Mathayo
8 Alipokuwa amekwisha kuteremka kutoka kwenye mlima umati mkubwa ulimfuata. 2 Na, tazama! mtu mwenye ukoma akaja na kuanza kumsujudia, akisema: “Bwana, ikiwa tu wewe wataka, waweza kunifanya safi.” 3 Na kwa hiyo, akinyoosha mkono wake, akamgusa, akisema: “Mimi nataka. Fanywa safi.” Na mara ukoma wake ukasafishwa kabisa. 4 Ndipo Yesu akamwambia: “Angalia kwamba huambii yeyote, bali nenda, ujionyeshe mwenyewe kwa kuhani, na kutoa zawadi ambayo Musa aliweka, kusudi iwe ushahidi kwao.”
5 Yeye alipoingia katika Kapernaumu, ofisa-jeshi mmoja akamjia, akimsihi sana 6 na kusema: “Bwana, mtumishi wangu mwanamume amelazwa katika nyumba akiwa na ugonjwa wa kupooza, akiteswa-teswa vibaya sana.” 7 Akamwambia: “Nifikapo huko hakika nitamponya.” 8 Kwa kujibu huyo ofisa-jeshi akasema: “Bwana, mimi si mtu mwenye kustahili kwamba wewe uingie chini ya paa yangu, lakini liseme neno tu na mtumishi wangu mwanamume ataponywa. 9 Kwa maana mimi pia ni mtu aliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari-jeshi chini yangu, nami humwambia huyu, ‘Shika njia yako uende!’ naye hushika njia yake na kwenda, na kwa mwingine, ‘Njoo!’ naye huja, na kwa mtumwa wangu, ‘Fanya hili!’ naye hulifanya.” 10 Aliposikia hilo, Yesu akawa mwenye kushangaa na kuwaambia wale waliokuwa wakimfuata: “Mimi nawaambia nyinyi iliyo kweli, Kwa yeyote katika Israeli sijapata imani kubwa sana kadiri hii. 11 Lakini nawaambia nyinyi kwamba wengi kutoka sehemu za mashariki na sehemu za magharibi watakuja na kuegama kwenye meza pamoja na Abrahamu na Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbingu; 12 lakini wana wa ufalme watatupwa ndani ya giza nje. Humo ndimo kutoa kwao machozi na kusaga meno yao kutakuwa.” 13 Ndipo Yesu akamwambia huyo ofisa-jeshi: “Nenda. Kama vile imani yako imekuwa, acha iwe hivyo kwa ajili yako.” Na yule mtumishi mwanamume akaponywa katika saa hiyo.
14 Na Yesu, alipokuja ndani ya nyumba ya Petro, aliona mama-mkwe wake amelala chini akiwa mgonjwa akiwa na homa. 15 Kwa hiyo akagusa mkono wake, na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia. 16 Lakini baada ya kuwa jioni, watu walimletea watu wengi waliopagawa na roho waovu; naye akafukuza hao roho kwa kusema neno, naye akaponya wote waliokuwa na hali mbaya; 17 ili kupate kutimizwa lile lililosemwa kupitia Isaya nabii, akisema: “Yeye mwenyewe alichukua magonjwa yetu na kuchukua maradhi yetu.”
18 Yesu alipoona umati wenye kumzunguka, alitoa amri kusukuma kwenda upande ule mwingine. 19 Na mwandishi fulani akatokea na kumwambia: “Mwalimu, hakika mimi nitakufuata wewe kokote ambako uko karibu kwenda.” 20 Lakini Yesu akamwambia: “Mbweha wana mapango na ndege wa mbinguni wana viota, lakini Mwana wa binadamu hana mahali popote pa kulaza kichwa chake.” 21 Ndipo mwingine wa wanafunzi akamwambia: “Bwana, niruhusu kwanza niondoke na kuzika baba yangu.” 22 Yesu akamwambia: “Fuliza kunifuata mimi, na acha wafu wazike wafu wao.”
23 Naye alipopanda ndani ya mashua, wanafunzi wake walimfuata. 24 Sasa, tazama! msukosuko mkubwa ukatokea katika bahari, hivi kwamba mashua ilikuwa ikifunikwa na mawimbi; hata hivyo, yeye alikuwa amelala usingizi. 25 Nao wakaja na kumwamsha, wakisema: “Bwana, tuokoe, tuko karibu kuangamia!” 26 Lakini yeye akawaambia: “Kwa nini mna moyo wa woga, nyinyi wenye imani kidogo?” Ndipo, akiinuka, akakemea zile pepo na hiyo bahari, na kukawa shwari kubwa. 27 Kwa hiyo wale watu wakawa wenye kushangaa na kusema: “Ni binadamu wa namna gani huyu, hivi kwamba hata pepo na bahari humtii?”
28 Alipofika upande ule mwingine, kuingia katika wilaya ya Wagadarene, walikutana naye wanaume wawili waliopagawa na roho waovu wakitoka kati ya makaburi ya ukumbusho, wakali isivyo kawaida, hivi kwamba hakuna mtu aliyekuwa na moyo wa kupita katika barabara hiyo. 29 Na, tazama! wakapiga mayowe, wakisema: “Sisi tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je, ulikuja hapa kututesa-tesa kabla ya wakati uliowekwa?” 30 Lakini mwendo mrefu kutoka kwao kundi la nguruwe wengi lilikuwa kwenye malisho. 31 Kwa hiyo wale roho waovu wakaanza kumsihi sana, wakisema: “Ukitufukuza, tutume kuingia katika lile kundi la nguruwe.” 32 Basi akawaambia: “Nendeni!” Wakatoka na kwenda zao kuingia katika wale nguruwe; na, tazama! kundi zima likatimua mbio kali juu ya genge kuingia katika bahari na kufa katika yale maji. 33 Lakini wachungaji wakakimbia na, wakienda katika jiji, wakaripoti kila kitu, kutia na jambo la wale watu waliopagawa na roho waovu. 34 Na, tazama! jiji lote likajitokeza ili kukutana na Yesu; na walipokwisha kumwona, wakamhimiza kwa bidii aondoke kutoka katika wilaya zao.