacho kilikuwa msingi wa kutaniko katika miaka hiyo ya 1960. Kufikia mwaka wa 1969, kulikuwa na wahubiri 75 waliotapakaa kotekote nchini Uganda kati ya watu milioni nane hivi, kukiwa na uwiano wa Shahidi mmoja kwa watu zaidi ya laki moja. Kufikia 1970, idadi ya watangazaji wa Ufalme iliongezeka hadi 97, kisha 128 katika mwaka wa 1971. Mwaka wa 1972, kulikuwa na Mashahidi watendaji 162 nchini Uganda.

Ijapokuwa ongezeko hilo lilikuwa lenye kutia moyo, akina ndugu hawakujitumaini kupita kiasi, badala yake, walimtumaini “Mungu anayeikuza.” (1 Kor. 3:7) Kile ambacho hawakujua ni kwamba katika miaka ya 1970 kungekuwa na mabadiliko makubwa maishani mwao nayo imani yao ingejaribiwa vikali. Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya dikteta Idi Amin mwaka wa 1971, mamilioni ya watu walitaabika na maelfu kufa. Kulikuwa na vita vya hapa na pale kati ya serikali na vikundi vya waasi. Mara kwa mara mipaka ilifungwa. Pia, kulikuwa na amri za kutotembea usiku. Watu wakaanza kutoweka. Wengine wakaanza kupelelezwa. Ndugu na dada zetu wapenda-amani nchini Uganda wangefanya nini chini ya hali hizo za msukosuko, vitisho, na jeuri?

“UTAWALA WA KIMUNGU” AU WA MWANADAMU?

Wakati huohuo, mipango ilikuwa ikifanywa mjini Kampala kwa ajili ya Kusanyiko la Wilaya la 1972 la “Utawala wa Kimungu,” la kwanza la aina hiyo nchini Uganda. Wajumbe walitazamiwa kuja kutoka Kenya, Tanzania, na hata Ethiopia. Wangekabiliana jinsi gani na hali ya taharuki iliyokuwako, ghasia za kisiasa na kikabila, na masaibu ya kuvuka mipaka? Je, kusanyiko hilo livunjwe? Akina ndugu walisali kwa ajili ya kusanyiko hilo, wakimwomba Yehova aelekeze na kufanikisha mipango ya kusanyiko na pia kwa ajili ya wajumbe.

Baadaye, hali ilionekana kuwa mbaya hata zaidi wajumbe walipofika mpakani na kuona watu wengi wakikimbia kutoka nchini! Wengi wao walikuwa wakiondoka kwa sababu ya amri ya serikali ya kuwafukuza wote wenye asili ya Asia ambao si raia—hasa Wahindi na Wapakistani. Wengine, kama vile walimu kutoka nchi za kigeni, waliondoka kwa kuhofia kwamba vikundi vingine pia vingefukuzwa. Licha ya hayo yote, wajumbe waliendelea kuwasili. Wangepata nini katika mji wenye mchafuko wa kisiasa?

Hata hivyo, kwa kushangaza mji wa Kampala ulikuwa mtulivu, nao ndugu na watu wenye kupendezwa walikuwa kwenye uwanja wa kusanyiko wakiwasubiri na kuwashangilia wajumbe waliokuwa wakiwasili. Pia walishangaa kwamba wenye mamlaka walikuwa wametoa idhini bango kubwa lenye tarehe na mahali pa kusanyiko liwekwe katika barabara kuu mjini Kampala. Wakati huo, kukiwa na msukosuko mkubwa, kichwa cha hotuba ya watu wote chenye maandishi mazito: “Utawala wa Kimungu—Tumaini Pekee la Wanadamu Wote,” kilikuwa kikipepea angani!

Programu ilikuwa shwari, kukiwa na kilele cha wahudhuriaji 937—hatua kubwa katika historia ya ibada ya kweli nchini Uganda. Baadaye, ingawa wajumbe walipata matatizo mipakani walipokuwa wakirudi makwao, bidii yao haikudidimia, na wote wakafika nyumbani salama. Katika mazingira hayo ya mchafuko wa kisiasa, watu wa Yehova walionyesha wazi kwamba wanamtii Mwenye Enzi Kuu. Naye Mungu akawafanya watu wake kuwa ‘wajasiri katika nguvu.’—Zab. 138:3.

George na Gertrude Ochola walikuwa miongoni mwa wenyeji waliohudhuria. Gertrude anasema: “Hilo lilikuwa kusanyiko langu la kwanza, ambapo nilibatizwa!” Lakini George hakuwa Shahidi wakati huo. Alikuwa shabiki wa soka naye alipendezwa zaidi na uwanja wenyewe. Hata hivyo, mwishowe alijiweka wakfu na kubatizwa mwaka wa 1975 nchini Kenya, baada ya kujifunza Biblia na pia kuchochewa na mwenendo mzuri wa mke wake.

Gertrude anakumbuka kwamba alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujifunza kweli kutoka sehemu za kaskazini za Uganda. “Mwaka wa 1972, nilipobatizwa,” asema, “nilidhani kwamba kwetu ni mbali sana. Lakini leo, kuna Jumba la Ufalme, makao ya wamishonari, na hata ofisi ya kutafsiri. Hilo hunisisimua sana kuliko nilipobatizwa!”

“MAJIRA YENYE TAABU”

Bila tahadhari yoyote, mnamo Juni 8, 1973, redio na televisheni zilitangaza kwamba vikundi 12 vya kidini, kutia ndani Mashahidi wa Yehova, vimepigwa marufuku. Serikali ilikuwa imewatia watu hofu na shaka kuhusu watu kutoka nchi za kigeni, ikidai kwamba ni wapelelezi. Ilizidi kuwa vigumu sana kwa wamishonari kuhubiri hadharani. Mashahidi wa Yehova nchini Uganda walikuwa katika kipindi cha “majira yenye taabu.” (2 Tim. 4:2) Ingekuwaje?

Tayari wamishonari wawili na wake zao walikuwa wameondoka mwaka huo kwa sababu maombi yao ya kuongeza muda wa kukaa nchini yalikuwa yamekataliwa. Kufikia katikati ya mwezi wa Julai wamishonari 12 waliobaki wakafukuzwa. Ndugu kutoka nchi za kigeni waliokuwa wamekuja kutumikia mahali penye uhitaji mkubwa walibaki kwa muda kwa sababu ya kazi zao za kimwili, hata hivyo hawakukaa kwa muda mrefu. Mwaka uliofuata, wote wakalazimishwa kuondoka.

‘IMARA NA THABITI’

Wahubiri waliobaki walihuzunishwa sana na kuondoka kwa ndugu na dada zao wapendwa wa nchi za kigeni. Hata hivyo, Yehova aliwapa nguvu za kuwa ‘imara na thabiti.’ (1 Kor. 15:58) Maneno ya ndugu Ernest Wamala yanaonyesha roho ya ushikamanifu ambayo akina ndugu walikuwa nayo. Ndugu huyo mzee alipojulishwa kwamba Mashahidi wamepigwa marufuku, aliuliza: “Watapigaje marufuku yaliyo moyoni mwangu?”

Wazee waliobaki, kama vile George Kadu na Peter Gyabi, wangeshughulikiaje mambo baada ya wageni wote kufukuzwa? Jambo moja lililowasaidia ni hali yao ya kiroho. Pia, walielewa vizuri desturi za kwao. Ndugu Gyabi asema: “Si rahisi kuikubali kweli na kumtumikia Yehova nchini Uganda, kwa kuwa kuna desturi nyingi zisizopatana na kanuni za Yehova. Ndugu wenye mapendeleo walihitaji kushikamana sana na maagizo yote ya tengenezo la Yehova.” Kujifunza vizuri kibinafsi kuliwasaidia wazee wenyeji wasipotoshwe na hekima ya wanadamu. Hivyo basi, kipindi hicho chenye majaribu mengi kiliwasaidia watu wa Yehova kufanya maendeleo kiroho badala ya kurudi nyuma.

Kwa upande mwingine, wengi nje ya kutaniko hawakuwa na utulivu. Wengi walikuwa wakinyanyaswa, hali wengine wakiishi katika woga kwa sababu ya wanajeshi. Uchumi ulikuwa mbovu kwa sababu ya ufisadi uliokuwa umekithiri. Nchi yenye kupendeza ilikuwa hoi. Je, shangwe ya watumishi waaminifu wa Yehova nchini Uganda ingedumu katikati ya majaribu hayo?

KUKUTANIKA KWA SHANGWE

Serikali ilifanya yote iwezayo kuzima mikutano yote ya kisiasa iliyoonwa kuwa tisho. Mashahidi wa Yehova hawakujiingiza katika mambo ya kisiasa, na wakati uleule waliendelea kutii agizo la Biblia la kutoacha kukusanyika pamoja ili kutiana moyo. (Ebr. 10:24, 25) Walihitaji ujasiri na busara ili kuendelea kukutanika pamoja chini ya upelelezi mkali wa wenye mamlaka waliokuwa wakiwashuku. Watumishi wa Mungu wangeendelea jinsi gani kufanya mikutano yao katika hali hizo?

