Mathayo
9 Basi, akiipanda mashua, akaanza kuvuka na kwenda katika jiji la kwake mwenyewe. 2 Na, tazama! walikuwa wakimletea mtu aliyepooza akiwa amelala juu ya kitanda. Alipoona imani yao Yesu akamwambia mwenye kupooza: “Jipe moyo, mtoto; dhambi zako zimesamehewa.” 3 Na, tazama! baadhi ya waandishi wakaambiana wao wenyewe: “Jamaa huyu anakufuru.” 4 Naye Yesu, akijua fikira zao, akasema: “Kwa nini mnafikiri mambo maovu katika mioyo yenu? 5 Kwa mfano, ni jipi lililo rahisi zaidi, kusema, Dhambi zako zimesamehewa, au kusema, Inuka na kutembea? 6 Hata hivyo, kusudi nyinyi mjue kwamba Mwana wa binadamu ana mamlaka juu ya dunia kusamehe dhambi—” ndipo akamwambia mwenye kupooza: “Inuka, chukua kitanda chako, na kwenda nyumbani kwako.” 7 Naye akainuka na kwenda zake nyumbani kwake. 8 Kwa kuona hilo umati ukaingiwa na hofu, nao ukamtukuza Mungu, aliyewapa wanadamu mamlaka ya namna hiyo.
9 Halafu, alipokuwa akipita kutoka hapo, Yesu akaona mara hiyo mtu fulani aitwaye jina Mathayo akiwa ameketi kwenye ofisi ya kodi, naye akamwambia: “Uwe mfuasi wangu.” Mara akainuka na kumfuata. 10 Baadaye, huku akiwa ameegama kwenye meza katika ile nyumba, tazama! wakusanya-kodi wengi na watenda-dhambi wakaja na kuanza kuegama na Yesu na wanafunzi wake. 11 Lakini kwa kuona hilo Mafarisayo wakaanza kuwaambia wanafunzi wake: “Ni kwa nini mwalimu wenu hula pamoja na wakusanya-kodi na watenda-dhambi?” 12 Alipowasikia, yeye akasema: “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali wenye kuugua wahitaji. 13 Nendeni, basi, na mjifunze kile ambacho hili lamaanisha, ‘Mimi nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana nilikuja kuita, si watu waadilifu, bali watenda-dhambi.”
14 Ndipo wanafunzi wa Yohana wakamjia na kuuliza: “Ni kwa nini sisi na Mafarisayo huzoea kufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?” 15 Ndipo Yesu akawaambia: “Marafiki wa bwana-arusi hawana sababu ya kuomboleza maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao, sivyo? Lakini siku zitakuja wakati bwana-arusi atakapoondolewa mbali kutoka kwao, na ndipo watakapofunga. 16 Hakuna mtu ashonaye juu ya vazi la nje kuukuu, kiraka cha nguo ambayo haijaruka; kwa maana nguvu yayo kamili ingevuta kutoka kwenye lile vazi la nje na mraruko ungekuwa mbaya zaidi. 17 Wala watu hawaweki divai mpya ndani ya viriba vya divai vikuukuu; lakini wakifanya hivyo, ndipo vile viriba vya divai hupasuka na ile divai humwagika na vile viriba vya divai huharibika. Bali watu huweka divai mpya ndani ya viriba vipya vya divai, na vitu vyote viwili huhifadhiwa.”
18 Alipokuwa akiwaambia mambo hayo, tazama! mtawala fulani aliyekuwa amekaribia alianza kumsujudia, akisema: “Kufikia sasa binti yangu lazima awe amekufa; lakini njoo uweke mkono wako juu yake naye atapata kuwa hai.”
19 Basi Yesu, akiinuka, akaanza kumfuata; pia wanafunzi wake wakamfuata. 20 Na, tazama! mwanamke mwenye kutaabika miaka kumi na miwili kutokana na mtiririko wa damu akaja nyuma na kuugusa upindo wenye matamvua wa vazi lake la nje; 21 kwa maana alifuliza kujiambia mwenyewe: “Kama tu nikigusa vazi lake la nje nitapona.” 22 Yesu akageuka kabisa na, akimwona, akasema: “Jipe moyo, binti; imani yako imekufanya upone.” Na kutoka saa hiyo yule mwanamke akapona.
23 Basi, alipokuja kuingia katika nyumba ya yule mtawala na kuona mara hiyo wacheza-filimbi na umati katika mvurugo wenye makelele, 24 Yesu alianza kusema: “Ondokeni mahali hapa, kwa maana msichana mdogo hakufa, bali analala usingizi.” Ndipo wakaanza kumcheka kwa kudharau. 25 Mara tu umati ulipokuwa umeagizwa kwenda nje, yeye akaingia na kushika mkono wake, na huyo msichana mdogo akainuka. 26 Bila shaka, maongezi juu ya hilo yakasambaa katika mkoa wote huo.
27 Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, wanaume wawili vipofu wakamfuata, wakipaaza kilio na kusema: “Uwe na rehema juu yetu, Mwana wa Daudi.” 28 Alipokuwa amekwisha kuingia katika ile nyumba, wale wanaume vipofu wakamjia, naye Yesu akawauliza: “Je, mna imani kwamba naweza kufanya hilo?” Wakamjibu: “Ndiyo, Bwana.” 29 Ndipo akagusa macho yao, akisema: “Kulingana na imani yenu acheni hilo litukie kwenu.” 30 Na macho yao yakapata kuona. Zaidi ya hayo, Yesu akawaagiza kwa kusisitiza, akisema: “Angalieni kwamba mtu yeyote asipate kujua hilo.” 31 Lakini wao, baada ya kufika nje, wakajulisha kwa watu wote juu yake katika mkoa wote huo.
32 Sasa walipokuwa wakiondoka, tazama! watu wakamletea bubu aliyepagawa na roho mwovu; 33 na yule roho mwovu alipokuwa amekwisha kufukuzwa yule bubu akasema. Basi, ule umati ukahisi mshangao na kusema: “Halikuonwa kamwe jambo lolote kama hili katika Israeli.” 34 Lakini Mafarisayo wakaanza kusema: “Ni kwa mtawala wa roho waovu kwamba yeye huwafukuza roho waovu.”
35 Na Yesu akaondoka ili kutalii majiji na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao na kuhubiri habari njema ya ufalme na kuponya kila namna ya maradhi na kila namna ya udhaifu. 36 Alipouona umati alihisi sikitiko kwa ajili yao, kwa sababu ulikuwa umechunwa ngozi na kutupwa huku na huku kama kondoo wasio na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake: “Ndiyo, mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo, ombeni Bwana-mkubwa wa mavuno atume wafanyakazi katika mavuno yake.”