Mathayo
2 Yesu alipokuwa amekwisha kuzaliwa katika Bethlehemu ya Yudea siku za Herode mfalme, tazama! wanajimu kutoka sehemu za mashariki walikuja Yerusalemu, 2 wakisema: “Yuko wapi yule aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake wakati tulipokuwa mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” 3 Aliposikia hilo Mfalme Herode akafadhaika, na Yerusalemu lote pamoja naye; 4 na alipowakusanya pamoja makuhani wakuu na waandishi wote wa watu akaanza kuulizia habari kutoka kwao juu ya ni wapi Kristo alipaswa kuzaliwa. 5 Wakamwambia: “Katika Bethlehemu ya Yudea; kwa maana hivi ndivyo imeandikwa kupitia nabii, 6 ‘Nawe, Ewe Bethlehemu la nchi ya Yuda, wewe si jiji duni zaidi sana kwa vyovyote miongoni mwa magavana wa Yuda; kwa maana kutoka kwako wewe atakuja mwenye kuongoza, atakayechunga watu wangu, Israeli.’”
7 Ndipo Herode akawaita wale wanajimu kwa siri na kuhakikisha kwa uangalifu kutoka kwao wakati wa kuonekana kwa ile nyota; 8 na, wakati alipokuwa akiwatuma Bethlehemu, akasema: “Nendeni mkamtafute kwa uangalifu mtoto mchanga, na mkiisha kumpata leteni ripoti kwangu, ili mimi vilevile nipate kwenda na kumsujudia.” 9 Walipokuwa wamemsikia mfalme, walishika njia yao wakaenda; na, tazama! nyota waliyokuwa wameona wakati walipokuwa mashariki ikaenda mbele yao, mpaka ikaja kutua juu ya alipokuwa yule mtoto mchanga. 10 Walipoona ile nyota walishangilia sana kwelikweli. 11 Nao walipoenda ndani ya ile nyumba wakaona huyo mtoto mchanga pamoja na Maria mama yake, na, wakianguka chini, wakamsujudia mtoto. Pia wakafungua hazina zao na kumtolea zawadi, dhahabu na ubani na manemane. 12 Hata hivyo, kwa sababu walipewa onyo la kimungu katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakaondoka kwenda nchi yao kwa njia nyingine.
13 Walipokuwa wamekwisha kuondoka, tazama! malaika wa Yehova akaonekana katika ndoto kwa Yosefu, akisema: “Inuka, chukua huyo mtoto mchanga na mama yake mkimbie kuingia Misri, na kaeni huko mpaka nikupe agizo; kwa maana Herode yuko karibu kutafuta huyo mtoto mchanga amwangamize.” 14 Kwa hiyo yeye akainuka na kuchukua pamoja naye yule mtoto mchanga na mama yake wakati wa usiku na kuondoka kuingia Misri, 15 naye akakaa huko hadi kufa kwa Herode, ili litimizwe lile lililosemwa na Yehova kupitia nabii wake, akisema: “Kutoka Misri nilimwita mwana wangu.”
16 Ndipo Herode, akiona ameshindwa akili na wale wanajimu, akaingiwa na hasira kali kubwa, akatuma nje na kuagiza wavulana wote katika Bethlehemu na katika wilaya zake zote wamalizwe, kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini, kulingana na wakati aliokuwa amehakikisha kwa uangalifu kutoka kwa wale wanajimu. 17 Ndipo likatimizwa lile lililosemwa kupitia Yeremia nabii, akisema: 18 “Sauti ilisikiwa katika Rama, kutoa machozi na kulia kwingi; ni Raheli aliyekuwa akitoa machozi kwa ajili ya watoto wake, naye hakutaka kupokea faraja, kwa sababu hawako tena.”
19 Herode alipokuwa amekwisha kufa, tazama! malaika wa Yehova akaonekana katika ndoto kwa Yosefu Misri 20 naye akasema: “Inuka, chukua huyo mtoto mchanga na mama yake na ushike njia yako uende kuingia katika nchi ya Israeli, kwa maana wale waliokuwa wakiitafuta sana nafsi ya mtoto mchanga ni wafu.” 21 Kwa hiyo yeye akainuka na kuchukua huyo mtoto mchanga na mama yake na kuingia katika nchi ya Israeli. 22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alitawala akiwa mfalme wa Yudea badala ya Herode baba yake, akawa aogopa kuondoka kwenda huko. Zaidi ya hilo, akipewa onyo la kimungu katika ndoto, akaondoka kuingia eneo la Galilaya, 23 na kuja kukaa katika jiji liitwalo jina Nazareti, ili kwamba lipate kutimizwa lile lililosemwa kupitia manabii: “Yeye ataitwa Mnazareti.”