Kwanza, walipanga mikutano iwe ikifanywa katika vikundi vidogo-vidogo katika nyumba za kina ndugu. Walipokusanyika wengi pamoja, walifanya ionekane kana kwamba ni mandari. Kwa mfano, mara moja kila mwezi kutaniko zima lilikutana pamoja kwa ajili ya hotuba na Funzo la Mnara wa Mlinzi. Ndugu walipanga mandari katika bustani ya umma au katika uwanja wa mtu fulani. Mbinu hiyo ilifua dafu kwa kuwa miongoni mwa wenyeji ni jambo la kawaida kwa marafiki au watu wa familia kukusanyika pamoja na kujifurahisha. Mbali na Biblia na vitabu walivyohitaji, akina ndugu walibeba vitu vilivyohitajika kwa ajili ya mandari na mapishi! Vikusanyiko hivyo viliwakumbusha jinsi Waisraeli wa kale walivyofurahia sherehe zao za ibada.—Kum. 16:15.

Wakati wa marufuku, makusanyiko ya mzunguko yaliyofupishwa yalifanywa kwa njia hiyohiyo. Licha ya jitihada za serikali za kuwazuia, akina ndugu hawakuacha kamwe kukusanyika pamoja au kuhubiri habari njema. Ndugu fulani hata waliweza kuhudhuria makusanyiko ya wilaya Nairobi na waliporudi waliwasimulia wenzao mambo yaliyoonwa yenye kutia moyo.

‘WENYE KUJIHADHARI KAMA NYOKA HATA HIVYO WASIO NA HATIA KAMA NJIWA’

Ndugu wenye madaraka waliamini kwamba ikiwa wangekuwa “wenye kujihadhari kama nyoka na hata hivyo wasio na hatia kama njiwa,” marufuku hiyo isingetekelezwa kikamili, nao utendaji wa kitheokrasi ungeweza kuendelea. (Mt. 10:16) Hivyo, kwa tahadhari kubwa, mapainia wa pekee waliendelea katika migawo yao, nao wahubiri wakaendelea kuhubiri nyumba kwa nyumba.

Wengine hawakufurahi kutembelewa na Mashahidi wa Yehova. Siku moja mwaka wa 70 na kitu, Peter Gyabi alikuwa akihubiri pamoja na Fred Nyende, aliyekuwa tineja wakati huo. Fred alikuwa mchanga mama yake alipojifunza kweli mwaka wa 1962. Hata hivyo, alikuwa amekua, nayo hali iliyozuka ilipima ukomavu wake.

Mwenye nyumba mkali—ambaye yaonekana alikuwa askari kanzu—aliwatambua ndugu hao kuwa Mashahidi wa Yehova. Aliwakamata na kuwalazimisha kuingia katika gari lake. Hawakujua litakalotokea kwa sababu kwa kawaida maelfu ya watu waliokamatwa hivyo hawakuonekana tena. Pia, ilikuwa kawaida kwa watu kuteswa, iwe kuna sababu au la. Wakiwa njiani kuelekea kwenye kituo cha polisi, Peter na Fred walimwomba Yehova awape nguvu za kuwa watulivu na kudumisha uaminifu. Mtu huyo aliwapeleka kwa ofisa mkuu, akiwashtaki na kuwauliza maswali yasiyo na mwisho. Hata hivyo, Peter na Fred walijionea wenyewe ukweli wa maneno ya Methali 25:15: “Kwa subira kiongozi hushawishiwa, na ulimi wa upole unaweza kuvunja mfupa.” Hata hivyo, hakuna mfupa wowote uliovunjwa alasiri hiyo. Kwa kuwa Peter aliwaeleza kwa utulivu kuhusu msimamo wetu wa kutii sheria na kushikamana kwetu na mafundisho ya Biblia, na pia kwa kuwa ndugu hao walijiendesha na kujibu kwa heshima, hatimaye chuki ya mkuu huyo ilianza kupungua. Matokeo?

Mkuu huyo alimwachilia Peter na Fred na kumwamuru mtu huyo aliyewakamata awarudishe katika eneo! “Dereva” wao aliyekuwa amedhalilishwa akakubali shingo-upande, nao ndugu hao wakamshukuru Yehova kwa kuwaokoa.

Makabiliano mengine na polisi hayakuwa yenye kuogopesha sana. Kwa mfano, familia ya Emmanuel Kyamiza na mke wake, pamoja na kikundi kidogo cha watu wenye kupendezwa, walikuwa wakifanya mikutano kisiri nyumbani kwao mjini Entebbe. Ili kuepuka kugunduliwa, Emmanuel alikuwa akibadili mahali pa kuongozea mafunzo ya Biblia. Baada ya muda, Emmanuel akadhani kwamba mbinu zake za kuwakwepa polisi zinafaulu. Siku moja, baada ya Emmanuel kumaliza kuongoza funzo la Biblia katika bustani inayoitwa Entebbe Botanical Gardens, polisi mmoja alianza kutembea kuelekea mahali alipokuwa huku naye akijaribu kuficha vitabu vyake visionekane. “Mbona unaficha vitabu vyako?” akauliza polisi huyo. “Tunajua mnalofanya. Tunajua ninyi ni Mashahidi wa Yehova. Hata tunajua mahali mnapokutanikia. Ikiwa tungetaka, tungekuwa tumewakamata kitambo sana. Lakini mnaweza kuendelea na mambo yenu.” Naye Emmanuel akaendelea—kwa uaminifu!

Baadaye, Emmanuel alipostaafu na kurudi kijijini kwao, aliendelea kuvumilia upinzani na dhihaka. Kama Yesu, ‘hakuheshimiwa katika eneo la nyumbani.’ (Marko 6:4) Hata hivyo, hata kufikia alipokuwa na umri wa miaka 70 na kitu, Emmanuel aliendelea “kusitawi wakati wa kuwa na kichwa chenye mvi,” naye alikuwa akiendesha baiskeli yake na kusafiri umbali wa kilomita 30 ili kuhudhuria mikutano. (Zab. 92:14) Leo, akiwa na umri wa miaka 80 na kitu, angali anatumikia kwa uaminifu akiwa mtumishi wa huduma, ijapokuwa haendeshi sana baiskeli yake kama zamani.

MAPAINIA WENYE KUSTAHIMILI

Ijapokuwa hali hazikuwa shwari, sikuzote ndugu na dada kadhaa walishiriki katika utumishi wa painia. Painia mmoja mwenye bidii wa enzi hizo ni James Luwerekera, soroveya wa serikali aliyebatizwa mwaka wa 1974. Punde baada ya kubatizwa alianza kufanya ukulima ili awahubirie habari njema jirani zake kijijini kwao. Mke wake pia alijifunza kwa muda, lakini kadiri wakati ulivyopita, alizidi kuwa mpinzani.

Kwa mfano, asubuhi moja, kukiwa na giza bado, James na ndugu kadhaa walifunga safari kuelekea Nairobi ili kuhudhuria kusanyiko la wilaya. Baadaye, waliposimamishwa na polisi katika kituo cha ukaguzi, ndugu hao walishangaa kuona mavazi ya James—nguo zake hazikuwa na mpangilio wowote wala hazikumtoshea. Mwanzoni aliwatania kwa kuwaambia alivaa mbiombio gizani. Lakini waliposisitiza kujua ni kwa nini, alikiri kwamba mke wake alificha nguo zake za mikutano ili asihudhurie kusanyiko na kwa hiyo alilazimika kuvalia nguo alizopata. Ndugu hao walimpa baadhi ya nguo zao, naye akawasili kusanyikoni akiwa amevalia ifaavyo.

Nyakati fulani upinzani nyumbani kwa James na katika ujirani ulikuwa usumbufu tu, lakini nyakati nyingine ulikuwa mkali zaidi. Hali iliendelea hivyo kwa miaka kadhaa. Wakati wote huo, James alivumilia kwa upole na kuwa mwaminifu hadi alipokufa mwaka wa 2005. Imani yake ingali yawachochea ndugu zake, na bila shaka, inakumbukwa na Mungu wake, Yehova.

“NDUGU ALIYEZALIWA KWA AJILI YA WAKATI WA TAABU”

“Rafiki wa kweli anapenda nyakati zote, naye ni ndugu aliyezaliwa kwa ajili ya wakati wa taabu.” (Met. 17:17) Ndugu nchini Kenya walikuwa rafiki za kweli wakati wa taabu na hatari zilizowakabili Mashahidi nchini Uganda katika miaka ya 1970. Waangalizi wanaosafiri na wawakilishi wa ofisi ya tawi walionyesha moyo mkuu kwa kuvuka mpaka na kuingia Uganda ili kuwategemeza na kuwatia moyo ndugu na dada zao wapendwa.

Ghasia za kisiasa zilizuka mwaka wa 1978 wakati ambapo jeshi la Uganda lilivamia eneo la Tanzania. Jeshi la Tanzania nalo likalipiza kisasi kwa kuipindua serikali ya Uganda mnamo Aprili 1979, hali iliyomlazimu dikteta wa Uganda aliyeogopwa sana, Idi Amin, kuikimbia nchi. Kuondoka mara moja kwa Amin kulileta mabadiliko mengi nchini Uganda. “Amin alipoondoka,” asema ndugu mmoja, “nayo marufuku ikaondoka.” Gazeti The Uganda Times lilitangaza hivi: “Wamishonari Wako Huru Kurudi.” Kwa mara nyingine tena, watu wa Yehova wakapata uhuru wa ibada!

“HATA IKIWA WATANIUA, NITAENDA”

Kufuatia ghasia zilizozuka baada ya serikali kupinduliwa, kulikuwa na uporaji mwingi nchini Uganda licha ya uhuru uliopatikana. Kwa sababu ya kuenea kwa uvunjaji wa sheria, kulikuwa na wizi na jeuri kwa kiwango kisicho na kifani. Hata hivyo, ndugu katika ofisi ya tawi ya Kenya walipanga mara moja Günter Reschke na Stanley Makumba wazuru Uganda na kuanza kufanya makusanyiko ya mzunguko.

“Majuma mawili kabla ya kufunga safari hiyo, baada ya vita,” akumbuka Günter, “tulikuwa na shule ya mapainia mjini Meru, karibu na Mlima Kenya. Nakumbuka nikisoma katika gazeti kuhusu mauaji mengi mjini Kampala, yanayotekelezwa usiku hasa. Baada ya kusoma kisehemu fulani kwa sauti, nilimaka: ‘Na hapa ndipo tunapopaswa kwenda juma lijalo!’ Kisha nikawaza, ‘Nitaukimbia mgawo wangu kama Yona?’ Papo hapo woga wangu ukaisha nami nikajiambia, ‘Hata ikiwa wataniua, nitaenda. Sitakimbia kama Yona.’”

Ndugu hao wakafunga safari yao, Stanley akatembelea makutaniko ya vijijini, naye Günter akatumikia miji mikubwa. “Mambo mengi yalihitaji kupangwa upya,” waripoti ndugu hao. “Ni wahubiri 113 tu waliokuwa watendaji nchini Uganda wakati huo. Kila mmoja alifurahi kukusanyika na ndugu zake tena kwa uhuru na kufanya kusanyiko hadharani. Hudhurio lilikuwa 241, jambo ambalo tulishangilia.” Ijapokuwa mbegu za kweli zilikuwa zimekanyagwa-kanyagwa, ni wazi kwamba bado zingeweza kuzaa matunda.

NYAKATI HATARI

Walipofika Mbale, karibu na mpaka wa mashariki wa Uganda, ndugu hao wawili waliokuwa wakizuru, Günter na Stanley, waliegesha gari lao mbele ya nyumba ambamo walilala usiku huo. Usiku waliwasikia wezi wakilipora gari lao. Günter alitaka kupiga kelele lakini akakumbuka kwamba mapema wiki hiyo wezi walimpiga risasi na kumwua mtu aliyejaribu kuwazuia wasiibe. Kwa hiyo, Günter akaamua kukaa kimya kwa kuwa uhai una thamani kuliko gari. Kulipopambazuka, wakakuta kwamba magurudumu mawili na kioo cha mbele cha gari vimechukuliwa. Walipiga ripoti kwenye kituo cha polisi, ambako waliambiwa, “Liondoeni hapo kabla wezi hao hawajarudi kulipora zaidi!”

Haraka iwezekanavyo, ndugu hao wakaondoka kuelekea Kampala. Walisafiri kwa shida. Gari lao halikuwa na kioo cha mbele, nao hawakuwa na chochote cha kujikinga dhidi ya mvua na upepo mkali ila blanketi ambayo Günter alijifunika na kofia ambayo Stanley alivaa. Kwa kuwa magurudumu yao mawili yalikuwa yameibiwa, walitumia gurudumu la akiba na lingine bovu waliloomba. Isitoshe, gurudumu lililoombwa lilipaswa kurudishwa kabla ya siku mbili kwisha! Ndugu hao walishikilia matumbo wakitumaini kwamba magurudumu hayo yatawafikisha.

Licha ya masaibu yote hayo, Günter na Stanley walilazimika kutumia barabara inayopitia msituni iliyokuwa na wanyang’anyi. “Mwendeshe mbio,” akawaambia mwenyeji wao, “msiruhusu gari lolote liwapite njiani.” Ndugu hao wenye moyo mkuu walipumua walipofika Kampala salama—tena haraka isivyo kawaida. Bila kupoteza wakati wakatafuta mtu arudishe gurudumu walilokuwa wameomba Mbale.

FURSA NA MATATIZO MAPYA

Mwaka wa 1980, Ndugu Reschke alizuru makao makuu huko Brooklyn, New York. Akiwa huko aliombwa atoe ripoti kuhusu Uganda. Baadaye, washiriki wa Baraza Linaloongoza walitaja kwamba kuna uwezekano wa kutuma tena wamishonari Uganda. Ulikuwa wakati barabara wa kufanya hivyo, kwa kuwa kwa mara nyingine tena ingewezekana kukusanyika pamoja nchini Uganda. Isitoshe, kufikia mwaka wa 1981 kulikuwa na wahubiri 175, na mwezi wa Julai mwaka huohuo, Uganda ilifurahi kuwa na kilele kipya cha wahubiri 206.

Hata hivyo, kwa sababu ya vita vilivyopiganwa kwa miaka kumi, kulikuwa na silaha nyingi mikononi mwa watu wafidhuli. Milio ya risasi na unyang’anyi yalikuwa mambo ya kawaida. Kwa tahadhari, wahubiri wa habari njema walijikakamua kueneza kotekote katika eneo magazeti na vitabu vyetu vya Biblia vyenye ujumbe wenye kufariji. Kwa wastani, kila mhubiri aligawa magazeti 12.5 mwezi wa Julai. Hata hivyo, kwa busara, utumishi wa shambani, sawa na shughuli nyingine, ulifanywa mchana kwa sababu usiku kulikuwa na hatari chungu nzima. Licha ya hatari zote hizo, ilionekana wazi kwamba kutakuwa na ongezeko.

WAMISHONARI WAKARIBISHWA TENA

Wahitimu wa Shule ya Gileadi, Jeffrey Welch na Ari Palviainen waliwasili Kampala kutoka Kenya mnamo Septemba 1982. Tangu mwanzo, Jeff na Ari walipata matokeo mazuri. “Watu walikuwa na njaa ya mambo ya kiroho,” akumbuka Jeff, “kwa hiyo magazeti yakiwa na habari zenye kuvutia, ‘yalijiangusha.’”

Mwezi wa Desemba, Heinz na Marianne Wertholz, kutoka katika Tanzu la Shule ya Gileadi huko Wiesbaden, Ujerumani, walijiunga na Jeff na Ari. Tangu mwanzo, akina Wertholz walichochewa sana na bidii ya ndugu zao wa Uganda licha ya kwamba walikuwa wakiishi katika hali mbovu na hatari.

“Huduma nyingi,” akumbuka Heinz, “kama vile maji na mawasiliano zilikuwa zimezorota. Kulikuwa na migogoro ya kisiasa. Mara kadhaa kulikuwa na uvumi wa kwamba serikali itapinduliwa, na wanajeshi waliweka vizuizi vingi barabarani. Milio ya risasi na unyang’anyi yalikuwa mambo ya kawaida hasa wakati wa usiku. Giza lilipoingia, barabara zilikuwa tupu. Kila mtu alikaa nyumbani akitumaini—na mara nyingi kusali—kwamba usiku utapita salama.”

Heinz na Marianne walikaa na familia ya Sam Waiswa huku wakiendelea kutafuta nyumba ambayo ingekuwa makao ya wamishonari. Ijapokuwa Sam alikuwa na taaluma ya kufundisha, hali za kiuchumi nchini humo zilikuwa zimewalemea sana hivi kwamba ukarimu wa familia yake kwa kweli haukuwa na kifani.

“Haikuwa rahisi kupata nyumba mahali salama,” asema Heinz, “kwa hiyo tulikaa kwa Sam kwa miezi mitano. Katika kipindi hicho tulipata kufahamiana vizuri. Nyakati nyingine walikuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku, hata hivyo, walikuwa na furaha sikuzote; nao watoto walikuwa watiifu na wenye heshima. Kwa kuwa maji ya jiji hayakutegemeka, watoto hao walikuwa wakienda kuteka maji kwa mitungi ya lita 20 na kuyabeba kichwani. Tuliporudi nyumbani kutoka shambani, sikuzote kulikuwa na maji ya kutumia. Bila shaka, tulijifunza kuhifadhi maji. Kwa mfano, tulitumia kiasi kidogo cha maji tulipooga, na kuyahifadhi ili yatumike vyooni.”

Mwezi wa Aprili 1983, miaka kumi baada ya wamishonari wa mwisho kuondoka nchini Uganda, wamishonari hao wanne wapya walipata makao mapya mahali palipokuwa salama kiasi. Ukosefu wa usalama na upungufu wa vitu ulifanya hali iwe ngumu, hata hivyo, upendo wa ndugu wenyeji ulifanya wasahau yote hayo.

“Sikuzote tulifurahia kuwahubiria watu habari njema,” asema Marianne. “Walipenda mambo ya dini, walikuwa na Biblia, nao walikuwa tayari kusikiliza. Walikuwa wenye urafiki na adabu. Na licha ya hali ngumu za kiuchumi na nyinginezo, walikuwa na tabasamu sikuzote.”

WENYE UMRI MKUBWA WATAKA KUFANYA MENGI ZAIDI

Wengi wenye umri mkubwa, ambao kulingana na utamaduni huheshimiwa sana, waliikubali habari njema nao wamemtumikia Yehova katika miaka yao ya uzeeni. Kwa mfano, Paulo Mukasa, mwalimu aliyestaafu, alikuwa na umri wa miaka 89 alipojifunza kweli. Baada ya kujionea vita viwili vya ulimwengu, utawala wa kikoloni, udikteta wenye jeuri, na misukosuko mingine ya kisiasa, sasa alikuwa na hamu ya kujifunza kuhusu Ufalme wa Mungu. Alifurahi sana alipojua kwamba Mfalme wa Kimasihi, Yesu Kristo, ‘atamkomboa maskini na mwenye kuteseka kutoka katika ukandamizaji na katika jeuri.’—Zab. 72:12, 14.

Paulo alipostahili kubatizwa miaka miwili baadaye, ndugu walikuwa na mashaka, ‘Kwa kweli tunaweza kumzamisha kikongwe huyu ndani ya maji?’ Hata hivyo, hawakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi. Huku kijana barubaru aliyetaka kubatizwa akisitasita kuingia ndani ya maji, Paulo, mwenye umri wa miaka 91 alibatizwa na kuibuka akiwa na tabasamu kubwa. Ijapokuwa hakuweza kutimiza mengi katika huduma, Paulo aliwahubiria kwa bidii habari njema ya Ufalme wote waliomtembelea hadi alipokufa miaka kadhaa baadaye.

Lovinca Nakayima alivumilia matatizo ya uzee na afya. Miguu yake ilikuwa imevimba sana hivi kwamba hangeweza kwenda popote pasipo usaidizi. Hata hivyo, kutaniko lilipotiwa moyo kufanya upainia msaidizi kwa angalau mwezi mmoja wakati wa majira ya Ukumbusho, Lovinca alitaka kujaribu. Kutaniko lilimsaidia kufanya upainia kwa kuwapeleka watu wanaopendezwa nyumbani kwa Lovinca ili kujifunza nao Biblia. Pia, wamishonari walimfundisha kuwaandikia barua watu wa vijijini, jambo ambalo angeweza kufanya wakati unaomfaa. Halafu, siku za Jumamosi, mzee wa kutaniko alikuwa akimchukua Lovinca na kumpeleka eneo la umma mjini Kampala, mahali ambapo angeweza kuketi na kuwahubiria wapita-njia siku nzima. Akiwa na furaha na kuridhika mwishoni mwa mwezi, Lovinca alisema, “Sasa naona kwamba ninaweza kufanya upainia—na kuufurahia pia!” Hakufanya upainia kwa mwezi huo mmoja tu, bali kutokana na utegemezo wa kutaniko, alifanya upainia kwa miezi 11 mfululizo!

“MTU HUSEMAJE . . . ?”

Miaka ya 1980, wahubiri wenye bidii nchini Uganda waliwakaribisha wamishonari wenye hamu waliozidi kumiminika nchini. Baadhi yao walikuwa wamishonari wapya waliohitimu kutoka Shule ya Gileadi, na wengine walilazimika kutoka katika migawo yao ya umishonari nchini Zaire (ambako leo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo). Kwa kuwa sasa kulikuwa na idadi kubwa ya wamishonari mjini Kampala na Jinja, maeneo yenye watu wengi yangeweza kuhubiriwa kikamili zaidi, nao wamishonari walifurahi kuona kwamba eneo la Uganda lilikuwa tayari kuvunwa. Shida haikuwa kuwapata watu wanaopendezwa na ujumbe wetu, bali kuwasaidia kufanya maendeleo.

Akiwa ametoka tu katika Shule ya Gileadi, Mats Holmkvist alikuwa na bidii sana, naye alikuwa na hamu ya kujifunza lugha ya wenyeji ili kuwasaidia watu wapendezwe na kweli. Wakati huo, Fred Nyende alikuwa painia wa pekee mjini Entebbe, naye aliutumia ujuzi wake wa kutafsiri na ukalimani kuwafundisha wamishonari kuzungumza kwa ufasaha Kiganda, lugha ambayo nyakati nyingine maneno yake huwa magumu kutamka. Mats alitoa jasho.

“Mtu husemaje, ‘Ufalme wa Mungu’ katika Kiganda?” akauliza Mats mwanzoni-mwanzoni mwa masomo yake.

“Obwakabaka bwa Katonda,” akamjibu Fred, kana kwamba yuaimba.

‘Jamani,’ akawaza Mats huku akighairi kwamba laiti hangeuliza. Hata hivyo, Mats alipiga hatua kubwa na hatimaye aliweza kukizungumza Kiganda vizuri.

KAZI YA UKUSANYAJI YATIA FORA

Licha ya hali ngumu nchini Uganda katika miaka 1980, watu wengi ajabu waliikubali kweli ya Biblia. Idadi ya wahubiri iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 130—toka 328 mwaka wa 1986 hadi 766 mwaka wa 1990. Vikundi vipya vilikuwa vikichipuka kote nchini. Mjini Kampala idadi ya makutaniko iliongezeka maradufu. Kutaniko la Jinja lilifurahi kuona idadi ya wahubiri ikiongezeka mara tatu, nacho kikundi cha Iganga muda si muda kikawa kutaniko rasmi.

“Kulikuwa na ongezeko kubwa sana,” akumbuka mzee mmoja wa kutaniko la Jinja, “hivi kwamba tukawa tukijiuliza wahubiri wote hao wapya wanatoka wapi. Kwa muda, tulilazimika kupanga wakati kila Jumapili ili kukutana na wale wanaotaka kuwa wahubiri.”

KUVUNA ENEO KUBWA ZAIDI

Mojawapo ya mambo yaliyochangia sana ongezeko hilo ni roho ya upainia ambayo akina ndugu walikuwa nayo. Kama wahubiri wa karne ya kwanza Paulo, Sila, na Timotheo, watumishi wa wakati wote nchini Uganda ‘walijitoa kuwa kielelezo cha kuigwa na wengine.’ (2 The. 3:9) Kukiwa na ongezeko hilo shambani, na vielelezo hivyo vizuri, wahubiri wengi wenye bidii walichochewa kufanya mengi zaidi katika huduma yao. Vijana kwa wazee, waseja na waliofunga ndoa, wanaume kwa wanawake, na hata wengine waliokuwa na majukumu ya kifamilia walijiandikisha kuwa mapainia. Kwa wastani, zaidi ya asilimia 25 ya wahubiri wote walishiriki katika utumishi wa upainia miaka ya mwisho-mwisho ya 1980. Wengine kati yao, wameendelea na utumishi wa wakati wote hadi leo hii.

Mapainia waliunga mkono kampeni za pekee za kuhubiri za kila mwaka zinazoitwa kampeni za Makedonia. (Mdo. 16:9, 10) Kampeni hizo zimefanywa kwa miaka kadhaa sasa. Kwa kipindi cha miezi mitatu, makutaniko yamekuwa yakihubiri maeneo ambayo hayajagawiwa yeyote au ambayo hayahubiriwi kwa ukawaida. Pia, mapainia wa kawaida kadhaa huwekwa rasmi kuwa mapainia wa pekee wa muda katika maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi. Matokeo yamekuwa yenye kutia moyo sana. Watu wengi walio wanyoofu wamethamini sana kampeni hizo, zilizowasaidia kuipata kweli, na vikundi vingi vipya na makutaniko yameanzishwa.

Katika kampeni moja, mmishonari Peter Abramow na Michael Reiss walipokuwa wakihubiri katika mji wa Kabale walimkuta Margaret Tofayo, aliyekuwa amejifunza Biblia awali. Alisadiki kabisa kwamba alifundishwa kweli, naye tayari alikuwa akiwahubiria wengine ijapokuwa hakuwa mhubiri. Ili kumsaidia kwa kadiri ambavyo wangeweza, wamishonari hao walimpa nakala pekee waliyokuwa nayo ya kitabu Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko. Ndugu hao walipomtembelea Margaret mara ya mwisho kabla ya kuondoka, aliwashangaza kwa kuwaandalia mlo wa pekee. Walichochewa sana na fadhili na ukarimu wake, hata hivyo, walisita walipopata kujua kwamba alikuwa amewachinjia kuku wake mmoja tu aliyekuwa naye. Walijua kwamba familia hiyo ilitegemea mayai ya kuku huyo. “Msijali,” akasema, “mmenipa kikubwa zaidi kuliko ninachowapa.” Baadaye alibatizwa na kutumikia akiwa mwaminifu hadi alipokufa.

Jambo lingine ambalo limechangia ongezeko kubwa ni jinsi ambavyo akina ndugu wamevitumia vitabu vyetu. “Ijapokuwa tunajaribu kunoa stadi zetu za kufundisha,” asema Mats, aliyetajwa awali, “Biblia na vitabu vyetu ndivyo hasa vinavyowavutia watu na kuwachochea kufanya mabadiliko maishani mwao. Hata wale ambao hawajui kusoma vizuri lakini wana kiu ya ile kweli, mioyo yao huchochewa na broshua zetu.”

KUSHINDA VIPINGAMIZI

Hata hivyo, pamoja na maendeleo ya miaka ya mwisho-mwisho ya 1980 kulikuwa na magumu pia. Mnamo Julai 1985, kulikuwa na mapinduzi mengine ya kijeshi. Kama awali, hali ya usalama ikazorota, vita vya wanamgambo vikapamba moto. Majeshi yaliyotimuliwa yakaanza kupora mali na kuwapiga watu risasi ovyoovyo. Kwa muda, kulikuwa na mapambano makali karibu na makao ya wamishonari mjini Jinja. Siku moja makao yao yalivamiwa na wanajeshi, hata hivyo wavamizi hao walipopata kuwatambua wamishonari, hawakuharibu chochote badala yake walichukua vitu vichache sana. Kisha, Januari 1986, serikali nyingine tena ikashika hatamu na kujaribu kurejesha utulivu nchini.

