Mathayo
Kulingana na Mathayo
1 Kitabu cha historia ya Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:
2 Abrahamu akawa baba ya Isaka;
Isaka akawa baba ya Yakobo;
Yakobo akawa baba ya Yuda na ndugu zake;
3 Yuda akawa baba ya Perezi na ya Zera kwa Tamari;
Perezi akawa baba ya Hezroni;
Hezroni akawa baba ya Ramu;
4 Ramu akawa baba ya Aminadabu;
Aminadabu akawa baba ya Nashoni;
Nashoni akawa baba ya Salmoni;
5 Salmoni akawa baba ya Boazi kwa Rahabu;
Boazi akawa baba ya Obedi kwa Ruthi;
Obedi akawa baba ya Yese;
6 Yese akawa baba ya Daudi mfalme.
Daudi akawa baba ya Solomoni kupitia mke wa Uria;
7 Solomoni akawa baba ya Rehoboamu;
Rehoboamu akawa baba ya Abiya;
Abiya akawa baba ya Asa;
8 Asa akawa baba ya Yehoshafati;
Yehoshafati akawa baba ya Yehoramu;
Yehoramu akawa baba ya Uzia;
9 Uzia akawa baba ya Yothamu;
Yothamu akawa baba ya Ahazi;
Ahazi akawa baba ya Hezekia;
10 Hezekia akawa baba ya Manase;
Manase akawa baba ya Amoni;
Amoni akawa baba ya Yosia;
11 Yosia akawa baba ya Yekonia na ya ndugu zake wakati wa uhamisho hadi Babiloni.
12 Baada ya uhamisho hadi Babiloni Yekonia akawa baba ya Shealtieli;
Shealtieli akawa baba ya Zerubabeli;
13 Zerubabeli akawa baba ya Abiudi;
Abiudi akawa baba ya Eliakimu;
Eliakimu akawa baba ya Azori;
14 Azori akawa baba ya Zadoki;
Zadoki akawa baba ya Akimu;
Akimu akawa baba ya Eliudi;
15 Eliudi akawa baba ya Eleazari;
Eleazari akawa baba ya Mathani;
Mathani akawa baba ya Yakobo;
16 Yakobo akawa baba ya Yosefu mume wa Maria, ambaye kwake Yesu alizaliwa, aitwaye Kristo.
17 Basi, vizazi vyote kutoka Abrahamu mpaka Daudi vilikuwa vizazi kumi na vinne, na kutoka Daudi mpaka uhamisho hadi Babiloni vizazi kumi na vinne, na kutoka uhamisho hadi Babiloni mpaka Kristo vizazi kumi na vinne.
18 Lakini uzaliwa wa Yesu Kristo ulikuwa katika njia hii. Katika wakati ambao Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, alipatwa kuwa ana mimba kwa roho takatifu kabla ya wao kuungana pamoja. 19 Hata hivyo, Yosefu mume wake, kwa sababu alikuwa mwadilifu na hakutaka kumfanya kuwa kitu cha kutazamwa na watu wote, alikusudia kumtaliki kwa siri. 20 Lakini baada ya yeye kuwa amefikiria-fikiria mambo haya, tazama! malaika wa Yehova alionekana kwake katika ndoto, akisema: “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumpeleka Maria mke wako nyumbani, kwa maana kile ambacho kimezaliwa ndani yake ni kwa roho takatifu. 21 Yeye atazaa mwana, nawe lazima umwite jina lake Yesu, kwa maana yeye ataokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.” 22 Yote haya kwa kweli yalitukia ili litimizwe lile lililosemwa na Yehova kupitia nabii wake, akisema: 23 “Tazama! Bikira atakuwa na mimba naye atazaa mwana, nao watamwita jina lake Imanueli,” ambalo litafsiriwapo humaanisha, “Pamoja Nasi Yuko Mungu.”
24 Ndipo Yosefu akaamka kutoka usingizi wake na kufanya kama malaika wa Yehova alivyokuwa amemwelekeza, naye akampeleka mke wake nyumbani. 25 Lakini hakufanya ngono naye mpaka alipozaa mwana; naye Yosefu akamwita jina lake Yesu.