Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g00 7/22 kur. 14-17
  • Mradi Mpya wa Mwisho Antaktika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mradi Mpya wa Mwisho Antaktika
  • Amkeni!—2000
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Kama Kuzuru Mihiri!
  • Lilipewa Jina Kabla ya Kugunduliwa
  • Damu Kwenye Barafu
  • Antaktika Bara Lililo Hatarini
    Amkeni!—2000
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2000
  • Majumba Yenye Kumetameta ya Baharini
    Amkeni!—1995
  • Kuvua Samaki Kwenye Barafu
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2000
g00 7/22 kur. 14-17

Mradi Mpya wa Mwisho Antaktika

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

SEHEMU fulani za Antaktika zaweza kuwa baridi sana, asema mwandishi mmoja, hivi kwamba “ukiangusha ufito wa feleji waweza kuvunjika kama kioo, . . . na ukivuta samaki kutoka kwenye shimo ndani ya barafu kwa muda wa sekunde tano ataganda . . . na kuwa mgumu kabisa.” Kwa sababu ya hali zake za kipekee na zisizo za kawaida, uzuri usio na mimea yoyote—nyakati nyingine unaokamilishwa na nuru yenye kuvutia kutoka kusini—Antaktika ni kama ulimwengu mwingine.

Lakini Antaktika ni sehemu ya ulimwengu huu. Kwa hakika, imelinganishwa na maabara kubwa ya asili ya kuchunguza dunia na angahewa lake, na vilevile mabadiliko ya kimazingira, kutia ndani yale yanayosababishwa na wanadamu. Wanasayansi wanazidi kuhangaika wanapofikiria uchunguzi huo. Wameona matukio mapya yenye kuogofya katika Maeneo ya Ncha za Kusini, na yanadokeza kwamba hali si shwari kabisa. Lakini kwanza, acheni tuone kwa nini Antaktika ni bara la pekee.

Kwanza, Antaktika—bara lililojitenga zaidi na mabara mengine ulimwenguni—ni bara la utofautiano. Lina uzuri mwingi kupindukia na halijavurugwa na utendaji wa wanadamu lakini halikaliki. Ndiyo sehemu yenye upepo zaidi ulimwenguni, yenye baridi zaidi, hata hivyo huathirika kwa urahisi. Ndilo bara lenye mvua ndogo zaidi kuliko bara jinginelo, lakini barafu yake ni asilimia 70 ya maji yasiyo na chumvi katika sayari yetu. Barafu hiyo iliyo na kimo cha meta 2,200 hufanya Antaktika kuwa bara refu zaidi duniani, likiwa na wastani wa meta 2,300 juu ya usawa wa bahari. Pia ndilo bara la tano kwa ukubwa duniani, na bado Antaktika halina wakazi wa kudumu isipokuwa usubi, aina fulani ya nzi asiye na mabawa mwenye urefu unaozidi sentimeta moja.

Ni Kama Kuzuru Mihiri!

Unapojasiria kutembea katika sehemu za ndani-ndani za Antaktika, utaona viumbe wakizidi kupungua, hasa ufikapo maeneo yanayoitwa mabonde makavu. Majangwa hayo ya nchani yenye ukubwa wa kilometa mraba 3,000 yapo hasa kwenye Milima ya Transantarctic—mfululizo wa safu za milima unaovuka bara hilo na kufikia urefu wa meta 4,300 katika sehemu fulani. Dhoruba za barafu hupita katikati ya mabonde makavu na kukausha mara moja theluji ambayo huenda ikaanguka. Wanasayansi wanaamini kwamba mabonde hayo yaliyopo duniani yanafanana na Mihiri. Kwa sababu hiyo, yalionwa kuwa eneo linalofaa kujaribia vifaa vya angani kabla ya kurusha chombo Viking kwenye Mihiri.

Na bado, hata mabonde makavu yana viumbe hai! Ndani ya miamba yenye kuvuja, katika mianya midogo ya hewa, huishi aina fulani za bakteria, mwani, na kuvu zilizo sugu. Hutegemea tu unyevu kidogo sana ili kuishi. Nje ya makao yao yasiyo ya kawaida kuna miamba iliyo ukiwa inayoitwa ventifact, yenye umbo la ajabu na inayong’aa sana kwa sababu ya kupigwa na pepo zisizokoma za Antaktika kwa karne nyingi.

