Mathayo
3 Katika siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Yudea, 2 akisema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbingu umekaribia.” 3 Huyu, kwa kweli, ndiye asemwaye kupitia Isaya nabii kwa maneno haya: “Sikilizeni! Mtu fulani anapaaza kilio nyikani, ‘Tayarisheni njia ya Yehova, nyinyi watu! Fanyeni barabara zake ziwe nyoofu.’” 4 Lakini Yohana huyuhuyu alikuwa na mavazi yake yakiwa ya nywele za ngamia na mshipi wa ngozi kuzunguka viuno vyake; chakula chake pia kilikuwa nzige na asali-mwitu. 5 Ndipo Yerusalemu na Yudea yote na nchi yote kandokando ya Yordani zikashika njia zao kumwendea, 6 na watu wakabatizwa naye katika Mto Yordani, wakiungama waziwazi dhambi zao.
7 Alipoona mara hiyo wengi wa Mafarisayo na Masadukayo wakija kwenye ubatizo, akawaambia: “Nyinyi uzao wa nyoka-vipiri, ni nani ambaye amewadokezea nyinyi kuikimbia hasira ya kisasi inayokuja? 8 Kwa hiyo basi tokezeni matunda yanayofaa toba; 9 na msijitangulize kujiambia wenyewe, ‘Kama baba tuna Abrahamu.’ Kwa maana nawaambia nyinyi kwamba Mungu aweza kuinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya. 10 Tayari shoka limelala kwenye mzizi wa miti; basi, kila mti usiotokeza matunda bora ni wa kukatwa na kutupwa ndani ya moto. 11 Mimi, kwa upande wangu, nawabatiza nyinyi kwa maji kwa sababu ya toba yenu; lakini yule anayekuja baada yangu ni mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye makubazi yake mimi sistahili kuyavua. Huyo atawabatiza nyinyi watu kwa roho takatifu na kwa moto. 12 Sepetu yake ya kupepetea imo mkononi mwake, naye atasafisha kabisa sakafu yake ya kupuria, na atakusanya ngano yake ghalani lakini makapi atayachoma kabisa kwa moto usioweza kuzimwa.”
13 Ndipo Yesu akaja kutoka Galilaya hadi Yordani kwa Yohana, kusudi abatizwe naye. 14 Lakini huyu wa mwisho akajaribu kumzuia yeye, akisema: “Mimi ndimi ninayehitaji kubatizwa nawe, na je, wewe unakuja kwangu?” 15 Kwa kujibu Yesu akamwambia: “Acha iwe hivyo, wakati huu, kwa maana katika njia hiyo yafaa kwetu kutekeleza yote yaliyo ya uadilifu.” Ndipo akakoma kumzuia. 16 Baada ya kubatizwa mara Yesu akapanda kutoka katika maji; na, tazama! mbingu zikafunguliwa, naye akaona roho ya Mungu ikishuka kama njiwa, ikija juu yake. 17 Tazama! Pia, kulikuwa na sauti kutoka katika mbingu iliyosema: “Huyu ni Mwana wangu, mpendwa, ambaye nimemkubali.”