Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
© 2024 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
MACHI 24-30
HAZINA ZA NENO LA MUNGU METHALI 6
Tunaweza Kujifunza Nini Kutoka kwa Chungu?
it-1 115 ¶1-2
Chungu
‘Hekima ya Kisilika.’ ‘Hekima’ ya chungu haitokani na kufikiri kwa kutumia akili bali inatokana na uwezo wa asili ambao wamepewa na Muumba. Biblia inasema kwamba chungu “hutayarisha chakula chake wakati wa kiangazi, na kukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” (Met 6:8) Aina moja ya chungu wanaopatikana kwa wingi zaidi nchini Palestina ni chungu wanaorejelewa kama wavunaji, au wakulima (Messor semirufus). Chungu hao huhifadhi kiasi kikubwa cha nafaka wakati wa majira ya kuchipua na ya kiangazi, kisha wanakitumia wakati wa majira ambayo ni vigumu kupata chakula, kutia ndani majira ya baridi kali. Mara nyingi, chungu huyo hupatikana karibu na uwanja wa kupuria kwa kuwa huko kuna mbegu na nafaka nyingi. Ikiwa mvua itafanya mbegu zilizohifadhiwa na chungu huyo ziloane, chungu hao wavunaji hubeba nafaka hizo na kuzianika juani ili zikauke. Mbali na hilo, ili kuizuia mbegu isichipuke inapokuwa katika hifadhi yao, wao hutafuna sehemu ya mbegu ambayo uchipukaji huanzia. Mtu anaweza kufahamu mahali ambapo chungu hao wavunaji wanaishi kwa kuangalia vijia vyao vinavyoonekana waziwazi na pia kwa kutafuta maganda ya mbegu yaliyo nje ya mwingilio wa nyumba zao.
Sifa za Kuiga. Kuchunguza chungu kunatusaidia kuelewa umuhimu wa himizo hili: “Mwendee chungu, ewe mvivu; zichunguze njia zake uwe na hekima.” (Met 6:6) Mbali tu na uwezo wao unaovutia wa kisilika wa kujitayarisha kwa ajili ya wakati ujao, tunavutiwa pia na uthabiti na ustahimilivu wao. Mara nyingi wao hubeba au kuvuta vitu ambavyo ni mara mbili ya uzito wao au zaidi, wanafanya yote wanayoweza kukamilisha kazi fulani, na kukataa kurudi nyuma hata wanapoanguka, kuteleza, au kubingirika kutoka kwenye mwinuko mkali. Kwa kuwa wana ushirikiano sana, wao huhakikisha nyumba zao ni safi kabisa na wanawajali wafanyakazi wenzao, hata nyakati nyingine wanawasaidia chungu waliochoka au waliojeruhiwa kurudi nyumbani.
APRIL 21-27
HAZINA ZA NENO LA MUNGU METHALI 10
Utajiri wa Kweli Maishani Unapatikanaje?
it-1 340
Baraka
Yehova Huwabariki Wanadamu. “Baraka ya Yehova ndiyo inayomtajirisha mtu, naye haichanganyi na maumivu.” (Met 10:22) Yehova huwabariki wale walio na kibali chake kwa kuwalinda, kuwaletea ufanisi, kuwaongoza, kuwapa mafanikio, na kuwapa mahitaji yao, na matokeo ni kwamba wanapata faida maishani mwao.