Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Maradhi ya Huntington Sina budi kutoa shukrani zangu za kutoka moyoni kwa ajili ya makala “Maradhi ya Huntington—Kuuelewa Msiba Unaoathiri Chembe za Urithi.” (Machi 22, 2000) Kwa miaka 20 nilimtunza mume wangu aliyekuwa na ugonjwa huo. Makala ya aina hii, iliyoandikwa kwa hisia na ufahamu, itavutia watu wengi.
N. G., New Zealand
Asanteni kwa makala hiyo. Maelezo yenu yalikuwa rahisi kuelewa kuliko ya daktari wetu. Miaka mitatu hivi iliyopita, uchunguzi ulionyesha kwamba mama yangu ana maradhi ya Huntington [HD]. Inaumiza sana kumwona aking’ang’ana kusema, kula, na kutembea. Jambo moja ambalo hamkutaja ni kwamba kumbukumbu ya mambo ya zamani hudumu zaidi kuliko kumbukumbu ya mambo ya karibuni. Kwa sababu hiyo, kuongea juu ya marafiki wa zamani au kutazama picha za wakati uliopita pamoja na mtu aliyeathiriwa sana na maradhi ya Huntington kwaweza kumsaidia na kumfariji.
J. M., Marekani
Miaka minne iliyopita uchunguzi ulionyesha kwamba mume wangu ana maradhi ya Huntington. Takriban mwaka mmoja na nusu uliopita, niliandikia wachapishaji wa Amkeni! kuomba habari juu ya hali hiyo. Nilipoona makala hiyo, nililia machozi ya kufarijika na shangwe.
D. B., Marekani
Ambukizo la Mchochota wa Ini Inaonekana kwamba kuna kasoro katika makala “Ambukizo la Damu Lililo la Kawaida Zaidi” katika “Kuutazama Ulimwengu,” kwenye toleo la Aprili 22, 2000. Mlisema kwamba virusi vya mchochota wa ini aina ya C hasa hupitishwa kingono au kupitia damu iliyoambukizwa. Kwa kweli, ambukizo kupitia kufanya ngono ni nadra sana na hufanyika tu chini ya hali za pekee, kama vile wakati wa hedhi.
C. A., Ufaransa
Huenda makala hiyo fupi ilitoa maoni yasiyofaa, kwa kuwa yaonekana kwamba virusi vya mchochota wa ini aina ya C huambukizwa sana kupitia matumizi ya dawa za kulevya zitiwazo mishipani kuliko kupitia mahusiano ya ngono. Kulingana na toleo la Februari 1996 la “Harvard Health Letter,” watu walio na wenzi wenye mchochota wa ini aina ya C hawako katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Hata hivyo, makala moja katika toleo la Agosti 19, 1999 la “The New England Journal of Medicine” ilitoa ripoti hii kuhusu kuenea kwa maambukizo ya mchochota wa ini aina ya C katika Marekani kutoka mwaka wa 1988 hadi mwaka wa 1994: “Sababu kuu zinazohusianishwa na ambukizo la mchochota wa ini aina ya C ni matumizi haramu ya dawa za kulevya na ngono hatari.” Pia ilisema hivi: “Ingawa kuenezwa kwa virusi vya mchochota wa ini aina ya C kupitia kufanya ngono ni nadra, . . . ile idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa wa kudumu wa mchochota wa ini aina ya C inafanya watu wanaofanya ngono ovyoovyo na wenzi tofauti-tofauti wawe katika hatari kubwa ya kuambukizwa.”—Mhariri.
Kutoboa Mwili Asanteni kwa makala “Vijana Huuliza . . . Vipi Juu ya Kutoboa Mwili?” (Machi 22, 2000) Nina umri wa miaka 16 na kwa muda fulani nimekuwa nikifikiria kutoboa mwili wangu. Ingawa nilitafuta maoni kutoka kwa watu kadhaa kuhusu jambo hilo, bado nilisita kufanya uamuzi. Hata hivyo, habari ya wazi na yenye kuarifu katika makala hiyo ilinisaidia kufahamu kwamba sipaswi kutoboa mwili wangu, ingawa kufanya hivyo ni mtindo unaopendwa sana.
E. C., Uingereza
Kwa kuwa mbeleni nilikuwa mwimbaji katika bendi iliyoimba muziki mchafu wa roki, niliiona makala yenu juu ya kutoboa mwili kuwa ya wakati unaofaa. Inashangaza kama nini kwamba watu wanatafuta umashuhuri kwa kufuata mitindo ya karibuni!
F. S., Marekani
Maadili Jana nilisoma ule mfululizo wa makala “Maadili Yamepatwa na Nini?” (Aprili 8, 2000) Maelezo halisi kama nini! Mfululizo huo waonyesha jinsi dhambi ilivyo yenye kuchukiza. Kwa kweli, kabla sijawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nilikuwa mtu wa maadili mapotovu sana. Hata sasa napambana na tamaa za mwili zenye nguvu. Hata hivyo, kwa upendo na utunzaji wa Yehova, msaada wa wazee wenye upendo, utegemezo wa ndugu na dada zangu Wakristo, na makala kama hizi, naelekea kushinda vita hiyo.
J.C.P., Marekani