Mathayo
7 “Komeni kuhukumu ili msipate kuhukumiwa; 2 kwa maana kwa hukumu mnayohukumu, mtahukumiwa; na kwa kipimo mnachopimia, watawapimia nyinyi. 3 Basi, kwa nini wautazama unyasi ulio katika jicho la ndugu yako, lakini hulifikirii boriti lililo katika jicho lako mwenyewe? 4 Au wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Niruhusu niutoe unyasi ulio katika jicho lako’; wakati, tazama! boriti limo katika jicho lako mwenyewe? 5 Mnafiki! Kwanza toa boriti lililo katika jicho lako mwenyewe, na ndipo utaona waziwazi jinsi ya kutoa unyasi ulio katika jicho la ndugu yako.
6 “Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, ili wasipate kamwe kuzikanyaga-kanyaga chini ya miguu yao na kugeuka kabisa na kuwararua nyinyi.
7 “Fulizeni kuomba, nanyi mtapewa; fulizeni kutafuta sana, nanyi mtapata; fulizeni kubisha hodi, nanyi mtafunguliwa. 8 Kwa maana kila mtu anayeomba hupokea, na kila mtu anayetafuta sana hupata, na kwa kila mtu anayebisha hodi utafunguliwa. 9 Kwa kweli, ni nani mtu yule miongoni mwenu nyinyi ambaye mwana wake huomba mkate—yeye hatamkabidhi jiwe, je, atamkabidhi? 10 Au, labda, ataomba samaki—yeye hatamkabidhi nyoka, je, atamkabidhi? 11 Kwa hiyo, ikiwa nyinyi, mjapokuwa waovu, mwajua jinsi ya kuwapa watoto wenu zawadi zilizo nzuri, si zaidi sana hivyo Baba yenu aliye katika mbingu atawapa vitu vyema wale wanaomwomba?
12 “Kwa hiyo, mambo yote mtakayo watu wawafanyie nyinyi, lazima mwafanyie wao pia hivyohivyo; hili, kwa kweli, ndilo ambalo Sheria na Manabii humaanisha.
13 “Ingieni kupitia lango jembamba; kwa sababu ni pana na yenye nafasi barabara inayoongoza kuingia katika uharibifu, na wengi ndio wanaoingia kupitia hiyo; 14 lakini lango ni jembamba na barabara ni yenye kufinyana inayoongoza kuingia katika uhai, na wachache ndio wanaoipata.
15 “Iweni wenye kulinda kuhusu manabii wasio wa kweli ambao huja kwenu katika mavazi ya kondoo, lakini ndani wao ni mbwa-mwitu walafi. 16 Kwa matunda yao mtawatambua. Watu hawakusanyi kamwe zabibu kutoka kwenye miiba au tini kutoka kwenye michongoma, je, hukusanya? 17 Hivyohivyo kila mti mwema hutokeza matunda bora, lakini kila mti uliooza hutokeza matunda yasiyofaa kitu; 18 mti mwema hauwezi kuzaa matunda yasiyofaa kitu, wala mti uliooza hauwezi kutokeza matunda bora. 19 Kila mti usiotokeza matunda bora hukatwa na kutupwa ndani ya moto. 20 Basi, kwa kweli kwa matunda yao mtawatambua watu hao.
21 “Si kila mtu anayeniambia, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbingu, bali yule anayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye katika mbingu ataingia. 22 Wengi wataniambia katika siku hiyo, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii katika jina lako, na kufukuza roho waovu katika jina lako, na kufanya kazi nyingi zenye nguvu katika jina lako?’ 23 Na bado ndipo hakika nitaungama kwao: Sikuwajua nyinyi kamwe! Ondokeni kwangu, nyinyi wafanyakazi wa uasi-sheria.
24 “Kwa hiyo kila mtu asikiaye semi zangu hizi na kuzifanya atafananishwa na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya tungamo-mwamba. 25 Na mvua ikamwagika na mafuriko yakaja na pepo zikavuma na kudunda dhidi ya nyumba hiyo, lakini haikuporomoka, kwa maana ilikuwa imepigwa msingi juu ya tungamo-mwamba. 26 Zaidi ya hilo, kila mtu anayesikia semi zangu hizi na hazifanyi atafananishwa na mwanamume mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. 27 Na mvua ikamwagika na mafuriko yakaja na pepo zikavuma na kugonga dhidi ya nyumba hiyo nayo ikaporomoka, na anguko layo lilikuwa kubwa.”
28 Basi wakati Yesu alipomaliza semi hizo, tokeo lilikuwa kwamba umati ulishangaa juu ya njia yake ya kufundisha; 29 kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, na si kama waandishi wao.