Punde si punde, serikali hiyo mpya ililazimika kukabiliana na adui mwingine mpya—UKIMWI. Ugonjwa huo ulipolipuka miaka ya 1980, Uganda ilikuwa mojawapo ya nchi zilizoathiriwa zaidi. Yadaiwa kwamba watu wapatao milioni moja wamekufa, wengi kuliko hata waliokufa katika kipindi cha miaka 15 ya msukosuko wa kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ugonjwa huo uliwaathiri jinsi gani ndugu zetu?

“Ndugu na dada kadhaa wapya waliingia katika kweli wakiwa na bidii sana,” aeleza Washington Ssentongo, painia wa kawaida, “kumbe baadaye wangeugua na kufa kutokana na UKIMWI. Walikuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI kabla ya kujifunza kweli.” Wengine waliambukizwa na wenzi wao wa ndoa wasio waamini.

“Nyakati nyingine, karibu kila mwezi kulikuwa na mazishi ya mtu tuliyemjua na kumpenda,” asema Washington, “na karibu kila familia ilifiwa. Pia kulikuwa ushirikina mwingi kuhusiana na UKIMWI. Watu wengi waliuhusianisha na uchawi au kulaaniwa. Maoni hayo yaliyopotoka yaliwaogopesha watu, yakachochea chuki isiyo na msingi, na kufanya iwe vigumu sana kusababu nao.” Hata hivyo, ndugu na dada zetu walifarijiana kwa ushikamanifu kwa tumaini la ufufuo na kuhakikishiana upendo wa kweli wa Kikristo.

Miaka ya 1980 ilipokuwa ikikaribia mwisho, watu walikuwa na matumaini makubwa nchini Uganda. Hali ya usalama ilikuwa ikirejea, nao uchumi wa nchi ulikuwa ukifufuka. Miundo-msingi iliboreshwa, na miradi mbalimbali ya kijamii ikaanzishwa upya au kutekelezwa.

Hata hivyo, kadiri watu walivyozidi kukazia sera za kisiasa, nyakati nyingine msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kutokuwamo haukueleweka. Kwa mfano, pindi moja wenye mamlaka walisimamisha ghafula ujenzi wa Jumba la Ufalme. Vibali vya kufanya makusanyiko fulani havikutolewa, na wamishonari fulani walilazimika kuondoka nchini baada ya vyeti vyao kumalizika muda. Kufikia mwishoni mwa mwaka wa 1991, kulikuwa na ndugu wawili tu wamishonari nchini. Ni hatua gani iliyochukuliwa?

Hatimaye, ujumbe wa akina ndugu ulikutana na wenye mamlaka na kuwaeleza msimamo wetu wa kutokuwamo. Baada ya wenye mamlaka kuelewa msimamo wetu, wamishonari waliruhusiwa kurudi nchini Uganda. Kazi ilisonga mbele pasipo vikwazo, na mwaka wa 1993, Uganda ilifurahi kuwa na wahubiri 1,000. Kisha, miaka mitano tu baadaye, idadi ya watangazaji wa Ufalme ikafikia 2,000. Leo hii, kuna wamishonari 40 hivi wanaofanya kazi nzuri kotekote nchini.

KAZI YA KUTAFSIRI YAHARAKISHA UKUSANYAJI WA WATU

Kiingereza hutumiwa kote nchini. Hata hivyo, Kiganda ndiyo lugha inayozungumzwa na wenyeji walio wengi, ijapokuwa lugha nyingine zaidi ya 30 huzungumzwa. Hivyo, jambo kuu ambalo limechangia ongezeko kubwa katika miaka ya karibuni ni maendeleo katika kazi ya kutafsiri.

“Ijapokuwa mama yangu alikuwa shahidi mwaminifu,” asema Fred Nyende, “alifaidika zaidi mikutanoni nilipotafsiri makala za funzo katika Kiganda. Jambo ambalo sikujua wakati huo ni kwamba nilikuwa nikipata mazoezi kwa ajili ya kazi kubwa zaidi ya kutafsiri.” Fred alimaanisha nini?

Muda mfupi baada ya kuanza kufanya upainia mwaka wa 1984, Fred aliombwa awafundishe wamishonari Kiganda. Mwaka uliofuata aliombwa ajiunge na kikundi cha watafsiri wa Kiganda. Mwanzoni, yeye na watafsiri wengine walifanyia kazi yao nyumbani walipopata nafasi. Baadaye kikundi hicho kikaanza kufanya kazi yao kikiwa pamoja katika chumba kidogo kando ya makao ya wamishonari. Wakati wa marufuku ya miaka ya 1970, matoleo kadhaa ya gazeti la Mnara wa Mlinzi yalikuwa yametafsiriwa katika Kiganda na nakala kadhaa kufanyizwa. Hata hivyo, baada ya muda, mradi huo ulisimamishwa. Mwaka wa 1987 ndipo gazeti la Mnara wa Mlinzi lilipoanza kuchapishwa tena katika Kiganda. Tangu wakati huo, kikundi cha kutafsiri kimeongezeka, nao watafsiri wamejitahidi kutafsiri vitabu vingi zaidi kwa ajili ya idadi inayozidi kuongezeka ya makutaniko ya Kiganda. Leo, karibu nusu ya makutaniko nchini ni ya Kiganda.

Baadaye, vitabu vyetu vilianza kutafsiriwa katika lugha nyinginezo. Kwa sasa kuna vikundi vya kudumu vya watafsiri wa Kicholi, Kikonzo, na Kinyankore. Isitoshe, vitabu kadha wa kadha vimetafsiriwa katika Kiteso, Kigbara, Kimadi, na Kitoro.

Vikundi vya Kicholi na Kinyankore vinafanyia kazi yao katika ofisi za kutafsiri mjini Gulu na Mbarara, ambako lugha wanazotafsiri zinazungumzwa na wengi. Hilo limewasaidia watafsiri kwenda sambamba na lugha zao na kutafsiri kwa njia inayoeleweka kwa urahisi. Kwa kuongezea, makutaniko yaliyo katika miji hiyo yanafurahia utegemezo wa watafsiri hao.

Bila shaka kazi ya kutafsiri inahitaji jitihada nyingi na gharama kubwa. Watafsiri wenye bidii wa Uganda, pamoja na vikundi vingine vya kutafsiri ulimwenguni pote, wamefaidika kutokana na mazoezi ya kuboresha ufahamu wa lugha na stadi za kutafsiri. Jitihada na gharama hizo hazikuwa kazi bure—watu wengi zaidi nchini Uganda, kutoka katika ‘makabila na vikundi vya watu na lugha,’ wanafaidika kwa kusoma ujumbe wa Biblia katika lugha zao wenyewe kuliko ilivyokuwa awali. (Ufu. 7:9, 10) Ndiyo sababu, kufikia mwaka wa 2003, kulikuwa na wahubiri wa Ufalme zaidi ya 3,000 nchini Uganda, na miaka mitatu tu baadaye, mwaka wa 2006, idadi hiyo ilifikia 4,005.

SEHEMU ZAIDI ZA IBADA ZAHITAJIWA

Zamani, mikutano ilikuwa ikifanyiwa katika nyumba za watu, vituo vya umma, na madarasa. Majengo ya kwanza kutumiwa kwa kusudi pekee la mikutano ya Kikristo yalikuwa majengo ya matofali yaliyoezekwa kwa nyasi sehemu za vijijini huko Namaingo na Rusese. Bila shaka jitihada za ndugu hao zilibarikiwa katika maeneo hayo mawili, na makutaniko yakasitawi huko.

Mijini, hata hivyo, hata jengo la wastani tu hugharimu pesa nyingi, na hali za kiuchumi nchini Uganda zilifanya ionekane kana kwamba kuwa na Majumba ya Ufalme ni ndoto. Jumba la Ufalme la kwanza la kudumu liliwekwa wakfu Machi 1988 mjini Jinja. Nayo ilikuwa kazi kwelikweli—kukata miti katika msitu ulio karibu, kubeba magogo kwenye barabara za matope, na kulijenga jumba lenyewe! Baadaye, ndugu wa Mbale, Kampala, na Tororo pia walijenga Majumba yao wenyewe ya Ufalme.

Ujenzi wa Majumba ya Ufalme ulipigwa jeki mwaka wa 1999 wakati ambapo kikundi cha ujenzi kilianzishwa kwa msaada wa Ofisi ya Uhandisi ya Kimkoa katika ofisi ya tawi ya Afrika Kusini. Ofisi hiyo iliweka rasmi ndugu tisa kutumikia katika kikundi hicho, idadi iliyotia ndani watumishi wawili wa kimataifa na wake zao. Ndugu hao wenye bidii walijifunza kazi hiyo haraka, nao pia wakawafundisha wengine. Kazi ya ujenzi ikapamba moto, na Majumba ya Ufalme 67 yakajengwa, kila moja likijengwa kwa wastani wa mwezi mmoja u nusu—muda mfupi ajabu ikizingatiwa kwamba vyombo vinavyotumia umeme ni vichache, maji hayapatikani kwa urahisi, na vifaa mbalimbali vya ujenzi havipatikani sikuzote.

Makutaniko mengi nchini Uganda sasa hufanyia mikutano yao katika Jumba la Ufalme, nayo yameona faida ya kuwa na jumba lao wenyewe. Kwa kawaida ni rahisi zaidi kwa watu wanaopendezwa kuja mahali rasmi pa ibada badala ya kwenda katika darasa, na kwa sababu hiyo hudhurio limeongezeka nayo makutaniko yamekua sana.

KUSHUGHULIKIA ONGEZEKO LA HARAKA

Ongezeko la haraka la makutaniko lilifanya iwe vigumu kupata mahali panapofaa kwa ajili ya makusanyiko. Ni nini kingeweza kufanywa ili kupata mahali panapofaa ambapo pangepunguza uhitaji wa kusafiri mbali, hasa kwa akina ndugu wa vijijini? Utatuzi ulipatikana wakati kibali kilipotolewa cha kujenga Majumba ya Ufalme yanayoweza kupanuliwa. Hayo ni majumba ya kawaida lakini yenye eneo la nje lenye paa na sakafu tu bila kuta za kando. Sehemu ya nyuma ya Jumba la Ufalme inapofunguliwa, eneo hilo lenye paa linaweza kutoshea watu wengi zaidi wakati wa kusanyiko. Majumba kama hayo yamejengwa Kajansi, Rusese, na Lira, na la nne linaendelea kujengwa Seta.

Yehova amebariki ukuzi wa kiroho nchini Uganda na kwa sababu hiyo mabadiliko ya kitengenezo yamehitajika. Kabla ya mwaka wa 1994, kulikuwa na mzunguko mmoja tu nchi nzima. Baadaye, mizunguko zaidi ilianzishwa ili kushughulikia idadi yenye kuongezeka ya makutaniko na vikundi na lugha mbalimbali zinazotumika. Leo, kukiwa na makutaniko 111 na vikundi 50, Uganda ina mizunguko nane, mitatu ikiwa ya Kiganda.

Apollo Mukasa, mmoja wa waangalizi wa mzunguko nchini Uganda, alibatizwa 1972. Mwaka wa 1980 aliingia katika utumishi wa wakati wote badala ya kufuatia masomo ya juu. Je, anajuta?

“Sivyo hata kidogo,” asema Apollo. “Nimejionea mambo mengi yenye kuthawabisha katika utumishi wa painia wa pekee na nikiwa mwangalizi wa mzunguko, nikitembelea makutaniko, na awali, vikundi. Nilithamini sana hasa mazoezi ya kiroho na kitengenezo niliyopata katika Shule ya Mazoezi ya Kihuduma.”

Mbali na Apollo, ndugu zaidi ya 50 kutoka Uganda wamepokea elimu hiyo yenye thamani kwenye Shule ya Mazoezi ya Kihuduma tangu 1994, wakati ambapo ilianza kufanywa katika ofisi ya tawi ya Kenya. Wengi wa ndugu hao hutumikia wakiwa mapainia wa pekee katika makutaniko madogo na vikundi, nao ni msaada mkubwa. Wengine ni waangalizi wanaosafiri.

Mwaka wa 1995 Halmashauri ya Nchi iliwekwa rasmi itumikie chini ya ofisi ya tawi ya Kenya. Mojawapo ya makao ya wamishonari mjini Kampala yakawa makao ya wajitoleaji nane wa wakati wote, kutia ndani kikundi cha watafsiri wa Kiganda. Septemba 2003, Uganda ikawa ofisi ya tawi.

“SASA TUKO PARADISO”

Kwa muda Halmashauri ya Nchi ilijitahidi kwenda sambamba na ukuzi wa vikundi vya watafsiri na ili kutekeleza shughuli zaidi za ofisi. Viwanja viwili kando ya ofisi ya Kampala vilinunuliwa ili kutimiza uhitaji huo. Hata hivyo, hatimaye sehemu kubwa zaidi ilihitajika ili kushughulikia ukuzi zaidi. Mwaka wa 2001, Baraza Linaloongoza lilitoa kibali uwanja wa ekari 10 ununuliwe kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya tawi, nje kidogo ya mji wa Kampala, karibu na Ziwa Victoria.

Mwanzoni, kampuni iliyofaa zaidi kufanya ujenzi huo haikukubali ombi letu kwa kuwa ilikuwa na miradi mingine mingi ya ujenzi wakati huo. Lakini ajabu ni kwamba, bila kutazamia, ilibadili nia na kwa kushangaza, ikatoa makadirio bora zaidi ya gharama za ujenzi wa ofisi mpya ya tawi. Inaonekana kwamba walipoteza kandarasi kubwa ghafula, na hivyo wakalazimika kukubali kujenga ofisi ya tawi haraka iwezekanavyo.

Januari 2006, familia ya Betheli ilifurahi kuhamia makao yao mapya yenye kupendeza, ya orofa mbili zenye vyumba 32. Mbali na makao, kuna jengo la ofisi mbalimbali, jumba kubwa la kulia, jiko, na dobi. Pia kuna mfumo wa maji-taka unaopatana na kanuni za kimazingira, bohari kwa ajili ya idara ya upakizi na usafirishaji, na majengo yenye karakana za udumishaji, uhifadhi wa maji, na mitambo ya umeme. “Sasa tuko paradiso,” akasema ndugu mmoja kwa furaha tele, “uzima wa milele tu ndio tunakosa!” Hotuba ya kuweka wakfu ilitolewa Jumamosi, Januari 20, 2007, na Ndugu Anthony Morris wa Baraza Linaloongoza.

UJUZI WA KWELI WAONGEZEKA

Katika nyakati za msukosuko na nyakati za utulivu, watu wa Yehova nchini Uganda wamejifunza maana ya ‘kulihubiri neno katika majira yanayofaa na majira yasiyofaa.’ (2 Tim. 4:2) Mwaka wa 2008, wahubiri 4,766 walifurahia kuongoza mafunzo ya Biblia 11,564 na watu 16,644 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo. Takwimu hizo, na pia uwiano wa mhubiri 1 kwa watu 6,276, zaonyesha kwamba mashamba yangali “meupe kwa ajili ya kuvunwa.”—Yoh. 4:35.

Wakati huohuo, ndugu na dada zetu nchini Uganda wamejifunza kwamba hali zinaweza kubadilika ghafula na imani yao kujaribiwa. Hata hivyo, wamejifunza kumtegemea Yehova, mwongozo wa Neno lake, na utegemezo wa ushirika wa akina ndugu ulimwenguni pote.

Malaika alimwambia nabii mkongwe Danieli kwamba “wakati wa mwisho . . . ujuzi wa kweli utakuwa mwingi.” (Dan. 12:4) Yehova ameibariki kazi, nao ujuzi wa kweli umekuwa mwingi nchini Uganda. Bila shaka, katika eneo hili, ambapo Mto Nile huanzia, maji mengi ya kweli yataendelea kububujika na kuwatosheleza wote walio na kiu ya kweli za kiroho. Yehova anapozidi kuibariki kazi ulimwenguni pote, tunatazamia kwa hamu wakati ambapo watu wote, kwa pamoja, watamsifu Yehova—milele!

[Maelezo ya Chini]

a Ripoti kuhusu simulizi la maisha la Ndugu Frank Smith ilichapishwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Agosti 1, 1995, ukurasa wa 20-24. Babake Frank, Frank W. Smith, na pia baba yake mdogo na mke wake, Gray na Olga Smith, walikuwa kati ya wahubiri wa kwanza kuhubiri Afrika Mashariki. Babake Frank aliugua malaria na kufa alipokuwa akirudi Cape Town, miezi miwili tu kabla ya Frank kuzaliwa.

b Kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova lakini hakichapishwi tena.

[Blabu katika ukurasa wa 84]

‘Ilikuwa ajabu kusikiliza mazungumzo kati ya Mmarekani na Mskoti katika redio barani Afrika’

[Blabu katika ukurasa wa 92]

“Watapigaje marufuku yaliyo moyoni mwangu?”

[Blabu katika ukurasa wa 111]

“Mtu husemaje, ‘Ufalme wa Mungu’ katika Kiganda?” “Obwakabaka bwa Katonda”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 72]

Maelezo Mafupi Kuhusu Uganda

Nchi

Uganda ni nchi yenye maumbile mengi. Ina misitu mikubwa, nyanda pana, mito na bahari kadhaa, na Milima ya Ruwenzori iliyo mirefu yenye theluji vileleni. Nchi hiyo ina ukubwa wa kilomita mraba 241,551, eneo linalotia ndani karibu nusu ya Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi barani Afrika.

Watu

Zaidi ya asilimia 85 ya watu wa makabila 30 hivi huishi vijijini.

Lugha

Kati ya lugha zaidi ya 32, Kiganda huzungumzwa na walio wengi. Lugha rasmi ni Kiingereza na Kiswahili.

Kazi

Uganda ni nchi ambayo hutegemea kilimo. Hukuza kahawa, majani ya chai, pamba, na mazao mengine ya biashara. Wakazi wengi wa nchi hiyo ni wakulima wanaojiruzuku kwa chakula wanachokuza wenyewe. Wengine hujiruzuku kutokana na uvuvi au utalii.

Chakula

Matooke (tazama picha), chakula kinachotengenezwa kwa ndizi, hupendwa na wengi wanaoishi sehemu ya kusini ya nchi hiyo. Ugali wa mahindi, viazi vitamu, na ugali wa ulezi (wimbi) au muhogo huliwa kwa mboga mbalimbali.

Hali ya hewa

Uganda ni nchi ya kitropiki yenye hali nzuri ya hewa. Nchi hiyo iko kwenye nyanda zilizo mita 1,500 hivi upande wa kusini na kushuka hadi mita 900 hivi upande wa kaskazini. Sehemu nyingi za nchi hiyo huwa na majira ya kiangazi na majira ya mvua.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 77]

Upendo wa Kweli wa Kikristo Wagusa Mioyo

PETER GYABI

ALIZALIWA 1932

ALIBATIZWA 1965

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Mzee wa kutaniko aliyesaidia katika kazi ya kutafsiri wakati wa marufuku. Yeye na mke wake Esta, wana watoto wanne ambao ni watu wazima sasa.

◼ WAMISHONARI wa kwanza Mashahidi wa Yehova walipofika Uganda, kulikuwa na ubaguzi wa rangi nchini, nao wazungu wengi hawakuchangamana na watu weusi. Upendo wa kweli wa wamishonari uligusa mioyo yetu, nasi tukawapenda sana.

Katika miaka ya 1970, tulifurahia kuhubiri na kushirikiana na wamishonari waliokuwa wakiishi Mbarara, kilomita 65 hivi kutoka kwetu. Siku moja, tulipokuwa tukienda kuwatembelea, wanajeshi walitusimamisha. Mmoja wao akatuambia: “Ikiwa mnataka kufa, endeleeni na safari yenu.” Tukaamua kurudi. Baada ya siku kadhaa, tukaanza kuwa na wasiwasi kuhusu wamishonari hao. Tulitaka sana kufika wanakoishi ili kuwajulia hali. Kulikuwa na ulinzi mkali sana. Nililazimika kutumia cheo changu katika hospitali na kibandiko cha hospitali kwenye gari kupita vizuizi vya barabarani. Tulifurahi sana kuwapata wamishonari hao wakiwa salama. Tuliwanunulia vyakula na kukaa nao siku kadhaa. Kisha tukawa tukiwatembelea kila juma mpaka kulipokuwa na usalama wa kutosha kuhamia Kampala. Kadiri hali zilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo tulivyozidi kujionea upendo wa kindugu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 82]

“Nilihisi Kwamba Singeweza Kusema Lolote”

MARGARET NYENDE

ALIZALIWA 1926

ALIBATIZWA 1962

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Dada wa kwanza nchini Uganda kuikubali kweli. Alikuwa painia wa kawaida kwa zaidi ya miaka 20. Angali mhubiri mtendaji.

◼ MUME wangu alipenda kujifunza Biblia pamoja na Ndugu Kilminster, naye alitaka mimi pia nijifunze kwa kuwa alijua ninaipenda sana Biblia. Kwa hiyo, mipango ikafanywa ili Eunice, mke wa John Bwali ajifunze nami.

Nilipendezwa na mambo niliyokuwa nikijifunza, hata hivyo, niliogopa kuwahubiria wengine. Nilikuwa mwoga kiasili nami nilihisi kwamba singeweza kusema lolote. Lakini Eunice hakuchoshwa nami, naye alinisaidia kuanza kwa kusoma andiko moja tu. Kisha, tulipokuwa tukitoka nyumba moja kwenda nyingine, alinifundisha kutayarisha mambo machache ya kusema kuhusu andiko hilo. Yehova alinitegemeza, nami hatimaye nikaushinda woga wangu.

Muda mfupi kabla ya kubatizwa, nilishangaa sana mume wangu alipoikataa kweli na kunitelekeza nikiwa na watoto saba. Hata hivyo, ndugu na dada walikuwa wazuri ajabu; walinisaidia kimwili na kiroho mimi na watoto wangu. Ndugu mmoja na mke wake kutoka nchi ya kigeni ambao walikuwa wakisafiri hadi Kampala kuhudhuria mikutano, walikuwa wakinichukua njiani mimi na watoto wangu katika gari lao. Nashukuru sana kwamba watoto wangu wanne pamoja na familia zao walichagua kumtumikia Yehova.

Baadaye, niliweza kufanya upainia wa kawaida. Ugonjwa wa yabisi ulipofanya iwe vigumu kwangu kutembea sana, nilikuwa nikiweka meza yenye vitabu nje ya nyumba yangu na kuzungumza na wapita njia. Kwa kufanya hivyo, niliweza kuendelea katika utumishi wa wakati wote.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 98, 99]

Mungu Alibariki Mavuno Yetu ya Kiroho

SAMUEL MUKWAYA

ALIZALIWA 1932

ALIBATIZWA 1974

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Kwa miaka mingi Samuel aliwakilisha tengenezo katika mambo ya kisheria, na pia alitumikia akiwa mzee na painia.

◼ SITASAHAU kamwe siku tuliyotembelea ofisi ya tawi ya Kenya huko Nairobi.

“Pini hizi zenye rangi tofauti-tofauti ni za nini?” nikauliza nilipokuwa nikitazama ramani ya Uganda.

“Haya ni maeneo yaliyo na watu wengi wenye kupendezwa,” akajibu Robert Hart, ndugu wa Halmashauri ya Tawi ya Kenya.

“Na hapa je, mtatuma mapainia lini?” nikauliza nikimwonyesha pini ya Iganga, nyumbani kwetu.

“Hatutumi mtu yeyote huko,” akasema. Kisha akanitazama kwa tabasamu na kusema, “Wewe ndiwe utakayekwenda huko.”

Nilishangazwa na jibu la Ndugu Hart kwa kuwa sikuwa painia, wala sikuwa nikiishi nyumbani. Hata hivyo, jambo hilo lilibaki akilini mwangu, na baada ya kustaafu, niliamua kurudi nyumbani na kuwa painia wa kawaida. Tulifurahi kuona kikundi kidogo cha wahubiri kikiongezeka na kuwa kutaniko kubwa lenye Jumba la Ufalme!

Patrick Baligeya alipotumwa Iganga akiwa painia wa pekee, tuliishi pamoja na kufanya upainia pamoja. Pia tulipanda mahindi ili kujitegemeza. Kila siku tulianza kwa kuchunguza andiko la siku, kisha kufanya kazi katika shamba la mahindi kwa saa kadhaa. Halafu mwendo wa saa nne hivi tukaanza utumishi hadi jioni.

Mahindi yetu yalipoanza kukua, baadhi ya majirani walidai kwamba tunapuuza shamba letu kwa sababu ya kazi ya kuhubiri. Tulijua kwamba mahindi yanahitaji kulindwa kwa sababu ya tumbili. Hata hivyo, hatukutaka kukatiza uvunaji wetu wa kiroho ili kufukuza tumbili.

Muda si muda tukaona mbwa koko wawili wakubwa karibu na shamba letu. Hatukujua wametoka wapi wala ni wa nani, lakini badala ya kuwafukuza, tukawa tukiwawekea chakula na maji kila siku. Hakuna tumbili waliokanyaga shamba letu maadamu mbwa hao walikuwapo. Kisha, baada ya majuma manne, mbwa hao wakatoweka ghafula, vile tu walivyokuja—nao ulikuwa wakati barabara kwa kuwa mahindi yetu hayakuwa hatarini! Tulimshukuru Yehova kwa mavuno tele tuliyopata. Zaidi ya yote, tulithamini sana kwamba Mungu alibariki mavuno yetu ya kiroho pia!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 101, 102]

Nilipotiwa Nguvuni, Yehova Alinipa Nguvu

PATRICK BALIGEYA

ALIZALIWA 1955

ALIBATIZWA 1983

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alianza utumishi wa wakati wote mara tu baada ya kubatizwa. Anatumikia akiwa mwangalizi anayesafiri pamoja na mke wake Symphronia.

◼ SERIKALI mpya ilipochukua mamlaka mwaka wa 1979, yeyote aliyekuwa na uhusiano wowote na serikali ya awali “aliombwa” aende kuzuizini. Kisha ikatangazwa kwamba yeyote asiyekubaliana na mpango huo angeonwa kuwa tisho na adui wa serikali hiyo mpya. Kwa sababu nilikuwa mwanamuziki katika jeshi, sikuwa na budi kwenda kizuizini.

Nikiwa kizuizini, nilijishughulisha kwa kusoma Biblia. Isitoshe, nilikuwa nikitafuta kweli nami nilipenda kuzungumza na wafungwa wenzangu kuhusu Biblia. Kizuizini, kulikuwa na Shahidi wa Yehova, John Mundua, aliyezuiliwa kwa sababu alikuwa mfanyakazi wa serikali naye alikuwa wa kabila lililoaminika kuwa linaunga mkono serikali ya awali.

John hakusita kunihubiria, nami nikaukubali mara moja ujumbe wa Ufalme. Tulikuwa na magazeti 16 tu ya Mnara wa Mlinzi na kitabu Good News—To Make You Happy,c lakini tangu mwanzo nilitambua kwamba mambo ninayojifunza ni kweli. Baada ya kujifunza Biblia kwa miezi mitatu, John aliona kuwa ninastahili kuwa mhubiri. Muda mfupi baadaye, aliondolewa mashtaka yote na kuachiliwa. Mawasiliano yangu pamoja na tengenezo la Yehova yakakatika. Hata hivyo, niliendelea kuongoza mafunzo kizuizini kwa kadiri ambavyo ningeweza.

Niliachiliwa Oktoba 1981. Nikarudi kijijini. Hakukuwa na Shahidi yeyote huko. Watu wa ukoo walijaribu kunishinikiza nijiunge na dini yao. Hata hivyo, Yehova aliona tamaa yangu ya kutaka kumtumikia naye akanitegemeza. Nilijua kwamba ninapaswa kufuata mfano wa Yesu. Kwa hiyo, nikaanza kuhubiri peke yangu, na baada ya muda usio mrefu nikawa nikiongoza mafunzo mengi. Siku moja mwenye nyumba alileta kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele na kusema, “Mambo unayosema yanalingana na mambo yaliyo katika kitabu hiki.”d huku akitoa kitabu Mtu huyo hakupendezwa sana na ujumbe wetu, mimi nami nilitaka sana kukisoma kitabu hicho pamoja na rundo la magazeti ya Mnara wa Mlinzi aliyokuwa nayo. Kwa hiyo, mtu huyo akakubali kunipa kitabu na magazeti hayo!

Hata hivyo, bado sikuwa nimekutana na Shahidi yeyote. Ndugu Mundua alikuwa ametaja kwamba kuna Mashahidi Jinja. Hivyo, nikaazimia kuwatafuta akina ndugu. Baada ya kusali karibu usiku kucha, nilirauka asubuhi na mapema na kuondoka hata bila kiamsha-kinywa. Mtu wa kwanza niliyekutana naye alikuwa na mfuko wa plastiki. Sikuamini macho yangu nilipoona gazeti la Amkeni! katika mfuko huo. Hatimaye nikawa nimempata mmoja wa ndugu zangu!

Mwaka wa 1984, nilifurahi kuhudhuria darasa la kwanza la Shule ya Utumishi wa Painia nchini Uganda. Wajua ni nani aliyehudhuria darasa hilohilo? Si mwingine ila John Mundua ndugu yangu mpendwa. Hadi leo hii, akiwa na umri wa miaka 74, anaendelea kutumikia kwa uaminifu akiwa painia wa kawaida.

[Maelezo ya Chini]

c Kilichokuwa kikichapishwa na Mashahidi wa Yehova. Hakichapishwi tena.

d Kilichokuwa kikichapishwa na Mashahidi wa Yehova. Hakichapishwi tena.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 113]

Hatimaye Aliipata Dini ya Kweli

Dada fulani alimwomba ndugu mmishonari, Mats Holmkvist, amtembelee Mutesaasira Yafesi. Alikuwa kasisi Msabato. Hata hivyo, alikuwa akipendezwa na ujumbe wa Mashahidi wa Yehova, naye alikuwa ametayarisha orodha ya maswali 20. Alipokutana na Mats akamkabidhi orodha hiyo.

Baada ya kuwa na mazungumzo ya Biblia kwa saa mbili, Mutesaasira akasema: “Hatimaye nimeipata dini ya kweli! Tafadhali usikose kuja kunitembelea kijijini. Kuna wengine pia ambao wangependa kujifunza kuhusu Mashahidi wa Yehova.”

Siku tano baadaye, Mats na mmishonari mwingine wakasafiri kwa pikipiki umbali wa kilomita 110 kupitia njia zenye matope katikati ya mashamba ya majani chai kwenda kumtembelea Mutesaasira katika kijiji cha Kalangalo. Akina ndugu walishangaa Mutesaasira alipowapeleka katika kibanda kilichoezekwa kwa nyasi ambacho kilikuwa na ishara “Jumba la Ufalme.” Tayari alikuwa amejenga kibanda ambacho kingeweza kutumiwa kwa ajili ya funzo la Biblia na mikutano!

Kulikuwa na watu wengine kumi waliopendezwa na kweli ambazo Mutesaasira alikuwa amewahubiria. Walianza kujifunza Biblia, na bila kujali umbali, Mats alijifunza nao mara mbili kwa mwezi. Watu hao walifanya maendeleo. Mbali na kutaniko lililo katika mji wa Mityana, katika kijiji cha Kalangalo watu zaidi ya 20 wamekuwa wahubiri. Naye Mutesaasira alifanya maendeleo haraka na kubatizwa. Sasa akiwa na umri wa miaka 70 na kitu, anatumikia akiwa mzee wa kutaniko.

[Ramani/Grafu katika ukurasa wa 108, 109]

MFUATANO WA MATUKIO—Uganda

1930

1931 Robert Nisbet na David Norman wahubiri Afrika Mashariki.

1940

1950

1950 Ndugu na Dada Kilminster wahamia Uganda.

1952 Kutaniko la kwanza laanzishwa.

1956 Ubatizo wa kwanza.

1959 Ndugu wa nchi za kigeni watoa msaada wa kiroho.

1960

1963 Wamishonari wawasili.

1972 Kusanyiko la kwanza la wilaya.

1973 Mashahidi wa Yehova wapigwa marufuku na wamishonari wafukuzwa.

1979 Marufuku yaondolewa.

1980

1982 Wamishonari waruhusiwa tena kuingia nchini.

1987 Gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kiganda laanza kutafsiriwa kwa ukawaida.

1988 Jumba la Ufalme la kudumu la kwanza lawekwa wakfu.

1990

2000

2003 Ofisi ya tawi yaanza kufanya kazi rasmi.

2007 Makao mapya ya ofisi ya tawi yawekwa wakfu.

2010

[Grafu]

(See publication)

Jumla ya Wahubiri

Jumla ya Mapainia

5,000

3,000

1,000

1930 1940 1950 1960 1980 1990 2000 2010

[Ramani katika ukurasa wa 73]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO

SUDAN

KENYA

UGANDA

KAMPALA

Arua

Gulu

Lira

Soroti

Ziwa Kyoga

Masindi

Hoima

Mbale

Tororo

Namaingo

Iganga

Jinja

Seta

Kajansi

Entebbe

Mityana

Kalangalo

Fort Portal

Rusese

Ziwa Albert

Mil. ya Ruwenzori

Ikweta

Ziwa Edward

Masaka

Mbarara

Kabale

KENYA

ZIWA VICTORIA

TANZANIA

BURUNDI

RWANDA

UGANDA

KAMPALA

KENYA

NAIROBI

Meru

Ml. Kenya

Mombasa

TANZANIA

DAR ES SALAAM

Zanzibar

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 87]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UGANDA

KAMPALA

Arua

Gulu

Lira

Soroti

Masindi

Hoima

Fort Portal

Masaka

Mbarara

Kabale

ZIWA VICTORIA

[Picha]

Ndugu Hardy na mke wake walizuru sehemu nyingi za Uganda kwa muda wa majuma sita

[Picha katika ukurasa wa 66]

[Picha katika ukurasa wa 69]

David Norman na Robert Nisbet walileta habari njema Afrika Mashariki

[Picha katika ukurasa wa 71]

George na Robert Nisbet na Gray na Olga Smith wakiwa na magari yao kwenye chelezo tayari kuvuka mto

[Picha katika ukurasa wa 75]

Mary na Frank Smith, kabla tu ya kufunga ndoa mwaka wa 1956

[Picha katika ukurasa wa 78]

Ann Cooke na watoto wake pamoja na Ndugu na Dada Makumba

[Picha katika ukurasa wa 80]

Tom na Bethel McLain, wamishonari wa kwanza kutoka Gileadi kutumwa nchini Uganda

[Picha katika ukurasa wa 81]

Makao ya kwanza ya wamishonari mjini Jinja

[Picha katika ukurasa wa 83]

Barbara na Stephen Hardy, wamishonari kutoka Gileadi

[Picha katika ukurasa wa 85]

Mary Nisbet (katikati) pamoja na wana wake Robert (kushoto), George (kulia), na William na mke wake, Muriel (nyuma)

[Picha katika ukurasa wa 89]

Tom Cooke akitoa hotuba kwenye Kusanyiko la Wilaya la “Utawala wa Kimungu” mjini Kampala

[Picha katika ukurasa wa 90]

George na Gertrude Ochola

[Picha katika ukurasa wa 94]

Licha ya marufuku, ndugu zetu waliendelea kukutanika pamoja

[Picha katika ukurasa wa 95]

Fred Nyende

[Picha katika ukurasa wa 96]

Emmanuel Kyamiza

[Picha katika ukurasa wa 104]

Stanley Makumba na mke wake, Esinala, mwaka wa 1998

[Picha katika ukurasa wa 107]

Heinz na Marianne Wertholz walihudhuria darasa la kwanza la Tanzu la Shule ya Gileadi nchini Ujerumani

[Picha katika ukurasa wa 118]

Vikundi vya Watafsiri

Kiganda

Kicholi

Kikonzo

Kinyankore

[Picha katika ukurasa wa 123]

Majumba ya Ufalme ya kisasa ni tofauti sana na majengo duni ya awali (kushoto)

[Picha katika ukurasa wa 124]

Ofisi ya Tawi ya Uganda

Halmashauri ya Tawi: Mats Holmkvist, Martin Lowum, Michael Reiss, na Fred Nyende; majengo ya ofisi (chini) na makao (kulia)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki