Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g04 8/8 kur. 3-4
  • Tamaa ya Kiasili ya Kujifunza

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tamaa ya Kiasili ya Kujifunza
  • Amkeni!—2004
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi ya Kusitawisha Tamaa ya Kujifunza
    Amkeni!—2004
  • Funguo za Elimu Nzuri
    Amkeni!—1995
  • Je, Ningeweza Kufanya Vizuri Zaidi Shuleni?
    Amkeni!—1998
  • Kulea Watoto tangu Uchanga
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2004
g04 8/8 kur. 3-4

Tamaa ya Kiasili ya Kujifunza

“Ndege huruka, samaki huogelea; mwanadamu hufikiri na kujifunza.”—JOHN HOLT, MWANDISHI NA MWALIMU.

MBAWALA aliyetoka kuzaliwa ana tamaa ya kiasili ya kusimama kwa miguu yake mirefu inayoyumbayumba na kumfuata mama yake. Kwa upande mwingine, kuna uwezekano kwamba mtoto wa binadamu hatakuwa ameweza kutembea anapofikia umri wa mwaka mmoja. Hata hivyo, wanadamu wamepewa ubongo wa ajabu sana ambao ni bora kuliko ule wa mnyama yeyote. Ubora huo unaonekana katika tamaa kubwa ya mtoto ya kutaka kuvumbua na kujua mambo.

Ili kutosheleza tamaa hiyo, watoto wenye afya hujaribu kufanya mambo mbalimbali. Ukiwapa kitu, watatumia hisi zao zote kukichunguza, hata watakionja! Na uchunguzi wao hauishii hapo. Kama kila mzazi anavyojua, watoto hukunja, hugonga, hutikisa, na kuvunja vitu wanapojaribu kuelewa na kutambua mazingira yao, na mara nyingi wanafanya hivyo wakiwa na furaha sana.

Tamaa hiyo kubwa ya watoto ya kutaka kujua huonekana wazi zaidi wanapoanza kuongea—hatua kubwa kwelikweli! Ghafula wanaanza kuuliza maswali mengi. Wazazi wengi hulemewa na maswali ya watoto wao yasiyokwisha, kama vile ‘Kwa nini?’ au ‘Hii ni nini?’ Mwandishi John Holt anasema hivi: “Wao hujifunza mambo mengi kwa uchangamfu wanaposisimuka ghafula.”

Kisha, miaka michache baadaye, watoto katika nchi nyingi huanza mkondo mpya wa kujifunza ambapo wanakutana na walimu, vitabu, madawati, na labda mamia ya watoto wengine wengi. Kwa kusikitisha, baada ya kukaa shuleni kwa miaka kadhaa, vijana wengi hupoteza hamu ya kujifunza shuleni. Wengine hata huanza kuiona shule kuwa yenye kulemea na yenye kuchosha. Huenda hawapendi masomo au walimu fulani. Au labda wanahangaika wanaposhurutishwa kupita kiasi kupata maksi za juu.

Maoni hayo yasiyofaa kuhusu kujifunza yanaweza kuendelea hata katika utu uzima na uzeeni na kuwafanya wasipendezwe na mambo yoyote yanayohusisha kufikiri sana, kujifunza, au kufanya utafiti. Wazee hukabili tatizo lingine, kwani wanaona kwamba uzee ni kizuizi cha kujifunza. Lakini kama tutakavyoona, maoni hayo hayafai.

Je, ungependa kuboresha uwezo wako na tamaa yako ya kujifunza licha ya umri wako? Ikiwa wewe ni mzazi, je, ungependa watoto wako wafaulu shuleni na kufurahia kujifunza wanapokuwa shuleni na baadaye maishani? Ikiwa ndivyo, tafadhali soma makala zinazofuata.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Watoto hupenda kujifunza

[Picha katika ukurasa wa 3]

Inasikitisha kwamba vijana wengi hukabili mfadhaiko na mahangaiko shuleni

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki