Mathayo
6 “Angalieni vizuri kwamba msidhihirishe uadilifu wenu mbele ya watu kusudi mwangaliwe nao; kama sivyo hamtakuwa na thawabu kwa Baba yenu aliye katika mbingu. 2 Kwa sababu hiyo wakati uendapo kutoa zawadi za rehema, usipulize tarumbeta mbele yako, kama vile wanafiki hufanya katika masinagogi na katika barabara, ili wapate kutukuzwa na watu. Kwa kweli nawaambia nyinyi, Wanapata thawabu yao kwa ukamili. 3 Lakini wewe, unapotoa zawadi za rehema, usiache mkono wako wa kushoto ujue lile ambalo mkono wako wa kuume unafanya, 4 ili zawadi zako za rehema zipate kuwa katika siri; ndipo Baba yako anayetazama katika siri atakurudishia wewe.
5 “Pia, wakati msalipo, lazima msiwe kama wanafiki; kwa sababu wao hupendezwa na kusali wakisimama katika masinagogi na kwenye pembe za njia pana waonekane na watu. Kwa kweli nawaambia nyinyi, Wanapata thawabu yao kwa ukamili. 6 Hata hivyo, wewe usalipo ingia ndani ya chumba chako cha faragha na, baada ya kufunga mlango wako, sali kwa Baba yako aliye katika siri; ndipo Baba yako atazamaye katika siri atakurudishia wewe. 7 Lakini mnaposali, msiseme mambo yaleyale tena na tena, kama vile watu wa mataifa hufanya, kwa maana wao huwazia watapata kusikiwa kwa utumizi wao wa maneno mengi. 8 Kwa hiyo, msijifanye wenyewe kama wao, kwa maana Mungu Baba yenu ajua ni vitu gani mnavyohitaji hata kabla nyinyi hamjamwomba.
9 “Basi, nyinyi lazima msali kwa njia hii:
“‘Baba yetu uliye katika mbingu, jina lako na litakaswe. 10 Acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia. 11 Tupe sisi leo mkate wetu kwa siku hii; 12 na utusamehe madeni yetu, kama vile sisi pia tumesamehe wadeni wetu. 13 Na usituingize katika kishawishi, bali utukomboe kutokana na yule mwovu.’
14 “Kwa maana ikiwa mwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa kimbingu atawasamehe nyinyi pia; 15 lakini ikiwa hamsamehi watu makosa yao, wala Baba yenu hatasamehe makosa yenu.
16 “Wakati mnapofunga, komeni kuwa wenye nyuso zenye huzuni kama wanafiki, kwa maana wao huumbua nyuso zao ili wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Kwa kweli nawaambia nyinyi, Wanapata thawabu yao kwa ukamili. 17 Lakini wewe, unapofunga, paka kichwa chako mafuta na osha uso wako, 18 ili upate kuonekana kuwa unafunga, si na wanadamu, bali na Baba yako aliye katika siri; ndipo Baba yako anayetazama katika siri atakurudishia wewe.
19 “Komeni kujiwekea akiba ya hazina duniani, ambako nondo na kutu hula kabisa, na ambako wezi huvunja na kuiba. 20 Badala ya hivyo, jiwekeeni akiba ya hazina mbinguni, ambako wala nondo wala kutu haili kabisa, na ambako wezi hawavunji na kuiba. 21 Kwa maana ilipo hazina yako, ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
22 “Taa ya mwili ni jicho. Basi, ikiwa jicho lako ni sahili, mwili wako wote utakuwa mwangavu; 23 lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa wenye giza. Ikiwa kwa kweli nuru iliyo katika wewe ni giza, jinsi lilivyo kubwa giza hilo!
24 “Hakuna awezaye kutumikia kama mtumwa mabwana-wakubwa wawili; kwa maana ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, ama atashikamana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kutumikia kama watumwa Mungu na Utajiri.
25 “Kwa sababu hiyo nawaambia nyinyi: Komeni kuhangaikia nafsi zenu kuhusu ni nini mtakula au ni nini mtakunywa, au juu ya miili yenu kuhusu ni nini mtavaa. Je, nafsi haimaanishi zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni kwa mkazo ndege wa mbinguni, kwa sababu hawapandi mbegu au kuvuna au kukusanya ghalani; na bado Baba yenu wa kimbingu huwalisha wao. Je, nyinyi si bora kuliko wao? 27 Ni nani kati yenu kwa kuhangaika aweza kuongeza dhiraa moja kwenye muda wake wa uhai? 28 Pia, katika lile jambo la mavazi, kwa nini mwahangaika? Twaeni somo kutokana na mayungiyungi ya shamba, jinsi yanavyokua; hayamenyeki kwa kazi, wala hayasokoti; 29 lakini nawaambia nyinyi kwamba hata Solomoni katika utukufu wake wote hakupambwa kama moja la haya. 30 Basi, ikiwa Mungu huvisha hivyo mimea ya shambani, ambayo ipo hapa leo na kesho hutupwa ndani ya joko, je, si afadhali zaidi sana yeye atawavisha nyinyi, nyinyi wenye imani kidogo? 31 Kwa hiyo msihangaike kamwe na kusema, ‘Tule nini?’ au, ‘Tunywe nini?’ au, ‘Tuvae nini?’ 32 Kwa maana vyote hivi ndivyo vitu ambavyo mataifa yanafuatia kwa hamu. Kwa maana Baba yenu wa kimbingu ajua mwahitaji vitu hivi vyote.
33 “Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme na uadilifu wake, na vitu vingine vyote hivi mtaongezewa. 34 Kwa hiyo, msihangaike kamwe juu ya siku ifuatayo, kwa maana siku ifuatayo itakuwa na mahangaiko yayo yenyewe. Waitosha kila siku ubaya wayo yenyewe.