Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
MACHI 6-12
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 1 MAMBO YA NYAKATI 23-26
“Ibada Hekaluni Inapangwa kwa Utaratibu Mzuri”
it-2 241
Walawi
Wakati wa utawala wa Daudi, kazi ya Walawi ilipangwa kwa njia nzuri. Daudi aliwaweka rasmi wasimamizi wa kazi, maofisa, waamuzi, walinzi, watunza-hazina, na pia idadi kubwa ya Walawi ambao wangewasaidia makuhani kwenye hekalu, nyua za hekalu, na kwenye vyumba vya kulia chakula. Walawi hao wangewasaidia makuhani katika shughuli zilizohusu matoleo, dhabihu, kazi ya kutakasa, kupima uzito wa vitu mbalimbali, na pia kazi ya ulinzi. Wanamuziki Walawi walikuwa wamepangwa katika vikundi 24, kama tu ilivyokuwa kwa makuhani, na walitumika kwa zamu. Kazi zilipangwa kwa kupiga kura. Kuhusu vikundi vya walinzi, migawo ya milango mbalimbali ilipangwa kwa kupiga kura.—1Nya 23, 25, 26; 2Nya 35:3-5, 10.
it-2 686
Kuhani
Katika utumishi wa hekaluni makuhani walipangwa katika vikundi vilivyosimamiwa na maofisa. Kura zilipigwa ili kupanga migawo mbalimbali. Zamu ya kila kikundi kwenye vile vikundi 24 ilikuwa na urefu wa juma moja, na walipangiwa zamu mara mbili kwa mwaka. Inaelekea makuhani wote walitumikia wakati wa sherehe kwa sababu watu walitoa maelfu ya dhabihu, kama ilivyokuwa wakati hekalu lilipowekwa wakfu. (1Nya 24:1-18, 31; 2Nya 5:11; linganisha 2Nya 29:31-35; 30:23-25; 35:10-19.) Kuhani angeweza kutumikia nyakati nyingine pia, muradi tu, asiingilie kazi ya makuhani waliokuwa wamepewa zamu. Kulingana na desturi za kirabi, wakati Yesu alikuwa duniani, makuhani walikuwa wengi, basi familia mbalimbali zilizokuwa katika kikundi kimoja ziligawana utumishi wa juma lao, na kila familia ingeweza kutumikia siku moja au zaidi ikitegemea idadi yao.
it-2 451-452
Muziki
Pamoja na maandalizi mengine ambayo Daudi alifanya kwa ajili ya hekalu la Yehova, Daudi aliwateua Walawi 4,000 kwa ajili ya utumishi wa kumsifu Mungu kupitia muziki. (1Nya 23:4, 5) Kati yao kulikuwa na Walawi 288 “waliozoezwa kumwimbia Yehova, wote wakiwa stadi.” (1Nya 25:7) Mpango huo mzima ulikuwa chini ya usimamizi wa wanamuziki watatu bora, yaani, Asafu, Hemani, na Yeduthuni (ambaye inaelekea aliitwa pia Ethani). Wanaume hao ni wazao wa wana watatu wa Lawi: Asafu alikuwa mzao wa Gershomu, Hemani alikuwa mzao wa Kohathi, na Yeduthuni alikuwa mzao wa Merari. Hivyo basi, familia tatu kuu za Walawi ziliwakilishwa katika mpangilio wa muziki hekaluni. (1Nya 6:16, 31-33, 39-44; 25:1-6) Asafu, Hemani, na Yeduthuni walikuwa na jumla ya wana 24, na wana hao walikuwa miongoni mwa wanamuziki stadi 288 waliotajwa hapo juu. Kila kikundi kilisimamiwa na mmoja wa wana hao aliyechaguliwa kwa kupiga kura. Chini ya msimamizi huyo kulikuwa na ‘waimbaji stadi’ 11, idadi iliyotia ndani watoto wake na pia Walawi wengine. Hivyo basi, ili kupata wanamuziki stadi 288 tunafanya ([1 + 11] × 24 = 288), kama ilivyokuwa kwa makuhani, wanamuziki hao pia walipangwa katika vikundi 24. Waimbaji wote walikuwa 4,000. Kati yao, 288 walikuwa wanamuziki stadi na 3,712 walikuwa ‘wanafunzi.’ Ukigawa wanafunzi hao kwa vikundi vyote 24, unapata kwa wastani waimbaji 155 kwa kila kikundi, inamaanisha kwamba kwa kila mwanamuziki stadi kulikuwa na Walawi 13 hivi waliokuwa na uzoefu tofauti-tofauti kimuziki. (1Nya 25:1-31) Ingawa makuhani walikuwa wapiga-tarumbeta, hawakujumuishwa pamoja na wanamuziki Walawi.—2Nya 5:12; linganisha Hes 10:8.
it-1 898
Mlinzi
Hekaluni. Muda mfupi kabla ya kifo chake, Mfalme Daudi aliwapanga vizuri Walawi na wafanyakazi wengine wa hekalu, kutia ndani walinzi ambao walikuwa 4,000. Kila kikundi kilikuwa na zamu ya siku saba. Walikuwa na wajibu wa kulinda nyumba ya Yehova na kuhakikisha kwamba malango yamefunguliwa na kufungwa wakati unaofaa. (1Nya 9:23-27; 23:1-6) Zaidi ya kufanya kazi ya ulinzi, baadhi yao walikusanya michango ambayo watu walileta kwa ajili ya matumizi ya hekalu. (2Fa 12:9; 22:4) Baadaye, kuhani mkuu Yehoyada alipomtia mafuta Yehoashi kuwa mfalme, walinzi wa pekee walipewa mgawo wa kulinda malango ya hekalu ili kumlinda Yehoashi aliyekuwa na umri mdogo asiuawe na Malkia Athalia aliyekuwa amenyakua ufalme. (2Fa 11:4-8) Mfalme Yosia, alipofanya kampeni ya kuondoa ibada ya sanamu, walinzi wa milango walisaidia kuondoa hekaluni vyombo ambavyo vilikuwa vikitumiwa katika ibada ya Baali. Vyombo hivyo viliteketezwa nje ya jiji.—2Fa 23:4.
MACHI 20-26
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 1-4
“Mfalme Sulemani Anafanya Uamuzi Usio wa Hekima”
it-1 174 ¶5
Jeshi
Utawala wa Sulemani ulileta mabadiliko katika historia ya jeshi la Israeli. Kwa ujumla, kulikuwa na amani alipotawala lakini bado alikusanya farasi na magari ya vita. (Ona GARI LA VITA.) Alinunua wengi kati ya farasi hao huko Misri. Walilazimika kujenga majiji makubwa kotekote katika eneo alilotawala ili kuwaweka farasi hao na magari hayo. (1Fa 4:26; 9:19; 10:26, 29; 2Nya 1:14-17) Hata hivyo, Yehova hakubariki mradi huo wa Sulemani, alipokufa na utawala wake kugawanywa, jeshi la Israeli lilidhoofika. Baadaye Isaya aliandika hivi: “Ole wao wanaoshuka kwenda Misri kutafuta msaada, wanaotegemea farasi, wanaotumaini magari ya vita kwa sababu ni mengi, na farasi wa vita kwa sababu wana nguvu. Lakini hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli, na hawamtafuti Yehova.”—Isa 31:1.
it-1 427
Gari la Vita
Kabla ya utawala wa Sulemani, jeshi la Israeli lilikuwa na magari machache tu ya vita. Hali ilikuwa hivyo hasa kwa sababu Mungu aliwaonya wafalme wasijipatie farasi wengi, kwa kuwa usalama wa taifa haukutegemea wingi wa farasi. Kwa sababu ya sheria hiyo hakungekuwa na magari mengi ya vita kwani yalikokotwa na farasi. (Kum 17:16) Samueli aliwaonya watu kuhusu madhara ambayo wafalme wa kibinadamu wangewaletea. Aliwaambia: “Atawachukua wana wenu na kuwafanya wawe waendeshaji wa magari yake ya farasi.” (1Sa 8:11) Absalomu na pia Adoniya walipotaka kunyakua ufalme, kila mmoja wao alijitengenezea gari la vita, na kulikuwa na watu 50 wa kukimbia mbele yake. (2Sa 15:1; 1Fa 1:5) Daudi alipomshinda mfalme wa Soba, aliwahifadhi farasi 100 waliokokota magari.—2Sa 8:3, 4; 10:18.
Mfalme Sulemani alipopanua jeshi la Israeli, aliongeza idadi ya magari ya vita kufikia 1,400. (1Fa 10:26, 29; 2Nya 1:14, 17) Zaidi ya Yerusalemu, kulikuwa na majiji mengine pia yaliyoitwa majiji ya magari ya vita yaliyokuwa yameandaliwa ili kutunza zana hizo za vita.—1Fa 9:19, 22; 2Nya 8:6, 9; 9:25.
MACHI 27–APRILI 2
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 5-7
“Moyo Wangu Utakuwa Humo Sikuzote”
it-2 1077-1078
Hekalu
Historia. Hekalu hili lilikuwepo hadi mwaka wa 607 K.W.K., ambapo liliharibiwa na jeshi la Babiloni likiongozwa na Mfalme Nebukadneza. (2Fa 25:9; 2Nya 36:19; Yer 52:13) Kwa sababu taifa la Israeli lilianguka tena na tena kwenye ibada ya sanamu, Mungu aliruhusu mataifa mbalimbali kudhalilisha Yuda na Yerusalemu, na hata wakati mwingine walipora hazina za hekalu. Wakati mwingine, hekalu halikutunzwa hata kidogo. Mfalme Shishaki wa Misri alipora hazina za hekalu (993 K.W.K.) katika siku za Rehoboamu mwana wa Sulemani, miaka 33 tu baada ya hekalu hilo kuzinduliwa. (1Fa 14:25, 26; 2Nya 12:9) Mfalme Asa (977-937 K.W.K.) aliheshimu nyumba ya Yehova, hata hivyo, akiwa na nia ya kulinda Yerusalemu alitenda bila hekima alipomhonga Mfalme Ben-hadadi I wa Siria kwa kumpa fedha na dhahabu kutoka kwenye hazina za hekalu, ili mfalme huyo avunje agano alilokuwa amefanya pamoja na Baasha, mfalme wa Israeli.—1Fa 15:18, 19; 2Nya 15:17, 18; 16:2, 3.
APRILI 10-16
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 8-9
“Alithamini Hekima”
it-2 990-991
Sulemani
Malkia alipoona utukufu wa hekalu na wa nyumba ya Sulemani, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi huduma ya vinywaji ilivyokuwa, mavazi ya watumishi waliohudumu mezani, na dhabihu za kuteketezwa alizotoa kwa ukawaida hekaluni, “alipigwa na bumbuazi.” Alichochewa kusema: “Kwa kweli sikuwa nimeambiwa hata nusu yake. Hekima yako na ufanisi wako umezidi kwa mbali habari nilizosikia.” Kisha akasema kwamba watumishi wa Sulemani walikuwa wenye furaha kwa sababu walitumikia mfalme kama huyo. Mambo hayo yote yalimchochea malkia huyo kumsifu Yehova, kumbariki Yehova Mungu, ambaye alilionyesha taifa la Israeli upendo wake kwa kumweka rasmi Sulemani awe mfalme wao ili atekeleze haki na uadilifu.—1Fa 10:4-9; 2Nya 9:3-8.
Hazina za Kiroho
it-2 1097
Kiti cha Ufalme
Kati ya wafalme wa Israeli, ni Sulemani tu ambaye kiti chake cha ufalme kimefafanuliwa kwa kina. (1Fa 10:18-20; 2Nya 9:17-19) Inaelekea kiti hicho cha ufalme kilikuwa kwenye “Ukumbi wa Kiti cha Ufalme,” mojawapo ya majengo yaliyokuwa juu ya Mlima Moria jijini Yerusalemu. (1Fa 7:7) Kiti hicho cha ufalme ‘kilikuwa kikubwa na kilitengenezwa kwa pembe za tembo na kufunikwa kwa dhahabu safi, kilikuwa na kifuniko cha mviringo mgongoni, na mikono pande zote mbili.’ Ingawa kuna uwezekano kwamba kiti hicho kilitengenezwa hasa kwa pembe za ndovu, inaelekea kwamba mbinu waliyotumia kukijenga ilikuwa sawa na ile iliyotumiwa katika ujenzi hekaluni, hivyo basi, inaonekana kwamba, kwanza kilitengenezwa kwa mbao, kisha walitumia pembe za ndovu na hatimaye kikafunikwa kwa dhahabu safi. Kwa mtazamaji, ilionekana kana kwamba kiti hicho kimetengenezwa kwa pembe za ndovu na dhahabu tu. Baada ya kutaja kwamba kiti hicho cha ufalme kilikuwa na ngazi sita, tunapata ufafanuzi huu mwingine: “Simba wawili walisimama kando ya mikono hiyo. Na kulikuwa na simba 12 waliosimama kwenye ngazi hizo sita, wawili kwenye kila ngazi, mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.” (2Nya 9:17-19) Kwa kawaida, simba wanawakilisha mamlaka ya utawala. (Mwa 49:9, 10; Ufu 5:5) Huenda wale simba 12 waliwakilisha makabila 12 ya Israeli, na labda pia walionyesha kwamba makabila hayo yalijitiisha kwa mtawala aliyeketi kwenye kiti hicho na walimuunga mkono. Kwa njia moja au nyingine kiti cha miguu cha dhahabu kilikuwa kimeunganishwa na kiti cha ufalme. Ufafanuzi huo unaonyesha kwamba kiti cha ufalme kilichotengenezwa kwa pembe za ndovu na dhahabu—chenye utukufu, na chenye kifuniko cha mviringo mgongoni pamoja na simba mbele yake—kilikuwa bora zaidi kuliko kiti kingine chochote cha ufalme cha wakati huo, iwe kiligunduliwa na wavumbuzi wa kiakiolojia, au kilikuwa kwenye michoro au maandishi fulani ya wakati huo. Mwandishi wa kitabu cha Mambo ya Nyakati alisema hivi kwa usahihi: “Hakuna ufalme mwingine wowote uliokuwa umetengeneza kiti kama hicho.”—2Nya 9:19.
APRILI 17-23
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 2 MAMBO YA NYAKATI 10-12
“Nufaika Kutokana na Ushauri Wenye Hekima”
it-2 768 ¶1
Rehoboamu
Rehoboamu alikuwa mwenye kiburi na alitumia mamlaka yake kimabavu, bila kuwajali wengine. Kwa hiyo, watu wengi walijitenga na ufalme wake. Makabila pekee yaliyoendelea kuunga mkono nyumba ya Daudi yalikuwa ni kabila la Yuda na la Benjamini, na pia makuhani na Walawi wa falme zote mbili, pamoja na watu wachache kutoka kwenye yale makabila kumi.—1Fa 12:16, 17; 2Nya 10:16, 17; 11:13, 14, 16.
Hazina za Kiroho
it-1 966-967
Roho Waovu Wenye Umbo la Mbuzi
Maneno ya Yoshua kwenye Yoshua 24:14 yanaonyesha kwamba Waisraeli waliathiriwa kwa kiasi fulani na ibada ya uwongo ya Wamisri kwa kipindi walichokuwa huko. Ezekieli alionyesha kwamba waliendelea kuanguka tena na tena kwenye ibada ya sanamu muda mrefu baada ya hapo. (Eze 23:8, 21) Kwa sababu hiyo, wasomi fulani wanasema kwamba amri iliyotolewa na Mungu kwa Waisraeli wakiwa nyikani kuwazuia “kutoa dhabihu zao kwa roho waovu wenye umbo la mbuzi” (Law 17:1-7) na pia Yeroboamu kuweka makuhani “ili wahudumu mahali pa juu na kuwatumikia roho waovu wenye umbo la mbuzi na ndama aliokuwa ametengeneza” (2Nya 11:15) kunaonyesha kwamba kulikuwa na aina fulani ya ibada ya mbuzi miongoni mwa Waisraeli. Ibada hiyo ilienea sana huko Misri, hasa kwenye Misri ya Chini. Herodotus (II, 46) anadai kwamba ni kutoka kwa ibada ya Misri ambapo Wagiriki walipata imani katika mungu Pan na pia katika satyrs, yaani, miungu wa misituni waliokithiri kwenye ukosefu wa maadili, ambao hatimaye walichorwa wakiwa na pembe, mkia wa mbuzi, na miguu ya mbuzi. Wasomi fulani wanasema kwamba kwa sababu miungu wa kipagani walidhaniwa kuwa nusu mnyama na nusu mwanadamu, dhana hiyo ilifanya Shetani pia achorwe akiwa na mkia, pembe, na kwato, na ilikuwa hivyo hasa miongoni mwa Wakristo wa Enzi za Giza.
Hata hivyo, haijasemwa wazi neno [hilo la Kiebrania, seʽi·rimʹ, yaani kihalisi,] “wenye manyoya” linarejelea nani hasa. Ingawa wasomi fulani wanasema kwamba wanarejelea mbuzi halisi au sanamu zilizokuwa na umbo la mbuzi, hakuna uthibitisho; maandiko mengine pia hayatoi uthibitisho wowote kwamba wazo hilo ni sahihi. Huenda maneno hayo yakaonyesha tu kwamba katika akili za wale walioabudu miungu hiyo ya uwongo, walifikiri kwamba miungu hiyo ilikuwa na umbo la mbuzi na ilikuwa yenye nywele nyingi mwilini. Au pia, huenda neno “mbuzi” katika maandiko hayo likatumiwa tu kuonyesha kwamba sanamu zote kwa ujumla zinadharaulika. Kwa mfano, katika maandiko mengi neno linalotumiwa kwa ajili ya sanamu linatokana na neno ambalo kihalisi linamaanisha “mavi,” hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba kiasili sanamu zilikuwa zimetengenezwa kwa mavi.—Law 26:30; Kum 29:17.