Lilipewa Jina Kabla ya Kugunduliwa

Tangu siku za wanafalsafa Wagiriki wa kale, ilidhaniwa kwamba kuna ardhi kubwa sana upande wa kusini. Kwa mfano, Aristotle, alidai kwamba kuna uhitaji wa kuwa na bara la kusini ili kusawazisha ardhi iliyojulikana kuwa katika Kizio cha Kaskazini. Kitabu Antarctica—Great Stories From the Frozen Continent chasema kwamba “kwa kuwa kizio cha kaskazini kilikuwa chini ya kundi la nyota la Arktos, Dubu, kwa hiyo, Aristotle (384-322 KWK) alisababu kwamba ardhi isiyojulikana kuelekea upande wa kusini lazima iwe Antarktikos—yaani, kinyume kabisa”—au upande unaoelekeana. Hivyo, kwa kweli Antaktika ni tofauti kwa sababu, ilipewa jina miaka 2,000 hivi kabla haijagunduliwa!

Mwaka wa 1772, mvumbuzi Mwingereza Kapteni James Cook aliabiri kuelekea kusini ili kutafuta lile bara lililodaiwa lilikuwa kusini. Aliingia kwenye visiwa vinavyopigwa na upepo mkali na vilima vikubwa vya barafu, au “visiwa vya barafu,” kama alivyoviita. “Baadhi yake,” aliandika, “vilikuwa na mzunguko upatao kilometa tatu, na urefu wa meta 20, na bado mawimbi ya bahari yalikuwa na nguvu kiasi cha kubeba vilima hivyo.” Akiwa ameazimia, Cook aliendelea kusafiri upande wa kusini, na katika Januari 17, 1773, meli zake, Resolution na Adventure, zikawa vyombo vya kwanza vya baharini kupata kuvuka Mzingo wa Antaktiki. Cook aliendesha chombo chake kwa kukwepa barafu ya baharini mpaka alipozuiwa hatimaye. “Singeweza kuona chochote upande wa kusini ila barafu,” akaandika katika kifaa chake cha kurekodia mwendo na safari ya meli. Kwa kweli, alikuwa amebakisha mwendo wa kilometa 120 tu kufika kwenye ardhi ya Antaktiki alipogeuka na kurudi nyuma.

Kwa hiyo ni nani aliyekuwa wa kwanza kuona Antaktika? Kwa kweli, ni nani aliyekuwa wa kwanza kufika huko? Hakuna mtu aliye na hakika kufikia leo hii. Huenda hata ilikuwa ni wavuvi wa nyangumi au wawindaji wa sili, kwa kuwa Cook aliporudi nyumbani, na kuripoti kwamba kulikuwa na sili, pengwini, na nyangumi wengi, wavuvi walikimbia hima-hima kwenye eneo hilo.

Damu Kwenye Barafu

Cook “aligundua kundi kubwa zaidi la wanyama wa mwitu ulimwenguni, na alikuwa mtu wa kwanza kujulisha ulimwengu juu ya wanyama hao,” akaandika Alan Moorehead katika kitabu chake The Fatal Impact. “Kuhusu wanyama wanaoishi Antaktika,” asema Moorehead, “[matokeo] yalikuwa ni maangamizi makubwa.” Kitabu Antarctica—Great Stories From the Frozen Continent chasema: “Kuelekea mwisho wa karne ya kumi na nane, kuvua sili katika kizio cha kusini kulifanana sana na hekaheka za kutafuta dhahabu iliyogunduliwa. Mahitaji ya ngozi ya sili huko China na Ulaya yameongezeka sana hivi kwamba sili wote waliokuwapo walitoweka na hivyo kukatisha tamaa wawindaji wa sili, ambao sasa walihitaji kwenda kutafuta sehemu mpya za kuwinda zenye makazi yasiyoporwa ya wanyama hao.”

Baada ya wawindaji wa sili kuharibu kabisa riziki yao, wavuvi wa nyangumi walianza kupora bahari. “Hakuna mtu atakayepata kujua ni nyangumi na sili wangapi waliouawa katika bahari ya kusini,” aandika Moorehead. “Je, ni milioni kumi au milioni hamsini? Hakuna haja ya kuhesabu; mauaji yaliendelea mpaka hakukuwa na chochote cha kuua.”

Hata hivyo, leo, sheria za kimataifa hulinda mimea na wanyama wote wa Antaktiki. Kwa kuongezea, kukosekana kwa wanyama-wawindaji wa ardhini pamoja na chakula kingi sana cha baharini hufanya pwani ya Antaktiki iwe mahali salama kwa ajili ya wanyama wa mwitu. Lakini kuna ishara za mashambulizi yasiyoonekana waziwazi huko Antaktika, ambazo huenda zisikomeshwe na mikataba ya kimataifa.

[Sanduku katika ukurasa wa 15]

NCHA ZILIZOELEKEANA

Ijapokuwa zinafanana kwa kiasi fulani, Ncha ya Kaskazini na Ncha ya Kusini ni ‘ncha zilizoelekeana kabisa’ katika njia nyingi kuliko tu mahali zilipo. Fikiria yafuatayo.

Eneo lote lililo karibu zaidi na Ncha ya Kaskazini lina barafu na bahari, ilhali Ncha ya Kusini iko karibu na sehemu ya kati ya bara la tano kwa ukubwa duniani.

Ncha ya Kaskazini imezungukwa na nchi zenye watu wengi za Amerika, Asia, na Ulaya, ilhali Antaktika imezingirwa na bahari kubwa, ambayo kwa kweli ndiyo yenye tufani zaidi katika sayari.

Makumi ya maelfu ya familia huishi karibu na Mzingo wa Aktiki, ambao pia ni makao ya maelfu ya mimea na wanyama. Hata hivyo hakuna mwanadamu aliye mwenyeji wa Antaktika. Viumbe hai pekee walio wa asili ya huko ni mwani, bakteria, kuvumwani, kuvu, aina mbili za maua, na aina chache za wadudu.

“Antaktika imeitwa bara linalodundadunda,” chasema kichapo Encyclopædia Britannica, “kwa sababu ya ongezeko la barafu linalotukia kila mwaka na kupungua kwa pwani zenye barafu upande wa mbele.” Kwenye kilele chake, mwamba wa barafu huenea umbali wa kilometa 1,600 mbali na bahari. Kupanuka na kunywea huko ni mara sita zaidi ya mwamba wa barafu wa Aktiki, jambo linaloifanya Antaktika iathiri zaidi halihewa ulimwenguni pote.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI YA ATLANTIKI

BAHARI YA HINDI

BAHARI YA PASIFIKI

Njia ya Drake

Kisiwa cha James Ross

Mwamba wa Barafu wa Larsen

PENINSULA YA ANTAKTIKI

Mwamba wa Barafu wa Ronne

Vinson Massif (mlima mrefu zaidi, meta 4,868)

Mwamba wa Barafu wa Ross

Ml. Erebus (volkeno hai)

MILIMA YA TRANSANTARCTIC

Ncha ya Kusini

Baridi kali zaidi iliyopata kurekodiwa duniani ilikuwa katika Antaktika—nyuzi Selsiasi -89.2

0 500 km 500 miles

[Hisani]

U.S. Geological Survey

[Picha katika ukurasa wa 16]

Pengwini aina ya “chinstrap” wakusanyika kwenye kilima cha barafu cha samawati kisicho cha kawaida

[Hisani]

© 2000 Mark J. Thomas/Dembinsky Photo Assoc., Inc.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyangumi mwenye nundu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sili wa kusini aina ya “elephant”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kwenye Ncha ya Kusini

[Hisani]

Picha: Commander John Bortniak, NOAA Corps

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mwamba wa Barafu wa Ross

[Hisani]

Michael Van Woert, NOAA NESDIS, ORA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki