Ekwedori
KATIKATI ya dunia na hata hivyo mbali zaidi sana na kitovu chayo—yakaa Ekwedori ikitagaa ikweta. Misitu yenye kutoa sitimu katika sehemu za bara zilizo chini hutofautiana na “miji ya bubujiko la milele” iliyo juu sana kwenye Milima Andes yenye miamba-miamba. Mikondo miwili tofauti baharini katika Pwani ya Pasifiki hushindania zamu yayo ya kuhuisha bara. Ule Mkondo wa Peru wenye baridi hutawala toka Mei mpaka Desemba, ukiletea yale majimbo ya kati hali ya hewa baridi kidogo, lakini iliyo kavu. Halafu kutoka Januari mpaka Aprili, ule mkondo wenye joto uitwao El Niño hutawala, ukipuliza hari na joto, ingawa huburudisha bara kwa mvua mpya ya kimajira.
Watu wa Ekwedori wanatofautiana katika kila njia kama vile nchi wanamoishi. Miongoni mwa yale makabila mengi ya Kihindi, pengine wale wanaojulikana zaidi sana ni Wahindi wa Otavalo. Nywele zao zikiwa kwa kawaida zimesokotwa kwa namna ya mkia wa nguruwe, wanaume huwa wamevalia kofia nyeusi iliyotengenezwa kwa manyoya pamoja na poncho ya rangi nevi-bluu juu ya suruali na shati nyeupe. Baadhi yao husafiri ulimwenguni pote, wakiuza katika nchi za ng’ambo blanketi, shali, na poncho zao zilizofumwa. Kwa upande mwingine, Wahindi wa Kolorado huvalia kidogo sana. Wanaume wao hutambulishwa kwa nywele zilizonyolewa kwa umbo la bakuli, na kupakwa namna fulani ya udongo wa rangi-machungwa-nyangavu.
Kisehemu kingine chenye maana cha idadi ya watu, weusi, chaweza kufuatilia nasaba yao moja kwa moja mpaka Jameika na Afrika. Hispania, pia, iliacha alama yayo katika sura ya uso na michoro ya ujenzi pia kama tokeo la mavutano ya watiishaji-nchi waliokuja kutafuta dhahabu. Sasa, ongeza vikundi vikubwa vya Wanamashariki, wafanya biashara Wayahudi, Waarabu, na Wazungu, nawe utakuwa na Ekwedori ya leo. Hao ni watu wakaribishaji-wageni ambao kwa kawaida husalimu wengine kwa salamu ya mkono na tabasamu changamfu. Urafiki huo umesaidia wengi wao kukubali ujumbe ambao umetajirisha sana maisha zao.
Habari Njema Zaja Ekwedori
Ilikuwa kwanza katika 1935 kwamba angalau baadhi ya watu katika Ekwedori wakasikia habari njema za Ufalme wa Mungu. Mwaka huo, wawili wa Mashahidi wa Yehova wakiwa safarini kwenda Chile, Theodore Laguna na mwenzake, walitumia miezi kumi wakihubiri hapa. Kisha, katika 1946, wamisionari kutoka Shule ya Gileadi waliopewa mgawo kwenda Ekwedori wakawasili katika jiji-bandari la Guayaquil. Wao walikuwa Walter na Willmetta Pemberton pamoja na Thomas na Mary Klingensmith.
Baada ya kushughulikia mambo ya kikawaida ya kisheria yaliyohitajiwa, upesi hawa wamisionari wa kwanza wakashika njia yao kwenda Quito, mji mkuu, unaokalia uwanda wa juu wa majivu ya volkeno zapata maili mbili juu ya usawa wa bahari. Kwa kuwa hakuna barabara zinazopitika zilizoenda kwenye mwinuko huo, wao walichukua garimoshi kutoka Guayaquil kwenda Quito. Wakikumbuka safari yao, walisema hivi: “Sisi tulikuwa afadhali kwa kutolazimika kupanda juu ya paa au kuning’inia kwenye pande, kama wengi walivyofanya. Wengi walibeba ndizi, mananasi, na kuku wakauze mbele zaidi njiani.”
Ili kuweza kupanda mwinuko wa ghafula juu ya kile kilichoitwa Pua la Ibilisi, garimoshi lile lilipitia-pitia kwenye mfululizo wa sehemu ya reli yenye kupota, ikienda juu na kurudi chini. Ilionekana kwamba walikuwa wakipanda juu ya ukingo mwembamba uliochimbwa upande wa genge. Lile garimoshi lilikuwa likipanda kidogo mwinuko ule kuelekea upande mmoja, na kutua, na kisha kurudi kinyume-nyume kuelekea juu katika kile kisehemu kingine cha mpoto ule. Tendo hili lilirudiwa mara kwa mara mpaka wakafika juu. Baada ya siku mbili, usiku ulipokuwa ukikaribia, wakakaribia walikokuwa wakienda. Kwa kuvutiwa sana, walitazama vilele vya volkeno vyenye kufunikwa na theluji, kile chenye kuvutia zaidi kikiwa Cotopaxi—mojapo volkeno za ulimwengu zenye kutenda zilizoinuka juu zaidi, kimo cha meta 5,897.
Maisha ya kimisionari ya kweli yakaanza sasa. Ilikuwa lazima makao yakodishwe. Chakula kilinunuliwa kila siku kwa kuwa hakukuwa na frigi. Jiko lenye kutumia kuni lilitumiwa kwa kupikia. Nguo zilifuliwaje? Si kwa mashine ya kufua ya otomatiki. Makonzi pekee yalisugua nguo moja moja juu chini juu ya ubao wa kufulia. Lakini kama vile mmoja wa wamisionari alivyosema: “Mimi sikumbuki kwamba tulinung’unika sana. Sisi tuliendelea tu na kazi ya kuhubiri.”
Huu pia ulikuwa ushindani kwa kuwa walijua Kihispania kidogo sana. Ijapokuwa hivyo, wakiwa na imani katika Yehova wao walianza kwenda nyumba kwa nyumba wakitumia kadi ya kutolea ushuhuda, sahani za santuri, na lugha nyingi ya kutumia ishara waliyojibunia wenyewe. Matokeo mazuri yakafuata upesi.
Mwekwedori wa Kwanza Apata Ukweli
Jioni moja wakati Walter Pemberton alipokuwa akitembea katika barabara moja nyembamba katika Quito ili apeleleze eneo, kivulana mmoja alimkimbilia kumuuliza ni saa ngapi na kisha akakimbia tena kurudi ndani ya nyumba kupitia mlango mmoja. Alipotazama ndani, Walter alimwona mwanamume mmoja akitengeneza jozi ya viatu. Akiongea Kihispania kisicho kizuri sana, Walter alijijulisha, akimweleza mwanamume huyo kwamba yeye alikuwa misionari, na akamuuliza kama angependezwa na Biblia. “Hapana, lakini mimi nina ndugu anayependezwa sana,” likawa jibu. Ndugu ya mwanamume huyo alithibitika kuwa Luis Dávalos, Mwadventisti aliyekuwa ameanza kushuku sana dini yake.
Mapema asubuhi iliyofuata Walter akatembelea Luis. Walter anasimulia hivi: “Kwa maarifa yangu machache ya Kihispania, nilimweleza kusudi la Mungu la kufanya dunia paradiso ambapo aina ya binadamu ingeishi milele chini ya Ufalme wa Mungu.”
Kusikia hivyo, Luis akajibu: “Hiyo inaweza kuwaje? Yesu alisema kwamba yeye alikuwa akienda zake mbinguni akawatayarishie mahali.”
Walter alimwonyesha kwamba Yesu alifikiria kundi dogo na kwamba kundi hili dogo lilikuwa na hesabu yenye mpaka, 144,000. (Luka 12:32; Ufu. 14:1-3) Alimweleza pia kwamba Yesu alinena juu ya kondoo wengine ambao si wa zizi hili lakini ambao wangekuwa na tumaini la kuishi hapa duniani.—Yoh. 10:16.
“Mimi nimefundishwa maisha yangu yote kwamba watu wote wema huenda mbinguni,” akasema Luis. “Mimi nahitaji uthibitisho zaidi juu ya hiki kikundi cha kidunia.” Kwa hiyo waliangalia maandiko mengine pamoja, baada yayo Luis akapaaza sauti hivi: “Ni ukweli!”—Isa. 11:6-9; 33:24; 45:18; Ufu. 21:3, 4.
Luis alikuwa kama mtu anayekufa kwa kiu jangwani, lakini akitamani sana maji ya ukweli. Mara hiyo yeye alitaka kujua mambo ambayo Biblia ilifundisha juu ya Utatu, kutokufa kwa nafsi, moto wa mateso, na mafundisho mengine. Ni wazi, Walter hakuweza kuondoka mpaka jioni sana. Siku ile ile iliyofuata Luis alijishughulisha akiwatolea ushuhuda marafiki wake wote na kuwaambia, “Nimepata ukweli!”
“Jibu kwa Sala Yangu”
Karibu na wakati huu Ramón Redín, mmojapo waanzishi wa harakati ya Adventisti katika Ekwedori, alikuwa pia amezinduliwa na dini yake. Migawanyiko katika kanisa ilimfadhaisha. Kwa kweli Ramón alishuku dini zote. Siku moja yeye alisali kwa Mungu hivi: “Tafadhali nionyeshe ukweli. Ukifanya hivyo, mimi nitakutumikia kwa uaminifu muda wote wa maisha yangu yanayobaki.”
Muda mfupi baada ya sala hiyo, mmojapo marafiki wake, Luis Dávalos, akamwambia kwamba yeye alikuwa na jambo la maana sana la kumwambia. “Ramón, je! wewe ulijua kwamba Waadventisti wa Siku ya Sabato hawana ukweli?” Ramón akajibu hivi: “Luis, nathamini kunihangaikia kwako, lakini uhakika ni kwamba hakuna dini yoyote inayofundisha ukweli wa Biblia, na kwa sababu hiyo, mimi sipendezwi na yoyote yazo.” Hata hivyo, Ramón alikubali gazeti la Mnara wa Mlinzi pamoja na anwani ya makao ya misionari na akaahidi kwamba angalau yeye angeongea na wamisionari aone kama wangeweza kujibu maswali yake. Kule kulikoonekana kama kutojali hakukuwasilisha hisia zake za kweli; yeye alikuwa na tamaa yenye kina kirefu ya kujua kama kuna kitu kama Ukristo wa kweli. Kwa hiyo alipoondoka nyumbani mwa rafiki yake, alitumia saa mbili akitafuta makao ya misionari.
Walter Pemberton, ambaye alikuwa angali anang’ang’ana na Kihispania, alifanya vizuri awezavyo kujibu maswali ya Ramón, kama vile: “Je! Mashahidi wa Yehova huruhusu watu wawe na uhuru wa kusababu juu ya Maandiko?” Walter akajibu: “Sisi hatumpi mtu yeyote wajibu wa kutenda kinyume cha dhamiri yake. Sisi tunataka watu wasababu juu ya Maandiko, kwa kuwa hiyo ndiyo njia ambayo kwayo sisi hufikia maamuzi sahihi.”
“Basi, Mashahidi wa Yehova hushika Sabato?” Ramón akauliza. “Sisi hushika mambo ambayo Biblia husema juu ya Sabato,” Walter akajibu.—Mt. 12:1-8; Kol. 2:16, 17.
Kwa kushangaza, ijapokuwa Kiingereza cha Ramón cha kusitasita na Kihispania kidogo cha Walter, ukweli ulianza kudhihirika akilini mwa Ramón. Ramón hukumbuka hivi: “Mimi nilivutiwa sana na hiyo saa ya kwanza hivi kwamba mimi nakumbuka nikijiambia, ‘Lazima hili liwe jibu kwa sala yangu!’”
Mazungumzo yaliendelea siku baada ya siku. Walter alikuwa akiangalia maandiko katika Biblia yake ya Kiingereza, naye Ramón alikuwa akifuata katika yake ya Kihispania. Siku kumi na tano baada ya ile ziara yake ya kwanza, Ramón Redín, pamoja na Luis Dávalos na Waekwedori wengine watatu, alikuwa miongoni mwa wale walioshiriki kutoa ushuhuda wa kikundi wa kwanza uliopangwa kitengenezo katika Ekwedori. Mungu alikuwa amejibu sala yake amwonyeshe ukweli, na Ndugu Redín amekuwa akifanya yoteyote awezayo ashike nadhiri aliyofanya kwamba angetumikia Mungu kwa uaminifu muda wote wa maisha yake yanayobaki. Sasa akiwa na umri wa miaka 87, Ndugu Redín hushangilia kuwa painia wa pekee.
Pedro Apata Jibu
Upesi mwanamume kijana ambaye alikuwa amekuwa akitafuta ukweli kwa zaidi ya miaka 17 alijiunga na kikundi hiki kidogo lakini chenye kukua. Wakati Pedro Tules alipokuwa mwenye umri wa miaka kumi, alimsikia padri akijaribu kueleza Utatu. Kwa kukosa kuuelewa, Pedro akamuuliza jinsi watu watatu wangeweza kuwa mungu mmoja. Jibu la padri lilikuwa pigo kichwani kwa rula, na mfululizo wa matusi. Pedro akajiambia: ‘Siku moja mimi nitajifunza yote haya yanamaanisha nini.’
Hatimaye, baada ya kutumia wakati fulani pamoja na Waadventisti, akaanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova. Lile “fumbo” la Utatu lilikuwa limeondolewa karibu mara moja. Alipata kujifunza kwamba halikuwa fumbo, bali ubandia. Yesu Kristo si, “Mungu Mwana,” kama wengine wasemavyo, bali yeye ni “Mwana wa Mungu.” (Yoh. 20:31) Yeye alivutiwa na uhakika wa kwamba Mashahidi wote huhubiri nyumba kwa nyumba, kazi ambayo wakati mmoja yeye alikuwa amejaribu kuwasadikisha Waadventisti wafanye. Yeye aliamini kwamba namna hii ya uevanjeli ilihitajiwa kabisa ili kufuata kielelezo cha mitume. (Mdo. 5:42; 20:20) Na bado, Pedro alisitasita kuamua.
Kwa miezi minne au mitano yeye aliendelea kuhudhuria mikutano ya Waadventisti huku akishirikiana na Mashahidi pia. Mwishowe, Walter Pemberton akamwambia hivi: “Pedro, lazima uamue. Ikiwa Waadventisti wanasema kweli, basi wafuate. Lakini ikiwa Mashahidi wa Yehova wana ukweli, basi shikamana nao. Yapasa ukweli uwe juu ya kila kitu.”—Linganisha 1 Wafalme 18:21.
“Jambo hilo lilinisaidia kufanya uamuzi bora niliopata kufanya katika maisha yangu,” asema Pedro, “na hivyo mimi nikabatizwa Agosti 10, 1947, katika wonyesho wa wakfu wangu.” Mwaka uliofuata Pedro akaanza kupainia, naye ameendelea kwa uaminifu katika utumishi wa wakati wote tangu hapo. Alikuwa ndiye Mwekwedori wa kwanza kupokea mazoezi ya Shule ya Gileadi, baadaye alirudi Ekwedori kusaidia kazi hapa.
Msaada Zaidi Kutoka Makao Makuu
Katika 1948 kazi ya kuhubiri ilipokea mwinuko halisi wakati wamisionari 12 zaidi walipopewa migawo Ekwedori, sita kati ya hao wakienda Quito na wale wengine sita walikwenda Guayaquil, jiji kubwa zaidi na bandari kuu ya nchi. Albert na Zola Hoffman walikuwa miongoni mwa wale waliotumwa Guayaquil. Hawakuwa wamewahi kamwe kuona watu wengi wenye udadisi na wenye kupendezwa kadiri hiyo! Albert Hoffman hulieleza jambo hilo hivi:
“Jumapili alasiri tulifanya kazi yetu ya kwanza ya kutoa ushuhuda tukiwa kikundi kando za mto ambako watu walipatikana kwa ukawaida. Tulitumia kinanda pamoja na sahani za santuri za Kihispania. Kwanza tulikuwa tukiwaambia kwamba tulikuwa na ujumbe mzuri ajabu na wa maana kisha tukapiga kinanda. Upesi umati mkubwa ulikuwa ukikusanyika kutuzunguka wasikilize.”
Hali moja na hiyo, walipokuwa wakifanya kazi ya magazeti barabarani, ikiwa wamisionari walisimama tuli katika sehemu za biashara zenye watu wengi, walizungukwa upesi na umati wenye urafiki. Baadhi yao walikuwa na maswali, na wengine walitaka kupata magazeti. Hili lilikuwa ono lenye kusisimua kwa hao wamisionari wapya kwa kuwa hawakuzoea kuona kupendezwa kama huko kukionyeshwa.
Pindi ambayo hukumbukwa hasa na hao wamisionari wa mapema ilitukia katika Machi 1949. Ilikuwa nini? Ziara ya kwanza ya eneo la dunia katika Ekwedori iliyofanywa na N. H. Knorr, msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, na katibu wake, M. G. Henschel. Katika Quito, watu 82 walikusanyika kusikiliza hotuba hii, “Wakati Umesonga Sana Kuliko Unavyodhani!” Katika Guayaquil, hotuba iyo hiyo iliratibiwa. Ndugu Knorr alipoona idili ya hao wamisionari wapya ya kuitangaza, akasema, “Msivunjwe moyo sana ikiwa watu wengi hawaji.” Ingawaje, walikuwa wamekuwa wakifanya kazi huko kwa miezi miwili na nusu tu. Lakini ikawa zamu ya kila mmoja kushangaa wakati watu 280 walipojitokeza, na wengine wasiohesabika walisikia hotuba hiyo kwa redio.
Tetemeko la Dunia Labadili Mgawo wa Wamisionari
Katika 1949 ilionekana kwamba inafaa kuanza kuelekezea fikira baadhi ya majiji yaliyozunguka Quito katika bara-mwinuko la Andes. Ambato likachaguliwa. Hata hivyo, katika Agosti jiji hili pamoja na miji iliyolizunguka ilipigwa na tetemeko la dunia ambalo ndilo lililokuwa lenye kukumba zaidi lililoipata nchi hii katika muda wa vizazi vingi. Vijiji vizima vikatoweka. Ilikadiriwa kwamba watu zaidi ya 6,000 walipoteza uhai wao. Ambato likawa machinjoni.
Mkumbo huo ulikuwa mkubwa mno hivi kwamba kufikia mwaka uliofuata makao yanayofaa ya kuishi yalikuwa yangali hayapatikani kwa ajili ya hao wamisionari wapya. Kwa hiyo ikaamuliwa kwamba wangepelekwa Riobamba, jiji jingine upande wa kusini. Jack Hall na Joseph Sekerak wakawa ndio wenye ile kazi ngumu ya kufungua eneo hili lisiloguswa. Lakini maendeleo yalikuwa ya polepole katika mji huu ulio peke yao na wenye kufuata sana Ukatoliki.
Kutumia Waliyojifunza
Siku moja Jack alipokuwa akitoa ushuhuda katika Riobamba, aliachia César Santos, mwanamume kijana aliyefunga ndoa kile kitabu “Let God Be True.” Yeye alivutwa sana na yale aliyokuwa akisoma hivi kwamba hakuweza kukiweka chini usiku huo mpaka alipokuwa amekisoma chote. Sura iliyotokeza tendo-mwitikio la mara hiyo ilikuwa “Utumizi wa Mifano Katika Ibada.” Alisoma hivi: “Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga . . . Usivisujudie wala kuvitumikia.” (Kut. 20:3-5) Sasa, César alikuwa amejitoa sana hasa kwa San Antonio, mtakatifu wa Kikatoliki, naye aliweka mfano wake nyumbani mwake. Lakini César alipoendelea kusoma yeye aliukunjia uso mfano wa huyo ambaye wakati mmoja alikuwa mtakatifu mwenye kupendelewa akasema, “Mimi nitakuteremsha chini mara hii.” Akamaliza kusoma sura ile, akainuka, akashika mfano ule, akaupeleka nje, na kuutupilia mbali.
Alipoanza kuwaambia watu wa ukoo na marafiki wake mambo aliyokuwa amejifunza, wao walifikiri ameshikwa na kichaa. Hata hivyo, juma moja baadaye yeye alitembelea Jorge ndugu yake mchanga, akamwomba asome kitabu kile. Jorge alivutiwa sana na mambo yacho yenye kupatana na akili na akachochewa sana na taraja la dunia paradiso. Mwezi mmoja baadaye yeye alikuwa nje katika utumishi wa shambani pamoja na wamisionari.
Ingawa hivyo, bado Jorge alikuwa na mambo fulani ya kujifunza. Siku moja alikuwa akila wakati Jack Hall alipokuja kutembelea. Mama ya Jorge alikuwa akiwapa damu iliyokaangwa kwa mafuta, mlo wa kawaida katika sehemu hii ya nchi. Jack alipopewa kidogo, yeye alikataa kwa upole na akatumia kwa faida fursa hiyo kueleza mambo ambayo Biblia husema juu ya damu. (Mwa. 9:4; Mdo. 15:28, 29) Mara hiyo Jorge akayakubali kwa moyo. Kwa mshangao mkubwa wa mama yake, yeye alikataa kumaliza chakula kilichokuwa katika sahani yake.
Upesi hata washiriki zaidi wa jamaa hii wangenufaishwa na ukweli.
Waazimia Kutumikia Mungu
Wakati mmoja Orffa, dada mkwe wa César mwenye umri wa miaka 18 alikuwa amemuuliza padri mmoja Mkatoliki amwambie ni nani aliyeumba Mungu. Padri huyo hakujua, hivyo akauliza pasta Mwevanjeli. Wala yeye hakuweza kujibu swali lake. Ndipo akamuuliza César, naye akaeleza kutoka kwa Biblia kwamba Yehova hakuwa na mwanzo wala mwisho. (Zab. 90:2) Ukweli huu rahisi ulitosha kuwasha ndani ya Orffa mwali wa upendezi ulioenea kwa dada zake wawili. Ujapokuwa upinzani imara kutoka kwa jamaa, yeye pamoja na Yolanda dada yake mchanga, walianza kujifunza Biblia na kuhudhuria mikutano kwa siri. Walipigwa na wazazi wao kwa sababu ya jambo hili kila wakati waliporudi nyumbani kutoka mikutanoni.
Kufikia wakati huu Lucía, mke wa César, aliyekuwa dada ya Orffa, alikuwa mwenye ubaridi kuelekea ujumbe wa Biblia wenye uharaka. Ndipo siku moja Orffa akamkemea, akisema hivi: “Ona tu ni mambo gani ninayolazimika kuvumilia kwa ajili ya ukweli!” alipokuwa akishusha nguo yake kuonyesha alama za mapigo na michubuko. Kutoka wakati huo kuendelea, Lucía akafanya maendeleo ya haraka.
Kwa wakati uliopo, padri alikuwa ametoa maagizo kwa mama ya Orffa amfukuze nyumbani, na mama alitii. Hata hivyo, jambo hili lilithibitika kuwa baraka. Sasa akiwa peke yake, Orffa akaanza kujitayarishia ubatizo, ndivyo na Lucía. Kwenye kusanyiko lililofuata ni nani aliyejiunga nao miongoni mwa wenye kubatizwa ila Yolanda, dada yao mchanga zaidi. Bila kujali jinsi angepokewa arudipo nyumbani, alikuwa amesafiri kwa basi zaidi ya kilometa 160 akabatizwe pamoja na dada zake. Wote watatu walisimama pamoja wakaonyesha azimio lao la kutumikia Yehova hata iweje!
Teto Dhidi ya Upinzani wa Makasisi
Wamisionari zaidi walipowasili mapema katika 1950, kuhubiriwa kwa habari njema kulianza kuenea upesi kwenye miji iliyo peke yayo katika bara la chini la pwani—Manta, La Libertad, Milagro, Machala, na mingineyo. Ukuzi wa haraka pamoja na vikundi vikubwa vya wahubiri waliokuwa wakishiriki huduma vilifadhaisha Kanisa Katoliki. Hili lilikuwa eneo ambalo kanisa lilikuwa limetawala kwa msaada wa watawala wa nchi, nalo halikuwa tayari kuvumilia ushindani wowote. Kwa upande mwingine, Wakristo wa kweli wana utegemezo wa roho ya Yehova isiyoshindika, na hakuna kiasi chochote cha mnyanyaso kinachoweza kukomesha tamaa yao yenye kuwaka ya kueneza habari njema za Ufalme wa Mungu. Tokeo likawa nini?
Pedro Tules anakumbuka hivi: “Katika viunga vya Quito katika kisehemu kinachoitwa Magdalena, baada ya padri kuwa amechochea wanaghasia dhidi yetu, mwanamume mmoja alimwendea na kusema, ‘Bw. Padri, wewe unafanya nini hapa?’ Padri yule akajibu: ‘Nalinda kundi langu dhidi ya watu hawa. Ni mimi pekee niliye na haki ya kuwafundisha juu ya Mungu.’ Yule mwanamume akajibu: ‘Hapana, wewe una haki ya kufundisha kanisani, lakini hapa nje barabarani na katika bustani za starehe wao wana uhuru kamili kufundisha Biblia. Wao hawadhuru mtu yeyote. Mpaka sasa mimi sikujua kuna watu kama hao, lakini mimi nataka nyinyi nyote mjue kwamba wao wanakaribishwa nyumbani kwangu wakati wowote.’”
Bado katika ujamii mwingine karibu Quito, padri mmoja alijaribu kufukuza Mashahidi watoke mjini. Walipokuwa wakivuka daraja, padri pamoja na wanaghasia wake walitisha kutupa wahubiri wale ndani ya mto. Muda uo huo mwanamume mmoja ambaye alikuwa ametembelewa na Pedro mara kadhaa akatokea. “Habari gani, Pedro,” akasema. “Kunatukia nini hapa?”
Katika kujibu, Pedro akasema, “Sisi tulikuwa tukifundisha watu Biblia kwa amani, lakini mtu huyu amechochea watu dhidi yetu naye anatufukuza tutoke mjini.”
Kusikia hivyo, mwanamume yule akachomoa bastola, akatembea kumwendea padri, na kupaaza sauti hivi: “Hei, wafanya nini wewe? Je! wewe hujui kwamba watu hawa wana haki zile zile kama zako? Unalofanya ni uhalifu dhidi ya sheria.” Padri alipojaribu kutetea vitendo vyake, mwanamume yule akajibu: “Mambo ambayo yametendeka hapa yatatokea katika El Comercio kesho!” Ilitukia kwamba yeye anafanyia kazi karatasi-habari hiyo, na kweli kulingana na ahadi yake, kesho yake mwenendo usio wa Kikristo wa padri huyo ulikuwa kichwa cha makala kuu ya karatasi-habari kubwa zaidi ya Quito.
Serikali Yaonya Wapinzani
Alfred Slough hukumbuka kisa kingine ambacho kilitukia alipokuwa akitumikia akiwa misionari: “Jamaa mmoja ‘shujaa’ alijisingizia kuwa anapendezwa kisha akanyakua nakala moja ya Mnara wa Mlinzi kutoka mikononi mwa dada mmisionari na kwa kiburi akairarua vipande vipande. Karibu na wakati huu nilimwona padri akiwa juu ya baiskeli yake mavazi yake yakiwa yanapeperushwa na upepo, akikaribia kasi kuhakikisha kuwapo kwetu.
“Upesi baada ya kuwasili kwake, kundi la wanaghasia likafanyizwa, likiongozwa na yule mwanamume aliyekuwa amerarua Mnara wa Mlinzi akisaidiwa na watawa wa kike wawili. Wengine walikuwa sana-sana ni watoto ambao walionekana wakijaza mawe katika mifuko yao. Tukiwa kikundi, sisi tulianza kutembea polepole ule mwendo wa nyumba kadhaa za mjini kuelekea kituo cha basi nao wale wanaghasia wakitufuata karibu-karibu. Wakati wa matembezi haya yenye wasiwasi wao waliridhika na kutupia kikundi chetu mawe madogomadogo. Kwa tokeo zuri, hakuna yeyote aliyeumizwa vibaya. Basi liliposimama, hatimaye wanaghasia wakasitawisha ushujaa mwingi na wakashambulia, wakitupa mawe makubwa walipokuwa wakikaribia. Kufikia wakati walipowasili kando ya basi, akina dada wote na watoto walikuwa wameingia ndani ya basi, kwa hiyo nikaruka ndani. Tuliondoka hali mawe na matope mengi yanatupwa ndani ya basi, huku wakaaji wa eneo hilo ambao walikuwa ndani ya basi pia wakipaazia sauti zao hao wanaghasia kwa kasirani, na kuwaita washenzi. Watu waliokuwa ndani ya basi walitupatia viti vyao kwa fadhili na wakatusaidia kupangusa matope, hivyo wakionyesha kwamba lililokuwa limetukia lilikuwa tendo la wachache tu walioongozwa vibaya, ambao bila shaka walikuwa wakifanya penzi la padri. Tulikuwa na fursa nzuri ajabu ya kutoa ushuhuda mwendo wote kurudi mjini.”
Vyombo vya habari viliitikia mara moja, kwa vichwa vya habari kama vile: “PADRI ACHOCHEA UHALIFU,” “KATIKA MAGDALENA WENYE KUSHIKILIA DINI BILA AKILI WASHAMBULIA FARAKANO LA MASHAHIDI WA YEHOVA,” “UKOSEFU WA UVUMILIANO WA KIDINI.”
Bila shaka, padri yule alikana kuwa alihusika katika tendo hilo la wanaghasia, akisema kwamba yeye alikuwa amekuwa katika sehemu nyingine ya ujirani. Jamii fulani fulani na halmashauri za Kikatoliki katika eneo hili zilitia sahihi pia katika ombi moja zikijulisha wazi kuwa hazikuwa na hatia. Lakini Wizara ya Serikali ilimpa agizo mkuu wa polisi atoe jibu hili: “Katiba na sheria za Jamhuri huruhusu uhuru wa kidini, na kwa sababu hii, sisi tukiwa wenye mamlaka tunawajibishwa kuwa macho kuona kwamba haki za wananchi wote hazitishwi. . . . Ingetamanika sana kwamba kutoka sasa na kuendelea visa vinavyofanana na kile kilichotukia tarehe sita ya mwezi huu visirudiwe, la sivyo mamlaka hii itawajibika kuadhibu wenye daraka kulingana na sheria.”
Ijapokuwa hivyo, usumbufu zaidi ungekuja, kwa sababu Kanisa halikuwa tayari kuachilia mateka walo waende.
Cuenca Gumu
Cuenca, lile jiji kubwa zaidi la tatu katika Ekwedori, lenye idadi ya watu 152,000, lilikuwa ngome kweli kweli ya Kanisa Katoliki. Kwa kuwa idadi hiyo ya watu haikuwa imepokea ushuhuda, Pedro Tules na Carl Dochow mhitimu wa karibuni zaidi wa Gileadi, walipewa mgawo waende huko katika Oktoba 1953. Ulikuwa mgawo mgumu sana na mara nyingi wenye kuvunja moyo.
Carl hukumbuka mfanya kazi mmoja wa nyumba wa kike mwenye kushikilia dini bila akili aliyesema hivi kwa wasiwasi, “Nyinyi hamwamini Bikira.” Carl alipofungua Biblia kwenye Mathayo 1:23, mfanya kazi huyo akaanza kutetemeka na kusema, “Sisi tumekatazwa kuisoma Biblia.” Kusema hivyo akarudi ndani ya nyumba kwa ghafula na kumwacha Carl akiwa anasimama mlangoni. Katika pindi nyingine mfanya kazi mmoja wa nyumba wa kike alikuwa akisikiliza kwa kupendezwa, lakini wakati mwanamke mwenye nyumba aliporudi nyumbani na kuona jambo lililokuwa linatukia, yeye alipiga teke mkoba wa vitabu wa Carl ukaanguka chini kwenye ngazi. Wakati mwingine Carl alifukuzwa na mwenye nyumba mwenye kasirani aliyekuwa anapunga-punga kipande cha kuni aondoke kwenye veranda. Kila wakati wamisionari walipokuwa wakitoa ushuhuda katika eneo la San Blas, padri alikuwa akipiga kengele za kanisa; na wakati watoto walipokuja mbiombio, yeye alikuwa akiwahimiza wawatupie wamisionari mawe.
Kwa muda wa miaka mitatu, hakuna hata mtu mmoja katika Cuenca aliyekuwa na ujasiri wa kuchukua msimamo kwa ajili ya ukweli. Mara nyingi Carl alikuwa akitembea-tembea kwa huzuni kuteremka kandokando ya mto na kusali kwamba Yehova ampe mgawo wenye mazao zaidi. Hatimaye alipewa mgawo kwenda kwenye jiji la pwani la Machala, lililokuwa na idadi ya watu wapole-wapole, na wenye akili zilizofunguka. Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya mwisho Cuenca kuona Mashahidi wa Yehova.
Jeuri ya Wanaghasia Kwenye Mkusanyiko
Riobamba, lile jiji ambako Jack Hall na Joseph Sekerak walikokuwa wamepelekwa katika 1950 wakafungue eneo, lilikuwa katika habari katika 1954. Katika Machi kusanyiko la mzunguko lilifanywa huko katika Jumba la Maonyesho Iris. Mambo yote yalienda sawa mpaka padri Myesuiti aliposhutumu Mashahidi wa Yehova katika redio na kusema kwamba wao hawakuwa na haki ya kufanya kusanyiko katika “jiji la Riobamba la Kikatoliki.” Yeye aliwataka watu wazuie mkutano wa watu wote ulioratibiwa siku iliyofuata. Lakini akina ndugu walijulisha polisi vitisho vyake.
Hotuba ya watu wote iliyokuwa na kichwa “Upendo, Ni Wenye Mafaa Katika Ulimwengu Wenye Ubinafsi” ilianza kama ilivyoratibiwa wakiwapo watu 130. Lakini katika muda wa dakika 10, makelele yenye kusema “Kanisa Katoliki liishi muda mrefu!” na “Waanguke Waprotestanti!” yaliweza kusikika kwa mbali. Dakika kwa dakika makelele hayo yakazidi kuwa makubwa kadiri wale wanaghasia walivyokaribia jumba la maonyesho.
Polisi wanane waliziba mwingilio wa jumba la maonyesho. Umati ule wenye kirui ulipokuwa ukiongezeka katika hesabu, polisi walichomoa panga zao na kuwasukuma warudi nyuma kwenye mkingamo; kutoka hapo kundi hilo liliendelea kuvurumisha mawe kwenye mwingilio. Hata hivyo, ujapokuwa msukosuko huu programu iliendelezwa mpaka umalizio wayo. Kwa kufaa, hotuba ya mwisho ilikuwa “Kuvumilia Mpaka Mwisho.”
Wasikilizaji walipokuwa wakiondoka jumbani, walipata hapo polisi wapatao 40 kuwapa ulinzi. Lakini akina ndugu walipokuwa wakienda zao kutoka eneo hilo lenye ulinzi wa polisi, hali ile ikawa yenye wasiwasi zaidi. Mahali pa makao ya kimisionari na Jumba la Ufalme palijulikana vizuri sana, na kundi kubwa hata zaidi la wanaghasia lilikuwa limekusanyika hapo. Kwa mara nyingine tena, ikawa lazima kuomba ulinzi wa polisi. Maofisa waliandamana na wamisionari kwenda kwenye makao yao na wakazingira nyumba usiku kucha. Kwa kutoweza kuwafikia Mashahidi, wanaghasia waliokuwa na kichaa walimwaga kirui chao juu ya jengo lile, wakitupa mawe na kuvunja karibu madirisha yote yaliyoelekea barabarani, wakizichukiza sana zile jamaa nyingine sita zilizoishi humo pia na ambazo hazikuwa Mashahidi wa Yehova.
Teto la Kitaifa Dhidi ya Ukosefu wa Uvumiliano
Akina ndugu walipokuwa wakitembea barabarani siku iliyofuata, waliendewa mara nyingi na watu ambao, ijapokuwa hawakupendezwa sana na kazi ya Mashahidi, walitaka kuonyesha kutokubaliana kwao na jambo lililokuwa limetukia jioni iliyotangulia. Kufikia siku ya pili taifa zima lilikuwa likiteta. Wimbi la makala za karatasi-habari zikipendelea uhuru wa ibada na kupigania haki za Mashahidi wa Yehova lilienea nchini kote kwa juma zima.
El Comercio, ile karatasi-habari mashuhuri zaidi katika mji mkuu wa taifa, ilieleza shambulio lile na kisha ikakumbusha zile Halmashauri za Kuhukumia Wazushi, mauaji ya Hitla, na matukio mengine yenye ukatili ya historia.
Mchangaji-habari za karatasi-habari mashuhuri ya Guayaquil, El Universo, aliandika juu ya “Matunda ya Ukosefu wa Uvumiliano” akasema hivi:
“Kusudi langu katika makala hii ni kumuuliza swali Rekta wa Shule ya Juu ya San Felipe, kwa njia ya moja kwa moja, ambapo wanafundisha utovu wa uvumiliano kufikia hatua ya kuwaanzisha wanafunzi wao vijana wawashambulie kwa fimbo na mawe Mashahidi wa Yehova wenye saburi . . . Rekta Reverendi Baba Myesuiti apaswa ajibu swali hili, ikiwa yeye ni mwanamume awezaye kukabili matokeo ya vitendo vyake. Kwa urahisi, swali ni hili linalofuata: Rekta angeonaje ikiwa katika mataifa ambako Wakatoliki ndio wachache wangetendewa katika njia ile ile anayofanya wanafunzi wake wawatendee Waprotestanti? . . . Wakatoliki katika ulimwengu mzima, wakiongozwa na Pontifu Mkuu Zaidi [Papa], wanaomba waonyeshwe uvumiliano. Wao wanaudai kwa namna zote za sauti; wanauomba katika Umoja wa Mataifa, kwenye Kongamano la Berlin, na kwenye mikusanyiko yote na katika mikutano yote ambako Mashariki na Magharibi hukutana pamoja. Yule Pontifu Mtakatifu na mkuu wa Ukatoliki, kwa upatani wa karibu sana na Churchill (Mprotestanti) na Eisenhower (Mprotestanti), huomba kutoka kwa Urusi na satelaiti [nchi zinazoiunga mkono] zayo uvumiliano, uhuru wa maaskofu wakuu na makardinali waliotiwa gerezani . . .
“Kuna tofauti gani kati ya kikundi cha Wakomunisti katika Chekoslovakia ambao, wakiwa na fimbo mkononi, hushambulia Wakatoliki wanaotoa sala hekaluni, na wanafunzi wa San Felipe ambao, wakiwa na fimbo mkononi, hushambulia Mashahidi wa Yehova katika Riobamba wanaposikiliza mahubiri juu ya ‘Upendo Katika Enzi Hii Yenye Ubinafsi’?”
Laana za padri Myesuiti wa Riobamba zilikuwa zimetokeza baraka kama vile katika kisa cha Balaamu, kwa kuwa Yehova alikuwa pamoja na watu wake.—Hes. 22:1–24:25.
Shauku Kubwa Zaidi kwa Kristo
Katika pindi ya wakati huu Carlos Salazar, kijana Mwekwedori aliyekuwa amejifunza ukweli katika United States ya Amerika, alichukua huduma ya wakati wote.
Carlos alikuwa mwenye umri wa miaka 16 tu wakati dada painia katika Jiji New York alipomwangushia mama yake Biblia pamoja na kile kitabu “This Means Everlasting Life,” naye akampa Carlos avisome. Kwa kuwa Carlos hakupendezwa na dini, aliviweka rafuni. Hata hivyo, siku moja alipokuwa akicheza katika Central Park, alivunjika mguu na hivyo akalazwa nyumbani. Akiwa na wakati, alikubali bila kutaka toleo la yule dada painia la kujifunza Biblia, lakini kwa sharti la kwamba dada huyo amfundishe Kiingereza kidogo. Yeye anasema: “Kadiri nilivyozidi kusoma kitabu kile, ndivyo nilivyozidi kusadikishwa kwamba huu ulikuwa ndio ukweli.”
Upesi Carlos akaanza kuhudhuria mikutano na kushiriki utumishi wa shambani, hata akawa anasimama kwenye kona za barabara kutoa magazeti. Ni kweli, mama yake ndiye alikuwa amempa kitabu kile, lakini alipoona akikisoma, akawa mwenye kasirani sana hivi kwamba alitisha kumrudisha Ekwedori. Mama alidhani kwamba hakuna Mashahidi Ekwedori. Kwa hiyo katika 1953, akiwa anasindikizwa na Rosa shangazi yake mkubwa, mfuasi mwenye kujitoa sana wa Roma Katoliki, Carlos akarudi Ekwedori.
“Carlos, sasa kwa kuwa umerudi Ekwedori, lazima uanze kuhuduria Misa tena,” akasema shangazi yake mkubwa.
Lakini Carlos hakuwa tayari kuachilia kitu chenye thamani kama tumaini la uhai wa milele. (Yoh. 3:36) Maneno ya Yesu, “Yeye ambaye ana shauku kubwa zaidi kwa baba au mama kuliko kwa mimi hanistahiki mimi,” yalikuwa na umaana halisi kwake. (Mt. 10:37, NW) Yeye alijibu hivi: “Shangazi Rosa, wewe huelewi wakati huu jambo ninalofanya. Lakini kwa kuwa sasa mimi nipo hapa Ekwedori, mimi nakusudia kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nawe lazima ustahi tamaa yangu.”
Baada ya Carlos kubatizwa katika 1954, alianza kupainia. Katika 1958 akawa Mwekwedori wa pili kualikwa kwenye Shule ya Gileadi. Yeye alipewa mgawo arudi kwenye nchi ya kwao, ambako ameendelea katika utumishi wa wakati wote. Hatimaye baada ya miaka kumi ya kumhubiria kwa saburi, aliona shangazi yake mkubwa akikubali ukweli pia; na akiwa na umri wa miaka 84, yeye anaendelea kuwa Shahidi mwenye kutenda.
Dada Wajasiri Watetea Habari Njema
Katika 1958 dada wawili waliokuwa wahitimu wa Shule ya Gileadi walitumwa Ekwedori pia. Unn Raunholm kutoka Norowei na mwenzake Julia Parsons kutoka Newfoundland walipewa mgawo kwenda Ibarra, jiji lenye kupendeza linalokaa katika bonde kaskazini mwa Quito. Uteteaji mwingine wa ujasiri juu ya uhuru wa ibada ulifanywa hapa. Unn ana kumbukumbu hizi dhahiri za yaliyotukia:
“Tulipoanza kueneza eneo letu katika jiji la Ibarra, tulipata kwamba kulikuwako miji midogo karibu karibu ambayo hatungeweza kufanyia kazi, kama vile San Antonio, ambako walitengeneza sanaa za miti zenye kupendeza pamoja na mifano mingi ya kidini. Mara habari zilipomfikia padri mwenyeji kwamba tulikuwa huko, yeye alikuwa akija akiwa anampanda farasi au akiwa anakimbia huku akifuatwa na mlolongo wa watu na kutokeza makelele mengi sana hivi kwamba tulikuwa tukilazimika kuondoka. Hivyo tuliamua kukazia fikira mji mdogo mwingine uitwao Atuntaqui uliokuwa karibu.
“Siku moja tulipokuwa tukifanya kazi karibu na kanisa, tuliona kikundi cha watu nje lakini hatukutoa uangalifu wowote mpaka sherifu wa pale alipokuja tulipokuwa. Yeye alikuwa mwanamume mwenye urafiki niliyekuwa nimetembelea hapo mbeleni; kwa kweli, yeye alikuwa amechukua fasihi fulani. Hata hivyo, wakati huu yeye alinihimiza hivi kwa wasiwasi, ‘Bibi, tafadhali ondoka mjini mara moja! Padri anapanga maandamano dhidi yako, nami sina watu wa kutosha kukulinda.’ Ilitukia kwamba yule padri wa San Antonio alikuwa amehamishwa kuletwa Atuntaqui, naye alikuwa ameanza tena vile vitimbi vyake.
“Kwa kuwa tulikuwa wanne tukihubiri siku hiyo, ilichukua wakati fulani kutafuta kila mmoja ili kuondoka. Kisha tukapata kujua kwamba basi liendalo Ibarra halingekuwa likienda mpaka baada ya saa moja. Kwa hiyo tukaelekea kwenye hoteli moja, tukitumaini kupata ulinzi humo mpaka basi liwasilipo. Tulipokuwa njiani kwenda humo tukaanza kusikia makelele. Umati ule ulikuwa ukitufuata! Bendera ya Vatikani ya rangi nyeupe na manjano ilipungwa-pungwa mbele ya kikundi hicho huku padri akiwa anapiga kelele kwa shime kama vile ‘Kanisa Katoliki liishi muda mrefu!’ ‘Waanguke Waprotestanti!’ ‘Ubikira wa Bikira na uishi muda mrefu!’ ‘Maungamo na yaishi muda mrefu!’ Kila wakati, umati ule ulikuwa ukirudisha mwangwi wa shime hizo neno kwa neno baada ya padri.
“Wakati ule ule tulipokuwa tunashangaa tufanye nini, wanaume kadhaa wakatujia na kutualika tuingie ndani ya Nyumba ya Wafanya Kazi wa mahali pale. Ilikuwa ya chama, nao walituhakikishia kwamba humo hakuna yeyote angeweza kutudhuru. Kwa hiyo wanaghasia walipokuwa wakisimama nje wakipiga makelele ya shime kama vile ‘Waanguke Wamesoni!’ ‘Waanguke Wakomunisti!’ sisi tulikuwa ndani tukishughulika sana na kazi ya kutoa ushuhuda huku watu wenye udadisi wakiwa wanakuja kuona ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Tuliangusha kila kipande cha fasihi tulichokuwa nacho.
“Tukikumbuka ule upendezi mwingi tuliokuwa tumepata katika Atuntaqui, tuliamua kuuzuru tena, lakini wakati huu tukianza kwa tahadhari kufanya kazi katika viunga vya mji. Hata hivyo, lazima mtu fulani awe alikuwa ameturipoti, kwa kuwa kengele za kanisa zilianza kulia kana kwamba zinapigwa na mtu mwenye kichaa na upesi tulisikia sauti kubwa ikituonya kwamba padri alikuwa akija njia hii akifuatwa na wanaghasia. Padri yule alinijia na kufoka maneno hivi: ‘Bibi, unajasiriaje kurudi hapa baada ya jambo lililotukia wakati uliopita!’ Nilijaribu kusababu pamoja naye, nikieleza kwamba katiba ya nchi ilihakikisha uhuru wa kidini. ‘Lakini, huu ni mji wangu!’ akasema. ‘Ndiyo,’ nikasema, ‘lakini mimi nina haki ya kuongea na watu hawa, nao wana haki ya kusikiliza wakitaka. Kwa nini usiwaambie watu wako kwamba ikiwa hawataki kusikiliza, si lazima wafungue milango yao tunapozuru, nasi tutamwendea mtu mwingine.’
“Ndipo padri yule alipogeukia ule umati na kusema: ‘Hakika mimi nitaondoka katika mji huu ikiwa watu hawa wanachukua hatua nyingine zaidi ya kuendelea mbele!’ Kusikia hivyo, baadhi ya waliokuwa wakisikiliza wakatuhimiza tuendelee na kazi yetu na wakaahidi kutuunga mkono dhidi ya padri. Hata hivyo, kwa kuwa sisi hatukutaka kuanzisha vita ya wenyeji kwa wenyeji, tukaamua kwamba ingefaa zaidi tuondoke na kurudi siku nyingine.”
Kurudi San Antonio
“Tulipoona kwamba padri huyu mkali sana alikuwa amehamishwa kuja kwenye mji huu, tuliamua kuzuru tena San Antonio, ule mji mwingine,” aendelea Dada Raunholm. “Kabla ya sisi kufanya ziara nyingi, kengele za kanisa zikaanza kulia na wanawake kadhaa wakaanza kukusanyika barabarani wakiwa na fimbo na vifagio mkononi. Mwenye nyumba mmoja alitukaribisha ndani, na tulipokuwa tukiongea, mlango ukabishwa kwa nguvu. Alikuwa sherifu wa mahali pale. Yeye alilituhimiza tuondoke mjini akisema: ‘Nyinyi mwajua jambo lililotukia katika Atuntaqui, nanyi mwajua kwamba hakuna haja ya kuja hapa kwa kuwa tayari sisi ni Wakristo.’ Mimi nikamuuliza kama anafikiri kwamba kuwajia watu fimbo zikiwa mkononi ndilo jambo Wakristo wa kweli wangefanya. Nilidokeza kwamba yeye aende nje na kuwaomba watu waende nyumbani. Akasema kwamba angejaribu, lakini akarudi karibu mara ile akisema kwamba hawakumsikiliza.
“Kusikia hivyo, jirani mwingine akatualika twende nyumbani kwake tukaongee na jamaa yake, hata akatusindikiza njiani kwenda huko. Tulipokuwa ndani, tulisikia mlango ukibishwa tena, na ikawa kwamba walikuwa ni polisi wakiwa na bunduki. Walikuwa wameitwa kutoka Ibarra na sherifu. Wakasema: ‘Tumeambiwa juu ya taabu yenu. Nyinyi endeleeni kwenda nyumba kwa nyumba, nasi tutakuwa papo hapo nyuma yenu.’ Tuliwashukuru kwa fadhili yao na tukadokeza kwamba wamtembelee padri wa mji, kwa kuwa ndiye aliyekuwa mchochezi wa matata yote haya.”
Polisi wakatekeleza dokezo lile. Tokea wakati huo na kuendelea, dada zetu hawakuwa na matatizo zaidi katika kutoa ushuhuda katika mji wa San Antonio.
Maeneo ya Pwani
Wamisionari wengine wawili, Ray na Alice Knoch, walipewa mgawo wa kuleta ujumbe wa Ufalme kwenye vijiji katika Pwani ya Pasifiki. Ili kufikia Manta, kijiji cha uvuaji-samaki chenye idadi ya watu wapata 10,000, walisafiri kwa basi kwa saa 16 kutoka Guayaquil. Wakiwa njiani ilikuwa lazima wavuke vijito ambavyo havikuwa na madaraja. Nyakati nyingine barabara ilikuwa yenye kuteleza sana kwa kuwa majani yalikuwa yamekua sana na kufunika njia hivi kwamba abiria walilazimika kushuka na kusukuma basi ili liweze kupanda ile miinuko mikubwa.
Kuhubiri nyumba kwa nyumba lilikuwa jambo kama ambalo walikuwa hawajapata kuona. Watoto wengi wenye udadisi, waliwafuata nyumba kwa nyumba kwa kuwa hawakuwa wamepata kuona watu wa kutoka ng’ambo. Kwa sababu watu walikuwa waiitikivu wa ukweli wa Biblia, kundi lilianzishwa upesi.
Halafu, Ray na Alice wakahamia La Libertad, kijiji kingine cha uvuaji-samaki katika pwani. Usafiri kwenda kwenye kijiji hiki ulifanywa kwa njia ya merikebu ya kukokotwa na ng’ombe. Kufikia wakati walipowasili, mavazi, fanicha, na kila kitu kinginecho kilikuwa na harufu ya zizi la ng’ombe. Lakini hapa katika La Libertad walimpata Francisco Angus, mwanamume wa asili ya Jameika ambaye alisikiliza ujumbe ule kwa makini. Alikubali funzo la Biblia. Katika muda wapata miezi sita yeye na Olga, mke wake, walikuwa tayari kushiriki utumishi wa shambani. Alice husema: “Jambo lililonivutia kuhusu Francisco lilikuwa kwamba baada ya kufanya kazi usiku kucha, yeye alikuwa akija nyumbani asubuhi, anaoga, na kuwa tayari kwa utumishi.” Baadaye yeye aliingia utumishi wa painia pamoja na mke wake, kisha akawa mwangalizi wa mzunguko, na sasa hutumikia akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.
Machala Wazaa Tunda
Kwa wakati uliopo, Carl Dochow na Nikolas Wesley, misionari mwingine, walianza pia kupata masikio yenye kusikiliza katika Machala, ule mji mkuu wa ndizi wa Ekwedori. Joaquín Palas mwenye mwili mnene, aliyekuwa na baa ya pombe, alisikiliza kwa upendezi wenye makini wakati Carl alipokuwa akieleza juu ya tumaini la kuishi juu ya dunia paradiso. Joaquín alikubali funzo kwa urahisi. Uthamini wake ulikuwa mwingi sana hivi kwamba alikuwa akifunga baa wakati wa funzo. Alipojifunza kwamba hakuna moto wa mateso wenye kuwaka, alisisimuka sana hivi kwamba alianza kutembelea baadhi ya majirani wake ashiriki nao aliyokuwa amejifunza. Hata hivyo, yeye alishtuka kidogo wakati jirani mmoja aliposema: “Joaquín, afadhali usafishe nyumba yako mwenyewe kwanza kabla ya kuja kuongea juu ya Biblia. Wewe hata hujafunga ndoa na mwanamke unayeishi naye.”
Wakati Joaquín alipouliza Carl afanye nini, jibu lilikuwa kwamba afunge ndoa kisheria. Siku yenyewe iliyofuata yeye na mwenzi aliyeishi naye walikwenda kwa wenye mamlaka wakapate hati zao. Halafu akaamua kwamba kwa kweli yampasa abadili kazi yake. Baa ya pombe ikauzwa, naye akaanza kutengeneza makaa ili ajiruzuku mwenyewe pamoja na mke wake. Baadaye wote wawili wakaingia kazi ya painia.
Jumba la Ufalme katika Machala lilikuwa jengo dogo lililokuwa na kuta za mianzi iliyopasuliwa ambazo ziliweza kupisha kwa urahisi nuru ya mchana na hewa. Pasipo akina ndugu kujua, mwanamke mwenye udadisi—jirani mmoja—alikuwa ametoboa tundu dogo ukutani ili kuona yaliyokuwa yakitendeka. Kwa miezi miwili yeye alitazama jinsi akina ndugu walivyokuwa wakisalimiana na jinsi walivyoshangilia kushirikiana kabla na baada ya mikutano. Mazingira haya ya kirafiki na yenye upendo, lilikuwa jambo ambalo mwanamke huyo alikuwa hajapata kuona kamwe katika dini alizokuwa amekuwa mshiriki wazo. Yeye alitaka kuwa sehemu ya mazingira hayo. Kwa hiyo, Floricelda Reasco akaanza kuhudhuria mikutano na upesi akawa dada katika imani na kisha painia mwenye bidii.
Upinzani Mkali Katika Portovelo
Kilometa chache kutoka Machala uko mji wa Portovelo wenye kuchimbwa dhahabu ukikaa vizuri chini ya Milima Andes. Huko aliishi Vicenta Granda, mwanamke Mkatoliki mwenye kujitoa sana aliyekuwa mmojawapo wahudhuriaji Misa waaminifu zaidi. Katika lile ambalo huitwa eti Juma Takatifu, yeye alifuata sana kawaida ya kidini inayoitwa rezar viacruzes. Kwa siku saba mfululizo yeye alikuwa akisali akiwa mbele ya michoro 12 iliyokuwa ikionyesha mateso ya Yesu kutoka wakati alipotiwa mbaroni mpaka kifo chake. Wenye kujitoa walifundishwa kwamba kufanya kawaida hii ya kidini kuliwapa msamaha kamili kwa dhambi zao zote walizofanya wakati wa mwaka.
Basi, Vicenta Granda alitaka kujua zaidi juu ya Mungu, kwa hiyo yeye akajipatia Biblia mbili, tafsiri Valera na Torres Amat. Tayari yeye alikuwa amezisoma tangu mwanzo mpaka mwisho mara mbili na sasa alikuwa na maswali mengi. Wakati Alice Knoch alipozuru nyumba yake, akitoa kitabu “Let God Be True,” yeye alikichukua mara moja nayo mawazo yake yakachukuliwa sana katika kukisoma hivi kwamba yeye alisahau kabisa kuwapo kwa Alice. Alice aliporudi, Vicenta alikuwa na hamu nyingi ya kumuuliza maswali. “Je! ‘Bikira Maria’ alikuwa na wana wengine?” “Jina la Baba ni gani? Sikuzote mimi nimetaka kujua lakini padri wetu husema kwamba jina lake si Yehova.” Mistari michache tu kutoka kwa Biblia yake mwenyewe ilijibu maswali yake. Akatosheka. (Mt. 13:53-56; Zab. 83:18) Ziara ya wakati unaofaa ya mwangalizi wa mzunguko na mke wake ilimpa msaada zaidi wa kibinafsi.
Kwa wakati uliopo, padri alipoona kwamba Vicenta alikuwa ameiacha dini ya Katoliki, alipanga afukuzwe hadharani kutoka kanisa. Siku moja alipokwenda sokoni, kikundi cha waliokuwa marafiki wake wa hapo kwanza walimzunguka na walitaka kumpiga kwa kuacha dini yake. Lakini mtu mmoja mjasiri aliyekuwa anasimama kando akaita polisi. Ilikuwa haiwezekani kabisa kwa yeyote kutoa ushuhuda nyumba kwa nyumba katika mji huu bila kupigwa mawe. Lakini Vicenta Granda alisema hivi: “Hata kama itagharimu uhai wangu, sitaacha kamwe kujifunza Biblia!”
Baada ya wakati yeye alihamia Machala, ambako ilikuwa rahisi zaidi kwake kufanya maendeleo kiroho. Katika 1961 yeye alibatizwa na baadaye mwaka uo huo akawa painia; yeye ameendelea katika utumishi wa wakati wote tangu hapo.
Baadaye, Joaquín Palas na mke wake walipewa mgawo kwenda Portovelo wakiwa mapainia wa pekee. Kwa kuwa hawakuwa tofauti, wao, pia, walipata upinzani mkali kutoka kwa padri, ambaye alihisi kwamba alitawala mji huu. Wakati mmoja padri alimwambia Joaquín kwamba ikiwa haondoki mjini kufikia tarehe fulani, padri angetuma watu wateketeze nyumba yake. Lakini kabla ya padri kutimiza tisho hili, nyumba yake mwenyewe ikashika moto!
Ijapokuwa jitihada za kukomesha kazi ya Ufalme katika mji huu, kundi lilianzishwa mapema katika miaka ya 1970, na leo ndugu zetu wanaweza kukutana na kuendeleza kazi yao ya kuokoa uhai kwa amani.
Si Wote Wanakubali Ukweli
Katika mandhari yenye uzuri wenye kuvutia sana kwenye miteremko ya magharibi ya Milima Andes kinakaa kijiji kidogo cha Pallatanga. Maruja Granizo alikutana na ukweli hapa kwa mara ya kwanza miaka 24 iliyopita wakati dada yake alipomtembelea. Yeye alivutiwa na yale yaliyosemwa juu ya ‘mwisho wa ulimwengu.’ Lakini yeye hakuitikia kwa upendeleo ule ule alipoambiwa kwamba jina la Mungu ni Yehova. Ijapokuwa hivyo, yeye bado alitaka kujifunza zaidi juu ya mambo ya kiroho. Kwa hiyo akamuuliza padri mwenyeji juu ya hali ya wafu na ufufuo. Padri yule alisukumia kando swali lake kwa dharau kwa kujibu kwamba watu wa aina ya pekee ambao huamini ufufuo ni wale wanaopatwa na jinamizi kwa sababu ya kula chakula kingi mno. Lakini jibu hilo la dharau halikupunguza kupendezwa kwake.
Baadaye dada yake alirudi pamoja na Nancy Dávila, dada kijana kutoka Machala. Nancy alikuwa na tabia yenye fadhili na upendo sana hivi kwamba Maruja alichochewa kujiambia mwenyewe hivi: ‘Huyu ndiye rafiki wa aina ninayotaka kwa ajili ya watoto wangu.’ Miongoni mwa maswali ya kwanza ya Maruja yalikuwa, “Wafu wako wapi? Na je! kuna ufufuo?” Maruja hukumbuka kwamba alipopata jibu kwamba wafu wamo makaburini wakingojea ufufuo na hawana fahamu, yeye alijawa sana na shangwe hivi kwamba alitaka kumwambia kila mtu ukweli huu mpya alioupata. (Mhu. 9:5; Yoh. 5:28, 29) Kwa hiyo yeye alimuuliza Nancy aandamane naye wazuru majirani wake kule juu milimani.
Lakini, kama ilivyokuwa katika maeneo mengine, padri alikuwa kama mfalme katika vijiji hivi. Hivyo walipokuwa njiani kutembelea kijiji ambako Maruja alizaliwa kule ndani sana milimani, kwa wazi maagizo ya padri yalikuwa yamewatangulia. Kwenye nyumba moja walipokewa na ishara kubwa iliyokuwa imechorwa maneno machafu.
Kwenye nyumba nyingine, mtu mmoja wa ukoo alisema hivi: “Padri asema kwamba wale wanaoenda huku na huku wakihubiri wapaswa wauawe kwa fimbo na mawe.” Maruja akajibu hivi: “Mkituua, basi ni nani ataenda gerezani—nyinyi au padri?”
“Ni sisi tutaenda,” akajibu yule mtu wa ukoo.
“Lakini fikirieni watoto wenu,” akasababu Maruja. “Ni nani atawaangalia mwendapo jela? Padri hajali ni nani anayeagiza auawe, kwa kuwa si yeye atatoa jibu. Sisi si mbwa. Tukiuawa, basi mtu fulani atafuatilia mashtaka nanyi mtalazimika kutoa jibu.”
Rekodi ya Uvumilivu
Baada ya kukaa miezi miwili katika Pallatanga, ilikuwa lazima Nancy arudi Machala, naye Maruja aliachwa tena peke yake akiwa pamoja na watoto wake wanne na mama mwenye umri mkubwa. Hata hivyo, yeye alihisi uhitaji muhimu wa kushirikiana na watu wa Yehova. Kwa hiyo alikwenda Riobamba akawatafute Mashahidi. Huko aliweza kuhudhuria kusanyiko la mzunguko na akabatizwa.
Kwa wakati fulani yeye alisafiri kwenda Riobamba kwa ajili ya ushirika wakati wowote alipokuwa na pesa. Baadaye, vijapokuwa vitisho vya majirani kudhuru Mashahidi au hata kuwaua, akina ndugu kutoka Riobamba walianza kumsaidia kutoa ushuhuda katika Pallatanga.
Mambo yalifikia upeo siku moja wakati akina ndugu kutoka Riobamba walipopanga kuonyesha mojapo sinema za Sosaiti katika uwanja wa mji wa Pallatanga. Mambo yote yalikuwa shwari mpaka jina Yehova lilipotajwa kwa mara ya kwanza. Ghafula watu wakaanza kupaaza sauti hivi: “Afadhali Maruja Granizo aondoke hapa, la sivyo sisi hatutachukua daraka la uhai wake!” Mtu fulani alirarua ile shiti iliyokuwa imeangikwa iwe kiwambo kwa ajili ya kuonyeshea picha kwa projekta. Kengele za kanisa zilianza kulia kana kwamba zinapigwa na mtu mwenye kichaa, nao watu wakaanza kutoka kwenye nyumba zao wakiwa na fimbo na mawe mikononi. Hivyo akina ndugu wakakusanya vifaa vyao mbiombio wakapanda basi waondoke mjini. Basi lilipokuwa likianza mwendo walihesabiwa kila mmoja, na ikaonekana kwamba Shahidi mmoja, Julio Santos, hayupo! Je! alikuwa ameshikwa na wale wanaghasia?
Ghafula wakaona mwanamume mnene akikimbia kuelekea kwenye basi, akiongoza wanaghasia, akitupa mawe, na kupaaza sauti hivi: “Wapigeni kwa fimbo na mawe!” Alikuwa Julio! Kwa njia fulani wanaghasia walikuwa wamemtenganisha na basi, hivyo kwa ujanja wa kufa na kupona ili ajiponyoe, Julio alijifanya kuwa mmoja wao. Alipolifikia basi, akaruka ndani, nao wakaenda zao kuelekea Riobamba.
Maruja na jamaa yake walikuwa pia wameingia ndani ya basi kwa ajili ya usalama. Lakini walipokuwa nje ya kijiji, wakashuka na kuanza kurudi nyumbani. Wangefauluje kufika nyumbani? Wanaghasia walikuwa wakiwatafuta. Mara kadhaa walilazimika kujificha wakati wanaghasia walipopita mbio karibu nao. Hatimaye usiku sana wakawasili nyumbani salama.
Ni nini yamekuwa matokeo ya uvumilivu wa miaka 24 katika eneo hili lililo peke yalo? Kwanza kabisa, yule padri aliyetokeza matata mengi sana katika Pallatanga alifukuzwa miaka 20 baadaye na watu wale wale wa mji, ambao walimshtakia ukosefu wa adili na wizi. Pole kwa pole watu wamekuwa wenye kuitikia sana ujumbe wa Biblia. Ingawa bado kuna kikundi kidogo tu hapa kilicho peke yacho, Maruja mwenyewe huongoza mafunzo ya Biblia 11. Katika 1987 mkahawa mkubwa ulipatikana kwa ajili ya Ukumbusho, na 150 walihudhuria. Ndiyo, Pallatanga ni Makedonia ya ki-siku-hizi, inayokingwa na milima yenye mandhari ya kuvutia sana, ikisihi tu kwamba mtu fulani avuke na kusaidia kikundi hiki kidogo kuhubiri habari njema kotekote katika eneo lacho kubwa mno.
‘Dini Pekee Ambayo Ina Ukweli’
Watu fulani, kama vile Jorge Salas, aliyeishi katika Ibarra, hata walikuwa wakitafuta Mashahidi wa Yehova. Kwa nasibu yeye alisoma kitabu kiitwacho La Gran Obra (Ile Kazi Kubwa), kilichoandikwa na Dakt. mmoja jina lake Berrocochea aliyeishi Uruguay wakati ule. Miongoni mwa mambo mengine, kitabu kile kilitaarifu kwamba dini pekee ambayo ina ukweli ilikuwa Mashahidi wa Yehova. Hiyo ndiyo Jorge alitaka. Kwa hiyo yeye aliamua kwenda Quito akawatafute Mashahidi, na wasipopatikana kule, yeye angeenda Guayaquil, au hata Uruguay ikihitajiwa kabisa.
Kule Quito, yeye alianza kutafuta Mashahidi saa 11:30 asubuhi. Alipochoka kutembea, alikodi teksi. Dereva wa teksi alipochoka kumbeba, alikodi mwingine. Adhuhuri yule dereva wa pili alikuwa anaanza kuona njaa naye alitaka kuacha. Hata hivyo, Jorge akasisitiza kwamba waendelee.
Hatimaye mtu fulani akamwonyesha mahali alipoishi Shahidi mmoja, na kutoka hapo yeye akasindikizwa kwenye lango la makao ya kimisionari. Arthur Bonno, aliyekuwa mpishi siku hiyo, akaja mlangoni akiwa amevalia aproni yake akamkaribisha ndani. Jorge akafikiri hivi: ‘Ikiwa mpishi ni mwana-ng’ambo na amevalia vizuri hivi, misionari ambaye atanitumikia atakuwaje?’ Baada ya muda mfupi misionari mmoja mwenye sura yenye kuonyesha sana kuwa ya Kihindi akawasili kumtumikia. Huyu alikuwa Pedro Tules. Kwa mara nyingine tena Jorge akashangaa akajiuliza, ‘Hii inaweza kuwa dini ya aina gani, ambayo Wahindi hutumikiwa na watu weupe?’ Yeye angegundua kwamba hii si ndiyo njia pekee ambayo katika hiyo Mashahidi wa Yehova ni tofauti. Upesi yeye mwenyewe aliacha maisha yake ya ukosefu wa adili, akafunga ndoa tena na mke wake aliyetalikiwa, na akaweza kumsaidia pamoja na walio wengi wa watoto wao wakubali ukweli.
Tofauti na Jorge, walikuwako watu fulani ambao hapo kwanza waliona afadhali Mashahidi waende zao.
Mfanya Biashara Mpolandi
Katika Guayaquil, John na Dora Furgala, waliokuwa wamehama kutoka Polandi, waliendesha duka la vifaa vya ujenzi lililojulikana sana na wajenzi, maseremala, na mafundi wote wa mabomba mjini. Zola Hoffman alimwangushia Dora trakti na akarudi wakati wa mwisho-juma kufanya ziara. Hata hivyo, John, mume wa Dora hakupendezwa kuona siku yake ya mapumziko ikikatizwa. Kwa hiyo yeye alikubali vitabu vyote alivyokuwa navyo Zola katika mfuko wake wa kutolea ushuhuda, akifikiri kwamba hiyo ingemaanisha hakutakuwa na ziara zaidi, kwa kuwa hatakuwa na kinginecho cha kuwatolea. Hata hivyo, Zola alituma misionari mmoja aliyesema Kipolandi, na funzo likaanzishwa pamoja na Dora.
Baadaye wakati akina Furgala walipoalikwa kwenye mikutano ya kundi, John alijibu hivi: “Dora aweza kwenda na kuniambia aliyojifunza.” John hakupata kuwa na shauku juu ya Biblia mpaka alipopatwa na pigo dogo la moyo naye daktari akamwagiza akae kitandani kwa siku 15. Ili ashughulishe akili yake, yeye alianza kusoma Biblia na vile vichapo. Ghafula, alihisi kama mtu anayefunguliwa macho yake kwa mara ya kwanza. Kila siku alikuwa akimwita mke wake na kusema: “Hei! Tazama! nimegundua jambo fulani jipya!” Upesi wote wawili wakabatizwa. Lakini kwa sababu ya biashara yao ya vifaa vya ujenzi, je! John angeweza kweli kuupa utumishi wa Yehova mahali pa kwanza?
Kwa John Furgala, kuwa mwanabiashara mashuhuri hakukuwa kizuizi kwa sababu yeye hakuaibikia habari njema. (Mt. 10:32, 33) Kuongezea vyombo na vifaa vya ujenzi vyake, yeye alisimamisha kiweko chenye kuvutia cha kuonyeshea vichapo vya Mnara wa Mlinzi. Wakati msaidizi wake alipokuwa akitimiza agizo la mteja, John alikuwa akimtolea ushuhuda. Katika siku zile ilikuwa desturi kumpa mteja bakshishi wakati aliponunua kiasi fulani cha vifaa. Badala ya hivyo, John alikuwa akimtolea mtu andikisho la bure la magazeti yetu. Halikuwa jambo lisilo la kawaida kwake kuangusha maandikisho 60 au zaidi katika mwezi mmoja.
Mwanasiasa Akubali Haki ya Kweli
Watu wa kila namna ya maisha—matajiri na maskini, wale walio gerezani na wale walio mashuhuri katika huu mfumo wa mambo—wanahitaji kupewa fursa wasikie ukweli. Rafael Coello alikuwa mmoja aliyekuwa akitafuta haki ya kijamii tangu ujana wake. Jambo hilo lilimfanya awe mwanachama wa Chama cha Kikomunisti katika 1936. Kwa miaka saba akashiriki machafuko na mateto. Akizinduka, yeye alikana kabisa uanachama pamoja nao akajitia katika vyama vingine kadhaa. Humo yeye alipata sifa mbaya na umashuhuri pia. Wakati mmoja alitajwa na rais wa Ekwedori kuwa balozi kwenye mkutano wa pekee wenye kuelekezwa na Umoja wa Mataifa. Na bado wakati mwingine, wakati chama cha upinzani kilipochukua mamlaka, alitiwa gerezani. Ilikuwa hapa katika jela kwamba Albert Hoffman alimtembelea na kumwachia kile kitabu “Let God Be True.”
Miaka saba baadaye mwanamume mwenye sura yenye fadhili alizuru makao ya Rafael Coello, ambaye husimulia hivi: “Mimi nilitambua mara hiyo kwamba alikuwa mtu fulani ambaye nilikuwa nimekuwa nikingojea bila mimi kujua. Albert Hoffman alikuwa akinitafuta tena.” Funzo lilianzishwa katika kitabu “This Means Everlasting Life.” Haikumchukua Rafael muda mrefu kupata jambo alilokuwa akitafuta miaka yote hiyo—uelewevu wa kwamba haki ya kweli itakuja kwa njia ya Ufalme wa Mungu tu. Ubatizo wake katika 1959 ulichochea kadiri fulani ya msisimuko, kwa kuwa yeye alikuwa amejulikana sana kuwa mwanasiasa kwa zaidi ya miaka 20.
Kama vile alivyokuwa mpiganiaji mwenye sulubu wa haki ya kibinadamu, sasa akawa mteteaji imara wa haki ya kimungu. Akitazama nyuma kwa muda wa miaka iliyopita, Ndugu Coello hukumbuka hivi: “Mimi nimependelewa kusema juu ya haki ya Yehova kwa watu wa vyeo vyote, kuanzia na waliokuwa marais hapo kwanza mpaka vibarua dhalili sana.” Akiwa anafahamiana sana na Palacio de Justicia (Jumba la Hukumu) katika Guayaquil kwa sababu alikuwa ametumikia humo akiwa hakimu katika mahakama ya rufani, yeye alirudi humo kutolea ushuhuda kila mmoja wa wale mahakimu na wanasheria wengi. Kama tokeo, akawa na watu wengi sana wa kupelekea magazeti waliokuwa hapo kwanza wafanya kazi wenzake.
Udugu wa Kimataifa
Kwa sababu akina ndugu wamepanda kwa wingi sana na wakamwagilia maji mbegu za ukweli wa Ufalme, watu wa aina zote wamesikia habari njema. Lakini ni Yehova ambaye ametoa ongezeko. (1 Kor. 3:6) Roho yake ikifanya kazi juu ya tengenezo lake lote lionekanalo imefanya hilo liwezekane.
Kwa kitia-moyo kilichopokewa kwenye Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Kimataifa 1958 katika New York, ndugu wengi walikuja Ekwedori kutumikia mahali ambako uhitaji ni mwingi zaidi. Wakati ziara ilipofanywa na msimamizi wa Sosaiti katika 1959, yeye aliongea na watu 120 waliokuwa wamekuja kutoka nchi za kigeni. Wapya wengi waliletwa kwenye maarifa ya ukweli kupitia jitihada zao. Baadhi yao walisaidia kuanzisha makundi mapya na kuzoeza ndugu wenyeji kwa matokeo mazuri kwa ajili ya madaraka ya kundi.
Katika 1967 Mashahidi Waekwedori walipata kwa njia nyingine bado ono la uhalisi wa udugu wetu wa kimataifa. Hiyo ilikuwa pindi gani? “Wana wa Mungu wa Uhuru” Kusanyiko la Kimataifa lililofanyiwa Guayaquil. Waliokuwapo kwenye kusanyiko hili walikuwa wakurugenzi wa Sosaiti pamoja na ndugu wenye kuzuru wapatao 400 kutoka nchi mbalimbali. Ulikuwa ushirika wenye shangwe kama nini pamoja na ndugu Waekwedori na watu wenye kupendezwa zaidi ya 2,700! Maneno mengi sana ya uthamini yalisikika kutoka kwa ndugu wenyeji na kutoka kwa wale waliozuru kutoka ng’ambo pia.
Roho Tofauti Katika Cuenca
Katika mwaka 1967 ilionekana inafaa kufanya jitihada nyingine ya kuanzisha habari njema katika Cuenca, jiji kubwa zaidi la tatu la Ekwedori. Hilo lingefanywaje? Mwanzoni, Carlos Salazar alitumwa kule akiwa painia wa pekee. Muda mfupi baada ya hapo, wahitimu wanne wa karibuni wa Gileadi wakawasili pia—Ana Rodriguez na Delia Sánchez wa Puerto Riko, pamoja na Harley na Cloris Harris kutoka United States.
Wakati ule shahidi pekee mwenyeji katika jiji hili la wakaaji zaidi ya 100,000 alikuwa Carlos Sánchez, kijana mwanamume aliyekuwa amepooza tokea kiunoni kwenda chini kutokana na aksidenti ya motokaa miaka kadhaa kabla ya yeye kujifunza ukweli. Kwa ajili ya kila mkutano wamisionari walikuwa wakimbeba kumteremsha kutoka chumba chake, na kumkalisha juu ya moto-skuta, kisha kumbeba kumpeleka orofa ya juu kwenye Jumba la Ufalme. Uso wake wenye tabasamu na mwelekeo wa kutazamia mazuri vilikuwa kitia-moyo halisi kwa kikundi hiki kidogo.
Kumbuka, Cuenca lilikuwa na sifa ya kuwa jiji la Kikatoliki lililo imara zaidi ya yote katika Ekwedori yote. Mojapo mambo ya kwanza yaliyonasa uangalifu wa wamisionari lilikuwa ile hesabu yenye kushangaza ya makanisa. Ilielekea kwamba kila mwendo wa majengo manne au matano ya mjini ulikuwa na kanisa moja. Nayo kathedro kubwa mno iliyokuwa kwenye uwanja mkubwa mjini ilikuwa inayazidi yote. Kila asubuhi muda mrefu kabla ya mapambazuko wamisionari waliamshwa na kengele za kanisa, zilizoita watu waje kwenye Misa ya mapema asubuhi. Wakati wa lile lililojulikana kuwa Juma Takatifu, mifano kutoka kwa yale makanisa mbalimbali ilichukuliwa nje na kufanyiwa gwaride kwenda juu na chini katika barabara za Cuenca. Ilikuwa ikichukua siku nzima kumaliza mwandamano huu wa mifano.
Kwa hiyo ilikuwa kwa tahadhari kubwa kwamba kikundi hiki kidogo cha Mashahidi kikaanza kufanya kazi nyumba kwa nyumba. Hadithi za vikundi vya wanaghasia wenye kurusha mawe zilikuwa zingali zinakaa-kaa akilini kutokana na jitihada za wakati uliopita za kufanyia kazi sehemu fulani fulani za jiji. Hata hivyo, kwa mshangao mkubwa wa wamisionari, hakuna jambo kama hilo lililotukia sasa. Tofauti kabisa na hilo, watu waliwakaribisha ndani ya nyumba zao katika ziara ya kwanza na kuchukua fasihi nyingi. Watu walikuwa wanakufa njaa kiroho.
Kuhusu mmojawapo mapadri wenye kupendwa na watu wengi katika Cuenca, Harley Harris husimulia hivi: “Daima sisi tulikuwa tukisikia juu ya padri mmoja kutoka Hispania jina lake Juan Fernández. Yeye hakuafikiana na askofu wa Cuenca kwa sababu alikataa kutoza bei tofauti kwa ajili ya namna tofauti za Misa. Kwake, Misa ilikuwa sawa. Tatizo lilikuwa kwamba yeye hakuwa akichuma pesa za kutosha kumtosheleza askofu huyo. La pili, yeye aliondoa karibu mifano yote katika kanisa lake. Hilo lilishangiliwa na wale Wakatoliki wenye kupendelea zaidi mabadiliko, hali wale wasiopendelea mabadiliko walichukizwa.
“Ndipo siku moja bibi mmoja akatuambia juu ya jirani yake aliyekuwa amekataa kutusikiliza na kisha akaripoti jambo hilo kwa Fernández yule padri. Kwa mshangao wake na wa wengine, yeye alimchambua peupe wakati wa Misa na kuwaambia wale waliokuwapo kwamba ikiwa yeyote anakuja penye milango yao akizungumza juu ya Biblia, yawapasa kusikiliza, kwa kuwa Biblia ina ukweli.
“Mimi niliamua yanipasa kukutana na padri huyu, na baada ya jitihada fulani niliweza kupata anwani ya kao lake. Nilimtolea mwaliko aje kwenye makao yetu na nilifurahia kumkaribisha kwa ziara ya saa mbili. Kwa kushangaza, yeye alikuwa na maarifa fulani ya baadhi ya mafundisho ya msingi ya Biblia. Nilipomuuliza yeye alifikiri Mkristo apaswa kuchukua msimamo gani kunapokuwa na pambano la kisiasa kati ya mataifa mawili, yeye alijibu mara moja: ‘Kuna msimamo mmoja tu ambao Mkristo anaweza kuchukua nao ni kutokuwamo, kwa sababu mmoja hawezi kutii amri ya Yesu ya kupenda na aue wakati ule ule.’ Mazungumzo yale yalimalizika kwa msingi mchangamfu na wa kirafiki, naye aliomba hesabu fulani ya vichapo vyetu.”
Hata hivyo, kwa sababu ya bishano lake na askofu, yeye alinyang’anywa wajibu wake wa kuwa padri na kurudishwa Hispania juma ilo hilo. Maelezo yake yalikuwa yamelegeza vifungo vya kiakili vya wengi wa watu wa mjini ambao baadaye walisikiliza ujumbe wa Biblia.
Ingawa hivyo, kulikuwako kitu fulani kilichoelekea kuwazuia watu wale wasichukue msimamo imara kwa ajili ya ukweli. Wengi walikuwa wakijifunza Biblia na kuja kwenye mikutano; lakini ilipofikia wakati wa kwenda nje katika utumishi wa shambani, karibu kila mtu hakuwa na ujasiri wa kufanya hivyo. Tulifikia uamuzi wa kwamba ilikuwa kuhofu jirani. Ni jambo gani lingeweza kusaidia kushinda kizuizi hiki?
“Mama, Mimi Siwezi Kufa Sasa”
Bob na Joan Isensee, waliokuwa wamisionari hapo kwanza, waliamua kulea jamaa yao katika Cuenca. Wakati Mimi, binti yao wa miaka 10 alipokuwa akicheza shuleni siku moja, alipondwa chini ya magurudumu ya lori lililokuwa limepakiwa takataka. Alikimbizwa mbiombio kwenye kliniki. Jitihada za kufa na kupona zilifanywa ili kuokoa uhai wake. Mama yake mwenye hangaiko alipowasili, Mimi alikuwa angali ana fahamu zake naye akamnong’onezea mama hivi: “Mama, mimi siwezi kufa sasa. Hata sijaongoza funzo la Biblia moja!” Na kwa hiari yake mwenyewe mtoto yule akawaambia wauguzi kwamba yeye hataki damu yoyote itumiwe katika kumtibu. Hilo lilikuwa ndilo ono la kwanza la kliniki hiyo kuhusiana na Mashahidi wa Yehova. Nalo lilithibitika kuwa moja lisilosahaulika.
Daktari akawasili. Yeye alisema kwamba upasuaji ulihitajiwa kabisa ili kujua ni dhara gani lililokuwa limefanywa katika viungo vya ndani. Baba alieleza kwamba hilo lilikuwa sawa kabisa, lakini “Tafadhali, damu isitumiwe, kwa sababu Biblia hukataza tumizi la damu kwa namna yoyote!” (Mdo. 15:28, 29) Daktari yule alishtuka sana. Alikuwa hajapata kamwe kuelekeana na upasuaji hatari kama huu pamoja na ombi la kwamba damu isitumiwe. Baba alisema kwamba hili lilikuwa daraka lake akiwa mzazi na si la daktari-mpasuaji. Yeye angekubali daraka kamili kwa ajili ya matokeo. Jambo pekee aliloomba ni kwamba, bila kuhalifu sheria ya Mungu juu ya damu, daktari afanye yote awezayo kuokoa uhai wa mtoto.
Kwa unyenyekevu daktari akajibu: “Kwa kuwa nina imani zangu mwenyewe za kidini na ninataka wengine wazistahi, mimi nitastahi zako. Nitafanya yale niwezayo.”
Kabla tu ya kupelekwa ndani ya chumba cha upasuaji, Mimi alimwambia baba yake hivi: “Usijali, Baba. Nimekwisha kusali kwa Yehova.”
Zaidi ya saa tano ndefu zikapita. Katika pindi ya wakati huo watu wengi waliojua jamaa ile au waliosikia habari ya aksidenti ile walikuja kwenye kliniki na kungojea matokeo. Kwa wakati uliopo wazazi walikuwa wakiwaeleza kwamba ikimpasa mtoto wao kufa, walikuwa na uhakikisho wa kumwona tena katika ufufuo. Hilo lilikuwa na tokeo gani kwa wengine?
Maneno kama haya yalisikiwa: “Mimi ni baba pia nami najua linalomaanishwa na kumpoteza mtoto; lakini wewe unaonyesha utulivu zaidi juu ya tukio hili kuliko vile mimi ningefanya.” Mwingine akasema: “Kama mimi ningekuwa na imani kama watu hawa, mimi ningekuwa mtu mwenye furaha zaidi anayeishi.” Jirani wa karibu, ambaye mume wake alikuwa amekufa wakati fulani kabla ya tukio hili, alikuja kuwafariji naye akaenda zake akiwa amefarijiwa mwenyewe. Alisema hivi: “Kwa miaka miwili, tangu kifo cha mume wangu, mimi nimeshuka moyo; lakini kuona nyinyi na imani yenu katika Mungu na tumaini mlilo nalo kumeniwezesha kupata furaha kwa mara ya kwanza.”
Lakini namna gani juu ya mtoto? Hatimaye ule upasuaji mrefu ukamalizika, nao wazazi wenye kuhangaika wakamkaribia daktari wapate ripoti yake. Madhara makubwa sana yalikuwa yamefanywa kwenye viungo vya ndani. Mshipa arteri uendao kwenye diaframu (kiwambo cha moyo) ulikuwa umekatika na zaidi ya nusu ya damu yake ilikuwa imepotezwa. Ini lilikuwa limekatwa-katwa katika sehemu mbalimbali. Kwa sababu ya mbano mwingi sana, tumbo lilikuwa limelazimishwa kutoka nje kupitia diaframu. Lile lori lilisimama kabla tu ya kupasua moyo.
Daktari alisema kwamba alithamini mwelekeo wa utulivu wa wazazi, kwa kuwa jambo hilo lilimwezesha kuanza upasuaji akiwa katika hali ya akili iliyotulia zaidi. Mimi alipata nafuu kwa muda mfupi sana, kwa mfurahio mwingi wa kila mmoja. Ono hilo lote lilitokeza ushuhuda mkubwa sana kwa kuwa habari zilisambaa kotekote jijini Cuenca. Stesheni ya redio ilisema habari ya imani yenye kutokeza na utulivu wa jamaa ya Isensee. Daktari mmoja mashuhuri alimwambia baba yule hivi: “Inakupasa kujua kwamba kisa hiki kinasemwa kuwa mwujiza halisi miongoni mwa watu wa jamii ya kitiba.”
Mwendeshaji Baiskeli Aingia Katika Mbio Tofauti
Mario Polo, mkaaji wa maisha wa Cuenca, alikuwa na sifa sana kwa kushinda shindano la kuendesha baiskeli la taifa zima miaka kadhaa mfululizo na akastaafu bila kushindwa. Kwa sababu nzuri, jiji la Cuenca lilijivunia sana mwana walo mwenyeji.
Wakati Norma, mke wa Mario alipoanza kujifunza pamoja na Mashahidi, yeye aliamua kukaa mara moja aone kama maswali yake mwenyewe yangejibiwa. Jambo la kwanza alilotaka kujua lilikuwa: “Ni nani yule kahaba anayetajwa katika kitabu cha Ufunuo?” (Ufu. 17:3-5) Yule misionari akajibu kwamba kwa kawaida sisi huanza na mambo rahisi zaidi ya Biblia. Lakini, kwa kuwa Mario alikuwa ametokeza swali hilo, misionari alieleza kwamba Biblia hutumia mfano wa mwanamke mwasherati anayeitwa Babuloni Mkubwa kuwakilisha shirika la ulimwenguni pote la dini ambazo hazijitengi na ulimwengu.—Yak. 4:4; Ufu. 18:2, 9, 10.
Tokea hapo na kuendelea, Mario akapendezwa sana na funzo la Biblia na akafanya jitihada kubwa kuhudhuria hata ingawa kazi yake ilikuwa umbali fulani kutoka mjini. Ndipo usiku mmoja yeye akaja kwenye makao ya kimisionari akiwa na uso wenye hangaiko. Yeye alikuwa amepata fasihi fulani kutoka kwa Waevanjeli ambayo ilishtaki Mashahidi wa Yehova vikali. Misionari alijibu kwamba ikiwa mashtaka hayo yaliyo dhidi yetu yalimhangaisha, njia bora ya kujibu mashtaka hayo ingekuwa kumwomba Mwevanjeli mmoja awepo aone kama angeweza kuyategemeza. Jambo hilo lilionekana kuwa haki kwa Mario. Kwa hiyo yeye na ndugu yule wakamtembelea yule pasta Mprotestanti aliyekuwa akigawanya fasihi ile.
Mario aliomba kwamba pasta aje nyumbani kwake atetee aliyokuwa amesema dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Alikuwa na wajibu wa kukubali mwaliko ule, la sivyo kutokuwapo kwake kungekuwa kukiri kwamba mashtaka yale yalikuwa ya bandia.
Walikuwapo watu kumi, kutia na marafiki na watu wa ukoo wa Mario, wakingojea wakati yule pasta akiandamana na mhubiri mwingine kutoka kanisa lake walipojitokeza. Utatu ulichaguliwa uzungumziwe. Kila wakati andiko liliponukuliwa ili kuunga mkono fundisho lile, Mario, mke wake, au mmojapo marafiki wao alikuwa akionyesha pasta kwa nini andiko hilo halikutumika. Misionari alisema machache sana.
Baada ya nusu saa hivi, yule pasta akatazama saa yake na kusema kwamba alikuwa na mwadi mwingine. “Lakini, Bwana, bado hujathibitisha jambo lolote,” akalalamika mmoja wa waliokuwapo. “Usituambie kwamba sasa unatuacha bila ulinzi dhidi ya mbwa-mwitu hawa, kama unavyowaita!” Yule pasta akaondoka, akisema kwamba angefanya mpango kwa wakati ujao, lakini yeye alikataa kujifunga wajibu kuhusu huo ungekuwa wakati gani.
Yeye alirudi siku moja akamwambia Norma Polo kwamba angerudi—lakini wakati ambapo Mashahidi wa Yehova hawapo. Hilo lilionekana kuwa jambo lisilo la haki kwa Mario, naye akaenda nyumbani kwa yule pasta na kumwaarifu kwamba angekaribishwa nyumbani kwake wakati tu Mashahidi wa Yehova wangekuwapo ili wajitetee. Sasa ilikuwa wazi kwa Mario ni nani waliokuwa na ukweli na ujasiri wa kuutetea.
Tokea wakati huo na kuendelea, Mario alizidi kufanya maendeleo bila kusita. Kabla ya muda mrefu yeye akaanza kushiriki huduma ya shambani papo hapo katika ujamii wake mwenyewe, na baadaye mke na binti yake wakajiunga pamoja naye.
Wakaaji wenyeji mbalimbali wa jiji lile walipoanza kujitambulisha wenyewe kuwa Mashahidi wa Yehova, athari juu ya wengine ilikuwa kubwa sana. Madaktari, wanasheria, watengenezaji vito, wakulima—watu mamia mengi kutoka katika kila namna ya maisha katika Cuenca—wamekubali ukweli sasa. Miaka ishirini iliyopita hakukuwa na kundi katika Cuenca. Sasa kuna makundi 11 katika eneo hili. Katika barabara za jiji ambako maandamano ya kidini yalikuwa yakiendelea kwa siku nzima wakati wa lile lililoitwa eti Juma Takatifu, dakika chache tu ndizo zinazohitajiwa kuona ni nini kinachopita—visalio vya enzi iliyopita. Kwa kutofautisha, sasa jina la Yehova linajulikana kutoka mwisho mmoja wa mkoa hadi ule mwingine.
Uhitaji: Kitia-Moyo
Wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya 1960 na ya mwanzo-mwanzo ya 1970, kazi ya Ufalme katika Ekwedori iliingia katika pindi ya upanuzi wenye amani. Uvutano wa dini nyinginezo, pamoja na uwezo wazo wa kuchochea watu ulipungua. Wahubiri walikuwa wakifanya kazi kwa bidii kueneza habari njema za Ufalme katika kila ncha ya nchi.
Katika 1963 walikuwako wahubiri 1,000 wakitenda katika huduma ya shambani. Miaka mitano baadaye hesabu hiyo ilikuwa imefikia 2,000. Kufikia 1971 jumla ilikuwa imepanda kufikia 3,000. Katika muda wa miaka mingine miwili tuliripoti wapiga mbiu ya Ufalme 4,000; mwaka uliofuata ilikuwa 5,000, na kufikia Oktoba 1975 tulikuwa tumefikia kilele cha 5,995.
Hata hivyo, ndipo, kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mingi, upungufu ukaingia. Kufikia 1979 jumla ya hesabu ya wahubiri watendaji wa habari njema ilikuwa imeshuka kufikia hesabu inayozidi kidogo tu 5,000. Ni jambo gani lilikuwa likitendeka? Inaelekea kwamba baadhi ya wale wapya hapa walikuwa wamechukuliwa na idili juu ya tarehe badala ya kujenga uthamini wa kweli kwa Yehova na njia zake. Kwa vyovyote, kufikia 1980 kulikuwako tena ongezeko kidogo na tena katika 1981, lakini maendeleo yalikuwa ya polepole.
Ni nini kilichokuwa kikizuia ongezeko, wakati nchi baada ya nchi ilikuwa sasa ikiripoti ukuzi mzuri katika eneo layo? Uasi-imani ulikuwa haujapata kusikiwa hapa. Kwa wazi hakukuwa na uchafu wowote ambao ungemfanya Yehova asitoe roho yake. Fikira nyingi ya sala ilielekezewa jambo hilo. Mataraja ya ukuzi yalikuwa mazuri sana, kwa kuwa 26,576 walihudhuria Ukumbusho katika 1981—wastani wa watu 5 wenye kupendezwa kwa kila mhubiri wa Ufalme.
Iliamuliwa kwamba kile ambacho ndugu zetu walihitaji kikweli ni kitia-moyo. Wazee na watumishi wa huduma walihitaji kukumbushwa juu ya daraka lao la kuongoza shambani. Wale waliokuwa wamekuwa wasiotenda walihitaji kuwa na funzo la Biblia likiongozwa pamoja nao kuwasha tena uthamini wao kwa ajili ya vitu vya kiroho.
Hivyo baada ya ripoti ya mwaka wa utumishi wa 1981 kujumlishwa pamoja, Halmashauri ya Tawi ilipanga kuwaalika wazee na watumishi wa huduma wote kwa mikutano mifupi katika majiji maalum kotekote nchini. Akina ndugu walishangilia sana habari zilizoshirikiwa pamoja nao. Kila mmoja aliondoka akiwa na roho iliyotiwa nguvu mpya kwa ajili ya kazi. Tokeo likawa ongezeko la asilimia 14 katika wahubiri na asilimia 19 katika mafunzo ya Biblia ya nyumbani kwa mwaka huo wa utumishi. Hudhurio la Ukumbusho liliruka asilimia 28, kufika 34,024! Kweli kweli mashamba yalikuwa meupe tayari kuvunwa.
Mvua Nyingi Sana
Sasa shida nyingine ikajitokeza. Kwa miezi kumi mfululizo, kutoka Oktoba 1982 mpaka Julai 1983, nchi ile ilipata mvua kubwa na mfuriko ambao haujapata kukumbukwa kwa miaka mia moja iliyopita. Katika Guayaquil na maeneo yanayozunguka, zaidi ya inchi 100 za mvua zilirekodiwa katika muda wa miezi michache. Madaraja yalifagiliwa mbali, miji ikaachwa imejitenga. Uwasiliano ukawa mgumu sana. Majumba ya Ufalme pamoja na nyumba za akina ndugu ziliharibiwa.
Lakini akina ndugu walipiga moyo konde kuendelea kufanya mikutano yao. Katika Babahoyo, ili wafike kwenye mikutano baadhi yao walilazimika kupitia katika maji yaliyokuwa yanawafika kiunoni. Kusini zaidi, katika Milagro, maji yalikuwa na kina cha kufika karibu magotini mle mle ndani ya Jumba la Ufalme. Lakini akina ndugu walikunja suruali zao tu wakashangilia mikutano ijapokuwa furiko.
Jitihada za moyo zilifanywa ili kudumisha uwasiliano na ndugu zetu, hata wale waliokuwa katika maeneo yaliyo peke yayo. Ilipojulikana kwamba baadhi yao hawakuwa na chakula na mahitaji mengineyo, tawi liliyajulisha makundi, nao ndugu zetu wenyeji wakaitikia kwa ukarimu. Kutoka kotekote nchini, akina ndugu waliandaa kwa fadhili pesa, chakula, mavazi, na dawa zilizohitajiwa. Katikati ya pindi hii yenyewe ya mvua isiyokoma, tawi liliratibu mkutano mwingine pamoja na wazee na watumishi wa huduma. Maono yenye kutia moyo yalishirikiwa, na madokezo yakatolewa kuhusu jinsi kazi ya kuhubiri ingeweza kuendelezwa ijapokuwa hali ya hewa ya mvua-mvua. Maneno ya Paulo yalionekana kufaa sana: “Lihubiri neno, fanya hivyo kwa haraka katika majira yanayofaa, katika majira yenye taabu.”—2 Tim. 4:2, NW.
Tokeo likawaje? Ripoti kutoka mengi ya makundi yaliyokuwa yameathiriwa vibaya na hali ya hewa yalionyesha maongezeko yenye kutokeza. Mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1983, ijapokuwa mvua, ndugu zetu walikuwa na wastani wa ongezeko la asilimia 17 katika wahubiri na walikuwa wamefikia kilele kipya cha 7,504. Katika pindi ii hii ya wakati, mafunzo ya Biblia ya nyumbani yaliruka kufikia asilimia 28! Kadiri ndugu zetu walivyozidi kufanya kazi katika eneo, ndivyo lilivyotokeza zao zaidi.
Uhitaji wa Kupanua Vifaa vya Tawi
Kazi ya Ufalme katika Ekwedori ni changa zaidi ikilinganishwa na kazi katika nchi nyingine nyingi. Utendaji wa kuhubiri wenye kuendelezwa ulianza muda unaozidi kidogo tu miaka 40 iliyopita. Kama vile ukuzi wa mtoto hutaka seti mpya za mavazi, ndivyo kupanuka kwa kazi ya Ufalme hapa kumefanya ihitajiwe kabisa kupata vifaa vikubwa zaidi vya tawi.
Mwanzoni ofisi ya tawi ilifanya kazi kutoka tu makao ya kimisionari. Kufikia 1957 vifaa vipya vilijengwa katika Guayaquil. Baadaye jengo hilo liliongezewa ukubwa. Katika 1977, wakati wa ziara yake ya eneo la dunia, Ndugu Grant Suiter alidokeza kwamba akina ndugu waanze kutafuta kisehemu cha uwanja kikubwa zaidi nje ya Guayaquil. Siku moja ndugu mmoja alikuja kwenye ofisi ya tawi na kutuuliza kama tungependezwa na kisehemu cha ardhi ambacho angependa kukitoa kama zawadi kwa Sosaiti. Kilikuwa nje tu ya Guayaquil. Tulisisimuka kama nini kukubali toleo hili!
Uhitaji mwingine wenye umuhimu katika wakati huo ulikuwa mahali ambapo makusanyiko ya wilaya yangeweza kufanyiwa—hata kama palikuwa mahali peupe. Baada ya kufyeka kwanza kisehemu hiki kipya cha ardhi, kusanyiko la kwanza likafanyiwa hapo. Upande ulioinuka wa kilima uliandaa uwanda-duara asilia, na akina ndugu walitandaza blanketi zao juu ya ardhi wazikalie. Kwa miaka kadhaa uwanja huu ulitumika kwa ajili ya makusanyiko ya wilaya na ya mzunguko ya upande wa pwani.
Hatimaye, mwishoni mwa 1984, kazi ikaanza ya kujenga Jumba la Kusanyiko zuri sana kwenye uwanja huu. Lingekuwa na nafasi ya kukaliwa na watu 3,000. Eka zaidi ya 80 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi huu. Hata hivyo, kilichohitajiwa kilikuwa zaidi ya Jumba la Kusanyiko. Kwa kibali cha Baraza Linaloongoza, mapema katika 1985 ujenzi wa jengo la tawi jipya ulianza kwenye sehemu nyingine ya ardhi ii hii. Ulikuwa wakati wenye kusisimua kama nini akina rafiki walipokuwa wakipata baraka za Yehova juu ya jitihada zao za kuumaliza ujenzi wote huu! Ujenzi ulianza kabla tu ya kuanzishwa kwa programu ya ujenzi ya kimataifa ya Sosaiti, lakini jengo hilo lilimalizwa chini ya mwelekezo wao. Akina ndugu walifurahi kupokea msaada wa ustadi kutoka kwa wafanya kazi wa kujitolea wa ujenzi wa kimataifa kutoka nchi 14. Msaada huu ulikuwa baraka iliyoje! Uthamini wetu wenye kina wamwendea kila mmoja aliyesaidia.
Mabadiliko Katika Usimamizi
Katika 1949 Albert Hoffman akawa mwangalizi wa tawi wa kwanza naye alisaidia sana kupanga kazi kitengenezo hapa wakati wa uchanga wayo. Ndipo katika 1950, uangalizi huo ulihamishwa ukapewa John McClenahan, aliyezoezwa Gileadi pia. Tena, katika 1970, ilihitajiwa kabisa kufanya mabadiliko fulani katika usimamizi. Mhitimu mwingine wa Gileadi, Harley Harris, aliwekwa awe mwangalizi wa tawi naye ameendelea kutumikia katika tawi tangu hapo. Kwa sasa tawi husimamiwa na halmashauri ya watu watano: Francisco Angus, Arthur Bonno, Harley Harris, Vern McDaniel, na Laureano Sánchez.
Dhabihu Maelfu Mengi
Historia ya kazi ya Ufalme katika Ekwedori ina mamia ya maelfu ya dhabihu za ndugu zetu—nyingine ndogo sana hivi kwamba hukosa kuonwa na sisi tulio binadamu, lakini hazikosi kamwe kuonwa na Yehova. Maneno kwenye Waebrania 6:10 hutumika kwa washikamanifu hao wote: “Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake.”
Wale waliokuja kutoka mabara mengine kutumikia hapa watakumbuka kwa muda mrefu vile vipingamizi vya kujaribu kujieleza kwa ulimi ambao walikuwa ndipo tu wameanza kujifunza. Lugha ya wenyeji ilisikika kwao kama mfululizo wa maneno yakimiminwa kwao kwa mwendo wa bunduki-mimina-risasi. Misionari mmoja alisema hivi: “Nilihisi kama kitoto kinachojifunza kuongea tena.”
Kisha namna gani zile nyakati walizokuwa wakifikiri kwamba wameanza kuiweza lugha lakini walikuwa wakisema jambo lililotoa wazo lenye kosa? Kama kielelezo, ndugu mmoja alikwenda kwenye duka la vifaa vya ujenzi na, baada ya kuangalia kamusi yake ya lugha ya Kiingereza na Kihispania, akasema hivi: “Quiero una libra de uñas” (Nataka ratili moja ya kucha). Yeye alikosea akaomba kucha (nails) aina tofauti ya nails (misumari)! Dada mmoja alikuwa anasimama katika basi wakati dereva alipoanza mwendo kwa ghafula, na kumrusha nyuma kifuani mwa mwanamume mmoja. Akifikiri kwamba alikuwa akiomba radhi, akasema hivi: “Con su permiso” (Kwa ruhusa yako). Abiria walikuwa na kicheko cha kutoka moyoni wakati mwanamume yule alipojibu hivi kwa uchangamfu: “Bibi, endelea tu.”
Dada Zola Hoffman, ambaye alibaki katika mgawo wake wa kimisionari katika Ekwedori mpaka mwisho wa mwendo wake wa kidunia, anakumbukwa sana kwa kazi yake ya kutoa ushuhuda bila hofu. Je! yeye aliogopa kuongea juu ya habari njema kwa yeyote? Hata kidogo! Eneo lake alilolipenda sana lilikuwa sehemu ya kibiashara ya Guayaquil. Huko yeye alijulikana na karibu kila mmoja—watekelezaji, wanasheria, mahakimu, na wengine wengi. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi wa mjini aliokuwa ametolea ushuhuda. Hivyo Jumba la Ufalme lilijaa pomoni mpaka kufurika, na kulikuwako watu waliosimama upande wa nje, mwendo wote mpaka upande mwingine wa barabara. Miongoni mwa waliokuwapo walikuwa baadhi ya wale watu 94 aliokuwa amesaidia kibinafsi waweke maisha zao wakfu kwa Yehova.
Ile sauti iliyokuwa imara wakati mmoja ya Ndugu Albert Hoffman sasa ni mnong’ono mzito tu. Kulitukia nini? Usiku mmoja, alipokuwa anaendesha gari lake kurudi nyumbani kutoka mkutanoni, yeye alisimama kwa ajili ya taa za kuongozea magari. Mwanamume mmoja asiyemjua, alimkaribia, akaweka bastola kwenye shingo yake, na kusema jambo fulani; pengine yeye alikuwa akidai pesa. Kwa kuwa Albert alikuwa akisikia kwa shida, yeye hakuitikia mara moja. Kwa kasirani, yule mwanamume akafyatua risasi. Ile risasi ilipitia moja kwa moja katika shingo ya Albert, na kukaa katika bega lake la kulia, ikikata mishipa ya sauti ilipokuwa ikipita. Lijapokuwa dhara hili kwa sauti yake, Albert huendelea kusema sifa ya Yehova, ingawa sasa hufanya hivyo kwa mnong’ono mzito. Yeye ana rekodi ya miaka karibu 60 katika utumishi wa wakati wote.
Mwingine anayejulikana kwa kupiga moyo konde kwake ni Herman Gau, aliyekuja kutoka Ujeremani pamoja na mke wake kutumikia mahali ambako uhitaji ni mkubwa zaidi. Yeye hupenda kutimiza mambo, na kufanya hivyo upesi, hata magumu gani yazuke. Kwa kuwa kundi dogo lililo katika mji Puyo wa msituni lilihitaji Jumba la Ufalme, Ndugu Gau alisababu hivi: “Acheni sisi twende nje ndani ya msitu tukakate miti fulani kwa ajili ya mbao.” Yeye aliona ule ulioonekana kuwa mti mzuri ulionyooka, lakini ndugu mwenyeji aliyekuwa pamoja naye alimtahadharisha hivi: “Mimi singekata huo kama ningalikuwa wewe. Una siafu ndani.”
“Hakuna siafu wanaoweza kunizuia kupata mti huu mzuri kwa ajili ya Jumba la Ufalme!” akasema Herman. Na hivyo wakaushambulia kwa panga zao. Wakati mti huu ambao ulikuwa na shimo ndani ulipoanguka chini, maelfu ya siafu wenye kasirani wakawashambulia ili kujikinga. Kwa jitihada ya kufa na kupona, akina ndugu wakatimua mbio na kutumbukia mtoni wakiwa na nguo zao zote. Tokea hapo na kuendelea, Herman alisikiliza wakati ndugu mwenyeji aliponena naye juu ya miti. “Lakini,” yeye husema kwa kicheko cha kutoka moyoni, “sisi tulijenga lile Jumba la Ufalme!”
Vijana Wakubali Ukweli
Hata hivyo, kuna jambo fulani ambalo ni gumu zaidi ya kujenga Majumba ya Ufalme. Hilo ni kulea watoto katika ukweli. Jorge na Orffa Santos wametumia karibu miaka 30 katika utumishi wa wakati wote. Pia katika pindi ya wakati huo wao wamelea watoto watano, ambao sasa wote wamo katika utumishi wa wakati wote wakifuata kielelezo kizuri cha wazazi wao. Lao ni ono moja tu miongoni mwa maono mengi ambayo huonyesha umaana wa kielelezo kizuri cha wazazi katika kuzoeza watoto katika njia iwapasayo kwenda.—Mit. 22:6.
Hata hivyo, Carlos Salazar hakupata malezi ya kiroho kama hayo. Tofauti na hivyo, wakati yeye alipochagua kumtumikia Yehova, yeye alifukuzwa nyumbani na mama yake na akaepukwa na ndugu na dada zake wa kimwili. Ijapokuwa hivyo, wakati wa miaka 34 ambayo yeye ametumia katika huduma ya wakati wote, amepata ndugu na dada wa kiroho zaidi ya 12,000 katika nchi yake ya uenyeji ya Ekwedori pekee—bila kutaja wale zaidi ya 3,000,000 ambao hufanyiza udugu wa kimataifa. Lo! jinsi yeye amekuja kuthamini ule uangalizi wenye upendo ambao Yehova huwapa wale wanaokuwa “yatima” kwa ajili ya habari njema!
Jim and Frances Woodburn wameonyesha bidii nyingi wakiwa wamisionari mume na mke, wakipanda mbegu za Ufalme kwa marefu na mapana. Wamezuru Sekondari nyingi, wakitoa kitabu Kupata Faida Zote za Ujana Wako. Kimetimiza uhitaji mkubwa sana shuleni katika kusaidia watoto wajifunze maadili bora zaidi, staha kwa walimu wao, na kufahamu hatari za dawa za kulevya. Kile kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? kilitolewa pia—kikiwa kitu kisicho na kifani, kitabu pekee kinachozungumzia mageuzi na kuonyesha pande zote mbili za lile suala. Walimu na wenye mamlaka wa shule waliwaruhusu Ndugu na Dada Woodburn waende moja kwa moja ndani ya madarasa na kuwatolea wanafunzi fasihi hiyo. Hata shule za kidini zinazoendeshwa na mapadri na watawa wa kike ziliitikia. Padri mmoja aliita wanafunzi wote wakusanyike pamoja kwenye jumba la shule na kusema: “Hiki ndicho kitabu mnachohitaji hasa, nami ningehimiza kila mmoja wenu apate nakala moja.” Kati ya zile shule zaidi ya 65 zilizotembelewa, hakuna hata moja iliyokataa kuruhusu akina Woodburns kuwatolea wanafunzi habari hii yenye umaana mkubwa! Nyakati fulani walikuwa wakiangusha vitabu zaidi ya elfu moja katika mwezi mmoja.
Mataraja ya Wakati Ujao
Tunapotembea katika barabara za Quito, Cuenca, Riobamba, na San Antonio leo, ni vigumu kuwaza kwamba wakati mfupi uliopita vita vikali vilipigwa hapa kwa ajili ya uhuru wa kuhubiri habari njema. Mahali pa vikundi vya wanaghasia wenye kupiga makelele pamechukuliwa na watu wenye amani ambao husikiliza ujumbe wa Biblia kwa staha yenye kina kirefu. Majengo ya ukumbusho kwa ushindi ambao Yehova ametupatia yanapatikana kila mahali sasa—Majumba ya Ufalme ambamo makundi 188 hukutana kujilisha Neno la Mungu.
Mwaka uliopita ulipata mpando mwingine katika wahubiri—kufikia kilele cha 13,352. Kuna mafunzo ya Biblia mengi karibu mara mbili ya wahubiri, na 66,519 walikuwapo kwa ajili ya Ukumbusho wa kifo cha Kristo—yote haya yakitoa wonyesho wa kwamba kazi nyingi ingali itafanywa hapa kusaidia wengine pia wakubali ukweli.
Lilikuwa jambo lenye kuburudisha kama nini kwamba wakati wa hari ya mnyanyaso Waekwedori wenye mioyo myeupe walikuja kutetea akina ndugu na dada, kuwapa “kikombe cha maji ya baridi.” Kama alivyosema Yesu, watu kama hao hawapotezi hata kidogo thawabu yao. (Mt. 10:42) Maelfu ya watu hapa kwenye ikweta, toka nyanda za misitu ya kitropiki kufika vilele vya milima yenye kufunikwa na theluji, tayari wamethawabishwa kwa maji ya ukweli yenye kuburudisha. Tamaa yetu ya moyo ni kwamba maelfu zaidi watanufaika kabla ya mfumo huu kukoma.
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 201]
Muhtasari wa Ekwedori
Mji Mkuu: Quito
Lugha Rasmi: Kihispania
Dini Kubwa: Roma Katoliki
Idadi ya Watu: 10,054,000
Wahubiri: 13,352
Mapainia: 1,978
Makundi: 188
Hudhurio la Ukumbusho: 66,519
Ofisi ya Tawi: Guayaquil
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BAHARI YA PACIFIKI
KOLOMBIA
IKWETA
Ibarra
Atuntaqui
San Antonio
EQUATOR
Quito
Manta
Ambato
Riobamba
Babahoyo
Guayaquil
Milagro
La Libertad
Andes
Cuenca
Machala
PERU
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 199]
[Picha katika ukurasa wa 202]
Thomas na Mary Klingensmith, kushoto, na Willmetta na Walter Pemberton walikuwa ndio wamisionari wa kwanza katika Ekwedori kutoka Shule ya Gileadi, 1946
[Picha katika ukurasa wa 207]
Pedro Tules, Mwekwedori wa kwanza kuzoezwa katika Shule ya Gileadi
[Picha katika ukurasa wa 209]
N. H. Knorr, kushoto, msimamizi wa tatu wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, na M. G. Henschel akisimama pamoja naye, pia kutoka makao makuu ya ulimwengu, walipozuru Ekwedori katika Machi 1949. Albert Hoffman, kulia, alikuwa mwangalizi wa kwanza wa tawi la Ekwedori. Baadaye alipigwa risasi na akapona
[Picha katika ukurasa wa 210]
César Santos aliacha ibada ya sanamu awe Shahidi
[Picha katika ukurasa wa 215]
Carl Dochow, misionari aliyezoezwa Gileadi, alikutana na ukinzani katika jiji la Cuenca
[Picha katika ukurasa wa 218]
Carlos Salazar, Mwekwedori wa pili kuhudhuria Shule ya Gileadi
[Picha katika ukurasa wa 220]
Unn Raunholm alitumwa Ekwedori akiwa misionari katika 1958
[Picha katika ukurasa wa 223]
Ray na Alice Knoch, wamisionari waliopewa mgawo kwenye vijiji vya Pwani ya Pasifiki
[Picha katika ukurasa wa 227]
Maruja Granizo, kushoto, pamoja na wajukuu wake na binti mkwe
[Picha katika ukurasa wa 230]
John Furgala, kushoto, nje ya duka lake la vifaa vya ujenzi
[Picha katika ukurasa wa 233]
Rafael Coello, aliyekuwa wakati mmoja hakimu katika mahakama ya Rufani, hutolea ushuhuda waliokuwa hapo kwanza washiriki wenzake kwenye Jumba la Hukumu katika Guayaquil
[Picha katika ukurasa wa 238]
Bob na Joan Isensee waliokuwa wamisionari hapo kwanza na watoto wao. Walielekeana na suala la damu
[Picha katika ukurasa wa 241]
Mario Polo baada ya kushinda mbio za kuendesha baiskeli. Mario na Norma, mke wake, sasa hutetea ukweli wa Biblia
[Picha katika ukurasa wa 245]
Makao ya Betheli mapya ya Ekwedori na eneo layo la kupokelea wageni
[Picha katika ukurasa wa 246]
Kifaa kipya cha Jumba la Kusanyiko cha mahali peupe na tawi jipya, linaloonekana kule nyuma