Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb92 kur. 116-185
  • Swedeni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Swedeni
  • 1992 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • “Waswedeni Mia Mbili Hivi Wameipokea”
  • Yafunikwa na Misitu
  • Ufalme Uliochangamana
  • Mbegu za Kwanza Zafika Swedeni
  • Kundi la Kwanza Lafanyizwa
  • Mbegu Zaidi Zachipuka
  • “Mnara wa Mlinzi” wa Mapema Katika Kiswedeni
  • Mkusanyiko Halisi wa Kwanza
  • Utumishi wa Wakati Wote—Nguzo ya Kazi
  • Ziara za Waangalizi Wasafirio Zaanza
  • Tawi Lahama-hama
  • Russell Apendezwa na Swedeni
  • Vita ya Ulimwengu ya 1 Si Tukio la Kushangaza
  • Ile Photo-Drama, Chombo Kingine
  • Akina Dada Wawa na Ushiriki Mkubwa Zaidi
  • Je! Mlango Ungefungwa Katika 1918?
  • Mitihani Migumu Katika Miaka ya 1920
  • Wakati wa Badiliko
  • Enzi Mpya ya Usimamizi wa Tawi
  • Kuunganisha Akina Ndugu Tena
  • Kutoa Ushuhuda Mazikoni
  • Hatua Yenye kuburudisha
  • Motokaa ya Kwanza—Ajabu Kubwa
  • Enzi ya Baiskeli
  • Kutumia Njia Zote
  • Upanuzi Kabla ya Vita ya Ulimwengu ya 2
  • Jitihada za Kumwonya Hitler
  • “Jamii” Mpya Yatambulishwa
  • “Acheni Kuwazuia”
  • Kupitia Ile Miaka Migumu ya Vita
  • Upinzani Walipuka
  • Kampeni Yawa na Matokeo Yasiyotakwa
  • Si Mapadri Wote Walipinga
  • Haya Zashindwa
  • “Haruni 1”—Kadi ya Ushuhuda
  • “Haruni 2”—Kinanda
  • “Haruni 3”—Kifaa cha Kupaaza Sauti
  • “Haruni 4”—Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
  • Matokeo Bora Sana
  • Kupiga Miguu Barabarani
  • Kutokuwamo kwa Kikristo Kwahatirishwa
  • Wenye Mamlaka Wajaribu Tendo la Kuwakatisha Tamaa
  • Tatizo Lenye Kukua
  • Gereza la Wafungwa
  • Rekebisho Laanza Kuonekana
  • Makasisi Wageuka na Kutuunga Mkono
  • Uamuzi wa Mwisho
  • Kiolezo cha Swedeni
  • Jaribio Jipya la Kutafuta Kuridhiana
  • Waacha Kanisa kwa Maelfu
  • Redio Si kwa Ajili ya Mashahidi wa Yehova
  • Jaribio la ‘Kutufunua Wazi’ Laleta Matokeo Yasiyotakwa
  • Uhitaji wa Tawi Jipya
  • Tendo Thabiti Lachukuliwa
  • Eneo la Kigeni Lasitawi
  • Makundi ya Lugha za Kigeni
  • Njaa kwa Ajili ya kweli
  • Kutoa Ushuhuda Miongoni mwa Watu wa Lapp
  • Sherehe za Ndoa za Kitheokrasi, Hatua Moja Mbele
  • Mratibu wa Tatu wa Halmashauri ya Tawi la Swedeni
  • Arboga—Mahali pa Kituo Kipya
  • Mradi wa Ujenzi Usio na Kifani
  • Majengo Mapya ya Tawi Yathaminiwa Sana
  • Matbaa Mpya Zaongezea Kazi Mwendo
  • Ukuzi Mzuri wa Faida za Ufalme
1992 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb92 kur. 116-185

Swedeni

Ripoti ya kitabu-mwaka 1992

KUTOKA katika lile giza lililofunika Ulaya kama vazi wakati wa zile Enzi za Katikati walitokea ghafula maharamia wenye kuteka nyara wakitumia meli kutoka kaskazini. Wanaume hao wenye nguvu wa Kijerumani kutoka Skandinavia, walipata ustadi wa kupiga vita vya baharini nao wakabuni mashua kubwa zenye kwenda kasi zilizowawezesha kueneza mamlaka yao pande za kusini, magharibi, na mashariki. Maharamia wa kutoka Norwei na Denmarki walisafiri baharini wakafika pwani za Uingereza, Ailandi, na bara la Ulaya, huku maharamia wa kutoka Swedeni wakielekeza mashua zao upande wa mashariki kuvuka mito na maziwa ya Baltiki na kuelekea kwenye misitu mikubwa mno ya miti jamii ya msunobari na pori za Urusi. Kuanzia mwisho wa karne ya nane, na kwa miaka yapata 250, meli za maharamia hao zilianza kutawala njia za maji za kaskazini zikitafuta biashara na utajiri.

Mwishoni mwa karne ya 19, Waswedeni walikuwa mwendoni tena kuelekea pwani za nchi za kigeni—wakati huu wakitafuta ushindi wenye amani. Walikuwa wamepata hasara ya mavuno, ukosefu wa kazi za kuajiriwa, na hata njaa kali. Wakitafuta maisha bora zaidi, Waswedeni zaidi ya milioni moja waliondoka nchini kati ya 1865 na 1914. Walio wengi wao walifanya makao katika Amerika Kaskazini, ambako walipata ufanisi wa vitu vya kimwili. Ingawa hivyo, baadhi yao waligundua kitu chenye thamani kubwa zaidi—maisha yenye utajiri yaliyotegemea imani iliyo hai—ambayo wangeishiriki upesi pamoja na marafiki na watu wa ukoo walioachwa nyuma huko Swedeni. Kasha hili la hazina lilifikaje hatimaye kwenye pwani ya Swedeni?

“Waswedeni Mia Mbili Hivi Wameipokea”

Wapata mwaka 1882, mweneza habari njema wa kawaida Mswedeni katika Amerika, Charles Seagrin, alisoma baadhi ya fasihi vya Charles Taze Russell, kutia na Food for Thinking Christians. Kwa kusadikishwa kwamba hii ilikuwa ndiyo kweli, yeye aliihubiri kwa juhudi miongoni mwa wahamiaji Waswedeni. Baada ya miezi sita ya kuhubiri, aliandikia Ndugu Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Society, akasema hivi: “Pindi ya wakati ambao mimi nimehubiri kweli hii Waswedeni mia mbili hivi wameipokea nao wanaishangilia na wanawaambia wengine. . . . Wengi wa taifa letu [Swedeni] wanaonekana kuwa na sikio lenye kusikia . . . Kama tungeweza kuwa na Chakula katika Kiswedeni pia kingekuwa chenye faida sana chini ya baraka ya Bwana.”

Barua hiyo ilimfanya Ndugu Russell akumbushe wasomaji wa gazeti Zion’s Watch Tower (Juni 1883) kwamba “Hazina ya Trakti kwa Kiswedeni” ya pekee ilikuwa tayari imeanzishwa kwa ajili ya kuchapa fasihi katika Kiswedeni. Hata hivyo, aliripoti kwamba hazina hiyo ilikuwa na dola 30 tu wakati huo. Aliongeza hivi akiwa na hakika: “Bwana-Mkubwa Wetu ni tajiri—ndiye mwenye ng’ombe [walio] juu ya vilima elfu, pamoja na vilima hivyo vyenyewe, na dhahabu na fedha yote ni Vyake. Akiona kazi hiyo inahitajiwa yeye atafanya uandalizi unaohitajiwa.”

Na “Bwana-Mkubwa Wetu” alifanya hivyo! Miezi minne tu baadaye, gazeti Zion’s Watch Tower lilitangaza hivi: “Ile hazina ya trakti kwa Kiswedeni ilifikia kiasi kikubwa hivi kwamba inastahilisha kuchapa nakala sampuli ya TOWER katika lugha ya Kiswedeni, itakayotumiwa kama trakti, miongoni mwa Wakristo Waswedeni na Wanorwei, hapa na katika Swedeni.” Miaka kumi baadaye, lile buku la kwanza la ule mfululizo wa Millennial Dawn—ulioitwa baadaye Studies in the Scriptures—lilichapwa katika Kiswedeni.

Hivyo msingi uliwekwa ili kupeleka mbegu za kweli ya Ufalme kwenye hii, iliyo kubwa zaidi kati ya nchi za Skandinavia. Lakini namna gani watu, tabia yao, desturi zao, na nchi yao? Je! “mavuno” mengi yangevunwa huko?—Mt. 9:37, 38.

Yafunikwa na Misitu

Mandhari ya Swedeni ni paradiso ya kijani kibichi na bluu. Hata hivyo, hiyo inaweza kuwaje na hali nchi hii iko katika sehemu ya kaskazini zaidi ya Ulaya, ikitagaa Mzingo wa Aktiki? Ikiwa inajaliwa kwa wingi sana na milima yenye fahari, nyanda zenye kuzaa sana, misitu ya miti ya jamii ya msunobari, pwani zenye mchanga-mchanga, na visiwa vyenye uzuri, Swedeni hukaa katika pepo zenye kutuliza zilizotiwa joto na Mkondo wa Ghuba.

Desturi isiyo na kifani ya “haki ya kila mtu” inawaruhusu watu kutembea bila kizuizi katika misitu na mashamba, waokote matunda aina ya beri na viyoga, waende kuogelea, au wafunge mashua bila kulazimika kuomba ruhusa. Kwa kuwa Swedeni ina eneo la nne kwa ukubwa katika Ulaya, ikitanuka kilometa karibu 1,600 kutoka kaskazini kufika kusini na kilometa 500 kutoka Bahari ya Baltiki upande wa mashariki kufika Norwei na Bahari ya Kaskazini upande wa magharibi, inatoa nafasi tele kwa wakaaji wayo karibu milioni 8.6. Kwa hiyo, kitarakimu, kila mtu ana nafasi ya kuishi ya hekta 5, ambazo karibu hekta 3 ni msitu, miti ya jamii ya msunobari, hiyo ikimpa kila mtu wastani wa miti 7,500 aifurahie. Je! wewe waweza kunusa harufu nzuri yenye kuburudisha ya misunobari hiyo ya rangi kijani kibichi yenye kusitawi sana?

Ufalme Uliochangamana

Ukiwa mmojawapo falme za ulimwengu za kale zaidi, Swedeni ina mazoea ya kidemokrasia ambayo yamedumu muda mrefu sana, ikiwa na bunge lenye mfumo wa vyama vingi. Karibu asilimia 95 ya Waswedeni ni wa Kanisa Lutheri la Serikali, ingawa idadi ndogo ndio wanaohudhuria kanisa kwa ukawaida. Hata hivyo, wakati wa makumi ya miaka ya karibuni, wahamiaji mamia ya maelfu wamegeuza Swedeni kuwa jamii iliyochangamana kidini na kitamaduni. Yule Mswedeni mrefu, mwenye nywele nyeupe kidogo au ya rangi kahawia na macho ya bluu, siye peke yake anayekuwa tena asili ya taifa.

Wakaaji wa Swedeni wanaandaliwa mfumo wa hali njema ya kijamii tangu kuzaliwa hadi kufa. Wanafurahia alawansi ya watoto, elimu ya bure, alawansi ya makao, mshahara mtu anapokuwa mgonjwa, utunzaji wa kitiba unaokaribia sana kuwa wa bila malipo yoyote, na malipo ya uzeeni na ya kulemaa, miongoni mwa utumishi mwingine mbalimbali unaotegemezwa na serikali. Ijapokuwa viwanda na mashine za Mvuvumko wa Viwanda havikufika pale mwanzoni, leo Swedeni ni miongoni mwa mataifa ya ulimwengu yenye viwanda vingi zaidi. Na asili ya roho ya kipekee ya Mswedeni inaelekea kukaa katika usadikisho wa makini wa kwamba jambo linalostahili kufanywa lastahili kufanywa vizuri. Lakini chini ya hali hizo zinazoonekana kuwa zenye kufaa sana za kuishi, je, mbegu ya Ufalme ingetia mizizi na kukua?

Mbegu za Kwanza Zafika Swedeni

Miaka mia moja iliyopita, wahamiaji Waswedeni ambao walikuwa wamepokea kweli kwa shauku katika United States walianza kupelekea watu wao wa ukoo na marafiki fasihi katika Swedeni. Baadhi ya mbegu hizo za kweli zilianguka katika nyumba moja ndogo katika kile kisiwa kidogo cha Sturkö, umbali fulani kutoka pwani ya kusini ya Swedeni. Huko zikachipuka upesi katika moyo wa mwanamume kijana.

Jioni moja katika 1898, August Lundborg, kapteni wa Jeshi la Wokovu mwenye umri wa miaka 25, mwenye nguvu na umbo lenye maungo, alitembelea Petter Larsson na familia yake katika Sturkö. Alipoachwa peke yake kifupi katika nyumba yao ndogo, macho yake yalianguka juu ya vile vitabu viwili—yale mabuku mawili ya Millennial Dawn, ya C. T. Russell. Alipokuwa akifungua-fungua kurasa, alipata ufafanuzi juu ya dhabihu ya ukombozi ya Kristo ambao ulimshangaza na kumfurahisha sana. Aliazima vitabu hivyo, akavisoma kwa hamu, na mara hiyo akaanza kuvitumia kufundishia kwenye mikutano yake.

Lundborg, mwanamume wa tendo, aliandikia Ndugu Russell barua, yenye tarehe ya Desemba 21, 1898: “Mpendwa Bw. Russell: Mwenye sahihi iliyo chini, ambaye hapo kwanza alikuwa kapteni wa Jeshi la Wokovu, kwa sababu ya nuru ambayo Mungu amempelekea kupitia kazi yako, M. DAWN, ameacha hivi karibuni, tengenezo lililotajwa.” Baada ya kuonyesha uthamini kwa kweli aliyokuwa amepata, Lundborg alimalizia hivi: “Ukitaka, nitafurahia sana kuingia katika kazi ya kolpota hapa Swedeni.” Bila kusita, Ndugu Russell alimpelekea Lundborg kwa posta seti 55 za yale mabuku matatu ya kwanza ya Millennial Dawn, akamhimiza awapelekee nakala wale waliokuwa hapo kwanza wafanyakazi wenzake wa “Jeshi.”

Lo, Lundborg alikata tamaa kama nini wakati vitabu vile vilipowasili! Havikutosha! Kwa muda mfupi, alikuwa ameviangusha vyote kwa waliokuwa hapo kwanza wafanyakazi wenzake na wengine. Upesi akamwandikia Russell ampelekee vingine. Alingoja na kungoja. Ilionekana kama havitakuja kamwe. Bila kukata tamaa kwa kutokuwa na fasihi, akaanza utendaji wake wa kolpota, akihubiri wakati wote nyumba kwa nyumba, huko Stockholm katika Mei 1899. Kwa shauku alipata maagizo ya vitabu ambavyo angepeleka baadaye. Hivyo kazi ya kupanda mbegu za Ufalme ikaendelea.

Kundi la Kwanza Lafanyizwa

Ndugu Russell alimpelekea Lundborg pia anwani ya mtu mmoja aitwaye S. Winter katika Denmarki, ambaye alikuwa ameanza kueneza mbegu za kweli huko, pamoja na upande wa kusini kabisa wa Swedeni. Bila kukawia Lundborg alimwalika wakutane Stockholm na kupanga mkutano wa Biblia—ule wa kwanza kabisa katika Swedeni. Watu wachache wenye kupendezwa walisongamana katika chumba kidogo cha jikoni cha familia moja ambayo ilikuwa imepata baadhi ya fasihi kutoka kwa Lundborg. Chumba hicho kilikuwa kinavuma kwa msisimuko huku watu hao wenye njaa ya kiroho wakimeza kwa hamu yale maneno ya kweli.

Kufikia mwisho wa 1899, kikundi hiki kidogo chenye bidii kikaanza kukutana kwa ukawaida Jumapili. Duka dogo lililojengwa kwa mbao lilikodiwa katika Apelbergsgatan kwa kronor mbili (senti 33 za U.S.) kwa kila jioni. Katika Alhamisi, Aprili 12, 1900, watu wanane wakakusanyika katika chumba kilichokodiwa katika Grev Magnigatan ili kuadhimisha Ukumbusho wa kwanza katika Swedeni. Walisali kwamba roho ya Mungu iharakishe ukuzi.

Miezi michache baadaye, walikodi mahali penye nafasi kubwa zaidi, nyumba yenye vyumba vingi kwenye Trångsund 8. Mkusanyiko wa kwanza ‘uliotayarishwa nyumbani’ ukafanywa humo katika Juni 20-27, 1901. Baadhi ya Wanafunzi wa Biblia kutoka Denmarki walihudhuria pia. Wakitaka kujaribu hali ya kupendezwa nje ya Stockholm, Waswedeni walipanga kuwe na mkutano katika mji wenye chuo kikuu wa Uppsala, kaskazini mwa Stockholm. Walijawa na furaha wakati watu wenye kupendezwa 150 walipohudhuria.

Sasa kweli ikaanza kusambaa zaidi. Chumba kidogo kilichokodiwa kwenye Kungsgatan 20 katika Stockholm kilitumiwa kikiwa ofisi na bohari la fasihi. Lundborg aliendelea “kupanda” kwa juhudi katika pande zote kwa kusafiri kwa miguu, gari, garimoshi, na meli. (Mt. 13:3-23) Katika 1902 aliripoti kwamba alikuwa amefanya kazi katika karibu majiji na miji yote katika Swedeni ya kati na ya kusini.

Mbegu Zaidi Zachipuka

Mbegu zaidi za kweli zilipofika pande nyinginezo za nchi, zilianza kuchipuka katika mioyo ya watu wengine wengi wenye bidii katika kazi, ambao walijiunga kwa haraka katika kazi. Siku moja katika 1902 katika jiji la Malmö, mwanamume mmoja kijana kwa jina P. J. Johansson alikuwa akitembea katika bustani, akatua kidogo mbele ya benchi. Aliona trakti moja hapo yenye kichwa Do You Know? (Je! Unajua?) Aliisoma, akatambua kwamba hiyo ndiyo kweli, na bila kupoteza wakati, akaanza upesi kutumika akiwa kolpota.

Katika Segmon katika sehemu ya magharibi ya Swedeni ya kati aliishi mfua chuma, Axel Gustaf Rud. Kwa miaka 35 alikuwa amekuwa mshiriki wa Kanisa Huru na pia mhubiri mwenye kupendwa na watu wengi. Alipata nakala ya Millennial Dawn aliyotumiwa kwa posta kutoka Amerika ya Kaskazini na watu wa ukoo wake. Wao walitaka kujua tu maoni yake juu ya kitabu hicho. Alisadikishwa sana kwamba hiyo ndiyo kweli hivi kwamba alijulisha wazi katika kanisa lake ndogo: “Kufikia sasa nimekuwa nikinena uwongo. Sasa nitanena kweli.”

Wakati yeye na washiriki wengine wapatao 30 walipoacha kanisa lake, gazeti la kila siku la kwao liliripoti kwamba lilisikitika kumpoteza “mhubiri kama huyo asiye na kifani.” Mmoja aliyekuwa hapo kwanza mwamini mwenzake aliomboleza hivi: “Sasa tunaweza kuamini nini kwa kuwa Rud ametuondolea moto wa mateso?” Upesi kundi la Wanafunzi wa Biblia likafanyizwa katika Grums, mji wa karibu.

“Mnara wa Mlinzi” wa Mapema Katika Kiswedeni

Akisonga mbele na kazi wakati wa 1902, Ndugu Lundborg alimsihi Ndugu Russell gazeti lichapwe katika Kiswedeni. Ndugu Russell alijibu hivi: “Ningali nashikilia imani ya kwamba kufanya kazi ya kolpota, pamoja na kueneza trakti, ni jambo lenye maana zaidi ya kutolewa kwa gazeti lolote katika lugha yoyote, nami napendekeza utumie wakati wako hivyo.”

Hata hivyo, Lundborg mwenye nia thabiti alisonga mbele na mipango yake. Kufikia mwishoni mwa mwaka huo, alikuwa amechapa na kugawanya toleo la kwanza la gazeti la kila mwezi, I Morgonväkten (Katika Kesha la Asubuhi). Lilikuwa na makala zilizonakiliwa kutoka Zion’s Watch Tower, hotuba za Pastor Russell, mashairi, na barua kutoka kwa wasomaji. Wakati Ndugu Russell alipotembelea Stockholm alipokuwa katika safari yake ya Ulaya katika Mei 1903, aliamua kwamba gazeti hilo lapasa kuitwa Zion’s Watch Tower, C. T. Russell akiwa mhariri. Hilo lilifanywa katika Januari 1904.

Mkusanyiko Halisi wa Kwanza

Wakati wa ziara ya Ndugu Russell katika Stockholm, mkusanyiko halisi wa kwanza ulifanywa Mei 3, 4, 1903. Alitoa hotuba kadhaa zenye kuchochea, ambazo zilitafsiriwa na aliyekuwa hapo kwanza mhudumu wa Kanisa la Serikali ya Swedeni. Wapatao 250, walihudhuria, nusu yao wakiwa “watu wa nje,” wapya wenye kupendezwa.

Akina ndugu na dada walijisikia wakiwa na shauku nyingi sana kwa Ndugu Russell. Kupitia maandishi yake, imani na mawazo yake yalikuwa yamekuwa yao, na sasa walisisimuka sana kumwona na kusikia ujumbe wake. Ndugu mmoja aliandika hivi: “Tulishangaa tulipoona umbo lake lenye fahari na uso wake kama wa kijana na wenye kuonyesha furaha, ingawa miaka ilikuwa tayari imetia mvi hapa na pale katika nywele zake nyeusi kichwani pake. Fadhili na upendo uliangaza macho yake yenye upole na hata hivyo yenye uzito. Usemi wake ulikuwa mchangamfu na wenye kunasa fikira lakini usio na namna yoyote ya kutia chumvi. Tulimpenda tangu mwanzo wenyewe.”

Akiwa na furaha kuu, Matilda Lindros, kolpota wa kwanza wa kike katika Swedeni, aliandikia tawi hivi: “Siku hizo huonekana kwangu sasa kama ndoto nzuri, lakini Mungu na anisaidie si kuzikumbuka tu bali pia kutumia kwa moyo wa kupenda mambo niliyojifunza, . . . na Bwana na asaidie watumishi wake wenye moyo wa kupenda na watiifu wakae katika hali hiyo mpaka mwisho!” Aliendelea akiwa mwaminifu, akatumikia Yehova mpaka kifo chake katika 1945 akiwa na umri wa miaka 91.

Ndugu Russell aliandika baadaye, akitoa muhtasari wenye kuonyesha kutosheka kwake na safari hiyo: “Mimi sitasahau kamwe ziara yangu kwenye [nchi za] Skandinavia, na wakati wote mimi nitasali na kutakia kazi huko baraka ya Bwana.”

Utumishi wa Wakati Wote—Nguzo ya Kazi

Imani ya Ndugu Russell na roho ya kusonga mbele ilisukuma baadhi ya wale waliojifunza kweli kwanza washiriki kwa uchangamfu kazi ya kuhubiri wakati wote. Tangu hapo, huduma ya wakati wote imekuwa nguzo ya kazi ya Ufalme katika Swedeni.

Wale makolpota wa mapema walianza kazi bila kusita, bila mazoezi yoyote ya pekee, mara nyingi bila makao ya kudumu, wakiwa tu na kazi ya nusu wakati ili kujiruzuku, na nyayo zao zikiwa ndizo njia pekee ya usafiri. Walitambua ukubwa na uharaka wa kazi yao, wakionekana ni kama kwamba wanakimbia nyumba kwa nyumba badala ya kutembea, wakieneza maeneo makubwa kwa haraka. Lundborg aliripoti kwa Ndugu Russell hivi:

“Sikuzote mimi hujaribu kuwa mwenye busara kadiri iwezekanavyo kwa kufuata njia ile ile mimi huiona kutoka kwa barua zako ambayo wewe hutumia katika Amerika, yaani, kutembelea nyumba zote kila mahali. Mimi huenda mlango kwa mlango, kikundi cha nyumba kwa kikundi cha nyumba (tokea asubuhi na mapema mpaka jioni sana), mpaka ninapokuwa tayari kwa mji unaofuata. Lakini ikiwa mahali hapo si pakubwa zaidi ya mahali ninapotembelea sasa (Mariefred, wenye wakaaji 1,100 hivi), si saa nyingi zinazohitajiwa.”

Ilipokuwa mbali sana isiwezekane kwenda kwa miguu, makolpota walitumia usafiri mwingine, mara nyingi wa gharama ya chini na wa mwendo wa polepole. Lakini wakati ulitumiwa kwa hekima. Ripoti iyo hiyo yasema pia: “Mimi husafiri kwa gharama ya chini. Nina mwili wenye nguvu unaoweza kuvumilia kutendewa vibaya mara kwa mara. Popote iwezekanapo, mimi husafiri kwa maji, nyakati nyingine kwa meli za kusafirisha mizigo. Nyakati fulani nalipia mahali pa kulala pa bei ya chini zaidi katika meli ya kubeba abiria (ambapo mahali pekee—mchana na usiku—ni sakafu iliiyo wazi). Wakati uliotumiwa katika [safari] hiyo nautumia kwa uangalifu kuongea na watu na kujifunza Biblia.”

Ziara za Waangalizi Wasafirio Zaanza

Ziara za ukawaida za waangalizi wasafirio zilihitajiwa ili kutia moyo na kusaidia makundi mapya yapangwe kitengenezo vizuri zaidi. Kwa hiyo ziara zikifanywa na wanaume waliokomaa walioitwa akina ndugu pilgrimu zilipangwa katika 1905. Charles Edberg, ambaye alikuwa amejifunza kweli katika United States na ambaye aliwasili kwa meli katika 1904, alikuwa ndiye ndugu pilgrimu wa kwanza, naye alichangia sana kupanga kitengenezo kazi ya Ufalme ya mapema nchini humo.

Ilitangazwa katika Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) kwamba makundi yapaswa kuandikia Sosaiti na kuomba ziara hizo. Makundi yalipaswa kupangia mikutano ambayo ingefanywa na ndugu huyo mwenye kutembelea na kumpa makao. Walishauriwa wasimfanyie mipango mingine ya pekee kwa sababu, kama vile gazeti Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) lilivyosema, “yeye haji kutumikiwa, bali kutumika.”

Kila mojayapo ziara za Ndugu Edberg ilikuwa ya angalau siku mbili. Kwa kuchochewa na mojayapo hotuba zake, msikilizaji mmoja alisema hivi baada ya ziara hiyo: “Nimejifunza mengi zaidi kutokana na hotuba hizo kuliko niliyokuwa nimejifunza kwa muda wa miaka 20 iliyopita.” Mwingine alisema: “Inastaajabisha ni mengi kadiri gani yaliyo katika Biblia ambayo hatujasikia wala kuona.” Ndugu Edberg hakujua hata kidogo kwamba ziara kama hizo kwa makundi zingekuwa zingali zinafanywa zaidi ya miaka 85 baadaye na waangalizi wa mzunguko na wa wilaya.

Tawi Lahama-hama

Katika miaka yayo ya mapema kabisa, ile ofisi ndogo ya tawi ya Swedeni—ambayo sana-sana fanicha iliyokuwamo ilikuwa vibweta vya fasihi na kitanda cha Ndugu Lundborg—ilihamishwa kutoka mahali pamoja kwenda mahali pengine katika sehemu ya kati ya Stockholm. Katika 1905 ilihamishwa kutoka chumba kilichokuwa sehemu ya nyuma kwenye Kungsgatan 20 ambacho kilikuwa kimeishiwa nafasi ikapelekwa kwenye sehemu ya nyumba yenye vyumba vingi kwenye Adolf Fredriks Kyrkogata 7. Vyumba vitatu vilikodiwa, kimoja kwa ajili ya mikutano, kimoja kwa ajili ya ofisi, na kimoja kwa ajili ya vibweta na kitanda cha Lundborg. Hata hivyo kabla ya mwaka kwisha, mwenye nyumba hiyo alitaka tena vyumba vyake, nayo ofisi ikahamishiwa Rådmansgatan 39 B.

Kazi ilipozidi kupanuka, hasa katika yale majiji mawili makubwa zaidi—Stockholm upande wa pwani ya mashariki na Göteborg upande wa pwani ya magharibi—Lundborg aliona inafaa zaidi kuendeshea utendaji wake mahali palipo katikati ya majiji hayo. Kwa hiyo, katika 1907, tawi lilihamishiwa Örebro, kilometa zapata 200 magharibi mwa Stockholm, ambapo lilikaa kwa muda wa karibu miaka 20.

Russell Apendezwa na Swedeni

Barua nyingi ambazo Ndugu Russell alimwandikia Lundborg zilionyesha kupendezwa sana na kazi katika Swedeni. Sikuzote zikiwa zenye kuonyesha uchangamfu na kutia moyo, zilikuwa wazi na zenye maagizo thabiti. Wakati mmoja, yeye aliandika hivi: “Tafadhali, pokea na sikuzote uwe na hakika ya upendo na huruma zangu, hata ijapokuwa nyakati nyingine ninaona inahitajiwa kabisa kuchambua.”

Katika 1909, wakati Russell alipotembelea Swedeni kwa mara ya pili, watu wapatao 300 walifanya mkusanyiko katika Örebro. Miaka miwili tu baadaye, alirudi na kutoa hotuba katika jumba lililo kubwa zaidi katika Stockholm juu ya kichwa “Hukumu ya Kile Kiti cha Enzi Kikuu Cheupe.” Kufikia wakati huo alikuwa amejulikana sana katika Swedeni. Jumba hilo lilijaa pomoni, na nafsi zipatazo 1,500 zilikatizwa tumaini kwa kuwa hazikuweza kuingia ndani. Kulikuwako msisimuko na kusemezana katika jiji. Wakati yeye na wenye kusafiri pamoja naye walipopanda garimoshi kwenda Copenhagen, umbo lake lenye kuvutia lilivutia sana mwenye kuanzisha garimoshi mwendo, ambaye alisimama tu akikodoa macho na kufungua wazi kinywa chake akasahau kutoa ishara garimoshi liondoke kwa wakati wake. Watu waliuliza: “Mtu huyo wa kifalme ni Nani?”

Ziara ya Ndugu Russell ya mwisho katika Swedeni ilikuwa katika 1912, ikiwa sehemu ya safari ya kuzunguka ulimwengu. Hotuba yake ya watu wote katika Circus, Djurgården, ilikuwa na kichwa “Ng’ambo ya Kaburi.” Dada mmoja alikumbuka msisimuko wa umati wa watu juu ya ziara yake kwenye mji wa kwao, Karlstad: “Jumba lililokodiwa kwa ajili ya mkutano lilijazana watu sana hivi kwamba ilihofiwa kwamba sakafu ingebomoka.”

Ndugu Russell aliendelea kuonyesha kupendezwa na Swedeni kwa kutuma akina ndugu huko kutoka makao makuu, miongoni mwao akiwa J. F. Rutherford, ambaye baadaye alipata kuwa msimamizi wa Watch Tower Society. Katika 1913 Ndugu Rutherford alitembelea majiji 15 yaliyo makubwa zaidi katika Swedeni na Norwei wakati wa majuma matatu tu. Nguvu zake, maarifa ya Biblia, na hotuba zenye kuchochea ziliwachochea ndugu wasonge mbele. Hotuba yake ya watu wote ilikuwa “Wafu Wako Wapi?” Ndugu mmoja alikumbuka mkutano katika Göteborg: “Wakati wa kutoa hotuba yake, Ndugu Rutherford alisema: ‘Mimi natoa dola 1,000 kwa yeyote katika wasikilizaji ambaye anaweza kuthibitisha kwamba mwanadamu ana nafsi isiyoweza kufa.’ Hakuna mtu aliyekubali kushindana na mwito huo.”

Wakati habari za kifo cha Ndugu Russell katika Oktoba 31, 1916, zilipofika Swedeni, ikawa wazi jinsi alivyokuwa amejulikana sana. Hesabu fulani ya magazeti ya kila siku yalimheshimu kwa matangazo ya kirafiki. Mengine hata yalichapisha mojayapo hotuba zake. Bila shaka, kupendezwa kwa Ndugu Russell na Swedeni kulikuwa kichocheo cha kusonga mbele na kazi ya Ufalme.

Vita ya Ulimwengu ya 1 Si Tukio la Kushangaza

Kufyatuka kwa Vita ya Ulimwengu ya 1 halikuwa tukio la kushangaza sana kwa Wanafunzi wa Biblia katika Swedeni. Miaka mingi kabla, walikuwa wamesoma katika fasihi vya Watch Tower kwamba kronologia (kuhesabu wakati) ya Biblia ilielekeza kwenye mwaka wa 1914 kuwa wakati ambao “machafuko ya ulimwenguni pote” yangetazamiwa. Tazamio lilikuwa kubwa sana mwaka 1914 ulipoanza hivi kwamba wengine hata walianza kujiwekea akiba ya vyakula. Hivyo wakati habari za vita vilipofika, walishangilia kukaribia kwa wokovu wao.

Ndugu Arthur Gustavsson, aliyekuwa mwenye umri wa miaka 11 wakati huo, alisema: “Mimi naweza kukumbuka waziwazi Jumapili, Agosti 2, 1914. Baba yangu alikuwa akiongoza mkutano katika Göteborg wakati huko nje tulisikia mvulana muuzaji wa magazeti akipaaza sauti hivi: ‘Mteketeo mkubwa wa ulimwengu umeanza!’ Ndugu waliokuwa ndani ya jumba wakaanza kutazamana mmoja na mwenzake. Baadhi ya mambo waliyokuwa wakitangaza juu ya 1914 yalikuwa yameanza kutimia.” Ndugu Gustavsson baadaye alitumika katika utumishi wa wakati wote kwa miaka 56 na akaendelea kuhubiri mpaka mwisho wa mwendo wake wa kidunia katika 1987.

Ijapokuwa Swedeni ilijiepusha na Vita ya Ulimwengu ya 1, chakula na vitu vingine vya lazima vilipata kuwa vichache. Makundi makubwa ya wafanyakazi wakawa wenye ghasia na kupanga misafara kwenda mashambani wakanyang’anye chakula katika mashamba. Hata hivyo, Yehova Mungu aliendelea kulisha vizuri kiroho watu wake katika Swedeni wakati wa miaka hiyo ya vita, hata ingawa uwasiliano na makao makuu ya Brooklyn ulikuwa wa mara chache sana. Gazeti Mnara wa Mlinzi lilichapwa bila kukatizwa. Hata lile buku la saba la Studies in the Scriptures lilifika Swedeni na likatafsiriwa na kuchapwa wakati wa vita hiyo.

Ile Photo-Drama, Chombo Kingine

Vifaa vya kuonyeshea Photo-Drama of Creation—sinema na slaidi yenye kuambatanishwa na sauti, ikionyeshwa kwa saa kadhaa—ilifika Swedeni pia wakati Vita ya Ulimwengu ya 1 ilipokuwa ikilipuka. Wenzi wawili wa ndoa Waswedeni-Waamerika, William na Bella Undén, waliwasili kutoka United States waonyeshe namna ya kutumia vifaa hivyo. Chapa ya Kiswedeni ya Mnara wa Mlinzi, toleo la Oktoba 15, 1914, lilionyesha kwamba ndugu walionyesha bidii na hamu nyingi kwa hiyo Photo-Drama:

“Ni lazima sasa tufikie upesi iwezekanavyo majiji yote makubwa na mitaa katika nchi yetu, . . . kwa kuwa sasa twaona anga za ghadhabu zikiwa juu ya vichwa vyetu na ainabinadamu ikitetemeka kwa hofu kwa sababu ya tufani ambayo tayari inatikisa utaratibu uliopo wa mambo.”

Wonyesho wa kwanza ulifanywa katika Örebro Theatre Septemba 25, 1914. Jumba hilo lilijaa pomoni, na barabara nje ilisongamana watu ambao hawakuweza kuingia ndani. Wonyesho uliendelea katika usiku wa siku zilizofuata. Gazeti Mnara wa Mlinzi laripoti: “Mmiminiko wa watu ulizidi kuongezeka, hivi kwamba kila wakati, askari polisi kadhaa wenye kuvaa yunifomu walishiriki kikamili katika kutusaidia katika jitihada zetu za kuzuia umati wa watu.”

Gazeti moja la habari kutoka Sundsvall liliripoti hivi katika 1915: “Shukrani kwa wale walinzi bora, hakuna ghasia iliyotukia, lakini sikuzote hali zenye kimya za kukata tamaa zilionekana wakati milango ilipofungwa hatimaye. Maelfu ambao hawakuweza kuingia ndani walitawanyika bila kutaka, na wale waaminifu zaidi walibaki muda wote ambao wonyesho uliendelea ili angalau wawe karibu na ajabu hiyo, muujiza huo.”

Kwa muda wa miaka mitatu iliyofuata, Photo-Drama ilionyeshwa katika mamia ya mahali. Katika 1915 pekee, ilionyeshwa mara 1,256. Ilitimiza kazi kubwa katika kufahamisha watu makusudi ya Yehova na kufanya Biblia iwe hai. Lile gazeti la habari lililonakiliwa juu liliongeza kwamba Russell na waamini wenzake “wanafanya kazi, kama inavyojulikana vizuri sana, kuyafanya Maandiko Matakatifu yajulikane na watu wengi, kwa njia ya kufafanua maandiko mbalimbali ya Biblia, ili kutoa wazo la kiakili juu ya Mungu.”

Akiwa mwanamke kijana, Elin Anderson alishiriki sehemu katika kuonyesha Photo-Drama. Akiwa na umri wa miaka 90, macho yake hutoa machozi akumbukapo hivi: “Mimi nilikuwa wa kikundi cha akina ndugu na dada 12 waliosafiri kuizunguka nchi tukiwa na seti moja ya Drama. Kazi yangu ilikuwa kuwaelekeza kwenye viti wahudhuriaji na kuwatumikia. Lilikuwa jambo zuri ajabu kuona watu hao wote wakija na kuona jinsi walivyovutiwa. Wengi walikuja kuiona tena na tena, wakisimama kwenye mistari kwa saa nyingi ili wapate kiti. [Ni] wakati usiosahaulika na wenye furaha!”

Kweli ilienezwa pia katika wakati huo wa vita kwa magazeti yaliyochapisha hotuba za Ndugu Russell. Hiyo ilianza kabla ya vita na ikaendelea mpaka 1916. Yote pamoja, magazeti ya habari matano yalitoa safu kadhaa au kurasa kamili. Baadhi ya magazeti ya habari hata yalichapisha hotuba hizo kwa ukawaida katika matoleo yao ya Jumamosi. Ulikuwa utangazaji wenye kutokeza katika siku hizo kabla ya redio na televisheni kuwa vifaa vya nyumbani.

Akina Dada Wawa na Ushiriki Mkubwa Zaidi

Karibu na wakati huo wenye kusisimua wa mwaka wa 1914, watangazaji wa Ufalme kadhaa walichochewa wabadili sana maisha yao. Hesabu kadhaa ya akina dada vijana—wakati ilipofikiriwa kwamba wanawake vijana wapasa kuolewa na kulea watoto—walichukua utumishi wa wakati wote bila kusita na wakabaki humo mpaka kifo chao. Kazi yao imebarikiwa sana, kwa kuwa Mashahidi wengine wa ki-siku-hizi wenye bidii kadiri iyo hiyo katika Swedeni waweza kuwaita mama, nyanya, au hata mama mzazi wa nyanya yao wa kiroho.—Yoe. 2:28.

Mwuguzi mmoja kijana, Ebba Palm, alitaka sana kusaidia watu waliokuwa wagonjwa kiroho hivi kwamba alivaa yunifomu yake ya mwuguzi katika kazi ya kuhubiri. Kwa kuwa yunifomu yake iliwakilisha cheo chenye kustahiwa sana, cha Sophia Sisters, milango ya makao mengi yaliyokuwa ya kisasa zaidi yalifunguliwa kwake. Wakati wa miezi yake mitatu ya kwanza akiwa kolpota, aliangusha vitabu vilivyojalidiwa 1,085 na vijitabu vingi sana.

Ellen, dada mkubwa wa Ebba, aliacha kazi yake ya karani wa benki akaanza kazi ya kolpota. Bidii yake ilikuwa yenye kutokeza. Baada ya kuolewa, yeye na mume wake pamoja walitumia mashua kutembelea watu waliokaa kandokando ya sehemu nyembamba za Bahari ya Baltiki zilizoingia ndani sana ya nchi kavu pamoja na ghuba ndogo-ndogo.

Anna Wickbom alikuwa binti ya kamishna wa polisi. Alikuwa ametumika akiwa yaya katika kao la kifalme la Urusi na baadaye akiwa mwalimu wa kibinafsi katika familia moja kabaila (ukoo mashuhuri). Yeye alifuta kazi hiyo yenye mshahara mnono ili awe kolpota katika eneo la nyumbani kwao. Kwa kumtambua, majirani walimpokea kwa staha. Ufahamu wake mzuri wa lugha nyingi ulimfungulia milango mingi.

Wakati mmoja, alitembelea kao lenye fahari. Mke wa kabaila aliyeishi humo alimtuma mlangoni mtumishi wake wa maandalizi akamwogopeshe Anna. “Leo mke wa kabaila atazungumza kwa Kifaransa tu,” akanguruma. “Hiyo itanifaa kabisa,” akajibu Anna kwa ukali. Wakati mke huyo wa kabaila aliposikia Kifaransa bora cha Anna, yeye, akisema kwa Kifaransa kibovu, aliona aibu akasihi: “Kiswedeni, tafadhali!” Bila shaka mke huyo wa kabaila alivutiwa sana hivi kwamba kwa miaka mingi alichukua fasihi kila alipotembelewa na Mashahidi.

Mwanamke mwingine kijana, Maja Lundquist, alijitolea awe mtumishi kwa miaka mitatu wakati wa kuonyeshwa kwa Photo-Drama. Alifurahia sana pendeleo hilo hivi kwamba lilimsukuma aendelee kwa bidii katika huduma ya wakati wote kwa miaka 53, mpaka kifo chake. Jambo alilopenda kipekee lilikuwa kutoa ushuhuda katika meli za kigeni. Kwa miaka mingi, mwanamke huyu mwenye umbo dogo mwenye bidii na mchangamfu alionekana mara nyingi penye gudi na ndani ya vyumba vya meli, akiwaambia makapteni na wafanyakazi wao juu ya Ufalme wa Mungu na kuangusha fasihi vingi sana katika lugha nyingi. “Bandari ndiyo eneo langu bora zaidi,” alizoea kusema.

Uthabiti, imani, na ustahimilivu wa dada kama hao mapainia zilikuwa sifa za pekee sana. Aliyekuwa mratibu wa Halmashauri ya Tawi ambaye sasa amekufa, Johan H. Eneroth, aliripoti wakati mmoja hivi: “Inagusa moyo kweli kweli kujifunza jinsi wanawake dhaifu na wanyonge wanavyotembea kwa miguu yao, kilometa nyingi sana na nyakati nyingine katika misitu isiyo na barabara, wakibeba mifuko mizito ya vitabu, wakapate kijiji fulani kidogo kilicho peke yake na kuleta ujumbe wa tumaini na faraja na uchangamfu kwa watu wanaoishi chini ya hali ngumu sana.”

Je! Mlango Ungefungwa Katika 1918?

Mwaka wa 1918 ulipokuwa ukianza, matazamio yaliongezeka miongoni mwa akina ndugu. Unabii mbalimbali ulidokeza kwamba ungekuwa ndio mwanzo wa “ufufuo wa kwanza” na kuchukuliwa mbinguni kwa jamii ya bibi-arusi wa Kristo. (Ufu. 20:5, 6) Je! hiyo ingetia ndani wapakwa-mafuta wote, kutia na wale wa mwisho waliokuwa hai duniani wakati huo? Je! mlango wa kuingia katika “karamu ya arusi,” iliyonenwa kwenye Mathayo 25:10, ungefungwa karibuni? Maswali hayo yalienea miongoni mwa akina ndugu, yakiongoza kwenye mazungumzo mengi sana. Kwenye Ukumbusho, Machi 26, mwaka huo, 1,714 walishiriki mifano. Wengi wao waliwaza walikuwa wameadhimisha tukio hilo kwa mara ya mwisho. Kwani, ilionekana kana kwamba hata kazi ilikuwa imepunguza mwendo! Ndugu mmoja pilgrimu, Ernst Lignell, aliandikia tawi hivi:

“Sisi tunatumaini kwamba hiyo ilikuwa pindi ya mwisho ya aina hii upande huu na kwamba mwadhimisho wetu utakaofuata utakuwa wa kunywa kikombe cha kushangilia katika Ufalme. Hata hivyo, mapenzi ya Baba yetu na yafanyike katika kila jambo! Ikiwa ingempendeza kutuacha tukae kwa muda mrefu kidogo hapa chini katika ‘bonde la uvuli wa kifo,’ sisi tunataka kutii uamuzi huo wake. Lakini kulingana na yote yanayoonekana, yaelekea wakati ni mfupi sana.”

Ingawa hivyo, Bwana-arusi alikuwa na mambo mengine mazuri ajabu akilini kwa ajili ya hao wa mwisho wa wapakwa-mafuta walio duniani. Katika 1919, kwenye ule mkusanyiko mzuri ajabu kwenye Cedar Point, Ohio, walikumbushwa juu ya pendeleo lao wakiwa mabalozi wa Bwana kutangaza Ufalme mtukufu wa Mungu uliokuwa ukija. Wakati mwangwi (mrudisho wa sauti) kutoka kusanyiko hilo ulipofika Swedeni, akina ndugu walishangilia na upesi wakajirekebisha wajipatanishe na utume huo. Kazi ikaongeza mwendo tena.

Tani nyingi za fasihi viliangushwa. Kile kijitabu Millions Now Living Will Never Die (Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe) na Where Are the Dead? (Wafu Wako Wapi?) vilikubaliwa kwa hamu. Nyakati nyingine makolpota walihitaji fasihi hivyo kwa haraka sana hivi kwamba walikuwa wakipelekea tawi simu ya kuandikwa wapelekewe “Milioni 500” au wawapelekee “Wafu 200”—ujumbe uliowatatanisha wafanyakazi wengi wa simu za kuandikwa.

Mitihani Migumu Katika Miaka ya 1920

Sasa, utendaji huu wa bidii haukupita bila kuonwa na yule adui mkuu, Shetani Ibilisi. Yeye alijaribu kuzima bidii ya akina ndugu kwa ajili ya kazi na kwa kueneza mawazo ya kukata tamaa. Kisha akajaribu kutumia udhaifu mbalimbali katika nyutu za kibinadamu, kuanzia karibu na 1920 na kufikia upeo katika 1925. August Lundborg, aliyekuwa amebeba daraka la tawi la Sosaiti kwa miaka 20, alianza kupoteza hali ya kujiona ifaavyo kuhusiana na tengenezo la Mungu. Akipuuza shauri na maagizo kutoka kwa tengenezo, alianza kutayarisha makala za Mnara wa Mlinzi kulingana na fasili yake mwenyewe. Akina ndugu wakavurugika. Kazi ikapungua mwendo. Wakati mwingi na jitihada zilitumiwa kwa upendo ili kumfanya mwenye kukosea atambue mwendo wake wenye kosa na kutubu.

Kwa busara, tengenezo la Mungu liliendelea kupinga hila za Shetani. Wakati Ndugu Rutherford alipopata kujua habari za matatizo hayo, alichukua tendo mara moja kwa kumtuma Ndugu A. H. Macmillan akatatue tatizo hilo, katika Mei 1921. Lakini Ibilisi hakukubali kushindwa. Upesi yale matatizo yakatokea tena, na kufanya Ndugu Rutherford kwenda Swedeni yeye binafsi katika 1922. Mkusanyiko ulifanywa katika Örebro kwa matumaini ya kuwatia ndugu moyo.

Baada ya kupata habari juu ya magumu mengine katika mwaka uliofuata, Ndugu Rutherford alipeleka barua iliyokuwa na tarehe ya Mei 23, 1923, kwa ndugu wote, akiwahimiza waendelee kujishughulisha na utumishi: “Wakati umefika wa kuchukua tendo la umoja kotekote katika Swedeni. Hapa ninasihi kila mmoja wa waliojitoa katika Swedeni washirikiane kwa umoja na upatano katika kutangaza kweli.”

Katika 1924 Ndugu C. A. Wise, ambaye wakati huo alikuwa ndiye makamu wa msimamizi, alitumwa Swedeni akasaidie. Ripoti yake ilimfanya Ndugu Rutherford atie Swedeni katika safari yake ya Ulaya katika mwaka wa 1925. Mkusanyiko kwa ajili ya Swedeni, Norwei, Denmarki, na Finlandi ulifanywa Örebro katika Mei wakiwako watu 500 waliohudhuria.

Wakati wa Badiliko

Kisha Ndugu Rutherford akatangaza kwa njia yenye kuridhisha kwamba ofisi mpya, Ofisi ya Ulaya Kaskazini, kama ile Ofisi ya Ulaya ya Kati iliyoanzishwa katika Switzerland miaka michache mapema kidogo, ingefunguliwa katika Copenhagen, Denmarki. Ofisi hiyo mpya ingesimamia kazi katika Swedeni, Denmarki, Norwei, na Finlandi, kutia na yale mataifa yenye kujitawala ya Baltiki—Estonia, Latvia, na Lithuania. Pia ingechukua uhariri halali wa Mnara wa Mlinzi. Matawi katika Swedeni, Denmarki, Norwei, na Finlandi yangeendelea kama hapo awali lakini yakiwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Ofisi ya Ulaya Kaskazini, William Dey kutoka London akiwa msimamizi. Tangazo hilo lilipokewa kwa shauku na walio wengi miongoni mwa wale watu 500 waliokusanyika.

Muda mfupi baada ya kusanyiko, Ndugu Lundborg alimjulisha Ndugu Rutherford kwamba yeye hataki tena kuwa na daraka juu ya tawi. Ndipo Ndugu Rutherford akaandika hivi: “Ndugu Lundborg akistaafu, itakuwa kulingana na chaguo lake mwenyewe, na kwa hiyo mimi namwomba Ndugu Dey amweke Ndugu Johan Henrik Eneroth asimamie ofisi hiyo. Mwajua kwamba yeye alizaliwa na kulelewa Swedeni, ajua watu na hali za huko, na zaidi ya yote amejitoa kabisa kwa Bwana.”

Enzi Mpya ya Usimamizi wa Tawi

Ndugu Eneroth alikuwa amejifunza juu ya kweli alipokuwa akitumika akiwa luteni wa kwanza katika Jeshi la Kifalme la Swedeni wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 1. Alipokuwa kazini katika Swedeni kaskazini, mama yake alimpelekea Buku la 4 la Studies in the Scriptures, lililoitwa “Vita ya Har–Magedoni.” “Kitabu hicho kilinifanya nitambue kwamba kuna vita yenye maana kubwa zaidi inayokabili ainabinadamu kuliko ile mataifa ya ulimwengu yalikuwa yakipigana,” akasema. Siku moja alijipa moyo akatembelea kao la Wanafunzi fulani wa Biblia. “Wazia sura ya uso wa mwanamume huyo na mke wake walipompata ofisa wa kijeshi akiwa anavaa yunifomu amesimama mlangoni pao akiomba funzo la Biblia,” akasema na kuongeza: “Mshangao wao wa kwanza ulipotulia, walinikaribisha kwa uchangamfu.”

Eneroth aliacha jeshi na upesi akaingia katika utumishi wa wakati wote. Katika 1920 alialikwa akafanye kazi kwenye tawi katika Örebro. Baadaye mwaka huo, aliachishwa kazi na Lundborg halafu akatumikia katika Denmarki mpaka alipowekwa asimamie tawi katika Örebro katika 1925. Kwa hiyo, baada ya aliyekuwa hapo awali kapteni wa Jeshi la Wokovu kuwa ameangalia tawi kwa miaka mingi, sasa Yehova aliruhusu aliyekuwa hapo awali luteni wa Jeshi la Kifalme la Swedeni achukue usimamizi.

Ndugu Eneroth alikuwa na umri wa miaka 32 tu alipokuwa mwangalizi wa tawi katika Swedeni. Alishikamana kwa uaminifu na mgawo wake kwa miaka 50 akimaliza mwendo wake wa kidunia kwa uaminifu katika Februari 7, 1982.

Kuunganisha Akina Ndugu Tena

Baada ya kuchukua kazi yake, Ndugu Eneroth, akisaidiwa na Ndugu Dey, alianza kusaidia akina ndugu wachukue tena kwa umoja kazi ya kuhubiri. Pamoja, walitumia muda wapata mwaka mmoja kutembelea makundi 70 hivi kotekote nchini. Ndugu Eneroth alitafsiri hotuba za Ndugu Dey. “Katika mahali pengi, tulilazimika kuwapangisha ndugu mistari kihalisi katika pande mbili, wenye kuunga mkono na wenye kupinga Sosaiti,” akasema Ndugu Eneroth.

Hivyo akina ndugu na dada walitiwa moyo kwa juhudi walitumaini tengenezo la Yehova na kusonga mbele na kazi. Pole kwa pole, walijipanga tena kitengenezo nao wakapata baraka kamili za Yehova kwa mara nyingine tena. Wapinzani walipiga kelele kwa kitambo nao wakajaribu kupanga mambo kwa njia yao, lakini—kama ilivyo katika hali nyingine zinazofanana na hiyo—upesi walipungua na wakatoweka kabisa wasionekane. Kwa mara nyingine tena, jitihada za Shetani za kukomesha kazi zilishindwa kabisa.

Ndugu Dey, Mskochi halisi na ambaye hapo kwanza alikuwa mkaguzi wa kodi katika London, alijua namna ya kuchanganua mambo katika ofisi ya Swedeni. Kuanzia Machi 1926, kichapo Bulletin (sasa huitwa Huduma ya Ufalme Yetu), kikiwa na maagizo juu ya utumishi na shuhuda zilizotayarishwa, kilipelekwa kila mwezi kwa wahubiri wote ili kuwasaidia katika kazi yao. Pia nchi iligawanywa kuwa maeneo ya ukubwa wenye kufaa zaidi. Yote hayo yaliwachochea akina ndugu wafanye upya jitihada zao, na kile Kitabu cha Mwaka cha kwanza, chenye tarehe ya 1927, kilikuwa na maneno yenye kutoa tumaini katika ripoti kutoka Swedeni:

“Kungali kuna mengi ya kufanywa kuhusiana na kupanga mambo kitengenezo, lakini ni shangwe kweli kweli kuona jinsi marafiki wanavyozidi kupata wazo, kwamba sasa tunapiga vita chini ya Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. Na wote walio waaminifu wanathamini sana gazeti MNARA WA MLINZI ambalo lazidi kuleta nuru, burudisho na kichocheo katika kila toleo linalokuja. Madarasa zaidi na zaidi yanachukua gazeti MNARA WA MLINZI kwa ajili ya funzo, nayo yaripoti baraka nyingi kutokana nalo.”

Kutoa Ushuhuda Mazikoni

Mashahidi wa Yehova walipata njia nyingine ya kutoa ushuhuda katika Swedeni kuanzia 1926 na kuendelea. Sheria ilitungwa ambayo iliruhusu maziko yafanywe bila usaidizi wa padri wa Kanisa la Serikali. Hivyo, maelfu ya waliofiwa wangeweza kufarijiwa kwa hotuba za Kimaandiko. Watu mamia ya maelfu ambao pengine hawangesikiliza kwa njia nyingine, wamesikiliza shuhuda kwenye maziko.

Martin Wenderquist ambaye sasa amekufa, na aliyekuwa mtendaji katika kazi ya Ufalme kwa miaka 67, aliombwa mara nyingi atoe hotuba za maziko. Alisema wakati mmoja hivi: “Kufariji watu wakati wa kuongoza mahubiri ya maziko ni jambo ambalo nimefanya mara zaidi ya 600 katika mahali tofauti-tofauti katika Swedeni na Finlandi. Ni vigumu kupata wasikilizaji wasikivu na wenye kuitikia zaidi wenye kuhudhuria maziko. Mafunzo mengi ya Biblia yameanzishwa baadaye, yakiongoza watu kwenye kweli.”

Hatua Yenye kuburudisha

Hatua ya kitheokrasi yenye kuburudisha ilikuwa kuhamisha ofisi ya tawi kuirudisha Stockholm katika Septemba 1926. Ndugu walipata mahali penye kufaa kwenye Drottninggatan 83, katikati kabisa ya jiji. Na ilifaa kama nini kwamba jirani ilikuwa kampuni ya uchapaji iitwayo Egnellska Boktryckeriet, ambayo, kwa kufaa sana, ilitumiwa kuchapa magazeti yetu kwa miaka 28!

Ofisi ilihamishwaje? Meli mbili zikiwa zimejaa kabisa zenye kupitia kwenye mifereji zilihamisha vifaa vyote vya tawi mwendo wa kilometa 200 kutoka kwenye jiji la bara la Örebro kuzipeleka Stockholm jiji la pwani. Familia ya Betheli ilifuata ikiwa ndani ya meli ya tatu. Safari hiyo ilichukua siku moja na usiku mmoja.

Miaka mitatu baadaye, jengo la mawe lenye orofa nne katikati ya jiji lilipatikana kwenye Luntmakaregatan 94. Ndugu Rutherford alitaka Sosaiti ilinunue. Na ndugu wengi wenye nia walikopekesha pesa za kulipa amana ya jengo hilo. Hatimaye, baada ya miaka mingi ya kuhama-hama, ofisi ya tawi ikakaa mahali hapo, ambapo pangetumikia faida za Ufalme kwa miaka 25 iliyofuata.

Motokaa ya Kwanza—Ajabu Kubwa

Katika 1927 Ndugu Rutherford aliruhusu tawi linunue motokaa yao ya kwanza, Aina ya A Ford mpya kabisa. Hata hivyo, haikuwa ya kutumiwa na wafanyakazi wa tawi ikiwa gari la anasa kwenye barabara za jiji. Ingetumiwa na ndugu wawili mapainia kwenye barabara ambazo karibu hazipitiki ili waende kwenye vijiji vilivyo mbali, ndani-ndani ya misitu katika Kaskazini ya Mbali, katika Lapland. Tokea Aprili hadi Septemba 1930, waliripoti ya kuwa walisafiri kilometa 11,000 wakaangusha vitabu zaidi ya 2,000 na vijitabu 4,000.

Gari hilo la Ford lilivutia watu katika sehemu hizo zilizo peke yazo, ambako magari yalionwa mara chache sana au hayakuwa yamepata kuonwa kamwe. Watu wengi wenyeji waliwaendea akina ndugu na kuwaomba fasihi ili tu wakaribie zaidi waone mashine hii ya ajabu na kunusa moshi wa mafuta yenye kuchomwa na injini, ambao kwao ulikuwa kama marashi. Walilisukuma kwa nia walipoombwa kusaidia ili litoke kwenye matope au wakaliburuta kwa farasi wao litoke katika mtaro.

Siku moja, ndugu hao wawili waliwatolea vitabu kikundi cha wafanyakazi ya barabara. Kwa kuwa hawakuwa na pesa, mmoja wao akasema: ‘Fuateni barabara hii mpaka mpate nyumba. Hapo ndipo tunakaa. Mpeni mtunza nyumba vitabu na kumwambia atoe kibeti changu chini ya mto na kuwalipa.’ Ndugu walipofika mahali hapo na kubisha mlango, hakuna mtu aliyefungua. Mlango huo ulikuwa umefungwa kwa kufuli. Hata hivyo, baada ya kuchunguza nje ya nyumba hiyo, walipata dirisha dogo lililofunguliwa juu ukutani, nao wakakumbuka unabii wa Yoeli 2:9 usemao: “Huingia madirishani kama aingiavyo mwivi.” Mmoja wao akapanda na kuingia ndani kupitia dirishani, akapata kibeti kile, akachukua kiasi kifaacho. Kisha akarudisha kibeti chini ya mto, akaweka vitabu kitandani na kwa uangalifu akatokea njia ile ile aliyokuwa ameingilia. Hawakupata kujua kamwe kama mfanyakazi huyo wa barabara alikuja katika kweli. Hata hivyo alipata vitabu vyake!

Enzi ya Baiskeli

Baiskeli zikiwa zinatumiwa na watu wengi katika miaka ya 1930, wale makolpota wenye kufanya kazi kwa bidii waliendesha baiskeli, kuwe mvua au jua, katika barabara zenye mawe, na zenye matope na vijia ili wafikie mashamba na vijiji vilivyokuwa mbali sana katika maeneo hayo makubwa mno. Dada Rosa Gustavsson, akiwa na imani yenye nguvu, na mwenye ucheshi, na baiskeli, husimulia juu ya kazi yake ya kolpota katika miaka ya 1930 akiwa na dada-mkwe wake, Mirjam Gustavsson:

“Tulienda parishi kwa parishi, tukiwa tunabeba mizigo mikubwa iwezekanavyo ikiwa imefungiwa juu ya baiskeli zetu—viatu, mavazi, taulo na mswaki, vyombo vya kupikia, na, cha maana zaidi ya yote, vibweta vya vitabu na vijitabu. Ajabu iliyoje! Sikuzote haikuwa rahisi kupata mahali pa kulala. Mara nyingi tulimsihi Yehova kwa sala atupe msaada. Nakumbuka siku moja, baada ya kufanya utumishi mchana kutwa tukiwa tumetengana, Mirjam nami tulikutana pamoja jioni sana. Pamoja, tuliendesha baiskeli huku mvua ikinyesha kuelekea nuru hafifu ambayo tuliiona kwa mbali. Ilikuwa nyumba katika shamba moja. Tulikuwa tunaona baridi hadi mifupani. Ilikuwa imekuwa siku ndefu, yenye kutumaliza nguvu. Ghafula, tukaitambua nyumba ile. Mioyo yetu ikashuka kwenye matumbo yetu. ‘Watu hao wanapinga!’ tukapaaza sauti huku tukitazamana. Huku akisita kidogo, Mirjam akaenda kwa woga kuelekea mlango na kuomba mahali pa kulala. Kwa mshangao na faraja kubwa, familia ile ikatualika ndani. Walitupeleka katika chumba kilicho bora zaidi katika nyumba hiyo, wakatupa mlo mtamu sana. Tukiwa tumeshiba na kutosheka, tuliondoka mezani tukaonyeshwa chumba cha kulala ambacho tungetumia. Loo, hatukuweza kuamini macho yetu. Vitanda vilikuwa vimetandikwa kwa mashuka ya kitani iliyo bora zaidi, kuliko vile sisi tungeweza kugharimia!

“Usiku ulipita upesi huku tukiwa na ndoto nzuri, nayo asubuhi ikafika upesi sana. Hata hivyo, baada ya kulishwa kiamshakinywa, tulijitolea kulipa. Lakini walikataa pesa zetu. Tungeweza kuonyeshaje uthamini wetu? Kitabu Deliverance kingewakumbusha namna tulivyojisikia. Kwa hiyo tukauliza, ‘Twaweza kuwapatia hiki kiwe kikumbusho cha uthamini wetu?’ ‘Aah, ndiyo, tunataka kitabu hicho!’ wakajibu kwa haraka. ‘Mmoja tunayejuana naye alituambia kwamba mlikuwa mmewapatia kimoja wakati mlipokaa naye, na alikipenda sana.’ Ni wazi kwamba, hilo lilitufundisha somo. Hujui kamwe ni tunda gani litatokea kutokana na angusho moja la fasihi ya Biblia.”

Ndugu Axel Richardson, mfupi kwa kimo lakini jitu kiroho, husimulia hivi: “Katika 1936, Asta, mke wangu mwenye umbo jembamba nami, tulipewa mgawo tutumike katika ile sehemu kubwa mno ya magharibi ya mkoa wa Jämtland yenye milima-milima. Mali ya kidunia pekee tuliyokuwa nayo wakati huo ilikuwa baiskeli mbili, hema moja, sanduku la godoro, na sanduku la mavazi. Lakini tulikuwa tumeazimia kabisa kueneza eneo letu, bila kuacha kambi yoyote ya Lapp iliyo peke yake au shamba la milimani likiwa halijatembelewa. Mara nyingi kila siku tulikwea na kuvuka milima isiyoisha yenye mawe-mawe makumi ya kilometa tukiwa tumevaa buti, nyayo zetu zikiwa zimevimba na kuuma, riziki yetu ya kila siku na vitabu vikiwa migongoni na mikononi mwetu. Axel hukumbuka jambo aliloona pindi moja wakati mke wake alipokuwa hayuko pamoja naye: “Mwanamume mmoja mwenye fadhili, ambaye sikumjua, alinivusha ziwa kwa motaboti yake bila malipo. Baada ya mwanamume huyo kuniacha pwani, nilimtazama akirudi ng’ambo ile nyingine. Nilitazama huku na huku. Nilikuwapo mahali hapo mimi peke yangu nikiwa na baiskeli yangu na mkoba mzito wa vitabu katika mahali palipo peke yake kabisa. Nilijisikitikia. Eneo hilo lote lilikuwa na nyumba tatu tu. Baada ya kuzitembelea, nililazimika kusonga mbele. Lakini namna gani? Upande mmoja lilikuwako lile ziwa na mlima wenye kusimama wima upande ule mwingine. Hakukuwa na uchaguzi. Baiskeli ikiwa juu ya bega moja na mkoba wa vitabu juu bega lile jingine, nilianza kukwea mlima ule. Baada ya kukwea kwa saa kadhaa za kazi ngumu yenye kunimaliza nguvu, kwa mtweto wenye kuonyesha kutulia nikaanza kuteremka upande ule mwingine. Mwanamume aliyeishi chini ya mteremko huo akaniuliza, ‘Jamani katika ulimwengu huu umetoka wapi?’ Alinikodolea macho kwa mshangao nilipoelekeza kidole kwenye mlima huo mrefu. ‘Wewe ndiwe wa kwanza kupitia njia hiyo,’ akasema, ‘na umefanya hivyo ukiwa juu ya baiskeli!’ Nilifurahi kuwa nilifanya jitihada hiyo kwa ajili ya habari njema.”

Kutumia Njia Zote

Kufikia katikati ya miaka ya 1930 mapainia wapatao 60, wakiwa na shughuli nyingi kama nyuki, walitumia njia zote za usafiri, kutia na vifaa vya kupitia juu ya theluji, viatu vya kupitia juu ya theluji, baiskeli, gari la kukokotwa na farasi, mabasi, magarimoshi, na mashua, ili kueneza habari njema kwenye pembe zote za nchi.

Wakati wa miezi mitatu katika 1935, ndugu wawili walitumia motaboti kutembelea visiwa 284 katika pwani ya mashariki na kusini mwa Stockholm na kuhubiria wakaaji walioko sehemu zilizo peke yake huko. Waliripoti kwamba kwa ujumla walikuta watu 1,053 na wakaangusha vitabu 428, na vijitabu 1,145, maandikisho 68, na nakala 496 za gazeti Golden Age. Visiwa kadhaa miongoni mwa visiwa hivyo vidogo vilikuwa havijapata kutembelewa kamwe kwa ujumbe wa Ufalme kabla ya mwaka huo.

Ustadi mwingi ulitumiwa katika kueneza habari njema. Katika Hjo kundi dogo la wahubiri wapatao kumi walikodi lori dogo wakati fulani mapema katika 1930 na kulifunika kwa hema. Lilikuwa gari lenye kufaa sana kwa utumishi wa shambani. Ustadi wao ulifanikiwa wakati baadaye mwenyeji wa gari hilo alipokuja katika kweli. Kisha akaliunda upya gari hilo likawa minibasi, ambayo iliendelea kutumiwa kwa miaka kadhaa katika kueneza kweli katika miji 6 na manispaa 132.

Katika 1939 mapainia wawili, David Börjesson na Elis Hulthén, walinunua lori lililokwisha tumika la tani 2.5. “Tuliliunda upya kwa bidii liwe kao lenye kuendeshwa kwa mota ili litumiwe katika utumishi wa painia,” asema Elis ambaye sasa amezeeka. Akiegemea kwenye fimbo yake ya kutembelea, yeye aendelea akiwa na mwanga wenye ucheshi katika macho yake:

“Ijapokuwa kuta zilikuwa zimetengenezwa kwa mbao za nyuzi-nyuzi, ilionekana kama motokaa yenye zana za vita, kwa kuwa tuliipaka rangi ya kijivu. Tulikuwa ndugu wanne waseja wenye nguvu, tukiishi katika ushirika mzuri katika kao letu lenye mwendo lenye kuonekana kama limeundwa kwa chuma. Tulipendezwa kutumia gari hilo katika mgawo wetu katika Swedeni ya kati.”

“Vita ya ulimwengu ya pili ilikuwa ikiwaka moto katika Ulaya wakati huo. Kama vile ingetazamiwa, watu fulani walikuwa wenye kushuku sana walipoona lori hilo la kijivu likiwa limeegeshwa katika ujirani wao. Watu wengine hata waliliogopa nao wakaliepuka kwa kupitia msituni. Nyakati fulani watu wenye kupinga walituma polisi watufuate. Usiku mmoja maofisa wawili wa polisi walikuja kuchunguza. Baada ya kusikiliza mahubiri yaliyorekodiwa, ambayo yaliwapa ushuhuda mzuri, waliondoka bila kutoa lalamiko. Wakati mmoja askari polisi mkuu alikuja kuchunguza tulikuwa watu wangapi katika kikundi chetu. ‘Lazima wawe angalau watu kumi katika lori hilo,’ ndivyo watu walivyokuwa wamemwonya. Katika pindi nyingine, mkulima mmoja alikuja akiwa anatoa machozi na kutusihi: ‘Tafadhali, vijana, iondoeni motokaa hii katika shamba langu. Tafadhali, fanyeni hivyo. Watu wamekuwa wakinitukana kwa kuwaruhusu mkae hapa.’

“Majira hayo ya baridi ya wakati wa vita yalikuwa yenye baridi kali sana. Usiku tulijaribu kupasha gari hilo joto kwa kipasha-joto chenye kutumia mafuta ya taa. Hata hivyo, mvuke uligeuka kuwa maji nao ukaanza kutiririka kwenye upande wa ndani wa kuta za chumba na kuanguka sakafuni na kugandamana. Asubuhi moja, David, akiwa katika mojawapo vitanda vya sehemu ya chini zaidi, alilalamika kwamba alikuwa mwenye baridi kama barafu. Si ajabu, mbao iliyokuwa chini ya godoro lake ilikuwa imegeuka kuwa bapa la barafu. Tulijaribu kumfariji kwa kumwambia: ‘Vitu vilivyogandamana havichakai.’ Sisi sote tulipata kuzoea taabu, nasi hatukupata kamwe kuwa wagonjwa. Hilo ‘gari lenye zana za vita’ lilisaidia watu wengi wenye maelekeo yanayofaa wapate kweli.”

Upanuzi Kabla ya Vita ya Ulimwengu ya 2

Kipindi kilichokuwa kabla ya vita ya ulimwengu ya pili kiliona upanuzi mkubwa. Kutoka 1925 kufika 1938, hesabu ya watangazaji wa Ufalme iliongezeka kutoka kwa wapatao 250 kufikia kilele cha 1,427. Wakati wa miaka hiyo, wahubiri hao wenye bidii waliangusha karibu vitabu na vijitabu milioni tano, bila kutaja maelfu ya maandikisho yaliyopatikana na makumi ya maelefu ya magazeti yaliyogawanywa.

Kwa kawaida wahubiri hao wajasiri walitoa ushuhuda kikamili. Hesabu ya shuhuda zilizotolewa kwa watu wote zilihesabiwa wakati wa pindi moja katika 1932: Wahubiri wapatao 300, wakishiriki sehemu katika kazi ya kutoa ushuhuda kila juma, waliripoti shuhuda 515,119. Hiyo ililingana na moja kwa 12 ya idadi ya watu wa Swedeni!

Jitihada za Kumwonya Hitler

Baada ya kile kipindi cha kuogopesha cha Nazi kuanza katika 1933 katika Ujerumani, ripoti zilifika Swedeni kwamba Mashahidi wa Yehova katika Ujerumani walikuwa chini ya mkazo mkubwa. Mwaka uliofuata tukio lenye kusisimua lilitukia wakati akina ndugu katika Swedeni walipoalikwa na makao makuu ya Brooklyn wajiunge na ndugu zao katika Ujerumani na katika nchi nyinginezo 48 wajieleze kwa niaba ya ndugu zao Wajerumani.

Baada ya mkusanyiko wa pekee katika makundi yote Jumapili, Oktoba 7, 1934, Hitler alipelekewa telegramu, zikihimiza: “Ukatili wenu juu ya Mashahidi wa Yehova unawashtua watu wote wema wa dunia nawe unalidharau jina la Mungu. Acheni kuwatesa Mashahidi wa Yehova; ama sivyo Mungu atawaharibu ninyi na chama chenu cha kitaifa.”

“Jamii” Mpya Yatambulishwa

Habari zenye kutokeza zilikuja kutoka kwenye mkusanyiko mkubwa katika Washington, D.C., katika 1935. Ndugu Rutherford alikuwa ametoa ushuhuda wa Kimaandiko kwamba ule “mkutano mkubwa,” au “umati mkubwa,” wa Ufunuo 7:9 ulikuwa sawa na ‘Wayonadabu,’ ile jamii ya kondoo wa Mathayo 25:31-46. (Yer. 35:18, 19) Wengi ambao walikuwa wamejidhania kwamba walikuwa wa kikundi cha pili cha kiroho sasa wakatambua kwamba walikuwa wa wale “kondoo wengine,” wenye tumaini la kidunia.—Yn. 10:16.

Telegramu moja iliyokuwa ikitangaza habari hiyo yenye kushangaza kutoka Washington, D.C., iliwasili wakati wa mojapo vipindi kwenye mkusanyiko wa kila mwaka wa Stockholm. Wasikilizaji walisomewa, nao msisimuko ukawa mkubwa sana miongoni mwa wajumbe hao 300. Ombi lilitolewa kwamba wote waliohudhuria wapaswa kuanza kutafuta hao kondoo wengine.

Itikio kwa ombi hilo linaonyeshwa katika ripoti ya mwaka wa utumishi wa 1936: “Katika Swedeni mkutano huo umeendelea kujidhihirisha . . . Wayonadabu 150 wameripotiwa kuwa wamejitoa kwa Bwana tangu Oktoba 1, mwaka jana [1935], nasi twajua mahali kadhaa ambako hesabu fulani wanangojea fursa ya kufanya hivyo. Katika kila mkusanyiko wa utumishi watu kadhaa wa jamii hiyo hujitokeza na kuanza kutoa ushuhuda.”

“Acheni Kuwazuia”

Kwenye mkusanyiko uo huo, jambo la maana kuhusu kikundi kingine miongoni mwa watu wa Mungu lilielezwa wazi. Ushiriki wa watoto katika kueneza habari njema ulizungumzwa. Chini ya kichwa “Acheni Kuwazuia,” Bulletin ya Kiswedeni ya Agosti 1935 ilitaarifu kwa muhtasari hivi:

“Inafaa kabisa. . . . Waacheni waanze kwa kuandamana na wazazi wao au mhubiri mwingine aliye mtu mzima. . . . Italeta baraka tu wakishiriki kazi hii—maadamu, bila shaka, kwamba inakuwa hivyo kwa sababu wamejifunza kutoka kwa wazazi wao au waandamani wao kumpenda na kumheshimu Mungu mkuu na kushangilia pamoja na Ufalme wake, kwa kadiri wanavyoweza kuelewa.” Wachanga hao walibubujika tu kwa msisimuko kusikia habari hizo kuu nao walikuwa na hamu kuanza kama kikundi cha farasi.

Kupitia Ile Miaka Migumu ya Vita

Acheni turudie nguzo ya kazi—utumishi wa painia. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 2, mapainia waliendelea kueneza kweli kwa bidii hata zaidi kotekote nchini, ujapokuwa upungufu wa pesa, chakula, mavazi, na mafuta. Ijapokuwa Swedeni iliepuka vita yenyewe, mamlaka za kiserikali ziliweka vizuizi na kuuza bidhaa kwa kipimo. “Ukiwa painia wakati wa miaka hiyo, ilikuwa lazima umtegemee Yehova kikweli,” asema Gustaf Kjellberg, ambaye katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1930 aliacha kazi yake ya maisha akiwa mpiganaji mieleka ajitolee kabisa kwa kweli. Gustaf, ambaye angali anapainia, akumbuka hivi:

“Wakati wa kiangazi (majira ya jua), mimi na painia mwenzangu tuliishi katika hema, lakini wakati wa kipupwe (majira ya baridi), tulikodi mahali pa kukaa katika makao ya watu binafsi. Mara nyingi hilo lilikuwa jambo gumu na lenye kugharimu sana. Katika jitihada za kusaidia, Sosaiti ilitupelekea maelezo ya jinsi ya kujenga gari linaloweza kukunjwa na ambalo lingeweza kukokotwa nyuma ya baiskeli. Mara hiyo tukaagiza tujengewe moja.

“Kulikuwa na baridi wakati wa kipupwe, kwa kuwa gari hilo la kukokotwa lilikuwa limejengwa kwa mbao za nyuzi-nyuzi. Kuongezea kulipasha joto kwa kuchoma kuni na tumba la mbegu za msunobari katika jiko la chuma, tulijikunja tukiwa na nguo zetu zote ili tupate joto kidogo. Usiku mmoja mwenzangu aliniamsha akilalamika kwamba hawezi kuinua kichwa chake. Na si ajabu! Nywele zake nzito zilikuwa zimegandamana kwenye fremu ya chuma ya kitanda chake kwa sababu ya barafu! Ilikuwa lazima nimfungue kwa kuyeyusha barafu kwa kutumia mikono yangu. Hata hivyo, katika wakati wote tulioishi katika gari hilo la kukokotwa, hatukupata kuwa wagonjwa kamwe na tuliweza kutumia siku ndefu tukihubiri habari njema. Ulikuwa wakati mzuri ajabu kama nini!”

Ingvar Wihlborg alitoa ushuhuda miongoni mwa watu wa Lapp na kueneza maeneo makubwa katika Kaskazini wakati wa miaka ya mwisho-mwisho ya 1930. Yeye hukumbuka hivi: “[Kule] kaskazini ya mbali kupita Mzingo wa Aktiki kilikuwako kile kisehemu cha nchi chenye wakaaji wachache, ambacho ni cha urefu wa kilometa 130, katikati ya Kiruna na mpaka wa Norwei. Ili nipate njia yangu, nililazimika kutembea kwa miguu au kutumia vifaa vya kuendea mbio juu ya theluji kufuata njia ya reli, jambo ambalo nilifanya mara mbili kwa mwaka. Jioni moja yenye baridi na giza, garimoshi lilitokea ghafula nyuma yangu. Mashine yalo yenye nguvu nyingi ya kupulizia mbali theluji ikanirusha juu sana hewani pamoja na vifaa vyangu vya kuendea mbio juu ya theluji na mfuko wangu niliofungia mgongoni kupitia mabegani nikaanguka katika bonde lenye kina kirefu. Basi, ilinichukua sekunde kadhaa kurudia fahamu zangu. Asante kwa taa za Hoteli ya Watalii ya Abisko, nilipata njia ya kutokea. Wafanyakazi wa hoteli waliduwaa nilipopiga hatua kuingia ndani huku nikionekana kama mtu wa theluji. Wakauliza ‘Jamani, katika dunia hii umekujaje hapa?’ ‘Kwa kupitia hewani,’ nikajibu kwa uchangamfu. Walikuwa wenye fadhili nao wakanipa kinywaji cha kakao chenye moto na sandwichi.”

Zijapokuwa hali ngumu za maisha za wakati huo katika Swedeni na majira ya baridi yenye baridi kali isivyo kawaida, hao mapainia wenye bidii hawakupunguza mwendo katika utendaji wao. Yehova aliendeleza mioyo yao ikiwa yenye joto. Kazi ilizidi kupanuka wakati wa miaka hiyo. Hesabu ya waabudu ikawa zaidi ya mara mbili, kutoka 1,427 katika 1938 kufika 2,867 katika 1945, baada ya vita hiyo.

Upinzani Walipuka

Wanenaji wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo walijaribu pia kuvunja moyo watu wa Mungu. Tawi liliripoti hivi:

“Kufikia wakati huu ni vigumu kupata gazeti la habari la aina au namna yoyote nchini ambalo halijachapisha makala moja au zaidi zenye kuonyesha chuki zikishutumu mashahidi wa Yehova kuwa ‘kikundi cha waungaji mkono adui wa siri wenye kufitini serikali wanaosaidiwa kifedha na nchi za kigeni,’ ‘walinzi wa kwanza wa ukomunisti,’ ‘manabii bandia,’ ‘maadui wa serikali na wa jamii,’ n.k., n.k., wakitumia maneno yote yaliyo ya kawaida ya kutuvunjia heshima. Ni wazi kwamba, jamii ya makasisi ndio walioyatokeza, . . . na maneno hayo machafu katika vyombo vya habari yalifikia upeo wakati baraza kuu la makanisa lilipokuwa limekusanyika katika mji mkuu katikati ya Mei.”

Mlipuko huu wa chuki ulianza baada tu ya Mashahidi kugawanya kwa bidii nyingi nakala 300,000 za kijitabu Fighting for Liberty on the Home Front. Katika kampeni yenye ghadhabu kali, jamii ya makasisi walianza kutumia njia yetu, wakitembelea watu nyumba kwa nyumba na kuwalazimisha wasome yaliyoandikwa dhidi yetu.

Kampeni Yawa na Matokeo Yasiyotakwa

Hata hivyo, kampeni hiyo ilikuwa na matokeo ya kwamba kazi ya Yehova ilitangazwa zaidi kotekote nchini kuliko ilivyopata kufanywa. Kwa nguvu na kitia-moyo kilichofanywa upya, watangazaji wa Ufalme walisonga mbele kwa furaha kuu kupitia “ripoti mbaya na ripoti nzuri.”—2 Kor. 6:8, NW; Zab. 143:10.

Mapainia walibarikiwa tena wakati wa mwaka wa utumishi wa 1944. Mapainia wa pekee walikuwa na sababu nzuri ya kushangilia wakati walipoweza kupanga kitengenezo makundi mapya 17. Wale mapainia wengine walipata furaha kuu pia wakati makundi mapya 11 yalipoanzishwa kama tokeo la jitihada zao. Mwaka huo makundi mapya 144 yaliundwa! Hivyo, ile kampeni dhidi yetu ikawa na matokeo yasiyotakwa na maadui. Kinachofuata ni kielelezo chenye kutoa mfano:

Baraza la Kanisa la Serikali katika parishi ya mashambani waliamua watoe madai ya kwamba dada wawili mapainia (1) waache kutembelea watu wakiwa na fasihi yao, (2) wamwamini Bwana Yesu, na (3) wapange makao nje ya parishi hiyo bila kukawia.

Yule mpangishaji nyumba ambaye akina dada hao walikuwa wamekodi makao kwake alishurutishwa pia na padri mwenyeji awaondoshe kutoka nyumba yake mara moja. Barua iliyomjulisha mpangishaji nyumba juu ya uamuzi huo wa kuwaondosha dada hao ilimalizia kwa maneno haya: ‘Kwa salamu za kutoka moyoni kwako na kwa wao (dada hao wawili).’ Mwenyeji wa nyumba na ndugu yake, wote wawili wakiwa waenda kanisani wa kawaida, wakachukizwa sana na mashtaka hayo bandia hivi kwamba waliacha kwenda kanisani wakaanza kuhudhuria mafunzo yaliyoongozwa na dada hao.

Si Mapadri Wote Walipinga

Dada mmoja painia alimwalika ndugu kutoka kundi la karibu aje kutoa hotuba ya watu wote katika eneo lake. Kwa mshangao wa kila mtu, padri mwenyeji alikuja, akasikiliza kwa makini, na kuandika mambo fulani. Baadaye aliuliza maswali mengi naye akakubali kwamba kanisa lilikosea katika mengi ya mafundisho yalo. Alilalamika kwamba watu hawangekuja kanisani hata kama angewahubiria kweli.

Ndugu huyo akasema kwamba padri huyo na wafanyakazi wenzake wapaswa kufanya kama vile Kristo na wafuasi wake walivyofanya, yaani, kwenda nyumba kwa nyumba. Padri huyo akajibu: “Ndiyo, twapaswa kufanya hivyo, lakini sisi ni waoga na wazembe mno kwa jambo kama hilo, na pamoja na hayo sisi tuna mengi sana ya kufanya kuhusu mambo ya kilimwengu.” Alipokuwa akiondoka, padri huyo alitoa salamu ya mkono kwa njia ya kirafiki na kumshukuru mnenaji kwa hotuba.

Haya Zashindwa

Kwa asili Waswedeni kidogo ni wanyamavu, na wengi si wenye kusema sana, wakihangaika kuwa watafanya makosa. Kwa hiyo, ni jambo lenye kutokeza kwamba Waswedeni wengi sana kadiri hiyo wameweza kushinda tabia hizo nao wanaenda nyumba kwa nyumba kwa ujasiri ili kutimiza amri ya Yesu kwenye Mathayo 28:19, 20 “enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, . . . ; na kuwafundisha.”

Yesu alisema pia kwenye Luka 18:27: “Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.” Kama vile Yehova alivyomsaidia Musa, alipolalamika juu ya kuwa si mnenaji mwenye ufasaha, kwa kumpa Haruni awe msaidizi wake, ndivyo Yeye amesaidia wahubiri katika Swedeni kwa kuwaandalia “Akina Haruni” mbalimbali, au vifaa vyenye kunena, kupitia tengenezo Lake, kama vile vielelezo vifuatavyo vitakavyoonyesha:

“Haruni 1”—Kadi ya Ushuhuda

“Haruni” mmoja kati ya hao ilikuwa ile kadi ya ushuhuda, iliyotolewa katika 1934 na ambayo ilitumiwa vizuri katika miaka ya 1940. Ilikuwa na mahubiri mafupi yaliyochapwa na toleo la vitabu. Bulletin ilieleza hivi: “Mtembeleapo makao, kadi hii yapasa kupewa yule mtu anayefungua mlango. Mwacheni aisome. Halafu, mpeni broshua—na mnalohitajiwa kusema tu ni kwamba hiyo ndiyo broshua iliyotajwa katika kadi.” Katika kuitumia ilifanyaje kazi?

Painia mmoja akumbuka: “Mimi nilifanya tu kama tulivyoambiwa. Na kwa kawaida ilifanya kazi vizuri sana. Ingawa hivyo, nyakati fulani kutoelewana kulitokea. Mtu alichukua tu kadi yangu na kuingia ndani na kufunga mlango, au alifikiri nilikuwa siwezi kusema na kwa huruma akachukua vitabu kadhaa. Wengine walinitolea sadaka ili wawe wenye kusaidia. Kulikuwa na matukio yaliyowapa wenye nyumba pamoja nami kicheko kingi.”

Kadi hizo zilisaidia si kuanzisha mazungumzo tu na wenye nyumba bali pia katika kueneza maeneo makubwa kwa wakati mfupi. Kwa furaha, si Waswedeni wote ambao si wasemaji sana. Baadhi ya wahubiri waliambia Sosaiti kwa ucheshi kwamba waliamini Bwana alikuwa amefanya mpango huo ili kuwasaidia ‘washinde tabia ya kupoteza wakati kwa kusema mengi mno.’

“Haruni 2”—Kinanda

“Haruni” mwingine alikuwa kile kinanda chenye kubebeka, pamoja na rekodi za mahubiri ya Biblia ya dakika tano. Kifaa hiki kipya kilitumiwa vizuri kwa miaka kadhaa.

Katika 1937 Ndugu Eneroth alirekodi hotuba za Jaji Rutherford katika Kiswedeni. Rekodi hizo zilipopatikana, wahubiri walikuwa na bidii nao waliingia katika maeneo kama kundi la nzige. Wakati wa miezi kumi ya kwanza, wasikilizaji 153,786 walipigiwa mahubiri 107,077. Ndugu Eneroth mwenyewe alikuwa miongoni mwa wale wa kwanza kutumia rekodi hizo. Alicheka-cheka alipokuwa akikumbuka hivi: “Baada ya kupiga mojayapo rekodi hizo kwa wenzi wawili wa ndoa katika Stockholm, mwanamke huyo alisema: ‘Sauti yako inasikika sana kama hiyo tuliyosikia. Lazima uwe uliisikiliza mara nyingi sana.’”

Mwanzoni, vinanda hivyo vyenye kubebeka kidogo vilikuwa vikubwa na vizito. Hata hivyo, upesi, aina ndogo yenye kukunjika ambayo ingeweza kuchukuliwa katika mkoba ikapatikana. Kilikuwa kimeundwa kwa ufundi sana hivi kwamba rekodi ilikuwa kubwa sana kuliko kinanda. Mhubiri alipomwuliza mwenye nyumba kama aweza kupiga hotuba ya Biblia iliyorekodiwa, mara nyingi mwenye nyumba alijibu: “Mimi sina kinanda.” Kwa haraka, mhubiri alinyanyua kinanda chake. Udadisi ulikuwa ukimshinda mwenye nyumba, naye mhubiri alikuwa akialikwa ndani. Baadhi ya watu hata waliuliza kama kinanda hicho kilikuwa cha kuuzwa. Hivyo wengi ambao kama sivyo hawangetega sikio wakasikiliza ushuhuda huo.

Mara nyingi kinanda kiliwasaidia akina ndugu wajisikie kuwa wajasiri zaidi katika utumishi. Ndugu mmoja husimulia: “Nilikuja katika shamba moja ambako kulikuwa na karamu kubwa ya kusherehekea ubatizo wa mtoto. Nilimwuliza mwenye nyumba kama naweza kupiga mahubiri ya Biblia yaliyorekodiwa. Kwa kuwa mwenyeji alifikiri ingeongeza hali ya kidini katika karamu hiyo, hasa kwa kuwa padri alikuwapo, wageni wote walikusanywa pamoja. Walisikiliza kwa makini, kutia na padri, ambaye, ingawa hivyo, alitimua mbio baadaye, na kushangaza wengi. Nilijibu maswali mengi. Wageni kadhaa walichukua fasihi pia.”

“Haruni 3”—Kifaa cha Kupaaza Sauti

Tawi liliunda vifaa vya pekee vyenye vipaaza sauti kwa kuunganisha kinanda na mfumo wa vipaaza sauti ambao ungeweza kuwekwa katika gari lenye kukokotwa kwa baiskeli. Hivyo mahubiri yaliyorekodiwa yangeweza kusikiwa kotekote katika mtaa mkubwa wenye nyumba. Utangulizi wa muziki ulipigwa ili kutokeza kupendezwa mwanzoni na ili watu wapate kufungua milango na madirisha yao na kusikiliza. Baada ya hotuba, akina ndugu walikuwa wakitembelea makao hayo wakijibu maswali mengi na kutoa fasihi.

Ndugu mmoja mwenye bidii alitaka majirani wake wasikilize mahubiri walipokuwa wakichimba viazi katika shamba. Aliweka kipaaza sauti juu sana katika msunobari na kuwasha kinanda. Sauti yenye nguvu, yenye kutamka maneno kwa ufasaha ilipojaa hewani, watu waliacha kufanya kazi na kusikiliza huku vinywa vyao na macho yao yakiwa yanatazama angani, wakifikiri ujumbe unatoka mbinguni!

Kufikia sehemu ya pili ya miaka ya 1940, matumizi ya kinanda yalikomeshwa. Kuanzia 1938 kufika 1943, vinanda vipatavyo 1,200 vilikuwa vikitumiwa na watu milioni moja na nusu walikuwa wamesikiliza mahubiri yaliyorekodiwa. Wakati wa pindi hiyo, hesabu ya wahubiri iliongezeka kutoka 1,427 kufikia 2,571.

Ni kwa nini matumizi ya kinanda yalikomeshwa? Njia yenye matokeo zaidi ya kuenezea habari njema ilitokea—kuhubiri na kufundisha kwa wahudumu wenyewe. Hiyo iliwezekanaje miongoni mwa Waswedeni ambao si wasemaji sana?

“Haruni 4”—Shule ya Huduma ya Kitheokrasi

Ni nini kilichopata kuwa kisababishi kikubwa zaidi cha kusogeza mbele kazi ya Ufalme katika Swedeni? Ni ile Shule ya Huduma ya Kitheokrasi ambayo kupitia kwayo Mashahidi walipokea mazoezi bora sana.

Katika 1944, mwaka mmoja baada ya shule hiyo kuanzishwa katika United States, ilianzishwa katika makundi yote katika Swedeni. Mwanzoni, akina ndugu peke yao ndio walioandikishwa. Ndugu mmoja aliwekwa rasmi na Sosaiti awe mfunzi. Umaana wa kuhudhuria kwa kawaida ilikaziwa kwa kuanza kila mkutano kwa kuita majina ya walioandikishwa, njia ambayo baadaye iliachwa.

Shule hiyo ilimaanisha kazi ngumu na kujichunguza nafsi sana kwa wanafunzi wengi. Ndugu mmoja akumbuka hivi: “Hata kabla ya mkutano, wale ndugu waliokuwa wameratibiwa kuwa na hotuba za wanafunzi usiku huo walitambuliwa kwa urahisi. Kwa kawaida walionekana wakiwa na nyuso zenye huzuni nao walitembea huku na huku kama kwamba wameduwaa.” Katika kundi moja mfunzi aliuliza wasikilizaji: “Ni jambo gani unalofanya kwanza unapopata mgawo wa kutoa hotuba?” Ndugu mmoja akajibu: “Mimi naanza kushikwa na hofu.”

Mwangalizi mmoja wa wilaya aliripoti hivi: “Wanafunzi wengi hujizoeza hotuba zao mara nyingi sana katika mahali fulani pa upweke nyumbani. Ndugu mmoja, ambaye akili yake ilizimika akiwa katikati ya hotuba yake, aliacha kusema, akakazia macho wasikilizaji wake kwa kitambo, akasema: ‘Nasikitika hii haikwenda vizuri sana.’ Akirudiwa na utulivu, akapaaza sauti, ‘Lakini laiti mngenisikiliza katika chumba cha kuni!’”

Mwangalizi mmoja wa mzunguko akumbuka hivi: “Baadhi ya akina ndugu walilazimika kupiga vita vikali ili kushinda wasiwasi wao. Ndugu mmoja alikuwa amepangiwa atoe hotuba yake ya kwanza ya mwanafunzi. Wakati wa mkutano, alipokuwa akingojea zamu yake kwa wasiwasi, alilazimika kwenda nje mara kadhaa. Hatimaye wakati alipokuwa jukwaani, utangulizi wake wenye kushangaza ulikuwa: “Nimetoka nje mara tatu kutapika.”

Ndugu mwingine hukumbuka hivi: “Mmoja wa wanafunzi wa kwanza katika kundi letu, mrefu mwenye sura nzuri, alikuwa ametayarisha hotuba yake vizuri sana hivi kwamba alikuwa ameikariri moyoni. Alijaa hakika. Lakini wakati wenyewe ulipofika, akajawa na wasiwasi, naye akashindwa kusema. Baada ya muda ulioonekana kama umilele, ghafula akasalimu wasikilizaji kwa Hamjambo! Neno hilo likafungua ulimi wake. Akapata tena uwezo wake wa kunena naye hatimaye akatoa hotuba nzuri sana ya mwanafunzi.”

Matokeo Bora Sana

Shule ya Huduma ya Kitheokrasi ilitokeza si wanenaji bora wa hotuba za watu wote tu bali pia walimu bora wenye uwezo wa kunena na watu milangoni na nyumbani. Akina dada walipoalikwa washiriki mazoezi hayo, wao pia walipiga hatua kubwa wakiwa watangazaji wa Ufalme.

Asante kwa shule hiyo, walio wachanga katika Swedeni wamefanya maendeleo mazuri pia. Imewachochea wavulana na wasichana wengi wawe watendaji kikamili katika kazi ya Ufalme. Mvulana mmoja wa umri wa miaka saba alimuuliza mwangalizi wa shule kama angeweza kujiandikisha. Mwangalizi akauliza, “Kwa nini?” Kijana huyo akajibu kwa haraka, “Ingawaje mtu hawezi kuwa mzembe katika maisha yake yote!”

Kupiga Miguu Barabarani

Akina ndugu Waswedeni wametumikia Yehova kwa bidii katika njia nyingine zozote ambazo tengenezo lake lilidokeza. Kwa mfano, wakati wa miaka ya 1940 na miaka ya mapema ya 1950, walipopata kujua kwamba akina ndugu katika United States na Uingereza walikuwa wakitumia vibao vilivyoangikwa mabegani nyuma na mbele na karatasi kubwa-kubwa, wakipiga miguu barabarani ili kutangaza hotuba ya watu wote katika mkusanyiko, mipango hiyo ilifanywa kwa juhudi katika Swedeni pia.

Jack Pramberg, ambaye alitumikia akiwa mwangalizi wa wilaya wakati huo na ambaye alifanya mipango mingi kama hiyo ya kupiga miguu, hukumbuka hivi: “Wakati wa majira ya baridi inakuwa giza mapema sana alasiri katika kaskazini mwa Swedeni, hivyo tulitumia mianga kuongezea mafanikio ya matangazo yetu. Katika mojayapo pindi hizo, kichwa cha hotuba kilikuwa ‘Nuru Pekee.’ Mwandamano huo wenye mianga ulipokuwa ukizunguka katika mji, taa za umeme zilizimika ghafula. Mji wote ukawa giza tititi. Hata hivyo, mianga yetu ilikuwa ikiwaka ikiangaza nuru kwenye karatasi zetu ambazo watu waliweza kusoma: ‘Nuru Pekee.’”

Sven-Eric Larsson, mwangalizi asafiriye, hukumbuka hivi: “Nyakati fulani akina ndugu walibeba ishara kubwa zikiwa juu ya fito ndefu katika barabara za mjini, zikitangaza hotuba ya watu wote kwenye mikusanyiko. Katika 1948, kwa ajili ya udadisi tu, wavulana wawili walihudhuria mkusanyiko katika Örebro. Walikuwa hawajaamua bado kuwa Mashahidi wa Yehova. Baada ya kipindi kimoja, bila kujua walikuwa akina nani, niliwapa tu karatasi moja kubwa na kuwaambia watakakoelekea wakipiga miguu. Huku wakisita-sita, waliichukua na kupiga miguu huku na huku katikati ya mji. Mmoja wao, Lars Lindström, amekuwa mzee wa kundi kwa miaka mingi sasa; na yule mwingine, Rolf Svensson, anatumikia akiwa mwangalizi wa wilaya.”

Kutokuwamo kwa Kikristo Kwahatirishwa

Ijapokuwa Swedeni imejaribu kujikaza sana idumishe kutokuwamo kwa kisiasa, ulinzi wenye nguvu pamoja na utumishi wa kijeshi wa kulazimishwa umedumishwa. Kwa hiyo, ukamilifu wa akina ndugu juu ya kutokuwamo kwao kwa Kikristo umejaribiwa. Kabla ya Vita ya Ulimwengu ya 2, kwa kawaida akina ndugu walichukua utumishi wa kulazimishwa wa kiraia badala ya ule wa kijeshi, wakatumikia wakiwa wazimamoto au wakatakuni, wakichimba mahali pa akiolojia, na kufanya utumishi mwingine mbalimbali wa kiraia. Halafu, Vita ya Ulimngwengu ya 2 ilipokuwa ikiendelea, walitambua kwamba kwa kweli walikuwa wakihesabiwa kuwa askari wakitumikia mamlaka za kijeshi. Hivyo, wakakataa utumishi huo.

Vifungo katika jela vyenye kurudiwa-rudiwa vikafuata, vikianza kwa hukumu za mwezi mmoja walipokataa kwa mara ya kwanza. Upesi baada ya kuachiliwa, walikuwa wakiitwa tena kwa ajili ya utumishi wa kijeshi na kupelekwa tena katika jela kwa kipindi kingine, sasa cha miezi miwili. Walipotoka tena, walilazimika kukabili utaratibu uo huo mara nne, tano, sita, au zaidi, na kila wakati kwa kawaida mwezi mwingine uliongezwa kwenye urefu wa hukumu iliyotangulia. Kwa muda wa miaka mingi, mamia ya akina ndugu walitiwa gerezani kwa jumla ya miaka karibu elfu moja. Werner Johansson, wakati huo akiwa painia, alihukumiwa kwa miezi 12—ikiendelea kwa kipindi cha miaka 13. Alisema:

“Kuandikishwa kinguvu jeshini wakati baada ya wakati na kupitia utaratibu mmoja wa mahakama baada ya mwingine na kuhama-hama kuingia na kutoka magereza tofauti-tofauti jinsi hiyo lilikuwa jambo lenye kujaribu sana. Nilikuwa na familia ya kutunza. Lakini upendo na kitia-moyo tulivyopokea kutoka kwa akina ndugu na dada vilikuwa msaada mzuri ajabu. Ingawaje, ulikuwa wakati wenye kusisimua, na fursa nyingi zilifunguka za kutolea ushuhuda wote waliohusika.”

Nyakati fulani akina ndugu walitukanwa na kukemewa na mawakili wa mashtaka wa serikali na mahakimu. Painia mmoja, Erik V. Johansson, akumbuka jaribu lake la kwanza la mahakamani: “Wakili wa mashtaka na hakimu walisema kwamba wangenifanyia matata nisipofanya wajibu wangu. Niliwaambia kwamba nilikuwa tayari kupatwa na yaliyompata Danieli alipotupwa katika tundu la simba. Kisha wakili wa mashtaka akasema: ‘Ingependeza kumtupa Johansson katika tundu la simba na kuona imani yake ina thamani gani.’ Kesho yake, nilipokutana na hakimu, alinikamata na kusema: ‘Wewe ni mtu mbaya kabisa, wapaswa kupigwa risasi, na pia labda utapigwa risasi.’” Basi, hilo halijatukia bado. Ndugu Johansson, sasa akiwa na umri wa miaka zaidi ya 80, angali hai na anasitawi akiwa katika utumishi wa wakati wote.

Wenye Mamlaka Wajaribu Tendo la Kuwakatisha Tamaa

Ilizidi kuwa wazi kwa wenye mamlaka kwamba hukumu za kutupwa gerezani hazingeweza kuvunja ukamilifu wa vijana hao. “Mahakimu na mawakili wa mashtaka wamekuwa wakishiriki mchezo ambao katika huo wamejiona wenyewe kuwa wapinzani hoi,” akaeleza aliyekuwa hapo awali mshiriki wa bunge la Swedeni kuhusu walivyotendewa Mashahidi.

Kuelekea mwisho wa vita, kwa kujichunguza nafsi, wenye mamlaka walifanya jitihada ya kubadili hali hiyo. Ghafula, waliagiza wale Mashahidi wa Yehova 126 waliokataa kufanya kazi ya kulazimishwa wafanyiwe uchunguzi wa akili. Kama wangalitangazwa kwamba walipungukiwa na akili, mahakama ingaliwatendea kwa njia tofauti. Ripoti ya tawi inasema hivi kuhusu jambo hilo:

“Uchunguzi huo mbalimbali ulifanyiwa miji mitatu tofauti, na kila mmoja wa hao waliochunguzwa aliulizwa maswali na padri na madaktari wawili kwa muda wa siku tano hadi sita. Akina ndugu waliotendewa hivyo walikubali kwamba lilikuwa jambo waliloona lenye kutia moyo sana, likiwapa fursa nzuri sana za kutoa ushuhuda. Mapadri waliotumikia kwenye uchunguzi huo mbalimbali walivurugika akili na kupatwa na wasiwasi sana hivi kwamba hata madaktari waliwacheka, na madaktari wenyewe walikubali kwamba, kwa kawaida, Mashahidi wa Yehova ni watu wenye akili zilizoelimishwa sana na wenye masadikisho yenye nguvu na wenye kufuata viwango vya juu vya adili.”

Tatizo Lenye Kukua

Chunguzi hizo za akili kwa Mashahidi ziliachwa upesi kwa kuwa hazikuleta matokeo. Hata hivyo, mahakimu, mawakili wa mashtaka, walinzi wa magereza, walinzi wa wafungwa, na hata mapadri wengi wa magereza walizidi kufadhaika. Wakili mmoja wa mashtaka alinukuliwa kuwa alisema hivi kwa bunge:

“Nijapokuwa wakili wa mashtaka, mimi siamini katika matisho ya adhabu katika kesi hii. . . . Sisi katika mwaka huu wa 1958, je, ni lazima tujilemeze kwa masalio kama hayo ya hukumu za kiuchawi, kama hivi zilivyo kikweli, zinazohusu watu ambao kwa vyovyote vile ni watu wasio na lawama? Inaogopesha kwamba wanalazimika kuwekwa pamoja na wateja wahalifu katika magereza yetu. Lazima nikubali kwamba wakati pekee ninapoaibikia kazi yangu ya maisha nikiwa wakili wa mashtaka ni wakati ninapolazimika kudai kwamba watu hao waadhibiwe kwa hukumu ya kufungwa gerezani.”

Gereza la Wafungwa

Kadiri vijana wengi walivyokubali kweli, ndivyo wengi walivyozidi kutiwa gerezani. Magereza yalisongamana wahalifu, na gharama za kutunza magereza zilipanda sana pia. Kwa kuwa ndugu zetu walilazimika kupenyezwa ndani hapa na pale watumikie vifungo vyao gerezani, Wasimamizi wa Kurekebisha Tabia walichukua hatua isiyo ya kawaida kwa kujaribu kuwaruhusu Mashahidi wa Yehova waendeshe gereza lao wenyewe.

Ujenzi ulifanywa na wafungwa wote, yaani, Mashahidi wa Yehova. Waliachwa peke yao kwa saa 12 kila siku bila walinzi wa gereza. Ofisa mmoja alikuwa akija mara kwa mara akiwa na chakula na vifaa vya kazi. Pindi kwa pindi, ofisa mmoja alikuwa akiweka rasmi ndugu wawili kuwa walinzi, hivyo wakawa na wafungwa wakilinda wafungwa. Wangeweza kuongoza mikutano yote na kupokea wageni siku kutwa kila Jumapili. Walitoa ushuhuda kwa barua. Hilo “gereza la wafungwa” liliripotiwa katika vyombo vyote vya habari kuwa jaribio la kipumbavu. Hata hivyo, akina ndugu waliliendesha kikamilifu. Hakukuwa watoro wala hakukutukia majaribio ya kutoroka.

Rekebisho Laanza Kuonekana

Pole kwa pole, washiriki wa bunge na maofisa wengine wa serikali waliona uhitaji wa kubadili mwongozo ule. Kadiri maofisa walivyoendewa na akina ndugu na watu wengine wenye kusikitikia wakiomba rekebisho, fikira zilielekezwa kwenye hali ile.

Ndugu mmoja ambaye alimfanyia kazi ya kupaka nyumba rangi mshiriki mmoja wa serikali alimjulisha jambo lile. Baadaye, mtu huyo alimwomba ndugu yule amsaidie kuhesabu gharama za Serikali za kuwaweka Mashahidi gerezani. Kwa kushangazwa na matokeo, aliahidi kwamba ataonyesha washiriki wenzake tarakimu hizo. Pia, mshona nguo katika Stockholm alikuwa na wateja waliokuwa washiriki wa bunge, naye aliwakumbusha mara nyingi juu ya hali ile, akiwahimiza wafanye jambo fulani kusahihisha tatizo hilo.

Katika Januari 1964 waziri wa ulinzi aliunda halmashauri ipendekeze sheria iliyosahihishwa. Wakilishi wawili wa ofisi ya tawi ya Sosaiti waliitwa waende mbele ya halmashauri hiyo wadokeze jambo jingine badala ya utumishi wa kulazimishwa. Hata hivyo, badala ya kufuata dokezo la kutuondolea utumishi wa aina yoyote, halmashauri ile ilipendekeza yafuatayo, kulingana na ripoti yao rasmi: “Kwa hiyo, halmashauri yaona kwamba yapasa kufikiria kwa uzito . . . kuwatangaza kwa muda Mashahidi wa Yehova kuwa wasiofaa, kulingana na kanuni ile ile ya mwongozo inayotumiwa kwa wazoelevu fulani wa kileo au watu mmoja mmoja wasioweza kushirikiana na jamii.”

Makasisi Wageuka na Kutuunga Mkono

Kutulinganisha na “wazoelevu fulani wa kileo na watu mmoja mmoja wasioweza kushirikiana na jamii” kuliwachukiza watu, kwa kuwa Mashahidi wa Yehova walijulikana kuwa raia wema na wenye kufuata sheria. Hata wenye mamlaka wa kanisa waliteta. Gazeti moja la habari lilinukuu washiriki wa baraza la makasisi la Härnösand kuwa lilisema:

“Kwa kufaa, halmashauri ile huliona kuwa suluhisho lisilotosheleza kusuluhisha hukumu ya kuwa na hatia ya [Mashahidi] kwa adhabu ya kifungo gerezani. Lakini kwa sababu tendo la sehemu hii ya tatizo humalizika kwa pendekezo la kuwaweka vijana wa Mashahidi wa Yehova katika kikundi kile kile kimoja cha watu wasioweza kushirikiana na jamii na wazoelevu wa kileo, halmashauri hiyo inashindwa kufuata mambo ya hakika ya jambo hilo na katika kuonyesha heshima ya kibinadamu.” Kuwekwa pamoja na kikundi hicho kulitukumbusha juu ya Yesu, ambaye kwa makosa aliwekwa miongoni mwa watu wa namna iyo hiyo.—Mt. 11:19.

Uamuzi wa Mwisho

Katika Mei 25, 1966, bunge liliamua kwamba uchunguzi wa kila kesi moja moja wapasa kufanywa wa kila aliyekataa utumishi kwa ajili ya dhamiri ambaye ni Shahidi. Kutokana na uchunguzi huo, serikali ingeamua isimwite kwa wakati uliopo kwa utumishi wa kijeshi. Ushindi huo baada ya miaka mingi ya kustahimili ulipokewa kwa shangwe kuu. Akina ndugu sasa wangeweza kusonga mbele katika kuhubiri habari njema bila kizuizi.

Telegramu moja ilipelekwa kwa makao makuu ya Sosaiti katika Brooklyn, U.S.A. Wenzi wa ndoa Waswedeni, waliokuwa wakihudhuria mkusanyiko mkubwa katika Baltimore wakati ule, walisisimuka kusikia Ndugu F. W. Franz, wakati huo akiwa makamu wa msimamizi wa Sosaiti, akisomea wasikilizaji telegramu hiyo. “Alipongeza wenye mamlaka wa Swedeni na akaiita Swedeni nchi iliyo kiolezo,” wao wakakumbuka.

Kiolezo cha Swedeni

Utaratibu uliofafanuliwa na serikali ya Swedeni umepata kuitwa kiolezo cha Swedeni na wenye mamlaka katika nchi nyinginezo, ambao wautumia ukiwa rejezo wakati walipojaribu kupata masuluhisho yanayofanana. Utaratibu huo ni nini hasa?

Kila mmoja anayeitwa lazima apate hati kutoka kwa wazee katika kundi lake ikishuhudia kwamba yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliyebatizwa na ni mhubiri wa kawaida anayeshirikiana na kundi lile. Ofisi ya tawi ya Sosaiti huthibitisha kwamba sahihi hizo ni za wale wazee waliowekwa rasmi. Mwenye kuitwa hutoa hati hiyo pamoja na ombi lililoandikwa la kuondolewa miongoni mwa wale wanaoitwa kwa ajili ya utumishi wa lazima wa kijeshi na baraza lake la kuandikisha jeshini kinguvu, ambalo humpa ruhusa ya kuondolewa katika utumishi wa kijeshi kwa wakati wa sasa. Utaratibu unaofanana na huo umepata kutumiwa kwa ajili ya akina dada kadhaa walioitwa kwenye kazi ya ulinzi wa kiraia.

Jaribio Jipya la Kutafuta Kuridhiana

Baada ya uamuzi huo kufanywa na bunge, majaribio yamepata kufanywa ya kutushurutisha tufanye kazi ya kulazimishwa badala ya utumishi wa kijeshi. Katika miaka ya mapema ya 1970, halmashauri ya serikali iliwekwa rasmi ipitie njia ya kushughulikia wakataaji wa kudhamiria. Kwa ajili ya usawa, wenye mamlaka walitaka Mashahidi wa Yehova watumikie kwa masharti kama yale ya vikundi vingine vya kidini na kufanya kazi ya kulazimishwa ikiwa badala ya ule wa kijeshi.

Wakilishi wa ofisi ya tawi walienda kuonana na halmashauri ile, wakieleza kwamba Mashahidi hawawezi kukubali kazi yoyote ile iliyo badala ya utumishi wa kijeshi, hata kazi hiyo iwe yenye kusifika kadiri gani. Walionyesha kwamba Mashahidi wa Yehova tayari wanafanya kazi ya kijamii katika huduma yao ya nyumba kwa nyumba, wakisaidia watu wasafishe maisha zao na kuwa raia wema, wenye kufuata sheria. Ndipo mmoja wa halmashauri alipotokeza wazo la kushangaza sana.

Alitaka kujua kama tungekubali kushiriki huduma hiyo ya nyumba kwa nyumba kwa wakati wote katika makundi yetu wenyewe kwa muda—unaolingana na ule wa utumishi wa kulazimishwa—na kuuripoti kwa wenye mamlaka ukiwa badala ya ule wa kijeshi. Akina ndugu walieleza kwamba utumishi wetu kwa Mungu hauwezi kamwe kuwa wa kulazimishwa au kuwa jambo la Serikali. Hatimaye, halmashauri ile ilidokeza ibaki na ule uamuzi wa 1966, wakikata maneno hivi katika ripoti yao ya mwisho: “Kulingana na maoni ya halmashauri, kwa wakati wa sasa, hakuna vikundi vingine vya kidini katika nchi yetu vinavyoweza kulinganishwa na Mashahidi wa Yehova.”

Waacha Kanisa kwa Maelfu

Mashahidi katika Swedeni si kwamba tu wamehifadhi salama kutokuwamo kwao katika mambo ya kisiasa bali pia wametii kwa ushikamanifu ile amri iliyo kwenye Ufunuo 18:4 ya kutoka katika Babuloni Mkuu, ile milki ya ulimwengu ya dini bandia. Kuhusiana na jambo hilo, Januari 1, 1952, ilikuwa tarehe yenye kukumbukwa. Sheria mpya ikiongoza uhuru wa kidini ilianza kutenda; iliwapa raia wote wa Swedeni haki ya kuacha Kanisa la Serikali bila kuwa na lazima ya kujiunga na tengenezo jingine la kidini lenye kutambuliwa na serikali.

Utaratibu ulikuwa kujaza tu fomu moja au kuandika juu ya karatasi tamaa ya kujiondoa kutoka ushirika wa kanisa, uwe na mtu mwingine wa kutia sahihi akiwa shahidi wako, na kuiacha hati hiyo katika ofisi ya padri wa parishi, ambapo kujiondoa huko kungeandikishwa bila kupingwa, kuulizwa maswali, au kuzugumzwa.

Waswedeni kwa ujumla hawakujifaidi na fursa hiyo, sana-sana kwa sababu ya kutojali. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova walipeleka fomu zao kanisani upesi ilivyowezekana. Mashahidi wote 5,000 katika wakati ule walijiondoa kwa umoja kama mtu mmoja. Makasisi wengi walistaajabu sana nao hawakuweza kujizuia wasiulize maswali. Miezi michache baadaye, tawi liliripoti:

“Ziara zao kwenye ofisi ya padri wa parishi katika jambo hili iliwapa mashahidi hao pindi nyingi nzuri za kutoa ushuhuda juu ya Ufalme. Katika visa kadhaa mapadri walipata fasihi na hata wakahudhuria mafunzo kama tokeo la mahoji hayo ili wapate kujua zaidi juu ya imani zetu. Trakti ya Biblia iliyotokea wakati uo huo ilifaa sana kuhusiana na jambo hilo. Padri mmoja alipendezwa sana hivi kwamba yule dada mwenye umri mkubwa, ambaye ndiye pekee mshiriki wa kampuni [kundi] katika kijiji hicho, amekuwa akiongoza funzo kila juma pamoja naye katika kitabu ‘Let God Be True’ tangu wakati huo; naye alimwambia ndugu painia mwenye kutembelea kwamba alikuwa na furaha kuu kwamba dada huyo anamtembelea kwa ukawaida na kuendelea kujifunza naye.”

Redio Si kwa Ajili ya Mashahidi wa Yehova

Redio katika Swedeni imekuwa ikitumiwa na Serikali pekee tangu utangazaji wa redio uanze. Matumizi hayo ya pekee, humaanisha kwamba baraza fulani, lenye kuwakilisha Serikali, lina mamlaka kamili juu ya utangazaji wa redio (na sasa wa TV pia). Kwa kuwa Swedeni ni nchi yenye kutawalwa kidemokrasia ambako ubaguzi wa kidini unaonwa kuwa kinyume cha sheria, tumefanya jitihada za kupata wakati wa kutoa matangazo ya redio.

Katika 1953 pasta mmoja alitoa hotuba ya redio ya dakika 30 ili “kufunua wazi” Mashahidi wa Yehova, bila kutoa nafasi tutoe maelezo. Baadaye ndugu wawili walitumwa kwa msimamizi wa idara ya programu za kidini, padri mmoja wa Kanisa la Serikali, wakaombe ruhusa ya kutangaza programu ya kutoa jibu. Mmoja wa ndugu hao akumbuka hivi:

“Yeye alitwambia waziwazi: ‘Mashahidi wa Yehova hawataruhusiwa kamwe kutoa matangazo katika Redio ya Swedeni. Sisi hatuwaoni nyinyi kuwa Wakristo.’ ‘Kwa nini?’ tukauliza. ‘Nyinyi hamwamini Utatu. Ndiyo sababu! Na, nimesikia kwamba nyinyi mnanukuu Biblia kwa ubandia katika fasihi vyenu.’ ‘Kuna kielelezo chochote?’ tukauliza. ‘Nina kimojawapo vitabu vyenu katika rafu yangu ya vitabu. Acheni niwaonyeshe.’ Akachomoa chapa ya Kiingereza ya ‘Make Sure of All Things’ (kitabu kinachojaa manukuu ya Biblia) pamoja na Biblia ya Kiingereza. Akaanza kuvilinganisha neno kwa neno, akaendelea kwa dakika kadhaa. Kwa kutopata tofauti yoyote, aliamka na kusema: ‘Hata hivyo, ni Wakristo tu wanaoruhusiwa kutoa matangazo ya redio,’ akatutoa nje.”

Jaribio la ‘Kutufunua Wazi’ Laleta Matokeo Yasiyotakwa

Katika Oktoba 1976 ofisa wa Redio ya Swedeni alitualika tushiriki sehemu katika mfululizo wa programu tatu ambazo, alisema, zingewaarifu watu juu yetu. Tulikubali baada ya kuahidiwa kwamba tungetendewa bila ubaguzi. Programu hizo zilitegemea sehemu zilizorekodiwa za mikutano yetu na mahoji.

Wakati wa kurekodi, ilipata kuwa wazi kwa akina ndugu kwamba programu hizo zilikusudiwa ziwe shambulio juu ya Mashahidi. Ndugu waliohojiwa walishambuliwa kwa maswali yenye kuumiza na kuchokoza. Hata hivyo, walijibu kwa utulivu na kwa kueleza mambo kama yalivyo kikweli. Kisha tepe hizo zilihaririwa na ofisa ili programu itoe wazo baya zaidi iwezekanavyo.

Baada ya utangazaji huo wa redio, ofisi ya tawi ilipokea barua na simu kutoka kwa wasikilizaji kutoka kotekote nchini, wakisema kwamba waliona tofauti kati ya Mashahidi na washambulizi wao na kwamba kweli iliweza kutambulikana. Tokeo likawa kwamba, katika Novemba 1976, mwezi mmoja baada ya utangazaji huo wa redio, tuliona kilele kipya cha wahubiri wa habari njema 16,693 katika Swedeni! Tuliona kweli katika Andiko hili: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa.”—Isa. 54:17.

Uhitaji wa Tawi Jipya

Wakati wa miaka ya 1940, hesabu ya wahubiri ilikuwa imeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka 1,726 katika 1940 kufika 3,702 katika 1949. Ripoti moja katika 1949 ilitangaza mataraja kwa ongezeko la wakati ujao: “Kutoka karibu kila kampuni, watumishi wa mzunguko wanaripoti kwamba kuna kupendezwa kwingi shambani kuliko vile wahubiri wenyeji wanavyoweza kukutunza.”

Pia walihitaji kuchapa magazeti wao wenyewe. Kufikia 1950 muunganisho wa ugawanyaji wa yale magazeti mawili ulikuwa umefikia nakala 123,000 kila mwezi. Uchapaji ulikuwa ungali unafanywa na kampuni ya kilimwengu. Ofisi ya tawi ilikuwa tu na chumba kilichochimbwa chini ya jengo kwa ajili ya mashine ya chapa aina ya Diegel iliyotiwa karatasi kwa mikono na mashine ya kupigia chapa fasihi vidogo vidogo. Kwa hiyo kifaa chenye nafasi zaidi kilihitajiwa sana. Utafutaji wa mahali papya penye kufaa ukaanza.

Tendo Thabiti Lachukuliwa

Lennart Thunberg, mchoraji ramani za ujenzi, hukumbuka hivi: “Tulipata mahali mbalimbali penye kupendeza katikati ya Stockholm. Kwa kuongezea, jamii katika Jakobsberg, kilometa zapata 20 kaskazini-magharibi mwa jiji, ilitutolea viwanja viwili vinavyopakana ili tuvinunue. Hata hivyo, sisi hatungeweza kuhamia nje ya jiji baada ya miaka 25 ya kukaa katikati ya jiji.

“Tulizungumza jambo hilo pamoja na Ndugu Knorr, wakati huo akiwa msimamizi wa Sosaiti, wakati wa ziara yake katika Swedeni katika 1951. Ndugu Eneroth nami tulipendekeza mahali mbalimbali katikati ya jiji. Lakini Ndugu Knorr, akiwa anatarajia mambo mengine, alituuliza tupate mahali fulani nje ya Stockholm. Tulitaja kwa kuguna juu ya vile viwanja katika Jakobsberg. ‘Songeni mbele mkavinunue!’ akasema kwa uthabiti.

“Wakati ule ule mkusanyiko wa kitaifa ulipokuwa ukiendelea kwenye Eriksdalshallen katika Stockholm, Ndugu Knorr alitaka mkataba huo utiwe sahihi mara moja ili aweze kufanya tangazo. Nilitimua mbio kwenda Jakobsberg na, baada ya kuwatafuta kwa saa nyingi, nikawapata wenyeji wa vile viwanja viwili, nao wakatia sahihi mkataba ule, nikatimua mbio kurudi kwenye mkusanyiko, na kumwarifu Ndugu Knorr, ambaye kwa uhakika alitangazia wajumbe hao wenye shangwe na uchangamfu mradi huo.”

Upesi kazi ya ujenzi ikaanza kwa mwendo kamili. Ndugu Thunberg aendelea hivi: “Akina ndugu kotekote katika Swedeni walituunga mkono kwa kutupelekea magunia ya viazi, ndama waliochinjwa mara hiyo, matunda, beri, na riziki ya vyakula vingine. Kifedha mambo yalienda vizuri pia. Ile kampuni iliyonunua mahali pale pa zamani ililipa pesa taslimu. Ile benki ambayo Sosaiti ilikuwa imetumia kwa miaka mingi ilitupa mkopo bila dhamana kwa sababu ya sifa njema ya Sosaiti. Pia ndugu wengi walikopesha tawi pesa na wakachanga kwa ukarimu. Dada mmoja hata aliuza biashara yake ili atoe mchango.”

Machi 31, 1954, ilikuwa siku ya kihistoria, yale Makao ya Betheli mapya yalipofunguliwa katika Jakobsberg. Familia ya tawi ilihama kutoka eneo dogo lililosongamana la meta za mraba 900 ikaenda katika vifaa vipya kabisa vyenye kutandaa katika meta za mraba 3,600, vyenye nafasi ya kutosha kwa vifaa vya ki-siku-hizi vya uchapaji. Kuanzia na toleo la Mei 15 na Julai 8, 1954, walichapa chapa zao wenyewe za magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Ikawa kwamba mahali hapo pangetumikia faida za Ufalme katika Swedeni kwa miaka 26.

Eneo la Kigeni Lasitawi

Baada ya Vita ya Ulimwengu ya 2, eneo jipya lilisitawi. Wafanyakazi wageni na familia zao kutoka nchi mbalimbali, sana-sana kutoka Finlandi na kusini mwa Ulaya, walimiminika ndani na kufanya makao. Maelfu ya wakimbizi kutoka kotekote duniani walijiunga na jamii ya Kiswedeni pia. Hivyo, idadi mpya ya mamia ya maelfu ya watu wa kigeni, wakisema karibu lugha mia moja, walikuwa tayari kupokea habari njema.

Kwanza, wahubiri walishauriwa wajaribu kupata taifa la mwenye nyumba na kupata kichapo katika lugha yake ili wamwangushie. Wale walioonyesha kupendezwa wangeingizwa pole kwa pole katika makundi yenye kusema Kiswedeni. Njia hiyo ilipotumiwa haikufanikiwa. Kwa kuwa wageni wengi walisita-sita kuja katika makundi, si maendeleo mengi yaliyofanywa.

Katika 1970 badiliko likafanywa. Wakati wa ziara yake ya eneo la dunia, Ndugu Milton Henschel, kutoka makao makuu ya Brooklyn, alipendekeza kwamba ndugu hao wenye kusema lugha ya kigeni wapangwe kitengenezo kuwa vikundi na makundi katika lugha zao wenyewe. Alisema kwamba mtu atakuwa haraka zaidi kiroho na kupata ufahamu wenye kina zaidi cha kweli anapojifunza katika lugha anayojua vizuri zaidi.

Makundi ya Lugha za Kigeni

Katika Desemba ya mwaka uo huo, kundi la kwanza la lugha ya kigeni, Kundi la Kifinlandi la Göteborg, liliundwa. Upesi, jingine likafuata katika Stockholm. Mwangalizi wa mzunguko aliyesaidia katika kupanga kitengenezo kundi hilo aliripoti hivi:

“Shauku na shangwe miongoni mwa ndugu Wafinlandi inapanda juu. Kutoka pande zote, akina ndugu na dada wenye kusema Kifinlandi wamejitokeza na, kana kwamba kwa usiku mmoja, wakakua wakawa kundi kubwa, lenye bidii. Ni kama kwamba mvua yenye joto imeangukia shamba lenye ukavu.” Makundi zaidi ya wenye kusema Kifinlandi yalitokea upesi-upesi mpaka kufikia 1990 yalikuwa 33, pamoja na vikundi 12. Yalipangwa kitengenezo kuwa mizunguko mitatu, yenye wahubiri zaidi ya 1,700 na mapainia 119.

Upesi kazi ikaendelea katika vikundi vya lugha nyinginezo. Katika 1971 mwangalizi wa mzunguko alifanya mkutano wa “kujaribia kupendezwa” kwa ajili ya watu wenye kusema Kihispania katika Stockholm. Wakaja 56. Ni jambo gani limetukia tangu hapo? Lars-Erik Eriksson kwenye ofisi ya tawi, anayesaidia kupanga kitengenezo kazi katika maeneo ya kigeni, huripoti hivi: “Sasa tuna makundi saba ya wenye kusema Kihispania kuongezea vikundi saba. Zaidi ya makundi na vikundi vya wenye kusema Kifinlandi na Kihispania, tuna moja la Kiitalia, manne ya Kiyugoslavia, matatu ya Kigiriki, na matatu ya Kiingereza, kuongezea vikundi kadhaa vinavyofanya mikutano katika Kiyugoslavia, Kigiriki, Kiingereza, Kiarabu, na Kituruki. Mipango inafanywa pia ya kupanga kitengenezo kundi la nne la Kiingereza, vikundi vitatu vya Kipolandi, na kikundi kimoja cha Kifaransa. Hivyo, watu zaidi ya 2,700 wamepatikana katika maeneo hayo ya kigeni na kuletwa pamoja katika makundi 50 na vikundi 28.”

Njaa kwa Ajili ya kweli

Mambo yafuatayo yaliyoonwa yaonyesha jinsi kazi hii inayofanywa miongoni mwa wakazi wahamiaji ilivyokuwa baraka kwa wengi. Celo Pertot, wa asili ya Italia, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akifanya kazi miongoni mwa makundi ya lugha za kigeni asimulia hivi:

“Dada Mswedeni aliniomba nimsaidie afanye ziara katika baadhi ya familia za Waitalia. Nilisita-sita kwa sababu tayari nilikuwa nimekuwa huko, na hawakuonekana wakipendezwa hata kidogo. Niliandamana naye bila kutaka. Tulikuta mwanamke mmoja ambaye sikuwa nimepata kumwona. Yule dada alipokuwa akimjulisha sisi ni akina nani kwa Kiswedeni, yule mwanamke akaanza kufunga mlango. Kwa haraka sana nikasema katika Kiitalia: ‘Sisi huongea juu ya tumaini tunalopewa na Ufalme wa Mungu.’ Akaanza kusikiliza. Tulipomtembelea tena, alisema hivi: ‘Kabla tu ya ziara yenu ya kwanza, nilikuwa nimepanga kujiua. Nilikuwa nimesali kwa Mungu: “Ikiwa wewe uko, kwa nini nimepoteza imani katika wewe, na kwa nini naona maisha yakiwa bila maana jinsi hii?”’ Basi, kupitia funzo la nyumbani, alipata maana halisi ya maisha. Kwa miaka mingi sasa, ametumikia akiwa painia, akiwa mwenye bidii na kujawa na maisha.”

Kabla ya kuhamia Swedeni, mwanamke mmoja alikuwa amejifunza na Mashahidi wa Yehova kwa wakati fulani katika Chile naye aliambiwa awatafute Mashahidi mara tu afikapo Swedeni. Alijaribu lakini bila mafanikio. Siku moja alikuwa akigeuza-geuza tu karatasi katika kijitabu cha maandishi ya namba za simu cha rafiki yake akakipata kikiwa katika hali yenye kuvurugika sana hata akaanza kukiweka katika hali nzuri. Ebu wazia alipata kuona nini! Jina la mwanamke mmoja likiwa limeandikwa mara mbili katika ukurasa mmoja, likifuatwa na maandishi haya, “estudio de la Biblia” (funzo la Biblia). “Huyo lazima awe Shahidi,” akawazia, na kwa kusisimuka akapiga simu akitumia namba hiyo. Alikuwa Shahidi! Jioni iyo hiyo alihudhuria funzo la kitabu la kikundi katika Kihispania. Sasa yeye ni mhubiri aliyebatizwa, mwenye furaha.

Mmoja wa waangalizi wasafirio alikutana na mwanamke Mhispania mlangoni. Kwa kuwa ndugu huyo aliweza kusema Kihispania, alialika mwanamke huyo kwenye hotuba na kuanza kumtolea ushuhuda. Mwanamke huyo alinaswa sana na mazungumzo hayo hivi kwamba alisahau simu, ambayo alikuwa ameiondoa juu ya kiangiko chayo akiitumia. Mume wake, aliyekuwa akisema naye akiwa mahali pake pa kazi, alingojea kwa hasira iliyozidi kupanda. Alikuwa akizuia simu isitumiwe, na mkubwa wake alikuwa anataka kuitumia. Kwa kukata tamaa sana, alienda nyumbani naye akawa na hasira hata zaidi alipopata kujua mgeni huyo alikuwa amekuwa nani. Ijapokuwa kituko hicho, mke wake alienda kwenye mkutano na akaendelea kuhudhuria mikutano na hatimaye mume wake akajiunga naye. Washiriki tisa wa familia hiyo wakapata kuwa Mashahidi waliobatizwa.

Kutoa Ushuhuda Miongoni mwa Watu wa Lapp

Kuhubiri miongoni mwa watu wa Lapp, baadhi yao wakiwa wangali wanaishi maisha ya kuhama-hama wakiwa na makundi yao ya kulungu wa Kaskazini yenye theluji nyingi, huwa nyakati nyingine jambo lisilo na kifani analopata mtu. Baada ya kuingia katika kao la mtu wa Lapp na ukiisha kumsalimu, usitazamie kuanza mazungumzo mpaka baada ya kupita kipindi fulani cha kimya. Pole kwa pole, huenda ukaanza kuzungumza juu ya hali ya hewa. Hatimaye unapoanza kuelekeza mazungumzo katika mambo ya Kimaandiko, huenda ukafikia mpaka wenye hatari.

Baadhi ya watu wa Lapp huiona Biblia kuwa takatifu sana hivi kwamba wanaona kuwa watu walio wengi hawastahili kuisoma. Gustav Kemi, mzee ambaye yeye mwenyewe ni mtu wa Lapp, asimulia hivi: “Unapozungumza na watu wa Lapp, hasa wale wenye umri mkubwa zaidi, unapata wazo la kwamba wafikiri hata hupaswi kuwa ukisema juu ya Biblia. Mwanamke mmoja wa kutoka Lapp mwenye umri mkubwa alisema waziwazi kwamba “mtu apaswa kulia machozi ya damu kabla hajawa mwenye kustahili vya kutosha kuifungua Biblia.” Mwingine wa kutoka Lapp aliambia mtoto aliyetaka kuangalia ndani ya Biblia: ‘Hapana, hapana. Biblia ni takatifu sana watoto hawapaswi kuitazama.’”

Hata hivyo, baadhi ya watu wa Lapp wameitikia kweli za Biblia na wakachukua msimamo wao upande wa Yehova, ijapokuwa nyakati fulani wafanya hivyo kwa mwendo wa polepole sana. Mtu mmoja wa Lapp alipata kitabu Salvation katika miaka ya mapema ya 1940. Alijifunza kitabu hicho na akayaweka moyoni aliyojifunza lakini akakaa kimya juu ya jambo hilo kwa miaka kumi. Halafu alitembelea mtu mwingine wa kutoka Lapp ambaye alikuwa Shahidi. Alitaka kujua kwa nini Mashahidi wa Yehova hawavuti sigareti au kunusa tumbako. Alitosheka na jibu; wakati uliofuata alipokutana na Shahidi huyo, alisema kwa furaha hivi: “Sasa mimi nimeacha kunusa tumbako. Watoto wangu wameficha vijikebe (mkebe mdogo) vyangu vyote vya kuwekea tumbako.” Alibatizwa upesi baada ya hapo.

Sherehe za Ndoa za Kitheokrasi, Hatua Moja Mbele

Sikuzote Mashahidi wa Yehova wamefanya kazi ili “kuthibitisha kisheria” habari njema. (Flp. 1:7, NW) Kwa kuwa ndoa ni mpango wa kimungu, wahudumu Mashahidi wanataka kuongoza sherehe za ndoa za Kikristo. Hata hivyo, kabla ya Machi 19, 1981, wenzi wa ndoa waliokuwa Mashahidi wa Yehova wangeweza kufunga ndoa ikiongozwa tu na mwandikishaji wa serikali. Tangu hapo, waangalizi wa kundi waliowekwa rasmi, na kupewa mamlaka kibinafsi na serikali, wanaweza kuongoza sherehe za ndoa katika Majumba ya Ufalme.

Ili wapewe mamlaka, waangalizi hao lazima wahudhurie mtaala kwa ajili ya waandikishaji. Wakiongozwa na makao makuu ya ulimwengu, tawi liliendesha mtaala huo, wenye fungu la sheria za ndoa, sheria ya majina, virekebishaji vya uandikishaji wa idadi ya watu, fungu la sheria za uhalifu ambako zinatumika, na mambo mengine mengi yanayohusiana. Halafu maarifa ya waangalizi na ustahili wao hujaribiwa na msimamizi wa mahakama ya wilaya ya kwao. Akiwapendekeza, serikali huwaweka rasmi.

Watu wengi wa ukoo wasio Mashahidi hutembelea Majumba ya Ufalme kuhudhuria sherehe za arusi, na kama tokeo wao hupokea ushuhuda mzuri, hata shauri zuri juu ya wajibu mbalimbali na mapendeleo ya ndoa. Baadhi ya wenzi wa ndoa waliofunga ndoa kabla ya mpango huu husema kwa ucheshi kwamba wangetaka kufunga ndoa upya chini ya mpango huu wa kitheokrasi.

“Nzuri, yenye kujaa shangwe, na yenye kujawa na ucheshi na uchangamfu,” ndivyo ripota mmoja wa vyombo vya habari alivyoieleza sherehe moja katika Jumba la Ufalme, akiendelea hivi: “Ndoa ya kitheokrasi haishikilii sana na kujawa sana na sherehe wala haijawi na mambo ya kujionyesha kama ilivyo katika Kanisa la Serikali. Inakusudiwa iwe tukio lenye shangwe bila kupoteza heshima yayo.”

Mratibu wa Tatu wa Halmashauri ya Tawi la Swedeni

Katika 1975 Ndugu Eneroth, mratibu wa Halmashauri ya Tawi wa pili, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 83, angeweza kutazama nyuma kwenye utumishi wake wa uaminifu wa miaka zaidi ya 50 akiwa katika cheo hicho. Lo, jinsi kazi ilivyokua wakati wa miaka hiyo—kutoka wahubiri wapatao 250 katika 1925 kufika 16,000 wakati huo! Akiwa na mwako wa shangwe na uradhi mchangamfu katika moyo wake, alitambua kwamba wakati ulikuwa umefika ndugu mwingine ashike daraka hilo. Baada ya kuwa amemsaidia Ndugu Eneroth kwa miaka mingi, Ndugu Bengt Hanson aliwekwa rasmi ashike madaraka ya mratibu.

Akiombwa asimulie sehemu ya historia yake ya kitheokrasi, Ndugu Hanson alikumbuka hivi: “Nikiwa na umri wa miaka 16, niliondoka katika shamba la baba yangu nikaenda mji uliokuwa karibu, ambako funzo la Biblia lilianzishwa na baadhi ya ndugu na dada zangu nami. Nikaanza kuhudhuria mikutano. Upesi nikatambua hilo lingemaanisha nini kwangu, yaani, kusoma kwa sauti, kuongoza katika sala, na kutoa hotuba mbele ya wasikilizaji. Hilo lingekuwa jaribu kwangu, kwa kuwa nilikuwa na matatizo makubwa katika kusoma kwa sauti na kufanya masomo darasani katika shule. Upendo kwa Yehova na tamaa yenye moto ya kujitoa kabisa kwa utumishi wa wakati wote vilikuwa msaada mkubwa kwangu. Lakini, lazima nikiri, nilihuzunishwa sana na kizuizi changu. Nilikuwa karibu kushikwa na hofu kuu ya ghafula nilipoombwa nitoe hotuba bila kujitayarisha kwanza.

“Ndipo, nikafanya jambo fulani ambalo lingekuwa la maana sana kwangu katika maisha yangu ya wakati ujao. Kwa kukata tamaa kabisa kwa sababu ya kizuizi changu, nilisali kwa Yehova nikamshukuru kwa kufungua moyo wangu upokee kweli, na kuahidi kutoa maisha yangu katika utumishi wake, ikihitajiwa, mpaka kifo. Niliahidi sitajiondoa kamwe.

“Kwa nini sala hiyo ikawa yenye kukata maneno sana hivyo katika maisha yangu? Kwa sababu, wakati wowote niliposhikwa na hofu, sikuzote nimeweza kuirejezea. Hiyo imenisaidia nishikamane na kazi zangu. Kwa hiyo, ninapotazama nyuma miaka 40 tangu nitoe sala hiyo, lazima niseme kwamba—nyakati nyingine kwa njia yenye ucheshi—Yehova amenifanya nitambue yote yaliyohusika.

“Tangu hapo na kuendelea, ilikuwa ni kama kwamba nilitupwa katika mgawo mmoja baada ya mwingine, ukitaka utumainifu kamili katika Yehova. Nilipokuwa na umri wa miaka 18, nusu mwaka baada ya ubatizo wangu, nilipewa mgawo wa kutoa hotuba za watu wote. Katika muda wa mwaka mmoja, nikawa painia. Miezi minane baadaye, niliitwa nije Betheli. Halafu nikatumwa nje katika kazi ya mzunguko, hata ingawa nilikuwa na umri wa miaka 22 tu. Nilipokuwa na umri wa miaka 30, nikapewa mgawo wa kazi ya wilaya, lakini kabla ya kuanza, mke wangu, Ulla, na mimi tukaalikwa tuhudhurie ule mtaala wa kwanza wa miezi kumi kwenye Shule ya Gileadi katika Brooklyn, katika 1961. Ndipo tulipopewa mgawo wa kufanya kazi Betheli katika Swedeni. Tungali hapa, tukimtumikia Yehova kwa furaha kwa nguvu zetu zote.

“Huenda wengine wakataka kujua kama nilipata kushinda kile kizuizi cha kwanza. Eeh, sitaki kusema kwamba nimekishinda, hata kama naamini kwamba ninafanya vizuri zaidi sasa. Naona kwamba maneno ya Bwana kwa Paulo kwenye 2 Wakorintho 12:9, NW, yatumika kwangu pia: ‘Fadhili zangu zisizostahiliwa zatosha kwako; kwa kuwa nguvu zangu zinakamilishwa katika udhaifu.’”

Arboga—Mahali pa Kituo Kipya

Katika Septemba 8, 1978, ndugu mwenye nguvu na mwenye bidii akiwa na msumeno wenye kutumia mota alikata na kuangusha mti wa kwanza katika eneo la msitu wenye mawe-mawe katika viunga vya Arboga. Kwa nini? Ili kutayarisha mahali pa kituo kipya cha kuendeshea kazi ya Ufalme! Hiyo ikamaliza kipindi kirefu cha kufanya mipango na kujadiliana na kuanza ujenzi wa majengo ambayo yangekuwa, kama vile ripota mmoja wa habari za magazetini alivyopaita, “yenye kutokeza zaidi na kubwa zaidi yaliyopata kujengwa na wafanyakazi wa kujitolea katika nchi hii.”

Tayari miaka kadhaa mapema familia ya Betheli ilikuwa imekuwa ikazidi yale majengo ya tawi yenye umri wa miaka 26 katika Jakobsberg. Baada ya sala nyingi zenye kutolewa mara nyingi, pamoja na miaka miwili ya kutafuta-tafuta mahali penye kufaa, tuliamua kujenga katika Arboga, ambapo ni mahali penye kufaa karibu na ile Njia Kuu ya 3 ya Ulaya yenye kupita magari mengi iliyo kati ya majiji mawili makubwa zaidi ya Swedeni, Stockholm na Göteborg.

Mradi wa Ujenzi Usio na Kifani

Katika muda wa miaka miwili na nusu iliyofuata, wafanyakazi wa kujitolea wapatao 5,000 kutoka Swedeni na nchi zilizo jirani walifanya kazi katika mahali pa ujenzi bila malipo kwa vipindi vifupi au virefu. Kwa kawaida, wafanyakazi hawaishi katika hoteli yenye starehe wanapokuwa wakifanya kazi, lakini Sosaiti ilikuwa imenunua hoteli kuukuu yenye nyumba nyingi pamoja na vyumba vingine mjini, ambavyo vilitengenezwa upya kisha vikatumiwa kuwa makao ya kuishi wafanyakazi hao wa kujitolea. Baada ya mradi huo kukamilishwa, hoteli hiyo iliuzwa.

Kazi ya ujenzi ilikuwa yenye kufurahisha sana. Lakini ilikuwa na matatizo fulani pia. “Hatutasahau kamwe majira hayo ya baridi ya kwanza,” Gunnar Heinstedt, mmoja wa wasimamizi, asema, akiendelea hivi: “Yalifikiriwa kuwa mojayapo majira ya baridi yenye baridi kali zaidi katika karne hii. Wakati wa vipindi fulani, tulipokuwa tukitayarisha msingi, hali ya joto ilishuka kufikia digrii -30 Celsius. Ardhi ilikuwa ngumu kama jiwe gumu sana. Ilitulazimu kufunika ardhi kwa chandarua na kupulizia chini hewa yenye joto, tukitumia dramu za mafuta kama vipasha-joto. Tukasonga mbele kwa ujasiri! Lilikuwa mojayapo mambo yaliyoonwa yenye kuleta shangwe sana katika kazi yangu ya maisha ya miaka 35 nikiwa mjenzi na mchoraji ramani za ujenzi.”

Majengo Mapya ya Tawi Yathaminiwa Sana

Ijapokuwa Desemba 23, 1980, ilikuwa mojayapo siku zenye giza zaidi katika mwaka huo wote katika Arboga—jua lilichomoza saa 2:55 asubuhi na likashuka saa 8:50 alasiri—ilikuwa ndiyo siku nyangavu zaidi na yenye furaha zaidi kati ya siku zote za kipindi cha ujenzi. Tawi hilo jipya liliwekwa wakfu kwa Yehova katika siku hiyo! Ndugu Milton Henschel wa Baraza Linaloongoza alitoa hotuba ya wakfu, akiwatia moyo akina ndugu waendelee kufanya mapenzi ya Mungu kwa nafsi yote wanapotumia jengo hilo jipya.

Mmojawapo washiriki wa familia ya Betheli alisema: “Katika ile siku tulipoondoka yale majengo yaliyosongamana katika Jakobsberg na kuhamia majengo haya ya Betheli mapya kabisa yenye nafasi tele, tulijiona kama ndama waliofunguliwa mahali walipofungiwa katika wakati wa majira ya masika.” Majengo hayo yana nafasi ya sakafu ya meta za mraba 20,000 na ardhi na mashamba yayo ya hekta 12 yenye msitu iliwapa familia ya Betheli hisia yenye kufurahisha ya uwazi na utulivu. Ile bustani yenye uzuri, vifaa vya tafrija, miti ya matunda, bustani za mboga, na bustani zenye kupendeza za maua vilifanyiza mazingira yenye kufaa kwa ajili ya wafanyakazi wa wakati wote, yakiwahimiza wazidishe utendaji wao.

Matbaa Mpya Zaongezea Kazi Mwendo

Kile kiwanda kipya kiliwaruhusu ndugu kutumia vifaa vya uchapaji vyenye matokeo zaidi. Waliacha kutumia zile mashine za kupiga chapa za kikale zenye mwendo wa polepole na kuanza kutumia mashine ya kupiga chapa ya M.A.N. kutoka Brooklyn iliyogeuzwa kuwa mashine ya kupiga chapa yenye kuzunguka inayochapa kwa kuhamisha maandishi kutoka chombo cha mviringo kwenye karatasi. Ilitumika kwa miaka zaidi ya mitano kisha mahali payo pakachukuliwa na mashine ya kupiga chapa ya rangi nne katika Mei 1989. Mashine ya kupiga chapa aina iyo hiyo ilianza kutumiwa mwaka uliofuata. Katika 1990 utokezaji wa kila mwezi ulifikia karibu nakala 800,000 za yale magazeti mawili katika Kiswedeni na Kinorwei. Inge Olofsson, mwangalizi wa kiwanda na mshiriki wa Halmashauri ya Tawi, asema hivi:

“Mashine yetu ya kwanza ya kupiga chapa, iliyoendeshwa kwa miguu, yenye kutiwa karatasi kwa mkono ya aina ya Diegel ya tangu miaka ya 1940, yasimama kwenye pembe moja ya tawi jipya ikiwa kama kitu fulani cha kale katika jumba la hifadhi ya vitu vya kale ikiwa kikumbusha cha usitawi mzuri ajabu wa kazi ambao tumejionea kwa miaka yote iliyopita. Yatukumbusha alivyosema Yesu: ‘Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.’”—Lk. 18:27.

Ukuzi Mzuri wa Faida za Ufalme

Wakati mtu anapofikiria jitihada za Ufalme katika Swedeni za muda wa karibu karne moja, vizuizi vilivyopatikana katika muda wote huo vyaonekana wazi, kama vile upendo wenye kukua wa vitu vya kimwili, kutojali kwa kidini na kutoamini kuwako kwa Mungu, upinzani ulio wazi na dhihaka, na tabia iliyo asili ya Waswedeni kwa ujumla ya kutokuwa wasemaji sana. Yajapokuwa mambo hayo yote, Mashahidi wa Yehova, kwa sababu ya upendo wao kwa jirani na kwa Mungu, walisonga mbele wakiwa na habari njema katika kila pembe. Watu wengi wangali wanavutiwa na ujumbe mzuri ajabu ambao Mashahidi wanawaletea.

Erik Nordström, mwangalizi wa wilaya, akumbuka hivi: “Mke wangu nami tulianza utumishi wa kusafiri miaka 37 iliyopita, nasi tumetembelea makundi zaidi ya 300 katika Swedeni tena na tena mara kadhaa, katika kazi ya mzunguko na ya wilaya. Tumesafiri kilometa 200,000 kotekote katika nchi hii ndefu na nyembamba. Wala hali ya hewa yenye baridi kali na pepo kali zenye theluji za Kaskazini, kuvuka Mzingo wa Aktiki, wala jua na joto la Kusini havingeweza kutuzuia.

“Naam, baada ya miaka 45 ya utumishi wa wakati wote, sisi tunaweza kutazama nyuma katika wakati wenye kusisimua wa maendeleo ya kiroho katika Swedeni. Tofauti na yaliyoupata ulimwengu wa kale, sikuzote jamii ya kitheokrasi imesonga mbele.”

“Faida za Ufalme zimeimarishwa katika kila sehemu ya nchi hii,” asema Rune Grahn, mwangalizi wa Idara ya Utumishi. Aripoti: “Sasa tuna makundi 388 yaliyotawanyika kotekote nchini—tokea ncha ya kusini zaidi mpaka mbali sana kuvuka Mzingo wa Aktiki kuingia katika nchi ya jua la usiku wa manane. Tuna mizunguko 15 ya Kiswedeni na 8 katika lugha za kigeni, ikikusanyika kwa ukawaida katika Majumba ya Kusanyiko manne, yakienea kijiografia nchini pote. Tulikuwa na kilele cha wahubiri wa Ufalme 22,742 katika Agosti 1990, karibu 1,700 kati yao wakiwa mapainia wa kawaida. Walikuwako 38,339 waliohudhuria Ukumbusho katika 1990, wakiahidi ongezeko zaidi kadiri Yehova aruhusuvyo kazi hii iendelee.”

Hatua kwa hatua, kazi katika Swedeni imefanya maendeleo katika muda wa miaka iliyopita. Akina ndugu na dada wameonyesha nguvu, imani, na uvumilivu. Kwa ushikamanifu na kwa moyo wa bidii wameendelea kutii matakwa ya Baba yao wa kimbingu kama yalivyoelezwa kupitia tengenezo lake. Kwa hiyo, wanatazamia wakati ujao wakiwa na uhakika wa baraka za Yehova zenye kuendelea. Wanazidi kusali kwamba wadumu wakiwa washikamanifu kwa Mungu wetu, ambaye anatenda mambo yenye kustaajabisha sana katika Swedeni na vilevile katika zile nchi nyingine zaidi ya 200. “Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, wewe ndiwe mfanya miujiza, ndiwe Mungu peke yako.”—Zab. 86:10.

[Chati katika ukurasa wa 185]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Swedeni 28,000

1950 4,460

1960 8,593

1970 11,696

1980 17,311

1990 22,742

Kilele cha Wahubiri

4,000

1950 178

1960 314

1970 754

1980 1190

1990 2,724

Wast. Mapainia

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 116]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Bahari ya Atlantiki

NORWEI

Bahari ya Kaskazini

DENMARKI

Copenhagen

SWEDENI

Kiruna

Mzingo wa Aktiki

Härnösand

Sundsvall

Uppsala

Arboga

Jakobsberg

Örebro

Grums

Stockholm

Göteborg

Malmö

Bahari ya Baltiki

FINLANDI

[Sanduku]

SWEDENI

Mji Mkuu: Stockholm

Lugha Rasmi: Kiswedeni

Dini Kubwa: Ulutheri

Idadi ya Watu: 8,574,698

Ofisi ya Tawi: Arboga

[Picha katika ukurasa wa 118]

Makimbilio yenye utulivu ni mengi wakati wa siku za vuli katika Swedeni

[Picha katika ukurasa wa 129]

Rosa na Arthur Gustavsson, walijishughulisha katika kuhubiri Ufalme pamoja kwa miaka 59

[Picha katika ukurasa wa 136]

Waangalizi kutoka nchi za Ulaya kaskazini. Kutoka kushoto kwenda kulia: Taylor (Latvia), Eneroth (Swedeni), Harteva (Finlandi), Dey (msimamizi wa ujumla), Lüttichau (Denmarki), Öman (Norwei), West (Estonia)

[Picha katika ukurasa wa 137]

Johan H. Eneroth alipata kuwa mwangalizi wa tawi katika 1925

[Picha katika ukurasa wa 139]

William Dey alipata kuwa mwangalizi wa ofisi mpya ya Sosaiti ya Ulaya Kaskazini katika 1925

[Picha katika ukurasa wa 140]

Ofisi ya tawi, Luntmakare-gatan 94, Stockholm, ilinunuliwa katika 1929. Ilitumikia faida za Ufalme kwa miaka 25

[Picha katika ukurasa wa 141]

Habari njema zilisafiri zikaingia ndani sana ya misitu ya Swedeni kaskazini

[Picha katika ukurasa wa 143]

Wote tayari kwa Jumapili ya kuhubiri nje ya Stockholm

Kikundi kutoka Lulea kitaingia karibuni ndani ya motokaa waende kuhubiri kusini tu mwa Mzingo wa Aktiki

[Picha katika ukurasa wa 145]

Asta na Axel Richardson walitumikia katika mkoa wa Jämtland wakati wa 1936

[Picha katika ukurasa wa 147]

Mashahidi wa mapema zaidi katika Hjo walitumia minibasi kueneza eneo moja la kilometa za mraba 5,000

[Picha katika ukurasa wa 150]

Hawajapata kuwa wacha-nga mno kutumikia Ufalme

[Picha katika ukurasa wa 155]

Vinanda vyenye kubebeka vilitumiwa kutangaza kotekote habari njema. Kwa nini zingeweza kuitwa “Haruni 2”?

[Picha katika ukurasa wa 160]

Wahubiri wachanga wa habari njema wakiwa pamoja na mama yao, katika Värnamo, 1946

Wanaume wenye karatasi zilizoangikwa mabegani mwao mbele na nyuma wakitangaza mkutano wa watu wote katika Stockholm

[Picha katika ukurasa wa 170]

Ofisi ya tawi ilikuwa katika Jakobsberg tokea 1954 mpaka 1980

[Picha katika ukurasa wa 176, 177]

Ofisi ya tawi na Makao ya Betheli katika Arboga, yaliyowekwa wakfu Desemba 23, 1980. Msimamizi wa Sosaiti, F. W. Franz, mwenye kuvalia kofia ngumu nyeupe, akitembelea mahali pa ujenzi kabla ya tawi kukamilishwa

[Picha katika ukurasa wa 178]

Halmashauri ya Tawi. Kutoka kushoto kwenda kulia, Åke Carlsson, Rune Grahn, Bengt Hanson, na Inge Olofsson

[Picha katika ukurasa wa 183]

Mashine mpya ya kupigia chapa yachukua mahali pa ile mashine ya kupiga chapa yenye kuzunguka ya zamani kidogo aina ya M.A.N. Mashine mpya ya kupiga chapa huchapa vichapo vya Biblia kwa rangi kamili

[Picha katika ukurasa wa 184]

Kutolea ushuhuda wavuvi katika Djupvik kisiwani Gotland na katika ua wa nyumba katika Ystad, jiji dogo katika upande wa kusini

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki