Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb90 kur. 66-147
  • Austria

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Austria
  • 1990 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • Jitihada za Kwanza za Kutoa Ushuhuda
  • Mwanzo wa Vuno la Baada ya Vita
  • Masikio Yenye Kusikiliza Kwenye Hotuba ya Kukumbukwa
  • Utendaji Katika Mikoa
  • Mkutano Wenye Ghasia Katika Vienna
  • “Sitakupungukia Kabisa”
  • Mazishi Yavuta Fikira
  • Mianzo Midogo, Jitihada Yenye Kuendelea
  • Kusonga Mbele Usoni pa Mbano
  • Wanyanyaswa kwa Kuwa Wakristo
  • Kulikuwako Baiskeli Moja Tu
  • Kupigania Haki za Kisheria
  • Makundi Mapya, Hudhurio Lenye Kukua
  • Upinzani Waongezeka
  • Kukaguliwa na Kunyang’anywa Fasihi
  • Msukosuko wa Kisiasa Waleta Vizuizi
  • Shirika la Nchini Lavunjwa na Wenye Mamlaka
  • Kuweka Ufalme Kwanza Vijapokuwa Vizuizi
  • Kwa Nini Walikuwapo?
  • Vizuizi Juu ya Mikutano
  • Kujitayarishia Mnyanyaso Uliotazamiwa
  • Vikosi vya Ujeremani Vyavuka Mpaka
  • Madai ya Mamlaka Mpya Zenye Kutawala
  • Uandalizi wa Chakula Kilichohitajiwa
  • Dada Wajasiri Wajaza Uhitaji Muhimu
  • Je! Shetani Alikuwa Akithibitika Kuwa Mshindi?
  • Aina Mbili za Mifuko ya Chakula
  • Msaada kwa Ndugu Msimamizi
  • Mikononi mwa Adui
  • Kutoa Ushahidi kwa Ujasiri Mahakamani
  • Kurudufisha Fasihi
  • Adui Atafuta Kirudufishaji
  • Je! Yeye Aliacha Msimamo Wake?
  • Wachanga Lakini Washikamanifu
  • Kutiwa Mbaroni Katika Usiku wa Ukumbusho
  • Msimamo kwa Ajili ya Kutokuwamo kwa Kikristo
  • Jitihada za Bure za Wakuu wa Nazi
  • Mazoezi ya Utumishi wa Kazi ya Taifa
  • Wauawa kwa Sababu ya Kutokuwamo kwa Kikristo
  • Maneno ya Imani Kutoka Seli ya Kifo
  • Watenganishwa na Watoto Wao
  • Mchanga Lakini Mwaminifu
  • Jihadhari! Wajasusi na Watoa-Habari
  • Jaribio la Mahakama Lisilo la Kawaida
  • Mtumishi Mnyenyekevu
  • Kutumia “Chakula” Haba
  • Wachache Warudi Nyuma
  • Kuvumilia Mateso ya Kambi
  • Utendaji wa Kitheokrasi Ndani ya Zile Kambi
  • Rekodi ya Uaminifu
  • Tutafanya Nini Kwanza?
  • Kisha—Siberia!
  • Mapainia Washiriki Vuno
  • Mipango ya Tawi
  • Upanuzi wa Vifaa vya Tawi
  • Eneo Lenye Lugha Nyingi
  • Kuwa Wakaribishaji Kwenye Mkusanyiko
  • Namna Gani Ndugu Kutoka Polandi?
  • Kusonga Mbele Kuingia Ndani ya Wakati Ujao
1990 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb90 kur. 66-147

Austria

MILIMA Alps ya Austria huvuma kwa sauti ya muziki. Ikijulikana sana kwa mitungo ya kimuziki ya hali ya juu mno iliyotokezwa na Haydn, Mozart, Schubert, akina Strauss, na wengineo, Austria ina sifa pia kwa uzuri wayo wa kiasili. Misitu mizito, maziwa-maji maangavu, na mabonde mapana hutenganisha mingi ya milima yayo ya Alps yenye kufunikwa na theluji, ambayo hufika ndani ya anga kwa njia yenye fahari kwa kadiri ya kimo cha meta 3,797. Hatimaye vilele hivi hushuka polepole na kuwa vilima na nyanda za chini za kilimo zenye rutuba zikitanuka kwa utaratibu upande wa mashariki. Upendezi wa mandhari hizi nzuri umeongezewa uzuri wa kiroho wa ukweli wa Biblia ambao uliibuka katika Austria miaka ya mapema ya 1900. Na tangu hapo, vilele vyenye kuinuka juu vya Austria na nyanda za chanikiwiti zimekuwa zikirudisha mwangwi kwa ‘nyimbo zikimsifu Mungu’ Yehova.—Zab. 149:6, NW.

Kwa karne nyingi Austria ilikuwa sehemu ya Milki Takatifu ya Roma ya taifa la Kijeremani. Baadaye iliunganishwa na Hangari katika Milki ya Austro-Hangari. Hivyo haishangazi kwamba asilimia 98 ya idadi ya watu husema Kijeremani na kwamba vikundi vya kikabila hutia ndani Wamagya (Wahangari), Wakroati, na Waslovene. Wakati Vienna ulikuwa ndio mji mkuu wa milki kubwa mno, pamoja na wakati wa vipindi vya baada ya vile vita vya ulimwengu, hesabu kubwa za watu walimiminika makundi makundi kuja kuishi katika jiji hili lenye kuvutia lililoko kwenye Mto Danube. Hivyo, zaidi ya asilimia 20 ya idadi ya watu wa Austria wapatao 7,555,000 hupatikana sasa katika Vienna.

Kwa karne nyingi dini rasmi katika Austria ilikuwa Ukatoliki wa Roma, kama ilivyoamrishwa na watawala wa Hapsburg. Hata leo, asilimia 84 ya idadi ya watu hudai kuwa Wakatoliki wa Roma, na kuna itifaki kati ya Austria na Vatikani ambayo huhakikishia Kanisa Katoliki utegemezo wa kifedha wa serikali. Asilimia nyingine 6 huorodheshwa kuwa Waprotestanti. Hata hivyo, tarakimu hizi hazionyeshi mwelekeo halisi wa watu kuelekea dini, kwa kuwa kujitoa kwa watu kwa matengenezo ya kidini kumepungua sana. Wengi wao hujizuia kuvunja waziwazi mafungamano yao ya dini ya kimapokeo kwa sababu hangaikio la Mwaustria wa kawaida ni, ‘Watu watasema nini?’

Jitihada nyingi na baraka ya roho ya Yehova imekuwa ikitakwa ili kupata watu mmoja mmoja wenye kuhofu Mungu na kuwafundisha njia za Yehova. Kama tokeo, leo katika Austria kuna watu zaidi ya 17,700 ambao wameonyesha kwamba hangaikio lao kubwa zaidi ni, ‘Mungu atasema nini?’ Hao wamefanyiza makundi 246 ya Mashahidi wa Yehova.

Jitihada za Kwanza za Kutoa Ushuhuda

Mwanzoni mwa karne ya 20, maisha ya kidini katika Austria yalifuata hatua zilizowekwa sana sana na Kanisa Katoliki la Roma. Ingawa Waprotestanti walikuwa na haki fulani ambazo zilikuwa zimeruhusiwa chini ya ile iliyoitwa eti Sheria ya Uvumiliano katika 1781, watu wengine walio wengi waliruhusiwa kuzoea dini yao kwa faragha tu. Ijapokuwa hivyo, Charles Taze Russell, msimamizi wa kwanza wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, aliamua kwenda Vienna katika 1911 akaelekeze uangalifu wake kwanza kwa jamii ya Wayahudi.

Akisafiri kwa garimoshi, aliwasili Vienna, ambapo jumba kubwa la Hoteli Continental lilikuwa limekodishwa kwa ajili ya Machi 22. Hotuba yake, iliyokusudiwa iwavutie Wayahudi wenye mioyo myeupe, ingekuwa “Usayuni Katika Unabii.” Idadi ya watu walio Wayahudi wangekuwa na tendo-mwitikio gani kwa maelezo yake juu ya unabii wa Biblia? Kutoka New York, rabi mmoja Myahudi alikuwa ametuma kwa simu ujumbe mrefu wa visingizio, akiwaonya Wayahudi dhidi ya Wanafunzi wa Biblia, kama walivyojulikana Mashahidi wa Yehova wakati huo. Kama tokeo, ingawa jumba lilikuwa limejaa pomoni wakati Ndugu Russell alipopanda jukwaani, aling’amua upesi kwamba yapata theluthi moja ya wale waliokuwa kati ya wasikilizaji walikuwa wamepiga moyo konde wamzuie kunena.

Baadaye Russell aliripoti hivi: “Kutoka mwanzo wenyewe wa hotuba yetu, walipaaza sauti na kupiga makelele kutoka sehemu zote za jumba na baadhi yao walionekana kama wamepagawa na mashetani. . . . Sisi tulijaribu kunena neno moja au mawili ili kuondoa hofu zao, lakini wapi. . . . Idadi kadhaa walionekana kuwa na hamu nyingi ya kututia mikononi mwao, lakini kikundi imara cha wenye akili zaidi kilifanyiza kinga kutuzunguka. Sisi hatukuwa na hofu, lakini wale waliojua wapinzani wetu vizuri zaidi walionekana wakituhofia sana. Kwa kuona kwamba hatungeweza kutimiza lolote, tuliwapungia mkono kwa tabasamu, kuonyesha kwamba tulikuwa tukiacha jaribio hilo, na tukaondoka jukwaani. Wayahudi wale wale walifungua njia mbele yetu na wakawazuia wapinzani wowote na kutuongoza kutoka jumbani . . . Wapatao kumi na watano walikuja siku iliyofuata na kutuuliza maswali zaidi kuhusiana na mpango wa kimungu.”

Kwa manufaa ya watafutaji ukweli wenye mioyo myeupe, mipango ilifanywa pia kutangaza kwa kupiga chapa maandishi yote ya hotuba ya Russell katika karatasi-habari Neues Wiener Journal (Jarida Mpya la Vienna).

Huu haukuwa wakati wa kwanza Ndugu Russell kuona Vienna. Miaka ishirini mapema, katika 1891, alikuwa amefunga safari iliyompeleka kutoka Dresden, Ujeremani, kupitia Vienna kufika Kishinev katika Urusi. Akitoa elezo juu ya hali kama alivyoielewa huko nyuma katika wakati huo, Ndugu Russell alitaarifu hivi katika Zion’s Watch Tower ya Novemba 1891: “Sisi hatukuona mwanzo au utayari kwa ajili ya ukweli katika Urusi, . . . hakuna kitu cha kututia moyo tutumaini vuno lolote katika Italia au Uturuki au Austria au Ujeremani.”

Ijapokuwa hivyo, jaribio zaidi lilifanywa kusaidia angalau baadhi ya watu wa hapa. Mapema katika 1914, Maxwell G. Friend (wakati huo akijulikana kwa jina Freschel, aliyezaliwa na wazazi Wayahudi) aliombwa aende Austria-Hangari kutoka Kao la Betheli katika Ujeremani ili akaeneze habari njema za Ufalme wa Kimesiya miongoni mwa Wayahudi. Huko Vienna aliweza kuanzisha funzo la Biblia la nyumbani la ukawaida pamoja na waandikishaji wawili wa Zion’s Watch Tower. Aliripoti hivi: “Wayahudi hawakuitikia habari njema wakati wowote, kwa sababu walitufikiria kimakosa kuwa wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo. Hawakupenda Jumuiya ya Wakristo kwa sababu ya zile karne nyingi ambazo ilikuwa imewafukuza toka nchi hata nchi na kuwaua bila huruma kwa moto na upanga.”

Katika muda wa miezi michache Vita ya Ulimwengu 1 ikafyatuka. Je! hiyo ingekomesha jitihada zote za kushiriki habari njema pamoja na watu wa Austria?

Mwanzo wa Vuno la Baada ya Vita

Katikati ya hofu kuu za vita ya ulimwengu, kulikuwako watu waliofikiria na kuongea juu ya mambo ya kiroho. Johann Brotzge, ajapokuwa kijana, alikuwa mmoja ambaye alikuwa na maoni ya kidini yenye kina kirefu sana. Katika mahali pake pa kazi katika jiji la Dornbirn, yeye alipelekea makaa-mawe mwanamume mmoja jina lake Degenhart, aliyekuwa msimamizi wa tanuri. Wakati wa mojapo safari zake za kupeleka makaa-mawe mapema katika vuli ya 1917, Degenhart alianzisha mazungumzo juu ya Ufalme wa Mungu. Upesi baada ya hapo kijana Johann aliandikishwa katika utumishi wa kijeshi. Je! zile mbegu za ukweli alizokuwa amesikia zingetia mizizi?

Baada ya kupatwa na hofu kuu za vita, Johann alirudi nyumbani. Yale maneno juu ya Ufalme wa Mungu yalikuwa yameacha uvutano mkubwa na yalikuwa yangali akilini mwake. Alianza kumtafuta Degenhart. Lakini loo, ilikuwa huzuni kama nini, kwa wakati uliopo Degenhart alikuwa amekufa. Hata hivyo, katika masika ya 1919, Johann Brotzge akaja kukutana na Otto Mathis pamoja na Xaver Klien, ambaye kufikia wakati huo alikuwa Mwanafunzi wa Biblia. Johann alipata fasihi yake ya Biblia aliyokuwa ameitamani kwa muda mrefu kutoka kwa Otto. Wanaume hao ndio waliokuwa Wanafunzi wa Biblia wa kwanza katika magharibi mwa Austria.

Kilometa zapata 680 hivi kutoka huko, upande wa mashariki wa nchi, ukweli ulipata mizizi katika moyo mwingine wenye kuitikia. Kijana Johannes Ehm alikuwa ameajiriwa akiwa mwalimu wa kufundisha muziki katika kijiji cha Deutsch Wagram katika uwanda wa Marchfeld, wakati wa miaka ya 1919 na 1920. Mume na mke waliokuwa marafiki wake walikaribisha mhandisi kutoka Ujeremani akae nao akiwa mpangaji. Mume na mke hao walimwambia Johannes kwamba mhandisi huyo, Bw. Goller, alinena juu ya mambo mapya na mageni kabisa. Alisema kwamba mwisho wa ulimwengu ulikuwa karibu, kwamba hakuna moto wa helo (mateso), na kwamba waamini walio wengi hawangeenda mbinguni, bali, siku fulani wangeishi juu ya dunia. Isitoshe, alishikilia kwamba angeweza kuthibitisha yote hayo kutoka kwa Biblia. “Je! wewe ungetaka kuhudhuria mazungumzo kama hayo?” mume na mke hao wakamuuliza kijana huyo aliye mwalimu wa muziki.

Kwenye mazungumzo hayo Johannes aliiona Biblia kwa mara ya kwanza kabisa maishani mwake. Baadaye alisema hivi: “Goller alionyesha utulivu na kwa utulivu akajibu maswali yangu yote—na hayakuwa machache!” Upesi Johannes aliagiza yale mabuku sita ya Studies in the Scriptures, yaliyoandikwa na C. T. Russell, na kwa hamu nyingi akaanza kujifunza hayo.

Kwa wakati uliopo, katika Klagenfurt kusini mwa Austria, Franz Ganster, kijana mtunza-hesabu, alifahamiana kwa barua na mwanamume mmoja katika Uswisi jina lake Egg. Kuandikiana kwao kulitia ndani mengi zaidi ya kukusanya stampu tu na kubadilishana picha za postikadi. Kwa kuwa tayari Egg alikuwa mmoja wa Wanafunzi wa Biblia, kijana wetu Mwaustria mtunza-hesabu alisikia ujumbe wa Biblia kutoka kwake. Ganster alipeleka agizo la fasihi yote ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi iliyopatikana wakati huo katika Uswisi, nayo ilipelekwa kibinafsi na mfanyiza mapipa jina lake Leopold König aliporudi Austria kutoka Uswisi katika 1921. Tutaona baadaye kilichoanzishwa na jambo hili.

Karibu na wakati uo huo, Mwanafunzi wa Biblia kutoka Ujeremani aliaachia kijitabu mume na mke walioishi katika Linz, sehemu ya kaskazini ya Austria. Kijitabu hicho kilikuwa na kichwa Millions Now Living Will Never Die. Baada ya kukisoma na kukipitisha kwa rafiki yao, mkulima mmoja jina lake Simon Riedler, walimwambia, “Kimeandikwa kwa mtindo wa kiajabu-ajabu.” Kwa hiyo Simon Riedler alikitupia jicho kivivi-hivi tu na kwa hali ya akili ya mashaka-mashaka hivi. ‘Pengine hakuna kitu ila upuuzi tu,’ akafikiri mwenyewe.

Ijapokuwa hivyo, alikisoma mara ya pili, kisha mara ya tatu. Je! hatimaye yeye angethamini vito vya ukweli vilivyo katika kijitabu hicho? Ndiyo, hata kufikia hatua ya kuhisi kuaibikia yale mashaka-mashaka yake ya kwanza.

Akitamani kupeleleza ujumbe huo kikamili zaidi, Simon aliandika barua kuipeleka Vienna kwenye anwani iliyopewa nyuma ya kijitabu hicho. Ni muda mrefu kadiri gani alikuwa ametaka kuwa na Biblia! Hivyo akaja kuwasiliana na Leopold König, yule mfanyiza mapipa aliyekuwa amerudi kutoka Uswisi na sasa alikuwa akitumikia akiwa kolpota. Wakati Ndugu König alipopelekea mkulima huyo chapa ya mfukoni ya Biblia ya Luther, pengine hakuwazia ile shangwe kuu ambayo Biblia hiyo ingesababisha. Hatimaye, Simon Riedler alikuwa na Biblia yake mwenyewe! Pamoja nayo, alisoma Zion’s Watch Tower na Food for Thinking Christians. Jamaa yake, watu wa ukoo, na majirani walimrundikia dhihaka. Lakini Simon Riedler alikuwa amepata ukweli; hilo tu ndilo lilikuwa jambo la maana. Kama alivyosema baadaye: “Moyo wangu ulikuwa umejaa, na midomo yangu ilikuwa ikifurika.”

Masikio Yenye Kusikiliza Kwenye Hotuba ya Kukumbukwa

Mwishoni-mwishoni mwa masika ya 1921, mhadhara juu ya kichwa chenye kuvutia “Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe” ulitolewa katika Sofiensäle (Jumba liitwalo Sofia) lenye nafasi kubwa katika jiji Vienna lenye mandhari nzuri. Tendo-mwitikio kwa ujumbe huo lilikuwa tofauti sana na lile ambalo Ndugu Russell alikuwa amekutana nalo miaka kumi mapema.

Ripoti moja kuhusu mkutano huo husema: “Ujumbe huo ulikuwa na tokeo kubwa sana. Tangazo lilitokeza wonyesho wa idili na kuzusha mazungumzo mengi katika barabara za jiji kabla ya mkutano huo kuanza. Jumba lilijazana na milango ilifungwa muda mrefu kabla ya mhadhara kuanza, huku mamia wakigeuziwa mbali. Umati huo ulisikiliza kwa kukaza fikira sana ujumbe huo mzuri ajabu wa kusimamishwa kwa Ufalme wa Mungu na ile ahadi ya Kibiblia yenye kufariji ya kwamba mamilioni wanaoishi sasa hawatalazimika kufa.” Jioni hiyo nakala 2,100 za kijitabu Millions ziliangushwa, na anwani 1,200 zilitolewa ili ziara za kufuatia zifanywe.

Miongoni mwa wale walioathiriwa sana na hotuba hiyo alikuwa Hans Ronovsky. Yeye hakuwapo kwenye Sofiensäle. Lakini majuma machache baadaye alipokuwa akitembea-tembea katika mojapo barabara za maduka za Vienna, uangalifu wake ulinaswa na karatasi iliyotangaza mhadhara uo huo, ambao ungetolewa kwenye Konzerthaus. Yeye alienda, si kushangilia wolzi (wimbo wa kimuziki) wa Strauss au mchezo wa kuigiza wa Mozart, bali kusikiliza ile melodia yenye kupendeza ya kweli za Biblia. Aliyosikia yalithibitika kuwa jambo la kubadili maisha yake.

Utendaji Katika Mikoa

Sasa uangalifu ulielekezwa kwenye vitovu vingine vyenye idadi kubwa ya watu kote kote nchini. Siku moja Franz Ganster alipokea postikadi kutoka Vienna. Ilimpasa akodishe jumba kubwa zaidi awezalo kupata katika Klagenfurt kwa ajili ya mhadhara ambao ungetolewa na Ndugu Emil Wetzel, ambaye alikuwa ametumwa kutoka Dresden, Ujeremani, kusimamia kazi katika Austria. ‘Basi, hiyo ingeweza kuwa lile jumba katika Hoteli Sandwirt,’ Ganster akafikiri mwenyewe, akitoka kwenda mara hiyo kutafuta mwenye hoteli hiyo.

“Mimi ningedokeza,” akasema meneja wa hoteli hiyo, “kuweka meza na viti katika jumba kulifanya lionekane kuwa limejaa zaidi, kwa kuwa kwa hakika ni watu wachache tu watahudhuria.”

Ganster akajibu kwa uthabiti, “Mimi nina agizo nikodishe jumba likiwa na viti tu.”

Sasa, ni nani angegawanya zile karatasi nyingi za mwaliko kwa ajili ya hotuba hiyo? Ganster, mwenyewe akiwa mwanamume mfanya kazi, alikuwa na wazo. Aliajiri wanaume kadhaa, nao wakagawanya karatasi za mkononi 3,000 katika jiji hilo. Kama hudhurio lilivyoonyesha baadaye, kwa wazi wao walifanya kazi nzuri. Meneja wa hoteli alikadiria kwamba watu 2,000 walihudhuria hotuba hiyo. Na si sakafu kuu tu iliyojazana watu bali veranda pia.

Miongoni mwa waliokuwapo alikuwa Richard Heide, mwanafunzi wa miaka 20. Baada ya kuona karatasi iliyotangaza ile hotuba “Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe,” alimwambia babaye: “Baba, mimi ninaenda kusikia hotuba hiyo hata yeyote aseme nini. Mimi nataka kujua kama huu ni udanganyifu tu au kama mna ukweli wowote!” Kwa hiyo akaenda, na baba yake na dada yake Therese wakaamua kuandamana naye.

Baada ya hotuba hiyo wasikilizaji wengi waliacha anwani zao, pamoja na ombi la fasihi. Ili kutimiza maombi hayo, Franz Ganster aliagiza ugavi wa kutosha wa Studies in the Scriptures. Alipokea kiasi kikubwa sana hivi kwamba bibi mwenye kumpangisha nyumba alishangaa angeweka wapi vifurushi vyote hivyo. Chumba chake kilijaa fasihi toka sakafuni hata darini, ikimwachia Franz mwenyewe nafasi kidogo sana.

Bw. Heide, kwa kusisimuliwa na hotuba hiyo, pia aliagiza yale mabuku saba ya Studies in the Scriptures, ambayo aliyasoma kwa hamu nyingi. Kabla ya muda mrefu kupita, mikutano ilikuwa ikifanyiwa nyumbani mwake. Mara nyingi, kufikia watu 30 walisongamana pamoja katika sebule yake.

Pia, katika Graz mikutano ilifanywa mapema kama masika ya 1922. Hotuba zilitolewa pia katika miji mingine ya kimkoa. Hivyo kazi ya Yehova ilikuwa ikiongezeka nguvu mikoani.

Lo, wahubiri hawa katika Klagenfurt walikuwa kikundi chenye bidii kama nini! Kwani, walikuwa hata hawajazamishwa bado. Haikuwa mpaka Julai 5, 1922, kwamba uzamisho ukatukia katika Vienna; kisha juma lililofuata ubatizo ukafanywa katika mkoa wa Karinthia ambako yale matunda ya kwanza ya eneo hili walizamishwa katika maji ya Wörther See wenye kupendeza. Hao walitia ndani Franz Ganster, Bw. na Bi. Heide (wazazi), watoto wao wawili Richard na Therese, na Bw. Kopatsch, ambaye baadaye alijulikana sana kwa bidii na uhuru wake wa kusema.

Kwa wakati uliopo jambo fulani lilikuwa limetukia katika Vienna ambalo lilizusha mazungumzo moto-moto si miongoni mwa watu wa Mungu tu bali pia miongoni mwa wengine.

Mkutano Wenye Ghasia Katika Vienna

Wakati alipokuwa akizuru ofisi za tawi mbalimbali katika 1922, Ndugu Rutherford, msimamizi wa pili wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, alitia ndani ziara katika Vienna kutoka Mei 30 kufika Juni 1. Mipango ilifanywa mhadhara utolewe katika Katharinenhalle (Jumba Katherine) lenye nafasi kubwa. Je! upokezi ungekuwa wenye kupendeleka zaidi ya wakati Ndugu Russell alipojaribu kusema katika Vienna miaka 11 mapema?

Wakati Ndugu Rutherford na mkalimani wake, Ndugu Conrad Binkele (kutoka Uswisi), walipopanda jukwaani, kila nafasi iliyopatikana katika jumba, kutia na vijia, ilijaa watu. Baadhi yao hata walikuwa wanakalia jukwaa, hata mpaka kufikia msemaji. Wengine walikuwa wangali wanajaribu kuingia. Hata hivyo, miongoni mwa maelfu waliokuwapo, mlikuwamo mamia kadhaa ambao walikuwa wamekuja si kusikiliza hotuba ile kwa utulivu, bali, kuikatiza. Wapinzani wa ujumbe wa Biblia walikuwa wameweka mabaradhuli wao kote kote katika wasikilizaji, hasa kuelekea nyuma ya jumba.

Mambo yote yalienda sawa kwa zapata dakika 40 za kwanza za hotuba. Hata hivyo, Ndugu Rutherford alikuwa ameonywa kwamba kungekuwako jaribio la kukomesha mkutano huo. Kwa hiyo kwanza alizungumzia yale mambo makuu ya hotuba yake, akiwa na kusudi la kuyaongezea maelezo baadaye. Lakini mara tu yale mambo makuu yalipokuwa yameshughulikiwa, ghasia ikazuka. Wafanya matata wapatao 200 kufika 300 walianza kupaaza sauti na kupiga-piga sakafu kwa nyayo zao kama kundi la ng’ombe lililovurugika. Vijana wanaume na wanawake waliruka na kukanyaga viti na kutoa ishara pande zote. Kana kwamba kwa pigo moja kali, wafanya matata hao wakakomesha ghafula hotuba ile.

Ndugu Rutherford alijaribu kuwasihi wasikilizaji watulie na kuonyesha tabia inayofaa, lakini wapi. Kwa mara nyingine tena alijaribu kusema kwa wasikilizaji kupitia mkalimani wake, akisema: “Nataka kuona kutoka wasikilizaji hawa ni wangapi wanataka kusikia mhadhara huu mpaka mwisho.” Walio wengi wa wasikilizaji waliinua mikono yao kwa kukubali. Lakini wale wenye ghasia walionyesha kwa kupaaza sauti kutokubali kwao. Kwa sauti imara sasa Ndugu Rutherford akasema: “Wale wasiotaka kusikia, tafadhali ondokeni jumbani mara moja na kuacha watu ambao wanataka kusikia wasikie.”

Kusikia hivyo, kasirani yote ya wasumbuaji ikaachiliwa. Viongozi wa machafuko hayo wakasukumiza njia yao kupitia vijia. Walipokuwa kama meta 5 kutoka jukwaani, wale wafanya matata wakaanza kuimba ile “Internationale.” Tendo lao lilikuwa lenye kichaa sana hivi kwamba walionekana kuwa walikuwa wamepagawa na mashetani.

Sasa meneja wa jumba lile akawasili na kuamuru kwamba msemaji aondoke jukwaani mara moja. Ndugu Rutherford alitumaini kwamba ghasia hiyo ingelipuka na kwamba polisi wangenyamazisha umati huo ili aweze kuendelea na mhadhara ule. Lakini haikuwa hivyo. Meneja alizima baadhi ya taa, lakini wapinzani wakaziwasha tena. Akifadhaika hata zaidi, meneja pamoja na wawili au watatu wa wasaidizi wake walikimbilia mimbara ya msemaji, wakamkamata Ndugu Rutherford kwa mkono wake, na kumburuta kuelekea nyuma asionekane.

Wale wanaghasia walipofika mbele ya jukwaa, walikuwa wangali wanaimba, na wachache wao walilia kwa sauti kubwa hivi: “Yuko wapi yeye? Yuko wapi yeye? Bendera yetu ni nyekundu!” Kwa kutoweza kumpata Ndugu Rutherford, wale wanaghasia waliweka askari-walinzi kwenye miondokeo. Lakini kwa wazi walishindwa kuona mlango mmoja kwenye upande wa nyuma wa jukwaa. Mlango huu, ambao kwa kawaida hufungwa kwa kufuli na makomeo, ulifunguliwa mara moja. Ndugu Rutherford na Ndugu Arthur Goux, aliyekuwa amekuja pamoja naye kutoka New York, walitimua mbio kuupitia, nao ukafungwa mara hiyo na kutiwa makomeo tena.

Ile karatasi-habari Neues Wiener Journal iliripoti: “Tamasha zenye kukashifu kwenye mhadhara wa Biblia”—“Wakomunisti wakomesha mkutano.”

Emil Wetzel, ambaye wakati huo alikuwa ndiye mwangalizi wa kazi ya Sosaiti katika Austria, baadaye aliandika kwamba wakati wa miezi sita yake ya kwanza katika mgawo huu karibu mikutano yetu yote ya hadhara ilikatizwa. Kwa upande mwingine, walikuwako watu wengi katika hudhurio ambao walikuwa wenye njaa ya ukweli, na mipango ilifanywa ili kuwatunza. Ili kuwezesha utunzaji huo, katika 1923 Sosaiti ilifungua ofisi yayo ya kwanza katika Austria, kwenye 12 Pouthongasse, Vienna.

“Sitakupungukia Kabisa”

Katika 1924, kwa mara ya kwanza, mkutano wa watu wote wa Shirika la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa ulifanyiwa Vienna. Mwaka uliofuata, mkusanyiko ulipofanyiwa Vienna tena, Johannes Schindler kutoka Dresden alikuwa miongoni mwa wajumbe. Hilo likawa jambo lenye kuleta badiliko maishani mwake. Jinsi gani hivyo? Mojapo hotuba ilimalizika kwa mwito huu: “Ni nani angependa kutumikia akiwa misionari msaidizi katika Austria?” (Leo tungerejezea mtu kama huyo kuwa painia.) Miongoni mwa ndugu sita walioitikia papo hapo alikuwa Johannes Schindler.

Kwanza Ndugu Schindler alirudi Dresden kumjulisha mwajiri-kazi wake kwamba angeacha kazi. Wakati ule, alikuwa akifanyia kazi Kiwanda-Ernemann-Zeiss-Ikon chenye kujulikana sana akiwa mtengenezaji vifaa vya optiki (vya kuonea) ambavyo ni sahihi sana. Lakini bila kazi hiyo, Ndugu Schindler angetunzaji mahitaji yake ya kimwili? Angeruhusiwa ajiwekee kwa matumizi ya kibinafsi kiasi fulani cha pesa zilizochangwa kwa ajili ya fasihi. Hata hivyo, katika Austria hakuna fasihi ingeweza kuuzwa nyumba kwa nyumba, na sheria hiyo ilifasiriwa kuwa ilihusu kazi yetu. Jambo pekee la kufanya lilikuwa kumwambia mwenye nyumba kwa fadhili hivi: “Ikiwa unataka kuchanga kitu fulani kuelekea utegemezo wa kazi hii ya kimisionari, uko huru kufanya hivyo.” Uhakika kamili katika Yehova ulitakwa ili mtu akubali mgawo huu chini ya hali hizi. Lakini je! Yehova hakuwa ameahidi watumishi wake hivi: “Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”?—Ebr. 13:5.

Akiwa na umri wa miaka 24, Ndugu Schindler alikuwa tayari amepata ujuzi kwa miaka miwili akiwa mpiga mbiu ya habari njema katika nchi ya kwao, Ujeremani. Sasa, akiwa na reichsmarks 100 mfukoni, alikuja Austria kuanza kazi yake katika na kuzunguka mji wa Wels katika Oktoba 17, 1925.

Yeye alijaribu kuishi kwa uwekevu zaidi iwezekanavyo. Hata hivyo, hata wakati wa mwezi wake wa kwanza alilazimika kugeukia akiba yake ya kifedha kwa ajili ya riziki. Mwishoni mwa miezi mitatu, akiba yake ikaisha. Kutoka wakati huo na kuendelea, imani yake na tegemeo lake katika Yehova lilitahiniwa kweli kweli. Na Yehova alitunza mahitaji yake katika njia Yake mwenyewe.

Kama kielelezo, jioni ya Jumamosi moja baada ya Ndugu Schindler kutumia pesa zake za mwisho kulipia kodi ya kile chumba ambamo yeye na painia mwenzake wangekaa usiku huo, mawazo yake yalisafiri mbele kwenye siku ya kesho. Yeye na mwenzake walimkaribia Baba yao wa kimbingu kwa sala. Jambo la kwanza Jumapili asubuhi, Ndugu Schindler alienda kwenye ofisi ya posta, iliyofunguliwa kwa saa moja tu Jumapili, akaone kama kuna barua yoyote. Alishangaa kama nini alipopewa furushi! Mlikuwa nini ndani? Mlikuwamo vijitabu 500 na barua ya maelezo ikisema kwamba vijitabu hivyo havikuhitaji kulipiwa.

Mahubiri kwenye kanisa la mahali hapo yalikuwa ndipo tu yamemalizika, na wanaume, kama ilivyokuwa desturi yao kufanya, walimiminika makundi makundi kwenye mikahawa ili wafurahie vinywaji vyao vya Jumapili na kucheza karata. Ndugu Schindler alikaribia mtunza-mkahawa, akamtolea kijitabu, na kumuuliza kama angeweza kusema pia na wageni kwenye zile meza. Ombi hilo lilikubaliwa.

Ndugu Schindler alikaribia meza moja na kuweka kijitabu kimoja mbele ya kila mwanamume kuzunguka ile meza, akisema: “Mamilioni wanaoishi sasa hawatakufa kamwe. Unabii huu wa Maandiko Matakatifu utatimizwa karibuni. Sisi hatuuzi vijitabu hivi, lakini ikiwa yeyote anataka kuchanga kitu fulani kwa ajili ya utendaji wetu wa kimisionari, yeye yuko huru kufanya hivyo.” Mara tu mmojapo wanaume alipokuwa ameweka chenji ndogo juu ya meza, wengine walichomoa vibeti vyao na kufanya vivyo hivyo. Hivyo Ndugu Schindler akaenda bila woga meza kwa meza akigawanya vile vijitabu.

Kulikuwa na mikahawa mingine pia katika kijiji hicho. Katika muda wa saa moja na nusu mfuko wake wa fasihi ulikuwa mtupu. Kwa mara nyingine tena Ndugu Schindler na mwenzake wakawa na pesa zilizohitajiwa kununua chakula na kulipia mahali pao pa kulala. Wakiwa na uhakika katika Yehova, wakatazamia siku ya kesho.

Mpaka kifo chake katika Desemba 23, 1986, Johannes Schindler alikuwa angali katika safu za mapainia, wakati huo akiwa katika Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani.

Mazishi Yavuta Fikira

Katika mwaka ule ule ambao Ndugu Schindler alianza kupainia katika Austria, Georg Gertz alitumwa kutoka Ujeremani kuja ofisi ya tawi ya Vienna. Akaja kujulikana sana kote kote katika yale majiji makubwa ya nchi kuwa msemaji mzuri sana.

Ndugu Heide wa Klagenfurt alipokufa, Ndugu Gertz alipewa mgawo wa kutoa hotuba ya mazishi. Ndugu Heide alikuwa amejulikana sana kwa ushiriki wake wenye bidii katika utendaji wa kuhubiri. Kwa msaada wa dairektori, alikuwa amepeleka sampuli za magazeti na trakti mbalimbali kama vile Ecclesiastics Indicted na The Fall of Babylon katika sehemu zote za Karinthia. Baada ya bahasha kupangwa kulingana na mahali ziendako, watoto wake walikuwa wakimsaidia kupeleka upakizi huo kwenye ofisi ya posta ukiwa katika kikapu cha kuwekea nguo za kufuliwa. Wakati kwa wakati Ndugu Heide alipokea barua kutoka kwa watu wenye kupendezwa katika miji na vijiji mbalimbali vya Karinthia, na ikiwa aliweza kuwatembelea kibinafsi, yeye alikuwa akifanya hivyo.

Hivyo Ndugu Heide alipokufa, halikuwa jambo la kushangaza kwamba wengi walionyesha upendezi katika mipango ya mazishi yake. Mazishi humaanisha mengi kwa watu wa mashambani wa Austria. Kwa upande mmoja, wanaweza kuyasifu sana, lakini kwa upande mwingine wanaweza kuonyesha kwa njia imara sana kwamba hayakuwapendeza. Basi, mahubiri haya ya mazishi, ya kwanza kwa yeyote wa Mashahidi wa Yehova katika Austria, yalihudhuriwa na watu wapatao 2,000. Na kwa kuwa Mwaustria hupenda kuongea juu ya mazishi, watu walikuwa wangali wakiongea juu ya mazishi haya hata baada ya miaka kumi.

Mianzo Midogo, Jitihada Yenye Kuendelea

Leo kuna makundi 16 katika na kuzunguka Linz, katika upande wa juu wa Austria. Lakini ukweli wa Biblia ulitia mizizi hapa polepole. Kidini, hii ilikuwa ngome ya Kanisa Katoliki, na haikuwa rahisi kupiga mbiu ya ujumbe wa Ufalme katika eneo hili.

Simon Riedler, yule mkulima mnyenyekevu, aliongea na wengine kwa idili katika eneo hili juu ya kweli za Biblia zenye thamani kubwa alizokuwa amejifunza. Karibu 1930, Ndugu Nasl kutoka Munich, Ujeremani, akaja kumsaidia, nao walipata watu wachache wenye kupendezwa. Ndugu Riedler alitolea kikundi hicho hotuba au akakisomea vichapo vya Sosaiti. Kwa kawaida watu kutoka 30 kufika 35 walikusanyika kwa ajili ya mikutano hii. Hata hivyo, kwa sababu ya mbano, kupendezwa kulidhoofika, na ripoti za baadaye hata kufika 1940 huonyesha kwamba kulikuwako dada mmoja tu mshikamanifu katika Linz.

Katika magharibi, karibu na mpaka wa Liechtenstein katika jiji la Feldkirch, ofisa wa forodha jina lake Wilhelm Coreth alikuwa akitolea wafanya kazi wenzake ushuhuda mapema kama 1922. Agathe Thaler na mama yake, waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Lauterach wakati huo, walisikia habari njema. Mazungumzo yakapangwa kwenye makao ya wazazi wa Agathe, akiwapo padri wa mahali hapo. Kati ya watu 20 na 25 walikuwapo. Padri yule hakuweza kukanusha kutokana na Biblia zozote za zile hoja zilizotolewa. Tokeo likawa nini? Jamaa yote ikakubali ukweli. Katika 1925 mji wa Dornbirn ukawa kitovu cha mikutano, na akina ndugu kutoka Uswisi iliyo karibu wakawa wakija kutoa hotuba. Johann Brotzge, ambaye alikuwa amesikia ukweli hapo kwanza mapema kama 1917, alikuwa amefanya maendeleo pia kufikia hatua ya kuweza kutoa hotuba.

Maendeleo yaliyokuwa yakifanywa kote kote nchini yalionyeshwa katika hudhurio kwenye Ukumbusho. Katika 1926 Vienna iliripoti 312, Graz 43, Klagenfurt 26, na mahali pengine mbalimbali jumla ya 52.

Katika mwaka uo huo, uangalizi wa kazi ya Ufalme katika Austria ulihamishwa kupelekwa ofisi ya tawi ya Ujeremani. Ndugu mwenye uwezo alitumwa Austria kuandalia usimamizi wa huko uliohitajiwa.

Kusonga Mbele Usoni pa Mbano

Kazi ya kuhubiri iliendeshwa chini ya hali ngumu katika siku hizo. Kila mmoja aliyeshiriki habari njema za Ufalme wa Mungu pamoja na wengine, hasa katika maeneo ya mashambani, alifahamiana upesi na jamii ya mapolisi.

Siku moja kikundi cha akina ndugu kilikuwa kimekodisha basi ili kuzuru vijiji fulani vya Waldviertel, eneo la mashambani upande wa kaskazini wa Vienna, wakafanye kazi ya kuhubiri huko. Tayari walitarajiwa walipowasili. Kwenye mwingilio wa kijiji, walijikuta wenyewe wakikabiliana na umati wenye uhasama wa wanakijiji wakiwa wamechochewa na padri mwenyeji. Miongoni mwa umati huo walisimama wanaume wakiwa na kofia za chuma na bunduki; walikuwa wa kikosi kiitwacho eti Heimwehr, askari wa mgambo, kikiungwa mkono na baadhi ya mapolisi wa mashambani. Mara tu akina ndugu walipokanyaga chini kutoka ndani ya basi, walishambuliwa na kunyang’anywa ugavi wao wote wa fasihi.

Ni wazi kwamba, wakati wa kufanya kazi katika maeneo ya mashambani baada ya tukio hili, akina ndugu walishuka basi nje ya vijiji na kuingia vijijini kwa njia za vizingo. Hata hivyo, mara hiyo maadui wa ukweli walipatanisha njia zao na zile njia mpya za akina ndugu. Baadhi ya maeneo yalikuwa mikononi mwa makasisi kwa njia imara sana, nayo jamii ya mapolisi ilikuwa na nia sana ya kushirikiana na makasisi katika kuchukua hatua dhidi ya akina ndugu.

Uhasama ambao akina ndugu walilazimika kukabili uligusa kila upande wa maisha yao na haukumalizwa hata na kifo chenyewe. Bw. na Bi. Geisberger, ambao waliishi karibu na mji mdogo wa Schärding, walikubali ukweli na wakajiondoa kutoka Kanisa Katoliki katika 1923. Kwa sababu ya hilo, muda mfupi baada ya hapo Dada Geisberger akapoteza kazi yake akiwa mwalimu wa ushonaji. Kisha, wakati mume wake alipokufa, padri wa kijiji alijaribu kuzuia mazishi yoyote kwa ajili ya Ndugu Geisberger kwenye makaburi ya wenyeji. Bila shaka, kisheria, hakuna mtu yeyote ambaye angekatazwa maziko. Kwa hiyo akina ndugu walimpelekea kamishina wa wilaya habari hiyo. Ni mipango gani ingeweza kufanywa kuzika mwanamume huyu aliyeamini na aliyejaribu kuishi kupatana na Biblia? Maziko yangekuwa katika ile sehemu ya makaburi iliyotengwa kuzikia watu waliojiua wenyewe. Angalau Ndugu Wetzel wa Vienna aliruhusiwa kutoa hotuba ya mazishi.

Wanyanyaswa kwa Kuwa Wakristo

Maandiko hayafichi uhakika wa kwamba katika ulimwengu huu magumu yanakuja kwa sababu ya kuwa Mkristo. Yesu Kristo aliambia wafuasi wake hivi: “Zingatieni neno nililosema kwenu, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana-mkubwa wake. Ikiwa wameninyanyasa mimi, watawanyanyasa nyinyi pia . . . Lakini watafanya mambo yote hayo dhidi yenu kwa sababu ya jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma mimi.” (Yoh. 15:20, 21, NW) Hilo lilithibitika kuwa ono la wale waliojaribu kutembea katika hatua za nyayo za Yesu Kristo katika Austria wakati wa kipindi hiki. Nyakati nyingine, kama vile Yesu alivyokuwa ameonya, upinzani ulikuja kutoka kwa washiriki wa karibu wa jamaa. (Mt. 10:32-39) Lakini hiyo haikuwavunja moyo akina ndugu katika Austria wasichukue msimamo wao upande wa Ufalme wa Mungu.

Beatrice Lojda alikuwa mwanamke msemaji wa harakati ya Sosholisti naye alikuwa amefanya kampeni ili achaguliwe kwenye Nationalrat (Baraza la Kitaifa, Bunge la Daraja la Chini). Mmoja wa wasichana marafiki wake—jina lake lilikuwa Bretschneider—ambaye alimjua kutokana na utendaji wake wa kisiasa, alikuwa amekuwa shahidi wa Yehova na kama vile ingetazamiwa alisema naye juu ya Ufalme wa Mungu. Beatrice alialikwa kwenye Hoteli Continental katika Vienna akasikie mhadhara. Hii ilikuwa hoteli ile ile ambapo Ndugu Russell alikuwa amejaribu bila fanikio kutoa hotuba huko nyuma katika 1911. Beatrice hakuamini katika Mungu na mwanzoni yeye alipuuza jambo lote hilo, akisema hivi: “Mungu angelazimika kujijulisha kwangu mimi kwanza!” Lakini alitaka kupendeza rafiki yake na kwa hiyo akahudhuria hotuba hiyo. Zijapokuwa hisia zake, hata wakati wa hotuba yeye hakuweza kujizuia kumwambia Dada Bretschneider mara kadhaa: “Huu ndio ukweli! Huu ndio ukweli!”

Haikumchukua Beatrice muda mrefu kujiondoa kutoka maisha ya kisiasa, kupatana na maneno ya Yesu kwa wanafunzi wake: “Nyinyi si sehemu ya ulimwengu.” (Yoh. 15:19, NW) Mara hiyo, magumu yakaanza. Mume wake akatisha kumtaliki ‘asiporudia fahamu zake,’ kama vile mumeye alivyolisema jambo hilo. Lakini yeye alisimama imara katika imani na akaendelea kufanya hivyo mpaka kifo chake.

Franz Monfreda wa Salzburg alikuwa amekuwa Mkatoliki mwenye bidii, lakini ukweli ulifikia moyo wake. Baada ya kuliacha Kanisa Katoliki katika Machi 12, 1927, aliweka maisha yake wakfu kwa Yehova Mungu. Jamaa yake haikufurahishwa na tendo hilo hata kidogo na hivyo ikarundika mashutumu na uhasama juu yake. Ulizidi sana hivi kwamba alipoteza nyumba pamoja na biashara yake. Imani yake ilitiwa katika mitihani migumu, kwa kuwa ilimchukua wakati fulani kupata kazi nyingine. Lakini yeye alikaa akiwa mwaminifu kwa Yehova. Yeye ana jambo gani la kusema juu ya siku hizo? “Leo mimi nafurahi kwamba nilishinda kipindi hicho na nikashikamana na ukweli. Mkono wa Yehova haukuthibitika kamwe kuwa mfupi mno.”—Linganisha Isaya 59:1.

Kulikuwako Baiskeli Moja Tu

Akina ndugu katika eneo la Riedlingsdorf, mkoa wa Burgenland, walionyesha bidii isiyo ya kawaida katika kazi ya Bwana. Eneo lao lilitapakaa sana, na ilikuwa vigumu sana kupata usafiri. Kujipatia pikipiki, achia mbali motokaa, lilikuwa jambo lisilowezekana kwao. Wengi wao hata hawakuwa na baiskeli. Hivyo baadhi ya akina ndugu walitumia njia inayofuata kwa ajili ya utumishi wa shambani:

Ndugu mmoja angeanza kwa kutembea, akizuru nyumba ili ahubiri huku akiendelea na safari yake. Ndugu wa pili angetangulia akiwa juu ya baiskeli yake kwenda mahali palipotangulia kuchaguliwa na kuacha baiskeli hapo. Ndipo yeye angeendeleza utendaji wake akitembea kwa miguu. Yule ndugu wa kwanza, awasilipo mahali pale ilipo baiskeli, angeiendesha kwenda kwenye mahali panapofuata walipotangulia kukubaliana. Kama baiskeli hii ingalikuwa na kipima-mwendo, bila shaka ingalikuwa na rekodi kubwa ya kilometa za kazi ya kuhubiri Ufalme!

Kwa kuwa akina ndugu walikuwa na Jumapili tu kwa ajili ya utumishi wa shambani, walitumia wakati huo kikamili. Nyakati fulani waliondoka nyumbani mwao saa 9:00 asubuhi na kurudi jioni-jioni. Jitihada ya moyo wote ilionyeshwa katika huduma yao.

Kupigania Haki za Kisheria

Kadiri kazi ya kuhubiri ilivyoenea zaidi, halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa akina ndugu kuitwa waonekane mbele ya wenye mamlaka wenyeji kwa sababu ya utendaji wao wa kuhubiri. Kadiri walivyoweza kufanya hivyo, walijitetea wenyewe. Katika visa fulani walipewa msaada wa kisheria. Lakini hatua za kisheria hazikuwapendelea sikuzote.

Hata hivyo, lilithibitika kuwa jambo gumu zaidi kuandikisha tawi la Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi la nchi hiyo kuliko kuzuia vifungo. Utambulisho wa kisheria likiwa tengenezo la kidini lilikuwa jambo lisilowezekana bado. Akina ndugu walijaribu kujiandikisha angalau kama shirika, lakini wenye mamlaka wa umma walipinga, wakitoa hoja hivi: ‘Kusudio lenu ni kufanyiza tengenezo la kidini, na tengenezo la aina hiyo haliwezi kufanyizwa chini ya sheria ya Austria.’

Akina ndugu walikata rufani kwa Mahakama ya Kikatiba, wakilalamika kwamba walikuwa wakinyimwa haki yao ya kisheria ya kufanyiza shirika. Tendo-mwitikio la mara moja la washiriki wa Mahakama ya Kikatiba ya Austria lilikuwa kukataliwa kwa rufani hiyo katika Desemba 7, 1929. Halafu, akina ndugu walijaribu kuandikisha shirika kwa ajili ya kugawanya Biblia na fasihi ya Biblia, bila uhusisho wowote katika kazi za kidini. Ombi hilo halikukataliwa. Kwa hiyo, katika Mei 24, 1930, shirika la nchi hiyo lilifanyizwa litumikie likiwa chombo cha kisheria kwa ajili ya akina ndugu.

Utambulisho wa kisheria wa Wachtturm-Gesellschaft haukumaliza kwa vyovyote magumu ambayo akina ndugu walishindana nayo. Lakini watumishi wa Yehova walishikamana na daraka lao la Kimaandiko. Wao walitambua kwamba ushuhuda lazima utolewe kwa maofisa pia.—Marko 13:11.

Makundi Mapya, Hudhurio Lenye Kukua

Ili wasianzishe upinzani mwingi, akina ndugu walikuwa wameamua kujizuia kufanya makusanyiko makubwa zaidi. Mchezo wa Photo-Drama of Creation tu, ambao ulionwa katika Vienna kwa mara ya kwanza katika 1922, ndio ungeonyeshwa katika ile miji midogo zaidi ya kimkoa pia.

Ijapokuwa hivyo, katika maeneo fulani hudhurio katika mikutano ya kundi lilikuwa kubwa kwa kadiri fulani. Ndivyo ilivyokuwa katika mji wa Leoben, ambako Eduard Payer alikuwa katika utumishi wa wakati wote. Kabla ya kuwasili kwake, hakuna mtu aliyekuwa amesikia juu ya Wanafunzi wa Biblia. Lakini yeye alihubiri kwa bidii nyingi, na upesi wapatao 200 wakawa wakihudhuria mikutano. Kufikia 1932 alikuwa akitumikia Graz, mji mkuu wa mkoa wa Styria. Kwa mara nyingine tena, mamia kadhaa walihudhuria mikutano huko. Miongoni mwa wale waliohudhuria alikuwa mshiriki wa hapo kwanza wa French Foreign Legion, Leopold Pitteroff, ambaye baadaye alitupwa ndani ya kambi ya mateso ambamo alibaki akiwa mwaminifu. Hesabu ya vikundi vya funzo la Biblia vilivyopangwa kitengenezo (au madarasa, kama yalivyoitwa wakati huo) katika Austria yalikuwa tayari yamekua kufika 30.

Upinzani Waongezeka

Badiliko lililotukia baadaye katika mandhari ya kisiasa lilikaribishwa sana na makasisi, waliokuwa ndio wapinzani wetu wakubwa. Dakt. Engelbert Dollfuss, Mkristo-Msosholisti, alichukua cheo akiwa chansela wa muungano katika Mei 20, 1932, naye akapokea simu ya barua ya pongezi kutoka kwa Kardinali Pacelli, waziri wa nchi wa papa. Mapunguzo ya uhuru wa kiraia yenye kuonekana wazi yalitukia wakati wa kipindi cha utawala wa Dakt. Dollfuss. Akijifaidi kwa werevu na hali ya dharura katika 1933, alivunja Bunge. Ndipo, akishika kamba zote za kisiasa mikononi mwake, alianzisha kile alichoita “Kiolezo cha Serikali ya Kikatoliki ya Kwanza Katika Ulaya.” Jamii ya makasisi ilimweleza Dollfuss kuwa mwanaserikali Mkatoliki halisi.

Chini ya hali hizi, je! lingekuwa jambo la kushangaza ikiwa majaribio ya kukataza mikutano yetu ya Kikristo yangefanywa? Katazo kama hilo lilifikilizwa upesi katika Graz, ambako mamia ya watu walikuwa wakihudhuria mikutano yetu. Akina ndugu hawakutishika. Walikata rufani mara hiyo, ambayo ilikuwa haina budi kuruhusiwa kwa sababu akina ndugu huwakuwa wamevunja sheria. Hata hivyo, wenye mamlaka ya umma waliondoa ruhusa ya ukazi wa baadhi ya mapainia na hivyo kuwalazimisha waondoke mjini. Karibu kila juma yalikuwako mashtaka ya uwongo dhidi ya akina ndugu. Jarida la Kikatoliki liliomba kwamba serikali ikomeshe kazi yetu ya Kikristo, ikifunua wazi ni nani aliyekuwa akisababisha vitendo hivyo.

Katika wakati ufaao kabisa tengenezo la Yehova liliandaa msaada wenye kujenga. Ingawa Ndugu Rutherford hakuweza kuja katika 1933 kama alivyokuwa amepanga, alituma N. H. Knorr na M. C. Harbeck, ambao walikutana na akina ndugu katika Etablissement ya Wimberger katika Vienna. Mkutano huo ulisaidia sana kuimarisha akina ndugu.

Kukaguliwa na Kunyang’anywa Fasihi

Kupatana na unabii wa Biblia kwamba mahali pa utawala wa kibinadamu pangechukuliwa na Ufalme wa Mungu wa kimbingu, vichapo vyetu vilikazia kabisa yale matokeo yenye kuhuzunisha ya utawala wa wanadamu. (Dan. 2:44; 7:13, 14, 27) Wenye mamlaka watawalao walichukizwa na taarifa kama hizo walipohisi kwamba hizo ziliwafunua kwa njia mbaya. Kama tokeo, kulikuwako mfululizo wa unyang’anyi wa fasihi yetu katika miaka ya mapema ya 1930.

Wakati wa 1933 na 1934 akina ndugu waliitwa mbele ya wenye mamlaka ya umma karibu kila juma wasikilize namna zote za malalamiko. Mara nyingi wenye mamlaka walidai kwamba mafungu fulani katika vichapo yafanywe yasiyosomeka. Ili kuhakikisha kwamba mafungu yote yaliyohusika yangefutwa, polisi aliwekwa pale pale penye ofisi ya Sosaiti. Siku fulani fulani kazi iliendelea kwa muda mrefu, hata mpaka usiku wa manane. Na kwa kuwa jicho la sheria huchoka nyakati nyingine mafungu fulani katika vichapo vile yalibaki yakiwa yanaweza kusomeka hata hivyo.

Msukosuko wa Kisiasa Waleta Vizuizi

Tofauti kati ya vile vikundi mbalimbali vya kisiasa iliongezeka kwa ghafula sana. Kile chama cha Social Democratic Schutzbund (majeshi yenye silaha ya Chama cha Sosholisti) kiliingia katika ukinzani. Upinzani wa jamii ya wafanya kazi ulipondwa-pondwa bila huruma katika Februari 1934. Chama cha Demokrasi ya Sosholisti kilipigwa marufuku. Vizuizi zaidi vya uhuru wa kibinafsi vikafuata.

Kana kwamba kuthibitisha kwamba enzi mpya ilikuwa imeanza, Austria ilipata katiba mpya katika Mei 1934. Maneno ya utangulizi yayo yalisikika kama imani ya kidini: “Katika jina la Mungu, Mweza Yote, ambaye kwake sheria yote hutoka, watu wa Austria wapokea hapa katiba hii kwa ajili ya Serikali yao ya kudumu ya Kikristo ya Muungano wa Ujeremani.” Lakini katika Ujeremani iliyo jirani, Hitla, Mkatoliki mwingine lakini ambaye alikubali nadharia tofauti ya kisiasa, tayari alikuwa ameimarika katika mamlaka. Na katika Julai muungaji mkono wa Chama cha Kitaifa cha Sosholisti cha Hitla alimuua kwa hila Dakt. Dollfuss, chansela wa Austria.

Ile miezi iliyofuata, chini ya serikali iliyoongozwa na Chansela Kurt Schuschnigg, haikuleta kitulizo kwa wale waliotafuta kikweli kutumikia “Mungu, Mweza Yote.” Wangali walinyang’anywa fasihi ya Biblia, na waliendelea kuburutwa mbele ya mahakama. Katika visa vingi mikutano ya Biblia ya watu wote ilikatazwa pia.

Shirika la Nchini Lavunjwa na Wenye Mamlaka

Hatimaye, kwa amri iliyotolewa katika Septemba 10, 1934, kamishina wa Vienna wa usalama wa muungano, akavunja Wachtturm-Gesellschaft, shirika halali lililotumiwa na Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, kufuatia rufani iliyokatwa na akina ndugu, amri hiyo ilifutwa na Ofisi ya Muungano ya Chansela ikitumia cheo chayo ikiwa baraza la utekelezaji kwa ajili ya usalama wa umma.

Lakini wenye mamlaka ambao hasa walikuwa na hamu nyingi ya kukomesha kazi yetu hawakupumzika. Katika Juni 17 na Julai 17, 1935, iliamriwa tena, wakati huu na msimamizi wa usalama wa muungano, kwamba “Wachtturm-Gesellschaft, Tawi la Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi Biblia na Trakti, Brooklyn, N.Y.,” ingevunjwa. Akina ndugu walijaribu tena kukata rufani juu ya amri hii lakini, wakati huu, isiwezekane.

Kuweka Ufalme Kwanza Vijapokuwa Vizuizi

Akina ndugu waliendelea kufanya kazi mlango kwa mlango, ingawa sasa kwa tahadhari. Ujapokuwa uangalifu wao, walikamatwa mara nyingi na kuhukumiwa ama kwenda jela au kulipa faini. Hata ingawa jela ingemaanisha majuma kadhaa ya kizuizi, wao walipendelea jela kuliko kulipa faini, kwa kuwa walifikiria fursa za kutoa ushuhuda humo.

Katika siku hizo za msukosuko na mashaka ya kiuchumi, Leopold Engleitner aliingia utumishi wa wakati wote. Katika Januari 1934 alihamia lile eneo alilogawiwa katika Styria ya Juu, ambako kufikia wakati huo ni ushuhuda mdogo sana ulikuwa umetolewa.

Usosholisti wa kitaifa tayari ulikuwa ukitumia uvutano wenye nguvu huko. Kama tokeo, katika mahali fulani fulani sheria ya kijeshi ilikuwa imetangazwa. Ndivyo ilivyokuwa katika Schladming, ambayo ilikuwa ikikaliwa na jeshi la mgambo kama tokeo la misukosuko ya Nazi. Kwa sababu ya hatari ya hali, Ndugu Engleitner aliweka kiasi kidogo tu cha fasihi katika mifuko ya jaketi yake ili asivute fikira. Akifanyia kazi kwanza viunga vilivyokuwa nje kabisa ya mji, aliwatolea fasihi watu wale tu alihisi kwamba angeweza kuwatumaini.

Siku moja yeye alikamatwa na kwa sababu ya hali ya kisiasa iliyokuwako, kwenye ofisi ya polisi aliulizwa kama alikuwa na silaha zozote. Ndugu yetu alijibu ndiyo, akatia mkono wake katika mfuko na kuchomoa Biblia akaiweka juu ya meza mbele yao. (Efe. 6:17) Wale maofisa walipokwisha maliza kicheko chao, wakamwacha aende zake.

Hata hivyo, makasisi waliudhikia mtumishi huyu wa Yehova. Wakati wowote alipoanza kazi yake ya kuhubiri katika mojapo vile vijiji vikubwa zaidi, makasisi walihakikisha kwamba wakazi wote wamearifiwa, kutia na jamii ya mapolisi. Ndugu Engleitner alitiwa mbaroni wakati baada ya wakati. Hukumu za jela zikafuata upesi. Mwanzoni ilikuwa kwa muda wa saa 48 kwa wakati mmoja, lakini hukumu zile zilizidi kuwa ndefu. Mwishowe, alilazimika kuhamishia utendaji wake mahali pengine.

Katika eneo lake jipya, katika bonde lililokuwa mbali kwenye jimbo la milima-milima, alikuwa mwangalifu asikose yoyote ya nyumba zile. Hata wakati hakuwamo mtu nyumbani, aliwaachia kitu fulani wasome.

Katika kisa kimoja, mfanya kazi ya shamba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuja nyumbani. Aliiona trakti, akaisoma kwa uangalifu, akaagiza fasihi zaidi, na akawa ndugu mwaminifu. Ilikuwa miaka 32 baadaye kwamba akakutana na Ndugu Engleitner kwa njia isiyotazamiwa kwenye mkusanyiko wa wilaya.

Kwa Nini Walikuwapo?

Kituko kimoja katika kijiji cha Riedlingsdorf hutoa picha iliyo wazi ya mkazo uliokuwapo. Mazishi yalipangiwa katika kijiji hicho, na Ndugu Ronovsky wa Vienna angetoa hotuba. Wakati ule mazishi yalitoa fursa pekee ya kutoa ushuhuda kwa kikundi kikubwa. Hata hivyo, ndugu yetu alipokaribia kaburi, alishangazwa na kikao kisicho cha kawaida. Alielekewa na wanaume 50 wa jamii ya mapolisi na jeshi la mgambo ambao, wakiwa na kofia zao za chuma vichwani na bunduki makwapani, walionekana wakiwa tayari sana kuchukua hatua. Jumla ya hesabu ya waliokuwapo ilikuwa yapata 100, kutia padri wa mahali hapo. Ndugu yetu alijaribu kadiri alivyoweza kutoa ushuhuda juu ya Yehova Mungu, Mwana wake, na tumaini la ufufuo. Lakini kwa nini wanaume hao wenye silaha walikuwapo?

Ilikuwa baadaye kwamba Ndugu Ronovsky akajifunza sababu ya kutano hilo lenye kushtua. Akina ndugu wa kutoka kijiji hicho walimwambia baadaye kwamba wale wanaume wa jamii ya mapolisi na jeshi la mgambo walishangazwa na maelezo yake ya kutoka Biblia kwa sababu padri wa mahali hapo alikuwa ameeneza uvumi kwamba Mashahidi walikuwa wakomunisti waliokusudia kupindua serikali.

Vizuizi Juu ya Mikutano

Kutoka 1935 na kuendelea, mikutano haingeweza kufanywa tena hadharani. Mafunzo yote ya Mnara wa Mlinzi yalikuwa yamekatazwa, hata katika nyumba za faragha. Nyakati nyingine, wenye mamlaka walibisha kwamba usalama wa umma ulihatarishwa, na nyakati nyingine, walisema kwamba watu Wakatoliki waliudhiwa na mikutano kama hiyo. Lakini Neno la Mungu liliamuru: ‘Msiache kukusanyika pamoja.’—Ebr. 10:25.

Akina ndugu waliendelea kukutana, lakini katika nyumba za faragha tu na katika vikundi vidogo vya watu wanane au kumi. Mahali pa mkutano palibadilishwa daima. Hivyo hawakuvuta uangalifu isivyostahili. Kwenye mikutano yao walizungumzia Maandiko kwa msaada wa Mnara wa Mlinzi na vichapo vingine, kama vile The Harp of God, Creation, Prophecy, Government, na Light. Pia walisikiliza hotuba za Biblia zikiwa katika mirekodio, wakati hizo zilipopatikana. Ijapokuwa marufuku ya serikali, pole kwa pole watu wa Mungu walizidi kuongezeka katika hesabu.

Hata wakati jitihada ya bidii ilipotakwa, akina ndugu walishirikiana kwa ukawaida na waamini wenzao. Kwa kuwa Vienna haliko mbali na jiji Bratislava la Chekoslovakia, au Pressburg, akina ndugu walikodi basi kila mwisho-juma wa pili kwa kusudi hasa la kusafiri kutoka Vienna kwenda Bratislava kufanya funzo la Mnara wa Mlinzi. Katika Juni 9, 1935, akina ndugu Waaustria walihudhuria mkusanyiko wa wilaya katika Maribor, Yugoslavia, na katika 1936 walikwenda kwenye mkusanyiko katika Lucerne, Uswisi. Hata hivyo, katika Austria yenyewe, mkazo ulizidi kupanda.

Kujitayarishia Mnyanyaso Uliotazamiwa

Ripoti kutoka Ujeremani zilitoa miono midogo juu ya mambo ambayo ndugu zetu walikuwa wakivumilia huko, na hilo lilifanya wahubiri katika Austria watetemeke kwa hofu. Walisali kwa Yehova kwa ajili ya imara iliyohitajiwa kuvumilia maumivu na mateso kama hayo, ikihitajiwa kabisa, na kukaa wakiwa waaminifu. Lakini mambo yalikuwa bado hayajafikia hatua hiyo.

Katika kiangazi cha 1937, wote ambao wangeweza kufanya hivyo walichagizwa wahudhurie mkusanyiko ambao ungefanyiwa Prague, Chekoslovakia. Ili kuwapa nafasi wale waliojiandikisha kwa ajili ya safari hiyo ya kutoka Vienna kwenda Prague, mabasi matatu yalihitajiwa. Ilikuwa safari ya siku nzima. Hata hivyo, si wote wangeweza kusafiri kwa basi. Ndugu Engleitner na wengine watano kutoka Bad Ischl na sehemu zilizo karibu walisafiri kilometa zaidi ya 360 kwa baiskeli.

Wale wote waliohudhuria mkusanyiko huo walikuwa na hisia kwamba ilielekea sana kwamba huo ungekuwa ndio mkusanyiko mkubwa wa mwisho ambao wangefurahia wakiwa huru. Vichwa vya mazungumzo vya hotuba vilifaa sana kusudi la kuwatayarisha akina ndugu kwa ajili ya nyakati za hatari zilizokuwa mbele. Wakati wa mkusanyiko huu ilitajwa kwa kurudiwa-rudiwa kwamba akina ndugu walikuwa wakikaribia kwa haraka sana wakati wa jaribu kali. Walitiwa imara kwa maagizo ya pekee kuhusu mwenendo chini ya mnyanyaso. Ili kuepuka kuhatirisha wengine ikitukia kwamba nyumba zinapekuliwa-pekuliwa, walitahadharishwa pia dhidi ya kuweka orodha zozote zenye majina ya Mashahidi wenzao. (Mt. 10:16) Uvumilivu thabiti wa akina ndugu katika Ujeremani ulikaziwa kuwa kielelezo chema cha kufuata. Wakusanyikaji walihimizwa wavumilie kwa uaminifu na kwa utii, wakiwa na tegemeo kamili katika Yehova, hata itukie nini.—Mit. 3:5, 6.

Na hivyo kusanyiko likaisha. Kwa mioyo mizito wakaimba, “Mungu awe pamoja nanyi mpaka tukutane tena,” kisha wakasema kwaheri ya kuonana kwa ndugu zao na kwa jiji lenye ukaribishaji-wageni la Prague. Machozi mengi yalitiririka katika kuachana kwa kuwa sasa ndugu zetu waling’amua ni kwa nini walikuwa wamehimizwa wahudhurie mkusanyiko huu.

Vikosi vya Ujeremani Vyavuka Mpaka

Kila kitu kilionyesha kwamba vikosi vya Ujeremani vingetarajiwa vipige miguu kuingia Austria karibuni. Baadhi ya watu walitazamia mvuvumuko wa kiuchumi mara tu Austria ilipotwaliwa na Ujeremani. Lakini wale ambao hawakukubaliana na nadharia ya Hitla walikuwa na wasiwasi juu ya kulipizwa kisasi. Kwa habari ya akina ndugu, wao walijua kwamba mitihani isiyoepukika ya ushikamanifu wao kwa Yehova ingekuja. Kama ilivyohofiwa, vikosi vya Hitla vilianzishwa mwendo navyo vilivuka mpaka wa Austria, vikafanya hivyo katika Machi 12, 1938.

Juma moja hivi kabla ya hilo, kwa kutazamia jambo lililokaribia kutukia, mali ya Sosaiti katika Vienna iliuzwa, na ndugu mwenye daraka, pamoja na mke wake, wakaondoka Austria kwenda Uswisi. Wakati akina ndugu katika Austria walipojua hilo, wao walishangaa, wakiuliza hivi: ‘Yote haya yanamaanisha nini?’ ‘Kazi itaendeleaje?’ ‘Sisi tutapata chakula cha kiroho kutoka wapi?’

Ndugu August Kraft (anajulikana pia kama Kraftzig), ambaye alikuwa amefanya kazi katika ofisi ya Sosaiti, alipewa pia chaguo la kuondoka Austria. Lakini yeye alijulisha wazi hivi: “Mimi nataka kukaa pamoja na kondoo.” Kwa upendo aliwatia moyo, akawaimarisha, na kuwatunza. Lo, jinsi wao walivyoshukuru kwa ajili ya ndugu na mchungaji huyu mwenye kumhofu Mungu ambaye kwa wororo aliwatunza hata ingawa jina lake tayari lilikuwa katika orodha ya wale waliokuwa wakiwindwa na Gestapo Wajeremani! Yeye alizidi kuhama-hama, akizuru akina ndugu katika Innsbruck, Klagenfurt, na sehemu nyingine za nchi. Kwa tahadhari sana alizuru makao ya akina ndugu jioni-jioni na kuondoka tena mapema asubuhi iliyofuata.

Madai ya Mamlaka Mpya Zenye Kutawala

Aprili 10 ilikuwa siku iliyojaa mkazo. Watu wa Austria wangepiga kura kama wangeafikiana na kutwaliwa kwa Austria na Ujeremani. Hata hivyo, hilo lilikuwa tayari limeamuliwa muda mrefu uliopita. Hakuna mtu angekosa kuona sihi zenye kukaza umma zilizoonekana kwenye karatasi za matangazo kote kote: “NDIYO yenu kwa ajili ya Hitla.”

Akina ndugu walifanya nini? Hata kama ndugu zetu wangetenda namna gani, walijua kwamba halmashauri za uchaguzi zilikuwa na njia za kupata kujua uamuzi wa kila mmoja wa wapiga kura ulikuwa umekuwa nini. Katika siku ya kupiga kura Johann Viereckl wa Vienna alienda msituni mapema asubuhi naye hakurudi mpaka usiku sana chini ya kisetiri cha giza. Mara tano wakuu wa halmashauri ya upigaji-kura walikuwa wamekuwa mlangoni pake, kulingana na yale ambayo Johann aliambiwa baadaye na majirani. Pasipo maafikiano yaliyotangulia kufanywa, ndugu wengine walifanya sawasawa na alivyofanya Johann ili kudumisha kutokuwamo kwao. Jambo moja ambalo sasa lilikuwa wazi kwa akina ndugu ni: Macho ya watawala wapya yalikuwa juu yao.

Ili kuonyesha ushirikiano wao pamoja na ule utawala mpya, watu walitakwa wapambe madirisha yao kwa bendera iliyokuwa na swastika. Katika mji mdogo wa Knittelfeld, Dada Altenbuchner aliishi katika jengo lenye vyumba vingi lililoelekea barabara ya mji. Wakati baada ya wakati, wawakilishi wenyeji wa utawala ule walimfikia, wakidai kwamba bendera ya swastika ionyeshwe kwenye madirisha yake. Walimjulisha kwamba ikiwa yeye hakuwa na nia ya kufanya hivyo, angevuna wonyesho wa uhasama wa majirani wake wote. Yaonekana wazi kwamba alikabiliana na uadui wenye umoja. Kwa sababu za kidhamiri yeye aliamua kwamba hangetundika bendera hiyo. Matokeo yakawaje? Alipewa amri ya kutoka mahakamani iliyomwamuru ahame nyumba yake iliyoelekea barabara ya mji na kwenda kwa nyingine aliyogawiwa iliyokuwa upande wa nyuma wa nyumba hiyo, ambapo haikutakwa kwamba bendera zionyeshwe—utatuzi ambao hakutarajia kamwe.

Uandalizi wa Chakula Kilichohitajiwa

Kwa muda fulani baada ya Hitla kutwaa Austria, akina ndugu walifaulu kufanya mikutano midogo katika Vienna—lakini kwa uangalifu. Ndugu mmoja alisimamia utunzaji wa kiroho wa vikundi vya funzo katika kila wilaya ya Vienna.

Mwanzoni Ndugu Kraft alienda Vorarlberg kuleta nakala za Mnara wa Mlinzi ambazo ndugu Waswissi waliingiza kisirisiri kuvuka mpaka. Akiwa njiani kurudi Vienna, alitua katika Innsbruck ili kuonana na Ndugu Defner na Setz, ambao walichukua nakala kwa ajili ya eneo la Tiroli. Ndugu Setz aliweka vitu hivi vyenye thamani kubwa chini ya kuni zilizokuwa zimerundikwa nyuma ya nyumba yake. Yote hayo yanasikika kuwa rahisi sana. Lakini usisahau kwamba Gestapo na wapasha-habari wao walikuwa kila mahali.

Dada Wajasiri Wajaza Uhitaji Muhimu

Bila kukawia, Ndugu Kraft alifanya mipango ili ugavi wa chakula cha kiroho kwa ajili ya akina ndugu uendelee baada ya yeye kutiwa mbaroni. Kwa nderemo dada wajasiri walijifanya wapatikane kwa ajili ya kazi ya kulisha kiroho. Therese Schreiber wa Vienna alikuwa mmoja wao. Ndugu Kraft alimfundisha jinsi ya kurudufisha nakala za Mnara wa Mlinzi kwa kutumia mashine iliyo rahisi kuendesha.

Ule utendaji wa kisiri-siri ulichukua wakati mwingi sana wa Therese, lakini alipata kazi ya kimwili ya nusu wakati iliyomwezesha kujiandalia kifedha yeye mwenyewe na mama yake. Yeye alijaribu kuwa mwenye tahadhari. Idadi fulani ya akina ndugu tayari walikuwa wametiwa mbaroni. Na kwa kuwa mama yake alikuwa anataabishwa na ugonjwa wa moyo, ingekuwaje kwa mama huyo ikiwa bintiye angetiwa mbaroni? Therese alimfariji, sikuzote akimtuliza kwa kumhakikishia kwamba hakika Yehova hangemwacha bila msaada.

Dada wengine wajasiri walitayarishwa pia kutumikia masilahi ya Yehova kwa njia yoyote iliyohitajiwa. Dada Stadtegger kutoka Wels alijitolea kusafiri kwenda magharibi kupelekea akina ndugu katika Tiroli vifaa vya funzo. Aliendelea kufanya hivyo mpaka alipoanguka mikononi mwa Gestapo. Bila kuhukumiwa kokote kisheria, alipelekwa kwenye kambi ya mateso ya Ravensbrück. Yeye hakurudi kamwe. Wakati fulani baadaye mume wake akatiwa kifungoni pia.

Je! Shetani Alikuwa Akithibitika Kuwa Mshindi?

Baada ya kuzuru akina ndugu tena na kuwaimarisha, katika Mei 1939, Ndugu Kraft alikaa muda mfupi tu katika nyumba yake ndogo katika Vienna kabla Gestapo hawajapiga bila huruma. Yeye alitiwa mbaroni katika Mei 25. Milango ya uangamizaji ya kambi ya mateso ya Mauthausen ikafunguka, na humo uhai wake ukakomeshwa. Huzuni kuu ilijaa mioyo ya akina ndugu waliposikia juu ya kifo chake. Yeye anakumbukwa kwa shauku kwa ajili ya upendo wake wenye kutokeza kwa Yehova na kwa ndugu zake.

Je! Shetani na mabaradhuli wake walikuwa wakithibitika kweli kweli kuwa washindi kwa kutia mbaroni na kufunga hao watumishi wa Mungu na kuua wengine? Tofauti sana na hilo! Kama inavyoonyeshwa na kisa cha Ayubu, ubishi wa Shetani ni kwamba mtu atatumikia Yehova ikiwa tu kila kitu kinaonekana kuwa sawa kwake. Hivyo kila Shahidi aliyethibitika kuwa mwaminifu chini ya magumu aliongeza kwenye ule ushuhuda mwingi kwamba Ibilisi ni mwongo mkubwa sana na kwamba Yehova ndiye Mungu wa kweli, ambaye walimpenda kwa moyo wao wote. Yehova atathawabisha sana washikamanifu wote kama hao.—Ayubu 1:6-12; 2:1-5; Yak. 5:11.

Aina Mbili za Mifuko ya Chakula

Ndugu ambaye sasa aliaminishwa daraka la kazi ya kuhubiri hakuwa akifanya kazi katika ofisi ya Sosaiti bali alikuwa na duka dogo la mboga ili kujiandalia mwenyewe na mke wake. Huyo alikuwa Peter Gölles. “Bila maagizo yoyote ya kitengenezo,” kama vile alivyolisema jambo hilo, yeye aliombwa aendeleze utendaji wa watu wa Mungu kadiri ilivyowezekana chini ya hali hizo zenye uonevu.

Kwa kuwa Ndugu Kraft hakuwa pamoja nao tena, Ndugu Gölles aliangalia urudufishaji na ugawanyaji wa vifaa vya Biblia vya funzo kotekote nchini. Yeye alifanya kazi kisiri-siri usiku katika vyumba vyenye baridi, na wakati wa mchana alionekana katika duka lake la chakula. Haikuwa salama kutumia usafiri wa posta, hivyo fasihi ilichukuliwa na matarishi. Michango iliyopatikana haikutosha kulipia gharama za usafiri, kwa hiyo Ndugu Gölles alitumia alichokuwa nacho mfukoni mwake mwenyewe. Kwa kuwa mara nyingi wateja walipata mboga zao na vyakula vikiwa vimepakiwa katika mifuko ya karatasi, wakati watu walioteuliwa walipoondoka dukani wakiwa na mifuko ya karatasi ambayo kidogo ilikuwa na vitu tofauti, hilo halikuonekana. Kwa muda fulani, matarishi na akina ndugu katika Vienna waliweza kupata chakula cha kiroho kutoka duka la Ndugu Gölles kwa njia hii.

Msaada kwa Ndugu Msimamizi

Tokea 1938 na kuendelea, ilizidi kuwa vigumu kudumisha uwasiliano na Uswisi na Uholanzi, ili kuingiza angalau nakala chache za Mnara wa Mlinzi nchini. Miwasiliano mingi ilikatizwa kwa sababu ya akina ndugu kutiwa mbaroni, na safari za garimoshi zikichukua juma au zaidi zilihitajiwa kabisa nyakati nyingine ili kupata chakula cha kiroho kutoka nchi za kigeni. Ndugu Gölles alijaribu kupata ugavi wa chakula cha kiroho kwa njia ya Pressburg, Chekoslovakia, Dada Kattner akiwa analeta vifaa vya funzo kutoka huko. Lakini upesi njia hii pia ilikatiliwa mbali.

Wakati wa siku hizo Ernst Bojanowski akaonekana katika mandhari ile. Yeye alikuja kutoka Ujeremani, lakini tayari alikuwa amekuwa akiwasiliana na akina ndugu katika Austria. Bojanowski alitolea Ndugu Gölles utumishi wake naye alifanya kazi pamoja na Dada Schreiber kurudufisha vifaa vya funzo. Bojanowski alitoa wazo la kuwa mtu mwenye ujasiri na mwenye uwezo mwingi wa kuanzisha mambo. Alienda safari za kupeleka fasihi pia. Hata alibatiza ndugu na dada wapya katika pindi tatu.

Msaada mwingine ulikuwa mashine ya kurudufisha iliyowekwa katika ghala la chini ya ardhi la nyumba ya mtunza bustani katika Vienna. Kuitumia kulitaka kazi nyingi sana kwa sababu ilikuwa lazima ifukuliwe kutoka mahali ilipofichwa kila wakati ilipotumiwa. Ijapokuwa hivyo, hakuna mtu aliyeona lililokuwa likifanywa, kwa sababu mwenye mali hiyo alikuwa amehama, na mtunza bustani tu, mmoja wa ndugu zetu, ndiye aliachwa kutunza nyumba ile.

Kuelekea magharibi karibu na mpaka wa Italia, Mashahidi wengine walikuwa wakisaidia. Dada Gelmi alikuwa akipanua slaidi za makala za Mnara wa Mlinzi ambazo Narciso Riet alileta kutoka Italia kwa kuvuka mpaka. Ndipo alipopiga chapa stensili kwa taipureta kwa ajili ya kurudufisha nazo nakala zilizokamilika zilipelekwa mahali palipo juu kwenye mlima. Kutoka hapo ugawanyaji ulifanywa. Dada Tammerl kutoka Innsbruck na Dada Entacher (mama na binti) kutoka Schwaz walishiriki kugawanya vifaa vya funzo kwa waamini wenzao. Wao waling’amua jambo ambalo lingetukia kwao ikiwa wangeshikwa, na walikuwa tayari kuelekeana nalo ikihitajiwa kabisa.

Mikononi mwa Adui

Ghafula wimbi jipya la kutiwa mbaroni likaanza, hasa wakati wa Septemba na Oktoba wa 1939. Neno lilizunguka miongoni mwa Mashahidi kwamba ndugu mmoja alikuwa amefunua majina kwa wenye mamlaka. Katika maandishi ya Gestapo ambayo sasa yanapatikana kwa ajili ya uchunguzi, unaweza kujisomea mwenyewe mambo haya mengi yaliyoandikwa kwa kalamu na karatasi. Ripoti hiyo ya Gestapo ya Vienna, yenye tarehe ya Novemba 2, 1939, husema hivi:

“Kuderna ambaye alitajwa katika ripoti ya kila siku ya Oktoba 31, 1939, ametaarifu kwamba utendaji uliokatazwa kisheria wa I.B.V. [Shirika la Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa] uliendeshwa mpaka hivi majuzi. Zaidi, yeye alifichua majina ya ndugu wenye kuongoza wa I.B.V. wa karibu wilaya zote za Vienna.”

Johann Kuderna alikuwa amekuwa mwamini mwenzi tangu 1924. Kwa sababu zisizojulikana tena, bila kukusudia, kwa wazi alikuwa ameanguka mikononi mwa adui.

Pigo zaidi lilikuwa kwamba ule usemi wa siri uliotumiwa na akina dada katika kugawanya magazeti uliingia pia mikononi mwa wenye mamlaka. Sasa ilikuwa rahisi kwao kufahamu lililomaanishwa na maneno “nakala 20 kwa ‘Resi’”; kwa sababu jina la kwanza la Dada Schreiber lilikuwa Therese, aliitwa Resi kifupi. Dada Schreiber alitiwa mbaroni na bila kuhukumiwa kokote kisheria akatiwa katika kambi ya mateso ya Ravensbrück. Namna gani mama yake? Alikuwa amekufa miezi miwili iliyopita.

Kutoa Ushahidi kwa Ujasiri Mahakamani

Baada ya muda fulani kupita, Dada Schreiber alirudishwa Vienna kutoka ile kambi ya mateso. Walikusudia kufanya nini naye? Yeye angepata kujua upesi. Wakati wa kuhukumiwa kisheria katika mahakama ya mkoa katika Vienna, aliona juu ya dawati hesabu fulani ya magazeti Mnara wa Mlinzi ambamo jina la Hitla lilionekana. Hayo yalikuwa yametokezwa kisiri-siri. Dada Schreiber alifikia mkataa kwamba walijua juu ya ushiriki wake katika kutokeza na kugawanya magazeti hayo.

“Je! wewe ulifanya mirudufisho hii?” hakimu akamuuliza kwa mkazo. Tayari kabla ya kutiwa kwake mbaroni Dada Schreiber alikuwa amesali kwa Yehova kwamba aweke maneno katika kinywa chake, ili aweze kutoa ushuhuda mzuri kwa ajili yake. Akisema kwa uthabiti “Ndiyo, nilifanya,” akakubali daraka.

Dada Schreiber alikuwa mwenye sura yenye kupendeza na alijiendesha kwa njia yenye kuheshimika. Hakimu yule, kwa wazi akiwa amevutiwa, alitaka kumwachilia. Lakini Gestapo walimweka kizuizini na wakamrudisha kwenye kambi ya mateso. Baadaye uhamisho kwenye kambi ya kufanya kazi ngumu uliokoa uhai wake, ingawa alilazimika kuvumilia miaka mitano na nusu ya kizuizi.

Kurudufisha Fasihi

Hizo zilikuwa siku ngumu kwa Ndugu Gölles wafanya kazi wenzi washikamanifu walipokuwa wakikamatwa mmoja baada ya mwingine. Yeye alijaribu kufanya yoteyote aliyoweza kuendeleza ugawanyaji wa chakula cha kiroho. Lakini ni nani angesaidia? Yeye alikumbuka kwamba dada mmoja alikuwa amemwendea miezi kadhaa mapema, akisema: “Ndugu Gölles, mimi ningependa kufanya jambo fulani kwa ajili ya kazi ya Bwana.” Alikuwa Hansi Hron (sasa Buchner), aliyekuwa amebatizwa katika 1931. Alikuwa ametumia miaka kadhaa katika nchi za kigeni. Sasa, katika wakati wa hatari, alirudi Austria. Na kutoka moyoni mwake alikuwa tayari kuchukua utumishi mgumu wa tarishi.

Ludwig Cyranek alijitolea kusaidia pia. Tayari yeye alikuwa ametumikia kifungo cha miaka miwili katika Ujeremani. Mara tu alipoachiliwa alichukua tena ile kazi ya kisiri-siri na akafanya ujuzi wake upatikane kwa akina ndugu katika Vienna. Yeye alishiriki ile kazi hatari ya kufanyiza nakala za Mnara wa Mlinzi.

Lakini je! mahali ilipokuwa mashine ya kurudufisha palikuwa pamefunuliwa pia? Kwa kutokuwa na uhakika wa jibu, akina ndugu walihamishia mashine kwanza mahali pamoja, kisha pengine. Huku Ndugu Cyranek akiandika stensili, Ndugu Joseph Schön kutoka Prague na Dada Anna Voll kutoka Vienna walimsomea maandishi, na Ernst Bojanowski, pamoja na ndugu mwingine, wakafanya kazi ya kurudufisha. Bado kutoka mahali pengine, Hansi Hron aliyachukua akawapelekee akina ndugu.

Kwa mara nyingine tena mashine ya kurudufisha ilihamishwa, na Ndugu Schön akapata mahali pa kuificha katika nyumba ya kukaa wakati wa kiangazi. Yeye na ndugu mwingine walifanya kazi ya kurudufisha humo. Wakati kazi hiyo ya kitheokrasi ilipokuwa imemalizika, Ndugu Schön alikuwa akiwapelekea akina ndugu vifaa vya funzo. Siku moja, kwenye kituo cha kupelekea vifurushi, aliombwa akae na kuzuru. Hilo lilikuwa kosa. Upesi akatiwa mbaroni.

Dada Hron alijifunza kutokana na ono hilo lenye kuhuzunisha. Yeye alipeleka vifurushi vyake haraka-haraka na kisha kwenda zake tena. Baada ya miezi sita hivi, akatiwa mbaroni pia. Lakini yeye alikuwa ametimiza tamaa yake ya moyoni ya “kufanya jambo fulani kwa ajili ya kazi ya Bwana.”

Kadiri wakati ulivyopita, ndivyo akina ndugu walivyopata kuwa na werevu zaidi katika kuficha fasihi na mahali pa vikundi vyao vya funzo. Hivyo, wakati upekuzi wa nyumba wa ghafula ulipofanywa na polisi hakuna fasihi iliyopatikana. Na kwa ajili ya mikutano yao, katika maeneo fulani akina ndugu walikuwa wakienda milimani au misituni kujifunza. Wakati mimea ya mahindi ilipokuwa imekua ikawa mirefu vya kutosha, vikundi vidogo vilikutana kati ya mistari ya mimea hiyo katikati ya shamba, ambapo hawangeweza kuonekana kutoka barabarani. Jinsi makala za funzo la Mnara wa Mlinzi zilivyokuwa zenye kufaa pia! Zilizotiwa kati yazo zilikuwa kama vile “Taifa Jaminifu” na “Uvumilivu Katika Ukweli.” Kweli kweli kilikuwa “chakula kwa wakati wake.”—Mt. 24:45.

Adui Atafuta Kirudufishaji

Wenye mamlaka ya umma walitayarisha pigo jipya. Walitaka kukamata Mashahidi wa Yehova wengi kadiri iwezekanavyo, lakini walikuwa wakijaribu kwa njia zote pia kukipata kifaa cha kurudufisha kilichokuwa kikitumiwa kufanyiza nakala za Mnara wa Mlinzi.

Faili za Gestapo zinazopatikana kwa ajili ya uchunguzi zina amri iliyotolewa katika Juni 8, 1940, inayosoma hivi: “Kwa amri ya RSHA [ofisi kuu ya usalama ya Serikali ya Ujeremani], Berlin, katika Juni 12, 1940, washiriki wote wa I.B.V. pamoja na watu wote wanaofanyia kazi harakati hii na watu wote wanaojulikana kuwa Wanafunzi wa Biblia wapaswa kupelekwa kifungoni. . . . Watu wanaopaswa kutiwa kizuizini wanatia ndani wanawake pia. . . . Tendo hili la polisi ya serikali linaathiri eneo lote la serikali ya Ujeremani na litatekelezwa ghafula katika Juni 12, 1940. Nyumba zitapekuliwa na wakati ule ule kutiwa mbaroni kufanywe, na vifaa vyovyote vya harakati ya Wanafunzi wa Biblia vitwaliwe.”

Shambulio hili la adui lilikuwa la ghafula sana hivi kwamba ni vigumu kurudia tena mambo yote madogomadogo. Lakini sisi tunajua kwamba katika mkumbo mmoja akina ndugu na dada 44 walitiwa mbaroni, kutia ndani tarishi wetu Hansi Hron.

Hata hivyo, ithibati inaonyesha kwamba adui alikusudia kutwaa zaidi ya watu. Hilo linafunuliwa katika hukumu ya mahakama moja ya Vienna yenye tarehe ya Januari 28, 1941. Inasoma hivi: “Ni baada tu ya uchunguzi mwingi ilipowezekana kupata mahali ambapo ile habari iliyopigwa chapa ilipofanyiziwa nakala, shimo likagunduliwa, na mashine ya kurudufisha, na taipureta pamoja na vifaa vingine vikapatikana na kutwaliwa.” Kusimanga kwa maadui wa watu wa Yehova kunaonyeshwa wazi na maneno hayo.

Je! Yeye Aliacha Msimamo Wake?

Baadaye, wakati Dada Hron alipokuwa akihojiwa, ofisa alikatiza mahoji hayo na kuondoka chumbani. Alipokuwa hayupo, jicho la Dada Hron liliangukia protokali, au rekodi ya mahoji pamoja na Ernst Bojanowski. Aliyosoma yalimshtua. Ilikuwa na majina mengi sana ya akina ndugu na mambo mengine mengi sana hivi kwamba hakuweza kujizuia kushuku kwamba Bojanowski alikuwa ameshirikiana na wenye mamlaka.

Je! ofisa huyo alikuwa ameweka karatasi hizo hapo kimakusudi, akitafuta kuvunja roho yake na kumfanya afichue habari zaidi? Protokali ya mahoji ya Bojanowski ilihifadhiwa wakati wa vita. Visehemu vyayo vilisomeka kama historia ya kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Austria kutoka 1938 mpaka Januari 1940. Si ajabu neno lilienea miongoni mwa akina ndugu: “Tulisalitiwa!”

Ili kushiriki utendaji fulani wa kiroho, kisiri-siri, Bojanowski alikuwa ameenda Ujeremani katika Desemba 1939. Wote wawili yeye na Anna Voll walikamatwa katika Dresden. Makala moja katika gazeti rasmi la utawala wa Nazi, Völkischer Beobachter, la Machi 21, 1941, huongezea picha hiyo. Humo tunasoma hivi:

“Dresden, Machi 20. Mahakama Maalum katika Dresden ilimhukumia kifo . . . Ludwig Cyranek . . . kwa msingi wa kudhoofisha nguvu za kijeshi katika kutenda kisadfa pamoja na ushiriki katika shirika linalopinga utumishi wa kijeshi na katika kuhalifu marufuku ya Shirika la Kimataifa la Wanafunzi wa Biblia Wenye Bidii . . . Ernst Bojanowski wa Berlin alihukumiwa pia kwa makosa ayo hayo, miaka 12 gerezani na kupoteza heshima kwa miaka kumi.”

Ludwig Cyranek, anayetajwa juu, alikuwa yule ndugu mwaminifu ambaye alijifanya apatikane mwenyewe bila woga kwa ajili ya kazi zaidi ya kisiri-siri baada ya kuwa tayari ametumia kifungo cha miaka miwili. Na Bojanowski? Je! yeye alikuwa amepigwa kinyama? Je! kuhangaikia kupita kiasi usalama wake mwenyewe kulimfanya afichue habari juu ya ndugu zake? Je! ile protokali ilikuwa imefanyizwa kibandia kwa sehemu? Sisi hatujui, lakini kulingana na akina ndugu katika Ujeremani, Bojanowski alikuwa gerezani kwa muda mfupi tu.

Wachanga Lakini Washikamanifu

Karatasi za kiserikali zilizohifadhiwa kutoka enzi ya Nazi hazifunui kila kitu. Lakini zinasimulia habari za wengi ambao ukamilifu wao kwa Yehova haungeweza kuvunjwa. Auguste Hirschmann (sasa Bender), ambaye wazazi wake walikuwa pia katika ukweli, alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 17 alipohojiwa na Gestapo. Msimamo wake imara unaonyeshwa katika ripoti hii ya Oktoba 1941:

“Yeye alifundishwa mafundisho ya I.B.V. na wazazi wake naye anadai kuwa Shahidi wa Yehova hata mpaka leo hii. Mtu huyo aliyetajwa jina alijifunza Biblia kwa kurudia-rudia pamoja na wazazi wake, ili yeye, kama anavyokubali mwenyewe, ‘aweze hivyo kuimarisha imani na ushikamanifu wake’ na awe na imara vya kutosha kushikamana na mafundisho yanayowakilishwa na I.B.V. . . . Hirschmann anakataa kutoa habari yoyote juu ya watu wa sadikisho lile lile. Lazima yeye aelezwe kuwa asiyefundishika.”

Elisabeth Holec, ingawa ni msichana dhaifu, mgonjwa-mgonjwa wa umri wa miaka 18, pia alikuwa imara na aliyepiga moyo konde katika msimamo wake kwa ajili ya ukweli. Katika protokali yao ya tarehe ya Desemba 17, 1941, wakuu wangeweza kusema tu hivi: “Elisabeth Holec angali anashikamana na mawazo ya I.B.V. na anakubali kuwa alikusanyika pamoja na watu wenye maoni yanayofanana [na yake]. Hata hivyo, yeye anakataa kutoa habari yoyote juu ya Wanafunzi wa Biblia wengine na anajulisha wazi kwamba hiyo ingekuwa usaliti, jambo lisilozoewa katika ‘Tengenezo’ lile.” Yeye pamoja na mama yake walipelekwa kwenye kambi ya mateso ya Ravensbrück, alimofia.

Lakini sasa twarudi kwenye 1939, ule mwaka uliofuata kutwaliwa kwa Austria na vikosi vya Hitla.

Kutiwa Mbaroni Katika Usiku wa Ukumbusho

Ukumbusho katika Aprili 4, 1939, ilithibitika kuwa siku ya mitihani mikali kwa ndugu wengi. Walifanya matayarisho yao, wakarudia tena yale mambo makuu ya hotuba, na wakatayarisha mifano. Lakini kulikuwako wengine ambao walifanya matayarisho pia.

Katika Bad Ischl watu watano walikutana katika nyumba ya Franz Rothauer kuadhimisha Ukumbusho. Walikuwa wamekusanyika kukumbuka umaana wa kifo cha Yesu Kristo katika utimizo wa kusudi la Yehova. Wao walijua vizuri sana kwamba Yesu alikuwa amepatwa na mitihani mikali ikiongoza kwenye kifo chake lakini kwamba alikuwa ameonyesha ukamilifu usiovunjika.

Ndugu Engleitner alikuwa amejitayarisha vizuri kutolea kikundi kidogo hotuba lakini hakuwa na habari iliyoandikwa. Hata hivyo, yeye alikuwa ndipo tu ameanza kunena wakati dirisha lilipobishwa kwa nguvu nyingi. Mwenye nyumba alifungua mlango, na wanaume watano wakaingia kwa kishindo ndani ya chumba walimokuwa akina ndugu. Wawili wa wajidukizi walikuwa washiriki wa Gestapo yenye kutia hofu, na watatu walikuwa wa kutoka ile SS (kikosi cha kupigana cha Chama cha Nazi). Akina ndugu waliamriwa wainue mikono na kukaa katika hali hiyo mpaka wapekuliwe. Wanaume hao walipindua kila kitu katika nyumba hiyo nao wakaghadhibika kwa sababu hawakupata fasihi yoyote ya Mnara wa Mlinzi.

Dokezo lao lilikuwa kwamba akina ndugu wajijulishe wazi kuwa washiriki wa madhehebu ya kidini ambayo yangesalimu amri za Führer (Adolfu Hitla) kwa moyo wa kupenda na kwamba hawakutaka kuwa na uhusiano wowote pamoja na Mashahidi wa Yehova. Bila shaka, hakuna yeyote wa akina ndugu aliyekuwa na nia ya kufanya hivyo. Kama tokeo, wote wakatiwa mbaroni. Yule pekee aliyeruhusiwa kurudi nyumbani ni Ndugu Engleitner, naye alikamatwa baadaye. Wale ndugu wengine walipelekwa mara hiyo gerezani katika Linz mji mkuu wa mkoa. Humo walijiunga na Mashahidi wengine wengi waliokuwa wametiwa mbaroni usiku huo. Upesi baada ya hapo akina ndugu walisafirishwa kupelekwa kwenye kambi ya mateso ya Dachau, hali akina dada walipelekwa Ravensbrück.

Alois Moser, Josef Buchner, na ndugu wengine katika Braunau na sehemu zilizo kandokando walikuwa na maono yanayofanana na hayo usiku huo. Wao pia walitiwa mbaroni wakati wa mwadhimisho wa Ukumbusho. Miaka mingi baadaye Ndugu Buchner angali alikumbuka hotuba ya Grünewald kamanda wa kambi wakati ndugu walipowasili Dachau: “Na sasa, nyinyi Wanafunzi wa Biblia, nyinyi mtabaki kuwa ‘orodha yenye kudumu’ ya Dachau. Nyinyi mtaoza apa hapa katika kambi hii. Nyinyi hamtatoka hapa; njia yenu ya kutokea itakuwa kupitia bomba la kutolea moshi.” Kwa maneno hayo yeye alimaanisha kwamba mabaki yao yangechomwa kwenye mahali pa kuchomea maiti.

Ndiyo, walikuwa wakitakwa wakabili kifo mikononi mwa maadui wa ibada ya kweli hata kama vile alivyokuwa amefanya yule ambaye kifo chake walikuwa wamekutanika kukumbuka. Walivumilia miaka sita ya mateso katika kambi za mateso kabla ya kuachiliwa mwishowe.

Msimamo kwa Ajili ya Kutokuwamo kwa Kikristo

Zamani sana mnabii Isaya alikuwa ameandika hivi: “Lazima itukie katika sehemu ya mwisho ya zile siku kwamba . . . vikundi vingi vya watu hakika vitakwenda na kusema: ‘Njooni, nyinyi watu, na acheni sisi twende juu kwenye mlima wa Yehova, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.’ . . . Naye hakika atafanya hukumu miongoni mwa mataifa na kunyosha mambo kuhusiana na vikundi vingi vya watu. Nao itakuwa lazima wafue panga zao ziwe majembe ya plau na mikuki yao iwe makasi ya kupogolea. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa, wala wao hawatajifunza vita tena.” (Isa. 2:2-4, NW) Kwa kutofautisha, utawala wa Nazi ulitaka kwamba wanaume wote wakakamavu wazoezwe katika ufundi wa vita. Mashahidi wa Yehova katika Austria walifanya nini?

Muda mfupi baada ya Nazi kutwaa Austria, amri ya serikali ilitolewa, ikitaka wote waliokuwa wamefanya utumishi wa kijeshi wakati wa Vita ya Ulimwengu 1 washiriki katika mazoezi ya uwanjani ya siku tatu. Kwa hiyo, Johann Rainer alijulishwa akapige ripoti kwenye makao ya askari jeshi katika Innsbruck.

Tamasha iliyoje! Wanaume mia nane walisimama kiaskari wale kiapo cha kijeshi. Mbele yao wote, Ndugu Rainer alikataa. Bila kukawia kokote, yeye alipelekwa kwenye chumba kimoja akahojiwe. Alipokuwa akiondoka chumbani, alimwona padri wa jeshi, ambaye jina lake lilikuwa Klotz, akiwa katika yunifomu yake ya kijeshi, msalaba mkubwa ukiwa unaning’inia kuzunguka shingo yake na kifua chake kikiwa kimepambwa kwa medali nyingi alizokuwa ametuzwa wakati wa Vita ya Ulimwengu 1. Kwa salamu ya “Heil Hitler!” padri huyo akakaribia ofisa ampe oni lake juu ya Ndugu Rainer.

Wakati fulani baadaye Ndugu Rainer aliletwa tena mbele ya maofisa kadhaa akahojiwe zaidi. Mmoja wa maofisa alisema kwamba yale ambayo yule padri alikuwa amewaambia hayakuafikiana na yale ambayo Ndugu Rainer alikuwa amesema. Ndugu Rainer akajibu kwamba wangeweza kusoma kwenye Mathayo 23 yale ambayo Yesu alikuwa amesema juu ya viongozi wa kidini kama hao, kwamba wao ni wanafiki. Ofisa mwingine akanena: “Mtu huyu anasema kweli!” Ijapokuwa hivyo, Ndugu Rainer alifungiwa, na kesi yake ikarejezewa mahakama ya mkoa. Kufikia hapo, mwenye biashara ya jumla ya vyakula ambapo ndugu alikuwa ameajiriwa aliwasiliana na mkuu wa polisi, akidai kwamba yeye hakuwa na mtu wa kufanya kazi ya Ndugu Rainer. Kwa hiyo akaruhusiwa arudie jamaa yake na kazi yake ya kuajiriwa.

Katika visa zaidi ya kimoja, watu wa ukoo wasio Mashahidi au waajiri kazi wenye uwezo mwingi wa kushawishi waliingilia mambo kwa ajili ya akina ndugu, mara nyingi kwa sababu walithamini sana ufuataji haki na kazi yenye bidii-nyendelevu ya akina ndugu. Lakini mambo hayakuwaendea vizuri hivyo wote.

Jitihada za Bure za Wakuu wa Nazi

Wapata mwaka mmoja baada ya vikosi vya Hitla kupiga miguu kuingia Austria, Hubert Mattischek alikuwa angali anaendeleza kazi ya kuhubiri bila kuacha. Lakini katika Machi 1939, gari lilifika karibu na nyumba yake na wakuu wawili wa Gestapo wakatoka ndani yalo. Ndugu Mattischek hakulazimika kukisia ni nani walitaka kuzuru. Yeye alikuwa bila wasiwasi na mtulivu.

“Lazima sisi tupekue nyumba kutafuta fasihi isiyo halali,” akasema mmoja wao. Kama tahadhari, Ndugu Mattischek alikuwa tayari amegawanya sehemu kubwa ya fasihi, na ile nyingine alikuwa ameiweka salama nje ya nyumba. Kwa hiyo upekuzi ukathibitika kuwa wenye kutamausha kwa wakuu hao.

“Utafanya nini wakati utaitwa karibuni ukafanye utumishi wako wa kijeshi?” akauliza mmoja wao.

Jibu lisilo la kusitasita la Ndugu Mattischek lilikuwa: “Mimi nitakataa kula kiapo au kufanya jambo lolote ambalo linahusiana na vita.”

Kusema hivyo mkuu wa pili akauliza: “Je! wewe unajua matokeo?”

Ndugu yetu akajibu, “Mimi nimekuwa nikiyajua kabisa kwa muda mrefu,” naye akatiwa mbaroni papo hapo.

Majuma kadhaa baadaye Ndugu Mattischek alijikuta mwenyewe katika gari la ng’ombe, pamoja na ndugu wengine, wakielekea kambi ya mateso ya Dachau. Kwa ujumla, Ndugu Mattischek alivumilia kukaa katika kambi za mateso tatu mbalimbali kabla ya malango ya uhuru kupembea afunguliwe.

Wakati akina ndugu walipowasili kwenye kambi ya mateso ya Mauthausen, yule kiongozi mwenye amri Spatzenegger aliye na sifa mbaya aliwakaribisha kwa maneno haya: “Hakuna Gipsi na hakuna Mwanafunzi wa Biblia atatoka hapa akiwa hai.” Wengi walifia humo.

Matoleo mengi yalifanywa ambayo yangewaruhusu akina ndugu kuepuka njia hii ya kuleta kifo. Kama kielelezo, mapema asubuhi moja wakati walipokuwa katika kambi ya mateso ya Mauthausen, Hubert Mattischek na ndugu yake Willi waliambiwa wapige ripoti penye lango la kambi. Kwa kueleweka, walihisi mkazo katika mishipa yao ya neva walipokuwa wakitembea kuelekea penye lango. Walipelekwa kwa Ziereis, kamanda wa kambi, aliyekuwa amezungukwa na kikundi cha viongozi wa chama wenye vyeo vya juu na wanaume fulani wa SS. Gauleiter (cheo cha kiongozi wa chama wa mkoa) wa Austria ya Juu, August Eigruber, alikuwapo pia.

Ziereis akajifanya mnenaji, na akigeukia wale ndugu wawili, akasema: ‘Gauleiter aliye hapa angewapeleka nyinyi ndugu wawili nyumbani kwenu mara moja. Mnalotakwa kufanya tu ni kutia sahihi kipande cha karatasi, kilichotayarishwa hasa kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova, na hilo lingewaepusha nyinyi na miaka mingi ya kuteseka.’

Kulikuwako kimya na mduwazo mfupi miongoni mwa wakuu waliposikia wale ndugu wakijibu kwa imara hivi: “Sisi hatutaki kuwa wasio waaminifu kwa Yehova Mungu na kwa imani yetu.”

Ziereis, yule kamanda, akageukia wale wanaume waliokuwapo: “Je! mimi sikutangulia kuwaambia?” Kwa wazi walikuwa wameongea mapema juu ya hali ya kutoshindwa ya Mashahidi wa Yehova.

Mazoezi ya Utumishi wa Kazi ya Taifa

Franz Wohlfahrt aliandikishwa katika Utumishi wa Kazi ya Taifa wa Reich (ya Ujeremani). Lakini alipofika kwenye kambi ya mazoezi, aling’amua kwamba shirika hilo lililenga pia kwenye mazoezi ya kabla ya kuingia jeshini. Yeye alikataa kuvaa yunifomu na kufunga mshipi kiunoni. Ndipo siku moja, vijana 300 na viongozi 100 hivi wa vyeo vya chini na vya juu pia wakapanga mstari kwenye ua wa kukutanikia, naye Franz Wohlfahrt akaamriwa apite akipiga miguu mbele yao mkono wake ukiwa umeinuliwa katika salamu ya Hitla, wakati ule ule atolee heshima bendera ya swastika. Badala ya hivyo, yeye alikumbuka jambo ambalo wale vijana watatu Waebrania walikuwa wamefanya walipoamriwa wasujudu mbele ya mfano ambao Nebukadreza alikuwa amesimamisha katika Babuloni ya kale. (Dan. 3:1-30) Lo, hilo lilimpa imara iliyoje! Yeye alifuata kielelezo chao cha uaminifu.

Siku nyingi hazikupita, na ndipo Dakt. Almendinger, mkuu wa cheo cha juu kutoka Berlin, akajaribu kibinafsi kufanya ndugu yetu kijana abadili nia yake. “Wewe hujui hata kidogo linalokungojea,” akataja Dakt. Almendinger wakati wa mazungumzo hayo.

“Oh, ndiyo najua,” akajibu ndugu yetu mwenye umri wa miaka 20. “Baba yangu alikatwa kichwa kwa sababu iyo hiyo majuma machache tu yaliyopita!” Dakt. Almendinger akashindwa. Hatimaye, Franz alihukumiwa miaka mitano ya kifungo kwenye Kambi ya Rollwald katika Ujeremani.

Wauawa kwa Sababu ya Kutokuwamo kwa Kikristo

Siku moja katika Septemba 1939, uvumi wenye kufadhaisha ulienea kotekote katika Salzburg, jiji moja lililo chini ya milima. Ulifanya watu wawe na wasiwasi—hata wale waliotarajia manufaa kubwa kutokana na utawala wa Hitla. Ni kitu gani walichokuwa wakinong’onezeana masikioni? Ilisemekana kwamba wanaume wawili walikuwa wamepigwa risasi mpaka kufa kwenye mahali pa kijeshi pa kupigia shabaha pa Glanegg karibu Salzburg.

Kilichoonekana mwanzoni kuwa uvumi kilikuwa ukweli mchungu. Wanaume hao, Johann Pichler na Josef Wegscheider, wawili wa ndugu zetu, walikuwa wameuawa na kikosi cha jeshi kwa sababu ya kukataa utumishi wa kijeshi. Lakini uuaji huo haukuendelea kwa njia laini kama makamanda wale walivyotarajia. Hao ndugu wawili walikuwa wamenena waziwazi kwamba haikuwa lazima kuwafunga macho, ingawa walifungwa macho hata hivyo. Kisha wakati amri ilipotolewa wale askari jeshi walikataa kupiga risasi. Ilikuwa ni baada tu ya askari jeshi hao kuonywa kwa mkazo kwamba wao wangeelekeana na hatua za kutiwa nidhamu wenyewe ikiwa wangeshindwa kutii, na ilikuwa ni baada tu ya amri kurudiwa mara ya pili, ndipo askari jeshi hao wakawapiga risasi hao wanaume wasio na hatia. Lakini mengi zaidi yalihusika.

Wakati wa jaribio katika Salzburg, hakimu na washiriki wake walikuwa wamejaribu kuwafanya washtakiwa wabadili nia zao. Hakimu alikuwa ameita wake za wanaume hao waje katika chumba cha mahakama, akitumaini kwamba kuwapo kwao kungevuta wanaume hao wakubali kushindwa. Tofauti kabisa na hivyo, mmoja wa wanawake hao alikuwa amenena maneno ya kuwatia moyo, akisema hivi: “Uhai wenu umo mkononi mwa Mungu.” Hilo lilikuwa limevuta sana hakimu hivi kwamba alikuwa amegonga-gonga meza kwa ngumi yake kwa fadhaa na kupaaza sauti hivi: “Watu hawa si wahalifu wala wasaliti, bali, ni kikundi cha waamini ambacho hesabu yao si wawili au watatu bali inafikia mamia na hata maelfu!” Ijapokuwa hivyo, sheria ilidai hukumu ya kifo.

Wakati wa siku iliyotangulia kuuawa kwao, Ndugu Pichler na Wegscheider walikuwa wametembelewa katika seli yao, na jaribio jipya lilikuwa limefanywa wapate kubadili nia zao. Walipoulizwa kama walikuwa na tamaa moja ya mwisho, wao walionyesha tamaa ya kupata Biblia. Ililetwa kwao na hakimu mwenyewe binafsi. Yeye aliwatazama wakiwa katika seli yao mpaka usiku wa manane na ndipo akaenda zake akisema: “Wanaume hao wote wawili katika saa yao ya mwisho walikuwa katika muungano pamoja na Mungu wao; kweli kweli walikuwa wanaume watakatifu!”

Uuaji ulipomalizika, majeneza hayo mawili yalitolewa yapate maziko ya faragha. Wapatao 300 walihudhuria mazishi, bila shaka ilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Kuimba kulitakazwa, na sala ilikatizwa hatimaye na maneno makali ya mkuu wa Gestapo kwa sababu aliiona kuwa ndefu mno. Pia Gestapo walikuwa wamekataza utumizi wa jina Yehova. Lakini hilo halikuzuia mmoja wa akina ndugu kulia kwa sauti hivi majeneza yalipokuwa yakishushwa: “Mpaka tuonanapo tena katika Ufalme wa Yehova.”

Baada ya matukio yaliyozunguka uuaji huu kujulikana katika Salzburg, kesi nyingine zote za uuaji zilihamishiwa Berlin-Plötzensee, Ujeremani.

Maneno ya Imani Kutoka Seli ya Kifo

Kutoka kitovu cha uzuizi cha Berlin-Plötzensee, Franz Reiter mwenye umri wa miaka 36 aliandikia mama yake katika Januari 6, 1940, hivi: “Mimi ninasadikishwa kwa imara katika imani yangu kwamba mimi ninatenda bila kosa. Nikiwa hapa, mimi ningali ningeweza kubadili nia yangu, lakini kwa Mungu hiyo ingekuwa utovu wa ushikamanifu. Sisi sote hapa twataka kuwa waaminifu kwa Mungu, kwa heshima yake.”

Yeye alisema “sisi sote” kwa sababu walikuwamo ndugu watano zaidi kutoka karibu na mji wa kwao ambao, kama yeye, walikabili kifo kwa kukatwa kichwa kwa mashine. Barua yake yaendelea:

“Kwa yale niliyojua, kama ningalikula kiapo [cha kijeshi], ningalitenda dhambi inayostahili kifo. Huo ungekuwa uovu kwangu. Singekuwa na ufufuo. Lakini nashikamana na yale aliyosema Kristo: ‘Yeyote atakayeokoa uhai wake ataupoteza; bali yeyote atakayepoteza uhai wake kwa ajili yangu, uyo huyo ataupokea.’ Na sasa, Mama yangu mpendwa na ndugu na dada zangu wote, leo mimi niliambiwa hukumu yangu, na msiogopeshwe, ni kifo, nami nitauawa kesho asubuhi. Mimi nina imara yangu kutoka kwa Mungu, sawasawa na ilivyokuwa sikuzote kwa Wakristo wote wa kweli kurudi nyuma katika wakati uliopita. Mitume wanaandika, ‘Yeyote aliyezaliwa kutoka kwa Mungu hawezi kufanya dhambi.’ Ndivyo ilivyo kwangu mimi. Hilo mimi niliwathibitishia, nanyi mngeweza kulitambua. Wangu mmoja mpendwa, usiwe na moyo mzito. Ingekuwa vizuri kwa nyinyi nyote kujua Maandiko Matakatifu vizuri zaidi bado. Ikiwa nyinyi mtasimama imara mpaka kifo, sisi tutaonana tena katika ufufuo. . . .

“Franz wako

“Mpaka tuonanapo tena.”

Baadhi ya waliopokea barua kama hiyo walikuwa wenzi waliofunga ndoa. Dada Endstrasser wa Graz alikuwa angali mke kijana wakati mtu wa posta alipompokeza barua yenye tarehe ya Desemba 15, 1939. Jaribu tu kuwazia hisia zake alipokuwa akiisoma:

“Mpendwa Erna,

“Ilitukia tu kama nilivyoamua . . . Usilie, kwa sababu sisi tumekuwa tamasha ya jumba la michezo kwa ulimwengu, na kwa malaika, na kwa wanadamu. (1 Kor. 4:9, NW) Salamu kwako kwa mara nyingine tena na busu katika roho.

“Dati wako

“Nitakuona tena katika Ufalme.”

Barua kama hizo zikionyesha imani kubwa zilikuwa kitia-moyo kwa wale waliokuwa wangali wakifurahia uhuru waonyeshe uaminifu. Wao, kwa upande mwingine, walijaribu kutia moyo ndugu zao waliotiwa kifungoni, ijapokuwa hatari yoyote ambayo hiyo ingemaanisha kwao wenyewe.

Kama kielelezo, barua ambayo Franz Zeiner alipokea alipokuwa gerezani katika Berlin ilitia ndani sihi hii: “Uwe imara katika imani kwa sababu Yesu Kristo atatusaidia sisi, ndivyo na Baba yetu mkuu wa kimbingu . . . ” Kama vile ingetazamiwa, barua hii ilikuwa imesomwa na mkaguzi. Franz Zeiner aliuawa Julai 20, 1940. Lakini namna gani Wilhelm Blaschek, aliyeandika barua hiyo akimtia moyo Franz awe imara katika imani? Yeye alipatikana, akatiwa mbaroni, na akahukumiwa Agosti 11, 1941, miaka minne ya kazi ngumu katika gereza kwa shtaka la ‘kudhoofisha vikosi.’

Watenganishwa na Watoto Wao

Mitihani ambayo wengine walielekeana nayo ilihusu watoto wao. Kwa sababu walikuwa wakifundisha watoto wao imani zenye msingi wa Biblia za Mashahidi wa Yehova, Richard Heide na Johann Obweger waliitwa waje mbele ya msimamizi wa Mahakama ya Wilaya ya St. Veit⁄Glan.

Baada ya hapo, Ndugu Heide alipelekewa amri ya mahakama iliyoamuru kwamba atanyang’anywa mtoto wake. Amri hiyo ilitoa hoja hii: “Ni hatari kuacha yeye [mwana, Gerhard] katika utunzaji wa babaye, kwa kuwa yeye ni Mwanafunzi wa Biblia naye hukataza mwanaye kutoa salamu ya Hitla na kuimba nyimbo za taifa.”

Gerhard alipewa atunzwe na mtu mwingine, na baba yake aliruhusiwa kumwona mara kwa mara tu. Baadaye, yeye na darasa lake lote la shule walipelekwa kwenye kambi ya watoto ya Lienz, Tiroli Mashariki, ambamo alikaa mpaka mwisho wa vita katika 1945. Lakini Gerhard hakusahau yale ambayo wazazi wake walikuwa wamemfundisha. Yeye amekuwa painia kwa zaidi ya miaka 38!

Mchanga Lakini Mwaminifu

Na namna gani binti ya Johann Obweger? Hermine alikuwa na miaka 11 tu wakati alipochukuliwa kutoka kwa wazazi wake na kuwekwa katika shule ya kugeuzia tabia. Lakini wazazi wake walikuwa wamefanya tumizi zuri la fursa zao kukaza kikiki ukweli ndani ya binti yao.

Wapinzani wa ukweli hawangeweza kuvunja ushikamanifu wa Hermine kwa Yehova. Jitihada kali zilizotiwa kumfanya aimbe wimbo wa kizalendo au atumie salamu ya “Heil Hitler!” hazikufanikiwa. Yeye alikataa kwa imara sana kuacha msimamo wake kwa vyovyote. Siku moja mwalimu alijaribu kumlazimisha avae jaketi ya yunifomu ya Chama cha Wasichana wa Ujeremani. Lakini hata wale watu wenye daraka wajaribu kadiri gani kumvalisha jaketi hiyo, wao hawakufaulu kamwe kumvalisha kupita viwiko, na hivyo wakaacha kujaribu.

Ijapokuwa wenye mamlaka wa shule walichukizwa, wazazi wake wangali waliruhusiwa kutembelea binti yao. Kama kawaida wao walikuwa wakitumia fursa hizo kumtia moyo asimame imara katika imani. Hermine alitiwa moyo pia na ushikamanifu wa ndugu yake Hans. Yeye alijua kwamba nduguye alikuwa gerezani na kisha katika kambi ya mateso kwa sababu yeye alikataa utumishi wa kijeshi. Pia yeye alijua kwamba alikuwa akivumilia kiaminifu. Hata hivyo, mmoja wa ndugu zake alijiunga na jeshi. Na kwa werevu walinzi wa shule walitumia hilo kuwa hoja katika jaribio lao la kuvunja ushikamanifu wake. Lakini wao hawakuwa wamefikiria kupiga moyo konde kwa Hermine. Jibu lake lisiloyumbayumba lilikuwa: “Mimi si mfuasi wa ndugu yangu. Mimi ni mfuasi wa Kristo Yesu!”

Kwa sababu ya nia yake ya kutoacha msimamo wake na kwa sababu walitaka kukomesha ziara za wazazi wake, wenye mamlaka walipeleka mtoto huyo kwenye konventi (kao la watawa) katika Munich, Ujeremani. Hata hivyo, katika Mei 1944 yeye aliruhusiwa aende nyumbani kwa siku chache. Hilo liliwashangaza sana wazazi wake. Lakini wenye mamlaka hawakutazamia jambo lililotukia sasa. Hermine alibatizwa alipokuwa huko, na Ndugu Ganster, aliyekuwa angali anaweza kutumikia ndugu zake kwa uhuru, alitoa hotuba ya ubatizo. Hilo lilimtia Hermine imara iliyoongezeka akae akiwa mshikamanifu kwa Yehova kwa wakati uliobaki mpaka mvunjiko wa mwisho wa utawala wa Nazi.

Jihadhari! Wajasusi na Watoa-Habari

Kwa sababu ya watoa-habari kuendelea kujasisi katika kila mji na kijiji—na zaidi ya yote, kujasisi kwa walinzi wa jengo na wengine waliofanyia Gestapo kazi—utendaji wa kiroho wa akina ndugu ulizidi kuwa mgumu. Siku moja Johann Viereckl alitaka kuzuru Peter Gölles, ambaye wakati huo alikuwa na daraka la uangalizi wa kazi ya kuhubiri katika Austria. Badala ya kwenda moja kwa moja kwa duka la Ndugu Gölles, Ndugu Viereckl alitua kwenye nyumba jirani aulizie mwanamke mfanya biashara aliyekuwa ameonekana kupendezwa katika ukweli na ambaye alijua Ndugu Gölles. Aliuliza habari za Peter Gölles na kama alikuwa ametiwa mbaroni. Hata hivyo, mwanamke huyo hakutoa habari zozote. Badala ya hivyo, yeye alimwambia ndugu avuke barabara aende kwenye duka la mwuza maua. Mwanamke huyo alisema kwamba ndugu angepata habari aliyoomba humo.

Hilo lilimfanya Ndugu Viereckl ashuku, kwa hiyo badala yake akarudi nyumbani. Upesi baada ya hapo yeye alijifunza kwamba Gestapo walikuwa wakingojea kwenye duka hilo la mwuza maua ili kuzuia na kukamata yeyote aliyetaka kumwona Ndugu Gölles. Kabla ya muda mrefu kupita, lile duka lilifungwa, kwa kuwa Ndugu Gölles na mke wake walipelekwa kifungoni katika Juni 12, 1940.

Jaribio la Mahakama Lisilo la Kawaida

Ndugu Gölles alishtakiwa kwa kuelekeza kazi ya Mashahidi wa Yehova katika Austria. Baada ya kufungiwa miezi mingi, aliletwa mbele ya hakimu aliyekuwa na sifa mbaya ya kutoa hukumu za kifo na ambaye kwa kasirani aliwaita Wanafunzi wa Biblia jipu juu ya watu wa Ujeremani. Wakili wa mashtaka wa umma alitaka hukumu ya kifo. Baada ya Ndugu Gölles kujibu mashtaka Kibiblia na wakili mtetezi wake akatoa hotuba yake, mahakama ikaahirishwa. Kabla ya jaribio kurudiwa, mambo yakabadilika kwa njia yenye kushangaza.

Mapema asubuhi Ndugu Gölles alisikia ufunguo katika mlango wa seli yake ukifungua. Mlinzi wa gereza akampungia mkono aje naye akampeleka kwenye chumba kilichotiwa makomeo. Ni nani aliyekuwa akimngojea humo? Ni yule hakimu, akiwa peke yake.

“Mimi nataka kukutajia,” akaanza yule hakimu, “kwamba ninahalifu sana kiapo changu cha cheo kwa kunena na mshtakiwa faraghani, lakini mimi nafanya hivyo kwa sababu sikuweza kupata pumziko au usingizi wowote tangu jaribio lile. Mimi ningejiona kuwa mwuaji kimakusudi ikiwa ningetangaza hukumu ya kifo kwako.”

Kukawa na kimya kabisa chumbani. Ndugu Gölles ndiye aliyenena hatimaye. “Shetani ndiye huleta hali kama hizo,” akasema. “Ndiye mwuaji hasa. Nawe, ni mtu tu atangazaye hukumu kwa msingi wa mambo hakika ya kesi ya mahakama.” Ile hali ya wasiwasi ikatulia.

“Mimi nitajaribu kuongoza mambo kwa werevu katika njia ya kwamba wewe hutapoteza uhai wako,” akaahidi yule hakimu. Ndipo akaongeza jambo ambalo lingekuwa na matokeo mabaya sana kwake: “Kwa kweli mimi sitaki kuonekana kama mtetezi wa Serikali, bali, mimi nataka kukusaidia uponyoke taya za kifo.” Ndipo hakimu huyo akaweka mkono mmoja juu ya bega la ndugu yetu, na kwa ule mwingine akafumbata mkono wa ndugu yetu.

Jaribio likachukua mwendo usio na upendeleo zaidi kufuatia kurudiwa kwalo, huku hakimu akitetemeka wakati wote. Mahakama haikukubali dai la hukumu ya kifo la wakili wa mashtaka, bali, ilihukumia Peter Gölles miaka kumi ya kifungo cha gereza, isipokuwa kuwe na punguzo. Yeye alitumia miaka mitatu na nusu iliyofuata katika kizuizi cha kukaa peke yake katika gereza la Stein, Austria ya Chini.

Mtumishi Mnyenyekevu

Wenye mamlaka ya umma walitambua ni sehemu yenye umaana kadiri gani katika kazi ya kisiri-siri aliyotimiza Peter Gölles, mtu huyu dhalili ambaye alikuwa amejitoa kabisa kwa Yehova. Protokali zilizohifadhiwa miongoni mwa maandishi ya Gestapo zilidhihirisha hilo. Kutokana na elezo lao mtu angeweza kuwazia kiongozi imara, mwenye nishati msukumo. Lakini sivyo kabisa! Yeye alikuwa mtu mwenye kiasi asiyetaka kamwe kujulikana. Baada ya utawala wa Nazi kukoma katika 1945, alishiriki katika kujenga upya tengenezo katika Austria na baadaye akarudi tena katika hali ya kutojulikana. Kwa miaka kadhaa alisaidia kutayarisha vifurushi vya fasihi kwenye Betheli ya Vienna kwa ajili ya upakizi. Kwa nia yake ya fadhili na urafiki, yeye pamoja na Helene, mke wake mwenye bidii, aliyemsaidia wakati wote, walikuwa chanzo cha kitia-moyo kwa akina ndugu, si chini ya mnyanyaso tu bali pia baadaye katika nyakati za baada ya vita.

Yeye alitumika kwa uaminifu mpaka kifo chake katika Septemba 2, 1975. Yeye hakudai kuwa wa baki la warithi-washirika wa Kristo, bali alionyesha uthamini wenye kina kirefu kwa “mtumwa mwaminifu mwenye akili” na alishirikiana naye kuangalia kazi katika Austria katika pindi ya nyakati ngumu sana.—Mt. 24:45.

Kutumia “Chakula” Haba

Wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya vita, kazi ya Mashahidi wa Yehova karibu ilemazwe kabisa katika sehemu iliyo kubwa ya Austria. Akina ndugu katika miji mbalimbali na vijiji waliweza kukutana pindi kwa pindi tu. Tahadhari kubwa ilitakwa.

Hata hivyo, katika Klagenfurt, utendaji wa kitheokrasi ulikuwa ukiendelea, inaonekana vizuri zaidi ya penginepo pote. Ndugu Ganster alimpa Peter Vajvoda fasihi aliyopokea, naye alikuwa akinakili kila toleo la Mnara wa Mlinzi. Wakati mmoja, Ndugu Ganster alichukua matoleo kadhaa ya Mnara wa Mlinzi, yakiwa yamefichwa vizuri mwilini mwake, akatembea kutoka Klagenfurt kwenda Krumpendorf (zapata kilometa 7) kuzuru jamaa ya Platzer na Dada Wanderer. Naye ni nani aliyepata kuwa akitembea kuelekea upande ule ule? Ofisa wa Gestapo, yule aliyekuwa akimhoji kwa ukawaida. Lakini ofisa huyo hakushuku lolote, nao wakatembea pamoja. Ingawaje, usikosee, hiyo haikuwa rahisi kwa Ndugu Ganster kufanya.

Katika Vienna urudufishaji wa Mnara wa Mlinzi huko ulikuwa umekoma wakati Ndugu Gölles alipotiwa mbaroni. Lakini akina ndugu walipokea chakula cha kiroho mara kwa mara kwa njia ya ndugu mmoja kutoka Uswisi aliyekuwa na kazi ya kimwili iliyomtaka asafiri Vienna. Akitumia uangalifu unaofaa, alileta pamoja naye nakala za Mnara wa Mlinzi. Ndugu mmoja alipopokea mojapo magazeti hayo, hakuruhusiwa kujiwekea mwenyewe. Kwa kuwa hakukuwa na nakala nyinginezo kwa ajili ya ndugu wengine, alikuwa akiisoma mara hiyo na kisha kuipitisha kwa ndugu mwingine anayestahiki kutumainiwa, si yeye binafsi, bali ikiwa imefungwa katika kikapu cha kununulia bidhaa au kitu kinginecho. Hivyo, vipande hivyo vyenye thamani kubwa sana vya fasihi vilifuliza kwenda kutoka mkono mmoja hadi ule mwingine. Chakula hicho cha kiroho kilikuwa cha umaana mkubwa kwa akina ndugu chini ya hali hizo zenye majaribu.

Wachache Warudi Nyuma

Ili kuvunja ukinzani wa akina ndugu na kuwavuta watie sahihi julisho-wazi likikana uhusiano wowote na Mashahidi wa Yehova, Gestapo walidai kwamba ndugu wengi walikuwa tayari wametia sahihi na walikuwa wameachiliwa. Huko kulikuwa kutia chumvi kubaya sana.

Gestapo waliaahidi kwamba kila mmoja aliyetia sahihi angewekwa huru na hivyo angejiepusha na miaka mingi ya kuteseka. Lililomaanishwa kwa kweli ni kwamba angebadilisha mateso ya kimwili na miaka mingi ya mateso ya dhamiri. Kwa wazi suala lilihusu ushikamanifu kwa Yehova na tengenezo lake. Walio wengi sana wa akina ndugu walikuwa wasioyumbayumba katika ukamilifu wao. Hata hivyo, walikuwako baadhi yao waliotia sahihi. Lakini si wote wa hao waliotia sahihi waliwekwa huru kikweli; kwa kawaida walibaki chini ya ulinzi wa daima.

Siku moja Agnes Hötzl alikuta wenzi wa ndoa katika Vienna ambao walikuwa wamekuwa katika kambi ya mateso kwa sababu ya ukweli. Hata hivyo, yeye hakujua hali ya kuachiliwa kwao. Akawasalimu, akijawa na shangwe. Bila kutamka neno moja, walimpita kana kwamba alikuwa mtu wasiyejua kabisa. Sasa akatambua jambo lililokuwa limetukia. Katika pindi nyingine yeye alikuwa karibu na mwingilio wa kiwanda kilichokuwa karibu na nyumba yake. Yeye hangeweza kuamini macho yake: Kifuani pa mmoja aliyedhani alikuwa ndugu, palikuwa na swastika! Yeye, pia, akampita, akitenda kwa hofu kana kwamba hakuwa anamjua. Hayo yalikuwa mapigo makali kwa waaminifu, lakini hiyo haikupunguza upendo wao mshikamanifu kwa Yehova na kwa wengine wa ndugu zao washikamanifu.

Kuvumilia Mateso ya Kambi

Katika 1939 Alois Moser wa Braunau na Josef Buchner wa Ranshofen, pamoja na ndugu wengine 142, walihamishwa kutoka kambi ya mateso ya Dachau kupelekwa kambi ya Mauthausen katika Austria ya Juu. Walipowasili Mauthausen karibu usiku wa manane na wakashuka kutoka magari ya ng’ombe ya reli, waliambiwa hivi: “Mauthausen si hospitali ya kutunzia wagonjwa kama Dachau. Sisi tutawamaliza nyinyi nyote.” Kulingana na makadirio, kutoka Agosti 1938 mpaka Mei 1945, jumla ya watu 206,000 walitiwa gerezani humo, na kulingana na rekodi, 35,270 wakafa.

Kwa miaka mitatu ya kwanza, ndugu zetu wote, bila kuacha hata mmoja, walifanyizwa kazi ngumu ya kimwili katika chimbo la mawe. Wakati wa kipupwe hali ya hewa ilikuwa baridi kupita kiasi. Mamia ya wafungwa kwa kweli waligandamana mpaka kufa katika chimbo la mawe. Wafungwa waliporudi kwenye kambi usiku, kila mmoja wao alilazimika kubeba jiwe kubwa kupanda “zile ngazi za kifo” 186 kuingia ndani ya kambi. Spatzenegger, yule kiongozi mwenye amri alitoa amri kwamba mawe yaliyo chini ya kilo 10 yalikuwa mepesi mno. Yeye aliamuru mawe ya kilo 40 au zaidi yawekelewe wafungwa, ambao wengi wao walizirai kwa kuishiwa nguvu kabisa. Mara nyingi, wale waliozirai waliuawa papo hapo.

Hatimaye Ndugu Moser na Buchner walipewa mgawo wa kukokota sleji (kigari kisicho na magurudumu) ambayo juu yayo miili mifu iliyo uchi kutoka sehemu mbalimbali za kambi iliwekwa. Kila maiti ilitambulishwa kwa kibandiko kilichokuwa na jina na nambari ya mfungwa kikiwa kimefungiliwa kwenye kidole kikubwa cha mguu. Mgawo huo uliwaleta kwenye makao ambamo sana-sana wafungwa waliotaabishwa na ugonjwa wa kuhara waliwekwa. Kwa fadhaa yao kubwa, walimpata August Kraft humo. Mateso hayo yote na ile hali mbaya sana ambamo walijikuta ilifanya hawa ndugu wawili watiririshe machozi. Lakini badala ya hivyo, Ndugu Kraft alikuwa akifikiria baraka ambazo alikuwa ameshangilia kutoka mkono wa Yehova, naye akasema: “Mimi nashukuru Yehova kwa kila kitu!” Kesho yake, Ndugu Kraft, pia, akawa analalia sleji ile, akiwa amekuwa akidumu katika kufuatia ule mradi wa “tuzo la mwito wa kuelekea juu” mpaka mwisho.—Flp. 3:14, NW.

Kwa upendo akina ndugu waliangalia masilahi ya mmoja na mwenzake. Wakati wengine walipokuwa dhaifu hasa, wale wengine walikuwa wakiwapa vijiko vichache zaidi vya milo yao haba kuwasaidia wajipatie tena nguvu iliyohitajiwa.

Utendaji wa Kitheokrasi Ndani ya Zile Kambi

Mle mle ndani ya zile kambi, utendaji wa kitheokrasi uliendelea, lakini kwa hadhari nyingi sana. Ushuhuda ulitolewa, mafunzo ya Biblia yaliongozwa, mikutano fulani iliendeshwa, na watu wachache walibatizwa.

Franz Desch alihamishiwa si mbali sana na Mauthausen kwenye kambi ya mateso ya Gusen. Yeye aliweza kujifunza Biblia na ofisa mmoja wa SS humo. Ni maendeleo kadiri gani yaliyofanywa? Basi, wazia shangwe kubwa ya wote wawili wakati, miaka mingi baadaye, walikutana wakiwa ndugu kwenye mkusanyiko!

Wafungwa wapya waliletwa ndani kutoka nchi nyingi mbalimbali. Ili kushiriki ukweli wa Ufalme pamoja nao, akina ndugu walitumia kadi za kutolea ushuhuda zilizoandikwa kwa lugha hizo. Kwa kuwa wafungwa waliruhusiwa kupokea barua, wale askari-walinzi wa SS walioingia makao ya wafungwa bila kushuku hawakung’amua kwamba wanaume hao hawakuwa wakisoma barua.

Katika kambi ya Gusen, kiwanda cha mtengeza-kufuli kilisimamiwa na Ndugu Karl Krause. Nacho kilikuwa kiwanda kisicho na kifani kama nini! Si kwamba tu kufuli ziliundwa na zikatengenezewa mahali hapo bali pia Wapolandi watano walibatizwa hapo kisiri-siri katika hori la mti lililotengenezwa hasa kwa kusudi hilo.

Ili kudumu wakiwa imara kiroho, akina ndugu walikuwa wakikutana katika vikundi vidogo usiku kuzungumzia maandiko ya Biblia. Pindi kwa pindi hata walipata Biblia. Kisha iligawanywa sehemu sehemu, ambazo zilipitishwa kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine. Wakilala chini ya vitanda vyao, walikuwa wakisoma katika wakati mdogo wa uhuru waliokuwa nao.

Akina ndugu hata walifaulu kuadhimisha Mlo wa Bwana wa Jioni. Wakiweza kupata mifano, walikusanyika wakati kila mtu mwingineye yote alipokuwa analala. Vyumba vya bafu na vyoo katika Gusen vilikuwa katikati ya makao ya wafungwa, kwenye umbali wapata meta 6. Katika chumba cha bafu kama hicho, kwa nuru ya mshumaa, waliadhimisha Ukumbusho. Chini ya ulinzi wenye upendo wa Yehova, kila kitu kilienda vizuri.

Rekodi ya Uaminifu

Maono mengi zaidi yangeweza kusimuliwa kuwa vielelezo vya uaminifu wa ndugu zetu wakati wa utawala wa Nazi juu ya Austria. Yale yaliyosimuliwa hapa yanawekwa kuwa tu vielelezo vya magumu yaliyovumiliwa na ule ushikamanifu usiovunjika ulioonyeshwa.

Kabla ya vikosi vya Hitla kuingia Austria, walikuwako wahubiri 549 katika nchi hii. Kwa ujumla, baada ya hapo 445 walitiwa gerezani kwa vipindi mbalimbali. Kati ya 1938 na 1945, 48 wa hao, kutia baadhi ya dada zetu, waliuawa. Kumi na watatu walipigwa mpaka kufa, wakauawa kwa gesi, au wakafanywa majeruhi wa majaribio ya kitiba yenye upotovu. Angalau wengine 81 walifia gerezani na kambi za mateso kwa sababu ya magonjwa au kuishiwa nguvu.

Takwimu hutumiwa inapohitajiwa kabisa wakati wa kusimulia habari za majeruhi wa pindi hiyo maalumu ya huzuni. Lakini hizo ni zaidi sana ya hesabu zisizo na hisia. Kila mmoja alikuwa ndugu au dada Mkristo, mume au mke pia, baba au mama, mwana au binti. Kwenye ile rekodi iliyofanyizwa kwa muda wa maelfu ya miaka na mashahidi waaminifu wa Yehova, hawa wameongezea ushuhuda wao kwamba upendo kwa Yehova husukuma watumishi wake waaminifu walaze chini hata uhai wao, ikihitajiwa kabisa, kuthibitisha ushikamanifu wao kwake akiwa Mungu na Mwenye Enzi Kuu wao.

Tutafanya Nini Kwanza?

Vita na utawala wa Nazi juu ya Austria vilikoma katika masika ya 1945. Upesi ndugu na dada zetu wakaanza kurudi kutoka kambi za mateso. Jambo la kwanza lililokuwa akilini mwao lilikuwa kufanya ushirika na wale ndugu wengine. Ingawa ilichukua jitihada kubwa kupangia mikutano tena, katika Julai 21, 1945, walikuwapo 27 kwa ajili ya mkutano wa kwanza uliopangwa kitengenezo baada ya vita katika Klagenfurt. Kufikia vuli, mikutano ilikuwa ikifanywa katika Vienna pia.

Ndugu waaminifu waliendelea kupanga kazi tena kitengenezo. Katika Vorarlberg, mkoa wa magharibi zaidi wa Austria, ndugu kadhaa walikutana pamoja na Franz Zürcher, Georg Gertz, na David Wiedenmann, wote kutoka ofisi ya Bern, Uswisi, wakazungumzia hatua zilizohitaji kuchukuliwa kuwezesha mikutano na kazi ya kuhubiri ianze tena. Kutoka Austria, Peter Gölles, Felix Defner, Leopold Pitteroff, na Franz Ganster walikuwapo. Ijapokuwa yale maono magumu ya miaka ya vita, tunda la Ufalme lilianza kujidhihirisha. Wale wahubiri 549 wenye kutenda katika 1937 waliongezeka katika hesabu kufika wapiga mbiu ya Ufalme 730 kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1946.

Baada ya kurudi kwake kutoka gereza, Peter Gölles alikuwa mwangalizi wa tawi wa kwanza wa Austria baada ya vita. Chumba chake katika Vienna, kwenye Florianigasse 58, kilikuwa ndicho ofisi ya tawi. Kisha, tokea Aprili 1947 na kuendelea, kazi ya ofisi ilifanyiwa katika jengo la shule, moja ambalo lilikuwa limeharibiwa vibaya sana na mabomu. Akina ndugu walirudufisha Mnara wa Mlinzi na pia vijitabu vyapata 4,000 humo. Therese Schreiber, aliyekuwa ametiwa gerezani kwa ajili ya sehemu yake katika kurudufisha fasihi ya Biblia, alikuwa amerudia kazi ile tena, akishiriki kazi ya kurudufisha. Katika Klagenfurt akina ndugu hata walirudufisha kitabu chote kizima cha Children (Watoto) na kukitia katika jalada gumu. Karatasi na wino vilikuwa haba na vigumu kupatikana, lakini, kwa msaada wa Yehova, akina ndugu waliweza kupata walivyohitaji.

Mwaka 1947 uliandaa fursa kwa ajili ya akina ndugu kushangilia mkusanyiko wao wa kwanza wa baada ya vita. Uliendelea kwa siku nne. Hudhurio la 1,700 huenda likaonekana kama dogo linapolinganishwa na mikusanyiko inayofanywa sasa, lakini lilikuwa umati mkubwa kwa akina ndugu Waaustria wakati huo, nalo lilitoa ithibati kwamba ulikuwako uwezekano wa ukuzi mwingi.

Baadaye mwezi huo, Jumamosi, Juni 21, hatua nyingine ya maana ilichukuliwa kuhusiana na kupanga kazi tena kitengenezo. Ndugu saba walikutana katika shule moja kupanga tena kitengenezo shirika la nchini la “Wachtturm-Gesellschaft, Zweigstelle der Watch Tower Bible & Tract Society, Brooklyn, N.Y.” Hivyo, chombo cha kisheria kwa ajili ya kutangaza fasihi kwa kupiga chapa kilipatikana tena.

Kisha—Siberia!

Mpaka Mei 1955, Austria ilikaliwa na vikosi vya Mataifa Mafungamani (U.S.A., Ufaransa, Uingereza, na Urusi) nayo iligawanywa kuwa kanda nne za kukaliwa. Kijiji cha Deutsch Wagram kilikuwa katika kanda ya Urusi. Ndugu Franz Malina aliishi huko. Yeye alijua kusema Kirusi, naye alitolea vikosi vya ukalizi ushuhuda kwa njia ya wazi sana, hata akawa akiongoza mafunzo ya Biblia pamoja na baadhi ya wanaume hao. Pia yeye alipata fasihi ya Biblia katika Kirusi na kuigawanya miongoni mwa askari-jeshi hao.

Utendaji wake haukukosa kuonwa. Mapema katika 1948 wanaume wawili waliokuwa na nia nzuri kumwelekea walimwonya hivi: “Franz, ondoka hapa; wanataka kukutia mbaroni. Kulikuwako fasihi yako ambayo Warusi walipatikana wakiwa nayo.” Lakini Ndugu Malina hakukimbia. Yeye aliamua kukaa pamoja na mke wake mgonjwa na watoto. Hata hivyo, haikuwa muda mrefu kabla ya yeye kutiwa mbaroni. Alizuiliwa kwa siku nane katika ofisi ya mahali hapo ya kamanda wa Urusi na hatimaye akahamishiwa kitovu cha wafanya kazi wa jeshi la Urusi. Wakati wa yale majuma sita aliyolazimika kutumia huko, aliwahubiria waziwazi askari-jeshi na maofisa pia, akiwaambia juu ya Ufalme wa Yehova. Mwishowe alihukumiwa miaka kumi ya kazi ngumu ya kulazimishwa kwa lile shtaka ambalo sasa linasikika kuwa lajulikana la ‘kuvunja vikosi moyo’ naye akapelekwa mbali sana Siberia.

Hatimaye akawasili katika lile eneo kubwa mno nyuma ya Milima Ural. Akiwa huko alienda kutoka kambi moja hadi nyingine, sana-sana kwa miguu. Ilikuwa haiwezekani kutoroka. Katika karibu kambi zote yeye alikuta akina ndugu kutoka sehemu mbalimbali za Muungano wa Urusi. Alipowasili katika kambi mpya, kama kawaida alikuwa akiwatafuta. Na alipowapata akina ndugu, walimtahini kuamua kama yeye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova kikweli. Walifanya hivyo kwa kumuuliza maswali kama vile: “Jamaa ya Yonadabu i hali gani?” na “Ni nani msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi?”

Wakiwa wamesadikishwa kwamba kwa kweli alikuwa ndugu, walimsaidia kwa upendo avumilie yale maisha makali, asiyozoea katika zile kambi. Kwa sababu ya umri wake aliitwa Baba. Katika muda wa miaka mitano, yeye alipata kujua kambi 30. Ndipo katika 1953, alipewa msamaha akarudi nyumbani. Kwa wakati uliopo mke wake alikuwa amekufa, naye binti yake mwenye umri mkubwa zaidi alikuwa amechukua daraka la kuwa mama. Je! Ndugu Malina sasa alivunjwa moyo? Tofauti kabisa na hivyo, katika muda wa siku chache tayari yeye alishika njia yake tena akihubiri habari njema nyumba kwa nyumba. Aliendelea kufanya hivyo mpaka kifo chake katika 1964.

Mapainia Washiriki Vuno

Wakati wa miaka mingi tangu Vita ya Ulimwengu 2, upanuzi mwingi katika kazi ya watu wa Yehova umetukia katika Austria. Mchango mkubwa katika ukuzi huu umefanywa na mapainia, mapainia wa pekee, na wamisionari wenye juhudi.

Miongoni mwa wafanya kazi hao wenye bidii ni Hans Rothensteiner na mke wake. Katika muda wa mwaka mmoja kutoka wakati walipopata ukweli kwa mara ya kwanza, walianza kupainia. Katika 1955 waliwekwa rasmi kuwa mapainia wa pekee. Mmojapo migawo yao ulikuwa eneo lenye kuzunguka Kaprun katika sehemu ya alpino. Hans anasimulia ono hili lifuatalo walilopata huko:

“Kwa mioyo yenye kuthamini, sisi tulianza kazi ya kutafuta kondoo za Bwana. Na hivyo, tulipata jamaa moja katika Walchen ambayo tayari ilikuwa imepokea fasihi fulani. Funzo lilianzishwa mara moja na jamaa nzima; pia walialika baadhi ya marafiki wajiunge nasi. Nyakati nyingine kufikia watu 12 walikuapo. Funzo liliendelea vizuri sana—vizuri sana hivi kwamba upesi jamaa hizo ziliamua kuliacha kanisa. Hata hivyo, ili kufanya hivyo, walihitaji hati zao za ubatizo. Kwa hiyo Lois, mmoja wa hao watu wenye moyo mzuri, akaenda kwa padri kupata hati zile kwa ajili yao wote. Kwa kuwa walikuwako watoto wengi katika jamaa hizi, walihitaji hati 17 zote pamoja.” Mazungumzo aliyokuwa nayo Lois pamoja na kasisi wa mahali pale yalienda kama hivi:

Lois: Habari za asubuhi. Mimi nahitaji hati chache za ubatizo.

Padri: Unamaanisha nini kwa kusema “chache,” na unazihitaji kwa nini?

Lois: Kwa sababu sisi tunataka kuliacha kanisa.

Padri: Oh, mwataka? Na wataka hati ngapi?

Lois: Niliandika. Oh, ndiyo, iko hapa; nahitaji 17 tu.

Padri: Nini? Ni nini kimetukia hivi kwamba wengi wenu sana hivyo mwataka kuliacha kanisa?

Lois: Eeh, sisi tumejifunza Biblia. Ni hivyo tu. Waona, wewe ulikuwa ukitufundisha mambo mengi ambayo si kweli hata kidogo, mambo ambayo wala Yesu wala Biblia haikusema!

Mazungumzo haya yaliendelea kwa muda, naye Lois akaondoka bila hati zile. Hata hivyo, katika tarehe ya baadaye, mazungumzo yalitukia pamoja na kasisi huyo wakati Hans alipokuwapo pia. Mwishoni mwayo, Lois alimwambia yule padri hivi: “Sasa, hukuweza kuthibitisha kabisa jambo lolote, na sasa zitoe hizo hati za ubatizo, lakini haraka zaidi, tafadhali.” Kasisi huyo hakuwa na la kufanya ila kukubali.

Sasa kuna kundi la wahubiri 90 katika kijiji hiki cha alpino.

Katika 1978, kotekote nchini kulikuwako 626 waliokuwa wakishangilia baraka za utumishi wa painia kutia mapainia wasaidizi 278. Lakini katika Aprili wa 1988, hesabu ya waliokuwa wakiripoti utumishi kama huo ilikuwa imeinuka kufika 1,925, kutia mapainia wasaidizi 1,102.

Mipango ya Tawi

Katika Agosti 1, 1965, Lowell L. Turner, ambaye alikuwa amehitimu karibuni kutoka mtaala wa mazoezi ya pekee ya miezi kumi ya kitengenezo ya Shule ya Gileadi, alipewa mgawo wa madaraka ya mwangalizi wa tawi. Baada ya karibu miaka kumi katika mgawo wake wa uangalizi, Ndugu Turner aliondoka Austria katika Julai 1975 kwenda kwenye mgawo mpya katika Luxembourg. Tangu Januari 1976 halmashauri ya ndugu kadhaa imekuwa ikiangalia tawi katika Austria.

Upanuzi wa Vifaa vya Tawi

Ofisi za tawi za Sosaiti kotekote ulimwenguni zimekuwa zikiongezea ukubwa wa vifaa vyazo kuangalia mahitaji yanayokua daima ya wasifaji wa Yehova. Je! imekuwa tofauti kwa vyovyote katika Austria? Kwa uhakika sivyo.

Baada ya wakati kupita lile jengo lililonunuliwa katika 1957, lililoko kwenye mojapo wilaya za bustani za Vienna, likawa dogo mno kwa ajili ya ofisi ya tawi. Hivyo katika wakati wa miaka ya 1970 na 1971, liliongezewa ukubwa ili kuandaa nafasi zaidi kwa ajili ya Idara ya Upakizi na kwa ajili ya Jumba la Ufalme. Lakini katika muda wa miaka michache, uhitaji wa upanuzi zaidi ukawa wazi. Mkono wa Yehova katika jambo hilo ulihisiwa wakati mmojapo majirani alipotoa kisehemu chake cha ardhi kinunuliwe. Wakati ujenzi wa majengo mapya ulipokuwa ukiendelea katika 1983, kiwanja kingine cha ardhi kinachoshikana na tawi kilitolewa ili tawi likinunue. Kwa kuwekwa wakfu kwa vifaa hivyo vipya katika kiangazi cha 1987, meta za mraba 5,000 zaidi za nafasi zikawa zinapatikana, ambazo ziliongeza zaidi ya mara nne nafasi iliyokuwako kabla ya hapo. Je! yote hayo yalihitajiwa kabisa kikweli? Hesabu ya Mashahidi waliokuwa wakitumikiwa na ofisi hii ilikuwa tayari imeongezeka ikawa mara tatu tangu lile jengo la hapo kwanza liliponunuliwa, na akina ndugu ofisini walikuwa wakifanya kazi katika makao yenye kusongamana sana.

Kabla ya mradi huo kukamilishwa, marekebisho mengi katika ramani ya vifaa hivyo yalihitajiwa ili kutimiza malalamiko ya majirani. Hilo lilitaka kazi nyingi sana ya ziada. Hata hivyo, ofisi ya tawi inakiri hivi: “Mwishowe, karibu mabadiliko yote yaliyohitajiwa kabisa yalithibitika kuwa kwa manufaa yetu. Katika visa vingi, iliwapasa akina ndugu kukubali hivi: ‘Sasa ni zuri zaidi ya vile tulivyolikusudia hapo mbele.’”

Eneo Lenye Lugha Nyingi

Si kila mtu anayeishi katika Austria aliye Mwaustria kikweli. Na si kila mtu anayeishi hapa anayeweza kusema Kijeremani kwa ufasaha, ambayo ndiyo lugha kubwa ya Austria. Kuna wafanya kazi wengi wageni hapa kutoka Yugoslavia na kutoka Uturuki. Tangu miaka ya mapema ya 1970, tawi limefanya mipango kufikia wafanya kazi hawa wageni kwa ujumbe wa Biblia. Mbegu ilianguka katika udongo wenye rutuba, na upesi iliwezekana kufanyiza vikundi vya funzo.

Sasa makundi tisa hufanya mikutano yao katika Serbo-Kroati tu (mojapo lugha kubwa zinazonenwa katika Yugoslavia). Pia kuna vikundi vya funzo katika Kituruki, Kihispania, Kipolandi, Kijapani, Kiingereza, na Kiarabu. Ndugu Letonja, anayetumikia katika Betheli ya Vienna pamoja na mke wake na ambaye kazi-maisha yake ya kitheokrasi ni ya tarehe ya kurudi nyuma miaka 50, anatusimulia jambo fulani juu ya kazi miongoni mwa hao wafanya kazi wageni:

“Katika 1971, mimi nilipewa mgawo nijiunge na wale ndugu watano waliokuwa wakihubiri habari njema kwa wafanya kazi wageni Wayugoslavia. Kwa kusudi hili mimi nilijifunza kunena lugha ya Serbo-Kiroati. Leo, katika 1988, kuna wahubiri zaidi ya 320 katika Vienna na viunga vyalo ambao ni wa kikundi cha lugha ya Serbo-Kiroati. Inaleta shangwe sana kufanya kazi pamoja na ndugu hawa. Wao wanafikiria sana jamaa. Bidii yao kwa ajili ya ukweli inavutia, nao hutiana moyo. Wengi wao hubaki katika utumishi siku nzima mpaka saa za jioni-jioni. Zijapokuwa hali ngumu za kufanya kazi za wafanya kazi wageni, hesabu kadhaa yao hufanya utumishi wa painia msaidizi kwa ukawaida. Mazungumzo yao yenye idili huwa sana-sana juu ya ukweli.

“Pia kuna hesabu kubwa ya Wagipsi miongoni mwao, ambao kwao kundi ni kama nyumbani. Angalau washiriki 25 kutoka jamaa moja ya Gipsi tayari wamezamishwa na zaidi ya watu wa ukoo wengine 19 wanapendezwa na ukweli. Ni baraka kweli kweli kufanya kazi pamoja na ndugu hawa.”

Kuwa Wakaribishaji Kwenye Mkusanyiko

Katika pindi ya nyakati ngumu wakati uliopita, sisi tulioko Austria tulivuka mpaka mara nyingi kuhudhuria mikutano ya kundi na makusanyiko makubwa zaidi. Sisi twakumbuka vizuri ule ukaribishaji wa upendo tulionyooshewa na akina ndugu katika maeneo tulikokwenda. Sasa wale walioko Austria wana fursa ya kuchukua zamu yao kuwa wakaribishaji.

Kwa kweli ilianza katika 1965, wakati kina rafiki 1,200 kutoka Ugiriki walipokuja kwenye mkusanyiko wa wilaya katika Vienna. Mipango ilifanywa ili wawe na programu nzima katika Kigiriki upande mwingine wa jengo lililotumiwa kwa ajili ya kusanyiko.

Kisha katika 1967 walikuwako ndugu 889 kutoka Yugoslavia waliohudhuria kusanyiko la wilaya katika Klagenfurt, kusini mwa Austria. Wao, pia, waliweza kushangilia programu katika lugha yao wenyewe. Hesabu ya waliokuja kutoka Yugoslavia iliongezeka. Katika 1968 hudhurio kwenye vipindi walivyopangiwa katika Villach lilikuwa 2,319.

Kwenye mikusanyiko yetu ya wilaya katika 1978, lilikuwa pendeleo letu kupanga kutoa programu katika Kihangari pia. Kwa kuwa wazee wachache ambao lugha yao asilia ni Kihangari huishi katika Austria, haikuwa vigumu sana kupangia sehemu hizo. Hata hivyo, majuma kadhaa kabla ya mkusanyiko ndugu wenye daraka la mambo ya kitengenezo walishangaa wakataka kujua hivi: ‘Je! ndugu kutoka Hangari wataweza kuvuka mpaka ili kuhudhuria mkusanyiko?’ Lilikuwa sisimuko kama nini wakati hudhurio kwenye programu ya Kihangari lilipopita alama ya 400! Tangu hapo, mikusanyiko yetu ya wilaya katika eneo la Vienna karibu sikuzote imetia ndani programu katika Kihangari. Katika 1986, kwa shangwe kubwa ya kila mtu, hesabu katika hudhurio kwenye vipindi hivyo iliinuka kufikia 1,781. Je! kulikuwako wengine ambao tungeweza kunyooshea ukaribishaji?

Namna Gani Ndugu Kutoka Polandi?

Kichwa cha mkusanyiko wa 1980 kilikuwa “Upendo wa Kimungu.” Ni kitu gani kingekazia hilo vizuri zaidi ya kuwapo kwa ndugu na dada 1,883 kutoka Polandi, wakisikia programu katika lugha yao wenyewe katika Vienna? Hema kubwa lilikipa makao kikundi cha Polandi, hali jumba moja kwa kila lugha lilitengwa kwa ajili ya vipindi katika Kihangari na Kikroati. Kwa ajili ya programu katika Kijeremani, Stediamu ilikodishwa mahali pale pale.

Mwenyekiti msaidizi wa mkusanyiko alifanya dokezo hili: “Ingekuwaje ikiwa, Jumapili, akina ndugu wa vile vikundi vingine vya lugha wangekuja kwenye stediamu pia kwa ajili ya wimbo wa mwisho?” Ofisi ya mkusanyiko ilikubali kwa idili.

Piga picha tu akilini mwako tamasha hii mwishoni mwa mkusanyiko: Upande mmoja wa stediamu walikuwako wajumbe 5,000 Waaustria—mbele yao kukiwa uwanja wa michezo wenye manyasi rangi chanikiwiti nyangavu. Tangazo likafanywa, ndipo miinuko iliyo upande mwingine wa stediamu ikaanza kujaa. Wakijipanga kulingana na vikundi vya lugha, akina ndugu wakaingia ndani na kusimama—Wayugoslavia, Wahangari, Wapolandi. Halafu, baada ya ishara kutolewa katika lugha nne, sauti karibu 8,000 zikaungana katika wimbo mmoja wa sifa: “Asante, Yehova.”

Ndipo yule ndugu aliyetoa maneno ya kumalizia akasema na akina ndugu kutoka Polandi: “Ikiwa, wakati utakaofuata, nyinyi mtakuwa wengi zaidi ya sisi kwenye programu ya Kijeremani, basi sisi tutawaachia nyinyi stediamu!” Baada ya programu kumalizika, akina ndugu hawakuachana kwa wakati mrefu. Ulikuwa mkusanyiko ambao ulivuta sana mioyo, na ukawatolea akina ndugu katika pande zote mbili za mpaka mengi ya kuzungumzia kwa wakati mrefu. Ikijawa na furaha ya kina kirefu, baadaye ofisi ya tawi iliandikia Baraza Linaloongoza hivi:

“Lilikuwa jambo ambalo ilikupasa ujionee. Ni wonyesho wenye kujaa nguvu kama nini wa kani yenye kuunganisha ya roho ya Yehova na ‘Upendo wa Kimungu’ wake. Hata muda mrefu baada ya wimbo kumalizika, akina ndugu walipungiana mikono. Hakuna mtu aliyetaka kuondoka. Ndugu mmoja alieleza hisia za wengi wa akina ndugu wakati aliposema: ‘Hili limekuwa ndilo kusanyiko la wilaya langu la kumi; hata hivyo, mimi sijapata kamwe ono lolote lililo kama hili, uchangamfu, weupe wa moyo, na shauku nyororo kama hiyo ya vifungo vya umoja. Mimi ningetaka kunyoosha mikono yangu na kuwakumbatia wote. Katika maana ya kiroho mimi nimefanya hivyo.’”

Mwaka ule ule uliofuata, 1981, matayarisho kwa ajili ya “Ushikamanifu kwa Ufalme” Mkusanyiko wa Wilaya yalipokuwa yakifikia hatua yayo ya mwisho, jambo moja lilikuwa wazi—wakati huu, tungeachia stediamu akina ndugu zaidi ya 5,000 kutoka Polandi. Na kwa mara nyingine tena akina ndugu katika Vienna na maeneo yanayozunguka walithibitika kuwa wakaribishaji wenye mioyo iliyofunguka.

Kwa kuongezea, kulikuwa na utajirishaji mwingine kwa kusanyiko hilo; Ndugu Theodore Jaracz na Daniel Sydlik wa Baraza Linaloongoza walikuwa wamekuja Vienna. Ilikuwa fursa nzuri kama nini kwao kushirikiana na akina ndugu kutoka Hangari na Polandi! Hotuba zao zenye kutia-moyo na wonano wa kirafiki, na uchangamfu wa kibinafsi pamoja na akina ndugu wa vikundi vyote vya lugha ulithaminiwa sana sana. Katika sehemu yake ya programu, Ndugu Sydlik alizungumza juu ya Barnaba, mwanafunzi Mkristo. Akina ndugu walisikiliza kwa makini sana. Baada ya maneno machache, msemaji na wasikilizaji walikuwa “moyo mmoja na nafsi moja,” kama mithali isemavyo katika Austria.

Tangu 1982 ndugu zetu katika Polandi wameweza kuwa na mikusanyiko yao wenyewe, lakini akina ndugu katika Austria huendelea kushangilia kuwa wakaribishaji kwa ndugu zao kutoka Hangari.

Kusonga Mbele Kuingia Ndani ya Wakati Ujao

Katika Austria kwa kawaida mambo huchukua mwendo wayo “kistarehe,” kama isemwavyo. Lakini hivyo sivyo ilivyo kuhusu kupiga mbiu ya habari njema za Ufalme wa Mungu. Hakukupata kuwa na ukuzi wenye kutazamisha, lakini hesabu ya wasifaji wa Yehova imezidi tu kuongezeka. Huko nyuma katika miaka ya 1950, mwangalizi wa wilaya mmoja alitia akina ndugu moyo, akisema: “Haipasi kutushangaza ikiwa siku moja kungekuwa na wahubiri 10,000 katika Austria.” Hilo lilisikika kuwa lenye kupendeza. Lakini Austria ni taifa dogo, lenye wakazi milioni 7.5 tu. Na wakati huo hakukuwa na wahubiri zaidi ya 5,000 katika nchi yote. Hata hivyo, katika 1971 sisi tulipita tarakimu ya 10,000, na sasa umati wa wasifaji wa Yehova katika bara hili umeinuka kufika zaidi ya 17,000.

Austria inajulikana sana kuwa bara la milima na muziki. Hata hivyo, katika maisha ya umati unaozidi kukua, “mlima wa nyumba ya Yehova,” ile hadhi iliyokwezwa ya ibada ya kweli, ndio ulio na umaana mkubwa zaidi ya yote kwao. Na ile melodia tamu zaidi ya zote inayoweza kusikiwa katika bara hili hutoka kwa wale wahubiri 17,705 wanaoshiriki kuimba ule “wimbo mpya,” wimbo unaotukuza Ufalme wa Yehova.—Isa. 2:2, NW; Zab. 98:1, 4-6.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 72, 73]

Muhtasari wa Austria

Mji Mkuu: Vienna

Lugha Rasmi: Kijeremani

Dini Kubwa: Roma Katoliki

Idadi ya Watu: 7,575,700

Wahubiri: 17,705

Mapainia: 1,398

Makundi: 246

Hudhurio la Ukumbusho: 30,216

Ofisi ya Tawi: Vienna

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

AUSTRIA

Ziwa Konstanke (Bodensee)

Dornbirn

VORARLBERG

Innsbruck

TIROLI

Alps za Mashiriki

SALZBURG

Bad Ischl

Salzburg

AUSTRIA YA JUU

Linz

Mauthausen

Mto Danube

Vienna

AUSTRIA YA CHINI

Ziwa Neusiedler

BURGENLAND

STYRIA

Knittelfeld

Graz

KARINTHIA

Klagenfurt

USWISI

JAMHURI YA MUUNGANO YA UJEREMANI

CHEKOSLOVAKIA

HANGARI

YUGOSLAVIA

ITALIA

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 66]

[Picha katika ukurasa wa 69]

Hoteli Continental, Vienna, ambapo C. T. Russell alijaribu kunena, Machi 22, 1911

[Hisani]

Kutoka Pictorial Archive of the Austrian National Library

[Picha katika ukurasa wa 74]

Simon Riedler, kushoto, na Franz Ganster walisikia juu ya ukweli kwa mara ya kwanza katika 1921

[Hisani]

Kutoka Pictorial Archive of the Austrian National Library

[Picha katika ukurasa wa 79]

J. F. Rutherford alinena katika Katharinenhalle, Vienna, 1922

[Hisani]

Kutoka Pictorial Archive of the Austrian National Library

[Picha katika ukurasa wa 81]

Programu ya mkusanyiko wa kwanza wa Wanafunzi wa Biblia katika Vienna, 1924. Mkusanyiko uliofuata ulileta badiliko kwa Johannes Schindler

[Picha katika ukurasa wa 83]

Jamaa ya Heide, 1924, Mashahidi Waaustria wa mapema

[Picha katika ukurasa wa 87]

Emil Wetzel alisimamia kazi katika Austria kutoka 1922 hadi 1926

[Picha katika ukurasa wa 95]

Leopold Engleitner, aliyetiwa gerezani katika 1934 kwa ajili ya kuhubiri

[Picha katika ukurasa wa 99]

August Kraft, alitiwa mbaroni na wanazi, Mei 25, 1939. Elezo la kumalizia la hati ya Gestapo juu ya Kraft

[Hisani]

DÖW, Vienna, Austria

[Picha katika ukurasa wa 108]

Therese Schreiber, kushoto, alirudufisha fasihi, na Hansi Hron (Buchner) alikuwa tarishi. Wote wawili walitiwa mbaroni

[Picha katika ukurasa wa 109]

Hati za Gestapo zafunua maarifa mengi ya kujua juu ya kazi-tata ya kisiri-siri ya kurudufisha

[Hisani]

DÖW, Vienna, Austria

[Picha katika ukurasa wa 115]

Alois Moser, kushoto, alikuwa katika gereza na kambi za mateso saba; Johann Rainer alikataa kula kiapo cha kijeshi; Franz Wohlfahrt alidumisha ukamilifu hata ingawa baba yake na ndugu yake waliuawa

[Picha katika ukurasa wa 117]

Mwingilio kwenye kambi ya mateso katika Gusen. Waokokaji Mashahidi wa Mauthausen⁄Gusen, 1945

[Hisani]

DÖW, Vienna, Austria

[Picha katika ukurasa wa 120]

Josef Wegscheider, kushoto, na Johann Pichler walipigwa risasi wakafa, Septemba 26, 1939, karibu na Salzburg

[Picha katika ukurasa wa 124]

Hermine Obweger, kushoto, alichukuliwa kutoka kwa wazazi wake akiwa na umri wa miaka 11. Auguste Hirschmann (sasa Bender) alichukua msimamo mbele ya Gestapo akiwa na umri wa miaka 17

[Picha katika ukurasa wa 126]

Peter Gölles alitiwa mbaroni katika Juni 12, 1940. Alihukumiwa katika nyumba hii ya mahakama na akatiwa gerezani katika chumba cha nyumba hii

[Picha katika ukurasa wa 137]

Franz Malina, aliyetiwa gerezani kwa miaka mitano katika kambi za mateso katika Siberia

[Picha katika ukurasa wa 140]

Lowell L. Turner, mwangalizi wa tawi kutoka 1965 hadi 1975, na mke wake, Margot

[Picha katika ukurasa wa 141]

Ofisi ya tawi na Makao ya Betheli, 1957

[Picha katika ukurasa wa 142]

Tawi lililoongezewa ukubwa, 1987

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki