Iceland
Unapofikiria Iceland huenda ukawazia nchi yenye barafu, theluji, na nyumba za barafu. Na hata unapotazama ramani huenda ukafikiri kwamba nchi hiyo ni yenye baridi kali mno, kwani iko mbali sana upande wa kaskazini, karibu na Mzingo wa Aktiki. Si watu wengi wanaoishi katika sehemu za kaskazini kama Iceland.
Hata hivyo, ingawa Iceland iko karibu na Mzingo wa Aktiki na jina lake linamaanisha nchi ya barafu, nchi hiyo haina baridi kali sana. Baridi hupunguzwa na mkondo wa bahari wenye joto unaoanzia karibu na ikweta. Hakuna nyumba za barafu nchini humo. Nchi hiyo imeendelea sana, na watu huishi katika nyumba za kisasa zinazopashwa joto kwa mitambo inayotumia mvuke na maji ya moto kutoka ardhini.
Kuna mambo mengi yenye kushangaza nchini Iceland. Katikati ya majira ya baridi kali, jua huchomoza kwa saa chache tu kila siku na usiku huwa mrefu. Katika majira hayo mianga ya kaskazini hutokea mara kwa mara, lakini ni kana kwamba jua halitaki kutokea hata kidogo. Kwa upande mwingine, katika majira ya joto, jua huangaza mchana na usiku. Katika sehemu ya kaskazini kabisa ya nchi hiyo, jua halitui kwa majuma kadhaa, na unaweza kuliona hata usiku wa manane.
Iceland huitwa nchi ya barafu na moto, na jina hilo linafaa. Barafu imefunika asilimia kumi hivi ya nchi hiyo. Pia kuna moto, kwa kuwa huko volkeno hulipuka mara nyingi, na mvuke hutoka ardhini katika sehemu nyingi. Kumekuwa na milipuko mingi ya volkeno, na katika karne kadhaa zilizopita milipuko hiyo imetokea kila baada ya miaka mitano au sita hivi. Vilevile kuna chemchemi nyingi za maji ya moto.
Nchi hii yenye watu wachache ina mazingira mazuri na wanyama wengi wa mwituni. Watalii wengi huvutiwa na hewa safi, maporomoko ya maji, milima yenye mawemawe, na nyika kubwa. Baada ya majira ya baridi kali, ndege wahamaji hurudi katika makao yao ya majira ya joto kwenye majabali ya pwani na maeneo yenye majimaji. Mmojawapo wa ndege hao ni buabua wa Aktiki, ambaye huhama kila mwaka kwenda Antaktiki, eneo la kusini kabisa la dunia. Ndege wa baharini aina ya puffin, somateria, na shakwe-bahari, huonekana kotekote kwenye majabali ya pwani. Kondoo hulisha mashambani, na farasi wadogo wa Iceland wanaostahimili baridi kali, hurandaranda milimani. Mapema katika majira ya joto, maelfu ya samaki aina ya samoni hurudi ili kutaga mayai, nao hurukaruka katika mito na maporomoko ya maji.
Maharamia Waskandinavia ndio mababu wa wenyeji 290,570 wa Iceland. Maharamia hao walihamia katika kisiwa hicho zaidi ya miaka 1,100 iliyopita. Wengi wao walitoka Norway nao waliongea lugha ya kale ya Waskandinavia. Lugha ya wenyeji wa Iceland ambayo imetokana na lugha hiyo ya Waskandinavia, haijabadilika kwa sababu nchi hiyo iko mbali kidogo na nchi nyingine na pia kuna vitabu vingi vya zamani katika lugha hiyo. Kwa hiyo, leo watu wanaweza kusoma hadithi za kale zilizoandikwa katika miaka ya 1200 hasa. Wenyeji wa Iceland wanajivunia lugha yao, nao hawapendi kuichanganya na maneno ya kigeni.
Watu wengi waliohamia nchi hiyo zamani za kale walikuwa “wapagani,” na jitihada za kwanzakwanza za kubadili dini ya watu wa Iceland wawe “Wakristo” zilifanywa mwishoni mwa miaka ya 900. Baadhi ya viongozi mashuhuri wa Iceland walibadili dini wakawa “Wakristo” mwishoni mwa karne hiyo, na katika mwaka wa 1000, bunge la Iceland, lilimwomba mmojawapo wa viongozi mashuhuri wa dini ya kipagani aamue ni dini gani iliyo bora. Kwa kustaajabisha, aliamua kwamba dini moja tu ilipaswa kufuatwa, yaani, “Ukristo.” Yaelekea, jambo hilo lilikubaliwa bila upinzani. Hata hivyo, agizo lake liliwaruhusu watu kuabudu miungu ya kipagani kisirisiri na kuendelea na desturi za kipagani. Ijapokuwa uamuzi huo ulitokana na masuala ya kisiasa hasa wala si ya kidini, huenda ulichangia kuwafanya wenyeji wa Iceland kuwa watu wenye kujiamulia mambo, walio tayari kukubali mawazo mapya kuhusu dini.
Leo, asilimia 90 hivi ya watu wa Iceland ni wafuasi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, ambalo ndilo kanisa la taifa. Karibu watu wote wana Biblia nyumbani, lakini si wengi wanaoamini kwamba Biblia ni Neno la Mungu.
Habari Njema Yafika Iceland
Mapema katika miaka ya 1900, wenyeji wengi wa Iceland walikuwa wamehamia Kanada kwa sababu ya magumu yaliyosababishwa na milipuko ya volkeno, baridi kali, na matatizo mengineyo. Baadhi yao walihubiriwa habari njema ya Ufalme wa Mungu kwa mara ya kwanza huko Kanada. Mmoja wao ni Georg Fjölnir Lindal ambaye alianza kufanya utumishi wa wakati wote muda mfupi baada ya kujiweka wakfu kwa Yehova Mungu. Ndugu Lindal alijua lugha ya Iceland, kwa hiyo, mwaka wa 1929, alipokuwa na umri wa miaka 40, aliamua kuhamia Iceland. Alifika Reykjavík Juni 1 mwaka huo, naye ndiye mtu wa kwanza kuhubiri habari njema nchini Iceland.
Ndugu Lindal alingoja kwa miezi mitatu ili vitabu vyake vifike, lakini mara vilipofika alianza kuhubiri akiwa na lengo la kumfikia kila mtu nchini humo. Mwishoni mwa mwezi wa Oktoba mwaka wa 1929, alikuwa amegawa nakala 800 za kitabu kimoja cha kujifunzia Biblia (The Harp of God), katika lugha ya Iceland. Wakati huo, aliandika hivi: “Tangu nilipofika, nimehubiri katika miji kadhaa yenye jumla ya watu 11,000 hivi. Iceland ina watu 100,000 hivi au zaidi, kwa hiyo kuna watu wengine wapatao 90,000 ambao ni lazima wahubiriwe pia. Itachukua muda mrefu kwa mtu mmoja kuwahubiria watu wote kwenye eneo hili, kwa sababu si rahisi kusafiri nchini humu. Iceland ni nchi yenye milima mingi na pwani yenye ghuba nyingi ndogo-ndogo. Hakuna magari-moshi, na barabara nzuri ni chache, kwa hiyo mara nyingi nimekuwa nikisafiri kwa meli.”
Hakuna malalamiko yoyote katika barua chache alizoandika kwa mkono, ambazo zimehifadhiwa katika faili yenye jina “Iceland.” Katika ile barua aliyoandika mwaka wa 1929, Ndugu Lindal alisema: “Ninafurahi sana kueleza juu ya jambo moja lenye kutia moyo lililotukia hivi majuzi. Nilipata nafasi ya kurudi mahali fulani ambapo nilikuwa nimehubiri. Nilikutana na watu kadhaa ambao walikuwa wamenunua vitabu nilipohubiri huko kwa mara ya kwanza. Mtu mmoja alisema hivi: ‘Nimesoma kitabu (Harp) mara mbili, na sasa ninakisoma kwa mara ya tatu. Ni kitabu kizuri. Asante kwa kunitembelea.’ Mwingine alisema hivi: ‘Kumbe umerudi. Kile kitabu ni kizuri sana. Mbona msichapishe vitabu vyote vya Hakimu Rutherford katika lugha ya Iceland?’ Nilimwambia kwamba vitabu vingi vya Ndugu Rutherford vinapatikana katika Kidenishi, naye akasema: ‘Niletee vyote ulivyo navyo, hata vitabu vya Pasta Russell, nami nitakuwa na vitabu vya kutosha kusoma katika majira yajayo ya baridi kali.’ Wengine walinishukuru kwa vitabu hivyo. Ninamshukuru Mungu kwa kuniruhusu kuwahubiria watu walio tayari kusikiliza ujumbe kuhusu ile kweli.”
Ilikuwa kazi kubwa mno kwa mtu mmoja kumhubiria kila mtu kwenye kisiwa hicho ambacho kwa ukubwa ni nusu ya eneo la Uingereza. Iceland ina urefu wa kilometa 300 hivi kutoka kaskazini hadi kusini, na kilometa 500 hivi kutoka mashariki hadi magharibi. Pwani yake ina urefu wa kilometa 6,400 hivi, nayo ina ghuba nyingi ndogo-ndogo. Hata hivyo, baada ya miaka kumi, Ndugu Lindal alikuwa amehubiri habari njema na kuwaachia watu vitabu kotekote kisiwani humo. Alisafiri kwa meli alipohubiri sehemu za pwani, na kutumia farasi wawili wadogo alipowatembelea wakulima mashambani. Farasi mmoja alimbeba Ndugu Lindal, na yule mwingine alibeba vitabu na mizigo yake. Ndugu waliopata nafasi ya kushirikiana na Ndugu Lindal kabla hajaondoka Iceland, wanasema kwamba alikuwa mtu mwaminifu, mwenye haya na mkimya, naye alichukua mambo kwa uzito. Alikuwa mtu mkubwa na mrefu hivi kwamba haikuwa rahisi kwa farasi wadogo wa Iceland kumbeba. Nyakati nyingine alipokosa farasi, Lindal alijibebea vitabu na mizigo.
Ndugu Lindal alipoanza kuhubiri huko Iceland mwaka wa 1929, hakujua kwamba angehitaji kuwa mvumilivu na mstahimilivu sana kabla ya kupata matokeo. Kwa muda wa miaka 18 hivi, Ndugu Lindal alikuwa Shahidi pekee nchini Iceland. Licha ya bidii yake, hakuna mtu hata mmoja aliyekubali Ujumbe wa Ufalme katika muda huo wote. Aliandika hivi mwaka wa 1936: “Tangu nifike Iceland, nimewaachia watu vitabu 26,000 au 27,000 hivi. Watu wengi wamevisoma. Yaonekana watu kadhaa wameamua kukataa kweli, lakini walio wengi hawajali hata kidogo.”
Hata hivyo, baadhi ya watu walithamini ujumbe aliowahubiria. Kwa mfano, mzee mmoja alikubali kitabu kimoja cha kujifunzia Biblia (The Harp of God). Ndugu Lindal alipomrudia miezi kadhaa baadaye, alikutana na binti ya mzee huyo aliyemwambia kwamba baba yake alikipenda kitabu hicho na alikisoma kwa makini kabla ya kufa. Kupatana na desturi fulani ya kipagani, alikuwa ameomba kitabu hicho kiwekwe ndani ya jeneza pamoja naye, nalo ombi lake likatekelezwa.
Hatimaye, mnamo Machi 25, 1947, wahitimu wa Shule ya Biblia ya Gileadi walifika Iceland na kujiunga na Ndugu Lindal ambaye alikuwa amekaa humo peke yake kwa muda mrefu. Aliendelea na utumishi wake nchini humo hadi aliporudi Kanada mwaka wa 1953. Miaka 16 baadaye, Páll Heine Pedersen, aliyekuwa painia wa pekee huko Iceland, aliamua kusafiri hadi Winnipeg, Kanada, kumwona Ndugu Lindal. Alitaka amweleze kuhusu kazi yake ya kuhubiri nchini Iceland, kwa kuwa wamishonari waliohubiri pamoja na Ndugu Lindal walikuwa wameondoka nchini. Alipokuwa likizoni huko Marekani, Ndugu Pedersen alisafiri kwa basi hadi Winnipeg. Lakini, alipofika alijulishwa kwamba Ndugu Lindal, aliyekuwa na tumaini la kwenda mbinguni, alikuwa amekufa asubuhi hiyo. Alikuwa amemtumikia Yehova kwa uaminifu hadi kifo.
Wavunaji Wengine
Kipindi kipya cha kuhubiri habari njema kilianza mwaka wa 1947, wakati wamishonari wa kwanza wawili kutoka Denmark, waliokuwa wamehitimu Shule ya Gileadi, walipofika. Mmoja wao ni Leo Larsen. Wamishonari wengine wawili, Ingvard Jensen kutoka Denmark na Oliver Macdonald kutoka Uingereza, walifika mwezi wa Desemba mwaka wa 1948. Wavunaji hao wapya waliendelea na kazi ambayo Ndugu Lindal alianzisha na waliwaachia watu vitabu vingi sana. Wakati wa majira ya baridi kali walihubiri jijini Reykjavík na maeneo yaliyokuwa karibu, na wakati wa majira mafupi ya joto walihubiri kwenye maeneo ya mashambani ya pwani. Ingvard Jensen anakumbuka pindi moja waliposafiri kwenda kuhubiri. Aliandika: “Katika majira ya joto ya kwanza nilipokuwa Iceland, nilijiunga na mmishonari mwingine katika safari ya kuhubiri mashambani. Kwa kawaida tulisafiri kwa basi au meli hadi eneo ambalo tulikuwa tumeamua kwenda kuhubiri, na tulibeba baiskeli, mahema, mifuko ya kulalia, vitabu, na chakula. Hivyo, jioni moja tulisafiri kwa meli kwenda katika mji wa Stykkishólmur, ulio kwenye pwani ya magharibi. Tulifika huko alasiri siku iliyofuata. Lengo letu lilikuwa kutembelea kila nyumba mjini humo kisha kusafiri kwa baiskeli hadi mji wa Borgarnes, umbali wa kilometa 100 hivi kutoka Stykkishólmur. Kulikuwa na meli iliyosafiri kila siku kutoka Borgarnes hadi Reykjavík. Safari hiyo ilianza vizuri. Ilikuwa katikati ya mwezi wa Juni na jua lilikuwa limewaka. Usiku wa kwanza tuliingia katika mifuko yetu ya kulalia baada ya kuhubiri katika sehemu fulani ya mji huo. Hata hivyo, tulisikia baridi sana usiku, na asubuhi tukagundua kwamba theluji yenye kina cha sentimeta kumi ilikuwa imeanguka usiku huo! Hatukuweza kurudi nyumbani, kwa kuwa meli ilifika kwenye mji huo mara moja tu kwa juma. Kwa hiyo, ilitubidi kufuata ratiba yetu, yaani, kuhubiri kwenye sehemu zote za mji huo, kisha kusafiri kwa baiskeli kwenye barabara ya milimani hadi mji uliofuata, huku tukiwahubiria wakulima walioishi karibu na barabara hiyo.”
Walifika Borgarnes siku nne baadaye. Walisafiri kwa baiskeli huku mvua iliyochanganyika na theluji ikinyesha na upepo ukivuma kilometa 100 hivi kwa saa. Hata hivyo, hawakufikiria sana hali hiyo mbaya ya hewa, kwa sababu wakulima waliowahubiria walikuwa wakarimu sana na sikuzote waliwakaribisha kwa kahawa na chakula. Ndugu Jensen anakumbuka kwamba walikula mara nane hadi kumi kila siku! Alisema: “Nilifikiri tungewaudhi watu hao kama tungekataa chakula, na tulitumia nafasi hiyo kuwahubiria kuhusu Ufalme wa Yehova uliosimamishwa.”
Katika miaka mitatu ya kwanza ambayo wamishonari walihubiri Iceland, ndugu hao waliwaachia watu vitabu zaidi ya 16,000. Hata hivyo, hawakufanya ziara nyingi za kurudia wala hawakupata mafunzo mengi. Watu walichukua vitabu lakini hawakukubali ujumbe. Kwa mfano, Ndugu Larsen na mkewe, Missie, ambaye alikuja kutoka Denmark mwaka wa 1950 ili aolewe naye, walienda hadi pwani ya mashariki ambako walihubiri katika mji wa Höfn, Eskifjördhur, Neskaupstadhur, na Seydhisfjördhur. Katika safari hiyo ngumu waliwaachia watu vitabu 300 na pia vijitabu 300 hivi. Ndani ya kila kitabu walikuwa wameweka kikaratasi chenye ujumbe mfupi wa Maandiko na anwani ya wamishonari huko Reykjavík. Kila mtu aliyechukua kitabu alialikwa kuandika barua ili apate habari zaidi kuhusu kweli, lakini hakuna mtu hata mmoja aliyeandika.
Mwaka wa 1952 iliamuliwa kwamba eneo la pwani ya kaskazini lilihitaji kuhubiriwa zaidi. Kwa hiyo, mnamo Juni mwaka huo, Oliver Macdonald na mkewe Sally, ambaye alikuja kutoka Uingereza mwaka wa 1949 ili aolewe naye, wakawekwa kuwa mapainia wa pekee na kutumwa Akureyri. Huko walipingwa sana na watu wa dini inayoitwa Ndugu wa Plymouth walioongozwa na balozi wa Uingereza mjini humo. Alikuwa na wafuasi wengi, na wengine walimsikiliza alipowashambulia Mashahidi katika hotuba zake, na katika makala alizoandika. Mapainia hao hawakuwa wamepatwa na upinzani kama huo walipokuwa Reykjavík, hata hivyo walipambana na shambulizi hilo bila woga, nao wakaendelea na kazi yao wakitumia kila nafasi kujibu mashtaka hayo ya uwongo. Baadhi ya magazeti yalichapisha majibu yao.
Mapainia hao walihubiri mjini humo, na vilevile mashambani, na kuwaachia watu vitabu. Kwa kawaida watu waliwakaribisha kwa chakula na kahawa, lakini hawakupata watu waliopendezwa kikweli na ujumbe wa Ufalme. Ndugu na Dada Macdonald walirudi Reykjavík mnamo Julai 1953, lakini kabla ya kuondoka Akureyri, walipanda mbegu za kweli, ambazo zilimea baadaye.
Msingi Wawekwa
Baada ya kupanda na kutia maji kwa miaka 27, hatimaye ndugu huko Iceland walianza kuona matokeo ya kazi yao. Mapema mwaka wa 1956, watu wapya saba walikubali ujumbe wa Ufalme, na kujiweka wakfu kwa Yehova. Hadi wakati huo, wengi wa wale waliopendezwa na kweli hawakusimama imara, ila Dada Iris Åberg kutoka Uingereza ambaye baadaye alihama nchi hiyo. Sasa watu wapya saba walikuwa wamebatizwa na msingi imara ulikuwa umewekwa. Hata hivyo, wamishonari na mapainia wote waliokuwa wamehubiri kwa bidii ili kweli itie mizizi nchini Iceland walikuwa wameondoka mwaka wa 1957, wengi wao kwa sababu ya matatizo ya afya.
Kwa hiyo, mwaka wa 1957, Dada Edith Marx, painia wa pekee kutoka Denmark ambaye alikuwa amekuja mwaka uliotangulia, alikabidhiwa madaraka ya kutunza lile kutaniko dogo. Wavunaji walihitajiwa ili kulisaidia kutaniko hilo dogo, ambalo lilijikuta limeachwa na ndugu waliokuwa wamewasaidia wale wapya kuijua kweli na kuwa imara. Muda si muda mapainia wa pekee kutoka Denmark, Sweden, na Ujerumani wakafika. Isitoshe, wahubiri na mapainia wengi walihamia Iceland ili kusaidia kuhubiri ujumbe wa Ufalme. Tangu wakati huo idadi ya wahubiri imeongezeka pole kwa pole.
Ongezeko hilo liliambatana na mambo mazuri kama vile ziara za mwangalizi wa mzunguko na makusanyiko ya wilaya ya kila mwaka. Na vitabu vingi zaidi vilihitajika katika lugha ya Iceland. Toleo la Januari 1, 1960, la Mnara wa Mlinzi ndilo lililokuwa la kwanza katika lugha ya Iceland. Gazeti hilo liliwasaidia akina ndugu sana katika kazi ya kuhubiri. Walifurahi kuwatolea watu gazeti hilo katika lugha yao! Na imani ya ndugu iliimarishwa pia kwa sababu wao wenyewe walifaidika na chakula hicho kizuri kila mwezi! Ilipotangazwa kwenye kusanyiko la mzunguko huko Reykjavík kwamba gazeti la Mnara wa Mlinzi lingechapishwa katika lugha ya Iceland, picha kubwa ya gazeti hilo ilionyeshwa nyuma ya msemaji. Ndugu walishangilia sana walipopokea zawadi hiyo mpya kutoka kwa Yehova!
Ndugu Pedersen anakumbuka kwamba alipofika Iceland mnamo Oktoba 1959, kulikuwa na kichapo kimoja tu kwa ajili ya kazi ya kuhubiri katika lugha ya Iceland, yaani, kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme,” na wenye nyumba wengi tayari walikuwa nacho. Watu waliojua kusoma Kidenishi, Kiingereza, Kijerumani, au Kiswidi waliachiwa gazeti la Mnara wa Mlinzi na Amkeni! katika lugha hizo. Hata hivyo, ingawa wengi walijua mojawapo ya lugha hizo, walielewa gazeti la Mnara wa Mlinzi vizuri zaidi walipolisoma katika lugha yao. Kazi ya kuhubiri ilisonga mbele gazeti hilo lilipopatikana katika lugha ya Iceland. Katika mwaka huo wa utumishi, wale wahubiri na mapainia 41 waliwaachia watu magazeti 26,479, na watu 809 walipokea gazeti hilo kwa njia ya posta. Idadi ya mafunzo ya Biblia iliongezeka pia.
Hatua nyingine muhimu ilikuwa kufunguliwa kwa ofisi ya tawi mnamo Januari 1, 1962. Ofisi ya tawi ya Marekani ndiyo iliyokuwa ikisimamia kazi ya kuhubiri nchini Iceland ambayo mwanzoni ilisimamiwa na ofisi ya tawi ya Denmark. Kisha, mwaka wa 1969, Mashahidi wa Yehova wakaandikishwa kisheria na Wizara ya Haki na Masuala ya Dini. Sasa Mashahidi wa Iceland walikuwa na haki sawa na zile za dini nyingine, na pia walipata idhini ya kuhalalisha ndoa na kuongoza mazishi.
Makasisi Wapinga
Ndugu walipata upinzani kutoka kwa makasisi mwezi uleule ambao ofisi ya tawi ilifunguliwa. Asubuhi moja, vichwa vikuu katika gazeti moja la kila siku vilitangaza kwamba askofu mkuu wa kanisa la taifa alikuwa amechapisha kijitabu kilichoonya juu ya Mashahidi wa Yehova, na kuwashauri watu wasiwasikilize. Kijitabu hicho kilikuwa na kichwa Onyo Kuwahusu Mashahidi wa Yehova (Vottar Jehóva—advörun). Magazeti mengine nayo yakachapisha habari kuwahusu Mashahidi wa Yehova. Ndugu mmoja aliyefanya kazi kwenye ofisi ya tawi alihojiwa, na mahojiano hayo yakachapishwa katika gazeti kuu la jioni linaloitwa Vísir. Makala hiyo ilieleza maoni yetu, na punde si punde magazeti mengine pia yakachapisha makala kuwahusu Mashahidi wa Yehova. Ushuhuda mkubwa ulitolewa kwa njia hiyo, na watu wengi wakasikia kuhusu kazi yetu. Wasomaji kadhaa waliandika barua ili kuwatetea Mashahidi na zikachapishwa katika magazeti ya kila siku. Askofu alitushambulia tena kwa kuchapisha “jibu” la barua hizo. Hata hivyo, gazeti Morgunbladid, ambalo ni gazeti kuu kushinda yote, likachapisha makala ya ukurasa mzima iliyoeleza kinaganaga kuhusu imani na kazi za Mashahidi wa Yehova.
Kile kijitabu chenye onyo kilisambazwa kotekote nchini. Usambazaji huo ulifanya Mashahidi wa Yehova wajulikane sana, jambo lililotusaidia kwa miaka mingi katika kazi yetu ya kuhubiri. Gazeti moja lilisema hivi kuhusu usambazaji huo: “Askofu amekuwa mkurugenzi wa kuwatangaza Mashahidi wa Yehova.” Mashahidi wa Yehova walijulikana hata katika maeneo ya mbali ambako hawakuwa wamehubiri. Watu fulani walifuata ushauri wa askofu, lakini wengi walitaka kujua kwa nini alitoa onyo hilo. Hata hivyo, upande wa kaskazini, huko Akureyri, kulikuwa na uhasama. Nyakati nyingine, vijana waliwarushia mawe Heinrich na Katherine Karcher, waliokuwa mapainia mjini humo. Miaka kadhaa baadaye, wapinzani wengine wa kidini huko Akureyri walichapa tena kile kijitabu cha askofu na kukisambaza. Wafuasi wa Kanisa la Pentekoste walifanya vivyo hivyo huko Reykjavík, wakidhani kwamba wataweza kukomesha au kuzuia kazi yetu ya kuhubiri.
Magumu ya Kupanga Makusanyiko
Makusanyiko yote yamekuwa pindi za shangwe kwa watu wa Mungu nchini Iceland. Ndugu hawakusita kupanga makusanyiko hata wakati wahubiri walipokuwa wachache. Kusanyiko la kwanza lilifanywa Julai 1951, wakati ndugu wawili, yaani, Percy Chapman kutoka Kanada na Klaus Jensen kutoka Brooklyn, walipotembelea Iceland wakiwa safarini kwenda kwenye makusanyiko mbalimbali huko Ulaya. Watu 55 walihudhuria kusanyiko hilo ijapokuwa kulikuwa na wahubiri wachache tu nchini Iceland wakati huo. Kusanyiko lililofuata lilifanywa miaka saba baadaye, mnamo Juni 1958, wakati mwangalizi wa eneo la dunia, Filip Hoffmann, alipotembelea ofisi ya tawi. Watu 38 walisikiliza hotuba ya watu wote. Tangu wakati huo makusanyiko yamefanywa kila mwaka.
Fridrik Gíslason ni mmojawapo wa ndugu wachache ambao walitoa hotuba kwenye makusanyiko katika miaka ya 1950. Anasema hivi: “Ninakumbuka kwamba nilikuwa mwangalizi wa Idara ya Chakula kwenye makusanyiko ya kwanzakwanza. Mimi mwenyewe nilifanya karibu kazi zote za upishi, na kwa kawaida nilikuwa na hotuba tatu au nne kila siku kwenye kusanyiko. Nilipofanya kazi jikoni nilivaa aproni, lakini nilivaa koti huku nikitimua mbio kwenda kwenye jumba la kusanyiko ili kutoa hotuba. Hata hivyo, nyakati nyingine iliwabidi ndugu kunikumbusha kuvua aproni. Sasa watu kati ya 400 na 500 huhudhuria makusanyiko, na kuna wazee wengi wanaostahili kutoa hotuba kwenye makusanyiko.”
Drama za Biblia ni sehemu yenye kusisimua na yenye kufundisha ya makusanyiko ya wilaya. Hata hivyo, kwa sababu wahubiri walikuwa wachache nchini Iceland, drama hizo zilitolewa kwa njia ya kaseti tu. Ili drama hizo zipendeze zaidi, ofisi ya tawi ya Denmark ilitayarisha onyesho la picha lililoambatana na sauti kwenye kaseti. Hata hivyo, ilichukua muda mrefu kutayarisha drama. Kwanza, zilitafsiriwa katika lugha ya Iceland. Kisha zikarekodiwa na ndugu wenyeji walioongea lugha hiyo. Isitoshe, muziki na sauti nyingine mbalimbali ziliongezwa kutoka katika kaseti ya Kiingereza. Iliwabidi ndugu wengine kuigiza zaidi ya sehemu moja, na kubadili sauti zao kupatana na yule mtu waliyemwigiza. Hatimaye, baadhi ya drama hizo ziliigizwa jukwaani.
Drama ya kwanza kuigizwa ilimhusu Malkia Esta, nayo iliigizwa kwenye kusanyiko la wilaya la mwaka wa 1970. Ndugu walifanya kazi na mazoezi kwa bidii sana. Lilikuwa jambo jipya kwa ndugu kuvalia mavazi kama yale yaliyovaliwa na watu katika siku za Biblia na kubandikwa ndevu usoni. Haikutangazwa kimbele kwamba drama hiyo ingeigizwa jukwaani, kwa hiyo ndugu walishangaa, na kufurahia sana jambo hilo lisilotazamiwa. Kwenye makusanyiko madogo, karibu wahudhuriaji wote hufahamiana na wote huketi karibu na jukwaa, hivyo wengine hujaribu kuwatambua ndugu na dada wanaoigiza. Baada ya kuona drama fulani dada mmoja alisema hivi: “Wazia, sikumtambua yeyote isipokuwa ndugu yule aliyemwigiza Mfalme Nebukadneza!” Alitaja jina la ndugu huyo, na alishangaa sana alipoambiwa kwamba amekosea. Ndugu wanathamini sana kazi ngumu inayofanywa na wengi wanaotoa hotuba na sehemu mbalimbali kwenye makusanyiko madogo. Wote hufaidika na mambo mazuri wanayojifunza kutokana na drama zinazotolewa katika lugha yao.
Makusanyiko ya Kimataifa Yaleta Shangwe
Kwa miaka mingi, ndugu wa Iceland wamefurahia kuhudhuria makusanyiko katika nchi nyingine. Ndugu watano kutoka Iceland walikuwa na pendeleo la kuhudhuria kusanyiko la kimataifa la Mapenzi ya Mungu huko New York mwaka wa 1958. Wengi walihudhuria Makusanyiko ya Waabudu Wenye Umoja huko Ulaya mwaka wa 1961, na mwaka wa 1963 wakahudhuria Makusanyiko ya “Habari Njema za Milele.” Wengine walifurahia kushirikiana na ndugu kutoka nchi nyingi kwenye Makusanyiko ya Kimataifa ya “Ushindi wa Kimungu” mwaka wa 1973. Zaidi ya wahubiri 100 kutoka Iceland walihudhuria Kusanyiko la Kimataifa la “Amani Duniani” huko Copenhagen, Denmark, Agosti 5-10, 1969. Hicho ndicho kikundi kikubwa zaidi kutoka Iceland kuhudhuria kusanyiko la kimataifa katika nchi nyingine. Mwaka huohuo, asilimia 80 ya wahubiri wa Iceland walihudhuria kusanyiko hilo katika nchi nyingine.
Ndugu wengi kutoka Iceland walikuwa wamepanga kuhudhuria kusanyiko hilo la mwaka wa 1969, kwa hiyo ofisi ya tawi ya Denmark ilipanga ndugu hao waketi pamoja. Kila asubuhi, kabla ya vipindi vya kusanyiko kuanza, ndugu kutoka Iceland walikusanyika kwenye sehemu yao ambako walielezwa mambo makuu ya programu katika lugha yao.
Mmoja wa wale waliohudhuria kusanyiko hilo ni kijana anayeitwa Bjarni Jónsson. Yeye ni mwana wa wakili aliyemiliki jengo lililokodiwa na ndugu kwa ajili ya makao ya wamishonari na ofisi ya tawi huko Reykjavík. Bjarni hakujua mengi kuhusu kweli, na hakukusudia kuhudhuria kusanyiko aliposafiri pamoja na ndugu hadi Copenhagen. Kwa nini basi alihudhuria kusanyiko hilo?
Kjell Geelnard, aliyekuwa msimamizi wa ofisi ya tawi wakati huo, alikuwa na mambo kadhaa ya kuzungumzia pamoja na baba ya Bjarni. Kjell alimweleza kuhusu kusanyiko la kimataifa huko Copenhagen na kuwahusu ndugu waliopanga kuhudhuria. Wakili huyo aliposikia jambo hilo aliuliza kama mwanaye mkubwa angeweza kuandamana na ndugu hao. Alimwambia Ndugu Geelnard kwamba mwanaye alikuwa amemaliza shule, na angependa kumlipia safari ya kwenda ng’ambo, kwa hiyo huenda safari ya Copenhagen ikamfaa. Kjell aliona wazo hilo kuwa zuri naye akamwambia wakili huyo kwamba ikiwa Bjarni angetaka kuhudhuria kusanyiko ili ajionee jinsi mambo yalivyo kwenye kusanyiko, angeweza kupanga ili apate mahali pa kulala huko Copenhagen. Wakili huyo alifurahi kusikia jambo hilo na kumwuliza mwanaye kama angetaka kujiunga na Mashahidi wa Yehova waliopanga kwenda kusanyikoni. Mwana huyo alikubali mara moja.
Ndugu waliwasiliana na Idara ya Mahali pa Kulala huko Copenhagen ili kumtafutia Bjarni mahali pa kulala. Walipata nafasi katika nyumba ya familia moja ya Mashahidi. Ndugu mmoja kutoka Marekani, ambaye alikuwa amepangiwa kukaa pamoja na ndugu kutoka Iceland anayeitwa Jakob, alikuwa amefuta ombi lake, kwa hiyo Bjarni akapata mahali pake. Hata hivyo, Jakob hakufika kwa sababu fulani. Kwa hiyo, Bjarni peke yake ndiye aliyeenda kwa familia hiyo. Ndugu kwenye Idara ya Mahali pa Kulala hawakuwaeleza watu wa familia hiyo kwamba Bjarni angekuja badala ya yule ndugu kutoka Marekani, kwa hiyo walifikiri kwamba mgeni wao ni Jakob.
Kwa kawaida, ndugu kutoka sehemu mbalimbali wanapokutana wao husimulia mambo yaliyoonwa. Ndugu wa Denmark walishangaa kwamba “Jakob” hakuwa na mengi ya kueleza. Kwa upande mwingine, Bjarni alivurugika kidogo wakati ndugu na dada waliomkaribisha walipomwita Jakob. Kwa kuwa Jakob ni jina linalotajwa katika Biblia, alifikiri kwamba huenda Mashahidi wa Yehova wana desturi ya kutumia majina yanayotajwa katika Biblia wanapoongea na waamini wenzao. Hali hiyo ya kutoelewana ilirekebishwa wakati ndugu mmoja aliyeishi katika nyumba ambayo Bjarni alikaa, alipokutana na ndugu kutoka Denmark aliyekuwa painia huko Iceland. Alimwuliza ndugu huyo kama “Jakob” alikuwa mpya katika kweli, kwa sababu alijua mambo machache sana kuhusu kazi ya kuhubiri huko Iceland. Painia huyo alimweleza kwamba mgeni wao si Jakob bali ni Bjarni, mwanafunzi wa shule kutoka Iceland aliyekuwa amesafiri pamoja na akina ndugu hadi Copenhagen. Ndugu na dada waliomkaribisha Bjarni walionyesha ukarimu na kumwalika akae nao kwa juma lingine ili atembelee sehemu mbalimbali za Denmark. Bjarni aliguswa moyo na fadhili hiyo.
Bjarni alihudhuria kusanyiko. Na ijapokuwa hakufaidika kikamili na programu kwa sababu hakujua mengi kuhusu kweli, yale aliyojionea na kusikia yalimvutia sana. Mara tu aliporudi Iceland, yeye na familia yao walianza kujifunza Biblia. Bjarni alifanya maendeleo makubwa katika kweli na kubatizwa mwaka wa 1971. Ametumikia katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi nchini Iceland tangu mwaka wa 1979.
Svanberg Jakobsson amekuwa mtafsiri kwenye ofisi ya tawi ya Iceland kwa miaka mingi na sasa yeye ndiye mwangalizi wa Idara ya Tafsiri. Alipokuwa mhubiri kijana, alihudhuria Kusanyiko la Kimataifa la “Ushindi wa Kimungu” huko London, Uingereza, mwaka wa 1973. Anasema hivi: “Ninakumbuka jinsi nilivyosisimuka nilipowatazama maelfu ya ndugu na dada wakimiminika kwenye uwanja wa kusanyiko. Nilishangaa kuwaona ndugu na dada wengi kutoka Afrika, wote wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni yenye rangi mbalimbali. Siwezi kamwe kusahau furaha ya kuwa pamoja na makumi ya maelfu ya ndugu, kusikiliza programu pamoja nao, kuimba pamoja nao, kusali pamoja nao, na kula pamoja nao.”
Sólborg Sveinsdóttir, aliyebatizwa mwaka wa 1958, alisafiri kwa meli kwa muda wa siku sita, pamoja na watoto wanne, ili kuhudhuria kusanyiko huko Copenhagen, Denmark, mwaka wa 1961. Sólborg alikuwa katika kikundi kidogo kilichokuwa mbali sana huko Keflavík. Alihisije baada ya kuhudhuria kusanyiko kubwa la kimataifa? Anasema hivi: “Nilivutiwa sana kusikia zaidi ya ndugu 30,000 wakiimba nyimbo za Ufalme katika lugha tano. Jambo hilo lilinigusa moyo sana. Mambo yote yalikuwa yamepangwa vizuri sana.”
Ijapokuwa iliwagharimu pesa nyingi, ndugu waliona inafaa kuhudhuria makusanyiko hayo ya kimataifa. Ilikuwa baraka kuhudhuria karamu hizo nzuri za kiroho zilizoandaliwa na Yehova, na kuwa pamoja na maelfu ya waamini wenzao.
“Mhudumu” wa Kiroho Azuru
Wengi wamehamia Iceland kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa wahubiri. Wote wamepambana kwa muda mrefu kujifunza lugha ngumu ya Iceland. Hata hivyo, nyakati nyingine kutoelewana kwa sababu ya lugha kunaweza kuleta baraka. Kwa mfano, Heinrich Karcher alikuwa akihubiri nyumba kwa nyumba, na kujitambulisha kama mhudumu, au mtumishi. Kwenye nyumba moja mwanamke kijana alifungua mlango, na mara alipojitambulisha, mwanamke huyo akamkaribisha ndani. Hakuelewa kusudi lake la kumtembelea kwa sababu katika lugha ya Iceland neno mhudumu laweza pia kumaanisha “mtumishi” au “mhudumu” katika hoteli. Mwanamke huyo alifikiri Heinrich alifanya kazi pamoja na mumewe aliyekuwa mhudumu kwenye hoteli moja katika eneo hilo. Alijua kwamba mume wake angefika baada ya muda mfupi, kwa hiyo, akaamua kumkaribisha mtu huyo. Walicheka sana walipogundua kosa hilo.
Mume wake alipofika, “mhudumu” huyo wa kiroho aliwahudumia mume na mke hao kwa kuwapa chakula kizuri cha kiroho ambacho walikipenda sana. Hata walimwomba Heinrich arudi pamoja na mkewe. Muda si muda wenzi hao wa ndoa wenye kupendezwa walianza kujifunza Biblia kwa ukawaida, nao wakaanza kuwahubiria watu wengine. Hata alipokuwa akifanya kazi hotelini, mhudumu huyo kijana aliwahubiria wote waliotaka kusikiliza. Baada ya muda wakabatizwa. Walifurahi kwamba “mhudumu” huyo wa kiroho aliwatembelea na kujitahidi kuwahubiria katika lugha yao.
Mambo mengi ya kuchekesha yametukia wakati ndugu kutoka nchi nyingine walipokuwa wakijifunza lugha ya Iceland. Kwa mfano, muda mfupi baada ya Sally Macdonald kufika Iceland, alitayarisha utangulizi huu: “Ninawatembelea watu katika eneo hili ili kuongea nao kuhusu mambo fulani yenye kupendeza katika Biblia.” Lakini alichanganya neno kutembelea (heimsækja) na neno kutesa (ofsækja), kwa hiyo, alikuwa akisema hivi huku akitabasamu: “Ninawatesa watu katika eneo hili.”
Kuhubiri Nyumba kwa Nyumba Pamoja na Kasisi wa Kanisa la Kilutheri
Kwa miaka mingi, Holger na Tove Frederiksen kutoka Denmark walitumikia kwa uaminifu kama mapainia wa pekee nchini Iceland, na kwa muda fulani wakafanya kazi ya mzunguko. Ijapokuwa ilikuwa vigumu kwa Tove kujifunza lugha ya Iceland, aliwasaidia wengi kukubali kweli kwa sababu ya shauku na bidii yake.
Pindi moja, walipokuwa wakifanya kazi ya mzunguko, Holger na mhubiri mmoja kijana walihubiri nyumba kwa nyumba katika kijiji kidogo. Walishangaa wakati kasisi wa Kanisa la Kilutheri alipojiunga nao. Kwa nini?
Muda mfupi kabla ya hapo walikuwa wamemtembelea kasisi huyo nyumbani kwake. Alionyesha urafiki wa kijuujuu na kuwakaribisha ofisini mwake. Baada ya kutupia jicho vitabu ambavyo walikuwa wakiwatolea watu, alisema hivi: “Vitabu hivyo vina mafundisho ya uwongo!” Kisha akasimama, akainua mikono, na kuwalaani kwa jina la Mungu. Alisema kwa sauti kubwa: “Ninawakataza msihubiri katika eneo la kanisa langu!” Holger alimwambia kasisi huyo kwamba hakuwa na haki ya kuwazuia wasihubiri na kwamba wangeendelea kuhubiri. Kisha kasisi huyo akasema, “Mkiendelea kuwahubiria watu katika eneo la kanisa langu, nitaandamana nanyi.” Holger alimwalika ajiunge nao.
Baada ya kasisi huyo kuandamana nao walipotembelea nyumba mbili za majirani wake, walikutana na Tove na dada mwingine, walioshangaa kumwona kasisi akienda nyumba kwa nyumba. Kasisi huyo aliwakaribisha wote nyumbani kwake kwa kikombe cha kahawa. Walifurahia mazungumzo ya kirafiki. Holger alifikiri kwamba kasisi huyo aliwakaribisha nyumbani kwake ghafula ili awazuie wasiwahubirie watu wote katika eneo hilo. Kwa hiyo, siku iliyofuata, walirudi na kuhubiri katika kijiji chote. Waliwaachia watu vitabu vingi na wengi walisikiliza.
Wazuiwa na Poromoko la Theluji
Ili kuwahubiria watu wa mashambani, mara nyingi ni lazima kusafiri kwenye barabara za milimani zinazokuwa na barafu na theluji wakati wa majira ya baridi na giza. Mnamo Desemba 1974, mwangalizi anayesafiri Kjell Geelnard na mke wake Iiris walitembelea mji wa Akureyri kwenye pwani ya kaskazini. Katika juma walilotembelea kutaniko la mji huo, waliamua kwenda kuhubiri Húsavík, mji ulio umbali wa kilometa 80 kutoka Akureyri. Waliandamana na Holger na Tove Frederiksen. Walihubiri pamoja katika mji wa Húsavík na maeneo yaliyo karibu kwa siku chache, kisha, wakamalizia ziara hiyo kwa kutoa hotuba ya watu wote yenye onyesho la picha kwenye shule fulani. Mkutano ulipoanza, dhoruba ilikumba eneo hilo na kuleta baridi kali, theluji, na mvua. Baada ya mkutano, wahudhuriaji walipokuwa wakijitayarisha kurudi nyumbani, umeme ulipotea kotekote mjini kwa sababu ya dhoruba hiyo ya theluji. Kulikuwa na giza ndugu walipotoka katika shule hiyo lakini wote walifurahi kwa kuwa waliweza kutazama lile onyesho la picha kabla ya umeme kupotea.
Ndugu na Dada Geelnard, pamoja na Ndugu na Dada Frederiksen, walihitaji kurudi Akureyri. Waliwauliza polisi na madereva wa mabasi na malori kuhusu hali ya barabara, nao wakawahakikishia kwamba mapema kidogo barabara haikuwa mbaya sana. Kwa hiyo, waliamua kuondoka mara moja, lakini ilichukua muda kufunga virago vyao katika mwangaza wa mishumaa. Walipoenda kununua petroli, mfanyakazi kwenye kituo cha petroli alilazimika kutumia pampu ya mkono. Hatimaye, mwendo wa saa tatu usiku walikuwa tayari kuondoka.
Kjell anasema hivi kuhusu safari hiyo: “Mwanzoni mambo yalikuwa shwari, lakini theluji ilizidi kuanguka kwa wingi. Nyakati nyingine ilikuwa vigumu sana kuiona barabara hivi kwamba Holger alilazimika kushuka na kutuongoza kwa tochi. Halafu gari letu likakwama kwenye theluji. Mara kadhaa tulifaulu kupita sehemu hizo zenye theluji kwa kulisukuma gari na kuondoa theluji kwa sepetu, lakini mwishowe tukakwama kabisa katika theluji nyingi sana iliyokuwa kama ukuta. Baadaye tuliambiwa kwamba theluji hiyo ilikuwa imeporomoka kutoka kwenye mlima uliokuwa karibu. Kwa kawaida safari ya kutoka Húsavík hadi Akureyri huchukua muda wa saa mbili, lakini tulikuwa tumesafiri kwa muda wa saa sita na tulikuwa tumefika katikati tu.
“Ilikuwa saa tisa usiku, nasi tulikuwa tumelowa maji, tumechoka, na tunasikia baridi. Wazia jinsi tulivyofurahi tulipoona mwangaza katika nyumba moja ya mkulima, iliyokuwa karibu. Jambo hilo lilitutupatia ujasiri wa kwenda kwenye nyumba hiyo na kubisha mlango. Holger, ambaye ni mpole, alibisha mlango wa mbele. Hakuna yeyote aliyeufungua, kwa hiyo, akaufungua, akaingia ndani na kupanda ngazi hadi kwenye chumba cha kulala na kubisha mlango polepole. Mkulima huyo na mkewe walishangaa lakini hawakushtuka. Walisema kwamba wakati walipoenda kulala umeme ulikuwa umepotea, kwa hiyo wakasahau kuzima taa!
“Tulijionea ukarimu wa watu wa Iceland. Mkulima huyo na mkewe walihamisha watoto wao waliokuwa wamelala hadi chumba kingine, ili sote wanne tupate vyumba viwili vya kulala, kisha wakatuandalia kahawa na mkate mtamu jikoni. Asubuhi iliyofuata baada ya kupata kiamsha kinywa, mwenye nyumba alisisitiza tungoje chakula cha mchana. Baada ya kula pamoja na familia hiyo, tuliendelea na safari yetu hadi Akureyri, kwa sababu malori mawili yenye vifaa vya kuondoshea theluji yalikuwa yameondoa theluji barabarani. Kwa sababu ya ukarimu wa mkulima huyo na mkewe tuliweza kuwaeleza kuhusu kweli ya Biblia.”
Kuhubiri Kwenye Meli ya Uvuvi
Miaka kadhaa iliyopita, Kjell Geelnard alikutana na mwanamume fulani kijana alipokuwa akihubiri. Mwanamume huyo anaitwa Fridrik. Yeye ndiye mtoto wa kwanza katika familia yao, naye alipendezwa na mambo ya kiroho na kufurahia mazungumzo ya Biblia. Alikuwa na maswali mengi na alitaka sana kuijua Biblia. Lakini, haikuwa rahisi kumpata, kwa sababu alifanya kazi kwenye meli ya uvuvi. Mara nyingi alikuwa baharini, naye alikaa nyumbani kwa siku chache tu kabla ya kusafiri tena. Hata hivyo, kwa kutazama ratiba ya meli na kumwuliza mama ya Fridrik, Kjell alifaulu kukutana na Fridrik, ama bandarini ama nyumbani. Kwa njia hiyo, ndugu walimsaidia kufanya maendeleo ya kiroho.
Mwishoni mwa mwaka wa 1982, Fridrik alialikwa kuhudhuria kusanyiko mjini Reykjavík. Wakati huo imani yake katika Yehova ilikuwa imeanza kuimarika, na aliomwomba amsaidie kupata nafasi ya kuhudhuria. Halafu, kwa ghafula mfanyakazi mwenzake akaamua kwenda safari ya uvuvi ambayo hakupaswa kwenda kwa sababu alikuwa likizoni. Kwa hiyo, Fridrik akapata ruhusa ya kutoenda safari hiyo na akahudhuria kusanyiko. Kusanyiko hilo lilimvutia Fridrik sana, ambaye sasa alikuwa na hakika kwamba alitaka kumtumikia Yehova.
Fridrik aliporudi kwenye mji wa kwao, alimweleza mchumba wake kuhusu uamuzi wake wa kumtumikia Yehova na mabadiliko ambayo angehitaji kufanya katika maisha yake. Alimwambia kwamba alitaka kumwoa, lakini ikiwa hangetaka kuwa mke wa Shahidi wa Yehova, afadhali avunje uchumba huo. Asubuhi iliyofuata mtu alibisha mlango wa nyumba ya wamishonari. Walipofungua walimkuta Fridrik na mchumba wake mlangoni. Fridrik alikuwa na ujumbe mfupi na wazi: “Helga anataka kujifunza Biblia!” Kwa hiyo, wamishonari hao wakapanga kujifunza pamoja na Helga. Baadaye siku hiyo, mmoja wa ndugu za Fridrik pia aliomba afundishwe Biblia. Katika juma hilohilo, Fridrik alimpeleka dada yake mdogo mkutanoni na kusema: “Unnur anataka kujifunza Biblia!”
Fridrik alitaka kubatizwa ili kuonyesha kwamba amejiweka wakfu kwa Yehova. Hata hivyo, kwanza alihitaji kuongeza ujuzi wake, na vilevile kupitia maswali ya ubatizo. Lakini tatizo lilikuwa kwamba alikuwa baharini mara nyingi. Basi, ikiwa Kjell hakuweza kumtembelea Fridrik nyumbani, vipi kazini? Walifanya nini? Fridrik alimwajiri Kjell kufanya kazi naye kwenye chumba cha injini melini. Mapema mwaka wa 1983, Kjell alipanda meli inayoitwa Svalbakur akiwa amebeba Biblia na vitabu vya kujifunzia Biblia.
Kjell anasema: “Sitasahau kamwe utumishi na kazi niliyofanya kwenye meli ya Svalbakur. Tulianza kazi saa 12:30 asubuhi na kumaliza saa 12:30 jioni. Tulikula chakula cha mchana saa sita, na wakati wa mapumziko ya asubuhi na alasiri tulikunywa kahawa. Baada ya kazi nilijifunza na Fridrik, na nilipata nafasi nyingi za kuwahubiria wafanyakazi wengine melini. Kila jioni tulijifunza na kuzungumzia mambo ya kiroho. Nyakati nyingine tulilala usiku wa manane. Tulikula chakula cha mchana haraka ili tuweze kuzungumzia andiko la siku katika chumba cha Fridrik.”
Bila shaka, wafanyakazi melini walishangaa kumwona mmishonari akifanya kazi pamoja nao. Mwanzoni, watu hao walimtazama Kjell kwa mbali, kwa sababu halikuwa jambo la kawaida kuwa na mmishonari kwenye meli. Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi hao walimsikiliza kwa makini. Mmoja wao alipendezwa sana, na alipojua kwamba Kjell na Fridrik walizungumzia andiko la siku baada ya chakula cha mchana, akataka kujiunga nao. Siku moja mazungumzo yalipoendelea sana wakati wa chakula cha mchana, mtu huyo alikasirika kidogo na kumwambiaa Kjell na Fridrik mbele ya wengine wote: “Twende tukasome andiko la siku sasa.”
Jioni moja, Kjell na Fridrik waliwaalika wafanyakazi wote kwenye chumba cha Fridrik ili kuzungumzia habari kuhusu ulevi kwenye gazeti fulani la Amkeni! Wafanyakazi saba walikuja kwenye mazungumzo hayo yaliyokumbukwa kwa muda mrefu. Wafanyakazi wa meli nyingine pia walisikia kuyahusu.
Kjell anasema: “Baada ya kuhubiri na kufanya kazi kwa majuma mawili hivi kwenye meli ya Svalbakur, tulirudi bandarini. Nilikuwa nimepitia maswali ya ubatizo pamoja na Fridrik na kujifunza habari nyingine nyingi za Biblia pamoja naye. Pia niliwahubiria wafanyakazi wengine melini, na kuwaachia magazeti na vitabu.” Fridrik alibatizwa mapema mwaka wa 1983. Helga, mchumba wa Fridrik, mama yake, na dada yake, walikubali kweli.
Kuongoza Mafunzo kwa Kutumia Simu
Si rahisi kuwahubiria watu wanaoishi kwenye maeneo ya mbali katika kisiwa hiki kikubwa. Simu imetumiwa kwa mafanikio ili kuwasiliana na watu wanaopendezwa.
Njia hiyo ya kuhubiri habari njema inawanufaisha watu wengi. Miaka kadhaa iliyopita, mwanamke aitwaye Oddný Helgadóttir, alimtembelea mwana wake na mke wa mwana huyo, ambao walikuwa wakijifunza pamoja na Mashahidi wa Yehova. Walipomweleza kuhusu yale waliyokuwa wakijifunza, alitaka kujifunza Biblia pia. Hata hivyo, Oddný aliishi katika eneo la mbali kwenye pwani ya kaskazini-magharibi mwa Iceland, umbali wa zaidi ya kilometa 300 kutoka kutaniko la karibu. Dada mmoja anayeitwa Gudrún Ólafsdóttir, alipojitolea kujifunza naye kwa njia ya simu, alikubali kwa furaha. Baada ya sala, Oddný alijibu maswali yote katika kitabu cha funzo kwa urahisi. Alipotayarisha funzo, Oddný aliandika maandiko yote ambayo hayakuwa yamenukuliwa ili aweze kuyasoma mara tu yalipotajwa. Hivyo, hakuhitaji kutumia wakati kutafuta maandiko walipokuwa wakijifunza. Pindi moja walijifunza nyumbani kwa Gudrún, kwa kuwa Oddný alikuwa ametembelea sehemu hiyo. Wote wawili waliona haya kidogo kwa sababu ilikuwa mara yao ya kwanza kujifunza ana kwa ana, kwa hiyo, Gudrún akapendekeza kimchezo kwamba waketi katika vyumba viwili tofauti vilivyokuwa na simu!
Oddný alipoielewa kweli, alianza kumhubiria mumewe, Jón. Mumewe alipendezwa, lakini Oddný hakujua kama ingefaa ajifunze naye. Aliambiwa kwamba angeweza kumfundisha lakini ingembidi kufunika kichwa alipoongoza funzo hilo. Zaidi ya kumfundisha mumewe, aliwahubiria majirani wake pia. Kisha akataka kubatizwa. Ili kuona kama Oddný alistahili kuanza kuhubiri, Gudrún alipanga ili mzee apitie pamoja naye maswali yaliyo katika kitabu Tumefanywa Tengenezo Tutimize Huduma Yetu kwa kutumia simu. Ilikuwa wazi kwamba alistahili ila tu hakuwa ameandikia kanisa lake la zamani barua na kueleza kwamba yeye si mfuasi wa kanisa hilo tena.
Juma moja hivi baadaye, Oddný alimpigia Gudrún simu ili kumjulisha kwamba alikuwa ameandika barua hiyo. Mumewe alikuwa amefanya vivyo hivyo. Huo ulikuwa uamuzi mkubwa kwake kwa kuwa hapo awali alikuwa mwenyekiti wa baraza la kanisa la eneo hilo. Baadaye, Oddný alibatizwa kwenye kusanyiko la mzunguko. Alifurahia kusanyiko hilo kwa sababu kabla ya kulihudhuria alikuwa amekutana na kikundi kidogo cha Mashahidi mara moja tu. Alihojiwa kwenye kusanyiko hilo na kuulizwa ikiwa ni vigumu kukaa mbali na ndugu wengine. Alijibu kwamba hakusikia upweke kamwe kwa sababu alijua kwamba nguvu za Yehova pia hufika hadi pwani ya kaskazini-magharibi mwa Iceland. Kisha akaongeza kwamba alisikitika kwa sababu mumewe hakuweza kuhudhuria kusanyiko hilo, lakini alikuwa amemhakikishia kwamba atahudhuria kusanyiko akiwa tayari kubatizwa. Na alitimiza ahadi yake! Muda si muda walihamia eneo lenye watu wengi ili waweze kuhudhuria mikutano kwa ukawaida.
Makao ya Wamishonari na Majumba ya Ufalme Yahitajiwa
Ndugu Nathan H. Knorr kutoka makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova alipotembelea Iceland mwaka wa 1968, aliona uhitaji wa kuwa na jengo linalofaa kwa ajili ya ofisi ya tawi na makao ya wamishonari. Kabla ya hapo, walikuwa wamekodi nyumba mbalimbali. Ndugu walianza kutafuta kiwanja ambapo wangeweza kujenga jengo moja lenye Jumba la Ufalme, makao ya wamishonari, na ofisi ya tawi. Wakati huohuo, ndugu walikodi nyumba nzuri kwenye barabara ya Hrefnugata, namba 5, mjini Reykjavík, na wale wamishonari sita wakahamia nyumba hiyo Oktoba 1, 1968. Nyumba hiyo ilikuwa kituo cha kazi nchini Iceland kwa miaka mitano iliyofuata. Baadaye, ndugu walinunua kiwanja kilichofaa kwenye barabara ya Sogavegur, namba 71, huko Reykjavík. Ujenzi wa ofisi ya tawi ulianza mapema mwaka wa 1972. Hiyo ilikuwa kazi ngumu kwa ndugu hao wachache wa Iceland kwa sababu hawakujua mengi kuhusu ujenzi. Hakuna ndugu aliyekuwa fundi wa ujenzi wala mwenye kampuni ya ujenzi, kwa hiyo iliwabidi kukodi kampuni ya ujenzi na kuwaajiri mafundi wasiokuwa Mashahidi. Wenye kampuni hizo walikuwa tayari kufanya kazi pamoja na ndugu. Ili wawe na mahali pa kulia chakula, ndugu walikodi sehemu ya nyumba kuukuu iliyokuwa karibu na kiwanja. Dada walipika chakula kwa zamu nyumbani kwao na kuwapelekea wafanyakazi.
Kupitia ujenzi huo, watu wengi walipata kuwajua Mashahidi katika eneo hilo. Watu wenye kampuni za ujenzi na wenye mamlaka mjini walikuwa na nafasi nzuri ya kuwajua Mashahidi wa Yehova. Nao wengine walipopita karibu na uwanja huo, walisimama ili waone jinsi ujenzi ulivyoendelea. Walipokuwa tayari kupiga plasta ndani, ndugu mmoja kutoka Denmark, ambaye ni fundi wa ujenzi, alikuja kusaidia. Pia, dada walisaidia sana katika kazi hiyo. Wenye mamlaka walipotembelea eneo la ujenzi, waliwaona dada wakiendesha mashine ya kuchanganya saruji. Mmoja wao alisema hivi: “Ninafikiri wanawake wa kanisa letu wanaweza kujifunza jambo fulani hapa. Bila shaka, makanisa yangejengwa kwa mafanikio zaidi kwa kufanya kazi badala ya kuzunguka-zunguka na kuomba pesa.” Jengo hilo liliwekwa wakfu Mei 1975, ndugu Milton G. Henschel alipotembelea Iceland na kutoa hotuba ya kuweka wakfu. Kwa miaka mingi jengo hilo lilitumiwa kama makao ya wamishonari na vilevile Jumba la Ufalme kwa makutaniko ya Reykjavík. Sasa jengo hilo ni ofisi ya tawi.
Jumba la Ufalme jipya na makao ya wamishonari huko Akureyri yalijengwa mwaka wa 1987. Umoja na undugu wa ulimwenguni pote wa watu wa Yehova ulionekana wazi wakati ndugu na dada 60 hivi kutoka Finland na Sweden walipokuja kuwasaidia ndugu wa Iceland katika ujenzi huo.
“Mbao Tamu”
Wawakilishi wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova wametembelea Iceland mara kwa mara, na ziara hizo zimewatia ndugu moyo sana. Tukio muhimu katika mwaka wa 1968 lilikuwa ziara ya Ndugu Knorr ambayo tumetangulia kutaja. Alitoa hotuba yenye kutia moyo, akasimulia mambo yaliyoonwa, na kuzungumzia maendeleo ya kazi ya kuhubiri Ufalme nchini Iceland.
Ndugu Henschel alitembelea Iceland kwa mara ya kwanza Mei 1970. Wamishonari kadhaa waliokuwa wamelemewa na usingizi walimkaribisha. Wamishonari hao walikuwa wamelemewa na usingizi si kwa sababu Ndugu Henschel alikuwa amefika asubuhi na mapema, bali kwa sababu walikuwa wamekesha wakitazama volkeno maarufu inayoitwa Hekla, ambayo ilikuwa imeanza kulipuka siku iliyotangulia.
Ndugu Henschel aliwatia moyo wamishonari na mapainia wa pekee hasa. Aliwaalika wote kwenye mkutano wa pekee na kusimulia mambo aliyojionea alipokuwa painia katika ile miaka ambayo uchumi ulikuwa umeshuka sana nchini Marekani. Aliwaeleza jinsi mapainia walivyobadilisha vitabu kwa kuku, mayai, siagi, mboga, miwani, na hata mtoto wa mbwa! Kwa njia hiyo, kazi ilisonga mbele katika nyakati hizo ngumu, nao mapainia hawakukosa mahitaji ya lazima.
Wageni wanaotembelea Iceland wanagundua haraka kwamba chakula ni tofauti na kile ambacho wamezoea. Aina moja ya chakula cha kipekee cha Iceland ni svid, yaani, kichwa cha kondoo kilichokatwa katika sehemu mbili na kuchemshwa. Wazia unatazama sahani yako na kuona nusu ya kichwa cha kondoo kikiwa na meno na jicho moja! Wageni wengi hawapendi hata kukiona. Samaki waliotoka tu kuvuliwa wanapatikana sikuzote. Chakula kingine cha kipekee ni hardfiskur: samaki ambaye ametolewa mifupa na kukaushwa. Samaki huyo hapikwi, bali huliwa pamoja na siagi. Kwa kawaida samaki huyo ni mgumu, na hupondwa ili awe laini. Basi, wamishonari walikuwa na hamu ya kusikia maoni ya Ndugu Henschel kuhusu chakula hicho. Baada ya kukionja wamishonari walimwuliza kama alikipenda. Alifikiri kidogo, kisha akajibu hivi kwa busara: “Sijawahi kula mbao tamu kama hii.”
Ndugu wanakumbuka ziara nyingine nyingi zenye kutia moyo za wawakilishi wa Baraza Linaloongoza. Ziara hizo zimewasaidia ndugu wa Iceland kuona kwamba ijapokuwa wao ni wachache na wanaishi mbali, bado wao ni sehemu ya undugu wa ulimwenguni pote wenye upendo wa Kikristo.
Uhusiano Mzuri Pamoja na Madaktari na Vyombo vya Habari
Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali yenye ndugu wanne ilianzishwa Iceland mwaka wa 1992. Ndugu wawili walienda Uingereza ili wazoezwe kufanya kazi hiyo, na wale wengine wawili wakaenda Denmark kwa kusudi hilohilo. Baada ya kuanzisha Halmashauri hiyo mpya, ndugu walipanga mkutano na kuwaalika wataalamu wa kitiba kwenye hospitali kubwa ya chuo kikuu. Watu 130 walihudhuria, wakiwemo madaktari, wauguzi, mawakili, na wasimamizi wa hospitali. Ndugu walikuwa na wasiwasi kidogo, kwa sababu huo ndio uliokuwa mkutano wa kwanza kufanywa pamoja na wataalamu wa kitiba. Hata hivyo, mkutano huo ulifanikiwa, na baadaye wakapanga kuwaona madaktari na wataalamu wengine kwenye hospitali mbalimbali. Ndugu hao pia walisitawisha uhusiano mzuri pamoja na madaktari wapasuaji kadhaa na madaktari wanaomtia mgonjwa ganzi kabla ya upasuaji. Kwa sababu ya uhusiano huo, matatizo yanayohusu matibabu yasiyohusisha damu yamezuiwa au kutatuliwa.
Sheria mpya kuhusu haki za wagonjwa ilipitishwa mwaka wa 1997. Sheria hiyo mpya inasema kwamba mgonjwa hapaswi kutibiwa bila kibali chake, na ikiwa mapendezi ya mtu aliyepoteza fahamu yanajulikana ni lazima yaheshimiwe. Sheria hiyo pia inasema kwamba ni lazima watoto wenye umri wa miaka 12 na zaidi waulizwe juu ya mapendezi yao kuhusu matibabu. Gudmundur H. Gudmundsson, ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali anasema hivi: “Kwa kawaida madaktari hutuunga mkono, na hakuna matatizo mengi. Hata upasuaji mkubwa hufanywa bila kumtia mgonjwa damu.”
Ofisi ya tawi iliwatia ndugu moyo wajitahidi kuwaachia watu wengi iwezekanavyo toleo la Amkeni! la Januari 8, 2000, ambalo linazungumzia upasuaji na matibabu yasiyohusisha damu. Ndugu kwenye ofisi ya tawi walitoa mapendekezo ya jinsi ya kutoa gazeti hilo na jinsi ya kujibu maswali kuhusu suala la damu. Mwanzoni baadhi ya ndugu walisitasita kutoa gazeti hilo, lakini muda si muda wakaona kwamba watu walitaka kujua habari hiyo. Waliwaachia watu zaidi ya nakala 12,000 za gazeti hilo. Hilo linamaanisha kwamba mtu 1 kati ya kila watu 22 alipata gazeti hilo nchini humo. Ndugu mmoja alisema hivi: “Kwa kuwa wengi walitaka mazungumzo, ilikuwa vigumu kumaliza eneo nililogawiwa.” Dada mmoja alisema: “Ni watu wawili tu waliokataa magazeti niliyowatolea!”
Mwanamke mmoja aliyekuwa akiongoza kipindi cha redio cha kila juma ambacho kilisikizwa kote nchini alipata gazeti hilo kuhusu matibabu yasiyohusisha damu. Katika kipindi chake alieleza jinsi alivyolipata, kisha akaeleza yale ambayo toleo hilo la Amkeni! linasema kuhusu jinsi matibabu ya kutia damu mishipani yalivyoanza. Alimalizia kwa kusema kwamba mtu yeyote anayetaka habari zaidi kuhusu matibabu yasiyohusisha damu anaweza kuwaomba Mashahidi wampe gazeti linalozungumzia habari hiyo.
Baada ya kusoma toleo hilo la Amkeni! watu wengi walielewa kwamba tuna sababu nzuri za kukataa kutiwa damu mshipani. Pia, walielewa kwamba Mashahidi wa Yehova hawataki kufa, bali wao hutafuta matibabu bora yaliyopo. Baadhi ya watu ambao hapo awali walikuwa wamepotoshwa juu ya msimamo wetu kuhusu damu walianza kusikiliza ujumbe wa Ufalme.
Majumba Mawili Yajengwa kwa Siku Nne
Ujenzi wa Majumba mawili ya Ufalme mwezi wa Juni ulikuwa tukio la kipekee sana kwa ndugu wa Iceland katika mwaka wa utumishi wa 1995. Moja lilijengwa Keflavík, na lile lingine huko Selfoss. Hayo ni Majumba ya kwanza kujengwa kwa muda mfupi nchini Iceland. Ujenzi wa yote mawili ulichukua siku nne tu na ulifaulu kwa msaada wa ndugu kutoka Norway. Ofisi ya tawi ya Norway ilituma vifaa vingi vya ujenzi, na ndugu na dada zaidi ya 120 kutoka nchi hiyo wakaja kusaidia kujenga. Maneno haya yalisikiwa mara nyingi mahali pa ujenzi: “Hili ni jambo la ajabu kabisa.” Ndugu nchini Iceland walikuwa wamesoma na kusikia kuhusu Majumba ya Ufalme yanayojengwa kwa muda mfupi, lakini sasa walijionea jambo hilo. Bila shaka, lilikuwa jambo la kustaajabisha kwamba kwa muda wa siku chache tu idadi ya Majumba ya Ufalme iliongezeka maradufu nchini Iceland!
Ndugu wa Iceland walipata Majumba mawili mapya ya Ufalme, na pia wakatiwa moyo kwa kushirikiana na ndugu na dada kutoka Norway waliojilipia nauli na kutumia siku zao za likizo ili kusaidia kujenga majumba hayo. Bila shaka, huo ni uthibitisho wa undugu wetu wa ulimwenguni pote! Ndugu wa Iceland pia walisaidia katika ujenzi huo. Wahubiri wenyeji 150 hivi walisaidia pia. Idadi hiyo ni karibu nusu ya wahubiri nchini Iceland.
Watu wa eneo hilo walipata ushahidi pia kupitia ujenzi wa Majumba hayo ya Ufalme. Vituo viwili vya televisheni vinavyorusha matangazo nchini kote vilizungumzia ujenzi huo katika vipindi vya habari na kuonyesha picha za majumba hayo mawili yaliyokuwa yakijengwa. Ujenzi huo ulizungumziwa pia katika vituo kadhaa vya redio na katika magazeti ya kila siku. Kasisi mmoja wa kanisa la Selfoss hakufurahi kwamba Mashahidi walitajwa mara nyingi katika vyombo vya habari. Kwa hiyo, katika gazeti la kila siku la eneo hilo, kasisi huyo alichapisha makala ya kuonya juu ya mafundisho hatari na ya uwongo ya Mashahidi wa Yehova. Alisema kwamba watu waliopungukiwa akili na wanaoweza kushawishika kwa urahisi walipaswa kujihadhari sana. Alipohojiwa kwenye redio alirudia maonyo hayo. Lakini maneno ya kasisi huyo hayakuwa na matokeo aliyotarajia. Badala yake, watu wengi walistaajabia ujenzi wa Majumba hayo ya Ufalme, na wengi ambao ndugu walikutana nao katika kazi ya kuhubiri walisema kwamba walishangaa kusikia maoni ya kasisi huyo.
Juma moja hivi baada ya onyo la kasisi huyo kuchapishwa, gazeti la kila siku lilikuwa na picha ya kuchekesha iliyochorwa. Katika sehemu ya mbele ya picha hiyo kuna kanisa, na nyuma kuna Jumba la Ufalme. Kuna mto kati ya majengo hayo mawili, na ndugu kadhaa wanaotabasamu na waliovalia vizuri wanatembea kwenye daraja kutoka kwenye Jumba la Ufalme wakielekea kanisani, wakiwa na mikoba yao ya utumishi. Nje ya kanisa, mwanamke anaruka kwa woga kutoka katika kiti chake cha magurudumu. Mtu aliyevunjika mguu na mwingine kipofu, wanatimua mbio huku wakipaaza sauti: “Kimbieni, kimbieni, Mashahidi wanakuja!” Yule kasisi amesimama kwenye ngazi ya kuingia kanisani, naye anaonekana kuwa ameshangaa. Wengi walipenda picha hiyo. Mhariri wa gazeti hilo na wafanyakazi wenzake walichagua picha hiyo kuwa picha bora ya kuchekesha ya mwaka huo, nao wakaikuza na kuibandika ukutani katika ofisi yao. Ilibaki hapo kwa miaka kadhaa.
Onyesho Latoa Ushahidi Mzuri
Katika mwaka wa utumishi wa 2001, onyesho lilifanywa kuhusu msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kutounga mkono siasa kabla na wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu ingawa waliteswa na Wanazi. Onyesho hilo lilifanywa katika miji mitatu, na jumla ya watu 3,896 wakahudhuria. Katika siku za mwisho za onyesho hilo zaidi ya watu 700 walisongamana katika jumba la onyesho mjini Reykjavík. Wakati wa onyesho hilo, video kuhusu msimamo wa Mashahidi wakati wa Nazi (Jehovah’s Witnesses Stand Firm Against Nazi Assault) ilionyeshwa mfululizo katika lugha ya Iceland kwenye sehemu hizo tatu. Watu wengi walitumia nafasi hiyo kutazama video hiyo pia.
Watu hao ambao hapo awali hawakujua kwamba Mashahidi waliteswa na Wanazi, walivutiwa na msimamo thabiti wa Mashahidi waliofungwa katika kambi za mateso. Profesa mmoja aliyekuja kutazama onyesho hilo mara kadhaa alisema kwamba alivutiwa sana, na kwamba amebadili maoni yake kuwahusu Mashahidi wa Yehova. Alivutiwa hasa na imani yenye nguvu ya Mashahidi waliofungwa katika kambi za mateso. Tofauti na wafungwa wengine, wangaliweza kupata uhuru kwa kukana imani yao.
Onyesho hilo pia lilizungumziwa kwenye kituo kimoja cha televisheni kinachorusha matangazo kote nchini na kwenye vituo vya televisheni na vya redio vya maeneo mbalimbali. Onyesho hilo lilipofunguliwa, kasisi mmoja wa Kanisa la Kilutheri alihudhuria pamoja na mkewe na binti yake. Muda fulani baadaye, ndugu mmoja alimwalika kasisi huyo kutembelea Betheli, naye akakubali. Siku chache baada ya ziara hiyo, mwanamke mmoja alimwendea kasisi huyo ili kumwuliza swali lililohusu andiko fulani la Biblia. Kasisi huyo alimtia moyo awasiliane na ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova, kwa sababu alikuwa na hakika kwamba wangemjibu. Baadaye, ndugu mmoja alijifunza Biblia pamoja na kasisi huyo.
Maendeleo Katika Kazi ya Kutafsiri
Mara nyingi imekuwa vigumu kwa wale wahubiri wachache nchini Iceland kutafsiri vitabu vyote kutoka kwa “mtumwa mwaminifu na mwenye busara” katika lugha ya Iceland. (Mt. 24:45) Katika miaka ya kwanzakwanza, vichapo vingi vilitafsiriwa na Mashahidi kutoka Iceland walioishi Kanada. Hatimaye kazi hiyo ilifanywa nchini Iceland. Wamishonari wa kwanza walipofika mwaka wa 1947, walipata kufahamiana na mshairi mzee aliyekuwa jirani yao. Alijua Kiingereza na aliwasaidia wamishonari hao kujifunza lugha ya Iceland. Alijitolea pia kuwasaidia kutafsiri. Hivyo, ndugu wakamwajiri kutafsiri kitabu, “Mungu na Awe wa Kweli” na kijitabu kimoja (The Joy of All the People). Jambo la kusikitisha ni kwamba alitumia maneno mengi ya kale na ya kishairi, na ijapokuwa mmoja wa wamishonari wapya na Ndugu Lindal waliisahihisha tafsiri hiyo na kuichapa upya, bado kitabu hicho hakikufaa kwa kuongoza mafunzo ya Biblia kama ilivyotarajiwa. Hata hivyo, kilisambazwa sana tangu kichapwe kwa mara ya kwanza, na jumla ya nakala 14,568 zilichapwa. Zaidi ya nakala 20,000 za kile kijitabu zilichapwa katika mwaka wa 1949. Baadaye, ndugu walimwajiri mtafsiri mwingine atafsiri kitabu kuhusu dini mbalimbali (What Has Religion Done for Mankind?)
Katika miaka hiyo, ndugu wachache walitafsiri vijitabu kadhaa. Kimojawapo ni “Habari Njema Hizi za Ufalme,” kilichotolewa mwaka wa 1959. Kijitabu hicho kiliwasaidia ndugu kuanzisha mafunzo mengi ya Biblia. Baada ya kijitabu hicho kuchapishwa, idhini ya kuchapisha Mnara wa Mlinzi katika lugha ya Iceland ilitolewa.
Vitabu vingi vizuri vilitafsiriwa na kutolewa katika miaka iliyofuata, kama vile: “This Means Everlasting Life” ambacho kilitolewa mwaka wa 1962; Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana, mwaka wa 1966; Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele, mwaka wa 1970; Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani, mwaka wa 1984; na Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele, mwaka wa 1996. Gazeti la Amkeni! limetolewa mara nne kwa mwaka katika lugha ya Iceland tangu mwaka wa 1982.
Kwa miaka mingi ndugu hawakuwa na kitabu cha nyimbo katika lugha ya Iceland. Nyimbo nne zilitafsiriwa na kuchapishwa mwaka wa 1960 kwa ajili ya kusanyiko. Na kwenye kusanyiko la wilaya mnamo Novemba 1963, ndugu walifurahi sana kupata kijitabu chenye nyimbo 30.
Kabla ya wakati huo, ndugu walikuwa wakiimba katika lugha mbalimbali mikutanoni. Günther na Rut Haubitz, mapainia wa pekee kutoka Ujerumani, walifika Iceland mwaka wa 1958. Rut bado anakumbuka kwamba ndugu kutoka nchi za kigeni walitumia vitabu vya nyimbo katika lugha yao kama vile Kidenishi, Kifini, Kiingereza, Kijerumani, Kinorway, au Kiswidi. Ndugu na dada wa Iceland waliimba katika lugha yoyote ile waliyoijua vizuri. Anasema, “Ilikuwa kwaya ya mchanganyiko kwelikweli!” Hatua kwa hatua, nyimbo nyingine za Ufalme zilitafsiriwa, na mwishowe kitabu chenye nyimbo zote 225 kikatolewa katika lugha ya Iceland mwaka wa 1999. Ndugu wanathamini sana zawadi hiyo bora kwa ajili ya kumsifu Yehova!
Kusanyiko la wilaya lililofanywa Agosti 1999 lilikuwa na jambo jipya kwa ndugu wa Iceland. Kitabu Sikiliza Unabii wa Danieli! katika lugha ya Iceland kilitolewa sambamba na kile cha Kiingereza. Msemaji alipokitangaza katika Kiingereza, wasikilizaji wote walipiga makofi. Lakini badala ya kuwaambia ndugu kwamba kitabu hicho kitatolewa baadaye katika lugha ya Iceland, aliwaonyesha nakala ya kitabu hicho katika lugha hiyo, akisema kwamba tayari kilikuwa kimetafsiriwa katika lugha ya Iceland! Wote walisisimka sana. Kitabu cha kwanza na cha pili cha Unabii wa Isaya—Nuru kwa Wanadamu Wote, pia kilitolewa sambamba na kile cha Kiingereza.
Betheli Yapanuliwa na Ndugu Waongezeka
Ofisi ya tawi ilirekebishwa mwaka wa 1998. Makao ya Wanabetheli yalinunuliwa ng’ambo ya barabara ili kuwe na nafasi kubwa zaidi kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya Idara ya Tafsiri. Katika miaka ya majuzi watafsiri wamefaidika kutokana na ziara za ndugu kutoka makao makuu huko New York. Ndugu hao wamewafundisha jinsi ya kutumia programu za kompyuta zilizotayarishwa na Mashahidi wa Yehova kwa ajili ya kazi ya kutafsiri.
Hivi majuzi, wawakilishi kutoka makao makuu walikuja ili kuongoza shule ya kuwasaidia watafsiri kuelewa lugha ya Kiingereza vizuri zaidi. Shule hiyo imewasaidia watafsiri kuelewa habari za Kiingereza vizuri zaidi kabla ya kuanza kuzitafsiri.
Ofisi ya tawi inaandika hivi: “Tunapofikiria miaka ambayo imepita, tunafurahi kwamba kulikuwa na watu ambao hawakuogopa kuanza kutafsiri katika lugha ya Iceland, ingawa hawakuwa na vifaa vya kutosha na hawakujua lugha hiyo vizuri. Ijapokuwa tafsiri hizo hazikuwa nzuri kama za leo, ‘hatudharau siku ya mambo madogo.’ (Zek. 4:10) Tunafurahi kuona kwamba jina la Yehova na Ufalme wake umejulikana nchini Iceland, na kwamba wengi wameijua kweli.”
Sasa kuna Wanabetheli wanane kwenye ofisi ya tawi. Wengine huja Betheli mara kwa mara kusaidia katika kazi. Jumba jipya la Ufalme limejengwa kwa ajili ya makutaniko yaliyo mjini Reykjavík badala ya lile lililokuwa kwenye ofisi ya tawi. Sasa kuna mipango ya kuipanua ofisi ya tawi ili kuwe na nafasi kwa ajili ya wafanyakazi wengi zaidi.
Kazi ya kuhubiri nchini Iceland imefanywa kwa ustahimilivu, kujidhabihu, na kwa upendo. Bila shaka, kazi ambayo wahubiri wa Ufalme wenye bidii wamefanya kwa miaka 76 si ya bure. Ndugu na dada wengi waaminifu wameshiriki katika kazi ya kuvuna. Wengi wamekuja kutoka nchi za kigeni ili kusaidia kuhubiri kwa miaka kadhaa, na kazi yao itakumbukwa kwa muda mrefu. Wengine wao wamebaki Iceland. Pia, wahubiri wenyeji wenye bidii, wanastahili pongezi kwa ustahimilivu wao.
Kuna wahubiri wa Ufalme wachache tu, lakini Mashahidi wa Yehova wanajulikana kotekote nchini Iceland. Kwa sasa kuna wamishonari saba wanaotumikia mashambani na katika makutaniko madogo kisiwani humo. Katika mwaka uliopita, watu 543 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo, na mafunzo ya Biblia 180 hivi yanaongozwa.
Huenda siku moja ndugu wa Iceland wakaona ongezeko kama lile linalotajwa katika Isaya 60:22: “Mdogo atakuwa elfu, na mnyonge atakuwa taifa lenye nguvu. Mimi mwenyewe, Yehova, nitaharakisha jambo hilo kwa wakati wake.” Mashahidi wa Yehova nchini Iceland wameazimia kumaliza kazi ambayo wamekabidhiwa na Mfalme Yesu Kristo, yaani, kuhubiri habari njema ya Ufalme. Wana hakika kwamba Mungu atafanya mbegu za kweli zimee katika mioyo inayoikubali na kuithamini kweli!—Mt. 24:14; 1 Kor. 3:6, 7; 2 Tim. 4:5.
[Sanduku katika ukurasa wa 205]
Mahali Ambapo Jina la Kwanza Huwa la Pili
Kupatana na mapokeo yao, wenyeji wa Iceland hawana majina ya ukoo: Watu hutumia jina la kwanza pekee. Jina la pili la mtoto hutokana na jina la babake ambalo huunganishwa na neno -son kwa mvulana na neno -dóttir kwa msichana. Kwa mfano, jina la pili la mwana wa mtu anayeitwa Haraldur ni Haraldsson, na jina la pili la binti ya mtu huyo ni Haraldsdóttir. Jina la mwanamke halibadiliki anapoolewa. Kwa sababu watu wengi wana jina lilelile, vitabu vya simu vinaonyesha jina la mtu, anwani, namba ya simu, na vilevile kazi yake. Rekodi za ukoo zinawawezesha wenyeji wa Iceland kujua majina ya mababu wao walioishi zaidi ya miaka 1000 iliyopita.
[Sanduku katika ukurasa wa 208]
Maelezo Mafupi Kuhusu Iceland
Nchi: Nchi hiyo, ambayo ni kisiwa, iko karibu na Mzingo wa Aktiki, na inazungukwa na Bahari ya Atlantiki Kaskazini, Bahari ya Greenland, na Bahari ya Norway. Kuna volkeno na chemchemi nyingi za maji ya moto na nyingine hurusha mvuke. Barafu hufunika asilimia kumi ya nchi hiyo.
Watu: Maharamia Waskandinavia, ambao walitoka Norway hasa, ndio mababu wa wenyeji wa Iceland. Wengi kati ya wenyeji hao ni wenye bidii, wenye kipawa cha kubuni, na tayari kukubali mawazo mapya. Watu wengi huishi karibu na pwani.
Lugha: Ingawa lugha ya wenyeji wa Iceland ndiyo lugha rasmi, watu wengi huongea lugha mbili au zaidi za kigeni, kama vile Kiingereza, Kijerumani, au mojawapo ya lugha za Skandinavia.
Kazi: Kazi ya uvuvi ni muhimu sana kwa uchumi wa Iceland. Samaki aina ya capelin, chewa, na heringi, huvuliwa kwa nyavu kubwa zinazovutwa na meli, na samaki wengi wanaovuliwa hutayarishwa na kuuzwa nchi za nje.
Chakula: Chakula cha kawaida ni samaki na kondoo. Kichwa cha kondoo kilichochemshwa hupendwa sana huko Iceland.
Hali ya hewa: Baridi hupunguzwa na mkondo fulani wenye joto katika Bahari ya Atlantiki. Kwa hiyo hakuna baridi kali sana nchini Iceland, lakini upepo huvuma sana katika majira ya baridi. Majira ya kiangazi yana joto la kiasi tu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 210]
Septemba 6, 1942: “Bado kuna painia mmoja tu katika nchi hii, kwa hiyo hakuna mengi ya kuripoti. Kuna watu 120,000 hivi nchini Iceland, na nyumba 6,000 hivi za wakulima. Hakuna njia nyingine ya kuzifikia nyumba hizo isipokuwa kwa farasi. Ili kuzitembelea zote, itambidi mtu kusafiri umbali wa kilometa 16,000 hivi na kuvuka milima na mito mingi. Hadi sasa ni watu wachache sana wanaopendezwa na ujumbe.”
Georg F. Lindal aliandika maneno hayo baada ya kuhubiri nchini Iceland kwa miaka 13. Alihubiri peke yake nchini Iceland kwa miaka mingine mitano.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 213, 214]
Walitumikia kwa Uaminifu
Oliver Macdonald ni mmoja kati ya wamishonari wa kwanza waliotumwa Iceland, naye alikuwa mhitimu wa darasa la 11 la Shule ya Gileadi. Alifika mnamo Desemba 1948 pamoja na Ingvard Jensen. Walisafiri kutoka New York hadi Iceland kwa meli ya mizigo. Safari hiyo ilichukua siku 14 na kulikuwa na dhoruba kwenye Bahari ya Atlantiki Kaskazini. Wote wawili walikuwa na kichefuchefu cha baharini karibu muda wote wa safari hiyo.
Mnamo Machi 1950, Ndugu Macdonald, au Mac, kama watu walivyopenda kumwita, alimwoa Sally Wild ambaye alikuwa amefanya kazi kwenye Betheli ya Uingereza. Mac na Sally walihubiri kwa bidii katika miaka hiyo ya kwanzakwanza, na watu ambao waliwafundisha bado wanamtumikia Yehova kwa uaminifu.
Mwaka wa 1957, Mac na Sally walirudi Uingereza, ambako Sally alikufa kutokana na kansa iliyokuwa imetambuliwa alipokuwa Iceland. Mac alirudia utumishi wa wakati wote baada ya Sally kufa. Kwanza alikuwa painia wa kawaida na baadaye mwangalizi anayesafiri kwa miaka 13. Mwaka wa 1960, alimwoa Valerie Hargreaves aliyekuwa painia wa pekee. Walifanya kazi ya mzunguko katika mizunguko mbalimbali nchini Uingereza, kuanzia kaskazini mwa Scotland hadi Visiwa vya Channel vilivyo karibu na pwani ya kusini ya Uingereza. Waliposafiri kuelekea sehemu ya kaskazini ya mzunguko wao hadi visiwa vya Shetland vilivyo karibu na pwani ya kaskazini ya Scotland, Mac alizoea kusema, “Tukisafiri kidogo tu kuelekea kaskazini tutafika Iceland!” lakini hakufikiri kamwe kwamba wangeenda Iceland.
Hata hivyo, Mac na Valerie waliwekwa kuwa wamishonari mwaka wa 1972 na kutumwa Iceland. Mac alikuwa msimamizi wa ofisi ya tawi na baadaye mratibu wa Halmashauri ya Tawi. Yeye na Valerie walikaa Iceland kwa miaka saba kisha wakatumwa Ireland kufanya kazi ya umishonari jijini Dublin na baadaye Ireland Kaskazini. Baada ya kutumika nchini Ireland kwa miaka 20, Mac alikufa kansa Desemba 1999, baada ya kuwa katika utumishi wa wakati wote kwa miaka 60. Valerie bado ni painia wa kawaida huko Belfast, Ireland Kaskazini.
[Picha]
Valerie na Oliver Macdonald walipokuwa Reykjavík katika miaka ya 1970
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 218]
Reykjavík
Reykjavík ndilo jiji kuu la Iceland. Mtu wa kwanza kukaa katika jiji hilo anaitwa Ingólfur Arnarson, naye alilipa jiji hilo jina Reykjavík, linalomaanisha “Ghuba ya Moshi.” Jina hilo linafaa kwa sababu ya mvuke unaotoka katika chemchemi za maji ya moto kwenye eneo hilo. Leo Reykjavík ni jiji la kisasa lenye shughuli nyingi, na lina watu 180,000 hivi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 223, 224]
Iceland Ni Kama Nyumbani Kwao
Páll Heine Pedersen ni mzaliwa wa Denmark. Alitumwa Iceland kama painia wa pekee mwaka wa 1959. Mwaka wa 1961 alihudhuria Makusanyiko ya Kimataifa mawili yenye kichwa “Waabudu Wenye Umoja” huko Ulaya. Alipokuwa huko alifahamiana na Violet, aliyekuwa amesafiri kutoka California, Marekani, ili ahudhurie baadhi ya makusanyiko hayo.
Baada ya makusanyiko hayo, Páll alirudi Iceland, naye Violet akarudi California. Waliandikiana barua kwa muda wa miezi mitano, kisha Januari 1962, Violet alienda Iceland kuolewa na Páll. Páll bado alikuwa painia, na alikuwa Shahidi pekee katika eneo lenye watu wachache, huko kaskazini-magharibi mwa Iceland. Waliishi katika mji mdogo ambako jua halichomozi kwa miezi miwili katika majira ya baridi kali. Ili kuwafikia baadhi ya watu katika eneo hilo, iliwabidi kusafiri kwenye barabara za milimani zenye miteremko mikali, ambazo mara nyingi zinateleza sana kwa sababu ya barafu. Walisafiri kwa pikipiki ambayo Páll alikuwa ameleta kutoka Denmark. Kwa sababu Violet alikuwa amezaliwa na kulelewa California ambako jua huwaka sikuzote, ndugu wengi walifikiri kwamba hangekaa nchini Iceland kwa muda mrefu. Lakini alikaa sana huko, naye akaipenda nchi hiyo na watu wake.
Páll na Violet walifanya kazi ya upainia pamoja mpaka binti yao, Elísabet, alipozaliwa mwaka wa 1965. Páll aliendelea na upainia hadi mwaka wa 1975, naye Violet alifanya kazi ya upainia mara kwa mara katika miaka hiyo. Mwaka wa 1977 waliamua kuhamia California kwa sababu Páll alikuwa na matatizo ya afya. Baada ya muda walitamani sana kutumika tena mahali ambapo palikuwa na uhitaji mkubwa wa wahubiri wa Ufalme. Walianza kazi ya upainia tena, na baada ya binti yao kumaliza shule na kufikia umri wa kujitegemea, wakatumwa Iceland kama wamishonari. Walifanya kazi ya umishonari na ya mzunguko kwa miaka michache. Halafu, mwaka wa 1989, Páll akaombwa atumike katika Halmashauri ya Ofisi ya Tawi. Kisha, mwaka wa 1991, Makao ya Betheli yakafunguliwa huko Iceland. Páll na Violet walikuwa kati ya Wanabetheli wa kwanza, nao wanaendelea na utumishi wao huko.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 228, 229]
Wanajulikana kwa Ukarimu Wao
Fridrik Gíslason na mkewe, Ada, walikuwa miongoni mwa wale watu saba waliobatizwa mwaka wa 1956. Oliver na Sally Macdonald ndio waliowafundisha kweli. Mwanzoni Fridrik pekee ndiye aliyejifunza Biblia, huku Ada akijishughulisha na kikundi cha washonaji wakati wa majira ya baridi kali. Shughuli za kikundi hicho zilipomalizika mwishoni mwa majira hayo, Ada alikuwa akiketi jikoni funzo lilipokuwa likiendelea. Hatimaye alianza kuwa na hamu ya kujua yale ambayo walijifunza katika Biblia, naye akaomba ruhusa ya kusikiliza bila kushiriki katika funzo hilo. Hata hivyo, baada ya muda mfupi alianza kushiriki kikamili.
Baadaye Funzo la Mnara wa Mlinzi katika Kiingereza lilifanywa kwa ukawaida nyumbani kwao. Walianza kuhudhuria mikutano iliyofanywa katika nyumba ya wamishonari. Fridrik anasema hivi: “Ninakumbuka tulifanya mikutano katika chumba kidogo kwenye orofa ya juu katika nyumba ya wamishonari. Chumba hicho kilitoshea viti 12, lakini watu wengi walipohudhuria, tulifungua mlango wa chumba kingine kidogo na kukitumia pia. Mambo yamebadilika kwelikweli. Leo kuna makutaniko matatu huko Reykjavík, na Jumba la Ufalme hujaa wakati wa mikutano!”
Fridrik na Ada wanajulikana sana kwa ukarimu wao. Ijapokuwa walikuwa na watoto sita, sikuzote waliwakaribisha ndugu nyumbani kwao. Katika miaka ya kwanzakwanza baada ya kutaniko kuanzishwa, wengi waliokuja Iceland kutoka nchi nyingine walifurahia kukaa nyumbani kwa Fridrik na Ada hadi walipopata makao yao wenyewe.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 232]
Biblia Katika Lugha ya Iceland
Biblia ilitafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Iceland miaka ya 1300. Biblia hiyo inayoitwa Stjórn ina sehemu za Maandiko ya Kiebrania zilizotafsiriwa na kufafanuliwa. Tafsiri kamili ya kwanza ya “Agano Jipya” ilichapishwa katika lugha ya Iceland mwaka wa 1540. Mtafsiri wa Biblia hiyo ni Oddur Gottskálksson, mwana wa askofu wa Hólar. Oddur alikuwa mfuasi wa Kanisa la Kilutheri alipokuwa Norway, na alikuwa amefahamiana na Martin Luther huko Ujerumani. Inasemekana kwamba baada ya Oddur kurudi Iceland, alifanya kazi hiyo ya kutafsiri katika kibanda cha ng’ombe, naye alipata magumu mengi kwa sababu hakutaka kumwudhi mwajiri wake, yaani, askofu wa Kanisa Katoliki huko Skálholt. Oddur alitegemea Biblia ya Kilatini inayoitwa Vulgate alipotafsiri, naye mwenyewe akapeleka tafsiri yake nchini Denmark ili ichapishwe. Mnamo mwaka wa 1584, Askofu Gudbrandur Thorláksson aliagiza Biblia nzima ya kwanza katika lugha ya Iceland ichapishwe. Biblia nzima ya kwanza kutafsiriwa kutoka lugha ya awali ya Kiebrania na Kigiriki ilichapishwa mwaka wa 1908. Ilirekebishwa na kuchapishwa tena mwaka wa 1912.
[Picha]
“Gudbrandsbiblía” ni Biblia nzima ya kwanza katika lugha ya Iceland
[Chati/Picha katika ukurasa wa 216, 217]
ICELAND—MFUATANO WA MATUKIO
1929: Georg F. Lindal, mhubiri wa kwanza nchini Iceland, afika.
1940
1947: Wamishonari wa kwanza kutoka Shule ya Gileadi wafika.
1950: Kutaniko dogo laanzishwa.
1960
1960: Gazeti la Mnara wa Mlinzi lachapishwa katika lugha ya Iceland.
1962: Ofisi ya tawi yafunguliwa Reykjavík.
1975: Ujenzi wa ofisi mpya ya tawi iliyopanuliwa wakamilishwa, na jengo hilo lawekwa wakfu.
1980
1992: Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali yaanzishwa.
1995: Majumba mawili ya Ufalme yajengwa kwa siku nne katika mwezi wa Juni.
2000
2004: Kuna wahubiri 284 huko Iceland.
[Grafu]
(See publication)
Jumla ya Wahubiri
Jumla ya Mapainia
300
200
100
1940 1960 1980 2000
[Ramani katika ukurasa wa 209]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
ICELAND
Húsavik
Hólar
Akureyri
Seydhisfjördhur
Neskaupstadhur
Eskifjördhur
Stykkishólmur
Borgarnes
Höfn
REYKJAVÍK
Skálholt
Keflavík
Selfoss
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 202]
[Picha katika ukurasa wa 207]
Kulia: Georg F. Lindal, 1947
[Picha katika ukurasa wa 207]
Chini: Ndugu Lindal na farasi wa Iceland mapema katika miaka ya 1930
[Picha katika ukurasa wa 212]
Baadhi ya wamishonari wa kwanza kutumwa Iceland, kutoka kushoto hadi kulia: Ingvard Jensen, Oliver Macdonald, na Leo Larsen
[Picha katika ukurasa wa 220]
Ofisi ya tawi ilikuwa katika jengo hili kuanzia mwaka wa 1962 hadi 1968
[Picha katika ukurasa wa 227]
Zaidi ya wahubiri 100 kutoka Iceland walihudhuria Kusanyiko la Kimataifa la “Amani Duniani” huko Copenhagen, Denmark, mwaka wa 1969
[Picha katika ukurasa wa 235]
Iiris na Kjell Geelnard huko Akureyri, Januari 1993
[Picha katika ukurasa wa 238]
Kulia: Meli ya uvuvi iitwayo “Svalbakur”
[Picha katika ukurasa wa 238]
Chini: Fridrik na Kjell
[Picha katika ukurasa wa 241]
Kulia: Oddný Helgadóttir
[Picha katika ukurasa wa 241]
Chini: Gudrún Ólafsdóttir
[Picha katika ukurasa wa 243]
Kulia: Jumba la Ufalme na makao ya wamishonari huko Akureyri
[Picha katika ukurasa wa 243]
Chini: Bjarni Jónsson mbele ya ofisi ya tawi
[Picha katika ukurasa wa 249]
Juu: Ujenzi wa Jumba la Ufalme huko Selfoss, mwaka wa 1995
[Picha katika ukurasa wa 249]
Kulia: Jumba la Ufalme la Selfoss
[Picha katika ukurasa wa 253]
Familia ya Betheli huku Iceland
[Picha katika ukurasa wa 254]
Halmashauri ya Ofisi ya Tawi, kuanzia kushoto kuelekea kulia: Bjarni Jónsson, Gudmundur H. Gudmundsson, Páll H. Pedersen, na Bergthór N. Bergthórsson