Luka
18 Ndipo yeye akaendelea kuwaambia kielezi kuhusiana na uhitaji wao wa kusali sikuzote wala si kukata tamaa, 2 akisema: “Katika jiji fulani kulikuwako hakimu fulani asiyekuwa na hofu ya Mungu na asiyekuwa na staha kwa mwanadamu. 3 Lakini kulikuwako mjane katika jiji hilo naye alifuliza kumwendea, akisema, ‘Hakikisha kwamba mimi napata haki kutoka kwa mpinzani wangu sheriani.’ 4 Basi, kwa muda fulani alikuwa hana nia, lakini baadaye akajiambia, ‘Ijapokuwa mimi sihofu Mungu wala kustahi mwanadamu, 5 hakika, kwa sababu ya kuendelea kwa mjane huyu kunisumbua, nitahakikisha kwamba apata haki, ili asifulize kuja kunipigapiga ngumi hadi nimalizike.’” 6 Ndipo Bwana akasema: “Sikieni lile ambalo hakimu, ijapokuwa si mwadilifu, alisema! 7 Basi, kwa hakika je, Mungu hatasababisha haki ifanywe kwa ajili ya wachaguliwa wake ambao wampaazia kilio mchana na usiku, hata ingawa yeye ni mwenye ustahimilivu kuwaelekea? 8 Mimi nawaambia nyinyi, Yeye atasababisha haki ifanywe kwao kasi. Hata hivyo, Mwana wa binadamu awasilipo, je, kwa kweli ataipata hiyo imani duniani?”
9 Lakini yeye aliwaambia kielezi hiki pia baadhi ya wale waliojiitibari wenyewe kwamba walikuwa waadilifu na walioona wale wengine kama si kitu: 10 “Watu wawili walipanda kwenda ndani ya hekalu kusali, mmoja Farisayo na yule mwingine mkusanya-kodi. 11 Yule Farisayo alisimama na kuanza kusali mambo haya akijiambia, ‘Ee Mungu, mimi nakushukuru ya kuwa mimi si kama wale watu wengine, wanyang’anyi, wasio waadilifu, wazinzi, au hata kama mkusanya-kodi huyu. 12 Mimi hufunga mara mbili kwa juma, mimi hutoa sehemu ya kumi ya vitu vyote nijipatiavyo.’ 13 Lakini yule mkusanya-kodi akiwa amesimama kwa umbali fulani hakutaka hata kuinua macho yake kuelekea mbinguni, bali alifuliza kupiga kifua chake, akisema, ‘Ee Mungu, uwe mwenye fadhili kwangu mimi mtenda-dhambi.’ 14 Nawaambia nyinyi, Mtu huyu aliteremka kwenda nyumbani kwake akiwa amethibitishwa mwadilifu zaidi kuliko mtu yule; kwa sababu kila mtu ajikwezaye mwenyewe atatwezwa, bali yeye ajinyenyekezaye atakwezwa.”
15 Sasa watu wakaanza kumletea pia vitoto vyao vichanga ili aviguse; lakini walipoona hilo wanafunzi wakaanza kuwakemea. 16 Hata hivyo, Yesu akaita vile vitoto vichanga kwake, akisema: “Waacheni hao watoto wachanga waje kwangu, na msijaribu kuwakomesha. Kwa maana ufalme wa Mungu ni wa walio kama hao. 17 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Yeyote yule asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mchanga hataingia kwa vyovyote ndani ya huo.”
18 Na mtawala fulani akamuuliza swali, akisema: “Mwalimu Mwema, ni kwa kufanya nini mimi nitarithi uhai udumuo milele?” 19 Yesu akamwambia: “Kwa nini waniita mwema? Hakuna mtu aliye mwema, ila mmoja, Mungu. 20 Wewe wazijua amri, ‘Usifanye uzinzi, Usiue kimakusudi, Usiibe, Usitoe ushahidi usio wa kweli, Heshimu baba yako na mama.’” 21 Ndipo yeye akasema: “Yote hayo nimeyashika tangu ujana na kuendelea.” 22 Baada ya kusikia hilo, Yesu akamwambia: “Bado kuna jambo moja linalokosa juu yako: Uza vitu vyote ulivyo navyo uwagawie maskini, nawe utakuwa na hazina katika mbingu; na uje uwe mfuasi wangu.” 23 Aliposikia hilo, akawa mwenye kutiwa kihoro sana, kwa maana alikuwa tajiri sana.
24 Yesu akamtazama na kusema: “Jinsi litakavyokuwa jambo gumu kwa wale walio na fedha kuingia katika ufalme wa Mungu! 25 Kwa kweli, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano ya kushonea kuliko kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” 26 Wale waliosikia hilo wakasema: “Nani aweza kuokolewa?” 27 Yeye akasema: “Mambo yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.” 28 Lakini Petro akasema: “Tazama! Sisi tumeacha vitu vyetu wenyewe na kukufuata wewe.” 29 Yeye akawaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Hakuna yeyote ambaye ameacha nyumba au mke au akina ndugu au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapata kwa njia yoyote mara nyingi zaidi katika kipindi hiki cha wakati, na katika mfumo wa mambo unaokuja uhai udumuo milele.”
31 Ndipo akachukua wale kumi na wawili kando na kuwaambia: “Tazameni! Sisi tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yaliyoandikwa kwa njia ya manabii kwa habari ya Mwana wa binadamu yatatimilizwa. 32 Kwa mfano, yeye atakabidhiwa kwa watu wa mataifa naye atafanyiwa ucheshi na kutendwa kwa ufidhuli na kutemewa mate; 33 na baada ya kumpiga mijeledi watamuua, lakini katika siku ya tatu atafufuliwa.” 34 Hata hivyo, wao hawakupata maana ya lolote la mambo hayo; lakini tamko hilo lilifichwa kutoka kwao, nao hawakuwa wakiyajua mambo yaliyosemwa.
35 Sasa alipokuwa akikaribia Yeriko mtu fulani aliye kipofu alikuwa ameketi kando ya barabara akiombaomba. 36 Kwa sababu alisikia umati ukisonga kupita alianza kuulizia habari hilo huenda likawa lamaanisha nini. 37 Wao wakaripoti kwake: “Yesu Mnazareti anapitia hapa!” 38 Ndipo akapaaza kilio, akisema: “Yesu, Mwana wa Daudi, uwe na rehema juu yangu!” 39 Na wale wenye kwenda wakitangulia wakaanza kumwambia kwa kusisitiza afulize kukaa kimya, lakini ndivyo naye alivyofuliza kupaaza sana sauti zaidi na zaidi: “Mwana wa Daudi, uwe na rehema juu yangu.” 40 Ndipo Yesu akasimama tuli na kuamuru huyo mtu aongozwe kwake. Baada ya yeye kukaribia, Yesu akamuuliza: 41 “Wataka nikufanyie nini?” Akasema: “Bwana, acha nipate kuona tena.” 42 Kwa hiyo Yesu akamwambia: “Pata kuona tena; imani yako imekufanya upone.” 43 Na mara hiyo yeye akapata kuona tena, naye akaanza kumfuata, akimtukuza Mungu. Pia, watu wote, walipoona hilo, wakampa Mungu sifa.